Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Khadija Nassir Ali (37 total)

MHE. KHADIJA NASSIR ALI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru nami kuweza kunipatia nafasi ya kuuliza swali fupi la nyongeza. Je, ni kwa nini Serikali isiwapeleke watoto hawa kwenye makambi ya JKT kwa ajili ya kupatiwa mafunzo ya stadi za kazi?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Bila shaka Mheshimiwa Khadija Binti Nassir alikuwa anamaanisha watoto wa Mitaani. Kama anamaanisha watoto wa Mitaani, hawawezi kupelekwa kwenye makambi ya majeshi ya JKT
kinyume na matakwa yao, kwa sababu watoto wana haki za msingi za kupatiwa ulinzi na Serikali yao.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa maana hiyo, wataendelea na sisi kama Serikali tunapenda waendelee kukaa kwenye familia; na kama kwenye Vituo vya Kulelea Watoto hawapati malezi stahiki, sisi utaratibu tunaoufanya kwenye Serikali ni kujaribu ku-trace familia wanazotoka na kuwapeleka kule ili waweze kuunganishwa na jamii yao.
MHE. KHADIJA NASSIR ALI: Mheshimiwa Naibu Spika nashukuru kwa kuniona, kwa kuwa tatizo la Jimbo la Kalenga linafanana kabisa na tatizo la Mkoa wa Kusini Unguja;
Je, ni lini Serikali itapeleka minara ya simu kwenye vijiji ambavyo bado havijafikiwa na huduma hii kwenye Mkoa wangu?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Khadija Ali anafahamu kwamba tumefungua ofisi Unguja ambayo kazi yake kubwa ni kuhakikisha mawasiliano yanakamilishwa katika vijiji mbalimbali Unguja na Pemba. Naomba nimhakikishie akitembelea hii ofisi atapata uhakika wa eneo hilo analoliongelea ratiba yake ikoje.
MHE. KHADIJA NASSIR ALI: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa majibu ya Serikali, nina maswali mawili ya nyongeza. Ikizingatiwa azma ya kujenga Tanzania ya viwanda, ni lini Serikali itajenga viwanda hivi?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali langu la pili, kwa nini Serikali isiwekeze kwenye kujenga viwanda vidogo vya drip kwenye hospitali za Rufaa za Mikoa nchini ili ku-supply drip kwenye hospitali husika kama ilivyokuwa zamani badala ya kuagiza drip hizo nje ya nchi jambo ambalo ni aibu kwa Taifa letu? Ahsante.
WAZIRI WA VIWANDA NA BIASHARA: Mheshimiwa Naibu Spika, sasa hivi tunajenga viwanda na niwatoe wasiwasi Wabunge wenzangu kuna kampuni mbili za media zimekubali kunisaidia kujibu maswali ya Wabunge kuanzia kesho. Wataonesha vipindi vyote, kiwanda hiki Mwijage naonyesha, hiki kinajengwa hiki kinajengwa. Hata hivyo, kwenye swali langu la msingi nimeorodhesha makampuni ambayo nimehamasisha, nimepiga sound, wakaja kuomba kuwekeza. Kwa hiyo kazi yangu ndiyo hiyo, nimeeleza viwanda vyote hivi wamekuja kuwekeza. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, kwa nini hospitali ndogo zisitengeneze drip. Nimshukuru Mheshimiwa Khadija, hospitali za kwetu nchini ukienda Tabora, Kagondo, Bugando wanatengeneza drip. Nitumie fursa hii kama kuna hospitali yoyote ambayo inataka kwenda kupata ile mitambo ya kutengeneza drip iwasiliane na Wizara ya Afya tuna utaratibu maalum. Viwanda vya kutengeneza drip siyo pesa za ajabu, ndiyo vile viwanda wanavyosema Mwijage anatembea navyo mfukoni, kweli ninavyo.
MHE. KHADIJA NASSIR ALI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa majibu mazuri ya Serikali na nina swali moja la nyongeza. Kwa vile hali ya kiusalama sasa Zanzibar ni shwari na naomba niendelee kuipongeza Serikali kwa hilo, je, Serikali ina mpango gani wa kuzidi kuimarisha hali hiyo?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza tunashukuru Mheshimiwa Khadija Nassir kwa kuona jitihada na mafanikio makubwa ya hali ya kuimarisha usalama sio tu kwa Zanzibar lakini Tanzania nzima na tunaomba Waheshimiwa Wabunge na wananchi kwa ujumla waendelee kutoa ushirikiano wao kwa vyombo vya ulinzi na usalama ili hali hiyo iweze kudumu. Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa upande wetu kama ambavyo nimejibu kwenye swali la msingi tutaendelea kuhakikisha kwamba hali hii inadumu kwa kuhakikisha kwamba tunaimarisha vitendea kazi na uwezo kwa maana ya uwezo wa kiutendaji wa vyombo hivi vya ulinzi tukitarajia kabisa ushirikiano kati ya wananchi na vyombo hivyo utaongezeka ili kuweza kupata taarifa za kiintelejensia kabla ya kuanza kufanya kazi za kuweza kuwakamata wahalifu ambao wamekuwa wakisumbua Taifa letu kwa kiwango fulani katika nchi yetu.
MHE. KHADIJA N. ALI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Kwa kuwa kilimo ndio uti wa mgongo wa Tanzania, ni lini Wizara itaingiza mitaala ya masomo ya kilimo na ufugaji kwenye Sekta ya Elimu?
Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Mwenyekiti, concern hiyo kweli imejitokeza wazi; na nakumbuka kipindi cha nyuma waliokuwa wanasoma sekondari, kulikuwa na somo moja linaitwa Agricultural Science na mambo ya Nutrition, lakini hapa katikati lilipotea.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba kwanza mitihani ya Form Six na ile ya Form ya Four mwaka 2016, somo hilo sasa limeshaanza kuingizwa. Utaratibu wa Serikali ni kuhakikisha kwamba somo hili la Agricultural Science na masomo mengine, kuhakikisha kwamba suala la kilimo linapatikana limeweza kufanyika hivyo. Nashukuru sana Walimu ambao wamejitokeza, nami nilienda kuwatembelea wakati ule wapo Hombolo wakifanya usahihishaji, wamesema vijana wametoa mwitikio mkubwa sana, inaonekana tunaendelea vizuri. Kwa hiyo, hilo tuondoe shaka, Serikali inalifanyia kazi vizuri.
MHE. KHADIJA NASSIR ALI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa majibu ya Serikali nina maswali mawili ya nyongeza.
Kwa kuwa Serikali yetu ya awamu ya tano imedhamiria kuifanya Tanzania kuwa Taifa la viwanda je, Serikali haioni muda muafaka sasa wa kuandaa mitaala ya stadi za kazi na ufundi?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili kwa kuwa mahitaji ya dunia sasa yamebadilika, je, Serikali haioni umuhimu wa kufanya marekebisho makubwa ya sera yetu ya elimu ya juu na elimu ya kati ili wahitimu waweze kushindana kimataifa?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, sera zetu mpaka sasa zimekuwa zikizingatia masuala ya kuwezesha stadi za kazi. Suala linalojitokeza katika ugawaji wa rasilimali na kuboresha ili ziendane na uhalisia hiyo ndio inakuwa ni changamoto. Kwa mfano suala la kujifunza kwa vitendo ni jambo muhimu sana, lakini wakati mwingine unakuta kwamba bajeti inapokuwa finyu ule muda wa vitendo unapunguzwa.
Kwa hiyo, Serikali itaendelea kuongeza jitihada katika maeneo hayo ikiwemo kuboresha vyuo vya ufundi kama vile vyuo vya wananchi ambavyo tumeshavichukua kwenye Wizara yetu pamoja na VETA, lakini pia kufungua vituo mbalimbali vya kujifunzia ukiacha katika mfumo rasmi hata mfumo usio rasmi ili baadaye hata wale wanaokuwa wanajifunza kupitia mifumo isiyo rasmi waweze kupata hizo stadi za kazi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa upande wa elimu ya
juu hivyo hivyo, wanafunzi wamekuwa wakifundishwa, lakini pia tumekuwa tukiangalia nchi mbalimbali zinaenda vipi kupitia workshops ambazo tunabadilishana mawazo, vilevile hata kupitia mitaala yetu. Kwa mfano siku nyuma elimu ya ujasiriamali ilikuwa haipo vyuoni, ilikuwa haifundishwi lakini sasa hivi tunazo degree, masters mpaka Ph.D za ujasiriamali. Kwa hiyo, tumekuwa tukifanya hivi na naamini tutaendelea kuzingatia kadiri tunavyopata mawazo mbalimbali ikiwemo ya kwenu Waheshimiwa Wabunge.
MHE. KHADIJA N. ALI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Serikali imekuwa ikiagiza tani laki nne za mafuta kila mwaka, wakati tuna malighafi za kutosha hapa nchini. Je, Serikali ina mpango gani wa kutumia mazao hayo ipasavyo ili kuweza kuokoa fedha za kigeni zinazopotea kwenye kuagiza mafuta hayo nje ya nchi? (Makofi)
WAZIRI WA VIWANDA, BIASHARA NA UWEKEZAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli tunatumia mafuta tani laki nne kwa mwaka na 70 percent inaagizwa kutoka nje. Tunahamasisha ulimaji wa alizeti; tuna mpango wa kulima migaze au michikichi Kigoma na Pwani; pindi tutakapokuwa tumejitosheleza, tutaweza kuzuia mafuta kutoka nje. Hatuwezi kufanya makosa ya kuzuia mafuta kutoka nje, matokeo yake ni kwamba mafuta yatapanda bei.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Kigoma wakiwa tayari, Pwani wakawa tayari na alizeti zikawa za kutosha, hatutazuia ugavi kutoka nje. Ugavi kutoka ndani utazuia mafuta yasije. Sisi ni member wa WTO na katika mpango wa WTO, bei ni nguvu ya soko inayomzuia mshindani asiingie kwenye soko letu.
MHE. KHADIJA NASSIR ALI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Kwa kuwa ajira hizi zimekuwa zikitajwa kwa ujumla wake, je, ni lini Serikali itatengeneza mchanganuo ili kupata uwakilishi mzuri kwa pande zote mbili za Muungano?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu ni lini, kinachofanyika sasa tupo katika hatua ya pili, hatua ya kwanza tumekamilisha utambuzi wa eneo ambapo bomba litapita. Hatua ya pili, tunakamilisha mazungumzo ili kuainisha maeneo na fursa muhimu kwa nchi zetu mbili lakini pia kwa nafasi za Tanzania Bara na Tanzania Zanzibar kwa masuala ya mafuta. Kwa sababu suala la ajira siyo la Muungano lakini fursa ziko palepale, utaratibu utakamilika baada ya majadiliano ndani ya mwaka huu lakini hatua ya pili itakuwa kuainisha fursa. Kwa hiyo, tutakapofikia hatua hiyo Mheshimiwa Mbunge tutawasiliana ili tuone namna ya kukamilisha na kuzinufaisha pande zote za Muungano.
MHE. KHADIJA NASSIR ALI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Serikali imekuwa ikitoa huduma bure kwa wagonjwa wa kisukari, kifua kikuu pamoja na UKIMWI, je, Serikali haioni sasa ni muda muafaka wa kuanza kutoa huduma bure kwa wagonjwa wa saratani ili kuwapunguzia wananchi gharama hiyo?
NAIBU WAZIRI WA WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA NA WATOTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, huduma za saratani kwa mujibu wa Sera ya Afya ya mwaka 2007 nchini Tanzania ni bure katika ngazi zote na kwa maana hiyo kila mgonjwa wa saratani atapata huduma zote anazohitaji bure (free of charge) wala hakuna gharama yoyote ile, kwa hiyo sio kwamba tutaanza lini tayari sera inasema hivyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ila kama mgonjwa haijajulikana kwamba ana saratani wakati anafanyiwa uchunguzi, haijathibitika kwamba ana saratani anaweza akachajiwa vipimo na vitu vingine lakini kuanzia pale atakapogundulika kwamba ana saratani atapata huduma zote bure.
MHE. KHADIJA NASSIR ALI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kuniona.
Mheshimiwa Naibu Spika, kumekuwa na malalamiko mengi kwenye Halmashauri zetu juu ya uhaba au ukosefu wa dawa lakini taarifa za Naibu Waziri hapa anasema kwamba dawa zipo. Sasa nilikuwa naomba tu Mheshimiwa Naibu Waziri atupe maelezo juu ya hili kwa kina zaidi. Ahsante.
WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Naibu Spika, nimeona nisimame kwa sababu Naibu Waziri ametoa majibu mazuri sana lakini bado mdogo wangu Mheshimiwa Khadija Nassir anauliza swali kuhusu upatikanaji wa dawa. Kwa hiyo, nataka kidogo nitoe uelewa, tunapima vipi upatikanaji wa dawa.
Mheshimiwa Naibu Spika, tunapima upatikanaji wa dawa, dawa ziko zaidi ya elfu mbili, elfu tatu, elfu nne, lakini katika ngazi ya MSD tumechagua dawa 135 muhimu zaidi kwa mujibu wa Mwongozo wa WHO kwamba hizo ndiyo dawa muhimu zaidi ambazo zinatakiwa kuwepo muda wote katika ngazi ya MSD katika nchi. Kwa hiyo, kama alivyosema Naibu Waziri, MSD kati ya hizo aina 135 za dawa, tuna zaidi ya asilimia 82. Kwa hiyo, Mkurugenzi wa Halmashauri au DMO anapoomba aina 100 za dawa atapata angalau aina 82 za dawa mara moja.
Mheshimiwa Naibu Spika, sehemu ya pili ya kupima upatikanaji wa dawa, katika zile dawa 135 tumechagua aina 30 za dawa ambazo tunaita life serving medicines, za malaria, maambukizi ya bakteria, HIV, dawa za akina mama wajawazito na kila kitu. Kwa hiyo, ndiyo maana Naibu Waziri sasa hivi na mimi ambavyo tunaenda kwenye vituo tunamuuliza Mganga Mkuu wa Wilaya katika zile tracer medicine 30 leo mgonjwa akiumwa ziko aina ngapi?
Mheshimiwa Naibu Spika, ninayo taarifa ya TAMISEMI, anachosema Naibu Waziri ni sahihi. Mikoa hii imeonesha kwamba sasa hivi hali ya upatikanaji wa dawa katika mikoa na katika vituo ni zaidi ya asilimia 80 mpaka 90. Kwa hiyo, huo ndiyo ufafanuzi na ndiyo ukweli…

WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Naibu Spika, lakini nataka kutoa changamoto moja, dawa hazipatikani bure, wananchi wanatakiwa kuchangia kupata dawa. Kwa hiyo, lazima pia tuwahimize watu wakate bima za afya.
Mheshimiwa Naibu Spika, tuko vizuri na nataka kurudia, hata NGOs kama SIKIKA ambazo zilikuwa zinatuandikia taarifa mbaya kuhusu hali ya upatikanaji wa dawa wametoa taarifa na kuthibitisha dawa ni zaidi ya asilimia 80. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pia Jarida la Kimataifa la Famasia limethibitisha hali ya upatikanaji wa dawa muhimu Tanzania ni zaidi ya asilimia 80. Kwa hiyo, tunamshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa kuwekeza kwenye upatikanaji wa dawa nchini Tanzania. Ahsante sana. (Makofi)
MHE. KHADIJA NASSIR ALI: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa majibu ya Serikali, nina maswali mawili ya nyongeza.
Kwanza, ni lini Serikali itatoa ruzuku ya moja kwa moja kwa kinamama wanaojifungua ili kuondoa kadhia hii?
Mheshimiwa Spika, swali la pili, Ilani ya Chama cha Mapinduzi ilielekeza kujenga vituo vya upasuaji kila kata. Je, ni lini Serikali itatekeleza agizo hili kibajeti? Nashukuru. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Spika, kwanza nampongeza Mheshimiwa Khadija Nassir Ali kwa kuuliza swali la kisera ambalo limetupa fursa ya kufafanua mambo mbalimbali ambayo ni kipaumbele kwa Wizara yetu kwa sababu yanahusu kupunguza vifo vya wakinamama wajawazito na watoto na yeye kama Mbunge mwanamama nadhani anaguswa na mtazamo wetu kwamba hiki ni katika vipaumbele vyetu pale Wizarani.
Mheshimiwa Spika, ruzuku kutoka Serikali kuu kwenda Serikali za Mitaa kwamba ni lini itatoka? Nadhani hakufanya mazingatio ya kutosha kwenye majibu yangu ya msingi kwa sababu tayari hapa hapa tu nimezungumza tuna zaidi ya bilioni 66 ambazo tunazipeleka kwenye Halmashauri mbalimbali nchini kwa ajili ya kufanya maboresho kwenye vituo vya kutolea huduma za afya nchini. Na hiyo ni ruzuku kutoka Serikali kuu.
Mheshimiwa Spika, vilevile kwenye bajeti ya afya Fungu Namba 52 tumeweka bajeti ya dawa mbalimbali ambazo zinaenda kusaidia kupunguza vifo vinavyotokana na sababu mbalimbali za uzazi. Kwa mfano, tumeweka bajeti ya Uterotonic drugs kama Oxycontisin ambapo tunapeleka kwenye Halmashauri moja kwa moja, kwenye vituo vya kutolea huduma za afya.
Mheshimiwa Spika, pia tumeweka bajeti mahususi ya kutoa dawa za magnesium sulphate ambazo zinasaidia kutibu ugonjwa wa eclampsia (kifafa cha mimba) ambazo hizi ni katika sababu kubwa ambazo zinapeleka kupoteza maisha wakati wa uzazi.
Mheshimiwa Spika, pia Serikali Kuu inasaidia sana kwenye kuimarisha mfumo wa upatikanaji wa damu salama kwenye vituo vyote vya afya nchini na hii ni moja kwa moja tunatoa sisi tunapeleka msaada kule chini. Kwa hiyo, ruzuku tunatoa na tunatoa kwa kiasi kikubwa sana. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, naomba nisisitize hapa kwamba Wabunge wenzangu wote na Halmashauri zote nchini watambue jukumu la kupunguza vifo vinavyotokana na uzazi ni la kwao wenyewe kwenye Halmashauri husika. Ni lazima tufanye uwekezaji kwenye vituo vya kutolea huduma za afya, hakuna namna nyingine. Sisi Serikali kuu tunasaidia tu kujenga uwezo wa vituo vyetu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, la pili, Ilani ya CCM haizungumzii kujenga vituo vya upasuaji kwenye kila kata, Ilani ya CCM inazungumzia ujenzi wa vituo vya afya (health centers) kwenye kila kata na zahanati kwenye kila kijiji. Ilani ya uchaguzi inakwenda sambamba na Mpango wa Maendeleo wa Afya ya Msingi wa mwaka 2007/2017 ambapo Halmashauri zote nchini zinapaswa kujenga vituo vya afya kila Kata na zahanati kwenye kila kijiji.
Mheshimiwa Spika, kwa msingi huo, jitihada bado zinaendelea kwenye Halmashauri mbalimbali nchini na sisi kama nilivyosema kwenye majibu yangu ya awali, tunaendelea kujengea uwezo lakini pia ku-support halmshauri zetu kutimiza azima hii iliyowekwa kwenye Ilani ya uchaguzi ya CCM. (Makofi)
MHE. KHADIJA NASSIR ALI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Kwa kuwa TIC ndiyo lango kuu la uwekezaji nchini, je, TIC inaisaidiaje EPZ kwenye kutekeleza majukumu yake vizuri? Ahsante.
WAZIRI WA VIWANDA, BIASHARA NA UWEKEZAJI:
Mheshimiwa Mwenyekiti, taasisi zote hizi mbili ziko chini yangu, kwa Kiswahili cha kawaida TIC ni receptionist, EPZ ndiyo anaandaa kama ni ubwabwa kwenye meza. Kwa hiyo wote wanashirikiana, ni mkono na mdomo. TIC ni receptionist, ni mpiga sound anakaribisha watu, EPZA anaweza kuwatendea inavyobidi. (Kicheko/Makofi)
MHE. KHADIJA NASSIR ALI:Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Kumekuwa na malalamiko mengi juu ya mlolongo mrefu ambao hauna ulazima kwenye mchakato mzima wa uwekezaji ambao huwakatisha tamaa wawekezaji wengi nchini. Je, Serikali ina mpango gani wa kupunguza kero hii kwa wawekezaji wetu? Ahsante. (Makofi)
WAZIRI WA VIWANDA, BIASHARA NA UWEKEZAJI:
Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Mbunge anasema yalikuwepo malalamiko; yalikuwepo malalamiko wakati ule sasa hayapo. Yeyote anayetaka kuwekeza anione mimi, kama upo mkoani muone Mkuu wa Mkoa, kama uko Dar es Salaam nenda Ofisi yangu ya Dar es Salaam. Mkuu wa Mkoa amepewa mamlaka ya kukaribisha wawekezaji na Mheshimiwa Rais amesema mwekezaji atakayekwamishwa mkuu wa mamlaka awe Wilaya au Mkoa ajione hayupo salama. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kama ulivyosema Mheshimiwa Mbunge yalikuwepo, sasa yamekwisha. (Makofi)
MHE. KHADIJA NASSIR ALI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kuniona. Ripoti ya CAG inaonesha kwamba mdaiwa mkubwa wa viwanda vyetu vya ndani ni Serikali hususan halmashauri zetu. Je, Serikali ina mkakati gani madhubuti ya kuanza kulipa madeni hayo ili kunusuru anguko la viwanda vyetu ambavyo tunavianzisha kwa nia njema? Ahsante. (Makofi)
WAZIRI WA VIWANDA, BIASHARA NA UWEKEZAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ndiyo, Serikali inadaiwa na Serikali sasa tunaongeza jitihada za kuhakikisha kwamba kila stahili ya Serikali inakusanywa na kile kitakachokusanywa ndicho kitawalipa wale. Hatujawalipa wale kwa sababu na sisi hatujalipwa kuna watu hawapendi kulipa kodi, hata ukisoma easy of doing business Tanzania tunafanya vibaya kwa sababu watu hawataki kulipa kodi, lakini katika nchi nyingine huwezi kupewa haki nyingine hata kwenda kuchumbia kama huwezi kuonesha tax clearance.
MHE. KHADIJA NASSIR ALI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Benki hii imekuwa ikikiuka taratibu za kibenki kwa muda mrefu sana jambo ambalo limepelekea BOT kuwapa karipio kali. Je, Serikali imejiridhisha vipi kwamba ubadilishwaji wa Menejimenti ndiyo dawa au suluhisho pekee la uendeleaji mzuri wa benki hii? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Kama alivyosema katika maelezo yake ya awali Mheshimiwa Waziri, ni kwamba baada ya kufanya mapitio ndani ya Benki yetu tukaona kwamba kulikuwa kuna upungufu, hatua ambazo tulizichukua moja ni kufanya mabadiliko ya Menejimenti na kuanzia mwezi Mei, tumeweka Mkurugenzi mpya, tumepitia mfumo wa utendaji na uongozi katika benki ile na kuajiri watumishi wapya ambao ni waadilifu, sasa hivi hatua ambazo zimechukuliwa kwa haraka na imetusaidia kuhakikisha kwamba hata ule mtaji wetu umezidi kukua na hasara kupungua.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naamini kabisa ndani ya muda mfupi, ndani ya mwaka huu tutakuwa tumepiga hatua nzuri na benki itarudi kwenye mstari. (Makofi)
MHE. KHADIJA NASSIR ALI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Pamoja na majibu ya Serikali, nina maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa kila Wilaya nchi nzima vijana wametenga maeneo kwa ajili ya shughuli za kiuchumi. Je, Serikali lini itaona umuhimu wa kutumia maeneo haya kwa ajili ya uzalishaji wa malighafi hizo?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu la pili, tumekuwa tukiona Serikali ikihamasisha wakulima wetu kulima mazao mbalimbali ya kibiashara bila ya kuwa na mikakati mizuri ya masoko na matumizi. Je, ni nini kauli ya Serikali juu ya hili? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA VIWANDA, BIASHARA NA UWEKEZAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Ni kweli Serikali imesisitiza na imeendelea kutenga maeneo kwa ajili ya vijana pamoja na wajasiriamali wengine. Serikali katika kusaidia hilo, kwa mfano katika bajeti ya mwaka 2017/2018 tayari kupitia SIDO imetenga shilingi bilioni saba kwa ajili ya kujenga sheds yaani sehemu za kufanyia kazi ikiwa ni pamoja na kuweka viwanda. Maeneo hayo yapo katika Mikoa ya Kagera, Geita, Simiyu, Mtwara, Manyara na Katavi, hiyo ni kwa kuanzia. Kwa hiyo, niseme tu kwamba itakapotokea sheds hizo zimekamilika, tutawahamasisha vijana pia kutumia fursa hiyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa upande wa masoko, tumekuwa tukiendelea kuhakikisha kwamba tunalinda wazalishaji wa mafuta walioko nchini lakini vilevile kwa kushirikiana na nchi zinazotuzunguka kuona kwamba mazingira ya biashara ya mafuta ya kula ushindani wake ni ule ambao hauiathiri nchi yetu. Kwa misingi hiyo, kwa kuangalia mafuta ya kula ambayo yanaagizwa kutoka nje na uhalisia wa kodi ambazo zinatolewa tayari kuna timu inafanya utafiti ili kuhakikisha kwamba masoko yanakuwa ya uhakika na watu wanazalisha kwa faida.
MHE. KHADIJA NASSIR ALI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kuniona. Kumekuwa na utaratibu wa kutengeneza mifumo yetu nyeti nje ya nchi jambo ambalo linaweza kuhatarisha usiri na usalama wa taarifa zetu.
Je, ni lini Serikali itaona umuhimu wa kutumia wataalam wetu wa ndani ili kuepuka matatizo ambayo yanaweza kujitokeza? Ahsante.
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imeunda Wakala wa Serikali Mtandao. Serikali Mtandao iko pale kwa kusimamia mifumo yote inaayoanzishwa ndani ya Serikali na kwamba mifumo yote iliyopo sasa imeanzishwa kwa kuhusishwa Serikali Mtandao. Naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba Kamati ya Bunge inayohusika na masuala ya Utawala na Serikali za Mitaa imependekeza na mimi nawaunga mkono kwamba Wakala wa Serikali Mtandao ibadilishwe iwe mamlaka ili iweze kusimamia mitandao yote na mifumo yote inayoanzishwa ndani ya Serikali.
MHE. KHADIJA NASSIR ALI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Tumekuwa tukiona wawekezaji wetu wa ndani wakijitahidi kuzalisha bidhaa mbalimbali zenye ubora wa hali ya juu.
Je, Serikali ina mkakati gani wa kibiashara wa kuzipa kipaumbele bidhaa zetu zinazozalishwa nchini ili kuweza kuendana na ushindani wa soko hili ambalo lipo huru na lenye ushindani mkubwa ili sasa kuweza kufanana na nchi nyingine zinavyofanya? Ahsante nashukuru. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA VIWANDA, BIASHARA NA UWEKEZAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Kimsingi kupitia itifaki mbalimbali ambazo tunakuwa tumezisaini tunajitahidi kuwa na ushindani wa haki. Hata hivyo kwa bidhaa ambazo zinazalishwa ndani zinapewa kipaumbele na tunahamasisha wadau kupenda kununua zaidi bidhaa zetu za ndani kuliko hata hizo za nje. Vilevile wakati mwingine pia kuna tozo ambayo inatolewa katika baadhi ya bidhaa zinazotoka nje ili kufanya bidhaa za ndani ziweze kuwa na nafasi nzuri zaidi katika ushindani. (Makofi)
MHE. KHADIJA NASSIR ALI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipatia nafasi ya kuuliza swali dogo la nyongeza. Je, Serikali ina mikakati gani ya kupunguza maambukizi mapya ya virusi vya UKIMWI katika Jamii? Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru.
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Swali lake ni refu kidogo; tuna mikakati gani ya kupunguza maambukizi mapya? Mikakati tuliyonayo ni mingi sana. Mkakati mkubwa wa kwanza ni kinga, kuzuia watu wasipate maambukizi ya UKIMWI kwa kutoa Elimu ya Afya kwa Umma.
Mkakati wa pili, ni tiba ambapo tunatumia zaidi ya kliniki zaidi ya 2000 za CTC (Care and Treatment Clinics) ambazo zimetapakaa nchi nzima mpaka kwenye ngazi za Vituo vya Afya kwa ajili ya kutoa dawa za ART (antiretroviral therapy) dawa za kupunguza makali ya virusi vya UKIMWI, tukiamini kwamba watu ambao wanatumia dawa, wanapungua virulence, wanapungua kiwango ambacho wanaweza wakaambukiza. Kwa hiyo, hata ikitokea bahati mbaya akafanya ngono ambayo siyo protected anaweza asimwambukize partner wake.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hivyo, tuna mkakati wa kuongeza sasa idadi ya watu ambao tunawatibu, kwamba kila atakayepimwa na kubainika na Virusi vya UKIMWI kuanzia Oktoba, 2016 atatibiwa hapo hapo, ataanza kupata dawa za kupunguza makali ya Virusi vya UKIMWI.
Mheshimiwa Mwenyekiti, huu ni mkakati mpya wa kisasa ambapo tumehama sana kwenye mikakati ambayo ipo preventive based tunahamia kwenye treatment based, kwamba badala ya kutoa tu kinga sasa tunatoa tiba zaidi. Kwa kufanya hivi, taratibu tutapunguza maambukizi mapya kwa kiasi kikubwa.
MHE. KHADIJA NASSIR ALI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Pamoja na majibu mazuri ya Serikali nina maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa takwimu hizo zinatokana na sensa ya mwaka 2012 na Tanzania sasa inakadiriwa kuwa na watu wasiopungua milioni 50, hii inaonesha wazi kwamba Serikali haina takwimu sahihi kwa sasa.
Swali langu la kwanza, Serikali haioni kwamba kukosekana kwa takwimu sahihi kunapelekea kushindwa kuwapatia mahitaji yao ipasavyo?
Swali langu namba mbili, je, ni lini Serikali itaona umuhimu wa kufanya takwimu ili kuweza kupata idadi kamili ya watu wenye ulemavu? Ahsante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, SERA, BUNGE, KAZI, AJIRA, VIJANA NA WENYE ULEMAVU (MHE. STELLA I. ALEX): Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nimpongeze sana mdogo wangu kwa ajinsi ambavyo anafuatilia masuala ya watu wenye ulemavu, lakini pia na yeye ni mdogo wetu yaani mdogo wa watu wote wenye ulemavu kwa sababu dada yake ni kiziwi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inatambua umuhimu wa takwimu kwa watu wenye ulemavu, na sambamba na hilo kama tunavyofahamu, sensa inafanyika kila bada ya miaka 10 ambapo kutokana na kwamba ilifanyika mwaka 2012 kwa hiyo tunategemea sensa nyingine ifanyike mwaka 2022; lakini kwa sababu ya umuhimu wa jambo hili yaani takwimu kwa watu wenye ulemavu tayari Serikali imeshaanza kufanya mazungumzo na kuangalia ni jinsi sasa tunaweza kupata takwimu hizi kabla ya wakati huo. Kwa hiyo nimhakikishie Mheshimiwa Khadija Nassir Ali kwamba hili suala Serikali imeliangalia kwa umuhimu wake kabisa kwa sababu ni makusudi na nia ya Serikali kuona kwamba inapanga bajeti zake kulingana na uhalisia wa mahitaji ya watu wenye ulemavu.
MHE. KHADIJA NASSIR ALI: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa majibu ya Serikali. Nina maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Spika, diaspora kwa umoja wao wamekuwa wakipigania kurudi nyumbani kufanya kazi. Tangu Awamu ya Tano ianze ni diaspora wangapi wameajiriwa katika sekta ya umma ili kutumia ujuzi wao katika kuisaidia Serikali?
Swali langu namba mbili, ni jinsi gani Serikali inawapa fursa diaspora katika uchumi wa viwanda? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA (K.N.Y WAZIRI WA MAMBO YA NJE NA USHIRIKIANO WA AFRIKA MASHARIKI): Mheshimiwa Spika, kama nilivyosikia swali ni kama moja hasa kwamba ni namna gani Serikali imejipanga kutoa fursa kwa ajili ya diaspora wetu.
Mheshimiwa Spika, Serikali imekuwa ikifanya makongamano ya mara kwa mara na diaspora ili kuweza kuwaonesha fursa zilizopo waweze kuwekeza nchini kwa sababu tunatambua potential kubwa iliyopo kwa diaspora kama ilivyo katika nchi nyingine.
Mheshimiwa Spika, vilevile kwa kutambua umuhimu na potential ya diaspora wetu Serikali sasa iko mbioni kuja na sera mahsusi ya diaspora ili kuweza kuweka mazingira mazuri ya namna ambayo wanaweza kushiriki katika kuchangia maendeleo ya nchi yetu.
Kwa hiyo, nimhakikishie tu Mheshimiwa Mbunge kwamba, tayari kuna mipango inaendelea na diaspora tayari wameshaanza kuwekeza katika maeneo mbalimbali. (Makofi)
MHE. KHADIJA NASSIR ALI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kuniona. Ripoti mbalimbali ikiwemo Ripoti ya MVS na REPOA inaoneesha kwamba hali ya njaa na umasikini nchini imeongezeka kwa mwaka 2018 ukilinganisha na miaka iliyopita. Je, Serikali ina kauli gani juu ya hili? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, napata taabu sana kusema kwamba hali ya njaa imeongezeka ndani ya mwaka 2018. Katika bidhaa zinazochangia mfumuko wa bei au inflation rate kuongezeka ni upatikanaji wa chakula. Inflation kwa mwezi wa Tatu ilikuwa asilimia 3.9. Hii ni indicator kwamba hali ya njaa kwa Tanzania haipo na mvua zimenyesha za kutosha, wananchi wetu wako katika amani kabisa ya upatikanaji wa chakula ndani ya Taifa letu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, namwomba tu Mheshimiwa Mbunge, yawezekana taarifa anazozisoma ni za mwaka 2016/2017 kulikokuwa na shida hiyo, siyo kwa mwaka 2018.
MHE. KHADIJA NASSIR ALI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru, lakini pia nimpongeze Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu mazuri. Nina swali moja la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ieleweke kuwa Zanzibar hatupati gawio la Yeared Budget Support. Tunapata gawio la Annual Year Budget Support ambayo ni 4.5% na imekuwa ikishuka kila leo, nafahamu pia kuna vikao vingi vya harmonization vinavyoendelea. Sasa nilikuwa napenda tu Serikali ituambie wamefikia wapi juu ya kuweka mambo haya yote sawa? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, kama swali lilivyojielekeza, liliuliza kuhusu Basket Fund ambao ndipo jibu langu la msingi lilipoeleza kulingana na sheria. Basket Fund ni kwa ajili ya Tanzania Bara kwa sababu na Zanzibar nao wanapata Basket Fund.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa ajili ya General Budget Support, kama alivyouliza Mheshimiwa Khadija Nassir, napenda kulieleza Bunge lako tukufu kwamba kwa mwaka 2016/2017 General Budget Support iliyopelekwa Zanzibar ilikuwa ni shilingi 5,656,500,000 lakini pia kwa mwaka huu hadi Machi tayari Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imeshapeleka shilingi 3,153,111,187.
Mheshimiwa Mwenyekiti, changamoto alizozisema Mheshimiwa Mbunge tunaendelea kuzishughulikia kwa pamoja tukifahamu umuhimu wa mapato kwa maendeleo ya Taifa letu.
MHE. KHADIJA NASSIR ALI: Mheshimiwa Spika, ahsante, naomba nielezee masikitiko yangu juu ya majibu ya Serikali ambayo amenipatia.
Mheshimiwa Spika, majibu ambayo Serikali imeleta yako kisera zaidi, nilitegemea yaje majibu ambayo kidogo yangeleta taswira na mwanga kwa vijana.
Mheshimiwa Spika, nashindwa kuelezea malalamiko yangu kwa vile tuko kwenye Mwezi Mtukufu wa Ramadhani lakini kwa kweli nimesikitishwa sana na majibu. Baada ya kusema hayo nina maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Spika, kwa vile Serikali imepanua fursa ya elimu kwa kuongeza Vyuo Vikuu vya Elimu ya Juu na Elimu ya Kati. Je, Serikali ina mkakati gani wa kuendana basi na mahitaji yaliyopo?
Mheshimiwa Spika, swali langu la pili, kwa kiasi gani Mfuko wa Vijana umeweza kuwagusa walengwa ukizingatia na hali halisi iliyopo? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, VIJANA NA AJIRA (MHE. ANTONY P. MAVUNDE): Mheshimiwa Spika, Serikali imekuwa na mipango mbalimbali ya kuwawezesha vijana na akina mama na msingi mkubwa wa uwezeshaji huo unatokana na sera. Kwa hiyo, nimuondoe tu hofu Mheshimiwa Mbunge ya kwamba majibu haya kwa sababu ya uwezeshaji na sera inatuelekeza hivyo ndiyo maana yalijikita hapo.
Mheshimiwa Spika, nikienda katika swali lake la kwanza la kujua kuhusu ongezeko la idadi ya wahitimu wa Vyuo vya Elimu ya Juu na Ufundi ikilinganishwa na nafasi za ajira. Kama Serikali na kwa mujibu wa taarifa ya mwaka 2014 ya Integrated Labour Force Survey ambayo imeeleza kinaga ubaga juu ya nafasi za ajira zinazotengenezwa kila mwaka lakini na watu wenye uwezo wa kufanya kazi kwa mwaka husika kwamba idadi imekuwa ni kubwa tofauti na nafasi za ajira ambazo zinatengenezwa.
Kwa hiyo, sisi kama Serikali tuliona njia nyingine mbadala ni kuanza sasa kuwabadili mitazamo vijana wetu hasa wahitimu wa vyuo vikuu na kuamini kwamba bado wanaweza wakafanya shughuli zingine za kiuchumi ikiwemo kilimo, ufugaji na biashara na sisi kupitia Mfuko wa Uwezeshaji wa Wananchi Kiuchumi na Mfuko wa Maendeleo ya Vijana kuweza kuwawezesha ili kuweza kufikia malengo yao.
Mheshimiwa Spika, sisi kwetu tafsiri kwa mujibu wa Sera ya Ajira ya mwaka 2008, ajira ni shughuli yoyote halali inayomuingizia mtu kipato. Kwa hiyo, tumeanza sasa kuwabadili mitazamo vijana wetu waanze kuamini kwamba si wote ambao wanaweza kwenda kukaa ofisini, lakini pia tunaandaa mazingira mazuri waweze kufanya kazi za kujiajiri.
Mheshimiwa Spika, la pili ameuliza kuhusu Mfuko wa Maendeleo ya Vijana; ni kweli, kwa mujibu wa Sheria ya Fedha, Sheria Na. 21 ya mwaka 1961, kifungu namba 21(1) kilianzisha Mfuko wa Maendeleo wa Vijana ambao lengo lake ni kuhakikisha tunawagusa vijana wengi zaidi kwa kuwasaidia kupata mikopo na mitaji na mikopo yenye riba nafuu.
Mheshimiwa Spika, mpaka ninavyozungumza hivi sasa, tayari tumeshafikia vikundi vya vijana 397 ambao tumeshatoa kiasi cha shilingi zaidi ya shilingi bilioni nne kwa ajili ya kuwawezesha vijana. (Makofi)
MHE. KHADIJA NASSIR ALI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya Serikali kuchukua hatua kali za kuzuia ukeketaji jamii zinazojishughulisha na ukeketaji zimekuja na njia mpya za kuwakeketa watoto wakiwa bado wachanga. Je, Serikali inalifahamu hili na kama inalifahamu ni hatua gani zimechachukuliwa mpaka sasa? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, mwezi wa sita nilipokuwa mgeni rasmi katika Maadhimisho ya Siku ya Mtoto wa Afrika pale Arusha liliibuliwa suala la ukeketaji wa watoto wachanga. Baada ya Serikali kubana na kutoa elimu ya kutosha na kwa watoto kujitambua mara nyingi watoto hawa ambao wana umri mkubwa wamekuwa wanatoa taarifa na sisi tumekuwa tunachukua hatua. Sasa kuna baadhi ya wazazi ambao wameendelea na sasa hivi wamehama kutoka kukeketa mabinti ambao umri umekuwa wamehamia katika kukeketa watoto wachanga.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi kama Serikali tunalitambua hilo na tumeshatoa maelekezo katika wizara yangu ya afya, maendeleo ya jamii, jinsia, wazee na watoto idara kuu ya maendeleo ya jamii kushirikiana na idara kuu ya afya kuweka utaratibu mahususi ambao tutaanza kubaini watoto wote ambao wanakeketwa wakiwa na umri mdogo hususani pale watoto wanapokuwa wanaenda kliniki. (Makofi)
MHE. KHADIJA NASSIR ALI: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kuniona. Kutokana na mazingira halisi ya watoto hawa chances za kupata maambukizi ya UKIMWI ni kubwa sana. Serikali sasa haioni umuhimu wa kuangalia afya za watoto hao kabla ya kuwapatia settlement ili kuepusha maambukizi mapya katika jamii? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Spika, tunatambua kwamba watoto ambao wanaishi katika mazingira hatarishi wako katika risk kubwa zaidi ya kupata ya kupata maambukizi ya magojwa mbalimbali za zinaa ikiwa ni pamoja na ugonjwa wa UKIMWI. Sisi kama Serikali mkakati wa kwanza ni kuhakikisha kwamba watoto hawa wanapata malezi mazuri ya familia zao na pale inaposhindikana jamii inahusika kabla ya sisi kama Serikali kuja kuchukua majukumu ya malezi haya.
Mheshimiwa Spika, vilevile mimi niendelee kuwaomba, kwa sababu watoto hawa wengi wako kule mitaani na wako katika jamii zetu, tuombe tu kwamba sisi kama jamii tushirikiane na Serikali katika kuhakikisha watoto hawa wanapata malezi stahiki. Kama Serikali tuna mpango mkakati mbalimbali ya kuzuia maambukizi ya UKIMWI.
Kwa mujibu wa takwimu za hali ya viashiria hali ya UKIMWI ya mwaka 2017 imeonesha kwamba vijana nao wamekuwa katika risk kubwa sana ya kupata maambukizi ya UKIMWI. Hilo tumelitambua tumeweka mipango mikakati mbalimbali ya kuwafikia na kufanya upimaji, lakini vile vile tumeweka mkakati wa kuhakikisha kwamba sasa hata ile dawa kinga ya pre exposure for prophylaxis tunaweza kuwapatia kwa baadhi ya makundi ikiwa ni pamoja na vijana.
MHE. KHADIJA NASSIR ALI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kuniona.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sera ya uchumi ya nchi yoyote inatakiwa kuwa na mahusiano ya moja kwa moja na sekta wezeshi kama sekta ya elimu ili kuweza kuleta matokeo chanya. Sasa Serikali haioni sasa kuna umuhimu wa kubadilisha mitaala yetu ya elimu ili kuweza kuendana na sera ya uchumi wa viwanda?
NAIBU WAZIRI WA VIWANDA, BIASHARA NA UWEKEZAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nimpongeze Mheshimiwa Khadija kwa kufungamanisha sera hii ya uchumi na namna ya kuwezeshwa kupitia elimu; na ndiyo maana hata kwenye majibu ya msingi tunazungumza hayo. Ni kwamba tunapozungumzia kufanya uwezeshi katika ujenzi wa uchumi ni lazima huyu mtu awe ameandaliwa kielimu lakini vile vile kimafunzo ya ujuzi.
Kwa misingi hiyo sera zetu zote sasa hivi zimekuwa zikifanya kazi kwa pamoja kuangalia maeneo gani yanaweza yakaongezewa nguvu na pia kuangalia kwamba sera zetu zinazungumza na kuweza kuleta matokeo chanya. Kwa hiyo, kupitia Wizara ya elimu vilevile kuna mafunzo ambayo yamekuwa yakitolewa katika vyuo vyetu vikuu, lakini vilevile katika vyuo vya ufundi ili kuwezesha kuona kwamba hawa wahitimu wanatekeleza majukumu yao vizuri katika ujenzi wa uchumi.
MHE. KHADIJA NASSIR ALI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kuniona. Vijana wote nchini wameamka na kuungana na Serikali yao katika kutekeleza kwa vitendo Sera ya Uchumi wa Viwanda, japokuwa katika majibu ya Serikali, Serikali imeshindwa ku-acknowledge jitihada za vijana katika kukuza uchumi wa nchi. Sasa Serikali ni lini itatambua na kuthamini jitihada za vijana katika kukuza uchumi wa nchi? Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA VIWANDA, BIASHARA NA UWEKEZAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza, naomba tu tufahamu kwamba, suala la kuwezesha vijana kiuchumi ni suala mtambuka. Sekta zote inabidi tushirikiane kwa pamoja ikiwemo Waheshimiwa Wabunge. Wizara kama ambavyo nimesema awali tumeshajipanga kuhakikisha kwamba tunakuwa na mkakati maalum wa kuwezesha makundi hayo ya kibiashara kuanzia katika maeneo yao ya kufanyia biashara na tunazidi kuhamasisha Halmashauri zetu, kwa mfano zitenge maeneo ambayo vijana wanaweza kufanyia kazi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, si jambo jema kuwaona vijana wakiwa wanazunguka zunguka tu mitaani, halafu yanajengwa majengo makubwa yanaachwa vijana hawaingii humo kufanyia kazi. Kwa misingi hiyo, tumejipanga na tunataka kuona kwamba vijana wanasaidiwa ili iwe ni rahisi kuwatambua na vilevile kuweza kupata huduma zote za msingi zinazohusiana na uwezeshaji. (Makofi)

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU, SERA, BUNGE, KAZI, AJIRA, VIJANA NA WENYE ULEMAVU: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, naomba kwanza nimpongeze Mheshimiwa Naibu Waziri na Wizara ya Viwanda na Biashara kwa kazi nzuri wanayoifanya katika kuwatambua vijana na kuwasaidia ili waweze kuingia kwenye sekta ya viwanda.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kulithibitishia Bunge lako Tukufu kwamba, Serikali imekuwa ikiwasaidia sana vijana na kuwawezesha katika sekta mbalimbali. Wizara ya Habari ya Michezo na Utamaduni wameshafanya kazi kubwa sana katika kutambua vipaji vya vijana na kuwajengea uwezo. Ofisi ya Waziri Mkuu tumeshasema tumetambua vijana waliokwishafanya vizuri kwa mfano, wale vijana wa kutoka Chuo cha SUA, wamefanya vizuri sana kwenye sekta ya kilimo, sasa tunawatumia hao kuendesha mafunzo ya kilimo cha kitalu nyumba katika nchi nzima ya Tanzania, huko ni kutambua juhudi zao na kuwawezesha zaidi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia tunaendelea kutoa mafunzo yenye ujuzi wa namna mbalimbali ili vijana wajiajiri na waajiriwe katika maeneo mbalimbali ya sekta za viwanda na sekta za biashara. Serikali inatambua sana na tutaendelea kutambua juhudi hizo kila siku na kuwawezesha vijana wa Tanzania. (Makofi)

MHE. KHADIJA NASSIR ALI: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa kuniona. Ni lini Serikali italeta marekebisho ya Sheria Bungeni ili umeme unaonunuliwa Tanzania Bara kwenda Zanzibar uweze kupatiwa msamaha wa kodi kama ilivyo bidhaa nyingine zinazozalishwa Tanzania Bara kwenda Zanzibar? Mheshimiwa Spika, ahsante.
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Spika, wakati tunapitisha Bajeti ya Wizara ya Nishati, Waziri wa Nishati alisema vizuri kabisa kuhusu jambo hili, kwamba nalo ni katika mambo ambayo yapo katika mijadala kuhakikisha kwamba kodi inayotozwa kwa umeme unaouzwa Zanzibar inafanyiwa kazi. Nimwombe Mheshimiwa Khadija Nassir pamoja na Wazanzibari wote na Watanzania wote jambo hili litafanyiwa kazi kwa muda muafaka kabisa.

MHE. KHADIJA N. ALI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Nashukuru pia kwa majibu mazuri ya Serikali, lakini nina maswali mawili ya nyongeza. Swali la kwanza, hotuba ya Wizara ya Viwanda na Biashara ya bajeti ya mwaka wa fedha wa 2018/2019 ilieleza kwamba tangu Serikali ya Awamu ya Tano iingie madarakani imeshajenga viwanda 3,036. Je, ni vijana wangapi wameweza kuajiriwa katika viwanda hivyo mpaka sasa?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu la pili, pamoja na juhudi nyingi ambazo Serikali inazifanya katika kuhakikisha vijana wanapata ajira na nyezo za kujiajiri. Ripoti ya UN Tanzania ya 2018 inaonesha kwamba kati ya vijana 87 ni vijana wanne tu ambao wanaweza kujikimu kiuchumi, hili suala linazidi kuwa baya au linazidi kuwa gumu siku hadi siku. Je, Serikali sasa ina mpango gani wa dharura kuweza kuwanusuru vijana katika udumavu huu wa kiuchumi?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU (KAZI, VIJANA NA AJIRA): Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwa kusema tu kwanza nampongeza sana Mheshimiwa Khadija kwa kazi kubwa anayoifanya kuwasimamia vijana wa nchi hii na amekuwa mtetezi wa kweli wa vijana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika swali lake la kwanza, ametaka kujua idadi ya vijana walioajiriwa katika viwanda. Nimwombe tu Mheshimiwa Mbunge kwamba kwa sababu idadi hii ya walioajiriwa kwenye viwanda siwezi kuipata hapa ndani Bungeni hivi sasa, lakini nitakachokifanya nitahakikisha kwamba tunafanya coordination na wenzetu kuweza kujua katika viwanda hivyo ambavyo vimeanza kutoa ajira kwa vijana ni asilimia ngapi ya vijana ambao wameshapata ajira mpaka hivi sasa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kutokana na mchango mkubwa wa sekta ya viwanda, tunaamini kabisa kundi kubwa la vijana ndiyo hasa waliopata nafasi ya kuajiriwa kwa sababu katika nguvu kazi yetu ya nchi Tanzania tuliyonayo asilimia zaidi ya 65 ni vijana, kwa hiyo automatically hapa kundi kubwa ambalo watakuwa wamepata ajira ni vijana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, ni namna gani Serikali tunakuja na mpango wa kukwamua vijana kutokana na udumavu wa kipato…
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mipango tuliyonayo mikubwa kabisa ni kuhakikisha kwamba tunawashirikisha vijana katika shughuli mbalimbali za kiuchumi. Lengo letu ni kuwapatia fedha za Mifuko ya Uwezeshaji ili wafanye shughuli za kiuchumi za kuweza kujisimamia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, huo ndiyo mkakati mkubwa wa Serikali kwa sasa. (Makofi)
MHE. KHADIJA NASSIR ALI: Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Pia napenda kumshukuru Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu yake mazuri. Nina maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Spika, kwa vile bado malalamiko ya waajiriwa ni mengi sana nchini na bado utaratibu haujafafanua vizuri ni namna gani ambavyo waajiriwa hawa wanaweza kupata stahiki zao na usalama wao wakati wakiwa katika maeneo ya kazi, Serikali ina kauli gani juu ya hili?

Mheshimiwa Spika, swali langu la pili, kwa vile bado ajira zetu za ndani hazina sheria ya moja kwa moja ambayo inawalinda waajiriwa, Serikali pia inasema nini juu hili?

Mheshimiwa Spika, ahsante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU (KAZI, AJIRA NA VIJANA): Mheshimiwa Spika, katika swali la kwanza kuhusu malalamikio, Ofisi ya Waziri Mkuu imekuwa ikiyafanyia kazi malalamiko na taarifa mbalimbali zinazowahusu wafanyakazi kwa kufanya kaguzi mbalimbali ambazo lengo la kaguzi hizi ni kutaka waajiri wote nchini wafuate utaratibu wa sheria unavyoelekeza kwa maana ya Sheria Na. 6 ya mwaka 2004 na Sheria Na. 7 ya mwaka 2004 ambazo zimetoa haki na wajibu kwa wafanyakazi pamoja na waajiri.

Mheshimiwa Spika, ofisi yetu imeendelea kuchukua hatua kwa waajiri wote ambao wanakiuka sheria na mpaka ninavyozungumza hivi sasa, tayari tumeshawafikisha Mahakamani zaidi ya waajiri 19 katika kipindi cha mwaka 2017/2018 ambao wamekiuka utaratibu wa sheria. Ndiyo maana Ofisi ya Waziri Mkuu itaendelea kufanya ukaguzi wa mara kwa mara ili kuepukana na malalamiko haya ya wafanyakazi.

Mheshimiwa Spika, sehemu ya pili ya swali lake Mheshimiwa Mbunge alitaka kujua kuhusu sheria ya kuwalinda wafanyakazi. Kwa mujibu wa Sheria Na. 6 ya Mwaka 2004, imeainisha bayana haki za mfanyakazi na wajibu wa mwajiri. Sheria hii ndiyo inayotumika katika kuwalinda wafanyakazi. Ndiyo maana Bunge lako Tukufu mwaka 2016 lilifanya marekebisho ili kuongeza meno zaidi katika Idara ya Kazi katika kuwalinda wafanyakazi kwa kuhakikisha kwamba ikitokea mwajiri anakiuka taratibu za kisheria kuhusu mikataba na masaa ya kazi, Afisa Kazi akienda kumkagua atakuwa na uwezo wa kumtoza faini hapo hapo ambayo ni kiasi cha fedha, ambapo pia baadaye atakuwa na compliance order haya yote yaende kwa pamoja. Lengo ni kufanya sheria hiyo iwe na meno na wafanyakazi wetu waweze kulinda haki zao.

Mheshimiwa Spika, ahsante.
MHE. KHADIJA NASSIR ALI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru namshukuru pia Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu yake. Nina maswali mawili ya nyongeza. Taarifa ya Mkaguzi Mkuu inaeleza kwamba kati ya lita 92,000 ya dawa hizo zilizosambazwa kwenye mikoa 26 ya Tanzania Bara ni lita 25,000 tu ndiyo ambazo zimeweza kutumika mpaka sasa. Ukizingatia dawa hizi zina life span, inawezekana kama hazijaharibika, sasa zinakaribia kuharibika. Serikali inatoa maelezo gani juu ya upungufu huo?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu la pili, kwa kuwa dawa hizi zilisambazwa kwa mkopo wenye thamani ya shilingi bilioni 3.1 na makubaliano yalikuwa kwamba Halmashauri husika ziweze kulipa fedha hizi, Serikali ina
mkakati gani kusimamia fedha hizi ili ziweze kulipwa? Ahsante?
NAIBU WAZIRI WA VIWANDA NA BIASHARA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Ni kwamba kimsingi dawa hizi ni muhimu sana na zinaua hasa katika maeneo yale ya mazalia. Sasa kama kuna Halmashauri zimechukua dawa hizo na zikaacha kupeleka kwenye maeneo hayo ya mazalia ya mbu kwa kweli wanatenda kosa kubwa kwa sababu wanawanyima wananchi haki yao ya kupona kutokana na kutokomeza viluwiluwi vya Malaria. Nawaomba wafanye hivyo mapema iwezekanavyo na wajue kwamba kufanya hivyo ni kurudisha nyuma jitihada za Serikali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile kuhusiana na madeni, ni kweli kabisa Halmashauri nyingi hazijaweza kulipa madeni waliyochukua dawa hizo. Kwa hiyo, nizitake pia Halmashauri kuhakikisha kwamba wanalipa madeni yao na kuyapa kipaumbele iwezekanavyo kuhakikisha kwamba wanalipa ili kutelekeza azma ya Serikali ya kukifanya kiwanda hicho kuwa endelevu.
MHE. KHADIJA NASSIR ALI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kuniona. Kumekuwa na masharti magumu sana katika kupata mikopo ukizingatia vikundi vya vijana wengi wanakuwa bado hawana zile dhamana ambazo zinahitajika. Serikali inatuambia nini ili na sisi vijana ambao hatukidhi vigezo hivyo tuweze kufaidika na mikopo hiyo?

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU (KAZI, VIJANA NA AJIRA): Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Khadija Nassir Ali, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nichukue fursa hii kumpongeza sana Mheshimiwa Mbunge kwa namna ambavyo anashughulikia masuala ya vijana na kuwa mstari wa mbele kuwatetea vijana wa Taifa hili la Tanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kutambua kwamba ipo changamoto kubwa sana ya upatikanaji wa mikopo katika kundi hili kubwa la vijana, Serikali kupitia Baraza la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi na mifuko mbalimbali ya uwezeshaji wananchi kiuchumi, imedhamiria kidhati kabisa kuwasaidia vijana wa Taifa letu kwa kuwakopesha fedha pasipo masharti magumu kama ambavyo wanayapata kupitia taasisi za kifedha. Tunao Mfuko wa Maendeleo ya Vijana ambao mpaka hivi sasa umeshakopesha zaidi ya shilingi bilioni 4.5 katika vikundi 237 vya vijana nchi nzima. Kwa hiyo, ni fursa ambayo vijana wanayo kupitia mfuko huu ambapo wanaweza kukopa bila masharti mengi ambayo yapo katika taasisi nyingine za kifedha. Kwa hiyo, nitoe rai kwa vijana wote nchi nzima ambao wanapenda kufanya shughuli za uzalishaji mali kuutumia Mfuko wa Maendeleo ya Vijana kwa ajili ya uwezeshaji.
MHE. KHADIJA NASSIR ALI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kuniona. Kwanza kabisa nipende kuzipongeza Serikali zote mbili kwa jitihada ambazo zimekuwa zikichukua katika masuala haya. Kwa kuwa jitihada hizi, wananchi wengi hawana taarifa nazo na hawana uelewa nazo, Serikali sasa haioni umuhimu wa kuanza kuweka utaratibu maalum wa kutoa taarifa hizi ili wananchi waweze kupata uelewa wa pamoja? Ahsante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS (MUUNGANO NA MAZINGIRA): Mheshimiwa Naibu Spika, nikushukuru. Nichukue fursa hii pia kumpongeza Mheshimiwa Khadija Nassir lakini pia nipokee ushauri wake, tufike mahali sasa tuanze kuziweka wazi taarifa hizi japo tumekwishaanza lakini kuweka kwa mapana zaidi. Kwa hiyo, napokea ushauri.
MHE. KHADIJA NASSIR ALI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Kwa kuwa, rate ya mama wanaojifungua watoto njiti imekuwa ikiongezeka nchini. Serikali ina mipango gani ya ziada kuweza kuwasaidia wamama wajawazito kuepukana na tatizo hilo, lakini pia ni sababu gani zinazowasababisha wamama wajawazito kujifungua watoto njiti? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, kikubwa sisi kama Serikali tunasisitiza sana, mama anapopata ujauzito kuhakikisha kwamba, anaenda kliniki na sisi katika kliniki tunaweza tukabaini visababishi ambavyo vinaweza vikasababisha mama kuzaa mtoto njiti na kuweza kuvitatua.

Mheshimiwa Mwenyekiti, na kwa kifupi tu visababishi ni vingi, moja ni uzito wa mama mwenyewe; ikiwa mama ana uzito mdogo au uzito mkubwa inaweza ikasababisha kuzaa mtoto njiti, maambukizi ambayo mama anaweza akayapata, matumizi ya vileo, stress ambazo anaweza akawanazo mama wakati wa ujauzito ni sehemu ya visababishi ambavyo vinaweza vikasabaisha mtoto kuzaliwa njiti.
MHE. KHADIJA NASSIR ALI: Mheshimiwa Spika, ninakushukuru kwa kunipa nafasi. Ukosefu wa Ofisi za Bodi ya Mikopo kwa upande wa Zanzibar umekuwa ukileta usumbufu mkubwa sana kwa wazazi na wanafunzi kusafiri kuja Dar es Salaam kwa ajili ya huduma hizo.

Mheshimiwa Spika, ukizingatia hali duni ya wazazi, ni lini Serikali itasogeza huduma hizo kwa upande wa Zanzibar. Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Spika, ni kweli kwamba kumekuwepo na changamoto hiyo ya ofisi kutoka Zanzibar, lakini naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge, kwamba tayari kuna jitihada za kuhakikisha kwamba ofisi inakuwepo Zanzibar.

Mheshimiwa Spika, pia, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba, pamoja na ofisi kutokuwepo, bodi ya mikopo imeendelea kurahisisha namna ya kuomba mikopo na kurejesha, kiasi kwamba unaweza ukafanya maombi na kurejesha popote ulipo kwa sababu siku hizi kuna teknolojia, lakini naomba vilevile nimhakikishie kwamba bado kuna jitihada za kuhakikisha Zanzibar nayo inakuwa na ofisi.
MHE. KHADIJA NASSIR ALI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kuniona, kufuatia mvua kubwa ambazo zinaendelea kunyesha nchini kumekuwa na uharibifu mkubwa sana wa miundombinu jambo ambalo limesababisha vifo kwa baadhi ya wananchi na kudhorota kwa shughuli za kiuchumi na za kijamii.

Je, Serikali ina mkakati gani maalum wa kuhakikisha kwamba baraka hii ya mvua inakuwa fursa na chachu ya maendeleo na siyo majanga kama ilivyo sasa hivi kwenye nchi yetu? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza tunao utaratibu kawaida kama sehemu ya mkakati wa kushughulikia hali mvua zinavyokuwa nyingi, ndiyo maana katika bajeti ya mwaka huu unayoendelea kupitia Bunge lako Serikali ilitenga bilioni 8 zaidi ya bilioni 8 kwa ajili ya kumudu dharura zinavyojitokeza, kwa hiyo mkakati tuko nao.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sababu mvua zimekuwa nyingi ndiyo maana tumeendelea kufanya utambuzi wa mahitaji hasa mvua zinavyoendelea, na hapa ninavyozungumza mpaka kufikia Januari tuna mahitaji ya shilingi bilioni 13.6 kwa ajili ya maeneo ya Mikoa 14 ambayo tumeitambua imekuwa na shida. Kwa hiyo, tunaendelea kupitia utaratibu wa kibajeti Serikali itafanya utaratibu wa kuona namna nzuri ya kutatua maeneo haya.

Mheshimiwa Naibu Spika, yako maeneo mengine yatahitaji mvua ikipungua ndiyo tuende tufanye marekebisho makumbwa, sasa hivi TARURA kushirikiana na TANROAD tunafanya utaratibu wa ku-harmonize yaani kufanya kazi kwa pamoja ili kutengeneza barabara mbadala kwenye maeneo ambayo yana shida ili wananchi waendelee kupata huduma ya barabara mvua zikipungua tutarudi kufanya marejesho makubwa kwenye maeneo ambayo yamepata athari kubwa. Kwa hiyo, utaratibu upo wa kibajeti tutaendelea kuufuata kwa kuzingatia taratibu na sheria ili tuone tunafanya vizuri katika maeneo na kuwanusuru wananchi na hali hii ya mvua kubwa zilizoendelea kunyesha. Ahsante sana.