Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon Munira Mustafa Khatib (3 total)

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2015, Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.
MHE. MUNIRA MUSTAPHA KHATIBU: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi hii ili niweze kuchangia bajeti hii. Naomba kwanza nimshukuru Waziri wa Fedha na timu yake yote kwa kutuletea bajeti ambayo inaweza kwenda kumkomboa maskini wa chini. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naamini Serikali ina nia njema ya kumkomboa mwanamke mwenye kipato cha chini. Hata hivyo, cha kusikitisha vijana ambao ni zaidi ya asilimia 60 wamepatiwa shilingi bilioni tano kwa ajili ya kuendeleza ujuzi. Hii fedha ni kidogo sana kwa sababu vijana wanao-graduate kila mwaka ni zaidi ya 8,000. Kwa hiyo, naiomba Serikali iongeze pesa hii. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kama kweli tunaka kwenda kwenye nchi ya uchumi wa viwanda basi naomba Serikali iwe tayari kwenda kwenye nchi ya viwanda. Kivipi iwe tayari kwenda kwenye nchi ya viwanda? Ni kwa kuvilinda viwanda vyetu vya ndani kwani bado viwanda vyetu vya ndani Serikali haiko tayari kuvilinda.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna Kiwanda hiki cha Urafiki ambacho Serikali inamiliki asilimia 49 lakini hawa wenzetu Wachina wana asilimia 50. Kiwanda hiki kinamilikiwa na Wachina si Serikali. Ukiangalia hapa kuna tofauti ya asilimia mbili tu ili Serikali kuweza kukimiliki lakini ndani ya bajeti hii ya 2016/2017 bado Serikali haijatenga fedha hii kwa ajili ya kukikwamua kiwanda hiki.
Mheshimiwa Naibu Spika, ukiangalia Meneja ni kutoka China hajui vision wala mission ya Kiwanda hiki cha Urafiki. Hivi kweli tunatengenezaje ajira kupitia viwanda? Hivi ni vipi tunaweza kuwakomboa vijana wa Tanzania kwa kupata ajira? Kama hatuko tayari tungetafuta njia nyingine ya kusaidia vijana lakini si kwa njia hiyo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pia kuna Kiwanda cha TANELEC ambacho kiko Jijini Arusha kinazalisha jenereta. Jambo la kusikitisha Serikali inaagiza transformer nje badala ya kununua kutoka kwenye kiwanda hiki. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kama kweli tungekuwa tayari kununua transformer katika kiwanda hiki basi tungepata ajira nyingi kwa vijana na tungeweza kupata fedha kwa ajili ya Serikali yetu. Leo wanatoka watu nje ya nchi kuja kununua jenereta katika kiwanda hiki cha TANELEC lakini sisi Watanzania tunaagiza bidhaa kutoka nje ya nchi. Nina imani bado Serikali haijaamua kuinua uchumi wa viwanda Tanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nizungumzie suala la asilimia 5 ambazo kila Halmashauri inatakiwa itoe kwa ajili ya kusaidia wanawake na vijana. Kama kweli tuko tayari kumsaidia kijana, kama kweli tuko tayari kumsaidia mwanamke basi naiomba Serikali iweze kuleta fedha hizi kwa wakati. Naiomba Serikali iweze kusimamia fedha hizi kuona zinapatikana ndani ya halmashauri kwa sababu halmashauri nyingi fedha hii wanasema hizifiki na vijana wengi hawapati fedha hii. Je, kijana huyu unataka kumsaidia kwa njia gani wakati fedha hii haimfikii? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pia napenda kuzungumzia suala la kiinua mgongo cha Wabunge. Wabunge wengi wameliongelea suala hili la kiinua mgongo cha Wabunge lakini niiombe Serikali yangu, naamini ni sikivu, Serikali ya CCM inavyoambiwa inasikia. Mbunge huyu katika jimbo lake anafanya harusi, maziko, matibabu na kila kitu. Leo hii unasema Mbunge huyu huyu katika kiinua mgongo chake cha mwisho ambacho anakwenda kujipanga kimaisha, umkate kodi, kweli Mbunge huyu unamtaka baadaye afanye kitu gani? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naiomba Serikali yangu kwa nia njema, naamini Serikali yangu ina nia njema, iweze kukaa na kulifikiria suala hili la kuwakata Wabunge kodi. Naamini Serikali yangu ni sikivu na suala hili Wabunge wengi wamelizungumza, watalifanyia kazi.(Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hayo machache, naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Ofisi ya Waziri Mkuu
MHE. MUNIRA MUSTAPHA KHATIBU: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante.

Mheshimiwa Mwenyekiti, na mimi nianze kwa kumpongeza Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa hotuba yake nzuri ambayo inayoweza kumkomboa mwananchi hasa maskini. (Makofi

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwa kuchangia sehemu ya madawa ya kulevya. Tunashuhudia Waziri Mkuu na Wizar aya Vijana jinsi inavyopambana na masuala ya madawa ya kulevya, lakini suala hili kwa kweli bado ni tatizo moja kubwa sana ndani ya Tanzania. Tunaona Mheshimiwa Waziri, askari wanakamata vijana wadogo wadogo kwa issue ya madawa ya kulevya, tunajisahau kuwa vijana wadogo siyo waingizaji wa madawa ya kulevya. Kuna wafanyabiashara wakubwa, kuna viongozi wakubwa, kuna watu maarufu. Je, Serikali imejipangaje kukabiliana na mapapa hawa na kuachana na ngedere wadogo hawa ambao wao ni watumiaji lakini tunajisahau kama kuna watu ndiyo waingizaji wa madawa ya kulevya; kwa sababu unamkamata kijana mdogo ambae anatumia tu madawa ya kulevya, ukimkamata bado madawa ya kulevya ndani ya nchi yetu yanaendelea kuingia na watumiaji bado wanaendelea kutumia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu sober house nashukuru Mheshimiwa Waziri Mkuu alisema kuna sober houses 22 ambazo tayari zimeanzishwa, lakini sober houses siyo solution ya kusema tunaondoa suala la madawa ya kulevya. Hizi sober house kwanza tukumbuka ni nyumba za watu binafsi, kwa hiyo, business bado inaendelea.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hawa vijana waliopo ndani ya sober house wanasema kwamba wakianza kupona baadhi ya sober house wanapewa tena yale madawa ya kulevya ili waendelee kuwepo ndani ya sober house, kwa sababu kijana mmoja aliyopo ndani ya sober house analipia shilingi 400,000, kijana yule akiondoka ile business imeondoka, kwa hiyo, naiomba Serikali ifumbue macho na kuangalia hizi nyumba za sober house ni tatizo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ushauri wangu kama tunataka tuendelee na sober houses ziwekwe ndani ya mwamvuli wa Serikali, hilo ni jambo la kwanza.

Pili, tunataka vijana hawa ambao tayari wameshaathirika na madawa ya kulevya wachukuliwe wapelekwe hospitali, watibiwe, wapatiwe tiba na watakapopona wapewe mtaji badala ya kuwapeleka sober house zile pesa wapewe mtaji kwa ajili ya kuwaanzishia biashara yao, kwa sababu vijana hawa wanakuwa na changamoto za maisha hawana mtaji wa kuanzishia biashara. Zile pesa vijana hawa wapewe kwa ajili ya kuanzisha biashara na wataweza kuachana na madawa ya kulevya na kufanya biashara zao binafsi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu suala la ajira. Naomba niongee ukweli kwa sababu nitakapoongea ukweli nitakuwa nimemsaidia Mheshimiwa Rais, tusimdanganye Mheshimiwa Rais tukimdanganya bado tutakuwa hatujamsaidia, ili tumsaidie tumwambie ukweli, vijana wamekosa imani na Serikali yao kwa suala la ajira, suala la ajira limekuwa changamoto tuwatafutie vijana ajira ili waweze kutatua mambo yao wawe na imani na Serikali yao. Tusipoangalia vijana hawa wote watakimbilia kwenye madawa ya kulevya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunajua Serikali kwamba haiwezi kuajiri vijana wote ambao wanamaliza shule, lakini tuangalie njia gani tutafanya ili kuweza kuwasaidia vijana kuweza kujikwamua na maisha. Kwanza tukae na mabenki, tuzungumze nayo, yapunguze urasimu, yaweze kuwapa vijana mkopo wenye riba nafuu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, benki zina urasimu mkubwa kijana kama mimi nisingekuwa Mbunge leo hii nahitaji mkopo naambiwa niende na hati ya nyumba natoa wapi? Naambiwa niende na hati ya shamba natoa wapi? Ni lazima tukae tufikirie ni njia gani ya kumkwamua kijana aweze kujiendeleza katika maisha yake. Kuna miradi ambayo kuwa Mheshimiwa Rais ameianzisha, lakini unashangaa wanatoka vijana kutoka Kenya, Malawi, sijui kutoka wapi ndiyo anakuja kusimamia ajira hizo, tunaiomba Serikali ya Chama cha Mapinduzi ajira hizi zote zisimamiwe na vijana wa Kitanzania, kama miradi ya umeme iliyoanzishwa Rufiji, standard gauge na ujenzi wa viwanja vya ndege ajira hizi zote tunaomba zipate vijana wa Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nichangie kuhusu afya ya akina mama; kama mwanamke na kama mzazi nitakuwa sijajitendea haki nisipochangia suala la afya ya akina mama. Tulimuona Naibu Waziri akifungua warsha yake kwa vifungashio vya akina mama na akisema kina mama wachangie shilingi 20,000. Bado kwa mwanamke shilingi 20,000 ambaye ana kipato cha chini ni kubwa sana, kwa nini asiseme vifungaishio hivi viwe bure au aweke shilingi 5000 ambayo anajua mwanamke huyo au mama huyu anaweza kuimiliki kila mwanamke wa kijijini, kila mwanamke maskini anaweza kununua vifunganishio hivi, shilingi 20,000 bado kubwa sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nichangie kuhusu mazingira. Kila siku tunamshuhudia mama yetu Mheshimiwa Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan akienda katika warsha za kuendeleza misitu, tusikate miti hovyo, lakini nikwambie ukweli, miti bado itaendelea kukatwa kwa sababu bei ya gesi bado kubwa sana. Mwananchi wa kawaida huwezi kwenda kumwambia anunue gesi shilingi 50,000 akaacha mkaa shilingi 20,000, miti bado tunayo lakini hatujajua ni jinsi gani ya kuweza kulinda miti yetu. Kwa hiyo, hiyo miti tunayopanda tutashindwa kuilinda kwa sababu sasa hivi hatujui ni jinsi gani ya kuilinda. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naiomba Serikali yangu isaidie akina mama maskini kwa kuweza kupunguza bei ya gesi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nichangie kuhusu asilimia 10 inayotokana na vijana, akina mama na asilimia mbili kwa walemavu. Tukiongea ukweli ndani ya Halmashauri yetu hii pesa haipatikani, naiomba Serikali itafute njia ya kuweza kusimamia Halmashauri hizi ili vijana waweze kupata hizi asilimia nne, wanawake wapate asilimia hizi nne, walemavu wapate hizi asilimia mbili jumla itakuwa ni asilimia
10. Halmashauri itakapotenga hii pesa tutakuwa tumepunguza lile tatizo la kusema ajira kwa vijana, watajua jinsi gani kwa sababu ajira zipo nyingi, kijana anaweza kujiajiri kwenye kilimo, uvuvi, lakini kijana huwezi kumwambia leo hii aende akalime kilimo cha locally au aende akavue uvuvi locally lazima atataka kulima kilimo cha kisasa cha kumwagilia maji, kilimo hicho ili uweze kulima uwe na milioni tano isipungue, sasa hizi asilimia 10 zitakazotolewa na Halmashauri zetu vijana hawa wataweza kujisaidia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niongelee suala la bandari kidogo tu, bandarini pamekuwa na urasimu mkubwa sana, sisi tunaosafiri kupitia baharini pale ndiyo tunaona. Kijana anasafiri na vitenge doti 10 tu anaambiwa sijui TRA achangie, ushuru wa bandari, hebu tufikirie kijana huyu vitenge 10 atapata faida shilingi ngapi, pesa yote ambayo anachajiwa pale bandarini ndiyo pesa yake yote anayopata faida. Kwa hiyo anakuwa anafanya business as usual.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba tuangalie tena amechangia Bara anaenda Zanzibar anachangia tena, naomba haya mambo tuyaangalie huu urasimu mdogo wa kuondoka na doti 10 hapa za vitenge, halafu kijana yule akienda Zanzibar anakuwa-charged.

T A A R I F A . . .

MHE. MUNIRA MUSTAFA KHATIBU: Mheshimiwa Mwenyekiti, naipokea taarifa hiyo tena kwa mikono miwili asilimia mia moja. Hivyo ndivyo ilivyo, tunaomba basi Serikali ikae ifikirie hili suala limekuwa tatizo sana kwa vijana wetu, hawatafika wakati wakaweza kujitegemea wenyewe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru sana, ninaunga mkono hoja asilimia mia moja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji
MHE. MUNIRA M. KHATIB: Mheshimiwa Mwenyekiti, nami nashukuru kwa kupata nafasi kuchangia jioni hii ya leo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwa kumpongeza Mheshimiwa Waziri, Naibu Waziri wake na timu yake yote, Katibu Mkuu na Naibu Katibu Mkuu kwa hotuba nzuri ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naipongeza Serikali kwa kauli yake ya kusema sasa suala la mafuta ndani ya nchi yetu siyo tatizo. Naipongeza sana Serikali. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Rais alipokuwa katika ufunguzi wa Kiwanda cha Singida alisema kuwa viwanda vya kuzalisha mafuta anaondoa VAT kwa asilimia 18. Naomba Serikali iniambie, imetekeleza vipi agizo hili la Mheshimiwa Rais kwa kuondoa VAT katika mafuta ya alizeti?

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama kweli tunataka tufikie katika uchumi wa viwanda basi la kwanza ni kuvilinda viwanda vyetu vya ndani. Siyo viwanda vya mafuta tu, hata viwanda vyetu vya maziwa, tunaiomba Serikali iweze kuangalia suala hili ya VAT ya asilimia 18. Tutapoondoa asilimia hii 18, kwanza tutaweza kuongeza uzalishaji ndani ya nchi yetu, tutaweza kupunguza kuagiza mafuta ndani ya nchi yetu, tutaweza kuwasaidia wakulima wetu kimaisha ndani ya nchi yetu, hata pia tutaweza kuondoa tatizo la wafugaji kwenye nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niongelee kuhusu SIDO. Katika taarifa ya CAG, SIDO inaonekana iko katika hali mbaya. SIDO inafanya vibaya ndani ya mikoa yetu na Tanzania kwa ujumla. Mwaka 2017/2018 imepangiwa shilingi bilioni 6 lakini ndani ya pesa hii haijapatikana hata asilimia 1.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ajira nyingi za vijana zinapatikana katika viwanda vidogo vidogo. Kama tungeisaidia vizuri SIDO basi tungeweza kuzalisha ajira nyingi kwa vijana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimetembelea SIDO ya Iringa ina wafanyakazi watatu tu ambao wameajiriwa na Serikali. Hivi tutafikiaje uchumi wa viwanda na tunawasaidiaje vijana? Naiomba Serikali iangalie namna ya kuajiri watumishi wa SIDO ndani ya mikoa yetu na wazisaidie.

Mheshimiwa Mwenyekiti, SIDO ina wafanyakazi watatu, waliobakia wote wanajitolea mpaka Mnunuzi Mkuu na Mhasibu ndani ya SIDO wanajitolea, hizi kazi zinaendeshwaje? Naiomba Serikali na Mheshimiwa Waziri uko hapo, uisaidie SIDO ili kuweza kufikia katika uchumi wa viwanda. Kama hatuwezi kuzisaidia SIDO zetu, basi hatutaweza kusaidia uchumi wa viwanda. Ndani ya SIDO kuna mashine za miaka 70 kabla mimi sijazaliwa ndizo zinatumika mpaka leo. Naomba hizi pesa ambazo zimetengwa kwa ajili ya SIDO, zifike na zitolewe kwa wakati. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna hii FCC imekuwa tatizo sana kwa wafanyabiashara. Wamekaa kwa ajili kupiga penalty tu. Naiomba Serikali wangekaa na hizi taasisi wakawapa wafanyabiashara elimu. Wakienda sehemu za kuchukua bidhaa wajue ni bidhaa gani ambazo zinatakiwa ziingie ndani ya nchi yetu ili wasiwe wanachukua mzigo ambapo kisa tu haukuandikwa Sumsung au haukuandikwa iPhone ukifika ndani ya Tanzania mzigo ule ikawa ni kuharibiana biashara kwa kuchomeana moto. Tungekaa tukafikiria, kuna wafanyabiashara mpaka wanaumwa, wengine wanakufa kwa sababu ya hii FCC. Namwomba sana Mheshimiwa Waziri akae basi aangalie Watendaji wake aweze kuwasaidia wafanyabiashara wengi. Juzi kontena nzima ya chupi imechomwa moto na FCC. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna viwanda vimebinafsishwa ambavyo vilikuwa haviwezi kufanya kazi.

Naiomba basi Serikali viwanda vile virudi katika mikono ya Serikali. Viko ambavyo havijabinafsishwa lakini vinamilikiwa na sekta binafsi na zipo share za Serikali. Naiomba basi Serikali ikaangalie viwanda hivi ili viweze kufanya kazi vizuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, juzi niliuliza swali hapa kuhusu Kiwanda cha Nguo cha Urafiki lakini sikupata majibu ya kutosha na ndani ya kitabu cha Mheshimiwa Waziri sikuona maelezo yoyote kuhusu kiwanda hiki. Naomba basi wakati anahitimisha aniambie suala hili la Kiwanda cha Urafiki limefikia wapi kuhusu zile shares ambazo tunazo na wenzetu wa China? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna Kiwanda cha Nyama Dar es Salaam, naomba Mheshimiwa Waziri akiwa anahitimisha pia aje aniambie. Pia kuna Kiwanda cha ZZK Mbeya, kilikuwa kinatengeneza vifaa vya kilimo. Naomba Mheshimiwa Waziri akija aniambie, kwa sababu mpaka sasa hivi wakulima wetu kutumia majembe ya mkono wakati sisi wenyewe tulikuwa tuna kiwanda kikubwa tu na hakifanyi kazi, itakuwa ni aibu. Kwa hiyo, naomba Mheshimiwa Waziri atakapokuja hapa aniambie kuhusu viwanda hivi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna suala hili la vinywaji vikali ambapo Serikali inapoteza kodi nyingi. Vinywaji hivi vikali vinakosa kodi kwa kubandika sticker bandia na hili suala kuna baadhi ya Waheshimiwa Wabunge wameliongea na ushahidi upo. Naomba basi Serikali iangalie inapoteza mapato kiasi gani katika suala hili la kubandika hizi sticker bandia katika vinywaji vikali. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu vinywaji vikali Serikali ingekuwa ina-charge ile spirit wakati inaingia hapa nchini badala ya spirit ikiwa imeshatumika ndani ya vinywaji vikali ndiyo inakuja kuchajiwa. Hizi spirit zinapoingia tu nchini zichajiwe. Kwa sababu hizi spirit zinachajiwa kwa kiwango kidogo tu zinazokwenda kwenye hospitalini na sehemu nyingine lakini kiwango kikubwa kinatumika katika vinywaji vikali. Kwa hiyo, Serikali ingekaa ikaangalia vizuri kwa upande wa spirit inapoingia nchini. Tusi-charge ndani ya vinywaji, bali tu-charge inapoingia tu ndani ya nchi yetu.
(Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana, naunga mkono hoja.