Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Dr. Mary Michael Nagu (41 total)

MHE. DKT. MARY M. NAGU: Mheshimiwa Mwenyekiti nakushukuru sana kwa kunipa fursa hii adimu ya kuuliza swali moja la nyongeza. Kama ilivyo Wilaya na Mlalo, Wilaya ya Hanang‟ ina bwawa ambalo lilikuwa likikusanya maji ya Mlima Hanang‟ kwa scheme ambazo zinaweza zikatumika kwa umwagiliaji. Ni miaka mitano sasa tumekuwa tukiomba bwawa hilo likarabatiwe na bado hatujafanikiwa.
Mheshimiwa Naibu Waziri anaweza kunisaidia kuwahakikishia wananchi wa Hanang‟ kwamba kama anavyoomba Mbunge wa Mlalo na Mbunge wa Jimbo la Hanang‟ analiomba hilo.
WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, naomba nimjibu Mheshimiwa Mary Nagu kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nilikumbushe Bunge lako kwamba kupitia Bunge hili tulipitisha Sheria Namba 5 ya mwaka 2013, Sheria ya Umwagiliaji na pia tulianzisha Tume ya Umwagiliaji. Katika mwaka wa fedha 2015/2016, Serikali imetenga bilioni 53 kwa ajili ya kuendeleza na kukarabati mabwawa ambayo yanajihusisha na shughuli za umwagiliaji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba tutafanyia mapitio, mabwawa haya yote ambayo yanaweza kuongeza maeneo ya umwagiliaji, lakini pia mabwawa mengine ambayo yatasaidia wananchi wetu kuweza kupata maji. Ni azma ya Serikali ya Awamu ya Tano kwamba tunataka tuongeze kiwango cha upatikanaji wa maji vijijini na mijini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hivyo, sehemu zingine tutatumia mabwawa, sehemu zingine tutatumia mito na sehemu nyingine tutatumia maziwa. Kwa hiyo, kazi hii tutakwenda kufanya, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba nitafika huko kwenda kuangalia bwawa analoliomba ili kusudi tuweze kuona nini kifanyike. Ahsante.
MHE. DKT. MARY M. NAGU: Mheshimiwa Naibu Spika, namshukuru sana Mheshimiwa Naibu Waziri kwa jibu zuri alilotoa. Pamoja na jibu hilo, naomba kuuliza maswali mawili ya nyongeza.
Kwanza, Hanang ni Wilaya ya pili kuwa na CHF iliyoboreshwa na CHF hii iliyoboreshwa haitaweza kunufaisha wananchi kama hakutakuwa na dawa za uhakika. Je, Serikali haioni ni vizuri pamoja na CHF iliyoboreshwa kuwe na duka la MSD?
Pili, Wilaya ya Hanang ina upungufu wa Wodi za akina mama na watoto na nimeshukuru sana kuona kwamba wodi ambayo italaza wanawake 16 inajengwa, lakini Mheshimiwa Naibu Waziri amekiri kwamba ni wanawake 200. Je, kuwa na wodi itakayolaza wanawake 16 itatosheleza mahitaji hayo?
Pamoja na hivyo, naomba Serikali ione umuhimu wa Wilaya ya Hanang ambayo imezungukwa na Wilaya nyingi kuwa na wodi za kutosheleza akina mama kulazwa.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli, kwanza siyo CHF peke yake iliyoboreshwa kwa Halmashauri ya Hanang, lakini kubwa zaidi napenda kumpongeza Mbunge huyu kwa sababu katika michakato yao ya kuhakikisha kwamba huduma ya afya inaimarika huko Hanang kwamba japo wana vituo vya afya vinne, lakini sasa hivi wanaendelea na ujenzi wa vituo vya afya sita. Kwa hiyo, naomba nimpongeze sana katika hilo.
Mheshimiwa Naibu Spika, kweli tumesema kwamba sasa hivi dawa zinapatikana kule Kilimanjaro na lengo ni kwamba kuhakikisha maduka ya dawa haya yanapatikana kila eneo; nilisema pale awali, tatizo kubwa ni changamoto ya bajeti, lakini nadhani kwa kadri tunavyokwenda, tutaangalia jinsi gani tutafanya kila maeneo maduka ya madawa haya yaweze kupatikana ilimradi kuwapelekea wananchi huduma kwa karibu zaidi.
Mheshimiwa Naibu Spika, suala la wodi ya wazazi, ni kweli kwamba ile haitoshelezi, lakini watu wanasema angalau tuna sehemu tumeanza. Sasa hivi kuna wodi ya wazazi ndani ya kipindi hiki cha mwaka 2016 na wodi ile itakamilika ambayo itakuwa ina uwezo wa kuchukua akina mama 16.
Lengo la Serikali ni kwamba tunatafuta fursa zote zinazowezekana ili mradi eneo lile ambalo population yake ni kubwa zaidi, kuhakikisha kwamba tunapata fursa mbalimbali za kuongeza nguvu angalau kuhakikisha wodi hizi zinaongezeka. Siyo Hanang peke yake, isipokuwa Tanzania nzima changamoto za wodi zimekuwa ni kubwa, lakini ni jukumu la Serikali kuangalia tunafanya vipi sasa ili mradi huduma ya afya iweze kuimarika na hususan tukiangalia Bajeti ya mwaka huu ya Wizara ya Afya ambayo itakuja, Waziri atakuja hapa kuelezea jinsi gani bajeti imejielekeza sasa katika miradi ya maendeleo kwa kiwango kikubwa sana ukilinganisha na pale awali.
MHE. DKT. MARY M. NAGU: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi leo.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa vile fedha za Mfuko wa Barabara ni asilimia 30 kwa TAMISEMI na asilimia 70 kwa Serikali Kuu, hatuoni kutokana na mahitaji kama haya ya makorongo aliyoyasema Mheshimiwa Bashe, sasa wakati umefika wa kugawa fedha hizo asilimia 50 kwa 50 na Wilaya ya Hanang‟ ina makorongo makubwa kutokana na uharibifu wa mazingira lakini Halmashauri kama alivyosema Mheshimiwa Waziri haina uwezo kabisa wa kujenga makorongo hayo?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS (TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA): Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli nakubaliana na Mheshimiwa Mbunge kwamba, Mfuko wa Barabara unagawanywa kwa asilimia maana mfuko ni mmoja, lakini Wizara ya Ujenzi inayoshughulikia barabara kwa maana TANROADS wanachukua asilimia 70 na Halmashauri zinachukua asilimia 30.
Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Mbunge anajaribu kusema hapa kwamba, kwa sasa ni kama vile tunahitaji kuongezewa nguvu kwenye Mfuko wa Barabara katika upande wa barabara zinazosimamiwa na Mamlaka za Serikali za Mitaa takribani ni sawa kwa sawa na zile barabara za Kitaifa zinazounga Mikoa kwa Mikoa kwa sababu uharibifu mkubwa umetokea zaidi huko.
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo hili ni la kisera na kwa hivyo siyo rahisi kulitolea jibu hapa, lakini sichelei kukubaliana na yeye kwamba kweli kwa sasa iko haja ya kuangalia kama tunaweza kubadilisha hizi namba hata angalau tukafika asilimia 40, sasa hili ni jambo la kisera siwezi kuliamua peke yangu hapa kusema ndiyo au hapana, Serikali tumesikia tuendelee kulitafakari tuone kama kuna haja ya kufanya hivyo.
MHE. DKT. MARY M. NAGU: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuuliza maswali mawili ya nyongeza. Namshukuru sana Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu mazuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa maji ya kijito cha Endagaw yamekuwa mengi kuliko utaalamu ulivyoona na kwa hivyo mfereji mmoja unaweza ukafanya ukuta uliojengwa kubomoka.
Je, Waziri anaweza kuwahakikishia watu wa Endagaw na wa Hanang kwamba huu upande wa pili utajengewa mfereji mara moja?
Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili, palipokuwa na kijito cha Endagaw kulikuwa na wananchi ambao walikuwa na shughuli zao na makazi yao na wakaondolewa kwa ajili ya skimu hiyo.
Je, Serikali inaweza kutusaidia kuwapa fidia wale watu ambao wameondoka pale kwa ajili ya mradi huu? Namuomba Mheshimiwa Waziri aweze kutembelea eneo hilo na kuona umuhimu wa maswali haya mawili ya nyongeza niliyoyauliza, ahsante.
WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa nimpongeze kwa kuibua swali hili. Tunasema kwamba ili tuweze kupata chakula cha kutosha lazima tuende kwenye kilimo cha umwagiliaji. Sasa hivi Taifa letu tumeshaanzisha Tume ya Umwagiliaji itakayosimamia eneo hili. Mpaka sasa Taifa linalima hekta 461 tu tunataka katika miaka mitano ijayo tufikishe hekta milioni moja. Sasa kwa kuanzia na hiki Kijiji cha Endagaw ambapo tayari tumeahidi kuendelea kujenga skimu ile, hizo laki nne tutazipeleka lakini tutaboresha kwa namna ambavyo anashawishi Mheshimiwa Mbunge ili wananchi wale waweze kupata faida ya kilimo cha umwagiliaji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pili nitakwenda kuangalia katika kuwahamasisha wale wananchi tutaona namna gani ya kuwafidia. Jambo moja zuri ni kwamba fidia nzuri ni ile kuwajengea skimu ambayo wataweza kuendelea kulima kuliko wakipewa fedha lakini wasiendelee kulima. Kwa hiyo, tutaangalia namna bora ya kuwafidia kwa kujenga skimu ili walime kilimo cha umwagiliaji.
MHE. DKT. MARY M. NAGU: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kunipa nafasi hii.
Kwa kuwa, Wilaya ya Hanang ni Wilaya ya wafugaji, na wananchi wamejitahidi sana kujenga hosteli kama ya shule ya Mreru, Mulbadau, Endasak na kwa kufuatia suala hilo; je, Serikali ipo tayari kusaidiana na wananchi, kuona kwamba zile hosteli na mabweni yaliyokuwepo toka wakati wa uhuru, tunaimarisha na kuboresha miundombinu ambayo ipo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Mbunge senior katika Bunge hili amesema jinsi gani Serikali itaboresha hizi shule, ni kweli shule ambazo zimejengwa muda mrefu lazima tuangalie ni jinsi gani tutaboresha miundombinu.
Mheshimiwa Naibu Spika, juzi nilikuwa katika Chuo cha Kigurunyembe, nimepitia shule mbalimbali. Kuna baadhi ya shule zamani zilikuwa zinafanya vizuri zaidi, lakini kutokana na uchakavu wa miundombinu ufanisi wake umekuwa chini sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, nilipotembelea shule ya Iyunga kule Mbeya ambayo bweni lake liliungua, nilivyoangalia nikaona ni kwa nini sasa shule nyingi ambazo zamani zilikuwa ni shule za vipaji lakini sasa hivi uwezo wake umekuwa chini, bunsen banner iliyokuwa inatumika mwaka 1980, ndiyo inayotumika mpaka mwaka 2017; jambo hili haliwezekani.
Kwa hiyo, Mheshimiwa Mbunge naomba nikuhakikishie kwamba, jukumu letu kubwa ikiwezekana katika Halmashauri tubainishe katika vipaumbele kwa sababu tumekuwa na tatizo kubwa sana la kufanya ukarabati katika shule zetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, tuungane kwa pamoja, tubainishe shule zilizochakaa katika mipango yetu ya Halmashauri katika bajeti tuliweke hili mapema, Ofisi ya Rais TAMISEMI itaweka nguvu kuhakikisha kwamba shule hizi sasa zinakuwa na ubora ili wanafunzi waweze kupata taaluma inayokusudiwa na shule zetu za Serikali ziwe shindani sawa na shule nyingine za private katika Jamhuri wa Muungano wa Tanzania..
MHE. DKT. MARY M. NAGU: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza namshukuru sana Naibu Waziri kwa majibu mazuri yenye kuwaletea matumaini wananchi wa Hanang. Sasa naomba niulize maswali madogo mawili, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kwa kutambua kwamba, Wilaya ya Hanang ilisahauliwa katika Awamu ya kwanza na ya pili, sasa atakubaliana na mimi, na ninahakika atakubaliana na mimi kwamba, vijiji hivyo vya Hanang alivyovitaja sasa vitakuwa Awamu ya tatu viwe vya kwanza katika kupewa umeme katika Awamu hiyo ya tatu?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili; najua kwamba, awamu ya kwanza na ya pili ilipewa vijiji vichache mpaka sasa havijapata umeme. Je, Naibu Waziri atakubaliana na mimi kwamba, katika muda mfupi unaokuja vijiji hivyo vichache vipate umeme basi, ili viwape matumaini wananchi wa Hanang?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Naibu Spika, nirekebishe kidogo kwamba, katika Jimbo la Hanang kwa kweli, hatukupeleka vijiji vingi! Ni vijiji saba tu ambavyo tulivipatia umeme kwenye REA awamu ya pili, lakini niongezee kwa Mheshimiwa Mbunge kama alivyosema vijiji 19 ambavyo vilikusudiwa kupewa umeme kwenye REA awamu ya pili vyote vitakamilika ndani ya siku 20 zilizobaki. Kwa hiyo, awamu ya pili itakamilisha vijiji vyako Mheshimiwa Dkt. Mary Nagu na vijiji vingine 44 ulivyoomba na vyenyewe vitapatiwa umeme kwenye REA awamu ya tatu.
Mheshimiwa Naibu Spika, nimhakikishie Mheshimiwa Dkt. Mary Nagu vile Vijiji vya Kisambalang, Dang‟aida, Dawidu, Mwanga na Wandolendode, vyote vitapatiwa umeme katika awamu ya tatu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili kuhusiana na uhakika kwamba, je, muda uliobaki kweli kazi iliyobaki itakamilika?
Mheshimiwa Naibu Spika, kazi ya kufunga miundombinu mikubwa kwenye Jimbo la Mheshimiwa Dkt. Mary Nagu imekamilika, kazi iliyokuwa imebaki sasa ni kusambaza transformer kama 10 ambazo tuliahidi. Bado transformer tano kukufungia Mheshimiwa Mary Nagu, mwezi ujao nadhani tutakamilisha transformer zote 10.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini baada ya kusema hayo, vile vijiji vingine 44 ambavyo umeviomba pamoja na shule za sekondari, vituo vya afya kwa bilioni 15.8 tulizokutengea nadhani tutakamilisha kazi yote Mheshimiwa Dkt. Mary Nagu.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia niwaombe sana Waheshimiwa Wabunge, pesa ambazo mmetutengea kwa mwaka huu, bilioni 587 ambazo ni kwa ajili ya kuwasambazia umeme vijijini, zote tutazitumia kwa kazi hizo na vijiji vyote vilivyobaki vitapata umeme kwenye mradi kabambe wa REA awamu ya tatu unaoanza mwezi Julai mwaka huu.
MHE. DKT. MARY M. NAGU: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi hii. Naomba kuuliza swali la nyongeza kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na kufanya bidii yote ya kutengeneza madawati kwa ajili ya watoto wa shule na kwa sababu madarasa hayatoshelezi kuna hatari ya madawati hayo kuharibika. Je, wakati haujafika sasa kuwa na mpango mzuri kama ulivyokuwa wa madawati kutengeneza madarasa hasa pale ambapo tunazingatia wananchi wameshajitolea kwa kiasi kikubwa? Je, ni mpango gani ambao Serikali unaweza ukaufanya ili tuwe na madarasa ya kutosha kuweka madawati ambayo tumeyatengeneza wote? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli, kwanza naomba tuongeze juhudi kubwa za Watanzania; Mheshimiwa Rais alipotoa maelekezo kwamba tuondoe tatizo la kero wanafunzi kukaa chini na wengine kukaa katika mawe sasa watanzania tushirikiane kwa pamoja kutengeneza madawati.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nikiri kwamba zoezi hili limefanikiwa kwa kiwango kikubwa sana lakini tulipongeze na Bunge lako hili kuhakikisha kwamba limeweza kutoa mgao wa madawati kwa Majimbo mbalimbali ili kuweza kupunguza ile kero ya madawati katika maeneo yetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli tatizo la kwanza ukipunguza maana yake tumetoa tatizo la wanaokosa shuleni, watoto elimu bure tumepata changamoto, tumepata madawati. Lakini sasa hivi tuna tatizo la vyumba vya madarasa hali kadhalika na vyoo, ndiyo maana katika mpango mkakati uliokuwepo hivi sasa katika bajeti hii ya mwaka wa fedha tunaoondoka nao tunaona kwamba kutakuwa na ujenzi wa madarasa katika maeneo mbalimbali na ujenzi wa matundu ya vyoo.
Mheshimiwa Naibu Spika, hata hivyo, naomba niwahimize Watanzania wote, japokuwa Serikali itakuwa na mpango mpana sana kuhakikisha kwamba tunaondoa kero ya vyoo na kero ya vyumba vya madarasa hali kadhalika nyumba za Walimu kama nilivyosema awali, lakini niwaombe Watanzania tuendelee kushirikiana kwa pamoja vile vile kama tulivyofanya katika madawati, basi tufanye tena katika nyumba za Walimu na madarasa. Mwisho wa siku tukipata elimu bora, itakuwa ni kwa maslahi mapana ya nchi yetu. Ahsante sana.
MHE. DKT. MARY M. NAGU: Mheshimiwa Spika, ahsante sana.
Mheshimiwa Spika, kwanza kabisa Serikali ningependa ijue kwamba kuna wananchi waliojitolea kwa kujua umuhimu wa walimu kujenga maboma kwa ajili ya nyumba za walimu, pamoja na madarasa.
Je, Serikali itatoa kipaumbele kwa wale wananchi ambao wameonesha umuhimu wa walimu na umuhimu wa elimu?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Spika, jibu ni ndiyo Serikali itatoa. Ndiyo maana hivi sasa tumeshaleta fedha karibu awamu mbili za Capital Development Grand, ambapo katika baadhi ya Halmashauri imeshaanza kuweka kipaumbele kumalizia nyumba za walimu. Maeneo niliyofika zile fedha zilizofika, utakuja kuona yale maboma ambayo mwanzo yalibakia sasa hivi utakuta yanakamilishwa. Kwa hiyo, hiyo ndiyo commitment ya Serikali, naomba nikupongeze na hili ni jukumu la kwetu sote Wabunge zile fedha zinavyopita ni lazima tuzisimamie vizuri, tuende tukamalize haya maboma yaliyopo katika maeneo yetu.
MHE. DKT. MARY M. NAGU: Mheshimiwa Spika, namshukuru Mheshimiwa Naibu Waziri kwa kujibu swali langu.
Mheshimiwa Spika, swali la kwanza, Bwawa la Gidahababieg siyo la umwagiliaji tu, maeneo yote yale hayana maji ya uhakika kwa hivyo litakuwa ni kwa ajili ya matumizi ya binadamu, mifugo pamoja na umwagiliaji ikiwezekana. Baada ya bwawa lile kuvunjika kutokana na athari za mvua mwaka 2006, nilifikisha suala hilo kwenye Serikali mwaka 2007 na mpaka leo hakuna lililofanyika. Nataka kujua kama ni kweli mchakato utaanza na bwawa hili lirudi kwa sababu ndiyo linakusanya maji ya mlima Hanang yanayomwagika na kupotea bure?
Mheshimiwa Spika, swali la pili, Vijiji vya Hirbadaw, Dajameda, Mwanga, Gidika, Lalaji na Wandela vyote vilikuwa kwenye Mradi wa Benki ya Dunia na maji hayakuweza kupatikana. Naomba nijue ni lini vijiji hivyo vitaanza kutafutiwa vyanzo vingine ili watu wale waweze kupata maji kwani Bonde la Ufa halina maji? Nashukuru sana.
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Spika, kwanza kabisa niseme kwa bahati nzuri nimetembelea Wilaya ya Hanang na wakati nikiwa kule tulishirikiana na Mheshimiwa Mbunge tukazunguka maeneo yote ambayo yanahitaji huduma ya maji.
Mheshimiwa Spika, katika swali lake la kwanza ameonesha kwamba Bwawa la Gidahababiegh sio kwa ajili ya umwagiliaji tu na kweli nilikwenda kwenye lile bwawa likishakamilika litatumika kwa umwagiliaji, mifugo na maji yale yakichakatwa yatatumika pia kwa matumizi ya majumbani. Sasa anauliza ni kweli bwawa hili litatengenezwa? Nimuahidi tu Mheshimiwa Mbunge kwamba tayari tumetenga fedha katika robo ya pili ya mwaka wa fedha huu tulionao. Fedha tunazo tayari na wakati wowote wataalam watatumwa kwenda kule kwa ajili ya kufanya survey. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pili kwenye hivi vijiji ambavyo havikupata vyanzo vya maji, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba tulitembea naye na kweli wakati tupo kwenye ziara tuliwaahidi wananchi kwamba haya maeneo ambayo hayakupata vyanzo vya maji kwenye bajeti ya mwaka 2017/2018 ambayo sasa hivi inaandaliwa tutahakikisha tunaweka fedha ili twende kukakamilisha miradi hiyo.
MHE. DKT. MARY M. NAGU: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa fursa hii ya kuuliza swali la nyongeza. Wilaya ya Hanang kama ilivyo Wilaya ya Siha inakabiliwa na changamoto ya upungufu wa Ardhi na tuna mashamba ambayo yalikuwa chini ya NAFCO ikiwemo Basotu Plantation na tuliomba kwamba shamba hili lirudi kwa wananchi; Mheshimiwa Waziri anaweza kutueleza ombi letu limefika wapi?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Fedha, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mary Nagu, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, ni kweli kabisa kwamba kuna maombi ya Shamba la Basotu Plantation ambalo lilikuwepo mikononi mwa NAFCO liweze kugaiwa kwa wananchi. Utaratibu ambao ulikuja kubadilika baadaye ni kwamba Halmashauri ya Wilaya ya Hanang’ ikabidhiwe hilo shamba ili wenyewe waweze kukodisha kwa wakulima wadogo, kwa sababu tayari jitihada za kugawa mashamba mengine ililileta mgogoro mkubwa sana ambao ulikuwa unatishia amani.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, kwa sasa utaratibu ambao umetumika ni huo wa kujaribu kukabidhi kwa Halmashauri huku jitihada zikiendelea za kuangalia namna bora ya kuweza kuligawa. Kwa hiyo, namtaka Mheshimiwa Mbunge aendelee kuwa mvumilivu tukiangalia utaratibu huu ili huko mbele ya safari tuweze kuligawa kwa utaratibu.
MHE. DKT. MARY M. NAGU: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niulize maswali mawili ya nyongeza kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Waingereza wanasema justice delayed is justice denied, na kwa vile imechukua muda. Je, Msajili wa Hazina, Hazina na Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi watakuwa tayari sasa kukamilisha uhakiki huu na kuwalipa hao wanaodai ambao walikuwa wafanyakazi wa NAFCO?
Swali dogo la pili, ili tumalize migogoro iliyo kwenye mashamba ya NAFCO, je, Serikali iko tayali sasa kurudisha shamba la Basutu plantantion kwa wananchi ambao wana upungufu wa ardhi mapema inavyowezekana?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kabisa kwamba justice delayed is denied, vilevile justice hurried is justice buried. Kwa hiyo, katika mukhtadha huo tunaendelea na uhakiki ili haki itendeke pande zote, tunatambua kwamba imechelewa lakini haki katika hili ni pamoja na Serikali kuweza kulipa malipo ambayo ni stahiki kwa sababu tukiyaharakisha sana inawezekana hata baadhi ya wafanyakazi wale tukawapunja.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba jitihada zinaendelea na tunashirikiana na Wizara ya Fedha taratibu zikikamilika wananchi wake wa Hanang ambao anawasimamia vizuri sana watalipawa haki zao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusiana na swali la pili la Basutu plantantion ni kweli kabisa kama anavyosema Mheshimiwa Dkt. Nagu kwamba shamba lile baada ya kuwekewa utaratibu ambao Halmashauri wanakodisha kwa wananchi, tayari kuna malalamiko yametufika kwamba utaratibu ule haujaweza kufanya lile ambalo lilitegemewa. Kuna malalamiko kwamba kuna wajanja wameingilia vilevile wale walengwa ambao walikuwa ni wananchi wa kawaida, maskini, wakulima wadogo wao inaelekea hawajanufaika katika mpango huu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara bado inaendelea kulichunguza suala hili na ikibainika kwamba lile lengo ambalo tulikusudia halifikiwi, Wizara itachukua utaratibu mwingine kuhusiana na shamba la Basutu plantantion.
MHE. DKT. MARY M. NAGU: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kunipa fursa hii. Kama ilivyo kwa Bwawa la Makambako, Wizara ya Maji iliahidi Wilaya ya Hanang’ kuchimba Bwala la Gidahababieg kwa miaka saba. Naomba niulize ni lini bwawa hilo litachimbwa ili wale watu waliopata matatizo kwa miaka mingi waweze kupata maji?Ahsante.
WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nijibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mbunge ambaye pia ndiye Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Maji, Kilimo na Mifugo kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli bwawa hili amekuwa analipigania kwa muda mrefu lakini katika bajeti ya mwaka huu tutaanza kwanza kufanya usanifu ili tuweze kujenga bwawa hilo. Baada ya kujua gharama ya ujenzi ni kiasi gani na michoro itakuwa namna gani, basi tutajenga bwawa hilo kwa mwaka huu wa fedha unaokuja 2017/2018.
MHE. DKT. MARY M. NAGU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa fursa hii. Naomba nimpe taarifa Mheshimiwa Keissy kwamba Wilaya ya Hanang ina Ziwa Basutu na ina samaki wengi sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa hatuna polisi wa kutosha na ndiyo maana tunashindwa kudhibiti hawa wavuvi wanaotumia nyavu ndogo ndogo. Je, Serikali haioni kwamba itakuwa vizuri sana kuwahamasisha wananchi wa Tanzania kuanzisha mabwawa mengi ya kufugia samaki na wazungu wanaita aqua culture kama namna ya kuwafanya wavuvi wakawa na samaki wa kutosha na wakaacha kutumia nyavu ndogo ili waweze kuendelea kuishi?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI:
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nikiri kwamba Jimboni kwa Mheshimiwa Dkt. Mary Nagu kuna uvuvi katika Ziwa Basutu ambao wananchi wake wanategemea sana na Serikali inatambua fika. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile nakubaliane naye kwamba kwa sasa jitihada kubwa duniani ni kuelekea kwenye uvuvi ambao tunaita ufugaji wa samaki (aqua culture) na tunatambua kwamba hata hapa kwetu, Serikali tayari imechukua jitihada za kutosha kuhahakisha kwamba tuna-diversify sasa kutoka kwenye uvuvi wa kutumia maji kuelekea kwenye ufugaji wa samaki. Ndiyo maana kuna mikakati mbalimbali inaendelea. Kuna Waheshimiwa Wabunge wanafahamu kwamba sasa kuna ufugaji unaitwa ufugaji wa vizimba (cage culture).
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile hata aqua culture sasa hivi Serikali inawezekeza katika ufugaji wa samaki kwa utaratibu wa aqua culture na tayari kuna vituo ambavyo vinazalisha vifaranga.
Kwa hiyo, kama kuna Mheshimiwa yeyote anataka kuwekeza au kusaidia wananchi wake wawekeze katika ufugaji wa samaki, awasiliane na mimi ili nimwelekeze pa kupata vifaranga.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tayari kuna mradi mkubwa unaitwa Sawfish ambao unajaribu kuhahakisha kwamba tunaanchia nafasi, rasilimali zetu za uvuvi kwenye maji ya kawaida kwa kuweza kuwekeza kwenye ufugaji wa samaki kwenye nchi kavu. Kwa hiyo, tuna jitihada hizo ndani ya Serikali.
MHE. DKT. MARY M. NAGU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nami nakushukuru kwa kunipa nafasi. Pia naishukuru Serikali kuchimba visima vya Dumbeta, Waranga, Hirbadaw, Gidika na Dawar lakini ndiyo imebakia hivyohivyo wamechimba visima lakini havitumiki kwa sababu hawakuweka pampu na hatukusambaza maji. Naomba niiulize Wizara ya Maji watasaidiaje Wilaya yangu ya Hanang kuona kwamba hivi visima vilivyochimbwa vinawapatia maji wananchi kwa sababu wanayasubiri na lile ni eneo kame sana? Naomba jibu la swali hili.
WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali moja la Mheshimiwa Mwenyekiti wangu wa Kamati ya Kilimo, Mifugo na Maji, Mheshimiwa Dkt. Mary Nagu, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli tumechimba visima na maji yamepatikana kinachofuatia sasa hivi ni suala la kitaalam, wanafanya pamp test kuhakikisha kwamba maji yaliyopo yana utoshelevu wa kutosha na ili waweze ku-design miundombinu itakayowezesha hasa kujenga matenki na mtandao wa mabomba ili wananchi waweze kupata maji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, maagizo yangu baada ya maji kupatikana Halmashauri sasa waanze kufanya kazi hiyo ili tuweze kutekeleza hiyo miradi na ndiyo utaratibu wetu, huwezi kutekeleza miradi bila kuanza kupata chanzo cha maji. Kwa hiyo, nimpongeze Mheshimiwa kwamba chanzo cha maji sasa amepata kinachofuatia ni kuweka miundombinu.
MHE. DKT. MARY M. NAGU: Mheshimiwa Spika, naomba nimshukuru Mheshimiwa Waziri kwa kulifanyia swali langu kazi ya kutosha. Naomba niulize maswali mawili ya nyongeza. Swali la kwanza, kutokana na kutenga Sh.253,913,281/= kwa ajili ya ununuzi wa vifaa vya maabara. Je, ni lini fedha hizo zitatolewa kwa sababu, zikichelewa watoto watakuwa wanakosa masomo ya sayansi ki- practical?
Mheshimiwa Spika, swali lingine dogo la pili ni kwamba, kutokana na kutenga shilingi milioni 70 kwa ajili ya kukamilisha ujenzi wa maabara zile ambazo bado hazijakamilika, ningependa kujua kwa dhati kutoka kwa Mheshimiwa Waziri, lini fedha hizo zitatoka? Nami naahidi kuwahamasisha wananchi wa Hanang kujitolea kwa kiasi ambacho kimepangwa?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE): Mheshimiwa Spika, ni azma ya Serikali kuhakikisha kwamba, hiki ambacho kimekusudiwa kwa maana ya kununua vifaa vya maabara na kukamilisha maabara inafanyika kwa wakati. Pindi pesa zitakapokuwa zimekamilika kupatikana hakika nimhakikishie Mbunge kwamba, pesa hizo zitapelekwa. Cha msingi tuhakikishe kwamba, zinafanya kazi iliyokusudiwa.
Mheshimiwa Spika, swali lake la pili, majibu yake ni sawa na lile la kwanza.
MHE. DKT. MARY M. NAGU: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi.
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kwamba vituo vya afya na zahanati tunavihitaji sana na Serikali inajitahidi sana katika kusaidiana na wananchi kuvijenga vituo hivi na zahanati hizo. Je, si itakuwa ni kazi bure kama tutakuwa na vituo vya afya na zahanati ambazo hazina watumishi ambao watawapa huduma Watanzania? Naomba Serikali ione hilo kwa sababu huduma ya afya ni ya msingi sana watu wetu wasiendelee kuteseka. (Makofi)
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nimpongeze Naibu Waziri kwa majibu mazuri aliyotoa, lakini nataka kutoa majibu ya nyongeza kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, wakati tunahakiki vyeti, watumishi wengi sana imebidi waachishwe kazi na moja kati ya idara ambayo imeathirika sana ni afya. Tumeambiwa katika baadhi ya maeneo hata zahanati zimelazimika kufungwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kulitaarifu Bunge lako Tukufu kwamba Serikali ilikwishatoa kibali cha ajira watu 50,000. Wizara yangu katika wale 50,000 kipaumbele namba moja ni afya na nataka nisema kama kuna Halmashauri yoyote ambayo huduma zimesimama kwa sababu watu wameondolewa na hawajapata watu mbadala waandike moja kwa moja kwangu watapatikana mara moja. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu suala alilouliza Mheshimiwa Mary Nagu, nataka niwaambie Watanzania waondoe mashaka. Tuendelee sisi wanasiasa, viongozi kuhimiza ujenzi wa vituo vya afya na zahanati pale ambapo inakaribia kukamilika au wakati inajengwa Wizara yangu ikipata taarifa itafanya maandalizi wapatikane watumishi kabla ujenzi haujakamilika. (Makofi)
MHE. DKT. MARY M. NAGU: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kunipa fursa. Naomba niipongeze Wizara na Serikali kwa kutengea fedha Mradi wa Endasak, Endagao na Endeshwal na Mradi wa Malama.
Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na hivyo miradi hii miwili imepangiwa shilingi bilioni 1.31 na bilioni 1.2 mradi wa pili na naishukuru Serikali kwa kuanza kutekeleza mradi, lakini imechukua muda mrefu sana. Naomba kujua kutoka kwa Mheshimiwa Waziri, ni lini kasi itaongezeka ili miradi hii miwili iweze kukamilika kwa sababu Wilaya ya Hanang ilivyo chini ya Rift Valley ina ukame na watu wanapata shida kubwa sana ya kutafuta maji?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI:
Mheshimiwa Naibu Spika, nikushukuru sana kwa kunipa nafasi hii lakini nimpongeze sana Mheshimiwa Mary Nagu, mama yangu kwa namna anavyowapigania wananchi wake. Kubwa ni kwamba sisi kama Wizara ya Maji jukumu letu ni kuwapatia wananchi maji. Zipo changamoto ambazo tumekumbana nazo, moja ni wakandarasi ambao wamekuwa wakifanya kazi kwa kusuasua.
Mheshimiwa Naibu Spika, labda nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge, sisi kama Wizara tumejipanga kwa mkandarasi ambaye atatuchelewesha katika kuhakikisha wananchi wanapata maji, hatuna sababu ya kujadiliana naye, tutamwondoa, tutamweka mtu ambaye ataweza kufanya kazi kwa wakati ili wananchi waweze kupata maji kwa muda uliopangwa. Ahsante sana.
MHE. DKT. MARY M. NAGU: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kumshukuru sana Mheshimiwa Naibu Waziri kwa kujibu swali kwa ufupi lakini kama tunavyotegemea, ahsante sana Mheshimiwa Naibu Waziri. Sasa naomba niulize maswali mawili madogo kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, maji ya Mji wa Katesh yanaendeshwa kwa umeme wa grid lakini bado gharama ni kubwa. Naomba Mheshimiwa Naibu Waziri anihakikishie kwamba atatuma wataalam kuona kwa nini gharama ile iko juu ili watu wa Katesh waweze kupata maji kwa sababu kwa sasa hivi wanapata mara katika wiki na ni hatari kwa mji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali lingine dogo la pili ni kwamba; ninamshukuru sana Mheshimiwa Naibu Waziri huyu kwa kuona umuhimu wa vijiji kuwa na umeme ili wanapochimba visima waweze kusukuma maji kwa nguvu ya umeme. Hata hivyo Wilaya yetu ni moja ya Wilaya ambayo imepata vijiji vichache. Je, Mheshimiwa Naibu Waziri anaweza kunihakikishia kwamba vijiji vyetu vingi sasa vitapata umeme wa REA na kwamba Mkoa wa Manyara ataanzia na Wilaya ya Hanang? Ahsante.
WAZIRI WA NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa kuhusiana na kutuma wataalam wakaangalie kama bei ni halisi, Mheshimiwa Mary Nagu kwanza nakupongeza sana kesho wataalam watakwenda kwenye site wataangalia ili wajiridhishe kama ni sahihi, nitawaagiza waende washirikiane na watu wako walioko kule. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusiana na vijiji ambavyo ameseme Mheshimiwa Mary Nagu, kwanza nakupongeza Mheshimiwa Mary Nagu, wakati wakati wa bajeti yetu ulitupatia vijiji vyako 44 ili tuvipelekee umeme. Sasa napenda kuwahakikishia wananchi wa Hanang kwamba vijiji vyako vyote 44 ulivyotupatia ikiwepo kijiji cha Gocho, kijiji cha Kaltaki, kijiji cha Gawindu pamoja na Kateto na vitengoji vyake vyote vitapata umeme Mheshimiwa Nagu.
MHE. DKT. MARY M. NAGU: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali moja la nyongeza.
Mheshimiwa Spika, kwanza nitashukuru sana kama TAMISEMI itakwenda kujua ukweli ni nini. Swali langu ni kwamba shule zile zilizotajwa za Katesh, Gendabi, Balangdalalu na Bassodesh sasa hivi kwa muda mrefu hazijapewa hela za chakula na ni shule za bweni. Taarifa hizo nimezifikisha kwa Mawaziri, nataka kujua, je, watoto waendelee kukaa bila chakula au kuna hatua ambazo zimechukuliwa? Ahsante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Spika, ni kweli siku ya Mei Mosi tulikuwepo pale Katesh na Mama Mary Nagu na alilileta tena jambo. Hata hivyo alilifikisha ofisini kwetu na ofisi ya Naibu Katibu Mkuu Elimu ilikuwa inashughulikia jambo hili. Kwa hiyo Mama Mary Nagu naomba vuta subira, tunadhani jambo hili linafikishwa mahali pazuri. Nadhani tutahakikisha kwamba watoto wale wanaweza kupata huduma kama ulivyopeleka katika maombi yale. (Makofi)
MHE. DKT. MARY M. NAGU: Mheshimiwa Spika, na mimi niungane na wenzangu kukupa pole na kushukuru na kufurahi kukuona leo Bungeni. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, ni kweli kama alivyouliza Mheshimiwa Mbunge aliyetangulia, Mohamed Kigua, kwamba kwa kweli miradi ya maji ina matatizo mengi na ni vizuri kwa kweli tathmini ikafanywa. Wilaya yangu ya Hanang ina visima vilivyochimbwa vina mwaka mmoja hakuna kuendeleza maji yakapatikana na watu wanatoa machozi pale, na mimi naomba na tathmini hiyo au Tume nayo iende kule Hanang kuona tatizo ni nini ili tuweze kusahisha wananchi wapate maji.
WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Spika, na mimi nichukue nafasi hii kukukaribisha. Karibu sana kwenye Bunge, tangu ulivyotuacha, tunaendelea vizuri.
Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la mama yangu Mheshimiwa Mary Nagu kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, kwanza kabisa kuhusu changamoto za miradi, Wizara yangu tayari imeunda timu ya wahandisi ambayo imeshaanza kazi, ambayo itakuwa inapitia maeneo yote ya changamoto. Ni wataalam wazuri, wataainisha changamoto zote ili tuweze kuzifanyia kazi.
Mheshimiwa Spika, pili, kuhusu miradi ambayo tumeshapata vyanzo vya maji kama kwa Mheshimiwa Mary Nagu kule Katesh, katika Programu ya Utekelezaji wa Miradi ya Maji kwanza tunatafuta chanzo, tukishapata chanzo ndiyo tunatafuta sasa fedha kwa ajili ya kuweka mtandao wa mabomba.
Kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mary Nagu kwamba bajeti inayokuja tutaweka fedha za kutosha ili tuweze sasa kuyachukua maji na kuyapeleka kwa wananchi. (Makofi)
MHE. DKT. MARY M. NAGU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Naomba kuuliza, hivi haionekani kwamba wanapokuja wataalam wa TAMISEMI kugawa upya vijiji na hata vitongoji wanaleta migogoro ambayo haiishi na maendeleo kusitishwa? Je, Waziri anasema nini kwa migogoro ambayo ipo na imewadhuru watu ambao wako kwenye maeneo hayo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPH G. KAKUNDA): Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilivyojibu kwenye maswali ya nyongeza ya muuliza swali la msingi, migogoro yote inashughulikiwa isipokuwa kuna baadhi ya maeneo ambayo kulikuwa na matatizo ya usajili wa vijiji na vitongoji ambapo baada ya kupitia upya taratibu imeonekana kwamba kuna baadhi ya maeneo taratibu zilikiukwa.
Kwa hiyo, kule ambako taratibu zilikiukwa, pengine usajili wa kijiji au kitongoji ulipenyezwa bila kufuata utaratibu rasmi wa Serikali, maeneo hayo baadaye yamefanyiwa marejeo ya kufuta usajili wa kijiji au kitongoji. Kwa hiyo, suala hilo likishafanyika inakuwa siyo mgogoro tena. Kwa hiyo, nimuombe Mheshimiwa Mbunge kama kuna migogoro ya aina hiyo basi tuwasiliane ofisini kwa Katibu Mkuu wa TAMISEMI ili kuweza kufuatilia vizuri zaidi na kurekebisha.
MHE. DKT. MARY M. NAGU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi hii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama ulivyo Mji Mdogo wa Igunga, Mji wa Katesh nao ulianzishwa kuwa Mamlaka Ndogo ya Halmashauri ya Wilaya ya Hanang, lakini ni kweli kwamba Halmashauri haiipi kipaumbele hii Miji Midogo iliyoanzishwa. Je, Serikali itaweka utaratibu mzuri wa kuona hii Miji Midogo iliyoanzishwa inapata hela au kuipandisha hadhi? Kama sivyo, miji hiyo itabaki inadumaa na wakati ndiyo inayotoa mapato makubwa kwa Halmashauri. Naomba Serikali iseme wataweka utaratibu huo lini ili Miji Midogo iwe na uhakika wa kuendelea? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE):
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nijibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Dkt. Mary Nagu, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, siyo nia ya Serikali kukiuka kile ambacho kinaitwa D by D. Kwa mujibu wa Katiba ni sisi ambao tuliamua kwamba tunapeleka madaraka kwa wananchi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, namwomba Mheshimiwa Mbunge, kwa kupitia vikao vyetu ambavyo naye ni Diwani anaporudi kule, sisi tukiwa Madiwani kule ndiyo ambao tunafanya maamuzi kuona namna iliyo bora ya kuhakikisha kwamba Halmshauri zetu zinafanya kazi iliyokusudiwa. Itakuwa siyo busara Ofisi ya Rais, TAMISEMI kwenda kuziingilia zile Halmashauri ambazo Waheshimiwa Madiwani wakikaa wana maamuzi ambayo ni sahihi nasi tunakuja kubariki kutokana na vikao vyao ambavyo ni halali.
MHE. DKT. MARY M. NAGU: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kunipa fursa hii. Kama ilivyo Liwale, Wilaya ya Hanang kila upande imezungukwa na migogoro ya mipaka kati yake na Mbulu, Singida na Kondoa. Nataka kujua TAMISEMI itachukua hatua gani, kwa sababu imekuwa muda mrefu mno, hatimaye watu watauana kule ili haya matatizo ya mpaka yanayotukabili yaweze kutatuliwa na watu waishi kwa amani? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Spika, ahsante. Migogoro ya mipaka iko mingi katika maeneo mengi lakini suluhisho la kwanza katika kutatua ile migogoro ni kwa pande zote mbili za maeneo husika kukaa. Kwa hiyo, pale wanapokuwa wamekaa wamekubaliana kwa pande zote mbili na hasa panapokuwa na utata, hapo ndipo Wizara inakuja kuingia kwa ajili ya kusaidia. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, niombe tu, pamoja na swali la Mheshimiwa Dkt. Mary Nagu na wengine ambao wana migogoro, pale inaposhindikana ndipo hapo tunatakiwa kuingilia kati kwa sababu huwezi kuingilia kati kabla pande zote mbili hazijakaa na kuridhia na kwa kuangalia zile GN zilizounda maeneo hayo ziko katika utaratibu upi.
MHE. DKT. MARY M. NAGU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakupongeza kwa kuendesha vizuri Bunge letu na ninakushukuru kwa kunipa nafasi hii ya kuuliza swali la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Wilaya ya Hanang ni moja ya Wilaya ambazo mvua hazina uhakika na ninaishukuru Serikali kwa kutoa fedha kwa ajili ya mradi wa Endagau wa umwagiliaji. Hata hivyo, mradi huo ulikuwa na mushkeli. Naomba kumwuliza Mheshimiwa Naibu Waziri kama wametoa fedha za kutosha kusahihisha yale mambo ya kitaaluma ambayo hayakwenda vizuri na umwagiliaji hauendi vizuri ili wananchi wa Hanang waweze kuwa na uhakika wa kupata chakula kutokana na umwagiliaji.
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara yetu imekuwa inafanya jitihada kubwa sana ya kutoa fedha katika kuhakikisha inakamilisha miradi mbalimbali. Itakuwa ni jambo la aibu na fedheha kwamba tunapeleka fedha halafu hazifanyi kazi kama ilivyotarajiwa. Nataka nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba baada ya Bunge tutafika hapo katika Jimbo lake ili kuweza kuhakikisha kama fedha zimepelekwa, nao kwa nini wasizitumie kama ilivyotarajiwa? Kama kuna ubadhirifu wowote, tutaweza kuchukua hatua kwa wale wahusika.
MHE. DKT. MARY M. NAGU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi. Naomba niulize swali la nyongeza kama ifuatavyo; vijiji vingi vya Wilaya ya Hanang havina maji na vile ambavyo vimebahatika kuchimbiwa visima, visima havijakamilika.
Je, Mheshimiwa Waziri ananiambia nini ili kuhakikisha vile visima vilivyochimbwa vinakamilika na wale waliobahatika kuwa na visima hivyo waweze basi kunywa maji na kutumia kwa matumizi mengine? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote kwanza napenda nimpongeze sana mama yangu Mheshimiwa Nagu amekuwa ni mtetezi mkubwa sana wa wananchi wake katika suala zima la maji. Amekuwa analipigania na amekuwa akifuatilia katika Wizara yetu ya Maji na Waziri wangu ambaye ni Mheshimiwa Kamwelwe aliwaagiza watu wa DDCA kwenda kuchimba visima vya maji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka niwahakikishie kwamba tutawaagiza watu wetu wa DDCA katika kuhakikisha vile visima wanavikamilisha kwa wakati, ili wananchi wako waweze kupata maji safi, salama na yenye kutosheleza. (Makofi)
MHE. DKT. MARY M. NAGU: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana…
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna unaoitwa Endagaw ambao namshukuru sana Mheshimiwa Waziri kufika kule na kuona changamoto ambazo zipo kwenye ule mradi wa umwagiliaji. Napenda kumuuliza Mheshimiwa Naibu Waziri katika changamoto alizoziona ni zipi ambazo sasa zimeondolewa ili wananchi wa Hanang waweze kunufaika na umagiliaji katika Mbuga ya Endagaw?
WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nimpongeze Mheshimiwa Dkt. Mary Nagu kwa jinsi ambavyo anafuatilia miradi katika Jimbo lake na alinibeba mpaka hilo eneo la Endagaw na nikafika pale nikakuta katika mifereji miwili iliyojengwa mmoja unatiririsha maji mmoja uko juu. Katika bajeti hii ambayo Waheshimiwa mmeipitisha tayari tumetenga fedha kwa ajili ya kwenda kurekebisha ule mfereji ili uwe unapeleka maji vizuri. (Makofi)
MHE. DKT. MARY M. NAGU: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Naipongeza na kuishukuru sana Serikali kwa kutoa fedha za kuweza kuimarisha upatikanaji wa maji Mji wa Kateshi ambao ni Makao Makuu ya Wilaya ya Hanang na wenyewe viongozi wapo hapo Gallery, naomba Mheshimiwa Waziri atuhakikishie kwamba ifikapo mwezi wa tisa ambapo ni ukame na hamna maji Kateshi kama maji hayo yatapatikana na nitaishukuru zaidi Serikali. Mheshimiwa Spika, ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Spika, awali ya yote kwanza nimpongeze sana Mheshimiwa Mbunge kwa kazi kubwa anayoifanya na amekuwa mfuatiliaji mkubwa sana katika suala zima la maji katika Mji wa Kateshi. Kubwa nimhakikishie utekelezaji wa miradi ya maji unategemeana na fedha, Serikali imeshatafuta fedha na imeshapata. Kwa hiyo, nimwombe Mhandisi wa Maji afanye kila linalowezekana katika kuhakikisha wananchi hawa ndani ya mwezi wa Tisa wanapata maji safi, salama na yenye kuwatosheleza.
Mheshimiwa Spika, lingine nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge, baada ya Bunge nitafika Kateshi katika kuhakikisha tunaongeza msukumo ili wananchi wake waweze kupata maji safi. (Makofi)
MHE. DKT. MARY M. NAGU: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kunipa fursa hii adimu. Wilaya ya Hanang’ ina Kituo cha Afya kimoja ambacho ndicho kinakarabatiwa sasa lakini kuna Wilaya kubwa haina Kituo cha Afya kingine. Nilimwomba Mheshimiwa Waziri Kituo cha Afya cha Basotu na Kituo cha Afya cha Endasak ambako kuna watu wengi ambao wanategemea huduma hiyo, atusaidie. Je, anaweza kutuambia ni lini ukarabati huo utaanza ili watu wa Endasak na Basotu waweze kunufaika na huduma ya afya? Mheshimiwa Spika, ahsante sana.
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Spika, naomba nikiri kwamba Mheshimiwa Mary Nagu, tena alikuja na wananchi wake tukiwa getini alileta hiyo hoja. Nakiri wazi pia kwamba Endasak na Basotu ni changamoto kubwa na ina population kubwa. Nia na mpango wa Serikali ni kwamba Mungu akijaalia kabla ya mwezi wa Tisa tutakuwa tumeshaanza ujenzi pale Basotu kwa kadri kama tulivyokubaliana siku ile. (Makofi) Mheshimiwa Spika, nashukuru.
MHE. DKT. MARY M. NAGU: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kuniona, nilikuwa nimetoka kidogo nje.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna barabara kule Manyara inafanana na barabara iliyoulizwa na muuliza swali la msingi, inaitwa Mogitu – Basotu - Hyadom na Hyadom ni hospitali kubwa ya rufaa kule ambayo inahudumia watu wengi wa Mkoa wa Manyara. Barabara hiyo ni ahadi ya Rais akiomba kura; je, process au mchakato wa kujenga barabara hiyo utaanza lini ili watu wanufaike na ile Hospitali ya Hyadom ambayo kwa kweli imekuwepo kwa miaka mingi? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA):
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la shemeji yangu, Mheshimiwa Dkt. Mary Michael Nagu, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, barabara hii ambayo anaizungumzia Mheshimiwa Mbunge ni barabara ambayo kwa kweli imekuwa ikisemewa na Waheshimiwa Wabunge wengi. Kwa hiyo, nimpongeze sana Mheshimiwa Mbunge pamoja na Waheshimiwa Wabunge wa Mbulu wana ushirikiano mkubwa maana wanaizungumzia sana barabara hii.
Mheshimiwa Naibu Spika, niseme tu kwamba wakati wowote wadau wote ikiwemo Waheshimiwa Wabunge tutakuwa na kikao cha kuzungumzia barabara hii ambapo sasa itakuwa inatoka Mbulu Mjini - Katesh - Hyadom - Sibiti tunaungana pia na mikoa ile ya upande wa Kanda ya Ziwa. Barabara hii usanifu wake na michoro imeshakamilika, hatua iliyopo sasa ni kuzungumza na wadau ili tuendelee na hatua nyingine kwa sababu zipo indication za kupata fedha kutoka Serikali ya Ujerumani kama sikosei kwa ajili ya ujenzi wa barabara hii. Kwa hiyo, natambua umuhimu wa muunganiko wa barabara hii.
Mheshimiwa Naibu Spika, wakati Bunge linaendelea kama wiki mbili zilizopita nimetembelea kipande ambacho kinakwenda kuunganisha barabara hii kikitokea Singida. Kutokana na umuhimu wa eneo hili la Hyadom kwa sababu ile hospitali ni kubwa na huduma nyingi sana kwa wananchi wengi kutakuwa na kipande cha kilometa 93 kutoka Singida kwenda Hyadom. Wakati naikagua ile barabara kwa sababu ilikuwa haipitiki, nimeenda mpaka Hyadom lakini nimeona pia logistics za barabara hiyo ambayo Mheshimiwa Mbunge anaizungumza.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo nimhakikishie tu Mheshimiwa Dkt. Mary Nagu na wananchi wote wa maeneo yake kwamba hii barabara sasa ujenzi wake uko karibu. Imechukua muda mrefu lakini wasiwe na wasiwasi, upo mpango mzuri wa kujenga barabara hii inayounganisha Mikoa ya Arusha, Manyara, Singida, Simiyu, Shinyanga pamoja na Mwanza. Hii ni barabara muhimu sana kwa sababu eneo hilo linazalisha sana mazao mengi na huduma ya afya kama nilivyosema ni muhimu sana kwa wananchi wa maeneo haya.
MHE. DKT. MARY M. NAGU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana. Wilaya ya Hanang ilipata vijiji vichache sana awamu ya kwanza ya REA na awamu ya pili. Hii awamu ya tatu Mheshimiwa Waziri ameniahidi atanipa vijiji vingi lakini vile tulivyokubaliana ameacha Gocho, Dumbeta, Gisambalang’ na Getasam. Mheshimiwa Waziri amesema atakwenda na mimi sasa anaahidi kila mmoja, sijui kama atapata nafasi ya kwenda na mama yake. Ahsante. (Kicheko)
WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana kwa swali la nyongeza la Mheshimiwa Mbunge.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa ni kweli nilimuahidi Mheshimiwa Mbunge kwamba nitakwenda Hanang, lakini kabla sijaenda Hanang tulimpa vijiji 47 vya kuanzia na tukamwongezea vijiji vingine 12, kwa hiyo, lazima tuvitembelee. Kati ya vijiji ambavyo tumeviongeza ni pamoja na Gocha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, niwahakikishie wananchi wa Hanang mbali tu na kuongozana na Mheshimiwa Mbunge lakini nitawatuma wakandarasi waanze kufanya kazi hizo ili wakati tunakwenda, tunakwenda kuwasha na wala siyo kukagua peke yake.
MHE. DKT. MARY M. NAGU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kuniona. Barabara zote zilizozunguka Mlima Hanang kutokana na mvua kutoka Gendabi, Hatgabadau, Katesh, Gitting, Gerodom na Gendabi zote zimeharibika. Naamini kwamba zitakuwa zimeoneshwa kwenye needs assessment. Je, Mheshimiwa Waziri anasemaje kwa sababu kuna makorongo makubwa yanayozuia akinamama kwenda hospitali na watoto kwenda shuleni?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPH G. KAKUNDA): Mheshimiwa Mwenyekiti, mazingira ya Mikoa hii ya Manyara na Arusha yanafahamika, hasa maji yanapoporomoka kutoka kwenye milima yana tabia ya kuharibu barabara kwa haraka sana. Kwa hali hiyo, kama ambavyo Mheshimiwa Waziri wangu amewaagiza Mameneja wa TARURA wote kufanya tathmini ya kina ili maeneo yale yaweze kupata uhakikisho maalum wa matengenezo ambayo yatahakikisha kwamba hayo maji hayaharibu kwa haraka barabara zetu katika maeneo hayo kama ambavyo imekuwa ikitokea. Napenda kumwahidi Mheshimiwa Dkt. Mary Nagu kwamba tutalifuatilia utekelezaji wa agizo hilo kikamilifu ili maeneo hayo ili tuweze kuyapa kipaumbele kinachotakiwa. (Makofi)
MHE. DKT. MARY M. NAGU: Mheshimiwa Mwenyekiti, naipongeza REA kwa kazi nzuri, lakini hata hivyo katika Wilaya yetu ya Hanang kuna changamoto nyingi ambazo tunaziona, kwa mfano kuna taasisi ambazo hazijapata umeme pale ambapo umeme umeletwa, kuna maeneo yanarukwa njiani wanakwenda kwingine, je, Waziri atakubali kuja kutembelea Hanang ili tuone changamoto hizo ili tuzisahihishe na kama anaweza kumtuma mkandarasi kuja kuona changamoto hizo?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru mama yangu, Mheshimiwa Dkt. Nagu na tumekubali huo mwaliko wa kutembelea kwa kuwa sisi Wizara yetu pamoja na Mheshimiwa Waziri na viongozi mbalimbali tumekuwa tukifanya ziara kwa kuwa miradi hii inatekelezwa vijijini. Kwa hiyo, naomba nimuagize pia mkandarasi Angelic, tuliwapa maelekezo wakandarasi wote taasisi muhimu za umma zipatiwe huduma hii ya umeme na maelekezo ya Serikali kupitia Mheshimiwa Rais pia mwenyewe kwamba vijiji visirukwe. Kwa hiyo, naomba nisisitize maelekezo haya yako palepale na tutafanya ziara katika maeneo yote likiwemo Jimbo la Hanang.
MHE. DKT. MARY M. NAGU: Mheshimiwa Mwenyekiti, namshukuru sana Mheshimiwa Naibu Waziri kwa kujibu swali langu vizuri. Swali la kwanza, kama Waziri alivyoeleza ni kwamba mfumo umebadilika lakini kama ilivyo kule Hanang bei bado haijashuka na madhumuni ya kuwa na mfumo huu wa sasa ni kushusha bei. Nataka kujua kwa nini bei haijashuka mpaka sasa?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu la pili, mfumo wa sasa unapaswa kuwafikia wakulima wote badala ya ule wa ruzuku kufikia watu wachache peke yake. Hata hivyo, nataka kujua kwamba huu ununuzi wa pamoja wa mbolea kama kweli umewanufaisha watu kama wanavyotarajia na kama Serikali inavyotaka na kama sivyo watuambie ni msimu upi mfumo huo wa sasa utanufaisha wakulima wote kuliko ilivyokuwa pale awali?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza naomba nimpongeze sana kwa jinsi ambavyo amekuwa akishugghulikia suala zima la mbolea na mfumo wa pamoja na ukizingatia yeye alikuwa ni Mwenyekiti wa Kamati yetu ya Kilimo, Mifugo na Maji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nikija kwenye maswali yake mawili ya nyongeza ni kwamba ni kweli bei haijashuka kwa sababu mfumo huu tumeuanza sasa hivi na matokeo yake mazuri tutayaona kuanzia msimu ujao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika lile swali lake la pili ni kwamba mbolea yetu ambayo tunasema ina bei elekezi ya Serikali tunapaswa tuwaambie wananchi wote wasubiri msimu unaotakiwa ili iuzwe kwa pamoja lakini vilevile hata wale wazabuni wetu tunataka wawe wanafanya order kwa wingi kwa pamoja.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile naomba nitoe ushauri, hata wale wafanyabiashara kwenye yale maghala yao wajenge kwa wingi ili maghala yale kulekule katika halmashauri wawe wanazalisha ili huu msimu unapofika basi wananchi na wakulima wetu waweze kupata mbolea zile kwa wakati na kwa pamoja inavyotakiwa.
MHE. DKT. MARY M. NAGU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana kwa kunipa fursa hii na nimpongeze Mheshimiwa Naibu Waziri kwa kujibu vizuri na Serikali kuwa na mkakati mzuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali ina mkakati gani wa kuongeza deposit rate, maana watu wengi hawaweki fedha benki kwa sababu riba ni ndogo sana na riba ya kukopesha ni kubwa sana. Kama mkakati huu ukitekelezwa benki itakuwa na fedha nyingi ya kukopesha kwa riba ndogo. Naomba jibu, je, Serikali ina mkakati gani kuhusu suala hili?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali moja la nyongeza la mtani wangu, Mheshimiwa Dkt. Mary Michael Nagu, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilivyosema kwenye majibu yangu ya msingi, Serikali inashughulika na Sera ya Sekta ya Fedha na nimeainisha hatua mbalimbali tulizozichukua. Moja katika taratibu zilizopunguzwa ni statutory minimum reserve rates za mabenki yetu. Tumeona sasa, kama nilivyosema tangu awali, riba zinapungua na hivyo hata deposit rate nayo itaweza kuongezeka ili kuona kwamba Watanzania wanaweza kuweka fedha zao katika benki zetu.
MHE. DKT. MARY M. NAGU: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi.

Mheshimiwa Naibu Spika, kama ilivyo Morogoro naishukuru sana Serikali kuona tatizo la Mji Mkuu wa Wilaya ya Hanang na kuweza kuwapangia zaidi ya shilingi bilioni 2. Naomba kuuliza naona kama speed ni ndogo, je, mradi ule utafikisha maji kata 20 kwa sababu wanachotaka kuona wananchi wanakunywa maji na wanatumia maji.
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nimpongeze Mheshimiwa Mbunge mama yangu Mheshimiwa Dkt. Mary Nagu, maeneo yenye changamoto kubwa sana ni katika jimbo lake lakini sisi kama Serikali tuna mradi mkubwa sana pale ambao tumeuwekeza kwa ajili ya kutatua tatizo la maji Hanang. Nataka nimhakikishie sisi kama Wizara na viongozi wa Wizara hii tunamwagiza mkandarasi lazima afanye kazi usiku na mchana, kama atashindwa kufanya kazi ile kwa haraka sisi tutamwondoa tutamweka mkandarasi ambaye anaweza kufanya ile na kuweza kukamilisha mradi kwa mujibu wa mkataba kama ulivyopangwa. Ahsante sana.
MHE. DKT. MARY M. NAGU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza kwa jambo muhimu kama hili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wanaofanya bidii na kushirikiana na Wabunge ni Madiwani na Wenyeviti katika kuhamasisha maendeleo katika maeneo yao; sasa kama Halmashauri inaweza kuwa na uwezo wa kulipa posho zaidi: Je, Serikali inaweza ikaruhusu Halmashauri ile yenye uwezo kuongeza posho kwa hawa ambao ndio wanaoweza kuongeza mapato hayo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. MWITA M. WAITARA): Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Kwanza nampongeza Mheshimiwa Mbunge sawa na Wabunge wengine wote ambao wameendelea kuwasemea Waheshimiwa Wenyeviti wa Mitaa na Waheshimiwa Madiwani, nao ni viongozi wenzetu na hakuna namna ya kuweza kuwapuuza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeeleza hapa kwamba wakati wa Bajeti kulikuwa na mjadala; na kweli kuna Waraka ambao umepelekwa katika Halmashauri zetu ambao unaelekeza fixed amount kulipwa kwenye posho za Madiwani ukiacha ile posho ya mwezi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimesema Mheshimiwa Waziri aliahidi mbele ya Bunge lako Tukufu na naomba niseme, bado ametoa ametoa maelekezo, ndani ya muda siyo mrefu sana, Waraka kutoka Ofisi ya Rais, TAMISEMI kupitia Katibu Mkuu utaenda kwenye Halmashauri zote na suala hili la kulipana Madiwani kulingana na uwezo wa Halmashauri litatekelezwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante.
MHE. MARY M. NAGU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana. Kwanza naishukuru Serikali kwa kutujengea Kituo cha Afya Hirbadawna kukarabati Kituo cha Afya cha Simbay, lakini ilituahidi kwamba itatusaidia kukamilisha Kituo cha Afya cha Bassotuna Endasak.Naomba jibu ili wananchi wa Hanang waweze kufurahi. Ahsante sana.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE): Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nijibu swali la Mheshimiwa Dkt. Nagu kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza naomba nipokee pongezi, yeye mwenyewe anakiri kwamba imefanyika kazi nzuri ya ukarabati wa vituo vya afya viwili kwake na ahadi yetu ya kukamilisha ukarabati wa ujenzi wa vituo vya afya kila kata iko pale pale.

Naomba Mheshimiwa Mbunge awaambie wananchi wawe na subira, lakini ni vizuri na wao wakaanza kujitokeza kwa zile kazi ambazo wanaweza kuanza kufanya ambavyo wananchi wake wamekuwa na mwitikio mkubwa waendelee kufanya na nasisi tutaunga mkono, lakini azma ni kuhakikisha kwamba hivyo vituo viwili navyo vinafanyiwa ukarabati.
MHE. DKT. MARY M. NAGU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kunipa nafasi hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa Kituo cha Afya cha Endasak na Basotu nilishaongea na Mheshimiwa Waziri atusaidie kuboresha ili vionekane kama ni vituo kwa sababu havina hata wodi na havijafikia hadhi ile lakini vinajulikana na wananchi kama ni Kituo cha Afya. Naomba nijue Mheshimiwa Waziri anasema nini kuhusu vituo hivi viwili vya Hanang?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kumshukuru mama yangu Mheshimiwa Dkt. Mary Nagu senior MP katika Bunge hili. Ni kweli niliongea na Mheshimiwa Dkt. Mary Nagu na bahati nzuri nimefika kule Hanang, ni mpango wa Serikali naomba nikuhakikishie Mheshimiwa Dkt. Mary Nagu kama tulivyozungumza ni commitment ya sisi Serikali tunatafuta fedha tutajitahidi kwa kadri iwezekanavyo vituo vile viweze kupata huduma kama tunayokusudia, kwa hiyo, hilo ondoa hofu Mheshimiwa Dkt. Mary Nagu.
MHE. DKT. MARY M. NAGU: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi. Mara chache nimeuliza kwenye sehemu ya Walimu. Nnataka kuuliza, kwa nini kwenye Shule za Halmashauri na nje ya Halmashauri Walimu wanatengwa na wake zao wanapelekwa shule nyingine hata zaidi ya kilomita 100? Hamwoni hiyo itaathiri familia ile ya Walimu na kwamba ni hatari kwa watoto kupata mimba?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. MWITA M. WAITARA): Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Nia ya Serikali tungependa kila mtu akae na mwenza wake karibu, kwa maana kwamba mume akae na mke na mke akae na mume. Hayo ndiyo yalikuwa mapenzi na matarajio ya Serikali.

Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kwamba Waheshimiwa Wabunge wenyewe mmekuwa mkilalamika kwamba kuna maeneo mengine walimu hawapo kwa sababu wanahama sana; na sababu kubwa ni hiyo kwamba anamfuata mume wake au mke wake au sababu nyinginezo.

Mheshimiwa Naibu Spika, tulisema, jambo hili baada ya kupata malalamiko hata kutoka kwa wananchi na Wenyeviti wa Halmashauri, Madiwani, Wabunge na wananchi wengine, kwamba kuna upungufu na kwa hiyo, ikama hai-balance katika maeneo yetu. Serikali ikalichukua na kulifanyia kazi.

Mheshimiwa Naibu Spika, tunatengeneza mfumo ambao kama Mwalimu anataka kuhama kutoka shule A kwenda shule B, pale anapotoka asilete shida, na hapo anapoenda asiende kujaza watu kuliko mahitaji yake. Mfumo huo unaikaribia mwisho. Ukikamilika, hii shida ya walimu kuhama na ku-balance haitakuwa shida, tutaimaliza hilo tatizo.

Mheshimiwa Naibu Spika, mfumo; hata Mbunge ukiomba, ukiwaambia mkoa mzima usambazaji ukoje, Halmashauri ikoje, hakutakuwa na shida. Kwa hiyo, naomba Mheshimiwa Mbunge avute subira. Pia Walimu wanalalamika sana, kuna mambo mengi ya uhamisho. Tutayafanyia kazi yote na hii kero itaisha. Ahsante sana.
MHE. DKT. MARY M. NAGU: Mheshimiwe Mwenyekiti, nakushukuru sana. Naomba niongeze swali dogo la nyongeza, kwamba kule kwangu kuna barabara ya kutoka Waama mpaka Masusu na hatimaye mpaka kule Lalaji na barabara nyingine ya Maskaroda na kwenda Lambo na kwenda Dareda ambapo zinaunganisha wananchi na hospitali na nilishatoa ombi: Je, Serikali inasemaje ili kunisaidia na watu wale ambao wana kilomita 20 kwenda kwenye hospitali wapate namna ya kufika? Nashukuru sana.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE): Mheshimiwa Mwenyekiti, nilipata fursa ya kwenda Jimboni kwa Mheshimiwa Dkt. Nagu kutatua mgogoro wa kijiji na tukafanikiwa kuutatua mgogoro ule. Ingekuwa vizuri sana Mheshimiwa Nagu kama ungeniambia tukapata na fursa ya kwenda kutembelea huko.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu lengo la Serikali ni kuhakikisha kwamba huduma ya usafiri na hasa kwenda hospitali kama ambavyo yeye amesema kwenye swali lake, ni vizuri tukawasiliana na Meneja wa TARURA tujue nini hasa ambacho kinatakiwa kifanyike ili wananchi wetu waendelee kupata huduma na hasa ya kwenda hospitali.
MHE. DKT. MARY M. NAGU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi. Moja ya wilaya ambazo zilipata maeneo machache sana mwanzoni ni Wilaya ya Hanang na sasa bado changamoto ni kubwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Waziri aliniahidi kwamba atatembelea Hanang, mimi nasubiri naomba awaambie wananchi wa Hanang ni lini atakwenda kule ili kuona changamoto zile na tushirikiane naye ili tuweze kuondoa hizo changamoto?
WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda nijibu swali moja la nyongeza la Mheshimiwa Dkt. Mary Nagu kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, tarehe 2, mwezi ujao, baada ya bajeti yetu kumalizika tutafuatana mimi na Mheshimiwa Mbunge, twende kwenye jimbo lake.