Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Julius Kalanga Laizer (34 total)

Mapendekezo ya Mpango wa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali katika Mwaka wa Fedha 2016/2017
MWENYEKITI: Mheshimiwa Julius Kalanga Laizer, atafuatiwa na Mheshimiwa Emmanuel Papian, atafuatiwa na Mheshimiwa Jamal Kassim Ally, atamalizia Mheshimiwa Peter Serukamba!
MHE. JULIUS K. LAIZER: Mheshimiwa Mwenyekiti, nami nitumie fursa hii kuwashukuru wananchi wa Jimbo la Monduli kwa kuniamini na kunituma kuwa mwakilishi wao katika jengo hili lakini pia nimshukuru Mungu kwa kuendelea kutupa afya njema hadi muda huu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mpango ulioko mbele yetu kwa mtazamo wa kimaandishi ni mpango mzuri sana, kama ambavyo wamesema wengine, nchi yetu tunalo tatizo la kutekeleza Mipango, lakini mmekuja na kaulimbiu hapa kazi tu, tunataka tuwapime katika hili. Kumekuwa na excuses nyingi na ni Tanzania pekee duniani nchi inayofanya trial and error kwa miaka 54 ya uhuru kutafuta msimamo wa uchumi wa nchi na elimu ya nchi yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mara ya kwanza tulikuja na Kilimo Kwanza, tukaja na BRN imekwama, leo tumekuja na nyingine ya viwanda ambao umekuwa ni wimbo wa Taifa kila wakati, kila wakati tunabadilisha. Amekuja Waziri hapa wa Elimu amebadilisha elimu yetu mara nyingi, tunamshukuru Profesa Ndalichako amesema yeye anarudisha ile division na ni kweli ali-sign vyeti vyetu.
Katika hili lazima tuwe na misingi inayodhibiti elimu, haiwezekani kila Waziri anayekuja anaamua yeye aina ya elimu tunayotaka, lazima kuwe na mjadala unaoshirikisha wadau hasa Walimu na wenye professional hiyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni aina gani ya elimu ya watoto wetu tunahitaji! Leo tunataka tuagize wageni kutoka nje kwa sababu ya gesi na tunajua tuna rasilimali hii ya gesi, lakini hatujafanya investment ya kuwasomesha vijana wetu kuanzia ngazi ya chini kuhusu rasilimali tuliyonayo. Ni ajabu kwenye nchi tuna gesi ya kutosha, tuna madini ya kutosha, lakini hatuna wataalam wa kutosha kwa sababu hatuwajengei msingi wa elimu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo tunaendelea kufundisha kwamba binadamu aliwahi kuwa sokwe, ndiyo masomo tunayofundisha watoto wetu, watategemewaje! Kwa hiyo haiwezekani tukawa na nchi ya namna hiyo kwamba mpaka leo hatujui aina ya elimu tunayotaka kuwapa Watanzania wetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na hayo kama walivyosema wenzetu katika suala la elimu tunawashukuru, kwa hii kaulimbiu ya elimu bure. Wengine wamezungumza sana habari ya miundombinu, lakini nashukuru na niseme niipongeze Serikali kwa kuleta fedha ya chakula yote kwa wakati katika Jimbo la Monduli katika shule zote za sekondari kwa wakati. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, namshukuru sana Waziri Mheshimiwa Simbachawene, nilimpigia simu na nikawashukuru sana. Hili ni jambo jema sana, lakini walimu wetu hawana mahali kwa kulala na mnafahamu maeneo ya vijijini. Tatizo la mipango ya nchi yetu, wataalam wengi wanafikiri nchi yetu ni Dar es Salaam, nchi hii siyo Dar es Salaam peke yake. Mnapanga mipango kwa kuangalia pale Dar es Salaam siyo kweli! Yako maeneo ya nchi hii mnatakiwa mfike muangalie namna ya kujenga rasilimali za Taifa zinufaishe Taifa letu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mnasema mnafanya tafiti lakini kwenye Majimbo ya Wabunge hao wote hata wengine wanaowashangilia wanaotoka CCM hamjafika kwenye Majimbo yao. Sasa hizi term of reference, hizi sampling mnazozichukua mnachukulia Dar es Salaam, mnachukulia wapi! Nchi yetu ni kubwa lazima mfike muone maisha ya Watanzania.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunazungumza uchumi wa kati, lakini uchumi huu hau-reflect maisha ya kawaida ya Mtanzania na hau-reflect kwa sababu hatu-invest katika miradi midogo inayosaidia Watanzania wenzetu.
Leo mnazungumza viwanda vikubwa, lakini hamzungumzi habari ya mifugo ambayo kwato ni rasilimali, nyama ni rasilimali, ni malighafi ya kubadilisha, ngozi, maziwa, lakini sehemu kubwa ya wafugaji wa nchi hii, eneo kubwa ni la wafugaji pamoja na kwamba mnatufukuza kila mahali, lakini hamzungumzi habari ya kubadilisha mifugo kuwa kama zao la biashara, bali mnaangalia kama wanyama waharibifu tu, kila siku kuwahamisha, kila siku kuwafukuza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tusipotazama sekta ya mifugo kwa mtazamo wa kuona kama zao la biashara kama mazao mengine, hatutaweza kuwaendeleza wafugaji wetu. Hatutaweza kwa sababu lazima kama tunatafuta masoko kwa ajili ya mifugo, ni lazima wananchi wetu watapunguza mifugo wenyewe kwa sababu wanajua kuna masoko ya kwenda kuuza mifugo yao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nijielekeze katika suala lingine la wanyamapori. Ni kweli nchi yetu ina wanyama wa kutosha, lakini kama hatuzungumzi namna ambayo wananchi wataona hawa wanyama ni faida kwao, hatuwezi kuwa na wanyamapori na wataendelea kufanyiwa ujangili kadri iwezekanavyo kwa sababu hatujali wananchi wanaozunguka maeneo yale.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwananchi anatakiwa aone wanyama wale ni muhimu, pale ambapo mazao yake yameharibiwa na wanyama basi fidia inayolingana na madhara yaliyofanyika, ifanyike kwa wananchi, yule mwananchi atamlinda yule mnyama. Ikiwa yule mnyama atakuwa ni sehemu ya kuharibu rasilimali zake, akija mtu wa kuua, anasema mwache aue tu, ananipunguzia kero ya kuharibu mazao. Kwa hiyo, tutazame kwamba wananchi wanaozunguka maeneo yale waone faida ya kuwa na wale wanyama, watawalinda wala hatutahitaji kupeleka bunduki.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri wa Maliasili anazungumza habari ya wanyama Monduli, maeneo mengi Simanjiro, hakuna magari ya kulinda wale wanyama. Hivi unafanyaje doria kama huna magari, huna silaha, huna wataalam. Huu ni mchezo na ndiyo maana wanyama wataendelea kuuawa. Unapiga simu watu watoke Ngorongoro waje kufanya doria Mto wa Mbu pale baada ya wanyama kuuawa, baada ya masaa sita, huyo jangili anayekusubiri masaa sita ametoka wapi!
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, kama tunataka kulinda wanyama wetu ambao ni chanzo cha mapato ya nchi yetu, ni lazima tufanye investment ya kutosha, tuwe na magari ya kutosha katika kudhibiti ujangili, maana wananchi wetu wanatoa ushirikiano lakini unapiga simu, wale watu wa game controller wanakuja baada ya masaa manne, baada ya masaa matano kwa sababu ya tatizo la gari.
Mheshimiwa Mwenyekiti, liko gari moja Monduli pale la Misitu, linaangalia Longido, Kiteto, Simanjiro na maeneo mengine ya Tarangire, gari moja la misitu tena bovu. Hatuwezi kulinda wanyama wetu kwa sura hiyo, lazima kama tunadhibiti ujangili tuhakikishe tunapata vifaa vya kudhibiti suala la ujangili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ni suala la afya. Hatuwezi kuwa na Taifa linalozalisha rasilimali kama afya zao zina mgogoro. Katika maeneo mengi tatizo hili la afya ni kubwa sana kwenye nchi yetu, tunajenga majengo lakini hakuna dawa, tunajenga majengo lakini hakuna watumishi. Hivi Taifa gani, ni nguvukazi gani itakayofanya kazi ya kuzalisha kama hawana afya nzuri? Kila siku tunazungumza habari ya upungufu wa dawa, lakini ni story ya kila siku Serikali kusema tunaendelea, tunaendelea kuboresha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaomba kwa kweli katika zahanati hizi lazima tuboreshe afya za watu wetu ili waweze kushiriki katika shughuli za uzalishaji. Vinginevyo hatutaweza kuwa na maendeleo katika uchumi, katika viwanda, kama jamii yetu inayoshiriki nguvukazi haina afya bora ya kufanya kazi hizo ambazo zinapaswa kufanywa kwa wakati.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo langu la mwisho, ni suala la kukuza uchumi na kukusanya mapato ya Serikali. Tunavyozungumza habari ya kukusanya mapato lazima tudhibiti pia mapato hayo yatumike kwa njia inayostahili kufanyika. Tumeshuhudia, Mheshimiwa Waziri Mkuu alienda akavumbua makontena ambayo tunaambiwa yameibiwa karibu 2000 sijui na mia ngapi, lakini business as usual, story hiyo imekwisha, hatusikii wale wenye makontena wamekamatwa na wamefunguliwa kesi za uhujumu uchumi kwa kiwango gani! Kwa hiyo, tulikuwa tunafanya show ya kwenye TV. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jana imezungumzwa hapa habari ya mabehewa hewa, unawashughulikia wataalam, lakini yule Waziri aliyekuwa anahusika katika kudhibiti suala hilo umemwacha. Hatuwezi kuwa na nchi ya double standard, unawaonea hawa, unawaonea huruma hawa, haiwezekani! Kama Mawaziri wamehusika, lazima Bunge lisimamie Serikali, Mawaziri waliokuwa wanasimamia Wizara wakati uhujumu unafanyika, washughulikiwe na ndiyo maana reports zote zinazohusu uhujumu wa uchumi haziletwi kwenye Bunge hili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mmekuwa na story ya tokomeza imefichwa; mmetengeneza Tume ya Majaji, imefichwa; mmekuwa na ile inayoshughulikia Migogoro ya Wakulima na Wafugaji, imefichwa; mmetengeza Tume nyingi za kuangalia hiyo ya bandari na wizi huo, umefichwa kwa nini? Ni kwa sababu wenyewe mnahusika na hivyo hamuwezi kujifunua kwa sababu ya utaratibu huo. Kama tunataka tujenge nchi yetu kila mtu atendewe haki.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hatuwezi kuwafukuza tu Wakurugenzi, tukawaacha wanasiasa wanaoingilia kazi za kitaalam wao wakiwa salama. Ndiyo maana hawaogopi kwa sababu wanaagiza maagizo kwa mdomo, wataalam wanachukuliwa hatua, yeye anabaki salama. Tuanze na hao tuliowapa dhamana ya kusimamia Wizara hizo wakati uharibifu unatokea wao walikuwa wapi! Kama hatuchukui hatua hiyo tutakuwa tunacheza ngoma ambayo haina mwisho wake. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nikushukuru sana. (Makofi)
Mpango wa Pili wa Maendeleo wa Taifa kwa kipindi cha Miaka Mitano kuanzia mwaka 2016/2017 – 2020/2021
MHE. JULIUS K. LAIZER: Mheshimiwa Mwenyekiti, na mi nikushukuru kwa kunipa nafasi ya kuchangia mjadala huu uliopo mbele yetu. Nami nianze katika maeneo machache.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la kwanza tunazungumza habari ya mipango ya nchi yetu kwa miaka mitano na kama tunazungumza mipango tujue pia madhara ya mipango ambayo iliwahi kujadiliwa hapa Bungeni kwa waliokuwepo na haikufanya kazi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunakumbuka kwamba miaka minne iliyopita nchi yetu ilijadili habari ya Sheria ya Manunuzi hapa katika Bunge na ikaleta mvutano mkubwa sana. Leo tunasema sheria hiyo ni mbovu kuliko sheria zilizowahi kutokea kwenye nchi yetu na kila mtu analalamika. Kwa hiyo, tunapojadili suala hili ni vizuri tukaweka maslahi ya Taifa letu mbele tukajadili na mkapokea ushauri kwa ajili ya kujenga uchumi wa Taifa letu. Sheria mbovu hizi ambazo ziko kwenye Taifa letu ni majanga kwetu sisi wote. Kwa hiyo ni vizuri mkapokea ushauri na mkaufanyia kazi kuliko kutazama tu imetolewa na watu gani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la kwanza nitaanza na elimu. Leo tunazungumza kwamba tunaenda kutoa bei elekezi ya ada za shule katika shule za binafsi na hii ni kwa sababu ya fear, hii ni kwa sababu ya hofu ya miundombinu mibovu na taaluma yetu katika nchi yetu. Kwa hiyo, kwa sababu tumeona shule za Serikali zinafanya vibaya tunawalazimisha wawekezaji wengine nao wa subsidize ada zao ili wafanye vibaya tuweze kujishindanisha nao, ni vizuri Serikali ikaiga na kufanya competition kwa kufanya mambo yafuatayo katika elimu kwa miaka mitano:
Mheshimiwa Mwenyekiti, moja, kuboresha miundombinu na maslahi ya Walimu. Bahati nzuri tunaambiwa Rais alikuwa Mwalimu, Waziri Mkuu alikuwa Mwalimu, Mheshimiwa Profesa Ndalichako alikuwa naye ni Mwalimu na asilimia kubwa ya Wabunge hapa ni Walimu. Leo unazungumza habari ya Mwalimu anayetembea kilomita mbili, tatu kwenda na kurudi kila siku shuleni, hana nyumba anategemea mshahara wake alipe nauli, anategemea mshahara wake alipe nyumba ya kupanga kule shuleni, halafu akafanye vizuri, hawezi kufanya vizuri! Kama tumeshindwa kujenga nyumba za Walimu tuwape Walimu fedha kwa ajili ya kupanga maeneo ya kuishi, tunawalipa shilingi ngapi? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ni madarasa na nyumba za watumishi hakuna katika shule nyingi za vijijini, mnategemea huyo mwanafunzi atafaulu kwa namna gani? Kwa hiyo, ni vizuri tukawa na mipango inayolenga kuboresha elimu yetu tukajishindanisha na shule za private kuliko kuwaambia shule za private washushe ada ili nao wafanye vibaya tuweze kujiona kwamba wote ni kundi la wajinga, haiwezekani! Ni wajibu wa Serikali kutoa elimu kwa wananchi wake, wahisani hawa wanatusaidia tusiwa-discourage kwa kuwalazimisha kufanya jambo ambalo hawawezi kufanya kwa ajili ya kuendeleza elimu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo langu lingine ni suala la mifugo, simwoni Mheshimiwa Waziri lakini nilitamani awepo, kwa sababu sisi ni wafugaji na sehemu kubwa ya Watanzania ukiwaacha wakulima ni wafugaji. Ukienda Mji wa Kajiado, Kenya asilimia 80 ya mapato yao yanatokana na mifugo na mifugo hiyo inatoka Tanzania, inatoka Shinyanga inakuja Arusha inasafirishwa inaenda Namanga inaenda Kenya. Kwa nini sisi tunashindwa kujenga viwanda kwa ajili ya ku-accommodate bidhaa zinazotokana na mifugo? Tunategemea kujenga uchumi wa viwanda kwa kutegemea wafadhili, lakini hatutaki kujenga viwanda vinavyo-accommodate bidhaa zinazozalishwa na wananchi wetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunayo maziwa, nyama, na ngozi, lakini hatuna viwanda vya namna hiyo. Nawaambia mwaka 2020 tutakuja kuzungumza habari ya utekelezaji wa mipango hii kwa asilimia 10 au asilimia 15 kama hatutakubaliana kuhakikisha bidhaa zinazozalishwa na wananchi wetu zinajengewa mazingira ya kupata soko la uhakika ili waweze kuzalisha zaidi. Kwa hiyo, tutashauri kuwepo na viwanda vya bidhaa zinazotokana na mifugo, ngozi, nyama na maziwa maeneo ya shinyanga, Arusha ili kudhibiti upelekaji wa mifugo yetu nchini Kenya na kwenda kuwanufaisha watu wengine.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mji ule unaishi kwa ushuru tu wa mifugo, lakini sisi hata soko tu la kuuza mifugo hatuna, hata kiwanda cha maziwa hatuna, halafu tunazungumza nchi ya viwanda!
Mheshimiwa Mwenyekiti, ili tuwe na viwanda vilevile ni lazima tuwe na miundombinu, ardhi tumetengeneza mazingira gani kwa ajili ya kufanya uwekezaji. Kwa hiyo, tunaposema mnapiga kelele hamna mipango mnatu-challenge lakini ukweli ndiyo huo! Huu siyo Mpango wa kwanza kuletwa na Serikali, umeshaletwa miaka mitano, lakini leo tukiwauliza mmetekeleza mipango ile kwa asilimia ngapi hakuna! Sasa tukisema hata huu hamtekelezi mnasema tunawapinga, tunataka mtu-prove kwamba tunawapinga bure kwa kufanya utekelezaji wa mipango hii mliyoleta kwa asilimia angalau themanini, kitu ambacho hakiwezekani, hamuwezi kufanya kwa sababu mnapenda kuandika lakini hamtaki kuweka mipango ya kupata fedha ya kufanya kazi hiyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo ni muhimu katika suala la viwanda, leo tunazungumza habari ya viwanda, lakini hatusemi kwa nini viwanda vilikufa, hatusemi kwa nini tulikwama na tumeweka mechanism gani ya kuendelea hapa. Sisi wenyewe ni mashahidi, katika watu wanaouwa viwanda nchi hii ni Serikali kwa kuwa-discourage wawekezaji wa ndani na kuwakumbatia wawekezaji wa nje. Maeneo mengi watu wanalalamika, mkulima anazalisha alizeti, unaweka kodi kwenye uzalishaji wa mafuta, lakini mafuta yanayotoka nje yanaingia na zero, halafu mnategemea mtu alime alizeti, mtu atengeneze kiwanda cha alizeti kama anaweza kuagiza mafuta nje bila kodi, halafu tunasema tunazalisha! Hatuwezi kuwa na viwanda vya namna hiyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Kenya leo tunazungumza wao wameweka asilimia arobaini ya manunuzi yao yote lazima yafanyike na local contractor ndani ya nchi yao, sisi tunasema bilioni mbili tu international competition. Hatuwezi kujenga nchi kama hatuwa-encourage wawekezaji wa ndani kufaidi uchumi wa nchi yao. Ndiyo maana leo tunawaambia Kiwanda cha Urafiki kinakufa kwa sababu asilimia hamsini na moja ni ya China, asilimia arobaini na tisa ni Serikali na Wachina wanataka kubadilisha kile kiwanda cha Urafiki iwe ni sehemu yao ya kuingiza bidhaa kutoka China na kufanya dumping katika nchi yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaiomba Serikali iangalie kiwanda cha Urafiki. Mheshimiwa Waziri tulikuambia kwenye Kamati na narudia kusema kwa kweli tunaomba Wabunge tuisimamie Serikali kwa sababu kuna hujuma na kuna ufisadi mkubwa katika Kiwanda cha Urafiki, kwa sababu Wachina wamepewa asilimia hamsini na moja, Serikali inashindwa kununua asilimia tatu tu, ili iwe na say katika kiwanda cha Urafiki. Hatuwezi kuendesha nchi yetu kama viwanda tulivyonavyo sisi tunaviua wenyewe kwa sababu tunaogopa kuwashughulikia watu waliotufikisha hapa, haiwezekani!
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Bunge katika hili tukubaliane katika mambo ya msingi kwa ajili ya Taifa letu, acheni ushabiki wa kivyama, kila mtu ameletwa hapa kwa maslahi ya wananchi wake na tuna wajibu wa kujibu tulichokifanya tukiwa huku Bungeni, hii ni nchi yetu sote yakiwa mazuri ni ya kwetu, yakiwa mabaya ni yetu sisi sote. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini lingine katika hilo suala la kiwanda cha Urafiki; tumeenda kiwanda ni kichafu, China wanasema wanataka kukifanya soko walete vitu vyao hapa wamalize wao, sisi tubaki kama watazamaji na bidhaa feki, ndiyo maana leo zimeingizwa simu chafu na simu feki nchini. Badala ya kuzungumza ni Sheria gani inaruhusu kuingiza tunazungumza kwenda kuwanyang‟anya Watanzania zile simu! Tudhibiti kwanza uingizwaji wa bidhaa feki, lakini siyo kuja kumuumiza mwananchi ambaye uliingiza bidhaa halafu yeye amenunua unamhukumu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo langu la mwisho ambalo nataka kusema katika hili, ni suala la Wanyamapori, kwa sababu tunazungumza habari ya utalii, lakini hatuzungumzi habari ya mwananchi anayekaa na wale wanyama anafaidi nini katika rasilimali ya Taifa lake. Leo wanyama wanavamia mashamba, leo wanyama wanavamia watu, hivyo wananchi hawaoni faida.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Waziri katika hili na katika Bajeti yake, kwa kweli tuoneshe mazingira ya kwamba, wananchi wale wanaokaa karibu na Hifadhi za Taifa wananufaika zaidi katika mapato yanayopatikana ili wao wenyewe washiriki kulinda rasilimali za wanyama wale waliopo kwa ajili ya maslahi ya Taifa letu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama wananchi wenyewe hawaoni faida ya wale wanyama wanaona kama ni kero, kwa kweli tutaendelea kupata shida na Hifadhi zetu hazitakuwa na tija kwa sababu wananchi wenyewe hawaoni manufaa ya yale maeneo ambayo wao yanawazunguka kwa ajili ya mapato ya maisha yao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini jambo la mwisho ni viwanda. Tumezungumza habari ya viwanda vyetu nini kiliviua. Mfano, tulikuwa na Kiwanda cha Nyama Simanjiro, lakini siasa iliua kile kiwanda, watu mia sita wakaacha kazi kwa sababu siasa ziliingia, kiwanda kikaonekana mtu ana interest zake za kisiasa ikaua. Kama hatutadhibiti mwingiliano wa siasa na rasilimali za Taifa letu kwa kweli hatuwezi kusonga mbele na siyo mashindano ya kutumbua majipu iwe ni mashindano ya kuwaelekeza wananchi wetu waende katika maslahi na haki. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kila mtu anataka kumfukuza mtu kazi, tunatengeneza Taifa la waoga ambao watumishi wetu hawatafanya kazi kwa uhuru na ndiyo tunawategemea kuzalisha katika nchi yetu. Wabadhilifu washughulikiwe lakini tusishindane kufukuza watu kazi, tushindane kuwaelimisha watu wetu, tusiwaoneshe dunia kwamba Watumishi wa Umma na Wataalam wote ni wezi. Tukijenga sura ya Taifa letu hivyo, tutaonekana watu wote ni wendawazimu. Haiwezekani siyo kila Mtumishi wa Umma ni mwizi kwenye nchi yetu, siyo kweli!
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa kila mtu anafukuza wengine wanafunga kiwanda huku, mwingine wanafunga geti huku, mwingine anafanya hivi huku, what kind of that nchi? Utawala wa Sheria uko wapi katika hilo? Tunatamani nchi yetu watumishi wapewe nafasi ya kufanya kazi na kuonesha matumizi ya taaluma zao walizosomea ili nchi yetu isonge mbele. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hakuna Mbunge aliyeiandika hii bajeti, wameandika wataalam, sasa kama tunawa-discourage Mawaziri wanasema tunarekodiwa, wanaogopa kusema hii bajeti haitoshi nchi haiwezi kusogea. Kwa mfano ameonesha mtu mmoja, Waziri wa Ardhi ameonesha kuthubutu na nampongeza na nitaendelea kumpongeza kwa kazi nzuri anayoifanya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tukiwa na watu wachache wanaothubutu kuwasaidia Watanzania kwa sura hiyo tutaacha alama ya utumishi kwenye Taifa letu. Kwa nini leo tuzungumze habari ya maadhimisho ya Sokoine, habari ya Nyerere kwa nini sisi tusiache legacy kwenye Taifa letu, tukaacha siasa tukaenda kwenye mipango inayotekelezeka kwa ajili ya kuisaidia nchi yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama hatutajenga utaratibu huo wa kupokea ushauri wa kitaalam kwa ajili ya maslahi ya Taifa letu tutaendelea kusema haya na nawaambia hamtatekeleza kama hamtaweka priority ya vipaumbele vichache na kutoa vikwazo vilivyoua viwanda vyetu na kuwapa wataalam nafasi ya kutumikia Taifa lao, kuliko kufanya kila jambo siasa. Kama kuna mambo ambayo Rais anasema yanawezekana na hayawezekani tumwambie hayawezekani professionally, hili haliwezekani! Twende kwenye yale mambo ya msingi ambayo hata taaluma inaruhusu kufanyika. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hatuwezi kusema tunajenga reli, tunasema tunajenga viwanda, tunatoa elimu bure kwa wakati mmoja kwa uchumi wa nchi yetu ambayo tunasema tunakusanya trilioni moja kwa mwezi, mara miezi kumi na mbili, trilioni kumi na mbili, lakini tunataka tujenge reli ya trilioni 300 na kutoa elimu kwa trilioni tano mpaka sita, hiyo hela itatoka wapi? it is impossible tuwe na priority ambazo tunatekeleza, tukasema jamani we have done this, kuliko kuwa na vipaumbele mia mbili halafu Wabunge hapa tunapiga makofi. Tunawaambia Serikali tengeni vipaumbele vichache ambavyo vinatekelezeka kwa ajili ya maslahi ya Taifa letu.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 20 16/2017 - Ofisi ya Rais, TAMISEMI, Utumishi na Utawala Bora
MHE. JULIUS K. LAIZER: Mheshimiwa Mwenyekiti, nami nitumie nafasi hii kukushukuru, kwa kunipa nafasi ya kuchangia katika Wizara hii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nianze kujielekeza katika elimu. Ni kweli kwamba tumeanzisha programu ya elimu bure; na kimsingi katika hili tunajua kabisa na ndiyo ilikuwa Sera ya CHADEMA kwamba inaenda kuwaondolea wananchi adha mbalimbali. Kuna maeneo ambayo tunataka kushauri na mkubaliane na sisi kama kweli tunataka kuboresha elimu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza ubaguzi uliopo katika mfumo wenyewe. Waraka uliotolewa ulionesha kwamba shule za day hawaruhusiwi kupata fedha za chakula kwa sababu wanafunzi wanakuja na kurudi nyumbani. Vilevile tufahamu kwamba ni mfumo ndiyo unabagua wanafunzi. Hakuna mwanafunzi anayependa kukaa day, wenzake walale boarding wasome usiku na watoto wa kike waende nyumbani wakaokote kuni. Ni mfumo! Sasa anapata hasara ya kukaa day, lakini bado anaenda shuleni mchana, hapati fedha ya chakula, lakini shule za bweni mnawapa fedha za chakula.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Jimbo langu la Monduli, ni kweli shule zetu zote ni bweni, lakini ziko shule ambazo ni za day katika mazingira magumu. Tuache ubaguzi katika suala hilo, kama tunatoa hela za chakula, tutoe pia kwa wanafunzi wa day wakiwa shuleni.
Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili, tatizo la Shule za Sekondari za Serikali, siyo ada. Siyo shilingi 20,000, naamini wote tunafahamu hata Waziri wa elimu anafahamu. Tatizo siyo shilingi 20,000 kila mzazi angaweza kutoa shilingi 20,000. Tatizo ni mzingira hasa majengo, madarasa, madawati, vitabu, maabara na vitu vingine vinavyosaidia kuboresha elimu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama sisi tuanenda kujificha kwenye kivuli cha shilingi 20,000 hatujawasaidia watoto wetu. Tutakuwa tunazalisha, kwamba tumeingiza watoto 2,000 darasani watatoka 2,000 lakini empty. Kwa sababu tunataka kuboresha kweli, tuache kwenda kujificha kwenye shilingi 20,000, twende katika kuboresha miundombinu ya wanafunzi, maabara na mazingira mengine yanayosaidia mtoto aweze kufanya vizuri, pamoja na vitabu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili, tunafahamu kabisa kada ya Walimu ina mazingira magumu sana ya kufanyia kazi. Shule nyingi za kijijini na Wabunge wengi wanatoka kijijini watakubaliana nami katika hili. Walimu wanatembea kilometa nne mpaka tano kwenda shuleni, halafu wanatumia nauli shilingi 2,000, shilingi 3,000 kila siku kwenda shuleni. Wakati huo huo anapanga mjini kwa sababu kule vijijini hata nyumba ya kupanga hakuna.
Mheshimiwa Mwenyekiti, halafu tunasema atumie mshahara wake kulipa nauli, atumie na kupanga nyumba, halafu unategemea wakati huo huo afanye vizuri, haiwezekani! Kama kweli tunataka kuboresha elimu yetu ni vizuri tukajali mazingira ya walimu kwa kujenga nyumba za Walimu katika shule zetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hata wakati Waziri wa Elimu anawasilisha hapa, alisema kwamba ni kwa namna gani mwalimu anaweza akakaa kilometa tano au kumi kutoka shuleni akaondoka asubuhi nyumbani halafu akafanya vizuri na watoto wakafaulu. Tusiangalie watoto tu, lakini tuangalie mazingira ya watumishi wetu wanaofanya kazi katika maeneo hayo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine nataka tukubaliane kama Bunge. Kama tunasema tunawapima watumishi wa umma kwa OPRAS, tuwapime Mawaziri nao kwa mfumo huo huo. Kabla hatujajadili bajeti yoyote katika miaka inayokuja, ni lazima Mawaziri na kila Wizara iwasilishe imetelekeleza kwa kiwango gani bajeti tuliyoipitisha kwa mwaka uliopita. Hii itatusaidia sisi Wabunge kuacha kupiga kelele hapa, kama tunapitisha bajeti ya bilioni tano, halafu Serikali haipeleki fedha, halafu tunakuja kumsulubu Mheshimiwa Waziri hapa, hakuna sababu ya kukaa kupitisha bajeti ambayo hatuwezi kuitekeleza. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tatizo kubwa kwenye nchi yetu ni mfumo wa upelekaji wa fedha katika miradi ya maendeleo ya wananchi, ndiyo hiyo tu! Sasa kama tunapitisha bajeti lakini hatupeleki fedha, ni kila siku tunasigana hapa maswali, miongozo kwa sababu kile ambacho tumetarajia kupata kwenye Majimbo yetu, hatuyapati. Ni lazima tupige kelele kwa sababu hatujapata. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naamini kama Serikali itapeleka fedha kwa wakati kwa kiwango kile hata kama ni kidogo, hakuna sababu ya Bunge kupoteza muda. Tungekuwa tunasema hapa tunashukuru kwa sababu tumetekelezewa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama hamjatekeleza, tutasema hamjatekeleza. Hii ni kwa sababu Serikali haipeleki fedha. Kwa hiyo, nashauri kila Wizara, wakati mwingine inavyopelekewa fedha kuwe na mgawanyo sawa wa kupeleka fedha wakati fedha zinapokusanywa. Siyo Wizara nyingine zinapewa, nyingine hazipewi. Bila hivyo, miradi yetu itaendelea kuwa haifanyi kazi vizuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ni wanyapori katika maeneo yanayopakana na Hifadhi za Taifa. Hili niseme kwa masikitiko makubwa. Katika Jimbo langu mpaka sasa, tembo wanavamia kila siku zaidi ya heka kumi ya mazao ya wananchi, lakini haturuhusiwi kuwapiga wale wanyama. Baadaye nataka Waziri wa TAMISEMI kwa sababu tunasema tunahitaji kuwa na chakula, lakini wanyama wale wanaharibu sana mazao na wakati mwingine tunasema Serikali ishiriki basi kufanya patrol ya kuwarudisha wale wanyama kwenye park ili wananchi wetu waendelee kufanya kazi zao kwa amani, lakini haifanyiki hivyo!
Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati mwingine nitahamasisha kwamba ni bora Wabunge wanaotoka katika maeneo hayo tuungane kuwakataa wale wanyama, kama ninyi Serikali hamwezi kutusaidia kuwarudisha katika park hizo, badala ya kuwaacha waharibu mazao ya wananchi wetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hakuna magari; hakuna askari, kila siku iendayo kwa Mungu kuanzia mwezi wa tatu katika Jimbo langu, heka kumi zinaliwa na wanyama. Tembo wanavuruga, wanavunja. Ukienda Halmashauri hakuna gari. Kwa hiyo, tunaomba katika hilo mtusaidie ili wananchi wetu, jasho lao lisiende bure.
Mheshimiwa Mwenyekiti, maji. Mimi katika hili kwa kweli nimshukuru sana Waziri wa Maji kwa kufika Monduli. Baada ya kuingia kwenye Wizara hiyo, tumepata angalau shilingi milioni 700 kwa ajili ya kupunguza madeni ya wakandarasi na sasa kuna maeneo mengine wameanza kupata maji. Nakushukuru katika hilo kwa sababu kwa kweli miradi hiyo imesimama zaidi ya miaka miwili. Mwaka 2015 hatujaletewa hata shilingi ya maji. Umeonesha nia, basi naendelea kukusitiza kwamba bado tunahitaji wanachi wetu wapate maji kwa wakati ambao bajeti yao imeshapitishwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili katika hilo la maji, naomba nishauri Serikali ifanye kama inavyofanya Road Fund. Ukiangalia Wizara ya Maji yenyewe ni centralized, kwamba wanapanga Wizarani bajeti, halafu wanapeleka kwenye Halmashauri. Kwa nini isipangwe kama inavyopangwa miradi mingine fedha zikaanzia kule chini halafu zikaenda zikafanya hivyo? Kwa sababu inaonekana wakati mwingine hata Halmashauri hatujui tunapangiwa nini katika Wizara ya Maji kwa sababu imefanyika centralization.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ni suala la miundombinu. Tunaona hili ni tatizo kwamba kila mtu analalamika miundombinu, lakini ni kweli barabara zetu zimeharibika, hazipitiki. Sasa unakuta katika Halmashauri barabara za vijijini hazipitiki; zahanati hazipo, akina mama wanajifungulia njiani, wengine wanakufa kwa sababu hakuna miundombinu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa kama dispensary zetu tunasema katika vijiji 12,500; vijiji 4,000 tu ndiyo vina dispensary, halafu barabara hazipitiki, kwa nini watu wasife njiani? Watakufa tu! Kwa hiyo, tunaomba tuzingatie kabisa na ili tusaidie wananchi wetu ni lazima angalau miundombinu hiyo iwe imeboreshwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niende kwenye suala la utawala bora. Ni kweli mnasema na sijamwona kaka yangu Mheshimiwa Lusinde, nataka nimwambie, Watanzania wote wanalipa kodi bila kujali vyama vyao na kinachopeleka maendeleo ni kodi ya wananchi na siyo kodi ya mtu mmoja mmoja wala Serikali iliyoko madarakani. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine mnazungumza habari ya utawala bora, na mimi niseme, mnasema sisi tunataka tuuze sura kwenye tv, siyo kweli! Serikali ilikuja hapa ikasema sababu mbili, kwa nini hawataki kurusha live.
Moja, wakasema gharama. TV za private wakasema tutaonesha sisi kwa gharama zetu. Jambo lingine mkasema watu hawafanyi kazi; lakini niwaulize, hivi wakati wa kufanya kazi ni wa asubuhi wakati wa Bunge au saa hizi wakati kila mtumishi ametoka kwenye Ofisi yake amekwenda nyumbani?
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama kweli hamna nia ya kudhulumu Bunge hili na kuzuia Watanzania wasijue tunachojadili, badilisheni kipindi cha Maswali na Majibu kiwe giza, halafu kipindi hiki cha mjadala ambao wananchi wanataka kuona kiwe live, kama kweli hamna nia mbaya. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mmeamua kujificha kwenye Kipindi cha Maswali na Majibu, kwa sababu kila mtu anauliza swali. Tunataka mijadala hii Watanzania wajue Bunge lao linajadili nini kuhusu maslahi ya maisha yao na mustakabali wa Taifa lao. Kwa nini tunaficha? Leo tumeeleza bajeti nzuri ya viwanda hapa, tunataka Watanzania waone Bunge linasema nini kuhusu habari ya viwanda. Tunaficha nini?
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli hakuna empire yoyote inayotakiwa misingi yake itikiswe. Serikali ya CCM imetikiswa kwa kutumia Bunge hili. Hawako tayari kuendelea kuona likitikiswa. Tusema hivyo! Huo ndio ukweli! Mnaficha ili wakati fulani msionekane kwamba mmeendelea kuonesha udhaifu kama ambavyo Wabunge wanaendela kusema hapa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, namshukuru sana Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa mambo makubwa ambayo amefanya na kwa kipindi kifupi tu. Miaka zaidi ya 30, ameturudishia ekari zaidi ya 12,000 kwa wananchi wa Monduli. Tunakushukuru na tunakuomba uendelee kuyamalizia yale, tunajua kuna figisufigisu zinafanyika lakini tutahakikisha kwamba mashamba yale yote yanarudishwa.
MHE. JULIUS K. LAIZER: Mheshimiwa Mwenyekiti, siungi mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Nishati na Madini kwa mwaka wa fedha 2016/2017.
MHE. JULIUS K. LAIZER: Mheshimiwa Naibu Spika, namshukuru Mungu kwa kupata nafasi ya kuchangia hotuba hii kwa maandishi. Matatizo ya REA phase II katika Jimbo langu na nchi nzima ni umeme kutofika kwenye taasisi nyingi katika maeneo ambayo umeme umepita na transformer kuharibika kwa muda mfupi baada ya kufungwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, suala la pili ni ombi la upatikanaji wa umeme wa REA phase III katika maeneo ya Kata ya Monduli Juu, Mfereji, Moita, Naalarami, Migungani, Majengo, Esilalei, Mswakini, Makuyuni na Lashaine.
Mheshimiwa Naibu Spika, tatizo lingine ni ubovu wa Sheria za Madini ambapo katika maeneo yenye mchanga na kokoto, watu wanaenda kukata leseni ya madini ofisi za madini bila kupitia vijijini. Kuna uharibifu wa mazingira unaosababishwa na uchimbaji wa kokoto katika Kata ya Nanja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Nishati na Madini kwa mwaka wa fedha 2016/2017.
MHE. AIDA J. KHENANI: Mheshimiwa Naibu Spika, kutokana na umuhimu wa Wizara hii ya Nishati na Madini na kutokana na changamoto mbalimbali zinazojitokeza katika Wizara hii hasa katika Mkoa wa Rukwa, napenda kuchangia mambo yafuatayo:-
Suala la TANESCO kuwadai wananchi pesa za nguzo. Suala hili limekuwa likileta shida kwa wananchi wetu hasa pale wanapohitaji huduma hii muhimu ya nishati katika Mkoa wa Rukwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, elimu kwa watu walio karibu na nguzo. Suala hili limekuwa na changamoto nyingi, hasa katika Mkoa wangu wa Rukwa. Naishauri Serikali kutoa elimu kwa wananchi wetu wajue athari zinazoweza kujitokeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, kukatika kwa umeme bila taarifa. Suala la kukatika kwa umeme katika Manispaa ya Sumbawanga limekuwa likiwaathiri sana wafanyabiashara, hasa pale wanapokosa taarifa ya kukatika kwa umeme na kuleta athari kubwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, suala la maeneo mengi kukosa umeme. Katika Mkoa wa Rukwa na Wilaya zake kuna shida kubwa ya kukosa umeme mpaka leo. Je, Serikali au Wizara ina mkakati gani wa haraka wa kupeleka umeme katika Wilaya ya Nkasi, Wilaya ya Kalambo na Sumbawanga Vijijini?
Mheshimiwa Naibu Spika, ni vigezo gani vinatumika katika kufikisha umeme vijijini, REA III? Kutokana na kutambua kuwa Mkoa wa Rukwa uko Tanzania, lakini ni maeneo mengi katika mkoa huu wananchi wengi hawajafikiwa wala kuwa na dalili zozote za kupelekewa umeme!
Mheshimiwa Naibu Spika, gharama halisi za mtu kuvuta umeme. Kumekuwa na hali ya manung‟uniko kwa wananchi wanapokuwa wanahitaji kuingiza umeme katika nyumba zao, wamekuwa wakiambiwa bei tofauti tofauti. Je, ni kiasi gani wananchi wanapaswa kutoa?
Mheshimiwa Naibu Spika, suala la kukatika kwa umeme mara kwa mara katika Manispaa za Sumbawanga na Nkasi. Hali hii imekuwa ikijitokeza mara kwa mara, je, Wizara inatambua suala hilo na je, kuna utaratibu wowote wa kumaliza tatizo hilo?
Mheshimiwa Naibu Spika, suala la madini yanayopatikana Sumbawanga. Napenda kujua kama Wizara inajua kuwa kuna madini yanapatikana Manispaa ya Sumbawanga? Kama ndivyo, wameweka mkakati gani? Kwani mpaka sasa mambo yanayofanyika ni kinyume kabisa na umiliki wa vitalu na madini yetu yanakwisha.
Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa Unaokusudiwa Kutekelezwa na Serikali Pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018
MHE. SUSAN L. KIWANGA: Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na mambo mengine naleta mapendekezo ya masuala kadhaa yakiwemo na ya kwenye Mpango wa Serikali wa mwaka 2017/2018.
Mheshimiwa Naibu Spika, Uanzishwaji wa Mkoa Mpya wa Ulanga kama RCC ya Mkoa wa Morogoro ilivyoridhia kuanzishwa kwa Mkoa wa Ulanga wenye Wilaya tatu, Kilombero, Ulanga, Malinyi. Pia napendekeza mpango uweze kupendekeza kuanzishwa Wilaya ya Mlimba ambapo utakapotangazwa Mkoa wa Ulanga uwe na Wilaya nne; Ulanga, Malinyi, Kilombero na Mlimba ili kusogeza huduma kwa wananchi. Pia mpango uoneshe kuwepo kwa Halmashauri ya Wilaya ya Mlimba ambapo mchakato wa upatikanaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Mlimba umeshakubaliwa na Baraza la Madiwani la Kilombero na hatua zinaendelea kufanyika.
Mheshimiwa Naibu Spika, napendekeza mpango ueleze ujenzi wa barabara ya kiwango cha lami ya Ifakara hadi Mlimba kilomita 153, pia Mlimba – Madeke – Njombe kuunganisha mikoa hiyo miwili. Umuhimu wa barabara hiyo unatokana na kupatikana kwa kilimo cha mpunga na shamba la uwekezaji la KPL Mngeta. Pia mradi mkubwa wa umwagiliaji wa Njage, kilimo cha miwa Ruipa na ujenzi wa kiwanda cha sukari, upatikanaji wa mazao ya biashara kama cocoa, ufuta, ndizi, matikiti na kadhalika.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia umuhimu wa barabara hiyo ni kumrahisishia mwananchi kusafirisha mazao, kwenda kufuata huduma za matibabu hasa kwa mama mjamzito na mtoto kwani hospitali ya Wilaya iko umbali wa kilomita 263 hivi na barabara haipitiki kipindi chote cha mwaka.
Mheshimiwa Naibu Spika, Mpango uingize upatikanaji wa maji katika Mji wa Mlimba ambapo Serikali ione umuhimu wa kusambaza maji yanayopatikana kwenye mito mikubwa iliyoko Mlimba kama vile Mto Mpanga na Mnyela baada ya kuchimba visima ambavyo vingi havina maji ya kutosha.
Mheshimiwa Naibu Spika, Mpango uweke ujenzi wa vituo vya afya kila Kata na hospitali ya Wilaya Mlimba. Pia ujenzi wa kituo cha Polisi Mlimba na Mahakama za Mwanzo katika Kata 16 za Jimbo la Mlimba. Vile vile Mpango uzingatie ajira za Walimu, watumishi wa afya hasa vijijini. Ahsante.
Hotuba ya Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018.
MHE. JULIUS K. LAIZER: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa wananchi wa Wilaya ya Monduli katika Kata ya Makuyuni na Esilalei wameunga mkono sera ya kuwa na kituo cha afya kwa kila kata na wamefika mahali pazuri kwa nguvu na michango yao, tunaomba Wizara itazame namna ya kuwa-support.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia, tuna tatizo la chumba cha upasuaji katika wilaya yetu, tunaomba Wizara itoe namna ya kusaidia ujenzi wa chumba cha upasuaji.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. JULIUS K. LAIZER: Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote, namshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutujalia afya njema sisi sote tulioko hapa na kuendelea kutupa pumzi ya uhai pamoja na kuwashukuru wananchi wa Jimbo la Monduli walioniamini kwa kunipa kura za kutosha kuingia katika Bunge hili kwa ajili ya kutetea masilahi yao. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nampongeza Mheshimiwa Waziri kwa maelezo yaliyoko kwenye kitabu chake. Haya ni maelezo ambayo na ninyi mtakuja kukumbuka kwamba mmesaliti nafsi zenu kwa taarifa hizi ambazo mmeziandaa. Historia ya dunia inaonesha kwamba katika vita ambavyo ni vikubwa siku zote, ni vita vya ardhi; na katika maeneo ambayo kwenye nchi yetu tumekosea ni katika ardhi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tumefanikiwa kudhibiti kabisa suala la ukabila na masuala mengine ambayo yangeweza kuleta mgongano katika Taifa letu, lakini katika vita ambavyo vitakuwa vikubwa kwenye nchi yetu ni suala hili la ardhi kama Serikali haitachukua hatua sasa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia taarifa ya Wizara, hakuna mahusiano kati ya Wizara ya Ardhi na Wizara ya Maliasili na Wizara ya Mifugo na Kilimo. Nataka tu nitoe tahadhari kwa Waziri pia wa Maliasili kwamba asitutafute ugomvi wa wafugaji. Kauli ambazo zimeendelea kutolewa kuonesha kwamba kila siku wafugaji ni wavamizi wa ardhi ambayo mmetukuta na wanyama hatutaweza kukubali leo wala kesho. Kama tukishindikana kwenye Bunge, tutarudi kwa wananchi wetu na hatuko tayari. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, wananchi wetu wamechomewa maboma Ngorongoro na maeneo mengine kwa sababu ya tatizo la ardhi. Ni wajibu wa Serikali kutatua matatizo yaliyopo badala ya kwenda kuwaumiza wananchi wetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, unaleta taarifa halafu hupewi bajeti. Tuna vijiji 12,000 zaidi nchi nzima, lakini mna mpango wa kupima vijiji 200 katika mipango ya matumizi bora ya ardhi. Tunapeleka wapi Taifa? Tunayo Ripoti ya Tokomeza iliyoletwa kwenye Bunge lililopita, sisi hatukuwepo, inayoonyesha namna gani ambavyo wananchi wamedhulumiwa na kupewa majanga makubwa kwa sababu ya maliasili na Mheshimiwa Waziri anadiriki kusema eti ile ripoti ilikuwa ya uongo. Halafu tunanyamaza, tunasema bajeti ipite. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Wabunge tusikubali bajeti hii ipite mpaka Waziri atuambie anahitaji bajeti kiasi gani kwa jili ya kutatua migogoro yote ya ardhi iliyoko kwenye nchi yetu. Hii ndiyo Wizara ambayo tukifanikiwa kuiweka vizuri, nchi yetu itakuwa na utulivu mkubwa sana, hii ndiyo Wizara ambayo tukifanikiwa kutatua migogoro ya wakulima na wafugaji, nchi yetu itakuwa na amani muda mrefu, hii ndiyo Wizara ambayo tukifanikiwa kuidhibiti vizuri, nchi yetu itakuwa na amani katika suala la wanyamapori na wananchi wake. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ili kila mtu afaidi katika Taifa hili, ni lazima kila mtu awe na haki ya kutumia ardhi kwa sababu hakuna maeneo mengine tunaweza kuwekeza bila kutumia ardhi. Mheshimiwa Waziri anatuletea shilingi bilioni 20 sijui, eti kwenye Wizara ambayo ni sensitive ambayo sisi wote ni watumiaji wa Wizara hiyo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka Mheshimiwa Waziri atakapokuja pamoja na hili suala la Mheshimiwa Rais kuhusu watu kuogopa, atuambie anahitaji bajeti ya kiasi gani ili atatue migogoro yote ya ardhi iliyoko nchini kati ya wakulima na wafugaji; kati ya wanyamapori na wananchi; ili matatizo haya yafike mwisho, pamoja na bomoa bomoa ambayo inaendelea kwenye nchi nzima. Kama bajeti ya Wizara haioneshi future ya matatizo hayo kwa nchi yetu, tunaelekea wapi?
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka Mheshimiwa Waziri anisaidie mambo matatu; kwanza atuambie, kwa nini benki za Tanzania hazithamini hati miliki za kimila katika mikopo kwa wananchi wetu na ni hati za Serikali? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine namuomba Mheshimiwa Waziri anisaidie kuniletea Kamishna wa Ardhi Monduli, kwa sababu kuna mashamba matatu ambao wengine walikuwa ni wamiliki wa nje na wameshafukuzwa tangu mwaka 1980 lakini maeneo yale ameendelea kuhodhi, yamekuwa mapori karibu eka 9000 na sisi hatuko tayari kuendelea kuiacha hiyo ardhi, tutaichukua asubuhi kama Serikali haitatumia utaratibu wa kumnyang’anya mtu huyo shamba hilo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeahidi hatuko tayari tena kupoteza ardhi ya Monduli kwa sababu maeneo mengi ya Monduli ni ya wanyamapori na maeneo mengine ni ya Jeshi na Monduli ni sehemu ya pekee ya nchi hii ambayo hatuna mgogoro kabisa na Jeshi pamoja na kwamba wamechukua eneo kubwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo dogo tulilobakiza walichukua wahujumu uchumi miaka 1980 na 1988 wakati wa mgogoro wa mama mmoja kule Namanga akapewa Lolkisale akaambiwa ni eneo la bure, wakachukua Mkuu wa Jeshi wa wakati ule, wakachukua akina Kinana na watu wengine, wanagawana kama ardhi haina wenyewe. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, wenyewe tumekuja. Tunao vijana wasomi, tutatetea ardhi kwetu kwa kila namna na hatutaitoa ardhi hiyo. Wako watu wanaotaka kudhulumu ardhi yetu lakini hatuko tayari kwa sasa. Mwisho, haiwezekani, Mheshimiwa Waziri nimeona migogoro michache, mengine tuachie. Mengine tutamaliza wenyewe, tuachie, lakini tusaidie mawili. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, moja, mgogoro wetu na Babati ambapo DC wa Babati amekuwa akiingilia kila siku maeneo ya Monduli bila kumshirikisha DC wa Monduli.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine nataka niombe mambo machache. Moja, nimesema lile suala la uhusiano wa Wizara zile na lingine kuna tatizo la Sheria za Ardhi, ambapo tatizo hili ni kwamba wanawapa Wenyeviti mamlaka ya vijiji kugawa ardhi, lakini hakuna sheria inayochukuliwa kwa Wenyeviti wale wanavyogawa ardhi ya wananchi kienyeji.
Mheshimiwa Mwenyekii, Wenyeviti wengi wametumia nafasi hiyo kudhulumu ardhi na kwa sababu hakuna sheria ya direct inayochukuliwa zaidi ya kuwavua madaraka na ardhi imeshakuwa na migogoro mikubwa katika maeneo mengi.
Pili, naomba Wizara ishirikiane na NDC kule Engaruka kwenye eneo la Magadi. Wanatuambia wanataka ardhi square kilometer 79,000 karibu eka 100,000; ardhi hiyo hatuna.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tumesema tutatoa eneo la kiwanda tu, maeneo mengine ya Mipango Miji watuachie sisi tutawauzia NDC, lakini hatutatoa bure. Maeneo mengine naomba Mheshimiwa Waziri Wizara yako ishiriki, ije watuambie wanataka ardhi kiasi gani kwa ajili ya kujenga kiwanda. Maeneo mengine watuachie ardhi yetu, sisi tutapanga namna ya kutumia, wao wasitupangie. (Makofi)
Mheshimiwa Waziri, suala lingine ambalo natamani lishughulikiwe, Mheshimiwa Waziri naomba usikilize vizuri, liko tatizo la shamba ambalo tuliruhusiwa na Mheshimiwa Rais mwaka 2005 kule Makuyuni. Shamba kitalu namba 7/2, Mheshimiwa Rais alipofuta shamba hili kwa mtu anayeitwa Stein ambaye alifukuzwa nchini mwaka 1980 tukapewa ardhi hiyo eka 9000 Makuyuni. Baadaye Hazina wakatuandikia barua kwamba tumwandalie hati. Hatuandai hati leo, wala kesho, wala milele, wala asiendelee kutusumbua. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Rais amesharudisha ardhi hiyo, hatuitoi, hatuitoi, hatuitoi! Tumeambiwa tuwatoe wananchi wetu kule eneo la Jeshi tukawape eneo lile, halafu leo tunaambiwa tumrudishie mtu ambaye sio raia! Hiyo ardhi hatuitoi leo wala kesho. Wala wasithubutu, wala wasijaribu maana hatuitoi. Tumegawana eneo hilo, tunasubiri mvua iishe tukaingie kwa sababu tulishamaliza. Hamuwezi kutuondoa kwenye eneo la Jeshi halafu tupewe ardhi na Mheshimiwa Rais halafu mtu mwingine aje kuturudisha. Mheshimiwa Rais mwenyewe atamke. (Kicheko/Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nasema kwenye uongozi wetu, hiyo ardhi hatuitoi. Watu wa Hazina kuendelea kutuandikia vi-memo wakome. Sisi huwa hatupigwi, wala hatujinyongi, lakini tunaitetea ardhi yetu kwa namna ambayo tunaweza tukiwa hai. Hatuitoi hiyo ardhi. Hatuitoi, Monduli siyo shamba la bibi!
Taarifa ya Mwaka ya Shughuli za Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji na Taarifa ya Mwaka ya Shughuli za Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii kwa Kipindi cha Januari, 2016 hadi Januari, 2017
MHE. JULIUS K. LAIZER: Mheshimiwa Mwenyekiti, na mimi nikushukuru kwa kupata nafasi ya kuchangia katika hoja iliyopo mbele yetu na nianze na migogoro kati ya watumiaji wengine pamoja na hifadhi zetu. Inawezekana tutapiga kelele kuhusu jambo hili, lakini tukubaliane tu kama Bunge kwamba Serikali inalea na inachangia sana mauaji na mapigano ya wananchi pamoja na wanajeshi wetu katika maeneo ya hifadhi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pasipo shaka Serikali ina tathmini ya watu waliouawa katika hifadhi. Juzi waliuawa watu wanne kule Arumeru, hakuna kauli ya Serikali wala ziara yoyote ya Serikali iliyotembelea eneo hilo. Ikitokea ugomvi kati ya mkulima na mfugaji Serikali itapeleka polisi, Serikali itapeleka kila kitu, lakini akiuawa mwananchi katika eneo la hifadhi wala Serikali haijali na ndiyo maana Serikali inatoza watu wakiua tembo dola 15,000 lakini mwananchi analipwa shilingi milioni moja akiuawa. Kwa nini tusiseme Serikali ina ajenda ya kuua watu wake kwa kisingizio cha uhifadhi wa wanyamapori? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika maeneo mengi ya hifadhi, zile buffer zone ambazo Serikali inasema mita 500, maeneo mengine kuna maji, lakini mwananchi anaambiwa buffer zone zile zinaanzia mita 500 katika eneo la mto ambalo kuna maji. Mwananchi atapataje nafasi ya kwenda kuyatumia yale maji? Ndiyo chanzo cha migogoro mingi. Maeneo mengine ukienda kama Ngorongoro, ukienda kule Sikonge, tumepata taarifa wananchi wameuawa wanapigwa risasi ya kisogo na askari, lakini Serikali imaficha. Jana tumepata taarifa ya kule Morogoro Serikali ya Mkoa chini ya Mkuu wa Mkoa waliwanyima Civil Society na Waandishi wa Habari kuingia kwenda kukusanya taarifa ya hali ya migogoro kati ya wakulima na wafugaji. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo naliona ni kwamba Serikali haijawa tayari kushughulikia matatizo haya. Kwa mfano, zimekuja ripoti mbalimbali, Operation Tokomeza, Ripoti ya akina Mheshimiwa Jenista Mhagama, wakati ule ilikwenda kutafuta tatizo la wafugaji na wakulima, Serikali imekalia ripoti, hakuna taarifa yoyote ambayo so far Serikali imeyafanyia kazi mapendekezo ya Wabunge! Hivi tutaendeea kukaa kwenye Bunge mpaka lini?
Mheshimiwa Mwenyekiti, nafikiri Bunge hili litoe Azimio, Serikali itoe commitment leo kwamba matatizo ya wafugaji na wakulima yataisha lini nchi hii? Vinginevyo tutagawa Taifa hili, vinginevyo tutawagawa wananchi wetu hawa, vinginevyo tutatengeneza uadui ambao ni mbaya kuliko uadui ulioko nje ya nchi yetu, kama Serikali haitoi commitment.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imesababisha haya kwa sababu Wizara hizi hawashirikiani, Waziri wa Kilimo anaenda peke yake, Waziri wa Ardhi anaenda peke yake, Waziri wa Maliasili anaenda peke yake. Naomba wakati naendelea hivi, tunaomba Kauli ya Serikali. Hivi kauli kubwa kuliko yote ni ipi? Rais amesema wafugaji wasisumbuliwe kwenye hifadhi mpaka Serikali itakapopata maeneo ya kuwapeleka, ananyanyuka Waziri wa Maliasili anasema ondokeni leo, bila kutuambia tunaenda wapi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni nani yule ambaye anaweza akatengua kauli ya Rais aliyesema tutengewe maeneo ya kwenda kwenye mifugo kabla ya kutuondoa katika maeneo yale? Waziri ananyanyuka anasema wafugaji waondoke, twende wapi? Mazingira ambayo tunayaonesha kama Serikali haitatengeneza utaratibu wa matumizi bora ya ardhi kwenye nchi yetu, migogoro hii haitakaa iishe.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tumepitisha sheria hapa ya kuweka chapa mifugo, tumepitisha sheria ya kutenga maeneo ya mifugo, lakini mpaka sasa hakuna hata sehemu moja ambayo Serikali ime-declare kwamba eneo hili ni la wafugaji. Matokeo yake wafugaji wanaondoka wanaenda kwenye mashamba ya watu na hakuna mkulima yuko tayari kuona mfugaji akilisha ng’ombe kwenye shamba lake. Hicho ni chanzo cha migogoro na hatuna kauli thabiti ya Serikali ya kutatua tatizo hili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tutaendelea kusikia wakisema tunalaani, tutaendelea kusema watu wakipelekwa mahakamani, lakini watu wanahonga na hakuna hatua zozote zinazochukuliwa. Hatuwezi kama Bunge kuona wananchi wetu wanauawa kwa sababu ya uzembe wa Mawaziri na uzembe wa Serikali yenyewe. Tunataka commitment ya Serikali tunamalizaje tatizo la wafugaji na wakulima nchini mwetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa nini miaka ya nyuma tulikuwa hatugombani? Ni kwa sababu ardhi ilikuwa inatosha, sasa ardhi imekuwa ndogo, Serikali haina mikakati. Mnasema Idara ya Ardhi watenge maeneo lakini hamuwapi bajeti. Kama kweli Bunge hili tunatamani kuwaunganisha Watanzania ni muhimu kuibana Serikali itoe commitment na schedule program ya kuhakikisha inamaliza tatizo hili ambalo la wakulima na wafugaji ambalo limekuwa kubwa kwenye nchi yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo ninaomba nilichangie ni suala la Wizara ya Ardhi. Wengine wamechangia na Kamati imeona kwamba tatizo kubwa ni kwamba kuna mashamba makubwa ambayo yamehodhiwa na watu ambao hawajayaendeleza. Nitasema mashamba manne tu Monduli, ambayo watu wanne wanamiliki zaidi ya ekari 32,000 na mpaka sasa hawajalima hata nusu ekari, lakini mpaka leo Serikali haitoi kauli kwamba mashamba hayo yanarudi lini kwa wananchi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunalo shamba la Sluiz, tunalo shamba la Tan Farm, tunalo shamba la Stein ambalo lina ekari 16,000 peke yake hajaendelezwa na Serikali imeendelea! Kwa nini migogoro isitokee? Kwa hiyo, tunafikiri kama Serikali imedhamiria kweli kuyarejesha mashamba haya kwa wananchi ni muhimu ikafanya haraka. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala langu lingine ni kuhusu ukame ambalo limekuwa kubwa. Mmesema tusiseme kuna njaa, tukisema hivyo tunafunguliwa mashtaka. Mimi nafikiri mtalifungia Bunge lote hili, hakuna Mbunge asiyejua kwamba wananchi wanaenda kwenye maeneo wakilalamika njaa na tunaona. Tunaona mifugo yetu ambayo ni rasilimali yetu ikiteketea, tunaona mashamba yakikauka. Ni kweli Serikali haijaleta ukame, lakini tusikatae kwamba kuna taizo la njaa linalotokana na ukame ili tuende tukajadiliane kama Taifa tunafanyaje kuwaokoa watu wetu wasife, kuliko kuendelea kusema kwamba hatuna tatizo, lakini tatizo hili linatumaliza. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hakuna mtu asiyeona kwamba mvua zimechelewa kunyesha, lakini Serikali inakataa hakuna njaa ili Watanzania hawa wafe, tunaogopa nini wakati ninyi hamjaleta ukame au labda ninyi ndiyo mmeleta ukame? Kama siyo ninyi msizuie watu kusema kuna tatizo. Anayeopata neema ya mvua ni ya Mungu tu. Sasa msiwacheke wale ambao neema hiyo haijawafikia, tukifanya hivyo tutasaidia Taifa letu kutafuta namna ambavyo tutapambana na majanga haya yaliyopo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo langu la mwisho, tunalo tatizo la hifadhi zetu na wafugaji. Tunataka Serikali ituambie kwa nini Serikali isishirikiane na wananchi wa vijiji katika maeneo yao katika kutafuta suluhu ya kukubaliana mipaka mipya ya hifadhi zetu na wananchi wetu? Katika eneo la Ngorongoro peke yake mnataka kuchukua square metre 15,000 kilometa 1,500 ya wananchi kwa kisingizio kwamba kuna wahamiaji haramu, naitaka Serikali wakati inafanya majumuisho ituambie…
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
MWENYEKITI: Ahsante Mheshimiwa Laizer.
Makadirio ya Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira
MHE. ALI HASSAN OMAR KING: Mheshimiwa
Mwenyekiti, ahsante. Kwanza nishukuru kwa kunipa nafasi hii. Pia nimshukuru Mwenyezi Mungu ambaye ametupa uhai na tumefika leo hapa kujadili masuala haya ya mustakabali wa nchi yetu katika Muungano na Mazingira.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ufunguzi wa neno langu kubwa ambalo napenda nilitumie ambao ni msemo wa wahenga unasema anayekufukuza akishaona hakupati basi nyuma huku hukurushia matusi. Kwa hiyo, namwomba Waziri wangu wa mambo ya Muungano, mambo ambayo yameandikwa yakawa presented hapa, haya mengine wewe yachukulie tu. Hawa wako mbali sana, kwa hiyo lazima watarusha maneno. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, napongeza utekelezaji wa mambo ya Muungano ambayo Mheshimiwa Waziri ameyataja kwenye kitabu chake kuanzia ukurasa wa 42 mpaka ukurasa wa 52 ambayo pamoja na mengine siyo ya kimuungano lakini ni ya ushirikiano ambayo ni sekta siyo za Muungano lakini tulishirikiana pamoja na Zanzibar. Kwa hili nakupa hongera sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kingine kikubwa ambacho nakisema hapa labda pengine kwa watu wengine ambao wanasema kwamba labda Serikali hii haina kipaumbele au haijaweka mtazamo mkubwa katika kuangalia masuala ya Muungano ili waelewe, tunaelewa sisi kuna fedha za maji ambazo zimepita katika Jamhuri ya Muungano mkopo kutoka India, ni zaidi au karibu robo ya bajeti ya Zanzibar ambazo zimeenda kule, wasiojua walijue hilo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimesema hili kwa sababu wakati mwingine mtu ukiambiwa kipofu siyo lazima kwamba haoni, inawezekana mtu akapofua fikra. Kwa hiyo, humu kuna watu wamepofua fikra zao, zile fikra zao ndiyo vipofu hawawezi kuona, hata kama wana macho hawataweza kuona, hata kama wana masikio hawataweza kusikia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la msingi labda nimnukuu Spika kwamba kumbe walemavu kweli wamo wengi humu, kwa sababu fikra pia nazo zinampeleka mtu kulemaa, akafikiria hata jambo la kuliona wazi asiweze kuliona. Kwa hiyo, hilo ni moja katika kuangalia mambo mazuri ambayo yamepangwa na yamefanyika katika Muungano. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kipengele ambacho Mheshimiwa amekizungumzia katika ukurasa wa 51, ushirikiano katika mambo ambayo siyo ya Muungano hasa katika masuala ya afya na nakwenda katika Bima ya Afya. Mfuko wa Bima ya Afya unafanya kazi Zanzibar, pia Mfuko huu wa Bima ya Afya unafanya kazi Tanzania Bara ambapo uko chini ya Wizara ya Afya. Jambo ninaloliomba hapa, muundo wa Halmashauri ambao uko huku ambao Wazee wanapata Bima ya Afya ni tofauti na muundo wa utawala kule Zanzibar ambapo mara nyingi Majimbo huwa yanajitegemea, tunajua Wazee kuna fedha zinatengwa kwa ajili ya kupatia Bima ya Afya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ombi langu au ushauri wangu, kwa nini tusiendeleze ushirikiano tukachukua katika ngazi ya Majimbo, likazungumzwa, likatazamwa kwamba linafanywaje ili tuweke huu ushirikiano katika kuwapatia wazee Bima ya Afya kama vile ambavyo wazee wanapata Bima ya Afya kupitia katika Halmashauri za Tanzania Bara.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo hili binafsi katika Jimbo langu niliwahi kulitekeleza lakini zikatokea changamoto. Kwa hiyo kutokana na hizo changamoto zilizojitokeza, mwaka huu tumesimama. Kwa hiyo, naiomba Serikali yangu sikivu, hapa tuweze kuliratibu hili kama linaweza kufanyika hata katika ngazi ya Majimbo, kwa sababu katika Serikali ya Zanzibar hakuna utawala ambao uko maalum katika Halmashauri ambao unapelekewa fedha ili kuhudumia sekta za jamii. Majimbo yenyewe pengine kupitia Mbunge na Mwakilishi wanaweza wakafanya hili jambo, kwa hiyo tunaiomba Serikali ya Jamhuri ya Muungano iliangalie hili kupitia mzungumzo ya Wizara hii ya Muungano.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine alizungumza hapa Mheshimiwa Shamsi Vuai kwamba tuangalie jinsi gani uchumi mkubwa unaweza ukasaidia uchumi mdogo. Hapa moja kwa moja nije katika corporate tax. Tunajua kwamba pay as you earn inapatikana kama ilivyopangwa na makubaliano yalivyo. Nafikiri Mheshimiwa Waziri hili analifahamu. Pia custom duty na excise duty kwa Zanzibar wanakusanya wenyewe, lakini corporate tax inakusanywa kwa mujibu wa kampuni iliposajiliwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa usajili mara nyingi, mtu atafanya usajili sehemu ambayo kuna urahisi wa kusajili na urahisi wa kusajili unakujaje, alipo regulator kwa mfano, benki nyingi sana haziwezi kuja ku-register Zanzibar, zita- register Tanzania Bara. Kwa hiyo, kwa kuwa zitakuja ku-register Tanzania Bara ina maana kwamba hata kodi yake itakuwa inalipwa Tanzania Bara. Kwa hiyo mapato haya yanayotokana na kodi ya kampuni tujaribu kuangalia kigezo kingine.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nazungumzia kigezo kingine kwa sababu makampuni haya yanafanya kazi katika mazingira ya Zanzibar, wanawatumia wateja wale wa Zanzibar, wanafanya shughuli zao pale na mazingira ambayo yamewekwa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar lakini bado corporate tax zao wanalipa kwa Tanzania moja kwa moja. Tunaomba kungekuwepo kigezo cha operation au kama itakavyoonekana katika mazungumzo kwamba pia hizi corporation tax pia ziwe zinakusanywa Zanzibar kwa portion ya zile benki au taasisi za simu zinavyofanya kazi kule.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine katika hili, tumebadilisha Sheria kadhaa ambazo zinahusiana na mambo ya mapato ikiwemo ku-charge transactions whether za kwenye simu, miamala ya kifedha, lakini bado miamala ya kifedha kwa kuwa kwamba hivi vyombo vimesajiliwa Tanzania Bara haziwezi kwenda Zanzibar. Kwa hiyo, tutafute mazingira kwa sababu na Zanzibar wanatumia hizi benki, Zanzibar wanatumia hizi transaction, miamala hii waweze pia kuipitia na Zanzibar waweza pia kunufaika. Hili ni jambo ambalo nashukuru sana kama litafanyika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo nianze na msemo mdogo unaosema kwamba muungwana ni yule ambaye akinena halafu anatekeleza. Mheshimiwa Naibu Waziri wa Muungano aliniahidi kwamba atakuja kunitembelea Jimboni na nashukuru akafanya uungwana ule akaja kunitembelea Jimboni, akaona mazingira niliyomuhadithia hapa, namshukuru sana. Namkumbusha tena Mheshimiwa Waziri aliwaahidi wananchi wangu baada ya kuja Jimboni kwamba atakuja kufanya jambo fulani la kimazingira ambayo aliyaona. Kwa hiyo namkumbushia na hili nalo pia aliangalie. Hili ni muhimu kama litafanyika kwa ajili ya kuboresha Muungano wetu na kufanya mambo ambayo yataweza kutusaidia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ni uvuvi wa bahari kuu. Katika uvuvi wa bahari kuu Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ilipanga kujenga bandari ambazo zitakuwepo Zanzibar pamoja na chombo cha kufanyia survey kwa uvuvi wa bahari kuu. Mpaka sasa hivi tunaona masuala haya yamekwama. Labda kupitia mazungumzo haya katika Wizara hii ya Muungano iweze kuangalia, kwa sababu Bandari ambazo ziko hata meli ziki-register kuja kuvua Zanzibar au kuja kuvua katika uvuvi wa bahari kuu, haziwezi tena kurudi kwa sababu mazingira ya bandari zetu kwa Tanzania Bara pamoja na Zanzibar siyo mazuri. Kwa hiyo, tufanye hayo mazingira yawe mazuri na tuweze kuendelea kunufaisha watu wetu katika uvuvi huu wa bahari kuu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya hayo, sina mengi ya kusema, naunga mkono hoja, Waziri wetu piga kazi.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano
MHE. JULIUS K. LAIZER: Mheshimiwa Mwenyekiti, nami nitumie nafasi hii kukushukuru pia kwa kunipa nafasi ya kusema maneno machache kwa dakika hizi tano.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara hii ni Wizara muhimu sana ni cross cutting Ministry kwa sababu Wizara zote zinaitegemea hii. Tuna matatizo makubwa ya upelekaji wa fedha ya miradi ya maendeleo katika Halmashauri zetu. Hili limekuwa ni tatizo sugu katika Halmashauri nyingi. Kwa mfano, katika Halmashauri ya Wilaya ya Monduli tumepelekewa milioni 200 tu kati ya shilingi bilioni 1.2 ambazo tulitengewa. Sasa katika mazingira ya sasa tunahangaika kupitisha bajeti, tunataka Waziri aje atueleze wana mikakati gani kuhakikisha kwamba fedha zote zilizobaki katika bajeti ya mwaka huu 2016/2017, zinapelekwa katika Halmashauri zetu kabla ya Juni mwaka huu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama sitapata majibu ya kuridhisha basi nitashika shilingi ya Waziri, kwa sababu hakuna sababu ya kupitisha bajeti mpya kama bajeti tuliyoipitisha hatupeleki kwenye Halmashauri zetu. Haitakuwa na maana kwa sababu akinamama wajawazito watafia njiani na wakati wa mvua barabara zetu hazitapitika na hata sekta nyingine zote hazitakuwa na ustawi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine nimeona katika kitabu tunashukuru kwamba barabara ya Loliondo – Monduli kwa maana ya Mto wa Mbu pamoja na Serengeti imeendelea kutengewa fedha. Barabara hii ni muhimu, tunaitengea fedha kidogo sana. Nataka Serikali ituambie mpango wa barabara hii itakamilika muda gani? Kwa maana mwaka huu itajengwa kilomita ngapi na mwaka unaofuata kilomita ngapi mpaka barabara itakapokamilika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, bahati nzuri namwona Waziri wa Viwanda. kule Engaruka yamepatikana magadi yenye ujazo wa trilioni nne, mpaka sasa hakuna barabara itakayofika katika eneo lile na wananchi wetu wapo tayari kutoa ardhi yao kwa ajili ya viwanda vile. Kwa hiyo, kama Serikali haitakuwa na commitment ya kupeleka miundombinu kwa maana ya angalau barabara na baadaye reli, ardhi ile tutaendelea kuitumia lakini wananchi wetu wapo tayari kutoa hata bure kwa ajili ya kujenga kiwanda kile. Kama hakuna commitment ya Serikali ya kupeleka miundombinu kwenye maeneo yale mtuambie ili wananchi waendelee kutumia maeneo yale wakajenge mpaka mtakapokuwa tayari kuleta miundombinu na kiwanda kianze na wakati huo gharama za fidia zitakuwa kubwa zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naiomba sana Serikali ituhakikishie ni lini barabara hii itakamilika kutoka Mto wa Mbu kwenda Loliondo kwa sababu ya umuhimu wa magadi yaliyopo Engaruka ambao sisi tupo tayari kuwapa ardhi kwa ajili ya kuanzisha kiwanda hicho.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili ni ahadi za Rais. Naomba Waziri atuambie Rais alivyopita katika Wilaya ya Monduli wakati anaomba kura aliahidi kutujengea barabara ya lami kutoka Monduli Mjini kwenda Monduli Juu kule kwa Sokoine. Pamoja na kwamba Waziri haandiki lakini nataka Serikali iniambie ni lini mchakato wa barabara hiyo utaanza kwa sababu Rais aliahidi au Serikali ituambie kwamba labda Rais alisema uwongo ili kujitafutia kura, kama ni kweli basi tuambiwe ni lini barabara ya Monduli kwenda Monduli Juu Serikali itaijenga kwa lami kama Rais alivyoahidi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo langu la mwisho ambalo naiomba Serikali iangalie ni upelekaji wa fedha za miradi katika barabara za Mkoa. Sisi tuna barabara moja hii barabara ya Loksale tunaona imetengewa shilingi milioni mia tatu ambayo ina kilomita hamsini, haiwezi kusaidia chochote. Pamoja na kwamba kwa kweli tunampongeza Meneja wa Barabara wa Mkoa kwa sasa anafanya kazi nzuri na anasimamia miradi mingi ya Mkoa kuliko wakati mwingine wowote. Tunamshukuru na tunaendelea kumuunga mkono katika hili, fedha mnazompelekea ni fedha kidogo sana hazitoshi tunaiomba Serikali ione namna ya kuongeza fedha katika Mfuko wa Barabara ili barabara zetu nyingi ambazo bado ni vumbi ziweze kupitika kwa wakati wote, tusipofanya hivyo hata huduma zingine hazipatikana na huduma hizi tunazozitoa zitakuwa haziwafikii wananchi wetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, naomba nikushukuru.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Maji na Umwagiliaji
MHE. JULIUS K. LAIZER: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kupata ufafanuzi wa vigezo vinavyotumika kugawa fedha za Miradi ya Maendeleo ya Maji Vijijini. Kwa mfano katika ukusara wa 140 jedwali 5(a) Monduli imetengewa shilingi 646,914,000. Jambo ambalo ni kinyume kabisa na matarajio ya mapendekezo ya bajeti ambayo ilikuwa bilioni nne. Ni namna gani tutatekeleza miradi ya wananchi kwa kiasi hiki kidogo?

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba Serikali itusaidie kuimarisha chanzo cha maji Ngaramtoni (kisima) ili kukidhi uhitaji wa maji ambapo kwa sasa miradi mingine imeanzishwa kwa kutumia kisima cha awali. Serikali haijapanga fedha miradi ya vijiji viwili; sehemu ya vijiji kumi ambavyo vilikuwa vimebaki awamu ya pili.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano
MHE. CATHERINE V. MAGIGE: Mheshimiwa Naibu Spika, Shirika la Posta limekuwa likiwalipa pension waliokuwa wafanyakazi wa Jumuiya ya Posta ya Afrika Mashariki kwa kipindi kirefu kwa niaba ya Serikali na Serikali inachelewa kurudisha shilingi bilioni nne ili Shirika la Posta liwalipe wafanyakazi hao.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba Serikali iwalipe pesa hizo ili Shirika la Posta liweze kuendelea kwa mafanikio.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano
MHE. JULIUS K. LAIZER: Mheshimiwa Naibu Spika, ujenzi wa barabara ya Mto wa Mbu hadi Serengeti – Mugumu, barabara hii ni muhimu kwa sababu pia imegundulika madini ya magadi pale Engaruka.

Mheshimiwa Naibu Spika, lini barabara hii itaanza kujengwa ikianzia Mto wa Mbu ili kurahisisha uanzishwaji wa Kiwanda cha Magadi Engaruka. Pia ni lini ahadi ya Rais ya kujenga kwa lami barabara ya Monduli kwenda Sokoine.

Mheshimiwa Naibu Spika, ni lini Serikali itatupatia daraja la kudumu barabara ya Lokisale – Monduli?
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii Kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2018 Pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2018
MHE. JULIUS K. LAIZER: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuchangia. Napenda kutumia nafasi hii, kipekee kabisa kumpongeza Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa John Pombe Magufuli kwa kauli yake ya kusaidia wananchi wanaoishi katika maeneo ya hifadhi kwa muda mrefu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa sababu wewe ni mzoefu katika nchi hii, Bunge hili limejadili mara nyingi operesheni mbalimbali zilizofanyika katika hifadhi ambazo ziliwaumiza wafugaji wa nchi hii kwa kiwango kikubwa sana, ni mtu tu asiye na akili timamu atakayeacha kumpongeza Mheshimiwa Rais Magufuli kwa jambo hili jema na la kiutu alilofanya katika kusaidia wafugaji. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, wako watu ambao hawataki kuona jema analofanya Mheshimiwa Rais katika kipindi hiki cha miaka mitatu, lakini hao hao ndio wanaoomba viwanja vya ndege katika maeneo yao viboreshwe lakini wakati huo huo wakipinga uagizaji wa ndege katika nchi yetu. Hao hao ndiyo wanaosema tupunguze deni la Taifa lakini wanachukua Rais akinunua ndege kwa cash ya fedha ya walipa Kodi wa Watanzania hii. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kipindi hiki cha Mheshimiwa Rais Magufuli cha miaka mitatu tumeshuhudia vituo 360 vya Afya vikijengwa katika nchi hii, ambayo ni historia, haijawahi kuitokea. Ndiyo maana wengine tunasema lazima tupongeze na kutambua kazi kubwa ambayo Rais huyu amefanya, katika muda mfupi ambao amekuwa katika madaraka haya. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tunazo Hospitali 60 zinajengwa kwenye nchi hii, nani ambaye haioni katika utawala huu wa Rais Magufuli. Nataka tuyaseme haya kwa sababu Watanzania wengi wanatambua na wako wengi wanaopambana kufifisha ndoto ya Rais, lakini nataka tumtie moyo kwamba hata wakati ule Yesu alivyokuwa amepingana na matendo yake, akawaambia hata kama hamniamini aminini kazi ninazozifanya. Kwa kazi hizi ambazo Rais anafanya tunazitambua na kumpongeza na kumtia moyo, asonge mbele Watanzania wako nyuma yake. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, katika hili la kumpongeza Rais, kwa dhati kabisa, naomba niipongeze Wizara ya Mifugo kwa mara ya kwanza wamesimama na wafugaji wa nchi hii na kutambua kwamba na sisi ni Watanzania walio huru katika Taifa hili na kutetea maslahi ya Wafugaji. Pamoja na changamoto zingine lakini katika hili tuko pamoja na Mheshimiwa Waziri, asonge mbele, tutamsaidia katika kusimamia Wizara ya Mifugo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tumekuwa tukijiuliza maswali mengi kwa nini katika nchi hii, hatujawahi kuona oparesheni ya wakulima katika maeneo ya hifadhi isipokuwa operesheni ya wafugaji. Ni kwa sababu wafugaji mara nyingi wana cash mkononi kwa sababu wana ng’ombe, kwa hiyo viashiria vinafanyika wakati mwingine sio halali, ni operesheni za kutafuta rushwa na kunyang’anya wafugaji wetu mali zao. Katika hili ndio maana nasema tunampongeza Rais na Wizara kwamba angalau sasa ile mianya ambayo watu wachache waliitumia kuwaumiza wafugaji imefungwa na ndio maana wengine wanapiga kelele, lakini sisi tuko nyuma ya Rais kwa kazi kubwa ambayo ameifanya. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nataka niseme mambo machache, nataka niombe Serikali watusaidie, wanazuia wafugaji wetu wasipeleke ng’ombe Kenya wanafanya operesheni ambayo sio halisia katika mipaka ya nchi yetu, lakini nataka niwauze Wizara ya Mifugo, Viwanda vyetu 82 vya maziwa nyakati za Nyerere mpaka kipindi cha Mwinyi kidogo, viko wapi? Viwanda vya nyama vilivyokuwa vinafanya kazi katika nchi hii, viko wapi? Kama ndani ya nchi yetu hakuna soko la uhakika kwa nini watuzuie sisi kwenda kutafuta soko huko linakopatikana na kama wanafikiri kuweka kodi kubwa kwa mifugo ni kuzuia mifugo isiende nje ya nchi, tunataka Wizara watuambie masoko ya kupeleka bidhaa yetu yako wapi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ni aibu, ni aibu kwenye Taifa linalozalisha ng’ombe nchi ya tatu Afrika, mali zetu za ng’ombe zinaenda nje bila kuongezwa thamani, tunapeleka kwato, maziwa, ngozi na nyama, halafu tunasema ipo Wizara inayojali mifugo, tunataka Serikali ituambie iko wapi mikakati ya Wizara ya kuhakikisha rasilimali hii ya Taifa ambayo ni neema kwa nchi yetu, inabaki kwa maslahi mapana ya Taifa letu na kuongeza pato la Taifa. Ni aibu kwa nchi ambayo ni ya tatu kwamba pato la Taifa halilingani na mifugo tuliyonayo na wakati mwingine tunasema mifugo yetu inaharibu mazingira, tunataka Serikali itupe mikakati ambayo Waziri wa Viwanda jana alituambia, kwamba wamepanga kuhakikisha kwamba tunachakata mazao ya mifugo, tunataka frame time, ni lini viwanda vya kuchakata mazao ya mifugo kwenye nchi vitasimamiwa na kuonekana kwamba vinakidhi matakwa ya wafugaji wa nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nataka Serikali kwa kweli katika hili ituambie, tunaridhika na pato la Taifa linalochangiwa na mifugo yetu, tunaridhika na upekaji wa ng’ombe zetu Kenya bila kuongeza thamani. Hivi Wakenya wanatuzidi nini? Tunaridhika na uamuzi wa Afrika Mashariki wa kuweka vikwazo vya ngozi na nchi kama Rwanda na Burundi ambayo hawazalishi ng’ombe lakini wanatuletea ngozi, wakati tulikuwa tukizalisha ngozi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ipo Mikataba tunaingia na nchi, lakini kwa kweli haina manufaa kwa nchi yetu, nchi zile zingine hazizalishi ng’ombe, hazina ng’ombe, lakini wanaamua, wao ukipeleka ngozi Uganda, Rwanda inaenda kama reject kwa hiyo, sisi tunakosa mapato na ngozi zetu zinakuwa useless. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Wizara ituambie kuwepo kwa Wizara hii, ni kutafsiri ndoto ya Rais ya Tanzania ya viwanda ambayo kila mwananchi ataona umuhimu wa kuwepo kwenye Taifa lake na umuhimu wa kuwa na rasilimali katika nchi yetu. Haiwezekani tukasema tuna viwanda kadhaa, lakini kama viwanda hivyo havibadilishi maisha na uchumi wa nchi yetu viwanda hivyo havitakuwa na maana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo naomba kabisa, wakati Waziri wa Mifugo anakuja kuchangia baadaye atusaidie ni kwa namna gani nchi yetu inaondokana na hili tatizo la kupeleka rasilimali na bidhaa ambayo haijachakatwa katika nchi zingine za wenzetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, la mwisho, tunalo tatizo pale Namanga, mfugaji akitaka kuvusha ng’ombe zake kwenda Kenya analipa si chini ya elfu 70 kwa kichwa cha ng’ombe, ipo Sh.30,000 wanaita ni fedha za ushuru wa Wizara, lakini ipo Sh.2,500 ya movement permit na kodi zingine za Halmashauri, hivi kwa nini ng’ombe peke yake tuyaangalie na mazao mengine tunayozalisha, wanakuwa na kodi kubwa kuliko mazao mengine yoyote kwenye nchi yetu? Tunaomba Waziri atuambie wakati wa bajeti hii ni kwa namna gani Serikali itapunguza kodi ambazo zimewekwa kwenye mifugo ya nchi yetu kwa sababu kuzuia tu isiende nje kwa kuweka kodi kubwa wakati huku ndani hakuna viwanda vya kuchakata, ni uonevu kwa wafugaji. Kwa hiyo naomba kwa kweli, kodi hizi zipunguzwe kwa kiwango kikubwa.

Mheshimiwa Spika, suala la ardhi, ni kweli tumesikia ushauri wa Kamati, lakini nami nampongeza Rais na nimpongeze Waziri wa Ardhi kwa dhati ya moyo wangu kabisa. Moja ya Wizara zinazofanya kazi na zinafanya vizuri katika nchi yetu, ni Wizara ya Ardhi na faida yake ni kwamba, wamekataa rushwa, sio kwamba hakukuwahi kuwepo Wizara katika nchi hii, lakini Wizara hii ina mchakato mkubwa sana wa rushwa. Sisi tunaamini hawa wamekataa rushwa ndio maana migogoro ya ardhi imepungua katika nchi yetu. Kwa hiyo tunawatia moyo, msikate tamaa, tunahitaji ardhi yetu kwa sababu imekaa muda mrefu haitumiki na sisi tunaihitaji.

Mheshimiwa Spika, tunajua wako wachache watakaotumiwa na watu wenye ardhi hiyo, lakini sisi tuko tayari kuungana na nguvu na shughuli za Wizara katika kurejesha rasilimali ardhi kwa nchi yetu na kwa Watanzania wanyonge ili waweze kutumia katika kuzalisha. Haiwezekani tukawa na ardhi lakini Watanzania walioko maeneo hayo hawana uhalali wa kutumia ardhi hiyo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tumeenda Misenyi wakati wa Kamati, ardhi kubwa iliyoko kule, Watanzania wamenyimwa kutumia, lakini Waganda wanaingiza mifugo, wanatoa jioni lakini ukienda Tanzania wanakwambia ni hifadhi. Hii si sawa, lazima ardhi yetu itumike kwa maslahi ya Watanzania ambayo Mungu ametupa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Wizara songeni mbele, lakini tunaomba mtuletee modality ya mchakato mzima wa kutatua migogoro ya ardhi katika nchi.

Mheshimiwa Spika, ahsante sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi
MHE. JULIUS K. LAIZER: Mheshimiwa Mwenyekiti, Mgogoro wa Mipaka kati ya Monduli na Arusha DC katika Kata ya Mfereji. Naomba kauli ya Wizara hii ya Ardhi, ni lini mgogoro huu ambao umekuwa ukigharimu maisha ya watu wetu kwa kuchomewa, mabomu na kujeruhiwa utatatuliwa?

Mheshimiwa Mwenyekiti, mgogoro wa Monduli na Babati utatatuliwa lini kama Waziri alivyoahidi mwaka jana?
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Maliasili na Utalii
MHE. JULIUS K. LAIZER: Mheshimiwa Mwenyekiti, nami ninakushukuru kwa kunipa nafasi, naomba Waziri atakapokuja kuhitimisha hapa aniambie ni lini wananchi wa Lokisale, Mswakini na Lemoti, ambao mazao yao yaliharibiwa na tembo takribani kwa mfululizo miaka kumi sasa mpaka siku ya leo Serikali haijawalipa, ni lini Serikali watalipwa fidia zao?

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeendelea kuwa wahifadhi wazuri na ndiyo maana sisi hatuli nyamapori, lakini kama wanyama wenyewe wanakuja kula mazao yetu na Serikali haioneshi kujali tutapata ukakasi katika kuwalinda wanyama hawa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nimesikia mtu mmoja akichangia akisema watu wa Ngorongoro wametoka 8,000 wamekuwa 90,000. Kabla hatujahoji idadi ya Watanzania walioko Ngorongoro ambao ni haki yao na wala siyo hisani kwa sababu ni Watanzania wenzetu, ni muhimu pia tuhoji miaka hiyo na leo wanyama walioko Ngorongoro ni wangapi na wameongezeka kwa kiasi gani na ni lini jamii yetu imehusika? Tuambiwe hata Mmasai mmoja aliyehusika kufanya ujangili katika Hifadhi ya Ngorongoro?

Mheshimiwa Mwenyekiti, hamuwezi kutuhukumu kwa kuwaangalia majangili ambao ninyi mnawafahamu na Serikali imeshindwa kuwashughulikia. Tunataka mtuambie ni lini jamii hiyo imehusika katika kufanya ujangili kwa wale wanyama, kama kweli hoja yenu ni ya ujangili? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili, nashukuru kwamba leo watu wa Kaliua wameguswa, kwa sababu mara zote tunasema wananchi wa Ngorongoro wanaokaa kule wana haki kwa sababu ni ardhi ya vijiji. Leo wananchi wa Kaliua nao wameguswa, nashukuru sana Mheshimiwa Mbunge mwenzangu nae anakubaliana kwamba vijiji vilivyosajiliwa wapate haki kwa sababu vimesajiliwa na viko kihalali. Ni vizuri kwa sababu wameguswa, tutaendelea kuwa wengi tunaotetea maslahi ya Watanzania wenzetu.(Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka niihoji Wizara, hivi lengo la Wizara ni uhifadhi peke yake au lengo la Wizara ni kuhakikisha kwamba uhifadhi na maisha ya Watanzania yanaendelea kuongezeka? Maana leo ardhi haiongezeki, lakini hatuwezi pia, kubadilisha nchi hii ikawa ni nchi ya uhifadhi peke yake. Haiwezekani tukawa na uhifadhi bila watu, hata haya mapato tunayopata kutokana na wanyama, kama hakuna Watanzania watakaohudumiwa na fedha hizo, hakuna sababu ya kuwa na uhifadhi huo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninadhani ili jambo hili liende vizuri ni lazima tujue kwamba, katika maeneo ya uhifadhi kuna watu pia na kuna wanyama. Tujenge mazingira mazuri ya kupanga matumizi bora ya ardhi ili wote tuweze kunufaika na ardhi hiyo. Tatizo hapa ambalo ninaliona Wizara haipo tayari kushirikiana na wananchi kutatua migogoro iliyoko katika maeneo ya uhifadhi. Inaonekana Wizara inatumia nguvu kubwa, inatumia Jeshi, inatumia Polisi, katika kuumiza na kuua wananchi wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali leo ituambie, hivi ni Serikali imebariki maumivu na mateso ya wananchi katika maeneo ya uhifadhi? Kama Serikali haikubaliani na uonevu na maumivu wanayopata wananchi wetu, hao askari wanaotesa watu na kuua watu, wanapata wapi mamlaka ya kufanya hivyo?

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama Serikali haikemei, na mimi nadiriki kusema kama Serikali haikemei uonevu na mauaji yanayofanyika kwa raia, maana yake Serikali imebariki uonevu na mauaji ya raia walioko katika maeneo ya hifadhi. Haiwezekani watu wauawe tu halafu Wizara imekaa kimya, Serikali imekaa kimya! Wabunge tunapiga kelele hapa, halafu tuseme Serikali haijabariki! Mimi naamini kama Serikali haitoi kauli maana yake Serikali imeagiza polisi na Askari wa Wanyamapori waue raia katika maeneo yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimalizie katika suala la uporaji wa mifugo katika maeneo ya uhifadhi. Kama walivyosema Wabunge wenzangu, hivi nani anayeharibu misitu kati ya ng’ombe na wakata mikaa? Hivi nani anayeharibu misitu kati ya wafugaji wanaofuga ng’ombe tu na wale wanaochoma mikaa na mikaa mmetoa kibali inauzwa kila mahali kwenye nchi hii?

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba tu Serikali i-admit leo, kama Serikali ina chuki na uadui na wafugaji, tujue kwamba Serikali haitaki ng’ombe kwenye nchi hii. Jana tulikuwa tunajadili bajeti ya Wizara ya Mifugo, tunaambiwa thamani ya bidhaa inayotokana na mifugo ni zaidi ya trilioni 17 ya nchi hii, leo tunadiriki kuona kwamba wafugaji hawana haki katika Taifa hili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hatukatai uhifadhi, lakini uhifadhi leo hii umefika hapa kwa sababu ya ukarimu wa wafugaji katika nchi hii. Kama ingekuwa ni watu wengine wameishi katika hifadhi wale wanyama wasingekuwepo leo, wafugaji tumekuwa tukiishi na wanyama bila madhara yoyote. Kwa nini leo ninyi, kwa sababu, mna nguvu, mna dola, mna jeshi, mna polisi, mnaona hatuna haki kuishi katika maeneo hayo ambayo ninyi mlitukuta katika maeneo hayo?
Mimi naomba…

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa mzungumzaji)

MWENYEKITI: Ahsante.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Maliasili na Utalii
MHE. JULIUS K. LAIZER: Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali iwalipe wananchi fidia ambao mazao yao yaliharibiwa na tembo katika maeneo ya Mswakini, Makuyuni, Lokisala, Lemooti na Monduli Juu. Pia ni lini Serikali italipa fedha za WMA zinazodaiwa na WMA ya Randilen? Ni muhimu Wizara hii ikarejesha fedha hizo kwa wakati.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa Monduli imezungukwa na Mbuga za Ngorongoro na Tarangire tunaomba Wizara ione namna ya kutupatia gari la doria ili kunusuru mazao na maisha ya watu wetu.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Ofisi ya Waziri Mkuu
MHE. JULIUS K. LAIZER: Mheshimiwa Mwenyekiti, nikushukuru kwa kunipa nafasi ya mimi kusema katika hotuba ya Waziri Mkuu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze katika hili suala la watumishi walioachishwa kazi, hasa wale watendaji wa vijiji, wa kata na madereva. Mimi naomba tu Waziri atuambie; hivi utu wa kibinadamu katika jambo hili umezingatiwa kwa kiwango gani? Kwa sababu kama Waziri ambaye anasimamia sekta hii na anayesimamia utaratibu huu anajua kabisa kwamba watumishi hawa waliajiriwa na Serikali miaka hiyo kwa sababu kulikuwa kuna uhitaji wake, lakini kwa sababu Serikali sasa imeona labda hawahitajiki tena imeamua kuwa-dump na kuwatupa kama watu ambao hawajawahi kulitumikia taifa hili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mnatengeneza visa na chuki ambazo ni janga katika Taifa letu na kwa kweli hii laana ya watumishi ambao mliwachukua kwa uhitaji wenu, kwamba njooni fanyeni kazi mkiwa darasa la saba, mkiwa kidato cha nne, hawajaweza kujiendeleza kwa sababu ya mazingira pia, halafu leo mnawaondoa kazini na vilevile hamlipi stahiki zao wala hamsemi, kwa kiburi hiki, hakuna ambaye atabaki salama kwenu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo ni muhimu mkatuambia hawa watumishi wanastahili au hawastahili. Kwa sababu mliwaajiri ninyi kwa sababu mlikuwa mna uhitaji, mlijua viwango vyao vya elimu na baadhi yenu hao madereva wa darasa la saba mliowaondoa waliwaendesha ninyi katika kutimiza majukumu yenu. Lakini leo kwa sababu mmepata uhitaji mmepata wengine mmewaacha hata hamtaki kulipa stahiki zao mnaamua kujadili siku mnayotaka; tunataka Serikali ituambie maslahi ya watumishi hawa walioondolewa kwa sababu ya kiwango cha elimu, maslahi yao na stahiki zao wanapewa lini. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, acheni uonevu kwa sababu hawa mliwachukua ninyi kwa sababu mlikuwa mnawahitaji. Leo mnawaondoa hata pensheni zao hamtaki kuwapa, leo mnawaondoa hata kuzungumza nao hamtaki kwa sababu mmemaliza kazi, mmewatumia halafu baada ya kuwatumia mmeamua kuwatupa na hili mmefanya hivyo makusudi kwa sababu mnafikiri mna dola, mna nguvu ya kuwatumia na kuwafanya mnavyotaka. Ni muhimu mkasema kama wana haki wapewe na kama hawana haki basi muwaambie kuliko kufanya kama hisani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, na hili nawashangaa katika Hotuba hii ya Waziri Mkuu anasema Serikali inaendelea kutatua migogoro katika sekta binafsi na katika maeneo mbalimbali. Mnapata wapi moral authority ya kutatua migogoro kama ninyi mnafukuza kienyeji bila kufuata utaratibu? Unakwenda kumsuluhisha nani wakati wewe mwenyewe hufuati utaratibu huo katika kufukuza watu? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo ni muhimu mkaelewa kwamba ninyi mmekosa uhalali wa kusuluhisha migogoro katika nchi hii kwa sababu hata ninyi hamfuati sheria na utaratibu katika kuwaondoa watumishi kazini. Watumishi wa Umma hawa mnawanyima ruhusa kwenda kusoma lakini mnataka muwaambie wajiendeleze, wajiendeleze kwa namna gani?

Mheshimiwa Mwenyekiti, huu sio ubinadamu na wala haufai kabisa, Waziri ambaye na wewe ni binadamu na una watoto unadiriki kushiriki katika dhambi ya namna hii ya kudhulumu watu jasho lao walilotumikia nchi kwa zaidi ya miaka 15 eti kwa sababu ni darasa la saba, lakini waliwaendesha katika mapori mkitafuta kura na vilevile mkifanya majukumu yenu, leo mnawaondoa bila kuwazingatia, huu si ubinadamu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo langu la pili, ukisoma katika Hotuba ya Waziri Mkuu ukurasa wa 35, imezungumzwa habari ya ujenzi wa viwanda na hili ni jambo jema sana na mimi napenda kulipongeza kama ni la ukweli. Hata hivyo mnavyozungumza viwanda mnasema mmejenga viwanda 3,306 lakini ukiwauliza hawa Wabunge ni Mbunge gani hata mmoja anaweza akasimama, hata kumi kuonesha viwanda vilivyojengwa kwenye maeneo yao? Hakuna hata mmoja. Hivi viwanda mnajenga wapi? (Makofi/Kicheko)

T A A R I F A . . .

MHE. JULIUS K. LAIZER: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa hii angenipa Mbunge wa kawaida ningeweza kumuelewa, yeye anatetea nafasi yake na taarifa hii haieleweke kwa sababu nchi hii si Mkuranga peke yake. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninasema haya kwa ajili ya lengo la kujenga nchi yetu, tunataka Serikali ituonyeshe viwanda hivyo 3,306 viko wapi kwa majina na vinanzalisha nini ili sisi Wabunge tuweze kushuhudia Serikali katika hili jambo, ndiyo dhana yetu.

Lakini la pili tunataka viwanda vioanishe na maisha ya Watanzania, unajenga viwanda lakini unasema hakuna masoko wakulima hawa hivyo viwanda mnalisha nini kama malighafi haitokani na Watanzania wanaofanya kazi? Ni muhimu mkatuambia ni zao gani leo ambao mmezalisha viwanda zao hilo limepata soko na wakulima wamefaidi nchi yao kwa sababu viwanda vimechukua zile malighafi, mnatengeneza viwanda vya white elephant alafu baadae nchi yetu ibadilike kuwa dampo la bidhaa kutoka kwa ajili ya kulisha viwanda vya ndani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni muhimu Serikali ituambie viwanda hivyo vimejengwa wapi msituambie hii habari, nimesikia jana mtu anasema eti mashine ya kukoboa na kusaga mahindi ni kiwanda, mnasema brenda ni kiwanda, mnasema cherehani tatu ni kiwanda naona Mheshimiwa Naibu Waziri ananipiga taarifa lakini kwa wakati wake ana nafasi ya kujibu…

T A A R I F A . . .

MHE. JULIUS K LAIZER: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba muda wangu ulindwe na Mawaziri mvumilie mtajibu, kwa nini mnakosa hata Wabunge wakuwatetea subirini mtajibu. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka niseme kwamba lengo letu ni jema tu, tunataka viwanda hivi visaidie unafuu wa maisha ya Watanzania tunataka mtuambie hiyo sera inayosema ina categorization viwanda mlete categorization ya viwanda hivyo kulingana na sera mnayosema, tatizo liko wapi? Kama cherehani ni kiwanda semeni, kwa sababu mnasema eti ikiwaajiri watu watatu ni kiwanda, cherehani kuna yule anayekata nguo na anayeshona ni kiwanda tayari mtuletee hizo categorization. Tunataka viwanda vya nchi vioanishe na maisha ya Watanzani ili malighafi tunayozalisha sisi tupeleke kwenye viwanda vyetu, leo mnazungumzia kwenye... (Makofi/Kicheko)

T A A R I F A . . .

MHE. JULIUS K. LAIZER: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba ulinde muda wangu. Mimi siweze kushabikia, kwanza ni kiwanda cha kutengeneza kansa kwa wananchi halafu kiwanda ni cha zamani, ni sawa sawa umejenga shule ukijenga darasa jipya unaona umefanya maendelezo mapya unafungua. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni vizuri tukaelewa, ukizungumza taarifa hii Wizara ya Mifugo, sekta ya mifugo imezungumzwa chini ya maneno 100, sekta ambayo inagusa asilimia kubwa ya Watanzania, imezungumzwa kwa kiwango ambacho nusu page halafu imezungumzwa kupiga chapa hivi ng’ombe ni chapa? Nchi ya pili Afrika kwa uzalishaji wa mifugo unazungumza habari ya chapa, ndiyo sera ya Serikali inakuja kuzungumza kwenye taarifa ya Mheshimiwa Waziri Mkuu?

T A A R I F A . . .

MHE. JULIUS K. LAIZER: Mheshimiwa Mwenyekiti, mwelekeo ndio chapa? Nimesema taarifa iliyozumnguzwa huko unazungmza habari ya chapa hivi mwelekeo ya Wizara ya Mifugo kwetu sisi wafugaji ni chapa? Ndiyo mwelekeo Mheshimiwa Waziri Mkuu ametuelekeza, chapa ndicho tunachosema katika eneo hilo hatujatendewa haki kama sehemu ya ufugaji wa nchi hii. Tunamahitaji mengi hakuna maeneo ambayo imeelekeza tufanye nini, mnatuambia chapa, milioni mbili sijui ngapi, mnaharibu ngozi, mmeleta sheria halafu mnazungumza badala ya kutusaidia tupate malisho, maeneo ya nchi hii ni mapori mmeshindwa kutupa ameneo mnazungumza chapa, halafu tupige makofi, hatuwezi kupiga makofi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nasema jambo langu la mwisho, kuhusu upatikanaji wa fedha katika miradi ya maendeleo na hili ni muhimu sana Serikali ikajua Wabunge tunataka nini. Mimi nafikiri ni muhimu kwa sababu mmeshindwa kupeleka fedha za miradi ya maendeleo, tuchague vipaumbele vya miradi michache halafu tukaitekeleza tukawa na miradi ya mfano, hutasikia tukigombana kwenye hili Bunge kama kila Mbunge atasema mlikuwa mmependekeza kutengeneza mradi wa maji na akauona mradi wa maji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mnaleta hapa figure za maneno ili kuionesha nchi mnayo fedha, lakini kwenye maendeleo ya miradi yetu hamtuletei fedha, miradi imebaki viporo. Tunaomba kama Serikali ina nia ya kusaidia wananchi tuangalie vipaumbele vya kila Halmashauri halafu tupeleke fedha hata kama ni mradi mmoja, lakini ukakamilika ukawanufaisha wananchi. Lakini zaidi ya hivyo mkiwa mnaongeza kila kitu trilioni hizo trilioni za kwenye karatasi hazitusaidii sisi, tunayo...

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maji na Umwagiliaji kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019
MHE. JULIUS K. LAIZER: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru, lakini kabla sijachangia naomba ninukuu maneno ya Mheshimiwa Rais mwaka 2015 wakati anazindua Bunge hili aliposema maneno haya; “Wakati wa kampeni nimekutana na malalamiko mengi na ukosefu wa maji vijijini. Serikali ya Awamu ya Tano itahakikisha kwamba inaongeza kiwango cha upatikanaji wa maji kufikia asilimia 85 vijijini na asilimia 95 mijini ifikapo mwaka 2020. Tutakamilisha miradi iliyokwishaanza na kuanza miradi mipya na tunataka tuwatue akina mama ndoo kichwani. Tunatambua umaskini hauwezi kuondoka nchini kama wananchi hawapati maji safi na maji salama.”

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunajadili bajeti ya Wizara ya Maji ambapo hata wewe pamoja na kuwa uko kwenye Kiti umeshindwa kuvumilia maana hupati nafasi ya kuchangia, umezungumza habari ya uhitaji wa maji katika eneo lako. Uhitaji wa maji katika Taifa hili imekuwa ni janga kubwa sana na Bunge hili ni lazima lifanye uamuzi ambao utaisaidia nchi hii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeangalia vitabu vilivyopita, nimeangalia Wizara ya Afya ina page 47; nimeangalia hotuba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu ina page 45, nimeangalia vitabu kama vitatu, vinne hivi. Kitabu hiki cha Maji kuonesha kwamba Serikali imeshindwa kutekeleza iliyoahidi inapage zaidi ya 280. Hii ni kuonesha kwamba maneno mengi ni kutafuta kujitetea badala ya kutekeleza kile ambacho tumeahidi. Kama Serikali ingetekeleza asilimia hata kumi ya kilichoandikwa humu, Taifa hili lingefika mahali pazuri na tungeondokana na tatizo la maji. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa ya REPOA ya mwaka 2018, asilimia 42 ya Watanzania wanakiri kwamba tatizo la maji limekuwa kero zaidi ya asilimia 34 ya mwaka 2014. Kadri siku zinavyokwenda, population ya Watanzania inaongezeka. Kwa hiyo, hata kama tungekuwa na maji kidogo miaka ya nyuma, kadri siku zinavyoenda lazima uhitaji wa maji uwe mkubwa. Mipango ya Serikali katika kutafiti, hebu tusaidieni mnataka Watanzania waishije ili akina mama waache kupoteza usiku na mchana kutafuta maji? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali ya CCM ambayo imeahidi kwenye Ilani ya CCM ya 2015, imesema itasaidia upatikanaji wa maji kutoka 67% mpaka 85%. Leo mnapeleka bajeti kwa asilimia 22, leo mnapeleka bajeti kwa asilimia 15, mnataka sisi tuamini nini mnachotuahidi? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukienda mbele, katika Kamati wanasema asilimia ya bajeti iliyopelekwa ni 22%, lakini Mheshimiwa Waziri anasema 56%. Kwa mujibu wa kanuni, taarifa zote zinazokuja Bungeni lazima zipitishie kwenye Kamati, Kamati i-verify. Nataka Mheshimiwa Waziri atuambie, tuamini taarifa ipi kati ya Kamati inayosema mmepeleka 22% na wewe unayesema tumepeleka 56%? Tunamdanganya nani hapa? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Taifa hili linahitaji maji. Mwaka 2017 tulisema tunataka angalau tuweke shilingi 50 kwa ajili ya maji vijijini, mkakataa. Mkatuambia mna fedha kutoka India dola milioni 500. Kwenye kitabu hakuna hata nusu page, hata nusu maneno uliyoahidi kwamba hizo fedha ziko wapi? Kwa hiyo, mnakuja mnadanganya Bunge ili tupitishe bajeti, lakini ukienda kwenye utekelezaji mnasahau hata maneno yenu ambayo mliyasema mwaka 2017. Fedha zile za India hiyo dola milioni 500 ziko wapi? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mnashindwa kutekeleza bajeti hii kwa sababu tunawashauri wekeni fedha kwenye mafuta, hamtaki. Mnatafuta fedha hampati; lakini mnakuja hapa Mheshimiwa Waziri unatuambia mmepeleka hela ya maji kwa asilimia 26, halafu usiliombe Taifa radhi kwa kuacha Watanzania wateseke, halafu mnasema mnawasaidia akina mama. Badala ya kuwasaidia kuwaondoa ndoo kichwani, mnawatwisha ndoo kichwani, yaani mnaweka juu ya ndoo. Hata Naibu Waziri amejiridhisha, anasukuma kila siku toroli ya madumu ya wanaotafuta maji. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ili kutekeleza ahadi hizi ni lazima Serikali ioneshe commitment nzuri ya kupeleka fedha. Naomba kama Bunge tukubaliane tuweke shilingi 50 ili tupate fedha ya kutosha kwa ajili ya miradi ya maendeleo ya vijijini. Bila hivyo hili tatizo litakuwa kubwa na maneno mazuri ya Mheshimiwa Waziri, ni mazuri sana na ni mengi mno, lakini utekelezaji wake kama hauna fedha huwezi kutekeleza. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niseme kuhusu Mamlaka ya Maji katika maeneo ya Halmashauri ambapo Serikali iliahidi kutekeleza kwa kusaidia fedha za ruzuku kwa ajili ya kujiendesha. Mheshimiwa Waziri atusaidie, kama Serikali iliahidi kutekeleza na kusaidia, kwa nini fedha haziendi na mpaka mwisho TANESCO inawakatia wananchi umeme na sisi tunakosa maji kwa kosa ambalo siyo la wananchi. Maana wananchi wanalipa bills zao lakini Serikali haipeleki. Kwa nini Serikali isiadhibiwe mnaadhibu raia ambao hawana makosa wala hawahusiki katika hili jambo?

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama mnashindwa kuchangia jambo hili, mseme hamuwezi kuliko kutudanganya na kuwaumiza wananchi wetu. Tukimpigia Mheshimiwa Waziri wa Nishati anasema sihusiki, tukimpigia mtu wa Hazina anasema hahusiki. Nani anahusika katika madeni haya ambayo mnawanyanyasa na kuwatesa Watanzania? Mnakata umeme kwenye maji ambayo akina mama wako hospitalini! Akina mama wanajifungua ninyi mnakata maji, hamjali. Sense of human iko wapi katika jambo hili na kosa siyo la kwao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme machache katika Jimbo langu, naomba Mheshimiwa Waziri anisaidie, ahadi ya Serikali ya kukarabati mabwawa katika Kijiji cha Esilalei ambao Mheshimiwa Rais aliahidi wakati wa ziara yake ya kuomba kura, inatekelezwa lini?

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna mradi wa maji wa Monalo na Mheshimiwa Waziri anakuja, maana alikuja Monduli. Tangu 2011 mpaka leo wananchi wanaendelea kulalamika hawapati maji na ule mradi umegharimu zaidi ya shilingi bilioni mbili. Huo mradi unakamilika lini na Serikali inapata ukakasi gani kuwashughulikia wote wanaokwamisha mradi huu?

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ni miradi ya umwagiliaji; katika miradi ya umwagiliaji Mheshimiwa Waziri anafahamu, alikuja na nilimtembeza pamoja na umri wake lakini alitembea. Tulienda Selela akaahidi, tulienda Mto wa Mbu akaahidi, tulienda Engaruka akaahidi kwamba watatupatia fedha kwa ajili ya ukarabati wa miundombinu ya umwagiliaji katika mabonde hayo. Kwenye bajeti hii sijaona hata mahali ametaja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri anatutakia nini? Mbona tulimpokea vizuri naye alituahidi mengi? Mbona sioni hata nusu ya alichotuahidi kutusaidia? Alituahidi kutengeneza kile chanzo cha maji Ngaramtoni Mheshimiwa Waziri alifika mwenyewe, Monduli ilikosa maji akatuahidi. Mheshimiwa Waziri tumemkosea nini au tulimpokea vibaya? Wananchi wa Monduli wamekukosea nini? Alituahidi! Hakuna kwenye kitabu chake hata mahali ametaja hata ahadi moja aliyoahidi, kosa letu nini? (Makofi)

Mheshimiwa Waziri ulikuwa unatudanganya uondoke au ulikuwa unamaanisha kutusaidia kutatua matatizo ya maji? Ninaomba uniambie, wananchi wa Monduli wanakuamini na uliwaahidi, katika ahadi zako zote, mwaka huu unatutekelezea nini? Hakuna hata moja umetaja. Mheshimiwa Waziri kwa nini? Tumekutembeza Jimbo zima, tumeweka mafuta zaidi ya magari 20 tumekusindikiza, tumeenda na wataalamu, tumekuletea maandiko Mheshimiwa Waziri. (Kicheko/Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nitoe mapendekezo matatu; moja, kwa kuwa miradi hii ya vijiji kumi na miradi mingi inaonekana haitoi maji kwenye nchi hii, naomba Serikali ifanye special auditing kwenye miradi yote ya maji ya nchi hii ili tujue ni miradi mingapi inafanya kazi na miradi mingapi haifanyi kazi mtuletee Bungeni. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, natamani nilishawishi Bunge tuweke azimio kwamba hatutapitisha bajeti ya Wizara hii mwakani mpaka mmetuletea special auditing ya miradi yote ya maji, maana mnatengea fedha miradi lakini ukienda kwenye mradi, hakuna maji. Tunataka kufanyike special auditing kwenye miradi yote ya maji nchi hii. Tufahamu ni miradi mingapi inatoa maji na mingapi haitoi maji. Tuna value for money. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niliwahi kumwambia Mheshimiwa Waziri kuwa katika Halmashauri ya Wilaya ya Monduli waliwahi kuleta fedha za consultant aliyekuwa anasimamia ile miradi hakufanya kazi, lakini Wizara ilituma fedha tulipe, nikasema hailipwi. Wizara inaniambia kwa nini unazuia, kwani ni hela zako? Nikasema huyu mtu hakufanya kazi, hakustahili kulipwa. Imekuwa ni uchochoro wa kupitisha fedha za Serikali. Wale wanaoitwa consultant wanawaambia walete engineer wanaleta hawa ma-technician wao mimi siwajui majina yao, lakini hakuna wanachofanya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine, ni muhimu Serikali ifanye tathmini ya miradi ambayo imetekelezwa na imekamilika na ambayo haijakamilika na iseme kwamba ni lini miradi hii itakamilika. Tumechoka na ahadi ya kwamba miradi itatekelezwa, miaka 10, miaka 15 mnatekeleza tu. Tutaanza lini mpya? Maana hakuna hata mradi mmoja mmeanza upya mnatekeleza ile ya zamani tu. Hata ule wa maji kutoka Ziwa Victoria kwenda Nzega ni ya zamani mnatekeleza. Mnamaliza lini mwanze hii mipya? Ni muhimu mkatuambia kila mradi unaanza lini na unakamilika lini ili wananchi wawe na imani ya kwamba Serikali inafanya kazi na wao kuna siku watapata maji. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Mifugo na Uvuvi
MHE. JULIUS K. LAIZER: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuchangia katika hotuba hii ambayo nitapata taabu kidogo kulingana na mazingira yenyewe ya sekta kwa sababu nina maslahi nayo mapana kwa asilimia mia moja.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia nitapata taabu kwa sababu Mawaziri wlaiopo katika Wizara hii wote ni vijana na ni marafiki zangu ambao tunafahamiana kwa muda mrefu lakini ambao kwa kweli katika Wizara hii wameshindwa kabisa kabisa kuonesha ujana wao katika Wizara husika. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, katika nchi yetu kuna makundi makubwa manne; kuna kundi la wafanyakazi, wakulima, wafugaji na kuna wavuvi. Kama Serikali inatafuta ugomvi kwa makundi haya yote manne hii Serikali inategemea ku-survive kwa mazingira gani?

Mheshimiwa Naibu Spika, miaka mitatu mfululizo hawajapandisha mishahara ya watumishi, miaka mitatu mfululizo wameshindwa kupeleka mbolea kwa wakulima, miaka mitatu mfululizo wameshindwa kutuletea hata shilingi ya wafugaji. Mheshimiwa Waziri, wanategemea nini?

Mheshimiwa Naibu Spika, kazi ya Serikali ni kwenda kuomba ridhaa kwa wananchi wakipewa wanakusanya kodi kwa niaba ya wananchi, wanapeleka huduma. Wao wanakusanya, hawatuletei huduma. Mkataba wetu kwa maana ya wananchi na Serikali tunakutana wapi?

Mheshimiwa Naibu Spika, inawezekana wakaona ng’ombe kama chakula, wakaona kama kitoweo wanavyoenda kunywa maziwa pale, wakala nyama, wakala samaki, wakala kuku, wakala mayai, wakashiba mkaja hapa wakaendelea. Sisi ni uchumi! Sisi ni maisha yetu! Mheshimiwa Waziri anakubalije kumeza dhambi hii? Anakusanya bilioni ishirini na sita kutoka kwetu halafu anaandika kwenye bajeti yake hajapeleka hata shilingi. Kama binadamu, yeye anajisikiaje? Huu ni unyang’anyi uliohalalishwa na sheria.

Mheshimiwa Naibu Spika, kweli Mheshimiwa Waziri, anatuletea bajeti, ndugu yangu, rafiki yangu kweli? Halafu amekusanya bilioni ishirini na sita, wameshindwa hata kutupa shilingi 100, kweli Mheshimiwa Waziri? Wafugaji wa nchi hii tumewakosea nini Serikali? Wizara zote wamepelekewa kidogo, sisi hata shilingi hawajatuletea, fadhila wanazotupa ni kutunyang’anya ng’ombe, fadhila wanazotupa ni kutunyang’anya samaki, nyavu, kutufilisi halafu kweli? Hata basi wangekuwa wanatunyang’anya, lakini wangeturudishia hata sehemu basi, kwa nini Wizara hii inyimwe fedha kuliko Wizara zote katika nchi yetu? Tumewakosea nini tuwaombe radhi? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa miaka yote ya nchi hii, Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Serikali haijawahi kupeleka ruzuku; kilimo ina ruzuku, sisi hatuna! Sisi tunataka watutengenezee mazingira tufuge, lakini kweli wanakusanya hela, wanatunyang’anya hela kwa nguvu halafu hawaturudishii hata kidogo?

Mheshimiwa Naibu Spika, Sera ya Mifugo ya Mwaka 2006 na Mheshimiwa Waziri anajua ambayo imefanyiwa marekebisho ya tatu mwaka 1983 na 1997, imeeleza changamoto nne za wafugaji. Moja, ilizungumza habari ya ukosefu wa mikopo na mitaji ikazungumza habari ya magonjwa, ikazungumza habari ya ardhi, malisho ya maji na maeneo mengine ya wafugaji.

Mheshimiwa Naibu Spika, miaka 13 baadaye serikali hii imeshindwa kutatua hata tatizo moja ambalo sera hii imeainisha kwenye kitabu cha Serikali. Wanahitaji miaka mingapi kutusaidia malisho na wanahitaji miaka mingapi kutusaidia majosho? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Waziri anasema amepeleka zero, kwetu sisi, tunataka watuwezeshe tu. Hii sera wametunga wenyewe, maeneo mengine inasema kabisa kwamba, matatizo haya yametokea kwa sabahu maeneo ya wafugaji yamevamiwa na wakulima na maeneo mengine yamevamiwa na uwekezaji wa National Parks, lakini ranch za Taifa wamewapa watu hawataki kuwarejesha wala hawataki kuendeleza. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, inaonekana katika nchi yetu kwa mujibu wa takwimu 60 hectors million ni kwa sababu maeneo yanafaa kwa ajili ya nyanda za malisho ya mifugo. Mpaka leo kwenye ramani ya nchi hii miaka 50 ya uhuru hakuna mahali hata pamoja kwa mujibu wa sheria ya mwaka 2010 iliyotangaza rasmi maeneo ya nyanda za malisho ya wafugaji, lakini wanayo sheria, hawatekelezi sheria wanatunyanyasa, hawatutengei maeneo ya malisho ya mifugo, tukiingia kwenye hifadhi wanatuuwa, tukiingia kwenye parks wanatuuwa, tukiingia kwenye maeneo ya mapori wanatuuwa, wanatunyang’anya ng’ombe wetu wanauza, sisi twende wapi? Watueleze leo? Tumepata soko Kenya, juzi wameenda wamezuia tusiuze, hawana masoko tupeleke wapi? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hakuna mahali pa kulisha, hakuna maji, hakuna dawa, hakuna ruzuku wanayotuletea. Tunataka kuuza, tumekosa masoko ndani tumepata masoko nje wanataka kutu-charge kodi kwa lipi walilowekeza? Kwa nini wanataka kuvuna pasipo kupanda? Kwa nini wao wanataka kuvuna pasipo kupanda? Wamewekeza nini kwenye mifugo wanatukamata kila siku? Wametuletea nini? Wanasema wasipeleke nje, tupe masoko basi; hakuna haki pasipo wajibu. Wizara wajibu wao ni nini katika hili wanalotu- charge kila siku? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, upelekaji wa fedha. Mwaka 2015/2016, walitenga shilingi bilioni nne hawakupeleka hata shilingi moja. Mwaka 2016/2017 walitenga bilioni nne hawakupeleka hata shilingi, mwaka jana bilioni nne hawakupeleka hata shilingi, miaka mitatu mfululizo, hivi wanafikiri sisi tunaishije? Wanatutaka nini wafugaji wa nchi hii? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, wao wamebaki kukusanya kodi na kutupiga na kutunyang’anya ng’ombe, lakini wao hawatuchangii chochote. Natamani wafugaji wa nchi hii siku moja, wiki moja tu wawanyime maziwa, wawanyime nyama, mayai, samaki, kama hawajafa humu ndani, kwa nini? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, utitiri wa kodi katika sekta ya mifugo. Hii Mheshimiwa Waziri naomba atuambie leo, mtu akitaka kuwa na Export License ya Mifugo anatakiwa kulipa Sh.2,500,000/=, lakini wakati huo huo anatakiwa kujisajili kwenye Bodi ya Nyama Sh.100,000/=,
lakini wakati huo huo anatakiwa alipe Movement Permit Sh.2,500/= kwa kila ng’ombe. Akipeleka pale Namanga anatakiwa kulipa Sh.20,000/= kwa kila ng’ombe, anatakiwa kulipa Market Fee Sh.5,000/= kwa kila ng’ombe, anatakiwa kulipa Sh.2,000/= mpaka Sh.3,000/= ya hela za Halmashauri.

Mheshimiwa Naibu Spika, ng’ombe mmoja tu akisimama wao wanachukua Sh.50,000/= hawajachangia chochote, hawajafanya chochote, wanadai hizo fedha. Kama mtu ana Transport License ya Mifugo anapeleka Kenya kwa nini wana-charge ng’ombe mmoja mmoja tena fedha? Kama sio wizi ni nini huu? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kama mtu ana Permit ya kusafirisha mifugo kwa nini wanatu-charge Sh.20,000/= kule Namanga? Tumewakosea nini sisi wafugaji wa nchi hii? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sisi tunafuga kwa tabu, sisi tunachunga, sisi tunaondoka asubuhi umekunywa uji unarudi saa 12.00 jioni. Tunateseka sisi kutafuta malisho, tunateseka kutafuta maji, badala ya kutuonea huruma wanatu-charge hata kile kidogo tunachotafuta. Hii sio fair, linaniumiza kwa sababu linanigusa. Kwa nini wanatuwekea tozo hizi? Kwa nini wameondoa tozo nyingine kwenye mazao mengine yote mifugo wameacha? Kwa nini watu-charge mara kumi kumi? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mimi nina leseni ya kupeleka ng’ombe Nairobi nimepata soko, unaenda kunizuia tena pale unani-charge Sh.20,000/= kila ng’ombe, nimekukosea nini? Kwa nini unatu-charge hiyo 20,000/=? Atuambie Waziri hizi tozo atapunguza lini, mbona kwingine wanapunguza? Au wana lengo la kuua mifugo? Waue basi tubaki hatuna, kwa sababu, huu ni unyang’anyi wa makusudi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inapata hasara katika sekta ya mifugo; nchi yetu ni nchi ya tatu Afrika kwa upatikanaji wa ng’ombe, lakini Mheshimiwa Waziri anajua tunapoteza zaidi ya bilioni mia moja ishirini kwa sababu ya uingizaji wa maziwa nchini, tunapoteza zaidi ya shilingi bilioni saba kwa sababu ya uingizaji wa nyama nchini. Tunapoteza zaidi ya bilioni hamsini na saba kwa sababu ya upelekaji wa ngozi nje.

Mheshimiwa Naibu Spika, hivi ni aibu gani Taifa linaloongoza kwa mifugo tunaongoza kuingiza nyama na maziwa na hii mifugo yote tunapeleka sisi Kenya wana- process wanatuletea sisi, kwa nini? Hivi hawajisikii aibu tunapoteza rasilimali za Taifa kwa mazingira ambayo Serikali inapaswa tu kuweka viwanda ili tuuze ndani humu? (Makofi) (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, wameshindwa kujenga viwanda, hakuna muunganiko kati ya viwanda na mifugo, tukipeleka nje wanatu-charge wanasema tusitoroshe, tutatorosha tu. Tutatorosha tu na naamini mpaka watengeneze barabara ya kuzunguka mipaka hii, ili wazuie ng’ombe tumeshauza wengi sana. Watutengenezee mazingira rafiki ndani ya nchi ili wafugaji wapate masoko wauze nchini. Wasitembelee migongo yetu kwa sababu wao wameshindwa kutimiza majukumu yenu, wajenge mazingira rafiki. Tunaomba watuambie hizo tozo wataziondoa wakati gani? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ushauri wangu. Naomba nitoe ushauri kwa Serikali, moja, wafugaji watengewe maeneo yao na yalindwe kisheria; Ranch za Taifa ambazo wawekezaji wameshindwa kuendeleza watupatie tuendeleze sisi, hata tukilipia kodi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili, watuondolee tu kodi kwenye dawa za uogeshaji wa mifugo na chanjo za mifugo, sisi tutanunua, lakini waondoe kodi ili na sisi tuweze kuendesha wenyewe.

Mheshimiwa Naibu Spika, tatu, mapori ya akiba yatolewe yarejeshwe kwa wananchi.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Maji na Umwagiliaji
MHE. JULIUS K. LAIZER: Mheshimiwa Naibu Spika, awali ya yote niungane na wenzangu kuwapa pole wazazi wote waliopoteza watoto wao katika ajali mbaya. Mungu aendelee kuwafariji na kuwatunza.

Mheshimiwa Naibu Spika, naamini kila mtu na hakuna hata Mbunge mmoja anayekataa kwamba, kuna tatizo la maji nchini, kila mtu anakiri hilo na tatizo hapa inaonekana ni fedha. Kama kweli Bunge hili lina wajibu wa kuisimamia Serikali na kupitisha bajeti ya Serikali ni lazima tuungane kwa pamoja kuhakikisha Serikali inaongeza fedha katika bajeti ya maji ili kuwasaidia wananchi wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, wewe ni mama na bahati nzuri kuna Wabunge wengi wa Viti Maalum wanaotokana na akinamama. Mimi kwa umri wangu huu sijawahi kuchota maji hata bombani kwangu pale ndani, nje ya nyumbani kwangu. Ni utamaduni na desturi ya Watanzania na ya
Waafrika wengi kwamba, akinamama ndio sehemu kubwa wanashughulikia matatizo ya watu majumbani. Kama kweli tunataka tuwasaidie kama sio kuwatwisha ndoo kichwani ni kuwatua ndoo kichwani, tuongeze bajeti kwa ajili ya kuwanusuru akinamama. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hata nyakati nyingine hata kazi za kufanya za kuwasaidia watoto wao hawafanyi, kwa hiyo jambo hili ni serious sana. Kama kweli, tuna nia njema ya kulisaidia Taifa hili, tuisaidie Serikali ikaongeze bajeti, heri hata ikasimamisha shughuli nyingine ili wananchi wakapate maji. Wakati wa kiangazi mwaka huu mnajua jinsi nchi yetu ilivyopita katika janga la ukame; kama hali ikiendelea hivyo nani atakuwa salama katika nchi yetu? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, mimi naamini kama tukiamua kama Bunge, tuirudishe bajeti Serikali ikaongeze fedha katika Wizara hii ya Maji ili wananchi wetu wapate maji. Kama tunakubaliana kuwasaidia akinamama hawa na si kwa unafiki, turudishe bajeti hii ili Serikali ione ni namna gani itafanya ili kuwasaidia akinamama kuondokana na tatizo la maji. Kama ni punda anayeswaga ni mama, kama ni ndoo ni mama anayebeba kichwani, kwa sababu hiyo na sisi wote tunatokana na mama, naomba tuungane kuwasaidia akinamama kuondokana na tatizo hili la maji. Hatujui mateso ya mtu anayebeba ndoo ya lita 20 kichwani kwa kilometa mbili au tatu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kama ni uchungu wanajua hawa akinamama, tuwasaidie kuondokana na tatizo hili la maji nchini. Sikusudii kuzungumza matatizo ya maji kwenye jimbo langu kwa sababu hata fedha mlizotenga hazifai hata kuzungumza, lakini kama tuna nia njema turudishe bajeti hii, Serikali ikapitie upya, ili jambo hili lipate kufikia muafaka. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naamini kama Serikali ina nia ya dhati ya kuwasaidia Watanzania; kama Serikali ina nia ya dhati ya kusimamia suala la maji nchini itasikiliza kilio cha Waheshimiwa Wabunge wengi hapa ndani ambao kila mmoja kwenye jimbo lake anajua adha ya kwanza tunayokutana nayo kama Wabunge wa vijijini ni suala la maji vijijini. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, wananchi wetu hata kwenye mikutano hawaendi kwa sababu ya maji; na naamini hata Waheshimiwa Wabunge hawa wanaosimamia Wizara hiyo wanatoka vijijini, wanajua matatizo na adha ya maji. Naibu Waziri alikuja Monduli, aliona mazingira ya Jimbo lile; miaka 50 ya uhuru wananchi wetu bado hawajui watachota maji wapi, miaka 50 ya uhuru tunahangaika na akinamama wanaendelea kununua ndoo sh. 500/=, hii haikubaliki mahali popote, lazima kama Bunge tuisaidie Serikali kutafuta Suluhu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ukienda Monduli maeneo ya Mfereji, maeneo ya Sepeko, maeneo ya Moita, maeneo ya Esilalei na maeneo mengine ya Lepurka ambayo ni kame, miaka 50 ya uhuru wananchi wale hawajawahi kuona maji ya bomba. Naomba Serikali isikie kilio cha Waheshimiwa Wabunge ikarekebishe bajeti hii ili iwafae wananchi wa leo na vizazi vijavyo kwa ajili ya maisha yao ya sasa na maisha yao ya baadaye.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba Waheshimiwa Wabunge tuache itikadi katika hili, tuisimamie Serikali ikarekebishe bajeti yake. Haiwezekani bajeti ya bilioni mia tisa unapunguza kwa asilimia 30 halafu hata ya mwaka jana umepeleka kwa asilimia 19 halafu upunguze, leo utapeleka kwa asilimia ngapi? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba Serikali itwambie ni kwa nini bajeti ya maji ambayo imetekelezwa kwa asilimia 20 imeshushwa kutoka ile bilioni mia tisa kuja bilioni mia sita, ni kwa nini? Ni vigezo gani vinatumika? Au ni mpango gani Serikali inao katika kuondokana na tatizo la maji nchini? Kama haiwezekani tu-admit kwamba hili ni Janga la Kitaifa na hili tatizo la maji sasa Serikali imeshindwa, ili tutafute namna nyingine hata wahisani kutusaidia. Hatuwezi kwenda

kwa namna hii kama hatukubaliani kusimamia suala la maji ambalo ni tatizo kubwa nchini. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nikushukuru.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi
MHE. JULIUS K. LAIZER: Mheshimiwa Mwenyekiti, nami nikushukuru kwa kunipa nafasi ya kuchangia bajeti hii iliyopo mbele yetu ambayo kimsingi wote tunakubaliana kwamba kilimo ni uti wa mgongo wa Taifa letu. Nataka nihoji kwa sababu katika mijadala mingi tumekuwa na hoja inayozungumzwa kwamba Serikali ina dhamira njema ya kuwasaidia Watanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka kuhoji kwamba dhamira ya kweli ya Serikali hii ya Chama cha Mapinduzi katika suala la kilimo na mifugo ipo wapi katika bajeti hii? Hivi dhamira ya kweli ya Serikali ni ya kutoa asimilia tatu ya bajeti yake kwa ajili ya sekta ambayo ni Uti wa Mgongo wa Watanzania? Tunataka Serikali ituambie kama asilimia 80 au 70 ya Watanzania ni wakulima na wafugaji, dhamira ya Serikali katika kuwasaidia wakulima na wafugaji hawa iko wapi?

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeshangaa katika kitabu cha Mheshimiwa Waziri huku wameweka ng’ombe huku mbele na samaki, huku nyuma wameweka kilimo ambacho kinaonesha mazao ya wananchi. Wao wamechangia nini, kwa nini wanajisifu kwa kitu ambacho hawachangii chochote katika kuwanufaisha Watanzania? Nini mmechangia katika mifugo wanaiweka huku wanaona imenawiri sana, nini wanachangia katika kilimo hiki wanachoona mazao yamenawiri sana?

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka Wizara ituambie hizi picha walizotumia kwenye kitabu hiki copy right yake iko wapi wakati hawachangii chochote, wanatenga bilioni 100 lakini mnapeleka bilioni tatu. Dhamira yao haiwasuti, wanachukua picha ya ng’ombe zetu wanaweka kwenye kitabu chao lakini Wizara hii hawachangii chochote katika kusaidia maisha ya wananchi, hatukubaliani nayo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili tunataka dhamira ya Serikali katika hili ionekane katika matendo ya kweli, kama dhamira haionekani katika matendo dhamira hiyo imekufa. Katika hili dhamira imekufa kwa sababu hakuna chochote ambacho Wizara imefanya, nchi hii inaongoza kwa mito na maziwa lakini hakuna hata mradi mmoja wa mfano Wizara imeanzisha kwa ajili ya kuonyesha kilimo cha mfano kwa Watanzania. Sasa wanajisifu nini kama Wizara?

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo Wizara hii inaendelea kukubaliana na utekaji na uuzaji wa mifugo ya wafugaji ambao peke yake katika Wizara hii ndiyo mifugo inauzwa hata bila ya hukumu ya mahakama. Ni mahali ambapo Wizara ya Maliasili inanyanyuka inauza ng’ombe inavyotaka. Ni wapi umeona kwenye nchi hii mali za watu zinataifishwa bila mahakama kutoa hukumu, Wizara imenyamaza. Wizara hii haioneshi ni namna gani inawasaidia wafugaji kuondokana na matatizo yanayowakabili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mbaya zaidi mnasema ni uti wa mgongo lakini wameitenga Wizara ya Maji na Mifugo katika bajeti hii hapa. Nataka nishauri Serikali, suala la maji kwa maana ya umwagiliaji lihamishwe kutoka Wizara ya Maji lipelekwe kwenye Wizara ya Kilimo na Mifugo kwa sababu huwezi kuendesha kilimo wala mifugo bila kuwa na maji ya uhakika. Tusipofanya hivyo, tutaona bajeti ya Wizara ya Maji inakuwa kubwa lakini Wizara hii ya Mifugo na Kilimo haitakuwa na chochote na wao hawatatekeleza miradi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inapata kigugumizi gani kuhamisha suala la umwagiliaji ikapeleka kwenye Wizara inayohusika na kilimo ili angalau tuwe na miradi michache kwenye Ziwa Tanganyika, Ziwa Viktoria ili angalau tuwe na miradi michache tunayosema kama nchi tumeweza kuzalisha. Ni nchi pekee tuna maziwa makubwa lakini kiangazi cha miezi miwili tu, mitatu nchi tunalia njaa halafu tunasema kwamba tufanye kazi, kazi ipi ambayo tunafanya kama Serikali haisaidii wananchi wake kuondokana na matatizo tuliyonayo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo nataka niishauri Serikali, kumekuwa na tatizo la muda mrefu kati ya wafugaji na wanyamapori lakini wameanzisha na zoezi la kuweka ng’ombe chapa. Ili waweze kufanikisha zoezi hili ni muhimu kuweka miundombinu ya maji katika maeneo ya wafugaji. Kama hawajaweka miundombinu mifugo itahama tu na kama itahama wataishia kutunyanyasa na kutunyang’anya mifugo yetu yote. Nataka niwaambie hawatakuwa wamewasaidia wafugaji ambao wameonekana kama kundi ambalo halina haki katika nchi yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, namba hili suala la kuweka ng’ombe chapa lisimame mpaka Serikali itakaposema ni kwa namna gani imeboresha mazingira katika maeneo haya ambayo wanataka mifugo iwepo. Huwezi kuniambia nichunge ng’ombe mahali ambapo hakuna maji. Bahati nzuri Naibu Waziri naye ni mfugaji, hivi anavyosema aweke chapa ng’ombe kule Ngorongoro wakati hajaweka masuala ya maji katika eneo hilo anategemea wale wapiga kura wake waende wapi? Nataka yeye mwenyewe awe mfano kwa kuisaidia Serikali kuona kwamba hawezi kutenga eneo la mifugo bila kuboresha mazingira ya upatikanaji wa huduma za maji na majosho katika maeneo husika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo langu la mwisho, kwa nini sekta ya mifugo haina ruzuku.
Hali ya Uchumi wa Taifa Kwa Mwaka 2016 na Mpango wa Maendeleo ya Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018
MHE. ANTHONY C. KOMU: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi nami niweze kuchangia katika mjadala huu ambao ni muhimu sana kwa Taifa letu.

Mheshimiwa Spika, kwanza nianze kwa kusema kwamba naunga mkono maoni yaliyotolewa na Kambi Rasmi ya Upinzani na niiombe sana Serikali kwamba mara nyingi ukitaka kwenda vizuri ni vizuri ukajiangalia kwenye kioo. Sasa haya maoni yaliyotolewa hapa kama Serikali ikiamua kujiangalia kwamba upande wa pili wanaonaje, inaweza ikasaidia sana na ikawa na mchango mkubwa na tukakwepa kwepa haya mambo ambayo jinsi tunavyokwenda mbele tunaendelea kuumbuka. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mimi kwa kweli napata shida sana Wabunge wenzangu ambao wanawakilisha Watanzania ambao tunajua hali zao wanavyosema kwamba hii bajeti ni bajeti ya aina yake, ni bajeti nzuri. Kwa sababu nikianza kwenye kuangalia vipaumbele, nashangaa kabisa kwamba tunavyoweka ndege katika nchi hii kama kipaumbele sijui tunatumia vigezo gani, kwa sababu ukienda kwenye huu Mpango wa Maendeleo wa Taifa ukurasa wa Nane kuna uchambuzi umefanyika pale unaoonesha key sector katika pato la Taifa, hakuna ndege na katika michango yote hakuna ndege. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Waziri wa Fedha Mheshimiwa Mpango anafahamu kwamba unapotaka kuwekeza kwenye kitu chochote ni lazima uende kwenye kuangalia ni wapi utapata matokeo makubwa (comparative advantage). Sasa inavyoamuliwa kwamba tukawekeze ndege wakati huu shilingi karibu trilioni moja, kwa sababu tumeshanunua ndege mbili, tumetenga billioni 500, tunachukua madeni yote ya ATCL na kadhalika.

Mheshimiwa Spika, ukiangalia kwenye hili jedwali ambalo nimelirejea, mchango wa kilimo ni asilimia 29 kwenye pato la Taifa. Hata hivyo, ukienda kuangalia leo kwenye bajeti ya kilimo cha umwagiliaji tumetenga billioni 24, tena hizo bilioni 24 bilioni 15 zinatoka nje, za kwetu tulizotenga ni bilioni tano. Leo hii tunanunua chakula kutoka nje ya nchi, ukienda kuangalia imports za nchi hii asilimia tisa ni chakula, tunawezaje kupiga hatua? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nashangaa kama tunakwenda kuweka pesa nyingi namna hiyo na tunasema na tunakaa hapa kweli tunajivuna kwa sababu najaribu ku-recall Mzee wangu rafiki yangu sana Mheshimiwa Keissy siku moja hapa Mheshimiwa Heche alisema anataka kiwanja Tarime, Keissy akasimama akasema kule kwao wanataka barabara tena za changarawe, leo hii tunakuja hapa tunapiga makofi kwamba eti ndege ni kipaumbele. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tukienda kuangalia competency yetu kwa maana ya soko la ndani silioni, ukienda kuangalia competency yetu Kimataifa kwa maana ya kushindana na kupata faida, sioni, hatuna economies of scale, hatuna ukubwa wa kuweza kushindana na ikawa ni faida. Kwa hiyo, suala la biashara ya ndege is a high risk business, ndio maana watu wanakwendaga kukopa sio kulipa cash.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, nafikiri kwamba huu ni mkenge ambao tumeamua kuuvaa na nafikiri kama tunawakilisha kweli Watanzania ambao siamini kama wanafika hata 10,000 ambao wanaweza wakawa na manufaa na hiyo ndege. Nafikiri tungesimama kama Bunge tukasema kwa kweli huu uwekezaji wa aina hii tumepotoka. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nikienda kwenye hoja yangu ya pili, nikienda kwenye hoja yangu ya pili…

TAARIFA .....

MHE. ANTHONY C. KOMU: Mheshimiwa Spika, siipokei kwa sababu haina ukweli wowote kutokana na rejea mbalimbali ambazo ziko mbele yangu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hoja yangu ya pili ni kwamba, bajeti hii ukiiangalia kwa makini ina asilimia kubwa sana ya kubahatisha, asilimia kubwa sana ya kupiga kamari. Kwa sababu tuna pesa ambazo tumesema trilioni 7.7 tunakwenda kukopa tena ndani kwa kiasi kikubwa, tuna trilioni 3.9 ambazo tunatarajia tupate kutoka nje ya nchi kwa maana ya misaada kwa maana ya mikopo na kadhalika.

Mheshimiwa Spika, ukweli na uhakika wa kupata fedha hizi ni mdogo sana, bado tuna tatizo la Zanzibar ambalo linatuletea matatizo. Kwa hiyo, nafikiri tukitaka kuwa realistic bado tuna kazi kubwa ya kufanya. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hoja nyingine ni kuhusu mradi wa makaa ya mawe ya Mchuchuma na chuma cha Liganga. Ukiangalia kwa kauli ya Waziri mwenyewe anasema huu ndio msingi mkuu wa kuchochea mageuzi ya viwanda katika nchi hii lakini ukienda kuangalia wanasema kila kitu kimekamilika, ukienda kujaribu kusoma katika Wizara zote unaona kwamba tatizo lililopo sasa hivi ni Serikali yenyewe haijatoa GN, are we serious?

Mheshimiwa Spika, kweli tuko serious kwamba tunataka kwenda kwenye mageuzi ya viwanda katika speed ya namna hiyo, wanasema mwekezaji amekwisha patikana na ameshatenga pesa, lakini Baraza la Mawaziri lilikaa mwaka jana likaamua kwamba wakapitie upya na kuona vivutio vile vilivyopo vina maslahi gani kwa Taifa. Ni jambo zuri lakini huoni kwamba hiyo ni ndoto katika hali ambayo

unasema unaye mbia lakini hujampa package ya incentives, maana yake utakapokuja kutoa hizo incentives anaweza aka- withdraw.

Mheshimiwa Spika, jambo la mwisho, ni hili linaloendelea la mchanga, naomba niungane na wote wanaosema kama Rais yuko serious na kwa kweli vita hii haikuanza leo, mnakumbuka kulikuwepo na Kamati ya Dkt. Chipokola ya mwaka 2004 na ukienda kuisoma haina tofauti na mambo ya Osoro ya jana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kulikuwepo na Kamati ya Lawrence Masha…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa mzungumzaji)

MHE. ANTHONY C. KOMU: Mheshimiwa Spika, siungi mkono hoja na naomba ile kinga ya Marais waliotangulia iondolewe.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Ofisi ya Waziri Mkuu
MHE. FRANK G. MWAKAJOKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa fursa hii na mimi niweze kuchangia hotuba ya Waziri Mkuu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kwanza nianze na suala ambalo limekuwa linazungumzwa sana Bungeni hapa leo, suala linalohusu Muungano wetu kati ya Zanzibar na Tanzania Bara. Inaonesha kabisa kwamba CCM wanataka kuvunja Muungano kwa sababu hawathamini kabisa kazi walizofanya Baba wa Taifa pamoja na Karume. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, huwezi kuamini, yapo matamko mabaya yanayotokea hapa kwa ajili ya kubeza Zanzibar kila siku. Watu tunasikia humu lakini hatujawahi kusikia hata siku moja kiongozi mkubwa wa Kiserikali wala Spika wa Bunge hili au Naibu Spika wamekemea jambo hili. Hili jambo ni hatari sana, watu wanalalamika ndani ya Bunge hili na sisi tumeungana kama Watanzania kwa sababu ya nchi mbili; Zanzibar pamoja na Tanzania Bara. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naomba suala linalohusiana na Muungano wetu kati ya Zanzibar na Tanzania Bara ni vizuri tukaheshimiana ndani ya Bunge hili lakini pia tukawaheshimu wananchi wote; wa Tanzania Bara pamoja na wa Tanzania Visiwani. Wakati Mheshimiwa Waziri Mkuu anakuja kumalizia hotuba yake tunahitaji kauli ya Serikali, inatoa onyo gani kwenye Bunge hili ili kauli za kubeza upande mwingine zisitokee tena. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi sote hapa ni Watanzania, lakini tunahitaji kuheshimiana na kukaa pamoja ili kudumisha Muungano wetu. Hatuwezi kudumisha Muungano kama tutaendelea kuona watu wengine ni bora kuliko watu wengine. Jambo hili kwa kweli si jema na halifurahishi na halipendezi, naomba kila mmoja aweze kumheshimu mwenzake. (Makofi)

T A A R I F A . . .

MHE. FRANK G. MWAKAJOKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nimepokea taarifa hiyo kwa sababu nahitaji zaidi Muungano.

T A A R I F A . . .

MHE. FRANK G. MWAKAJOKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, wanasema mficha maradhi, kifo humuumbua. Sisi hatutaki kifo kituumbue na ndiyo maana tunazungumza, tunasema Muungano ni muhimu kuliko kitu chochote. Kama kweli taarifa anayoitoa ndugu yangu Mheshimiwa Lugola, siku zote wanavyoongea hapa kwa nini hataki kuwaambia Wabunge kwamba acheni kuzungumza maneno haya ni mabaya, mmekaa kimya humu mnashangilia mnafikiri ni jambo jema wakati wenzetu wanaumia na wananchi wa Zanzibar hawajisikii vizuri, kwa hiyo lazima tukemee jambo hili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine nataka kuzungumzia utawala bora. Katika nchi hii sasa utawala bora haupo kabisa. Huwezi kuamini katika nchi hii leo Waziri anaweza kumuagiza Mkuu wa Mkoa au Mkuu wa Wilaya, tena kamuagiza kwa barua, lakini hawezi kutekeleza. Hii nchi imekuwa nchi ya namna gani, hakuna utawala bora kabisa yaani sasa hivi Mkuu wa Wilaya ana nguvu kuliko Waziri, Mkuu wa Mkoa ana nguvu kuliko Waziri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye Mji wetu wa Tunduma kuna mgogoro ambao umekaa kwa muda mrefu sana; kuanzia Agosti, 2017 mpaka leo, Waheshimiwa Madiwani hawajakaa vikao kwa sababu ya amri ya Mkuu wa Wilaya. Wakati anakuja kuzungumza hapa Mheshimiwa Waziri Mkuu atueleze, Mkuu wa Wilaya ana mamlaka gani ya kuzuia Baraza la Madiwani katika maeneo yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kila mmoja anajua ukisoma Ibara ya nane (8) kwenye Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania utaona uanzishaji wa Serikali za Mitaa, ilikuwa ni kupeleka mamlaka na madaraka kwa wananchi wenyewe na ikaeleza kwamba kutakuwa na vyombo madhubuti ambavyo vitakuwa vinasimamia Serikali za Mitaa katika maeneo yao. Leo Mkuu wa Wilaya anakwenda kuzuia Baraza la Madiwani kwenye Mji wa Tunduma lisifanye kazi, Waziri ameandika barua kwamba Baraza la Madiwani liendelee kukaa, Mheshimiwa Mkuu wa Wilaya na Mkuu wa Mkoa wamegoma wamesema kwamba haitakiwi wakae.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunataka tujue sababu ni nini? Pia tunataka tujue kwa nini Mkuu wa Wilaya na Mkuu wa Mkoa wanakuwa na mamlaka, wanatumia sheria gani? Waziri Mkuu anajua, Waziri wa TAMISEMI anajua, Waziri wa TAMISEMI ameandika barua mbili, zote akilitaka Baraza la Madiwani likae, lakini Mkuu wa Wilaya na Mkuu wa Mkoa wanakataa. Leo mnasema kwamba utawala bora upo kwenye nchi yetu? Utawala bora hakuna kwenye nchi yetu na leo Mawaziri wengi hawaheshimiki kwa sababu Wakuu wa Mikoa na Wakuu wa Wilaya wameshapewa madaraka makubwa kuliko Mawaziri wetu, jambo hili linatusumbua sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ndiyo maana Wakuu wa Wilaya sasa hivi wanawaweka ndani Waheshimiwa Wabunge, akiamua tu anamweka ndani. Juzi hapa Mheshimiwa Mnyeti alikuwa anamwambia Mbunge wa Kiteto kwani Mbunge ana mapembe kuliko wewe, muweke ndani, ukiwaweka ndani mimi najua kwa kuwapeleka. Hizi ni dharau kubwa na inaonesha jinsi gani nchi yetu imeshindwa kuheshimu utawala bora. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka kusema tena kwamba, tusifikiri tutapata uchumi kama hatutajenga demokrasia ya kweli katika nchi hii. Uchumi ni demokrasia, kama hakutakuwa na maafikiano kati ya Watanzania wote; wa Vyama vya Upinzani pamoja na Serikali iliyoko madarakani tusitegemee kwamba, tunaweza tukapata maendeleo katika nchi hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nchi hii ni ya kwetu wote na si nchi ya mtu mmoja na si nchi ya chama kimoja, wote tuko sawa tunahitaji kupata haki sawa lakini tunashangaa leo Chama cha Mapinduzi wameonekana wao wana haki zaidi kuliko vyama vingine, wana haki zaidi kuliko mtu mwingine yeyote, kitu ambacho tunakuwa tunakosea sana. Tujenge demokrasia ya kweli katika Taifa hili, uchumi wa kweli utajengwa katika Taifa hili, lakini tukiendeleza zana za ubabe zinazoendelea katika nchi hii, tusahau kabisa uchumi wa Taifa hili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, viko vigezo vingi tunvyoviona sasa hivi. Ukijaribu ukiangalia hata bajeti ya mwaka 2017/218, ukienda kwenye kilimo imetekelezwa kwa asimilia 11, ukienda kwenye madini imetekelezwa kwa asilimia sijui tatu, ukienda kwenye maji imetekelezwa kidogo. Mpaka leo karibu bajeti nzima ya Serikali haijafikia hata ya mwaka jana ya utekelezaji wa asilimia 38 ya shughuli za maendeleo. Leo hii tumekaa hapa tunasema eti nchi inakwenda vizuri au inafanya vizuri wakati hakuna kinachoendelea. Tusifiche ugonjwa kifo kitatuumbua tu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo nataka kulizungumza ni kuhusiana na umeme. Nakumbuka sana wakati tunaanzisha gesi katika Taifa hili Serikali ilizunguka nchi nzima kutangaza kwamba kukatika kwa umeme sasa hivi tutasahau na mambo mengine, Watanzania mkae mkao wa kula, anzisheni viwanda umeme unakuja. Leo hakuna anayezungumzia umeme wa gesi tena, watu mmeanza kuleta mradi wa Rufiji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mradi wa Rufiji ili uweze kutekelezeka na kuisha unahitaji shilingi trilioni saba, mwaka huu 2018 tumetenga shilingi bilioni 700 tafsiri yake ni kwamba mradi huu utatekelezwa miaka kumi. Je, Mheshimiwa Rais ambaye anaanzisha mradi huu atakuwepo miaka kumi ijayo. Mradi huu inawezekana ukatekelezwa ndani ya miaka 20 wakati huo shilingi inaendelea kushuka thamani kwa maana hiyo mradi huu unaweza kuja kutekelezwa kwa shilingi trilioni labda 20 mpaka 30, huu mradi tunataka kuharibu fedha. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa ushauri wetu tulikuwa tunaomba mradi wa gesi ambao umeanzishwa Mtwara hizi shilingi bilioni saba badala ya kupelekwa kule Rufiji zikapelekwa Mtwara ili gesi ile isambazwe Dar es Salam, Morogoro, Tanga na maeneo mengine ili wananchi waendele kutumia umeme ambao unatumia gesi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini…

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa Mzungumzaji.)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019
MHE. ALLAN J. KIULA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kuweza kunipatia nafasi nami kuchangia Wizara hii muhimu kabisa, na mimi niseme niweze kusikika na Mheshimiwa Waziri aweze kuona namna ya kusaidia mambo mengine.

Kwanza kabisa, nampongeza Rais, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli kwa kazi kubwa anayofanya katika sekta mbalimbali ikiwemo Sekta ya Afya kwa sababu pamoja na kwamba tunapitisha, bajeti lakini Serikali ndiyo inatoa pesa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la pili, naipongeza Wizara, Waziri, Naibu na Watendaji wake Wakuu. Ile sera ya kuboresha vituo vya afya; Kituo cha Kinyambuli tulipata shilingi milioni 400 na kinaendelea vizuri kabisa. Pia tangu niingie Bungeni nimekuwa nikijadili sana suala la Wilaya mpya kutokuwa na Hospitali za Wilaya. Kwa hiyo, nashukuru sana tumeweza kupata shilingi bilioni 1.5 mwaka huu na tunaenda kujenga Hospitali ya Wilaya. Huo ni ukombozi mkubwa sana kwa wana Mkalama. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kabla sijaendelea, yako mambo ambayo pia ni muhimu ukisimama uweze kusema. Kama liko jambo lina trend kwenye mtandao halafu unakaa kimya na unaona linaharibu sura ya Serikali, hatuwezi kukaa kimya.

Mheshimiwa Naibu Spika, ndiyo maana tunaona kwamba hapa na pale watu wanajaribu kutoa ufafanuzi wa baadhi ya mambo. Sisi sote kama Waheshimiwa Wabunge tunajua kwamba Ripoti ya CAG inapotolewa, hizi oversight committees pia kama PAC, LAAC na PIC tutakaa na tutaleta ripoti Bungeni na ripoti hiyo itajadiliwa. Kwa hiyo, ni vyema watu wakatambua hilo. Huwezi ukamnyooshea mtu kidole au unamtukana halafu akawa amekaa kimya. Kwa hiyo, Kauli ya Serikali imekuja muda muafaka kabisa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nakupongeza, kama watu wameona kwamba ulivyopunguza muda wa maswali halafu karuhusu Kauli ya Waziri ili wananchi waone, kama wao wameenda kwenye mitandao, sasa umefanya kitu gani cha ajabu? Hilo ni jambo la lazima. Unajua watu wanasema mkuki kwa nguruwe...Sasa jambo hilo ni muhimu na uendelee kufanya hivyo hivyo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tukiendelea na uchangiaji katika hoja ya Wizara, Mheshimiwa Waziri lipo suala la Hospitali ya Kansa ya Ocean Road. Hospitali hiyo ni muhimu sana na wananchi wetu wanapata huduma muhimu.

T A A R I F A . . .

MHE. ALLAN J. KIULA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru, hata hivyo, taarifa hiyo siipokei kwa sababu wao wanapenda kusema halafu sisi tusiseme. Sasa tutasema. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Hospitali ya Ocean Road inatoa huduma, nzuri lakini wananchi wetu wanapata shida sana. Mheshimiwa Waziri umekiri kwenye ripoti yako kwamba waiting time ni wiki sita watu kupata huduma pale, mnataka m-reduce mpaka wiki mbili. Sasa kuna mitigation gani inafanyika hapo ndani ya wiki sita na watu wanapoteza maisha? Mheshimiwa Waziri unajua kabisa nimeshapoteza wananchi wangu wa Mkalama kwa kusubiri huduma hiyo.

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine ni suala la dawa. Mheshimiwa Waziri umezungumza suala la duka la dawa kuwa na dawa toshelevu. Tunaomba jambo hilo liwekewe mkakati, bajeti iwekwe ya kutosha kwa sababu yako maduka nje ya Muhimbili ambayo yanauza hizo dawa kwa bei ghali na wananchi hawawezi kumudu gharama hizo. Sasa jambo hilo linachafua taswira ya Ocean Road na inaonekana kama ni jambo la makusudi na kwa bahati mbaya daktari hawezi kusubiri mgonjwa afe anamwambia nenda mahali fulani utapata dawa. Picha wanayopata wananchi ni kwamba hayo maduka ni ya madaktari husika. Kwa hiyo, tunawapaka matope madaktari wetu na jibu sahihi ni hospitali yetu kuwa na dawa za kutosha.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Waziri natambua kabisa kwamba TAMISEMI wanaweza kutupatia gari na labda Halmashauri inaweza kununua. Nimekuwa nikizungumza sana suala la ambulance.

Mheshimiwa Naibu Spika, juzi juzi tu ametokea Diwani wangu mmoja amepata stroke, amecheleweshwa hospitali kwenda Singida kwa sababu hakuna usafiri, na mimi ni Mbunge. Sasa tunaomba jambo hilo kwa vyanzo vyovyote vile tuweze kupata gari la wagonjwa. Mkalama hatuna gari la waonjwa. Lile ambalo lilijibiwa na TAMISEMI ni gari lililochoka, Wilaya ilivyogawiwa tulipewa, linatugharimu sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuokoe maisha ya wananchi. Tunaomba tufikiriwe kwa jambo hilo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna suala zima la hoja za watumishi wa afya…

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa Mzungumzaji
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018
MHE. JULIUS K. LAIZER: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza napenda kuipongeza Wizara na Mheshimiwa Waziri kwa juhudi wanazofanya katika kuyapatia ufumbuzi masuala ya migogoro ya ardhi nchini ikiwemo Monduli. Mheshimiwa Waziri anakumbuka mwaka jana 2016 Machi alipokuja Monduli alikabidhiwa mashamba 13 yaliyofutwa na Rais kwa ajili ya wananchi lakini mpaka sasa wananchi wamezuiwa kutumia ardhi pamoja na kwamba wao wameshapanga matumizi na kubainisha maeneo ya malisho na eneo la kilimo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa masikitiko wamiliki wa awali waliyapeleka malalamiko kwa DC na DC kuzuia wananchi kutumia ardhi hiyo, mpaka itakapoenda tume ya kuchunguza kama mchakato wa kufutwa ulifuatwa. Masikitiko yetu ni kwamba Rais ameshafuta mashamba je, kuna mtu mwingine mwenye mamlaka zaidi ya Rais? Naomba kauli ya Mheshimiwa Waziri kuhusu mashamba ambayo Rais ameshayafuta lakini bado wananchi wananyimwa kuyatumia. Naomba Ofisi yake itoe waraka wa kuelekeza namna bora ambayo wananchi wanaruhusiwa kutumia ardhi hiyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo Mheshimiwa Waziri alitoa agizo kuhusu Ndugu Olemilya Mollel aliyejichukulia ardhi kinyume na taratibu ambapo pia aliagiza yeye kuondoa walinzi wa jeshi wenye silaha wanaolinda ardhi yake ambayo ni pori tu, miti na majani, (agizo lake halikutekelezwa) badala yake wananchi sasa wanakamatwa na kutozwa hadi milioni moja kama faini na mwenye shamba (naomba kauli yake ili kunusuru wananchi).

Mheshimiwa Mwenyekiti, uanzishaji wa Baraza la Ardhi Wilaya ambapo sisi tumetoa jengo tayari. Tunaomba kupatiwa Afisa Ardhi Mteule. Tunaomba wananchi wapewe angalau miaka mitano ya kulipia nyumba za NHC.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano
MHE. SAED A. KUBENEA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi nami ya kuchangia. Kwanza nieleze masikitiko yangu kwenye Wizara hii juu ya uamuzi wa Serikali wa kuvunja nyumba za wananchi wa Ubungo, Kimara na maeneo mengine ya Dar es Salaam hasa baada ya Mahakama kutoa amri ya kuzuia ubomoji ule. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ubomoaji umefanyika kinyume cha taratibu na namwomba Waziri kwa kuwa nyumba za wananchi wa Dar es Salaam zimevunjwa na tayari Benki ya Dunia imesimamisha msaada kwa Serikali kwa ajili ya ujenzi wa hizo barabara, kwa kuwa ujenzi umekiuka taratibu, kanuni na haki za binadamu zimevunjwa, nataka Serikali iwafidie wananchi wa Ubungo ambao nyumba zao zimevunjwa bila kufanya tathmini ya kile kilichovunjwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wasiwasi uliopo ni kwamba sasa Serikali italazimika kulipa fidia ili mradi uendelee, lakini fidia hii ilinalipwaje kwa nyumba ambazo tayari zimevunjwa. Kwa hiyo, naiomba Serikali iangalie utaratibu mzuri kabisa wa wananchi wa Ubungo kufidiwa nyumba zao zilizovunjwa. Nyumba hizi zimejengwa katika mazingira magumu, watu hao wengine walikuwa watumishi wa umma, wamejitolea katika Taifa hili wamelipwa kiinua mgongo chao, wamejenga mabanda yao, nyumba zimevunjwa kinyume na sheria ya barabara.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mara ya kwanza tumeona barabara inakatwa kutoka mita 121.5 katikati ya barabara. Wataalam wanasema mita 121 ni uwanja wa mpira. Kwa hiyo, hivyo ni viwanja vya mpira viwili ndiyo inajengwa barabara ya Dar es Salaam. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili, ni juu ya barabara ambazo zimetajwa katika kitabu cha Waziri, katika ukurasa wa 203 imetajwa barabara ya Nzega, Tuge hadi Tabora. Kwa mujibu wa taarifa zilizopo, barabara hii ilishakamika miaka miwili iliyopita leo inatengewa fedha na Wabunge hapa wapo hapa ambao wana barabara zao hazijajengwa. Kule Rufiji barabara haijajengwa tokea wakati wa Bibi Titi Mohamed, Mbunge anasimama hapa analia asubuhi, anaomba ijengwe barabara, lakini barabara inapelekwa Tabora.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ATCL. Wabunge wamezungumza na watu wengi wamezungumza kwenye nchi hii juu ya mchakato mzima wa ubinafsishaji wa Shirika la Ndege la Taifa (ATCL). Mchakato ulitawaliwa na viriba, ulitawaliwa na udanganyifu na haukufuata taratibu zozote za ubinafsishaji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa shirika likabinafsishwa lakini baadaye Serikali ikalazimika kununua hisa zake ilizouza katika Shirika la Ndege la Afrika Kusini, Shirika likarudi Tanzania, Serikali ikamiliki hisa za ATCL, leo tunafufua shirika ni kazi nzuri nawapongeza kwa kufufua shirika mmefanya kazi nzuri. Sisi wazalendo wa nchi hii tulikuwa tunalililia shirika hili liwe shirika letu la umma.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna watu wameingiza nchi hii hasara kubwa kwenye ATCL. Tarehe 9 Oktoba, 2007, ATC ilisaini mkataba wa ukodishaji wa ndege aina ya Air bus na Kampuni ya Wallis Trading Company. Taarifa zilizopo ukaguzi wa ndani haukufanyika kujua ubora wa ndege wala Shirika la Anga la Tanzania halikushirikishwa. Matokeo yake baada ya muda mfupi ndege ile ikafa na ikawa ATC inalipa kati ya dola 3,700 kwa kila mwezi hadi kufikia deni la shilingi bilioni mia mbili na milioni mia tano tisini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ndege hii ambayo ilikodishwa na Serikali ya Tanzania ilifanya kazi muda mfupi sana hapa nchini. Hadi mwezi Juni mwaka 2009 ndege hii ilipelekwa matengenezo nje ya nchi na baadaye ikapelekwa Ufaransa. Makadirio ya matengenezo ya ndege yalifikia dola za Marekani milioni 593.6 na deni liliongezeka hadi kufikia shilingi milioni 3.039.

T A A R I F A . . .

MHE. SAED A. KUBENEA: Mheshimiwa Mwenyekiti, hajui analolifanya kwa hiyo nimemsamehe tu. (Kicheko/ Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunazungumza historia na bila kuzungumza historia katika nchi hii, hatuwezi kujenga nchi, hakuna nchi isiyo na historia duniani, tunazungumzia ATC jinsi ilivyokufa, jinsi ilivyouawa na jinsi inavyofufuliwa. Kama hatujaangalia tulikotoka, tulikojikwaa, tutakwama mbele. Shirika hili huyo Mbunge haelewi kwamba tayari ATC imefunguliwa kesi nyingine London. Waziri wa Katiba na Sheria anajua, Mwanasheria Mkuu wa Serikali anajua, Balozi Migiro anajua, viongozi wa Serikali wanajua kwamba tuna kesi mpya imefunguliwa London mwaka huu tunadaiwa zaidi ya dola milioni 38 zaidi ya bilioni 80, anazungumza nini huyu? Anazungumza nini?

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunazungumza ATC na tayari Serikali ya Tanzania imelipa pound elfu15 kwa malipo ya awali ya Mawakili, London. Tunazungumza ATC ambayo Mwanasheria Mkuu wa Serikali wakati huo alishauri mkataba usifungwe lakini ulisainiwa mkataba wa hii ndege na Kampuni ya Wallis bila kufuata taratibu. Leo watu wameenda London wamefungua kesi wanatudai kuna hatari ya Bombardier zetu zikakamatwa tena ndiyo kitu tunachokizungumza hapa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunazungumza hatari ya ndege zinazonunuliwa na fedha za walipa kodi kukamatwa tena, kukamatwa kama ilivyokamatwa ile Q400 kule Canada. Tunazungumza anakwambia tujenge hoja, hizo ndiyo hoja. Tuna nia ya kujenga Taifa letu, tuna nia ya kujenga ATC mpya, lakini hatuwezi kujenga ATC mpya bila kusaidia shirika hili likaondokana na huu mzigo wa madeni ambao linao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, shirika hili linadaiwa zaidi ya bilioni 100 kwa mujibu wa taarifa za Serikali yenyewe na Serikali imebeba huo mzigo wa madeni, ni vizuri, ni jambo zuri. Hata hivyo, ni lazima tuhakikishe ATC inakwenda vizuri, watendaji waliopo ATC wanapewa uwezo, wanapewa uhuru wa kuendesha ndege zao. Ni bahati wamepata Mkurugenzi mpya ambaye alikuwa Boss kule katika Mashirika ya Ndege ya Afrika, amerudi hapa amekuja kuongoza ATC alikuwa Engineer wa ATC kabla ATC haijabinafsishwa, amerudi kwa uzalendo wake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali hii ina utaratibu mbaya wa kutumia watu wanaotoka nje, lazima waambiwe wasifanye mchezo huo. Wamemchukua Tido Mhando London BBC wakamleta TBC, amekaa mwaka mmoja wamemfukuza. Wamechukua mtaalam kutoka South Africa amekuja TIC amekuja hapa wamemu-harass ameondoka. Amekuja mtu Profesa Waziri wangu...

T A A R I F A . . .

MHE. SAED A. KUBENEA: Mheshimiwa Mwenyekiti, Tido Muhando aliajiriwa BBC alikuwa Mkuu wa Idhaa ya Kiswahili labda Mheshimiwa Amina alikuwa hajui wakati huo kwamba Tido alikuwa Mkuu wa Idhaa ya Kiswahili. Amerudi hapa Tanzania akawa Mkuu wa TBC, ameondolewa bila mkataba wake kuelezwa. Mtu ambaye alikuja TIC ameondoka, Profesa. Kwa hiyo, ninachozungumza ni kwamba wataalam wetu wanaoletwa Tanzania ambao walikuwa wanafanya kazi nje ya nchi, wameacha kazi yenye mishahara mkubwa, wenye marupurupu mazuri, yenye usalama yakinifu, wakarudi Tanzania kuja kufanya kazi, ni lazima walindwe.
(Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, unapomuomba mtu aje kufanya kazi huwezi kumleta mtu halafu ukawa unambabaisha babaisha. Kwa hiyo, ili ATCL iendelee ni lazima wafanyakazi wapewe vipaumbele na Menejimenti iachiwe ifanye kazi yake bila kuingiliwa na wanasiasa. Ndege zinachelewa kwa sababu ya Wabunge sisi baadhi yetu tunachelewa Airport. Kwa hiyo, route ya ndege ya kutoka Mwanza …(Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa Mzungumzaji)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019
MHE. JULIUS K. LAIZER: Mheshimiwa Mwenyekiti, uvunaji wa magadi Engaruka mradi wa kimkakati. Mheshimiwa Waziri anatambua wananchi wa Engaruka - Monduli wameridhia kuachia hekari 75,000 kwa ajili ya ujenzi a kiwanda cha magadi, lakini changamoto kubwa ni barabara. Pamoja na nia ya Serikali kutaka kujenga barabara ya Mto Mbu - Loliondo lakini ujenzi huo utachukua muda mrefu sana. Je, ni nini mkakati wa kujenga barabara hicho, ni lini kiwanda hiki kitajengwa wananchi waruhusiwe kuendeleza maeneo yao mpaka Serikali itakapokuwa tayari.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kiwanda cha nyama Makuyuni kimekamilika lakini tumemkosa mwekezaji wa kuendesha kiwanda hicho. Ni nini mikakati ya Wizara kutusaidia kupati mwekezaji?
Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa Unaokusudiwa Kutekelezwa na Serikali Pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020
MHE. INNOCENT L. BASHUNGWA: Mheshimiwa Mwenyekiti Asante sana kwa kunipa nafasi hii niweze kuchangia mapendekezo ya mpango wa Maendeleo ya Taifa 2019/2020.

Mheshimwa Mwenyekiti, nianze kwa kuungana na Waheshimiwa Wabunge wengi waliochangia kwa kumpongeza Mheshimiwa Rais wetu Dkt. Pombe Magufuli kwa utendaji wake wa kazi mzuri, ametimiza mwaka wa tatu lakini tumeona Mheshimiwa Rais wetu akitekeleza kwa vitendo ule usemi kwamba penye nia pana njia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaendelea kumpa moyo Rais wetu na tuombe Watanzania waendelee kumuunga mkono ili miradi mikubwa ya maendeleo ambayo Rais wetu ameonesha kwamba Watanzania tukithubutu tunaweza tuweze kuiitekeleza iweze kusaidi kizazi hiki na vizazi hii na vijavyo.

Mheshimiwa Mweyekiti, pia nitumia nafasi hii kumshukuru Waziri Mkuu hivi karibuni alitembelea Mkoa wa Kagera kuangalia mwenendo wa msimu wa kahawa. Mheshimiwa Waziri Mkuu aliweza kutatua changamoto nyingi katika ziara, lakini pia alitoa maelekezo ya namna bora ambayo Serikali inahitaji kujipanga ili msimu ujao wa kahawa wakulima wetu waweze kufaidika na kilimo cha kahawa na katika hili niweze kushauri Serikali badala ya kusubiri msimu ukikaribia ndipo twende kwenye kukabiliana na changamoto za msimu basi on quarterly basis Serikali iwe inaita wadau, tunajadili namna ya kujipanga vizuri ili msimu wa kahawa na wa mazao mengine unapofika basi tujikite kwenye kutekeleza na kusimamia mazao haya ya biashara ili yaweze kuwasaidia wakulima lakini yaweze kuchangia kwenye pato la Taifa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nimshukuru sana na nimpongeza Mheshimiwa Waziri Dkt. Mpango pamoja na shemeji yangu Dkt. Ashatu kwa mapendekezo kama rasimu, nasema kama rasimu kwa sababu ni mapendekezo bado na sisi Wabunge tuna nafasi ya kuboresha na nitumie nafasi hii kuwapongeza sana Kamati ya Bajeti hata muda wangu usipotosha, Kamati ya Bajeti wamatoa mapendekezo mazuri naunga mkono asilimia mia moja naamini Mheshimiwa Waziri kama mkiachukua yale pamoja na mapendekezo mazuri ya Waheshimiwa Wabunge basi tutakuwa na mapendekezo ya mpango mazuri sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya utangulizi huo nianze kuchangia mapendekezo ya mpango kuhusu suala la ufungamanishaji wa uchumi na maendeleo ya watu na nita-argue katika sehemu tatu ambazo ili tuweze kufungamisha uchumi na maendeleo ya watu lazima tuwe na Taifa lenye afya na nguvu kazi. Na katika hili niipongeza Serikali katika sekta ya afya Serikali imefanya kazi nzuri kwenye vituo vya tiba kote nchini dawa inapatikana na Serikali tunaona ikiendelea kujenga vituona katika hili Mheshimiwa Waziri kwa vile tupo kwenye mapendelezo ya mpango basi vile vituo vya afya viwili vya Nyabioza na Kanoni katika Wilaya ya Karagwe vile kwenye mapendekezo ya mpango. (Makofi)

Mheshimwia Mwenyekiti, jambo la pili ambalo ningependa kusisitiza na kuipongeza Serikali ni kuleta Mamlaka ya Maji Vijijini. Na katika hili Mhemimiwa Waziri tuombe sana Serikali pia ingalie kuwa kama kuna uwezekana zile shilingi 100 ambazo zinatoka kwenye mafuta zinaenda kwenye barabara kwa sababu ya umuhimu wa kuwatua akina mama ndoo nchini basi ikiwezekana iwe 75 kwa 75 halafu tukimaliza changamoto za upatikanaji wa maji safi na salama nchini turudi tena kwenye ile ratio ya 100kwenda kwenye mchango wa barabara na 50 kwenda kwenye mfuko wa maji hii itasaidia kutatua changamoto ya maji nchini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo ningependa kuchangia na kusisitiza sana pamoja na jitihada nzuri ya Serikali elimu bila ada lakini bado kuna changamoto kubwa ya upungufu wa madarasa, upungufu wa matundu ya vyoo, maabara katika shule za sekondari hazikamilika na hosteli kwa ajili ya vijana wetu wasichana. Sasa nipende katika kwenye mapendekezo ya mpango hili mlione ni jambo muhimu sana kwa sababu CDG haziendi lakini Serikali kupitia vipaumbele tumeona hela ikienda kusaida kwenye miradi mbalimbali ya maendeleo kwenye sekta nilizozitaja, lakini tukumbuke kwamba kuna miradi viporo upande wa zahanati, upande wa shule na kwenye mapendekezo haya basi tuiombe Serikali iangalie kwa uzito huo kama tulivyofanya Mheshimiwa Rais alivyosimamia zoezi la madawati nchini basi hali kadhalika twende kufanya hivyo kwenye shule za msingi, matundu ya vyoo na maabara kwa ajili ya sekondari nchini.
(Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo ningependa kuchangia ni haya mazao ya vipaumbele. Kuna wengine wamezungumzia takwimu ya post harvest losses asilimia 30 ya mazao ya wakulima yanaharibikia mashambani. Lakini ukienda viwanda Mheshimiwa Mwenyekiti viwanda vinahitaji malighafi za wakulima hawa Kamati ya Viwanda na Biashara tulivyotembea viwandani sasa hivi robbot ndizo zinafanya kazi zime-replace ajira za Watanzania, lazima ajira hizi tuzitengeneze kwenye sekta ya kilimo, mifugo na uvuvi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti lakini ukiangalia post harvest losses asiliamia 30 mkulima anahangaika lakini zao lake 30% linaharibika shambani na huku viwandani wanahitaji hizi malighafi nitolee mfano...

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa Mzungumzaji)

Eeh, naunga mkono hoja.
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2017 na Mpango wa Maendeleo ya Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019
MHE. JULIUS K. LAIZER: Mheshimiwa Spika, nami nakushukuru kwa kunipa nafasi. Nitasemea maeneo machache na nianze na suala la viwanda. Hakuna mtu ambaye anapinga suala la ujenzi wa viwanda kwa sababu inatusaidia kukuza uchumi kama Taifa, lakini kuondokana na tatizo la umaskini kwa mwananchi mmoja mmoja. Hoja yetu hapa ambayo tunataka Waziri wa Fedha atuambie, hivi lengo la viwanda hivi tunavyojenga ni kwa ajili ya nani, tunajenga viwanda hivi ili tuwe na viwanda vingi katika Taifa hili au tunajenga viwanda ili tuwasaidie wananchi wetu kuondokana na umaskini katika Taifa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, siyo mara ya kwanza nchi hii kuwa na viwanda, lakini vimekufa si mara ya kwanza nchi hii kuwa na ndege lakini zimekwisha, kwa hiyo suala siyo kuwa na miradi mikubwa, suala ni kuwa na miradi mikubwa lakini endelevu (sustainable development project). (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mpaka leo miaka mitatu tunaimba sera ya viwanda lakini hakuna hand out guideline ya nchi inayoeleza muktadha mzima wa viwanda vitakavyosimamiwa nchi hii. Hivi akiondoka Rais huyu akaja Rais mwingine hili suala la viwanda si limekufa? Kama tuna millennium ya 2025 kwa nini tusingekuwa na program ya Taifa kama Taifa ambapo kila mwananchi na kila sehemu anayo inayoonesha namna suala la viwanda vitakavyoendelezwa katika nchi yetu.

Mheshimiwa Spika, huwezi kuendeleza viwanda kama hauna kodi stahiki ambazo zinasimamiwa kwa muda fulani ambao mwekezaji atawekeza, tunabadilisha kodi kila mwaka tunafanya trial and error ile tunayosoma kwenye biology kwamba unatengeneza kaboksi halafu panya anaenda huku anakosa mlango, anaenda anakosa mlango, ndiyo maana kila mwaka wanarekebisha Sheria ya Kodi, kila mwaka wanakuja wanasamehe kodi hii, wanaanzisha kodi hii, kwa nini tusingekuwa na program ya nchi inayoonesha kwamba ni kodi gani tuache kwa sasa ili tu-invite wawekezaji halafu watu waweze kuwekeza, lakini wanafanya uwekezaji hawaja-base katika rasilimali watu.

Mheshimiwa Spika, ukiangalia katika bajeti ya Mheshimiwa Waziri, hakuna mahali popote Wizara inazungumza habari ya ujenzi wa vyuo vya kati ili vijana wetu wanaomaliza form four waweze kupata ujuzi waende wakafanye kazi kwenye viwanda vyetu. Ndiyo maana watajenga viwanda lakini wataanza kuomba vibali vya kupata expert kutoka nje kuja kufanya kazi katika viwanda vya nchi yetu kwa sababu hatujawaandaa vijana kufanya kazi katika viwanda. Maana yake viwanda tutakuwa tunajenga kwa ajili ya watu wengine lakini siyo kwa ajili ya Taifa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, leo nilikuwa nasema asubuhi nchi hii inazalisha zaidi ya vijana laki tatu wa kidato cha nne kila mwaka ambao hawaendelei na kidato cha tano. Waziri wa Elimu amenijibu kisiasa kwamba wataenda kwenye Vyuo vya Ualimu ambapo wanaenda lakini hawaajiri na wao sera ya elimu wanasema kuanzia miaka ijayo wanafuta kidato cha nne kuanzia sasa shule ya msingi zinafundishwa na watu wenye Diploma, hivi mtu aliyemaliza form four anaweza kusoma Diploma kwa kuunganisha au mpaka aende Certificate? Kwa hiyo ni muhimu tuwe na viwanda ambavyo tumeandaa vyuo vya kati na vya juu vinavyoandaa vijana wetu kwenda kufanya kazi katika viwanda tunavyovijenga. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kuhusu rasilimiali kwa maana ya malighafi, hakuna muunganiko kati ya viwanda, kilimo chetu na mifugo yetu. Bajeti mbili zimepita tu hapa kwa mbinde, tena baada ya kwenda kukaa party caucus Bajeti ya Kilimo, na bajeti ya Mifugo na Uvuvi, lakini walitupa matumaini na Kiti cha Spika kilitupa matumaini kwamba wakati wa Bajeti Kuu Serikali ita–subsidize kule ambavyo tulikuwa tumelalamikia katika kupeleka ruzuku na katika kusaidia uwekezaji katika sekta ya kilimo na mifugo.

Mheshimiwa Spika, nimesoma kitabu hiki hakuna, hakuna amendment yoyote ya kuiongezea bajeti Wizara hizo, hivi Waziri wa Kilimo atafanyaje kazi, Waziri wa Mifugo atafanyaje kazi kama hana fedha. Kwa hiyo ni muhimu kama kweli wangekuwa wanatujali na wanataka kuunganisha Sekta ya Mifugo, Kilimo na Viwanda wangeleta bajeti ambayo itasaidia kule wakulima wetu walime kisasa. Haiwezekani ukajenga kiwanda cha kutegemea kilimo cha msimu, kwamba unasubiri mvua inyeshe halafu mwenye kiwanda afunge kiwanda kwa sababu hamna mazao kwa ajili ya kuendesha kiwanda. Ni lazima tuwe na sustainable projects ambazo mwekezaji wa kilimo akiwekeza awe na uhakika wa kupata raw material mwaka mzima bila ya kutegemea mvua ambayo hatujui kama inanyesha au hainyeshi, miradi hiyo iko wapi? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hu ni mwaka wa tatu Serikali iliahidi kuleta miradi ya kimkakati ambapo mpaka sasa tunavyoongea siyo Liganga siyo Mchuchuma siyo Engaruka siyo General Tyre hata mmoja hauja-mature. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, agizo la Serikali tangu tunaanza Bunge hili ni kwamba tutakuwa na miradi hiyo ya kimkakati, Liganga na Mchuchuma tulikuwa tunasikia tukiwa nje ya Bunge tumekuja ndani ya Bunge, mpaka leo hawajatekeleza. Miaka mitatu hii hata Watumishi wameshindwa kuwapandishia mishahara halafu wanasema wana-control inflation hawaja-control inflation imeji-control yenyewe kwa sababu purchasing power hakuna, wananchi hawana fedha, kwa hiyo kama hawana fedha huwezi kupima inflation kwa sababu hakuna mtu anayenunua. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba Serikali ituambie, kwa sababu uchumi wa nchi hii hauwezi kujengwa na kila mtu kuwa mtaalam katika eneo lote. Tunataka kama tuna maono ya kuwa na viwanda, tuwape wataalam watuandalie programu ya kuwa na viwanda katika Taifa hili. Tuache hizi kauli za kisiasa za kutetea kitu ambacho hatuoni, tunatamani kama ni viwanda kila mtu aone, siyo wanatuletea vile viwanda 3,600 kwenye makaratasi, lakini mnatuambia tu, tupelekeni site hamna ujasiri huo, kwa nini? Kwa sababu wana-politicize miradi mingi badala ya kuangalia uhalisia. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, suala siyo kuwa na viwanda vingi, suala ni kuwa na viwanda vinavyosaidia kubadilisha maisha ya wananchi. Hata kama tungekuwa na kiwanda kimoja, kinachobeba mazao yote ya wakulima wetu, hicho kiwanda ni bora, kuliko kuwa na viwanda 100 ambavyo vyote malighafi unaagiza kutoka nje. Kwa hiyo ni muhimu tuwe na lengo la Taifa kusaidia wananchi katika miradi hiyo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, niseme jambo lingine, historia inaonesha Serikali zinapita, Serikali iliyopita ilikuwa inasema Kilimo Kwanza, imemaliza imeondoka, imekuja Serikali ya viwanda. Kilimo Kwanza hatujafanya na tungefanya Kilimo Kwanza viwanda vingejengwa automatically kwa sababu raw material zingepatikana vya kutosha na watu wangejenga. Mpaka leo hakuna mkakati wowote Serikali imewekeza katika kusaidia kilimo.

Mheshimiwa Spika, naomba nishauri mambo machache, ni muhimu Waziri wa Fedha, Mheshimiwa Mpango kama anataka kusaidia Taifa hili, Serikali ilete mpango mkakati wa kusaidia sekta ya kilimo katika nchi hii ili iweze kuzalisha kwa tija. Kwa sababu mazao si mazao tu lazima mazao yawe na ubora unaostahili. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, umefanya hii kazi kwenye industry ya utalii, ukiiangalia Arusha yote na Kaskazini ambavyo tuna utalii wa kutosha, lakini tunaaagiza nyama kutoka Kenya, tunaagiza material ya kwenye hotel, hata nyanya kutoka nje, ni kwa sababu uzalishaji wetu hauna viwango. Kwa hiyo siyo kuzalisha nyanya tu, siyo kuzalisha matunda tu ni lazima tuzalishe katika ubora unaostahili.

Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 – Wizara ya Madini
MHE. JULIUS K. LAIZER: Mheshimiwa Naibu Spika, nami ninakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuchangia Wizara hii, kwa kweli niwe muungwana kwamba mnyonge mnyongeni lakini haki yake mpeni. Historia ya uchumi wa madini kwenye nchi yetu kuanzia siku za nyuma na hapa tulikofika, hauwezi kabisa kuacha kutambua juhudi zinazofanywa na Serikali katika kudhibiti utoroshaji wa madini nchini kwetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna dhamira ya kweli katika kushughulikia jambo hili. Hata hivyo, katika dhamira hiyo hiyo ni lazima tutambue kwamba misingi ya wizi wa madini kwenye nchi yetu ulianzia wapi na hatuwezi kulinda rasimali za nchi hii kwa mtutu wa bunduki wala kwenye majukwaa ya siasa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tatizo kubwa naloliona ni sheria zetu haziko katika mazingira mazuri ya kulinda rasimali ya Taifa. Kwa hiyo, naamini katika nia njema hii ya Serikali, ni lazima tutambue sheria zetu ndiyo kinga pekee katika vizazi vyote kusaidia kusimamia rasilimali ya Taifa hili. Inawezekana Rais huyo akawa na nia njema lakini kama hatujaweka misingi imara kwa ajili ya kusimamia rasilimali zetu hizi, atakuja Rais mwingine tutarudi kule kule tulikotoka. Kwa hiyo, hatutamani ulinzi wa rasilimali zetu utokane na utashi wa mtu mmoja au kikundi cha watu wachache. Tunatamani ulinzi wa rasilimali zetu utokane na utashi na sheria za nchi ambazo zimesimamiwa vizuri na ambazo zinalazimisha viongozi kusimamia sheria hizi. Tusije tukatoka mahali ambapo tunaenda mbele tunarudi nyuma. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya utangulizi huo, naomba niseme mambo machache. Ukiangalia katika ahadi ya makenikia ya dola milioni 300, ambapo mpaka sasa hivi hatujapokea, hii ni kwa sababu ilikuwa ni utashi wa wale wenye makinikia kuahidi, lakini ingekuwa ni jambo la kisheria fedha zetu tungeshapata, hatujapata kwa sababu ilikuwa inaonekana kama ni hisani. Kwa hiyo, ndiyo maana nasema, lazima tuwe na sheria ambazo zinalinda rasilimali zetu.
(Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niseme kidogo kwenye changamoto zinazowakabili wachimbaji wadogo na ni muhimu Mawaziri wakatuelewa katika hili. Hatuchukii kabisa walioko katika maeneo yale Serikali kukusanya kodi. Kwa mfano, madini ya ruby ambayo bei yake imeshuka kwa sababu ninyi mnataka tukate kama inavyokatwa tanzanite, madini haya hayafai kukatwa na ninyi mnachukua muda mwingi sana kutoa mwelekeo kwamba ni namna gani mnataka madini yale yasimamiwe. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, walikuja Naibu Mawaziri wawili kule Longido kwetu, wakatoa ahadi za kutosha mpaka leo hawajatekeleza. Ni muhimu sana mkashughulikia jambo hili kwa haraka, siyo mnafanya ziara tu tunakuja tunawapokea mnatupa matumaini na matumaini hayo hamyatekelezi. Wachimbaji walioko kwenye maeneo yetu wanapata changamoto nyingi sana kwa sababu madini haya yameshuka bei kule Mundarara na mpaka leo hatujajua nini msimamo wa Serikali katika hilo. Wamekuja watu wawili ni vijana wakatuahidi kwamba tutaleta hizi sheria mara moja, hakuna kitu. Naomba leo waniambie hili suala la Mundarara linamalizika lini. Tena Waziri akasema Wamasai tunajenga, tunajenga kweli, sisi hatuoi kama Wasukuma, sisi tukipata fedha tunajenga, tunanunua vitu vingine, sasa watuambie ni lini suala hili la Mundarara litafika mwisho kuhusu madini ya ruby ili wananchi wetu waweze kunufaika na madini haya. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la pili kwenye hilo, eneo la madini ya Mererani. Naomba Wizara waseme, nani anayepaswa kusimamia wachimbaji wadogo, Polisi wamegeuza wachimbaji wadogo wa Mererani kuwa chanzo chao cha kupata fedha. Wale wanaofanya biashara ya madini siyo wachimbaji, wananunua wakauze, lakini wakishatoka kununua yake madini watu wanakamatwa wanaambiwa lipa kodi. Sasa anayekusanya kodi ni TRA au Polisi? Wasaidieni wananchi hawa, wanaumizwa kabisa barabarani na bahati mbaya wale Polisi wamejua maeneo yao, akikutwa na jiwe anaambiwa lipa kodi, sasa analipaje kodi wakati hajauza.

Mheshimiwa Naibu Spika, ule ni ujasiriamali tu, kuna wanaochimba lakini kuna wale wanaookota kwenda kuuza. Ni utafutaji wa riziki, watu wanateseka katika kutafuta lakini wanachajiwa kodi ambayo hauna sababu ya msingi. Lazima mtupe maelekezo ya wale wachimbaji wadogo na wale wafanyabiashara wa madini watakavyonufaika na watakavyolipa kodi.

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la tatu, Mheshimiwa Waziri Rais aliwahi kusema kwamba suala la utoaji wa leseni lizingatie wananchi wanaokaa kwenye maeneo yale. Tuna tatizo la mchanga wa kujengea wale watu wanaenda kushika PR kwenye mashamba ya wananchi, kwenye vyanzo vya maji, wanapewa huko kwenye Kanda wakija huku hawaelewi chochote, hawasilikilizi wananchi, wanawaondoa wananchi, hatuna manufaa nayo, wanatuachia mashimo. Ni muhimu mbadilishe ile sheria ili mtu anayetaka leseni ya madini kwenye eneo fulani aanzie kule kijijini na hakutakuwa tena migogoro kwa sababu wananchi watakuwa wameshiriki kuanzia mwanzo mpaka mwisho, kuliko kuja kuingia kwenye migogoro ambayo hauna sababu ya msingi. Hii sheria naomba muipitie muone namna ambayo mnavyoweza mkafanya.

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine, tuna tatizo la ufisadi katika Wizara hii katika sehemu ya watumishi. Wako Makamishna Wasaidizi 12, miezi sita sasa wamesimamishwa kazi na Katibu Mkuu wa Wizara na wameajiriwa watu wengine katika nafasi hiyo, kwa hiyo, kuna malipo mara mbili, yaani wale walioko kazini na wale ambao hawako kazini. Kama Serikali inaona Makamishna hawa hawatoshi, wastaafisheni kwa maslahi ya umma muwalipe mafao yao, kuliko kuwalipa Makamishana Wasaidizi 24 kwa wakati mmoja, wakati uhitaji wenyewe ni 12. Wale ambao mmewarudhisha nyumbani, wapeni maslahi yao, kama hamuwapi, warudisheni kazini, kuliko kuwaweka nyumbani halafu, wengine wanalipwa. Hii ni hasara kwa Serikali kwa kulipa watumishi pasipokuwa na sababu ya kufanya hivyo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la mwisho, ni suala hili la makinikia na ulinzi wa ukuta wa Mererani. Ukuta wa Mererani ni hatua ya kwanza ya kudhibiti rasilimali zetu na madini haya nami naiunga mkono, lakini tukiendelea na utaratibu huo hivi huo ukuta tutalinda kwa mtutu mpaka lini, tutalinda na Jeshi mpaka lini?
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020
MHE. JULIUS K. LAIZER: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuchangia jioni ya leo. Nianze kwa kuunga mkono hoja, lakini niseme, namshukuru Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwa kazi kubwa anayoifanya ya kulijenga Taifa letu na kujenga uchumi wa nchi yetu kwa kipindi chake. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia naomba nimshukuru sana Mheshimiwa Waziri wa Nchi, TAMISEMI, kwa kazi kubwa ya kizalendo anayoendelea kuifanya, waendelee kufanya kazi Watanzania wanaona huduma ambayo Wizara yake inafanya kwa Watanzania. Katika wanaopiga kelele hakuna jimbo hata moja la kwao ambalo hajafika na kuweka alama ya utumishi katika miradi mbalimbali ya maeneo yao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ukiangalia wakati mwingine hawasemi, wale wananchi, wanyonge wa Taifa hili wanaohitaji afya, wanaohitaji elimu uliowahudumia ni shukrani mbele za Mungu na wao wanakushukuru. Kwa hiyo, msikatishwe tamaa na maneno ya watu waliokata tamaa wenyewe. (Makofi/Kicheko/Vigelegele)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukimkuta binadamu asiyeshukuru hata moja jema, ujue binadamu huyo aidha amekata tamaa mwenyewe, au hajui hata anachotakiwa kushukuru au kukipinga. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni ngumu sana kuamini kwamba wapinzani wote kwenye Bunge hili wana akili sawa, kwamba wote…..

MHE. PASCAL Y. HAONGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

MWENYEKITI: Eee, taarifa!

T A A R I F A

MHE. PASCAL Y. HAONGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kumpa taarifa mzungumzaji wa sasa kwamba, anaposema kuna watu wamekata tamaa, ni kwamba yeye ndiye amekata tamaa kwa sababu alikimbia mapambano amekwenda kujisalimisha upande wa pili.

MWENYEKITI: Hiyo siyo taarifa, endelea.

MHE. JULIUS K. LAIZER: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niseme mambo machache kuhusu eneo la jimbo langu, kwamba Mheshimiwa Waziri nakushukuru kwa sababu umetupa milioni 800 kwa ajili ya vituo vya afya. Hata hivyo, Mheshimiwa Waziri akumbuke ana deni la kituo cha Naalarami, alienda mwenyewe alifika, lakini ana deni kubwa la soko la Mto Mbu, ambalo yeye aliahidi lakini sijaona kwenye kitabu, kwa hiyo, wakati anajibu, naomba anisaidie kwamba ni lini soko hilo tutalijenga.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka niseme mambo machache, nimemsikiliza Mheshimiwa Msigwa, kaka yangu, amezungumza akasema, Rais amefanya uamuzi na lazima tuangalie uamuzi tunaofanya na matokeo ya uamuzi huo. Naomba nimtajie mambo kumi aliyofanya Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa miaka hii michache na matokeo yake kwa Taifa hili, kwa sasa na vizazi vijavyo. Halafu mwisho wapime na Watanzania wapime, kama wao hawakubaliani na haya ambayo anafanya, Watanzania watapima mwaka 2020 na watafanya uamuzi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, uamuzi wa kwanza wa Serikali hii…

MHE. FRANK G. MWAKAJOKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

MWENYEKITI: Mheshimiwa Frank kaa, muda wetu umekwisha, Mheshimiwa muda wetu umekwisha kaa, taarifa nilishafunga, kaa Mheshimwa Frank kaa chini.

MHE. JULIUS K. LAIZER: Mheshimiwa Mwenyekiti, muda wangu. Rais amefanya uamuzi wa kulifufua Shirika la Ndege, ili kusaidia usafiri wa ndani na nje ya nchi kwa ajili ya utalii na kupata mapato ya Taifa hili. Nataka mmoja asimame aseme ndege haina faida kwenye nchi hii ili Watanzania wapime ni nani anayesema ukweli na nani mchawi wa maendeleo yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Taifa hili ili liwe na uhakika wa uendelezaji wa viwanda na uchumi endelevu, lazima tuwe na umeme wa uhakika. Rais amefanya uamuzi ili tutafute umeme wa maji kwa ajili ya uchumi wa Taifa hili na hao na wao kama wajasiriamali watatumia umeme huo, nataka atuambie, ni nani kati yenu ambaye hataki umeme kwa ajili ya maendeleo ya nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Rais na Serikali imefanya uamuzi wa kujenga miundombinu ya Standard Gauge kwa ajili ya kusafirisha mazao na kusafirisha na kujenga uchumi wa nchi yetu. Nani kati yao ambaye hakubaliani na miundombinu salama kwa ajili ya uchumi wa nchi yetu na uwekezaji wa taifa hili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la tano, Mheshimiwa Rais wa nchi hii amefanya uamuzi wa kutengeneza taifa la watu wenye afya njema, kwa kuamua kujenga vituo vya afya 300 na zaidi ya hospitali za wilaya zaidi ya 60 ili Watanzania wapate afya njema, afanye kazi kwa ajili ya uchumi wa nchi yetu. Nani hataki afya ya Taifa hili iweze kutengemaa. (Makofi)

WABUNGE FULANI: Oyeee. (Makofi)

MHE. JULIUS K. LAIZER: Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la sita, Katiba ya nchi yetu inasema, elimu ni haki ya msingi ya kila Mtanzania. Mheshimiwa Rais amefuta ada watoto wetu wanasoma elimu bure ili kupata haki kwa aliye na fedha na asiye na fedha. (Makofi)

MHE. MCH. PETER S. MSIGWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

MHE. JULIUS K. LAIZER: Mheshimiwa Mwenyekiti, na sisi Waheshimiwa Wabunge…

MWENYEKITI: Muda wetu umekwisha, Mheshimiwa Msigwa, nilishatoa taarifa tatu huku na huku nne.

(Hapa baadhi ya Wabunge walizungumza bila kufuata utaratibu)

MWENYEKITI: Don’t question me.

MHE. JULIUS K. LAIZER: Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Rais amefanya uamuzi wa elimu bure ili Mtanzania asiye na fedha na mwenye fedha waweze kupata haki yao ya Kikatiba ya kupata elimu. Tusijilinganishe tulioko ndani tunaweza kulipa ada kuna Watanzania walioko vijijini ambao hata Sh.5,000 kwa siku ni tabu kwake, hivi leo tubeze uamuzi ambao ukienda kwenye kitabu hiki, ukurasa wa 198, Mheshimiwa Mwakajoka anajua ni kiasi gani cha fedha cha elimu bure kimeenda katika Jimbo lake. Kama ninyi ni waungwana simameni waambieni wapiga kura wetu wakatae elimu bure, wakatae fedha zinazopelekwa kwenye Majimbo yenu ili irudi tuamini kwamba hamthamini elimu bure. (Makofi)

MBUNGE FULANI: Yes.

MHE. JULIUS K. LAIZER: Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la saba, moja ya tatizo lililopo kwenye nchi yetu ni uchumi wetu haukulindwa na rasilimali zetu zilitumika vibaya. Tumetunga sheria hapa ya kulinda rasilimali za Taifa, leo husikii habari ya utoroshaji wa madini, husikii habari ya ujangili kwa wanyama wetu, halafu ninyi mnataka kuona siyo uamuzi? Nataka tupime matokeo kwa kupata wanyama wazuri pamoja na utalii kwa ajili ya uchumi wa Taifa letu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, uamuzi wa kutunga Sheria ya Kudhibiti Madawa ya Kulevya na uamuzi kutoa ardhi kwa ajili ya wakulima na mimi nasema Taifa hili liko salama… (Makofi/Vigelegele)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
Muswada wa Sheria ya Fedha wa Mwaka 2017.
MHE. RAPHAEL J. MICHAEL: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kunipa muda huu wa kuchangia.

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la kwanza nianze kwenye suala la vyanzo vya mapato ambavyo vimeondolewa katika Halmashauri zetu. Dhana ya decentralization ilikuwepo kwa sababu ya kutaka kuipunguzia Serikali majukumu. Bahati nzuri nchi yetu imepita katika hatua mbalimbali mpaka kufikia hatua za sasa ya ugatuaji wa madaraka kwa maana ya decentralization by devolution (d by d).


Mheshimiwa Naibu Spika, sijajua ni kitu gani kinaifanya Serikali Kuu ipate raha ya kukimbizana na mapato madogo ya kawaida ikiyaacha mapato makubwa ambayo hata Mheshimiwa Rais ameyaona yanayopotea, ambapo wangeweza wakapata fedha lakini wakimbizane na mapato madogo kama property tax na bill boards (mapato ya matangazo).

Mheshimiwa Naibu Spika, utaratibu huu wa Serikali Kuu ya Awamu ya Tano utazidhoofisha mno Halmashauri hata kama tungejitetea kwa kiwango gani, kwa kiwango chochote tunachojitetea, utaratibu huu utazidhoofisha sana Halmashauri.

Mheshimiwa Naibu Spika, rai yangu kwa sababu sasa tunajadili sheria; na kwa sababu tayari bajeti imeshapita, namwomba Mheshimiwa Waziri atuambie kwa ukweli kabisa, kwamba ni kiasi gani atazirejeshea Halmashauri baada ya TRA kukusanya. Kiwango hicho kitamkwe kwenye sheria, kwamba ni kiwango gani kitarejeshwa Halmashauri baada ya fedha hizo kukusanywa. Mwaka 2003 Mheshimiwa Mramba aliondoa kodi zilizokuwa zinaitwa kodi zenye matatizo kwenye Halmashauri zetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Waziri Lukuvi aache Mheshimiwa Waziri anisikilize, halafu watajadili mambo yao.

Mheshimiwa Naibu Spika, ninachotaka kukizungumza hapa ni kwamba ushauri wangu kwa Mheshimiwa Waziri, ni kwamba lazima kwenye sheria itamke bayana ni kiwango gani kinachorejeshwa katika Halmashauri zetu baada ya kukusanywa, ndiyo hoja yangu ya msingi. Kwa sababu mwaka 2003 Mheshimiwa Mramba alipokuwa Waziri wa Fedha kuna vyanzo viliondolewa hapa na tukaambiwa tutarejesha katika Halmashauri lakini mpaka leo Halmashauri hasa za mijini hazipati hata shilingi moja…

T A A R I F A . . .

MHE. RAPHAEL J. MICHAEL: Mheshimiwa Naibu Spika, taarifa yake nimeipokea kwamba kwa mara ya kwanza Majiji yaliyo mengi yamechukuliwa na UKAWA. Inawezekana sitaki kuizungumzia Serikali kwamba ina hiyo ni bad intention, inawezekana kuna intention mbaya ya kudhoofisha Upinzani.

Mheshimiwa Naibu Spika, nataka nijirejeshe kwenye hoja kwamba niamini Serikali ina nia njema, kama ina nia njema niamini kwamba wanapaswa kutusikiliza tunachoshauri na ushauri wangu kwa Waziri ni kwamba inawezekana kwa mtazamo wa Serikali hii na mtazamo wa Waziri wanadhani TRA ina uwezo wa kukusanya kuliko Halmashauri zilivyokuwa zinakusanya, jambo ambalo siyo kweli kwangu mimi ninavyoamini.(Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kama ni hivyo na kwa sababu tayari tumeshapitisha sheria, ninachoomba Mheshimiwa Waziri atuoneshe tu kwa kiwango gani minimum ambacho kitarejeshwa katika Halmashauri zetu baada ya kukusanya. Tuna kodi ya retention ya ardhi ya asilimia 30 mpaka leo ni ugomvi hairudi katika Halmashauri zetu. Nilikuwa nakusanya shilingi milioni 700 ya property tax katika Halmashauri ya Manispaa ya Moshi, wamerudisha shilingi milioni 163 tangu wameanza kukusanya wao! Najiuliza shilingi milioni 500 niliyokuwa nakusanya kwenye bill board itarudishwa kwa namna gani?

Mheshimiwa Naibu Spika, ndiyo maana naomba Mheshimiwa Waziri kwenye mabadiliko ya sheria anasema, hiyo hela itaenda Hazina na atarejesha kwa kiwango kile kulingana na bajeti ya Halmashauri. Namshauri Waziri atamke kwamba ni kwa percentage gani minimum ambacho lazima Serikali ikirejeshe Halmashauri na kwa wakati, huo ni ushauri wangu wa kwanza. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la pili, sifa moja kubwa ya kodi ni watu kuridhia kodi kulipa (tax compliance), sasa leo tunapokuja kwenye Bunge tukaambiwa kwamba kuna watu watakaolipa kodi lakini hawapaswi kupelekewa maendeleo tunahamasisha wananchi wasilipe kodi na lazima Serikali ikubali kwamba imeteleza. Haiwezekani watu walipe kodi halafu muwaambie hamuwapelekei maendeleo kwa sababu ya mfumo wa kisiasa mliokubaliana nao Kikatiba. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nchi hii imekubali mfumo wa Vyama vingi vya Siasa yenyewe tena katika Bunge la Chama kimoja cha siasa, mkajitengenezea Kanuni zenu wenyewe kwamba tupige kura za ndiyo, hapana na abstain. Sasa leo watu wakifanya uamuzi huo wa kidemokrasia ndani ya Bunge mnawaadhibu vipi walipa kodi? Kama mnaamua kwamba hamuwezi kupelekea wananchi maendeleo kuanzia leo, muwatangazie kwamba wale ambao hawapelekewi maendeleo wananchi milioni sita waliochagua Opposition wasilipe kodi! Nadhani ingekuwa imekaa vizuri, vinginevyo mnalipasua Taifa la Tanzania na hatuwezi kukubaliana na jambo kama hili.(Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, suala la sheria zinazohusiana na makosa yanayofanywa kulingana na Sheria za Fedha za Serikali za Mitaa, mapendekezo ya Serikali ni kwamba adhabu ziongezwe kutoka 200,000 mpaka 1,000,000.

Mheshimiwa Naibu Spika, wananchi wanaofanya makosa ya kutema mate kule Manispaa ya Moshi ni wananchi maskini. Moshi mtu akitema mate chini anatozwa 50,000, leo kwa sheria hii tunayopitisha hapa atatozwa 200,000 mpaka 1,000,000. Sh.50,000/= walikuwa hawawezi kulipa, leo mnataka wakalipe sh.200,000/= mpaka Sh. 1,000,000/=, watatoa wapi hizo fedha? Kwa nini tunatunga sheria za kuwaumiza Watanzania wetu, hivi tungeongeza tu ikawa hata Sh.100,000/=, tungepata shida gani? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mapendekezo yangu kwa Serikali na kwa Mheshimiwa Waziri, hii sheria faini zibaki sh.100,000/= mpaka sh.200,000/= kulingana na aina ya makosa na kifungo kisizidi mwaka mmoja, lakini kusema mtu afungwe miaka miwili au kwa pamoja vyote alipe na faini ya sh.200,000/= mpaka sh.1,000,000/= ni kwenda kuwaletea matatizo wananchi yasiyo ya lazima.

Mheshimiwa Naibu Spika, nashauri Serikali kwamba kodi ya majengo ioneshwe wazi katika sheria kwamba pamoja na kusamehe nyumba za tope, nyumba za tembe na nyumba zingine za majani, pia wajane na yatima watakaokuwa wameachiwa nyumba wapate msamaha kupitia kwenye sheria. Kupitia kwenye sheria yenyewe itamke kabisa kwamba wajane na yatima watasamehewa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, wazee wa zaidi ya miaka 60 tayari sheria ya mwanzo ilikuwa inawatamka siyo jambo jipya kwa Serikali hii, isije ikaonekana kwamba Serikali hii imeanzisha jambo jipya, tangu sheria ya mwanzo ya Urban Authorities Rating Act, No. 289 ilikuwa inatambua kwamba Wazee wote wanaoishi katika nyumba zao, wenye zaidi ya miaka 60 walikuwa hawapaswi kulipa kodi ya propery tax. Sasa hivi tuongeze Wajane na Yatima na Watu wenye Ulemavu. Sizungumzii wagane kwa sababu wagane najua wengine wana uwezo hata wakipata hiyo shida. Nazungumzia wajane, yatima na Watu wenye Ulemavu. Naomba sana hoja hiyo iingizwe kwenye marekebisho ya Sheria ya Jedwali la Serikali.

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo, nashukuru kwa nafasi ya kuchangia na naunga mkono mawazo yote ya Kambi Rasmi ya Upinzani.