Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Emmanuel Papian John (3 total)

MHE. EMMANUEL P. JOHN: Naomba kuuliza ni lini tunaweza kupata fedha za nyongeza kwa ajili ya mafuta ili watu hawa waweze kupata huduma ya kliniki kwenye maeneo hayo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAMISEMI, UTUMISHI NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kama nilisema katika jibu langu la msingi kwamba, ni kweli Halmashauri ya Kiteto ina changamoto kubwa sana kijiografia na hili tunakiri wazi na ndiyo maana hata bajeti ukiipeleka wakati mwingine inakutana na changomoto kubwa sana! Kwa hiyo, maelekezo yetu kama Ofisi ya Rais TAMISEMI ni kwamba niwashauru wananchi wa Kiteto hasa ndugu zetu wa Halmashauri Wakurugenzi na timu yake wahakikishe kwamba wanaweka mkazo wa kutosha katika kipindi hiki cha mpito kabla hatuaanza mwaka mpya wa bajeti. Wafanye udhibiti wa kutosha katika own source ili wakikusanya mapato ya ndani, japo kipindi hiki kilichobakia cha kumaliza mwaka wahakikishe kwamba wanakusanya fedha nyingi ili gari muda wote ziweze kufanya kazi na akina mama waweze kupata huduma. Lakini nikiri ni kweli Halmashauri ya Kiteto ni moja ya Halmashauri ambazo tunatakiwa tuziangaliye karibu. Ahsante!
MWENYEKITI: Ahsante. Mheshimiwa Emmanuel Papian.
MHE. EMMANUEL P. JOHN: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Kutokana na hali ya Kiteto ilivyo na wote mnafahamu, ningependa Mheshimiwa Waziri aniambie ni lini angeweza kufika Kiteto na kuzungukia hayo maeneo kama Waziri wa Ardhi, aweze kuona na kufanya mikutano ya hadhara ili aweze kuzungumza na wananchi wamweleze kero zao zaidi ya hapo?
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine, naomba Wilaya ya Kiteto ipimwe maeneo yote kwa maana ya kila mtu ajue kipande chake cha ardhi ili kuepusha ile migogoro inayoendelea kwa sababu leo tunaendelea, lakini bado kuna vuguvugu la migogoro inayoendelea. Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBANI NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza ameuliza ni lini tutazungukia Kiteto na kufanya mikutano ya hadhara. Naomba nimhakikishie tu kwa sababu zoezi hili la migogoro utatuzi wake utafanyika kwa nchi nzima na kama ambavyo Wizara imeshatoa kitabu cha migogoro, hivyo, muda unakapowadia katika suala zima la kuanza kuzungukia maeneo hayo na Kiteto pia tutafika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali lake la pili ameulizia ni lini sasa ardhi yote ya Kiteto itapimwa. Kama Waziri alivyotoa kwenye bajeti yake tumeanza na wilaya tatu ambazo ni wilaya za mfano ambazo tunakwenda kuanza nazo kazi na wameshaanza katika Mkoa wa Morogoro.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini suala la upimaji ni suala ambalo linagharimu pesa nyingi na kama tulivyoeleza wakati tunatoa maelezo wakati tunamalizia bajeti, tulisema kwamba, halmashauri pia zinapaswa kutenga pesa kiasi kidogo ili kuweza kuanza upimaji katika maeneo yake, wakati Wizara pia inajipanga katika kuhakikisha kwamba ardhi ya nchi nzima inapimwa.
MHE. EMMANUEL P. JOHN: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kutuona, kambi mbadala tuko wachache lakini tunajipanga kukuletea orodha yetu upange Baraza la Mawaziri vizuri hapo. (Kicheko/Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na majibu mazuri ya Waziri, lakini napenda kuuliza swali la nyongeza. Wilaya ya Kiteto tuna Kata za Songambele, Magungu, Dongo, Raiseli na Sunya zenye jumla ya vijiji karibu 21. Vijiji hivi vyote vilipangiwa kwenye Awamu ya II ya REA. Napenda kuuliza, ni lini tutapatiwa umeme katika awamu hii ili maeneo hayo yaweze kuwa na umeme? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali moja la nyongeza la Mheshimiwa Papian, Mbunge wa Kiteto, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza, niruhusu tu nisahihishe kidogo alichosema Mheshimiwa Mbunge, vijiji vilivyobaki siyo 21, tunakuongezea, viko 22 Mheshimiwa Mbunge. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo, napenda sasa nijibu kwamba vijiji vyote ambavyo amevitaja vya Songambele, Dongo, Raiseli pamoja na Sunga vitapata umeme kwenye REA Awamu ya Tatu inayoanza mwezi Julai.