Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Josephine Johnson Genzabuke (44 total)

MHE. JOSEPHINE J. GENZABUKE: Ahsante Mheshimiwa Naibu Spika. Pamoja na majibu mazuri ya Naibu Waziri, nina maswali mawili ya nyongeza.
Kwa kuwa Serikali imekuwa ikitenga fedha kwa ajili ya barabara hii, lakini hazipelekwi. Mara tatu mfululizo imekuwa ikitenga fedha hazipelekwi; mara ya kwanza shilingi bilioni nne; mara ya pili mwaka 2015/2016 zilitengwa shilingi bilioni 10 hazikwenda.
Je Serikali inaweza kulihakikishia Bunge hili na wananchi wa Mkoa wa Kigoma kuwa fedha zitatengwa sasa na kupelekwa Kigoma ili barabara hii iweze kukamilika? (Makofi)
Swali langu la pili, Kidahwe – Kasulu kuna mkandarasi ambaye yupo pale lakini amesimama kwa sababu hajaweza kulipwa fedha zake. Je, ni lini mkandarasi huyo atalipwa ili aweze kuendelea na kazi ya ujenzi wa barabara hiyo?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sehemu ya swali lake la kwanza naomba kuthibitisha kwamba ndivyo itakavyokuwa.
Kwa swali lake la pili, naomba kumhakikishia kwamba wakandarasi wote Tanzania nzima tumeshaanza kuwalipa madai yao ikiwa ni pamoja na huyo mkandarasi. Kwa hiyo, muda siyo mrefu huyu mkandarasi atarudi site na kuanza kukamilisha hiyo kazi.
MHE. JOSEPHINE J. GENZABUKE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, nina maswali mawili ya nyongeza. Kwa kuwa kwa muda mrefu sana kumekuwepo mgogoro wa wananchi na Serikali kwa maana ya Hifadhi za Serikali na wananchi wamekuwa wakilalamika sana kwa sababu watu wameongezeka lakini ardhi haiongezeki:-
Je, ni lini sasa Serikali italeta sheria Bungeni ili ifanyiwe marekebisho kuweza kumaliza mgogoro baina ya wananchi na Serikali?
Swali la pili, kwa kuwa kuna mgogoro mkubwa na wa muda mrefu katika Hifadhi ya Pori la Kagerankanda na Serikali; na wananchi wamekuwa wakipata shida sana kutokana na shida iliyopo kwa sababu kwa muda mrefu hifadhi haijafanyiwa marekebisho ya kupimwa mipaka:-
Je, ni lini sasa Mheshimiwa Waziri tutafuatana kuja Kasulu kwa ajili ya kumaliza suala la Mipaka katika Wilaya ya Kasulu katika eneo la Kagerankanda?
NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza, ametaka kujua ni lini Serikali italeta sheria ambayo itakwenda kumaliza migogoro kati ya Serikali na Wananchi.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niseme tu, kama nilivyojibu kwenye swali la msingi, mgogoro uliopo pengine unaweza kuwa umchangiwa pia na baadhi ya watumishi wetu, kwa sababu 2002 mhifadhi aliyekuwa katika ile mbuga alikwenda akabainisha mipaka ambayo ilikosewa, matokeo yake ikabidi warudie tena 2009 baada ya mhifadhi mwingine kubadilika.
Mheshimiwa Naibu Spika, mhifadhi alipobadilisha tena naye mgogoro ukawa mkubwa zaidi. Ndiyo maana hapa sasa Serikali ilibidi iingilie kati katika kuangalia ile GN iliyokuwepo na kuweza kujua mipaka halisi ni ipi. Kwa sababu mgogoro umekuwa mkubwa zaidi, ndiyo maana pia Mkuu wa Wilaya ya Wanging‟ombe akaunda Tume kwa ajili ya kutaka kutatua.
Mheshimiwa Naibu Spika, nimelizungumza hili la mipaka kwamba lina matatizo, tutakwenda kushirikiana Wizara zinazohusika kwa sababu huu mgogoro hauhitaji kutungiwa Sheria, ni namna tu ya kutafsiri mipaka katika eneo ambalo lina mgogoro. Wananchi wanadai wako nje, lakini mipaka ya hifadhi, wahifadhi wanasema wako ndani ya hifadhi. Ndiyo maana nimesema, hapa tutakaa Wizara yangu ya Ardhi, Wizara ya TAMISEMI pamoja na Wizara ya Maliasili na Utalalii ili tumalize huo mgogoro.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali lake la pili ameongelea pori la Kagerankanda; nalo lina mgogoro na wananchi na akataka tuongozane kwenda Kasulu kwa ajili ya utatuzi.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba, baada ya kikao hiki cha Bunge na baada ya kukutana Wizara zote zinazohusika na migogoro hiyo kama ambavyo imewasilishwa na Waheshimiwa wabunge na siyo huu mgogoro wa Kasulu tu na migogoro mingine, tutapanga ratiba maalum ya kufika katika maeneo ili tuweze kutatua.
Mheshimiwa Naibu Spika, kinachofanyika sasa ni kujua chanzo cha mgogoro: Je, ni Wizara inatakiwa kwenda na Wizara nyingine au uko kwenye mipaka kwa maana ya TAMISEMI au ni hifadhi pamoja na ardhi ili tuweze kujua?
Mheshimiwa Naibu Spika, tukishabainisha kwa sababu orodha tunayo kwa Majimbo yote au kwa nchi nzima, basi tutatatua kulingana na nature ya mgogoro wenyewe.
MHE. JOSEPHINE J. GENZABUKE: Mheshimiwa Spika nakushukuru. Naitwa Genzabuke.
Mheshimiwa Spika, ukosefu wa viwanda katika Mkoa wa Tabora ni sawa na ukosefu wa viwanda katika Mkoa wa Kigoma. Kwa muda mrefu sana Mkoa wa Kigoma umekuwa kama uko kisiwani kwa maana ya ukosefu wa miundombinu ya barabara za lami na umeme. Hata hivyo, kwa juhudi zinazofanywa na Serikali inayoongozwa na Chama cha Mapinduzi, mkoa ule umeanza kufunguka na siyo muda mrefu utafunguka kabisa. Je, Waziri yuko tayari sasa kuwahamasisha wawekezaji kuja kuweka viwanda katika Mkoa wa Kigoma?
WAZIRI WA VIWANDA, BIASHARA NA UWEKEZAJI: Mheshimiwa Spika, ni kweli katika maeneo ambayo nimepewa maelekezo mahsusi kushughulikia ni pamoja na Mkoa wa Kigoma. Napenda kutambua mchango wa Wabunge wa Mkoa wa Kigoma kwa ujumla wenu namna mnavyonipa ushirikiano katika kushughulikia suala hili. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, miradi iliyoko mbioni kwenda ni Kigoma Sugar, nimemomba Mkurugenzi Mtendaji wa TIC anipe update kama ilivyokuwa jana, Kigoma Sugar tumefikia wapi. Ameniletea taarifa, nimesema arudie anieleze kwa maandishi yule mwekezaji anasema nini nataka update ya jana, Kigoma sugar iko njiani.
Mheshimiwa Spika, simenti watalaam wa cement wamebainisha kwamba, katika Mkoa wa Kigoma ndiko kuna chokaa nyingi. Kwa hiyo, nakwenda kuwashawishi wenye viwanda, wanaotengeneza clinker Dar es Salaam, itengenezwa clinker Dar es Salaam iletwe Kigoma tuweze kutengeneza cement.
Mheshimiwa Spika, suala la tatu mawese; mpango wa kaya moja kulima heka moja, kaya laki moja, tulime heka laki moja tutengeneze shamba kubwa la mawese nalifanyia kazi na mwekezaji ameshakubali na kiwanda kitagharimu bilioni 15, ni kazi yangu, ni kazi yenu. Atakayenichangamkia ndiyo nitakwenda kwake!
kunipa nafasi ili niulize swali la nyongeza.
Kwa kuwa ukosefu wa vifaa tiba katika Wilaya ya Chamwino ni sawasawa kabisa na ukosefu vifaa tiba uliopo katika Wilaya ya Kasulu. Wilaya ya Kasulu haina ultra sound, lakini mpaka sasa hivi ninavyoongea Wilaya ya Kasulu haina vifaa-tiba vya kupimia sukari (test strips), na hili linasababisha wagonjwa kuweza kupoteza maisha kwa sababu wanapopima vipimo kinakosekana kipimo cha sukari wakati mwingine wanaweza kupoteza maisha kwa sababu wanapima…
Mheshimiwa Naibu Spika, ndiyo. Sasa ni lini Serikali itahakikisha inapeleka ultra sound Kasulu lakini sambamba na vifaa vya kupimia sukari? Ahsante
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Josephine Gezabuke, Mbunge Viti Maaalum kutoka Mkoa wa Kigoma, ambaye amerudi tena baada ya wananchi kumpa ridhaa kama ifauatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli Kigoma kuna changamoto hiyo kama alivyosema Mbunge. Lakini jibu langu lile litakuwa vilevile kama jibu la awali. Mkoa wa Kigoma ni Mkoa ambao upo pembezoni zaidi, kwa hiyo hata kufanya ile referral system ni changamoto kubwa sana. Sisi kama Serikali naomba tuseme kwamba eneo la Mkoa wa Kigoma tutalipa kipaumbele maalum katika kipindi hiki na naomba nikwambie kwamba jukumu langu kubwa baada ya Bunge la Bajeti miongoni mwa mikoa ambayo natarajia kuitembelea ni Mkoa wa Kigoma.
Mheshimiwa Naibu Spika, jukumu kubwa tutakalolifanya ni kuwahimiza watu katika suala zima la ukusanyaji wa mapato.
Mheshimiwa Naibu Spika, imani yangu kubwa ni kwamba tutakapokusanya mapato vizuri, kama nilivyoelekeza katika maeneo mablimbali, kwamba tukitumia mifumo ya electronic zile collection zetu zitakuwa kubwa, na zitatuwezesha kununua vifaa tiba. Lakini kwa Mkoa wa Kigoma kuwa Mkoa wa pembezoni kama Serikali tutaupa kipaumbele. Mheshimiwa Genzabuke kwa sababu wewe ni mwakilishi wa wakina mama na watoto, naomba nikwambie kwamba tumesikia lakini tutaangalia jinsi ya kufanya ili Kigoma ipewe kipaumbele cha msingi. (Makofi)
MHE. JOSEPHINE J. GENZABUKE: Mheshimiwa Naibu Spika nakushukuru kwa kunipa nafasi ili niulize swali la nyongeza, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa ni muda ni muda mrefu sana mgogoro wa Kagera Nkanda umekuwa ukiongelewa humu Bungeni lakini maka sasa hakuna ufumbuzi ambao umeshapatikana. Na kwa kuwa watu wanaongezeka lakini ardhi haiongezeki, ni lini Serikali italeta sheria Bungeni ili ifanyiwe marekebisho kusudi mipaka iweze kusogezwa wananchi wapate maeneo ya kulima?
NAIBU WAZIRI MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nitoe taarifa tu kwamba ni kweli migogoro inayohusisha mipaka kwenye hifadhi iwe hifadhi za misitu na hifadhi za wanyamapori ni mikubwa na ni kweli sasa imekuwepo kwa muda mrefu. Lakini napenda tu nitoe taarifa kwamba kama nilivyojibu kwenye swali langu la msingi sasa tunakwenda kupata ufumbuzi wa matatizo haya, tutapiga hatua na kuweza kuyapunguza matatizo haya kama sio kuyamaliza baada ya zoezi tunalolitaja ambalo litashirikisha Wizara sita kwenda kuangalia hasa uhalisia wa matatizo kwenye mipaka hii.
Mheshimiwa Naibu Spika, nimesema awali na isichukuliwe kwamba utatuzi au ufumbuzi wa changamoto za ardhi iko kwenye hifadhi za taifa peke yake, hapana, ndiyo maana tunasema sasa tunakwenda kwa ujumla wetu Wizara sita zote ambazo ni watumiaji wa ardhi ili tuweze kwenda kubaini kwamba ni kweli kuna uhaba wa ardhi au kuna matatizo mengine yanayosababisha watu kuingia kwenye hifadhi? Kwa hiyo, tutakwenda kuchakata na kuangalia mahitaji yapi ya ardhi yanahitaji ardhi ambayo tunaweza kuipata wapi kabla hatujaingia kwenye hifadhi ambako kumezuiliwa kwa mujibu wa sheria.
MHE. JOSEPHINE J. GENZABUKE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ili niulize maswali ya nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, nina maswali mawili ya nyongeza.
Kwa kuwa Mkoa wa Kigoma unapakana na nchi za Burundi na DRC, na kwa kuwa eneo kubwa la mpaka halina ulinzi, hali inayopelekea wahalifu kupita na kupitisha silaha nzito kuingia Tanzania, wahalifu hao kwa kushirikiana na raia wasiokuwa waaminifu hufanya ujambazi na unyang‟anyi.
Je, Serikali iko tayari kufanya utafiti wa kukagua mpaka upya na kubaini maeneo yasiyokuwa na ulinzi ili kuweza kuweka ulinzi maeneo yasiokuwa na ulinzi? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, swali langu la pili; kwa kuwa mara nyingi vituo vya polisi hukabiliwa na ukosefu wa mafuta, hivyo kuwafanya polisi kushindwa kufanya kazi yao kikamilifu. Je, Serikali iko tayari kuongeza bajeti ya vituo vya polisi, hasa Mkoa wa Kigoma ili polisi waweze kukabiliana na majambazi hao?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, swali la Mheshimiwa Genzabuke limekuja wakati muafaka kwa sababu jana tulikuwa tuna kikao kizito ambacho kilikuwa kinahusisha Wakuu wa vyombo vyote vya usalama vilivyopo nchini, vilivyo chini ya Wizara ya Mambo ya Ndani. Moja katika ajenda ya msingi ambayo tulizungumza ilikuwa ni hiyo.
Ninachotaka kumuelezea tu kwa sasa hivi ni kwamba tumetoa jukumu hilo kwa Idara ya Uhamiaji ambayo kazi hii wameshaianza kufanya huo utafiti ambao anauzungumza wa kubaini vipenyo vyote ambavyo vinakisiwa viko vipenyo takribani 248 nchi nzima. Kuazia Mkoa wa Kagera, nchi nzima kwa maana ya mikoa yote ambayo imepakana na nchi jirani. Kwa hiyo, tumeshaanza hiyo kazi na pale itakapokamilika wataliwasilisha hilo andiko Serikalini.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia haina maana kwamba hivi tunavyozungumza kuna tatizo kiasi kikubwa hivyo, kwa sababu kuna kazi kubwa ambayo inafanywa na vyombo hivi vya usalama, ikiwemo kuendesha doria na misako katika maeneo hayo ambayo ni maeneo tete. Lakini kutoa elimu vilevile kwa wananchi pamoja na Wenyeviti wa Mitaa na Vitongoji wa maeneo ambayo yanapakana na mipaka hiyo pamoja na kuimarisha vitendea kazi.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusiana na swali lake la pili ambalo amezungumzia changamoto ya mafuta; ninataka tu nimueleze kwamba moja katika majukumu ya msingi ya Wizara yetu hii ambayo tumefanya kwa mafanikio makubwa ni kuhakikisha kwamba kuwepo kwa wakimbizi katika maeneo hayo ambayo yapo katika Mikoa inayopakana na mikoa hii ambayo ina machafuko ikiwemo Kigoma, kusilete athari kwa wananchi na badala yake kuwe kuna manufaa. Katika kufanya hivyo tumeweza kuzungumza na mashirika haya ambayo yanahudumia wakimbizi kuweza kuchangia, siyo tu kwa maendeleo ya jamii ya wananchi ambao wanaishi pale, lakini hata kwa vyombo vya usalama wakati wa kutekeleza majukumu yao. Moja katika mafanikio hayo ni kwamba hivi tunavyozungumza UNHCR wametoa magari sita, pikipiki mbili kwa kambi tatu za Nyarugusu, Mtendeli na Nduta, na gari moja aina ya Land Cruiser kwa Ofisi ya RPC. Pia shirika hilo huwa linatoa mafuta kwa kuwalipa posho ya shilingi 15,500 kwa siku, kwa askari ambao wanalinda kambi.
Mheshimiwa Naibu Spika, sambamba na jitihada za Serikali ambazo zinafanyika kuweza kuimarisha bajeti ya polisi ya mafuta kadri hali ya uchumi itakavyoimarika. Kwa hiyo, kuna kazi ambayo inafanyika tu na imekuwa na mafanikio kwa kiasi kikubwa, hata hivyo tunazitambua changamoto ambazo Mheshimiwa Genzabuke amezungumza na hii mikakati niliyoizungumza ni moja kati ya njia ambazo tunakabiliana nazo.
MHE. JOSEPHINE J. GENZABUKE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi.
Kwa kuwa kulikuwa na ahadi ya Rais Mstaafu Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete kununua meli katika maziwa makuu matatu kwa maana ya Ziwa Tanganyika, Ziwa Victoria na Ziwa Nyasa, na katika bajeti hii ya Mawasiliano na Uchukuzi kuna ununuzi wa meli moja ya Ziwa Victoria, lakini hivi karibuni Waziri wa Katiba na Sheria alisikika akipongeza uundwaji wa meli mpya ya mizigo na abiria katika Ziwa Nyasa. Je, ni lini sasa meli mpya itapelekwa katika Ziwa Tanganyika ili tuachane na meli ya MV Liemba?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kiongozi wetu wa Serikali ya Awamu ya Nne alitoa ahadi ya kuleta meli mpya katika maziwa yote makuu matatu na ahadi hiyo ilirudiwa na Rais wa Awamu ya Tano Dkt. John Pombe Joseph Magufuli kwamba atatekeleza ahadi hiyo ambayo mwanzo ilitolewa na Mheshimiwa Kikwete.
Mheshimiwa Naibu Spika, nimhakikishie hili tuliloliongelea katika jibu langu la swali la msingi ndiyo kuanza kutekeleza ahadi ya viongozi hawa wakuu, tunaanza na meli ya MV Victoria na unafahamu kwamba wakati kuna meli ndogo inatengenezwa kule Nyasa baada ya hapo tutafuatia na meli katika
Ziwa Tanganyika na hatimaye ahadi hizo za viongozi wakuu zitatekelezwa katika kipindi hiki cha miaka mitano tulichoahidi. Tuanze na hatua moja halafu tutasonga mbele.
MHE. JOSEPHINE J. GENZABUKE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Kwa kuwa wananchi wa Kasulu wengi wao kwa kutokujua mipaka inaishia wapi; wamekuwa wakilima mpakani mwa pori la Kagera Nkani na kwa sasa mazao yao yako tayari wanahitaji kuvuna.
Je, Serikali iko tayari kumuagiza Mkuu wa Wilaya awaruhusu wananchi waweze kuvuna mazao yao huku utaratibu mwingine ukiwa unaendelea?
WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Naibu Spika, maagizo yametolewa mahususi kabisa kuhusu suala hilo kwamba Wizara pamoja na Wakuu wa Wilaya wawaruhusu wananchi ambao wamelima ndani ya hifadhi zetu waweze kuvuna mazao yao kabla hawajaondoka katika maeneo hayo.
Kwa hiyo, nimkumbushe tu Mkuu wa Wilaya juu maagizo hayo na awaruhusu wananchi wachukue mazao yao.
MHE. JOSEPHINE J. GENZABUKE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi. Kwa kuwa Mkoa wa Kigoma ni kati ya mikoa ambayo iko pembezoni na viko vijiji ambavyo vimepakana na nchi jirani ya Burundi na vijiji hivyo havina mawasiliano. Je, Serikali iko tayari kushawishi makampuni kupeleka minara katika Vijiji vya Kitanga (Kasulu), Kilelema (Buhigwe) na Nyagwijima (Kibondo)?
NAIBU WAZIRI UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Naibu Spika, tupo tayari na kwa kweli ndicho tunachokifanya siku zote hizi. Mheshimiwa Mbunge anafahamu kwamba katika suala la mawasiliano mipakani ni priority namba moja.
MHE. JOSEPHINE J. GENZABUKE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi. Kwa kuwa Mkoa wa Kigoma ni kati ya mikoa ambayo iko pembezoni na viko vijiji ambavyo vimepakana na nchi jirani ya Burundi na vijiji hivyo havina mawasiliano. Je, Serikali iko tayari kushawishi makampuni kupeleka minara katika Vijiji vya Kitanga (Kasulu), Kilelema (Buhigwe) na Nyagwijima (Kibondo)?
NAIBU WAZIRI UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Naibu Spika, tupo tayari na kwa kweli ndicho tunachokifanya siku zote hizi. Mheshimiwa Mbunge anafahamu kwamba katika suala la mawasiliano mipakani ni priority namba moja.
MHE. JOSEPHINE J. GENZABUKE: Mheshimiwa Naibu Spika nakushukuru kwa kunipa nafasi, nina swali moja la nyongeza. Tatizo la ukosefu wa Mahakama katika Wilaya ya Chunya ni sawasawa na tatizo llililopo katika Mahakama ya Herujuu. Jengo lililokuwepo la tangu enzi za ukoloni limebomoka kabisa hivyo huduma ya Mahakama wanakaa chini ya miti. Je, ni lini Serikali itatoa pesa kwa ajili ya ujenzi wa Mahakama ya Herujuu?
WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nikiri mbele yenu kwamba hali ya miundombinu ya Mahakama nchini si nzuri. Nikielekeza macho tu, upande wa Mahakama za Mwanzo tunahitaji ili tuwe na access to justice sawasawa tuwe na Mahakama za Mwanzo katika kila Kata. Tuna kata zaidi ya 3,900 nchini lakini Mahakama tulizojenga mpaka sasa hazizidi 900, kwa hiyo pengo ni kubwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, namwomba Mheshimiwa Josephine Genzabuke, kuhusu mahitaji halisi katika eneo lake, tunaomba atuandikie hiki ndiyo kipindi ambacho tunaangalia mahitaji kufuatana na demand iliyopo katika maeneo yote tuliyonayo. Kwa hiyo tunasubiri ndani ya siku mbili, tatu atatufikishia hayo mahitaji ya jimbo lake.
MHE. JOSEPHINE J. GENZABUKE: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Pamoja na majibu ya Mheshimiwa Waziri, nina maswali mawili ya nyongeza. Swali la kwanza; kwa kuwa, wananchi wanaoingia kwenye hifadhi ya misitu siyo kwamba wanaingia kwa sababu ya ukatili ni kwa sababu ya kukosa maeneo ya kuishi na kulima.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mfano; wananchi wa Wilaya ya Kasulu wanaoingia kwenye pori ya Hifadhi ya Kagerankanda ni kwa sababu watu wameongezeka, ardhi ni ile ile, maeneo ya kilimo yamekuwa ni kidogo. Je, kwa nini, Serikali isiwaruhusu waendelee kulima wakati Serikali inaandaa utaratibu mwingine wa kupima mipaka. (Makofi)
Swali la pili; kwa kuwa, ongezeko la watu ni kubwa sana, kwa nini, Serikali isitenge baadhi ya maeneo ya misitu ili wananchi waruhusiwe kuishi na kuwapunguzia tatizo hili la kuhangaika kutafuta maeneo ya kulima?
Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante.
WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kwamba wako wananchi ambao wameingia na wamejenga ndani ya maeneo ya misitu na wanakaa humo kufanya shughuli za kibinadamu. Sheria zetu za nchi zinakataza wananchi kuingia na kujenga, kulima ndani ya hifadhi zetu. Kwa hiyo, naomba niwahamasishe wananchi hawa wafuate sheria na wafuate sheria bila shuruti. Kwa hiyo, waondoke kwenye maeneo ya hifadhi na washirikiane na Halmashauri pamoja na Serikali za vijiji vyao kuwapangia maeneo mengine ya kuishi.
Mheshimiwa Naibu Spika, ongezeko la watu ni phenomena ambayo inatokea dunia nzima. Siyo jambo la Tanzania peke yao, kama ambavyo mmeona, nchi ambazo zinaendelea na zile ambazo zimeshaendelea, idadi ya wakulima inaendelea kupungua mpaka kufikia asilimia 20 katika nchi nyingi za Ulaya au kule Marekani, hii inatokana na watu kufanyakazi zingine, siyo lazima wote tuwe wakulima, kufanya kazi zingine ambazo mahitaji yake ya ardhi ni madogo kama vile ufugaji wa samaki, ufugaji wa nyuki kuanzisha viwanda vidogovidogo kama nilivyoeleza kwenye swali langu la msingi ili kuhakikisha kwamba maisha yetu yanaendelea, lakini na misitu yetu inakuwepo ili maisha yetu yaendelee kwa ustaarabu ambao unatakikana.
MHE. JOSEPHINE J. GENZABUKE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali mawili ya nyongeza pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri. Swali la kwanza, katika Wilaya ya Kasulu katika kijiji cha Makere lakini pia katika Wilaya ya Kakonko wananchi wamekuwa wakipata kipato chao kwa kuchimba chokaa, lakini mara nyingi wamekuwa wakizuiliwa kufanya shughuli hiyo. Je, Wizara ya Madini na Wizara ya Maliasili iko tayari kukaa pamoja na wananchi hao ili kuweza kutatua tatizo hilo na kuwawezesha kuwa wachimbaji rasmi? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, swali langu la pili, je, Serikali ina mkakati gani wa kuhakikisha inatenga eneo la wachimbaji wadogo ili kuepusha migogoro inayoweza kutokea baadaye?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa
Naibu Spika, kwanza nimpongeze Mheshimiwa Genzabuke wakati tunatenga eneo la Kakonko mwaka 2002 alitupa ushirikiano mkubwa sana. Kwa hiyo, nakupongeza sana Mheshimiwa Genzabuke kwa kufuatilia maisha ya watu wa Kigoma. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini kuhusiana na maswali yake mawili, la kwanza alitaka kujua namna sisi pamoja na taasisi ya maliasili tunavyoshirikiana ili kuwawezesha wananchi hawa kupata maeneo na kufanya uchimbaji kwa ajili ya kuongeza pato lao.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nimshukuru Mheshimiwa Mbunge, Sheria ya Madini ya mwaka 2010 katika kifungu cha 95 pamoja na Sheria ya Mazingira zinakubaliana kwamba mtu yeyote anaweza akamilikishwa leseni katika eneo lolote ikiwa ni pamoja na maeneo ya reserve na hifadhi kinachotakiwa ni kupata kibali cha maandishi. Tumekuwa tukifanya hivyo Mheshimiwa Genzabuke ndiyo maana katika eneo la Makere kuna leseni 15 za uchimbaji wa chokaa, lakini katika maeneo mengine ya Lugufu kuna leseni saba za uchimbaji ambayo pia yako kwenye hifadhi. Kwa hiyo, hilo halina shida, lakini kama ulivyosema tutaendelea kukaa na wenzetu ili wananchi wa Kasulu na maeneo ya jirani waendelee kunufaika na uchimbaji wa madini. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusiana na kutenga maeneo. Kama ambavyo nimejibu katika swali la msingi na ambavyo nimesema katika swali langu la nyongeza la kwanza ni kwamba tunaendelea kutenga maeneo kwa ajili ya wachimbaji wadogo nchi nzima. Kwa sasa tumeshatenga maeneo saba katika Mkoa wa Geita na katika Mkoa wa Kigoma katika eneo linaloitwa Kinyo na Janda tutatenga maeneo hayo kwa ajili ya wachimbaji wadogo wa chokaa katika Wilaya ya Kasulu.
MHE. JOSEPHINE J. GENZABUKE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, nina maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza, kwa kuwa wapo wazabuni ambao walitoa huduma hiyo ya kusambaza vyakula na vifaa mbalimbali katika shule zetu zikiwemo na shule za watoto wenye ulemavu, lakini wazabuni hao wengi wao wana miaka zaidi ya mitano hawajaweza kulipwa pesa yao na walio wengi wamekopa benki na wengine nyumba zao zimeuzwa na wengine ziko hatarini kuuzwa. Je, Serikali iko tayari kufanya uhakiki wa madeni hayo ili kuweza kuwalipa wazabuni hao? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, swali langu la pili, kwa kuwa wapo wazabuni wapya ambao walitoa huduma ya kusambaza vyakula shuleni wao wamelipwa lakini wazabuni wa zamani hawajalipwa. Je, Serikali iko tayari kuwalipa wazabuni wa zamani ambao walitoa huduma ya kusambaza vyakula shuleni ambao hawajalipwa lakini wapya wamelipwa? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu swali la kwanza la kufanya uhakiki wa madeni haya ili walipwe, ndiyo maana nimesema kwamba ni kweli, kuna madeni mbalimbali hasa wazabuni waliotoa vyakula katika shule zetu kabla programu ya elimu bila malipo kuanza. Jambo hili kweli limesababisha wazabuni wengi kupata mtikisiko lakini ndiyo maana ilibidi Serikali kuyapitia madeni haya yote tukijua wazi kwamba lazima kuna mengine siyo sahihi maana katikati hapo tulibaini baadhi ya madeni mengine ni hewa.
Kwa hiyo, Serikali imefanya mchakato wa ku-analyse madeni yote haya ili kutambua deni halisi la Serikali. Naomba niwahakikishie Waheshimiwa Wabunge na wazabuni wote waliotoa vyakula shuleni kwamba Serikali itafanya kila liwezekanalo kuwalipa.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini katika hii concern kwa nini wazabuni wapya wanalipwa lakini wa zamani hawajalipwa ni kama nilivyosema kwamba utaratibu wa sasa tunapeleka fedha moja kwa moja kule shuleni. Kwa hiyo, kila mwezi mgao wa Serikali ukipeleka kule na fedha ya chakula inakuwepo. Ndiyo maana sasa hivi sitarajii sana kuona kwamba kuna wazabuni watadai kwa sababu fedha zote ambazo zinatakiwa zielekezwe katika ulipaji wa chakula tunazipeleka kila mwezi.
Kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba Serikali tunalibeba na sisi kama Watanzania na Serikali tutahakikisha kwamba wazabuni wetu wa ndani lazima tuwalinde ili waendelee kufanya biashara yao kwa sababu ndiyo watajenga uchumi wao katika nchi yetu hii.
MHE. JOSEPHINE J. GENZABUKE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ili niweze kuuliza swali moja la nyongeza. Matatizo yaliyopo Momba ni sawa kabisa na matatizo yaliyopo katika Mkoa wa Kigoma ikiwa ni katika Wilaya ya Kakonko na Buhigwe. Wilaya hizo ni mpya na zimekuwa zikipata huduma kutoka kwenye Wilaya Mama. Ni lini Wilaya ya Kakonko na Buhigwe zitapatiwa Hospitali ya Wilaya? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Naibu Spika, anavyosema Mheshimiwa Mbunge Genzabuke ni kweli Kakonko wanatumia Kituo cha Afya cha pale Kakonko, hali kadhalika Buhigwe hawana Hospitali ya Wilaya. Kipindi kile nilivyofika Kakonko na Buhigwe tulifanya makubaliano fulani juu ya nini kifanyike kama mipango ya awali kurekebisha hali hii.
Mheshimiwa Naibu Spika,pale Buhigwe kwanza tunaenda kufanya ukarabati mkubwa wa Kituo cha Afya cha Buhigwe kwa kukipatia wodi ya upasuaji na wodi kubwa ya wazazi na vifaa vyote vinavyowezekana. Jambo hili tunalipanga kama Mungu akijalia kabla ya mwezi Agosti tutakuwa tumelitekeleza.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, tutashirikiana na wenzetu wa Kakonko kuona ni jinsi gani tufanye, lakini nikifahamu fika kwamba jana nilikuwa naongea na Wabunge wahusika wa maeneo haya na Mheshimiwa Mbunge pia na tuliona hata ikama ya Madaktari walioenda kule ni wachache na katika mchakato ule wa ajira zitakazokuja hapo baadaye tutaongeza idadi ya wataalam kwa sababu ukiachia miundombinu lakini suala la human resources ni jambo la msingi. Haya yote kwa Mkoa wa Kigoma tutayapa kipaumbele ili wananchi wa mkoa huu waweze kupata huduma za afya ya msingi.
MHE. JOSEPHINE J. GENZABUKE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa Mkoa wa Kigoma kwa muda mrefu umekuwa haupati watumishi kwa sababu upo pembezoni lakini pia wakimbizi wameingia kwa wingi katika Mkoa wa Kigoma pamoja na kwamba wana hospitali zao kwenye makambi lakini kutokana na binadamu wasivyoweza kuzuiliwa wanaingia kwa wingi katika miji yetu hali inayosababisha wagonjwa kuwa wengi kwenye hospitali zetu. (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kulikuwa na suala la concern ya dawa katika Hospitali ya Kibondo ambalo mwanzo nilili-skip. Hata nilivyofika pale site Kibondo nilitoa maelekezo kuhusu matumizi mazuri ya Basket Fund. Maeneo yote nilikopita nimekuta kwamba japokuwa tumepeleka fedha za kutosha kwenye Basket Fund, lakini Waganga wetu wa Wilaya wameshindwa kuhakikisha zile fedha zinatumika kwa ajili ya kuwasaidia wananchi wetu. Ndiyo maana nimetoa maelekezo kwamba itakapofika mwezi wa Sita, Halmashauri yoyote ambayo Serikali imepeleka fedha lakini zile fedha zimeshindwa kununua dawa na vifaa tiba kuwasaidia wananchi, tutasema kwamba, ma-DMO wao hawatoshi katika maeneo yetu hayo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini suala la watumishi, japokuwa tatizo la watumishi ni tatizo kubwa sana, lakini ukiangalia katika mgawanyo wa Madaktari, Kigoma tumepeleka madaktari 10 lakini mikoa mingine imepata madaktari watano. Tunajua japokuwa Madaktari kumi wameenda katika Mkoa mzima wa Kigoma, bado hawatoshi, lakini tutakapokuja katika ajira mpya Mkoa wa Kigoma tutaupa kipaumbele. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba muelewe ndugu zangu, Kibondo pale kwa ndugu yangu Mheshimiwa Nditiye tumepeleka Madaktari watatu, Kasulu tumepeleka Madaktari wawili, halikadhalika Uvinza tumepeleka Madaktari na RAS Kigoma tumepeleka takribani Madaktari wanne. Lengo letu ni kuhakikisha Mkoa wa Kigoma na mikoa mingine ya pembeni iweze kupata…
Mheshimiwa Mwenyekiti, tutawapa kipaumbele watu wa Kigoma kupata Madaktari wa kutosha.
MHE. JOSEPHINE J. GENZABUKE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Namshukuru Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu yake mazuri lakini nina maswali mawili ya nyongeza.
Kwa kuwa wananchi wa Wilaya ya Kakonko kwa sasa wanapata huduma katika Kituo cha Afya cha Kakonko na kituo hicho kimezidiwa kwa sababu msongamano wa watu ni mkubwa. Kituo hicho kinahudumia wananchi kutoka hadi Mkoa jirani wa Kagera kwa maana ya wananchi wa Nyakanazi, Kalenge pia na wakimbizi kwa sababu katika Wilaya ile kuna kambi za wakimbizi, Waziri amesema kwamba mwaka 2017/2018 zimetengwa shilingi milioni 500.
Je, Waziri yupo tayari sasa kutokana na jinsi wananchi wanavyopata shida pamoja na waganga na wauguzi kwa sababu watu wakiwa wengi waganga nao wanachanganyikiwa, yupo tayari kufuatilia hizo shilingi milioni 500 ziweze kwenda mara moja Kakonko kwenda kuwasaidia wananchi? (Makofi)
Swali la pili; kwa wakati huu ambapo Wilaya ya Uvinza haina Hospitali ya Wilaya, wananchi wanapata huduma katika vituo vya afya na zahanati, lakini vituo hivyo vya afya pamoja na zahanati havina watumishi wa kutosha.
Je, katika mgao huu wa wafanyakazi ambao wataajiriwa kwa sasa, Serikali iko tayari kabisa kupeleka watumishi wengi wa kutosha kwenda kusaidia katika Wilaya ya Uvinza ambayo haina Hospitali ya Wilaya? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPH G. KAKUNDA): Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kumshukuru sana Mheshimiwa Genzabuke kwa jinsi ambavyo anafuatilia huduma hasa kwa wanawake katika Mkoa wa Kigoma.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika swali lake la kwanza, napenda kumthibitishia kwamba fedha hizo ambazo zimetengwa kwenye bajeti ya 2017/2018 nitazifuatilia na kuzisimimamia mimi mwenyewe binafsi kuhakikisha kwamba zimekwenda haraka.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika swali la pili, wiki hii iliyopita tumekamilisha upatikanaji wa watumishi 2,008 ambao sasa hivi wanaendelea kugawanywa katika Halmashauri mbalimbali. Leo hii nitahakikisha kwamba Halmashauri ya Wilaya ya Uvinza imepata watumishi wa kutosha angalau kwa mahitaji ya asilimia 50. (Makofi)
MHE. JOSEPHINE J. GENZABUKE: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru.
Mheshimiwa Naibu Spika, Wilaya ya Kakonko ni kati ya wilaya mpya na mpaka sasa Wilaya hiyo haina Hospitali ya Wilaya. Eneo hilo la Kakonko limepakana na Mkoa wa Kagera na wananchi wengi wanakuja kutibiwa katika Kituo cha Afya cha Kakonko kwa kuwa hawana hospitali jirani yao. Serikali iliahidi kupeleka shilingi milioni 500, mpaka sasa shilingi milioni 500 hizo hazijapelekwa katika Wilaya ya Kakonko. Nilitaka kujua, je, ni lini Serikali itapeleka milioni 500 ili wananchi wa Kakonko waweze kupata huduma ya matibabu? (Makofi)
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli Kakonko ni sehemu yenye changamoto kubwa na Mheshimiwa Mbunge nakumbuka hata tulivyokuwa kule kipindi kile tumeona idadi kubwa ya watu kutoka Burundi wakitibiwa pale katika kituo kile cha afya.
Ni kweli tumetenga shilingi milioni 500 na nimuhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba fedha zile zilikuwa zinaenda awamu kwa awamu. Ni imani yangu kwamba sasa hivi kwa muda huu ninapozungumza katika ile batch ya mwisho zitakuwa zimefika. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, ondoa hofu ndani ya kipindi hiki nina amini, lakini nita-cross check leo hii kwa nini hazijafika kwa sababu tumeshazitengea zile fedha ziende Kakonko kwa ajili ya uboreshaji wa kituo kile cha afya. (Makofi)
MHE. JOSEPHINE J. GENZABUKE: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi. Kwa kuwa vipo vikundi vya akina mama ambavyo vimeanzishwa na kuunda SACCOS, lakini halmashauri hawatoi pesa hiyo asilimia 10 kuvipatia vikundi hivyo na wakati vikundi hivyo havijaweza kukopeshwa na mabenki au taasisi mbalimbali za kifedha.Je, ni kwa nini sasa Serikali isiagize Halmashauri ili vikundi hivyo navyo vilivyoundwa kama SACCOS viweze kukopeshwa pesa hiyo? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. GEORGE J. KAKUNDA): Mheshimiwa Naibu Spika, namshukuru Mheshimiwa Genzambuke kwa kuzidi kuvijali vikundi vya SACCOS ambavyo vimeanzishwa kwenye Halmashauri nyingi hapa nchini ikiwemo Halmashauri ya Kasulu pale anakotoka.
Hili suala ni wazo zuri na mimi naomba sana sana badala ya kulijibu hapa haraka haraka tulichukue tukalifanyie kazi zaidi kwa sababu malengo Mfuko wa Vijana na Wanawake ni kukopesha wale vijana ambao wanajishughulisha na kazi za uzalishaji mali moja kwa moja. Sasa hili suala la kusema kwamba tuwakopeshe halafu na wao wakopeshane ni wazo jipya ambalo linahitaji kujadiliwa zaidi kitaalam ili tuweze kutoa maelekezo. Ahsante sana.

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU, SERA, BUNGE, KAZI, VIJANA, AJIRA NA WALEMAVU: Mheshimiwa Naibu Spika nakushukuru. Pamoja na majibu mazuri sana yaliyotolewa na Mheshimiwa Naibu Waziri, naomba tu niliarifu tu Bunge lako Tukufu kwamba pamoja na kuendelea kulifanyia kazi jambo hili naomba kuendelea kuwakumbusha Waheshimiwa Wabunge kuwa katika kutoa mikopo kwa vijana kupitia Mfuko wa Vijana wa asilimia tano, zile zinazotengeneza asilimia 10 kwenye Halmashauri tayari Serikali ilishagiza vijana kupitia halmashauri zao waunde SACCOS za vijana ili waweze kunufaika na mikopo hiyo na kupitia kwenye hizo SACCOS waweze kujikopesha na mikopo hiyo iwe revolving. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, hata hivyo pamoja na vijana ni lazima pia kuwaangalia na akina mama. Serikali kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu na hasa Baraza la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi limeanza kuweka mkakati maalum wa kuhakikisha linafikia vikundi vya VICOBA na SACCOS za wanawake na vijana katika nchi nzima ya Tanzania. Nimuombe sana Mheshimiwa Genzabuke, kwa kuwa kupitia Baraza la Taifa la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi tuna mifuko takribani 17 ya kuwawezesha wananchi Mheshimiwa Genzabuke awasiliane na mimi tuwaelekeze akina mama hawa wa Kigoma wanaweza wakasaidiwaje. (Makofi)
MHE. JOSEPHINE J. GENZABUKE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, kwanza naipongeza Serikali kwa kubadilisha utaratibu wa awali kwa sababu utaratibu wa awali wakulima waikuwa hawanufaiki. Nina maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa msimu wa mvua katika maeneo mbalimbali hapa nchini unatofautiana, kwa mfano, katika Mkoa wa Kigoma mvua za kupandia ni za mwezi wa Oktoba. Je, Serikali iko tayari sasa kuhakikisha mbolea inawafikia wakulima mapema zaidi kuliko ilivyo sasa? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa, wapo mawakala waliofanya kazi kubwa ya kusambaza mbolea kwa wakulima. Na kati ya mawakala hao wapo waliofanya kazi kwa uadilifu mkubwa na uaminifu, lakini wapo ambao hawakuwa waaminifu na Serikali ilituma watu kwenda kuhakiki madeni kwa mawakala hao nchi nzima.
Je, ni lini Serikali itawalipa mawakala waliofanya kazi kwa uadilifu, ili waweze kulipa madeni waliyokopa katika benki mbalimbali, wakiwemo mawakala wanawake ambao wanateseka sana kudai pesa zao? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, VIJANA NA AJIRA: Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza la kuhusu utofauti wa misimu ya mvua na mbolea kuwafikia wakulima kwa wakati.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimuondoe hofu tu Mheshimiwa Mbunge ya kwamba Wizara ya Kilimo inatambua kwamba pembejeo ya mbolea ni kati ya virutubisho muhimu sana, ili kumfanya mkulima wa Kitanzania aweze kulima kilimo cha tija. Sasa katika mpango wa Wizara ni kuhakikisha kwamba katika mfumo huu mpya ambao tunakwenda nao wa bulk procurement mbolea hizi ziweze kuwafikia wakulima kwa wakati, ili waweze kutumia kwa ajili ya kilimo chao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, na kwa sababu ya Maputo Declaration ya mwaka 2003 ambayo katika Ukanda wa Nchi za Kusini mwa Afrika imesema kwamba Tanzania ni kati ya nchi ambazo zinatumia kiwango kidogo cha virutubisho kwa hekta moja ambayo kwa mujibu wa Declaration hii inapaswa kila hekta moja vitumike virutubisho kilo 50 na sisi tupo katika kilo 19. Kwa hiyo, kwa kuona umuhimu huo Serikali sasa itahakikisha kwamba, mbolea hii inawafikia wakulima kwa wakati, ili waweze kulima kilimo cha tija.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali lake la pili amezungumza kuhusu uhakiki wa malipo ya mawakala.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama alivyosema Waziri wa Kilimo wakati wa bajeti yake ni kweli, wako mawakala ambao walifanya kazi hii kwa uaminifu, lakini ambao bado hawajalipwa malipo yao. Tayari Mheshimiwa Waziri Mkuu ameshaiagiza Wizara ya Fedha na Mipango kufanya uhakiki kwa Mikoa yote 26, isipokuwa Dar es Salaam peke yake ili ndani ya mwezi mmoja mawakala hawa ambao walisambaza pembejeo waweze kulipwa pesa zao. (Makofi)
MHE. JOSEPHINE J. GENZABUKE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Naomba kuuliza swali moja, Mkoa wa Kigoma Wilaya Tano zinapakana na nchi jirani ya Burundi na kati ya Wilaya hizo zina vijiji ambavyo vimepakana kabisa na nchi ya Burundi na wakati mwingine zinapata mawasiliano kutoka Burundi. Je, ni lini Serikali itakaa na makampuni ili kuweza kupeleka minara katika vijiji vya Kalalangabo, Mtanga na Kiziga? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Mwenyekiti, Vijiji hivyo vya Kalalangabo namshukuru amenitajia hapa nimhakikishie tu kwamba katika zabuni itakayofuata ambayo mkazo mkubwa ni katika maeneo ya mpakani na zabuni inayofuata ni ya mwezi wa 10, vijiji hivyo tutavifikiria. (Makofi)
MHE. JOSEPHINE J. GENZABUKE: Mheshimiwa Spika, ahsante. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, nina maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Spika, katika Hospitali ya Wilaya ya Kasulu kuna upungufu mkubwa wa Madaktari na Wauguzi, Muuguzi mmoja anahudumia wodi moja akiwa peke yake hali inayosababisha azidiwe na shughuli. Wagonjwa wanawalalamikia Wauguzi kwamba hawawahudumii lakini ni kutokana na kuzidiwa na kazi nyingi. Je, ni lini Serikali itapeleka Waganga na Wauguzi ili kumaliza tatizo liliko katika Wilaya ya Kasulu? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, swali langu la pili, katika Mkoa wa Kigoma kuna kambi tatu za wakimbizi. Wilaya ya Kasulu kuna Kambi ya Nyarugusu, Wilaya ya Kakonko kuna Kambi ya Mtendeli na Wilaya ya Kibondo kuna Kambi ya Nduta. Wagonjwa wanapozidiwa katika kambi mbili ya Mtendeli na Nduta katika Wilaya ya Kibondo na Kakonko, wale wa Nduta hupelekwa katika Hospitali ya Wilaya ya Kibondo na wale wa Mtendeli hupelekwa katika Kituo cha Afya cha Kakonko. Je, ni lini Serikali, kwanza, itapeleka pesa za kumalizia Hospitali ya Wilaya katika Wilaya ya Kakonko na kupeleka Wauguzi na Madaktari? Pili, katika Wilaya ya Kakonko ni lini nao watapelekewa Waganga na Wauguzi wa kutosha ili kumaliza matatizo yaliyopo katika hospitali hiyo? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE) :
Mheshimiwa Spika, katika jibu langu la msingi nimekiri upungufu wa waganga pamoja na watumishi wa afya kwa ujumla wake. Pia nimeeleza jinsi ambavyo katika bajeti ya 2018/2019 walivyoomba kupatiwa Waganga 1,667.
Mheshimiwa Spika, lakini ni nia njema ya Serikali ya kuhakikisha kwamba huduma ya afya inatolewa. Nimepata nafasi ya kwenda Kasulu na tatizo ambalo nimekutana nalo pale Kasulu ni pamoja na kutokuwepo vituo vya afya vya jirani ili hospitali ya wilaya iwe na sehemu ya kupumulia. Katika utaratibu mzima wa Serikali wa kuhakikisha kwamba huduma ya afya inapatikana ya kutosha. Miongoni mwa wilaya 67 ambazo zinaenda kupata hospitali za wilaya, Wilaya za Kigoma zitakuwepo ikiwa ni pamoja Uvinza, Buhigwe pamoja na Kasulu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kama hiyo haitoshi, Kakonko kuna Kituo cha Afya kinaitwa Gwamanumbu na Lusesa nao wanaenda kupata kituo cha afya ambacho kina hadhi ya kuweza kufanya operesheni. Hii yote kwa ujumla wake unaona jinsi ambavyo Serikali ina nia njema ya kuhakikisha kwamba afya kama jambo la msingi linaenda kupatiwa ufumbuzi.
Mheshimiwa Spika, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge, Waziri wa Utumishi na Utawala bajeti yake imesomwa jana na sisi TAMISEMI pamoja na uhitaji wetu kibali cha ajira tunapata kutoka kwao. Naamini katika maombi haya ya wahudumu pamoja na Waganga 1,667 tutapata wa kutosha na tutaenda kupunguza huo uhaba wa watumishi.
Mheshimiwa Spika, yeye mwenyewe ni shuhuda kwamba kuna mashirika ambayo yamekuwa yakishirikiana na Serikali kwa sababu suala la wakimbizi huwezi uka-predict kwamba watakuja wangapi. Naamini kwa ushirikiano ambao umekuwa ukioneshwa hakika huduma ya afya itaenda kuboreshwa na tatizo hili litapungua.
MHE. JOSEPHINE J. GENZABUKE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru na swali moja la nyongeza. Mji wa Kibondo unakaabiliwa na tatizo kubwa la ukosefu wa maji, na mji huo uko kilimani. Pampu zinazosukuma maji kusambaza ndani ya mji wa Kibondo zimechakaa, ni lini Serikali itapeleka pesa kwa ajili ya mradi wa maji Wilayani Kibondo?
WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali moja la Mheshimiwa Mbunge Genzabuke kuhusiana na matatizo ya maji ya Kibondo, kwanza Mheshimiwa Genzabuke pamoja na wananchi wa Jimbo la Kibondo nikufahamishe tu kwamba tayari tunasaini mkataba wa mkopo wa fedha nafuu kutoka Serikali ya India na katika ya fedha hizo sehemu ya fedha itashughulikia utoaji wa maji, huduma ya maji katika mji wa Kibondo, kwa hiyo sasa hivi vuta subira mambo baada ya muda mfupi yatakuwa mazuri. (Makofi)
MHE. JOSEPHINE J. GENZABUKE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Katika Mkoa wa Kigoma ipo NGO ambayo imezunguka kwa muda wa wiki mbili katika Wilaya zote saba ikiwatoza wanawake shilingi 10,000 na kuwapigisha picha kwa kuwaahidi kwamba Serikali itatoa mikopo kupitia Mfuko wa Makamu wa Rais, Mheshimiwa Samia Suluhu. Ninataka Serikali inieleze, je, mpango huo wa kutoa pesa kupitia Mfuko wa Mama Samia upo? (Makofi)
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU, SERA, BUNGE, KAZI, AJIRA, VIJANA NA WENYE ULEMAVU: Mheshimiwa Mwenyekiti, shughuli zote za uwezeshaji wananchi kiuchumi katika nchi yetu ya Tanzania zinasimamiwa na Sera ya mwaka 2004 na Sheria ya Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi ya mwaka 2004 ambayo inaruhusu uanzishwaji wa taasisi mbalimbali kisheria.
Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa kuhusu taasisi hiyo zilishapatikana ndani ya Serikali na Ofisi ya Makamu wa Rais ilishatoa tamko la kuikana taasisi hiyo kwamba haihusiki nayo. Ninaomba nichukue nafasi hii kuagiza uongozi wa mkoa wa Kigoma kuifuatilia taasisi hiyo na kuikana na kuipa maelekezo kwamba Ofisi ya Makamu wa Rais haihusiki na jambo hilo. Kama wanaendesha shughuli hizo kwa kutumia sheria na taratibu nyingine, wanapaswa kujieleza kwa kutumia sheria na taratibu nyingine walizozifuata, lakini siyo Ofisi ya Makamu wa Rais. Kama wataendelea kuwadanganya wananchi kwa kutumia Ofisi ya Makamu wa Rais, Serikali haitasita kuchukua hatua kali dhidi ya taasisi hiyo. (Makofi)
MHE. JOSEPHINE J. GENZABUKE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Katika Wilaya ya Kakonko takribani kata sita zimepakana na nchi ya Burundi na Kata ya Lugenge na Kasuga nazo pia zimepakana na maeneo hayo ambayo hayana mawasiliano kwa njia ya simu. Mawasiliano ni hafifu na ni shida kabisa, nataka kujua, ni lini Serikali itapeleka minara katika maeneo hayo kiusalama kwa sababu maeneo hayo yamekaribiana na nchi ya Burundi? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nichukue nafasi nikupongeze Mheshimiwa Mbunge kwa sababu kuna mambo mengi kweli unafuatilia katika maeneo haya. Ni kweli maeneo haya yaliyo mpakani yana usumbufu mkubwa hii ni pamoja na mwingiliano kwa sababu niwahi kutembelea maeneo haya utaona kabisa kwamba tunapata mawasiliano kutoka nchi za jirani. Tutahakikisha tu Mheshimiwa Mbunge tunajenga minara ili pia iweze kupunguza ule mwingiliano wa mawasiliano ambayo yanatokea nchi za jirani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nikuombe pia tuwasiliane nina orodha ndefu hapa ili tuje tuone maeneo haya kama hatujaya-cover basi tuendelee kupeleka minara mingine.
MHE. JOSEPHINE J. GENZABUKE: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri nina maswali mawili ya nyongeza. Kwa kuwa zaidi ya wafungwa katika Gereza la Kasulu ni wakimbizi hali inayochangia gereza hilo kubeba mzigo mkubwa. Je, Serikali iko tayari kukaa na Shirika la UNHCR ili iweze kuchangia pesa katika Gereza la Kasulu?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali langu la pili; kwa kuwa miongoni mwa huduma nyingine za wafungwa ni pamoja na usafiri; na kwa kuwa gereza la Kasulu ninakabiliwa na ukosefu mkubwa wa gari la kubebea mizigo, lori la kusombea vitu mbalimbali ikiwa ni pamoja na kuni za kupikia chakula; je, ni lini Serikali itapeleka pesa kwa ajili ya kununua gari kwa ajili ya gereza la Kasulu? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI:
Mheshimiwa Naibu Spika, nataka nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba UNHCR wamekuwa wakishirikiana na Serikali katika kukabiliana na changamoto mbalimbali za wakimbizi, lakini hata na wananchi ambao wanazunguka maeneo husika. Kwa hiyo hili jambo tunalolifanya si jambo ambalo linalotakiwa lianze sasa hivi.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusiana na suala la gari tuna changamoto kubwa sana ya uhaba wa magari katika Jeshi la Magereza, kwa hiyo kwa sasa hivi siwezi kutoa ahadi yoyote kwa sababu gari hizo hazipo; lakini zikapopatikana nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba tunachukua changamoto yake kama moja ya vipaumbele.
MHE. JOSEPHINE J. GENZABUKE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Pamoja na majibu ya Mheshimiwa Naibu Waziri, sijaridhika sana, nina maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kutokana na athari kubwa sana zilizoletwa na ujio wa wakimbizi Mkoani Kigoma, ongezeko la watu, miundombinu isiyotosheleza, ni lini hasa mpango kabambe utaletwa? Naomba commitment ya Serikali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu la pili, ujio wa wakimbizi ndani ya Mkoa wa Kigoma, Makambi ya Wakimbizi ya Kibondo, Kasulu na Kakonko yamesababisha uharibifu mkubwa wa mazingira; je, Serikali inalijua hilo? Ni mikakati gani ya Serikali katika kusaidia Mkoa wa Kigoma kutokana na athari hizo?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI:
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali lake la kwanza naona halijawa wazi zaidi, lakini kwa nilivyolielewa, ameuliza kuna mpango gani kabambe? Nadhani alikusudia mipango ambayo Serikali inafanya kwa kushirikiana na Jumuiya za Kimataifa katika kuhakikisha kwamba shughuli na huduma za maendeleo katika jamii, wananchi ambao wanazunguka makambi yale wanafaidika. Kama hivyo ndiyo, basi nataka nimhakikishie Mheshimwa Mbunge kwamba kuna miradi mingi ambayo imeshatekelezwa kwa kushirikiana na Serikali na mashirika haya ya kimataifa chini ya UNHCR katika kuboresha huduma za jamii katika maeneo husika, kama ambavyo nimezungumza katika sekta ya afya, masoko, maji, elimu na kadhalika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali lake la pili kuhusiana na mazingira, ni kweli nakubaliana na Mheshimiwa Mbunge kwamba ujio wa wakimbizi katika Mkoa wa Kigoma kwenye makambi yetu umeleta athari kwenye eneo la mazingira. Kwa kutambua hilo, ndiyo maana Serikali imechukua jitihada mbalimbali ili kuhakikisha kwamba inakabiliana na changamoto hiyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, moja katika mambo ambayo tumefanya, kwanza ni matumizi ya majiko ambayo wanaita majiko ya ubunifu, ambayo sasa hivi badala ya kutumia kuni kukata miti ovyo, aina ya upikaji na uandaaji wa chakula kwa wakimbizi umebadilika kwa kutumia teknolojia ambazo zinapunguza athari kwa mazingira.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hali kadhalika ukataji miti ambapo fito zilikuwa zikitumika kwa ajili ya ujenzi wa nyumba, umepungua kwa kiasi kikubwa. Sasa hivi nyumba ambazo zinajengwa ni za kudumu kwa kutumia matofali, pamoja na kutoa elimu kwa wakimbizi na jamii husika juu ya umuhimu wa kuweza kudhibiti mazingira.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, hayo ni miongoni mwa mambo ambayo Serikali imekuwa ikifanya kuhakikisha kwamba athari ya mazingira inapatiwa ufumbuzi katika maeneo hayo ambayo yana makambi ya wakimbizi.
MHE. JOSEPHINE J. GENZABUKE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Kwa muda mrefu sana katika Wilaya ya Kasulu, eneo la Kagera Nkanda wananchi walikuwa wakizuiliwa kulima. Mwaka jana tarehe 21 Mheshimiwa Rais alipokuja Wilaya ya Kasulu wananchi walimpokea kwa nderemo na vigelegele akawaruhusu kwenda kulima katika pori la Kagera Nkanda, lakini hivi sasa ninavyoongea tarehe 21 mwezi huu, wananchi wameambiwa waondoe mazao katika eneo hilo la Kagera Nkanda.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka kauli ya Serikali, ni kwa nini wananchi waliruhusiwa na Mheshimiwa Rais kulima katika eneo hilo na leo wanaondolewa kwa kutaka kupigwa ndani ya wiki moja? Naomba kauli ya Serikali. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kwamba Mheshimiwa Rais alitoa maagizo kwamba lile eneo ligawiwe kwa wananchi ili waweze kulitumia katika shughuli zingine za kibinadamu za uzalishaji. Naomba nimhakikishie tu kwamba agizo la Mheshimiwa Rais alilolitoa linatekelezeka na lazima liheshimike, kama kuna mtu analikiuka hilo tutashughulika nae. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kikubwa ambacho kinatakiwa sasa hivi kufanyika ni kuhakikisha kwamba baada ya Rais kutoa lile eneo, taratibu za kisheria ya kuondoa na kuweka mipaka mipya lazima zifanyike. Kwa hiyo, wale Watendaji ambacho tunakifanya sasa hivi ni kuhakikisha kwamba sasa tunarekebisha ile mipaka, ili kusudi yale maeneo yaliyogawiwa kwa wananchi yabaki kwa wananchi na yale mengine ambayo yanatakiwa kubaki kama hifadhi yaendelee kubaki kama hifadhi.
MHE. JOSEPHINE J. GENZABUKE: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi. Kabla ya kuuliza swali naomba uniruhusu niwape pole wananchi wa Jimbo la Buyungu kwa kupoteza Mbunge wao. Naomba wawe watulivu katika kipindi hiki kigumu.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika Mji wa Kakonko bado lipo tatizo kubwa la upatikanaji wa maji. Katika mji huo maji hutoka mara tatu kwa wiki katika visima viwili; kimoja ni kisima cha Mbizi ambacho kinatumia pampu na cha pili ni kisima cha Kanyovi kinachotumia solar. Nashukuru Serikali katika bajeti hii kwa kutupangia pesa. Je, ni lini sasa mradi huo utaanza katika Mji wa Kakonko? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI:
Mheshimiwa Naibu Spika, nampongeza Mheshimiwa Mbunge kwa namna ya kipekee anavyowapigania wananchi wake katika suala zima la maji. Nitumie nafasi hii kulishukuru sana Bunge lako Tukufu kwa kutuidhinishia kiasi cha Sh.727,345,000,000 yote hii katika kuhakikisha tunaenda kutatua tatizo la maji.
Mheshimiwa Naibu Spika, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge, baada ya bajeti hii kuu kupitishwa sisi kama Wizara ya Maji hatutakuwa kikwazo katika kuhakikisha wananchi wake wanapata maji. (Makofi)
MHE. JOSEPHINE J. GENZABUKE: Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, nina maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza; katika Kata ya Mwilamvya ndipo yalipo machinjio ya ng’ombe, mbuzi na kondoo. Eneo hilo hupata maji mara mbili kwa wiki au mara tatu, lakini hivi sasa ninavyoongea eneo hilo halina maji na ni muda wa mwezi mzima maji hayapatikani katika eneo hilo.
Je, Serikali iko tayari kutoa pesa kwa mpango wa dharura ili eneo hilo la machinjio liweze kupatiwa maji? (Makofi)
Swali langu la pili, katika Halmashauri ya Wilaya ya Kasulu DC ipo miradi ya maji ambayo haijakamilika, imefikia asilimia 85 mpaka 95 lakini imekwama kwa ajili ya ukosefu wa pesa; je, ni lini sasa Serikali itamalizia miradi hiyo kwa kupeleka pesa ili miradi hiyo iweze kukamilika na wanawake waweze kuondolewa adha ya upatikanaji wa maji? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI:
Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Awali ya yote nampongeza sana Mheshimiwa Mbunge, ni mama shupavu, jasiri, mfuatiliaji na mhangaikaji wa matatizo ya wananchi wa Kigoma hasa katika suala zima la maji.
Mheshimiwa Naibu Spika, sisi kama Wizara ya Maji hatutakuwa kikwazo kwa wananchi wako wa Mwilamvya hususan katika eneo hilo la Machinjio katika kuhakikisha wanapata maji safi ili waendelee na usafi, wakati mwingine usafi ni uhai wa mwanadamu.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali lake la pili kuhusu suala zima la miradi ambayo haijakamilika, nitumie nafasi hii kulishukuru Bunge lako tukufu na wewe mwenyewe kwa Wizara yetu ya Maji kuidhinishiwa fedha na katika Mji huo wa Kasulu umetengewa kiasi cha shilingi 1,466,000,000.
Mheshimiwa Naibu Spika, namwomba Mheshimiwa Mbunge kwa kushirikiana na sisi Wizara na viongozi katika kuhakikisha tunasimamia fedha zile ili ziende zikamilishe miradi ambayo haijakamilika ili wananchi wake waweze kupata maji, salama na yenye kuwatosheleza.
MHE. JOSEPHINE J. GENZABUKE: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Pamoja na majibu maswali mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, nina maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza, kabla ya kuuliza swali langu, naomba nichukue nafasi hii kupongeza Halmashauri ya Kusulu TC kwa kuweza kufanya vizuri kwa kutoa pesa hizo kila baada ya miezi mitatu.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali langu la kwanza, kwa kuwa wanawake wengi, vijana pamoja na walemavu wameweza kuhamasika kufungua vikundi lakini zipo Halmashauri ambazo zinasuasua na nyingine kutokupeleka pesa hizo kama sheria inavyotaka. Je, Wizara iko tayari sasa kutoa agizo ili Halmashauri hizo ziweze kutoa pesa kwa wakati?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, zipo Halmashauri ambazo bado ni changa mfano Halmashauri ya Kakonko pamoja na Buhigwe, makusanyo yao sio mazuri sana, ni kidogo. Je, Serikali inatoa kauli gani kwa kuzisaidia Halmashauri hizo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. MWITA M. WAITARA): Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Naomba nijibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Josephine, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza naomba nimpongeze Mheshimiwa Mbunge wa Viti Maalum kwa kujali wanawake na kuwasemea ili waweze kupata mikopo na kujikwamua kiuchumi. Hii kazi inafanywa na Wabunge wote wa Viti Maalum kama nilivyosema jana.

Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli wakati wa bajeti bahati nzuri nimehudhuria kikao cha Kamati ya Utawala wa TAMISEMI, naomba niwapongeze wajumbe wakiongozwa na Mwenyekiti, Mheshimiwa Rweikiza kwa kazi nzuri waliyofanya katika mjadala ule. Kila Mkoa, Halmashauri, Mkurugenzi, Katibu Tawala alihojiwa na kutoa maelezo namna ambavyo amesimamia ukusanyaji wa fedha na kupeleka kwenye vikundi.

Mheshimiwa Naibu Spika, hii hoja ya kusuasua kutokupeleka fedha ni jambo la kisheria na maagizo yametoka naomba nirudie, Wakurugenzi, Wakuu wa Mikoa na Makatibu Tawala kwa maelekezo ya Kamati ya Utawala na TAMISEMI kwa mwaka wa fedha ujao kama kuna mtu atakuwa hajapeleka fedha hizi kikamilifu na kusimamia marejesho hali yake itakuwa mbaya sana. Haya ni maagizo ya Kamati na sisi kama Wizara tumeyachukua.

Mheshimiwa Naibu Spika, la pili, maelekezo ni kwamba hakuna Halmashauri changa katika jambo hili, kama umekusanya Sh.100 umetoa makato yale ambayo ni ya msingi na makato mbalimbali ambapo yametolewa kwenye Halmashauri inayobaki 10% yake peleka kwenye vikundi vya vijana, wanawake na watu wenye ulemavu. Kwa hiyo, hata kama utakuwa umekusanya Sh.5, ondoa makato yote ya msingi ambayo yameelekezwa na Serikali inayobaki 10% peleka, usipopeleka sheria itachukua mkondo wake.
MHE. JOSEPHINE J. GENZABUKE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Tarehe 10 Agosti, 2018, Waziri wa Nishati alizindua mradi wa REA III katika Mkoa wa Kigoma katika Kijiji cha Lusesa, Kata ya Lusesa na akaahidi kwamba baada ya mwezi mmoja umeme utawaka katika kata hiyo na viunga vyake vinavyozunguka kata hiyo, lakini mpaka leo umeme haujawaka. Nataka nijue ni lini Serikali itaagiza wanaohusika na umeme waweze kuwasha umeme katika kata hiyo?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la dada yangu Mheshimiwa Josephine Genzabuke kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, nimpongeze kwa kweli kwa kazi kama Mbunge wa Viti Maalum kufuatilia masuala ya sekta ya nishati mkoani kwake. lakini kama ambavyo amesema uzinduzi katika Kata ya Lusesa ulifanyika mwaka 2018 mwezi Agosti, ni wazi kabisa kulikuwa na changamoto ya mkandarasi katika Mikoa ya Kigoma na Katavi na niwashukuru Wabunge wa mikoa hiyo pamoja na wananchi kwa subira yao namna ambavyo waliliridhia. Hata hivyo, nataka niseme mkandarasi huyu wa CCCE Etern anaendelea na kazi. Hata hivi karibu Mheshimiwa Waziri amewasha vijiji kama vitatu katika Wilaya ya kibondo.

Kwa kuwa Mheshimiwa Mbunge amesema katika Kata ya Lusesa ambapo imezinduliwa na ahadi ilitolewa na kwamba mpaka sasa hivi bado vijiji vya Kata hiyo ya Lusesa havijawashwa, naomba nilichukue ili niwasiliane na Meneja wa TANESCO wa Mkoa wa Kigoma pamoja na mkandarasi, kwa vile uzinduzi ulifanyika kwa kata hii na ni wazi lazima ilikuwa kazi ifanyike kwa haraka na umeme uwake, pamoja na kwamba mkandarasi hana muda mrefu.

Kwa hiyo nitoe maelekezo kwamba agizo la Mheshimiwa Waziri litekelezwe katika Kata hii ya Lusesa, vijiji hivyo ambavyo vimeanishwa viwashwe na nimwahidi Mheshimiwa Mbunge, baada ya hili Bunge la Bajeti, tutafanya naye ziara katika Mkoa wa Kigoma. Ahsante sana.
MHE. JOSEPHINE J. GENZABUKE: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, nina swali moja la nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika Wilaya hizo nilizozitaja, vipo vijiji ambavyo ukipiga simu mawasiliano unayoyapata ni ya nchi jirani ya Burundi siyo Tanzania. Kwa mfano, katika Wilaya ya Kakonko ipo Kata ya Mgunzu, kipo Kijiji cha Kigra na Chulazo ambavyo mawasiliano yake ni ya shida. Hata katika wilaya nilizozitaja viko vijiji ambavyo havikuweza kutajwa kwenye jibu la Waziri ambavyo mawasiliano yake bado ya wasiwasi. Je, Serikali iko tayari kuendelea kuhamasisha makampuni kujenga minara katika maeneo hayo ili wananchi waweze kupata mawasiliano ya uhakikika?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ENG. ATASHASTA J. NDITIYE): Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali moja la nyongeza Mheshimiwa Josephine Gezabuke, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, awali ya yote kwanza nimpongeze sana Mheshimiwa Josephine Gezabuke kwa jinsi anavyopambana kuhakikisha kwamba wananchi katika maeneo mbalimbali hasa ya Mkoa wa Kigoma na maeneo mengine ambayo yapo mpakani ya nchi yetu yanapata mawasiliano ya uhakika bila muingiliano kutoka nchi nyingine za jirani. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini kwa kujibu swali lake, Serikali kupitia Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) tumeendelea kuwasiliana na nchi jirani ili sheria iliyowekwa kutokana na Mkataba wa East Africa Communication uwe unaweza kutekelezwa vizuri. Utaratibu unataka mnara wa mawasiliano uwekwe kilometa 5 toka eneo la mpaka kwa kila nchi ili wananchi wanaohusika waweze kupata mawasiliano kutoka nchi husika lakini kuna maeneo ambayo kwa nchi za wenzetu wamekiuka utaratibu huo. Katika kikao kinachotegemewa kukaa mwezi Februari, 2020 tunategemea East African Communication wata-resolve suala hilo kwa sababu kuanzia Julai limekuwa likijadiliwa ili kuhakikisha wananchi ambao wanapaswa kupata mawasiliano ya nchi husika wanaendelea kupata bila kuingiliana na watu wengine. Hilo linahusu vilevile na muingiliano wa masuala ya redio. Ahsante.
MHE. JOSEPHINE J. GENZABUKE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Kwa kuwa Serikali imeamua zao la mchikichi lilimwe Kigoma na liweze kuwa zao la biashara na Waziri Mkuu kwa kuweka msisitizo ameenda Kigoma mara tatu kufuatilia zao hili la mchikichi; na kwa kuwa wananchi wameamua kuitikia mwito huo wa kulima zao hilo…

MWENYEKITI: Swali.

MHE. JOSEPHINE J. GENZABUKE: Mheshimiwa Mwenyekiti, je, Serikali iko tayari sasa kuhakikisha wananchi wanapata mbegu na kuanza kulima zao hilo?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO (MHE. OMARY T. MGUMBA): Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Genzabuke, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali tuko tayari kwa ajili ya uzalishaji wa miche ya michikichi na kuigawa kwa wakulima. Sasa hivi tumeshatenga zaidi ya shilingi bilioni 5 kwa ajili ya kuanza uzalishaji mwaka huu na mwaka huu mwezi Septemba, miche zaidi ya milioni moja itakwenda sokoni. Tumeshaingia mkataba na sekta binafsi kuzalisha miche milioni tano kwa msimu huu unaokuja na ndani ya miaka mitatu tunategemea kuzalisha miche zaidi ya milioni 20 na kuigawa Tanzania nzima.
MHE. JOSEPHINE J. GENZABUKE: Mheshimiwa Spika, ahsante. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, nina maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Spika, kwa kuwa muda wa miradi hiyo kutokukamilika umekuwa mrefu sana, je, Serikali iko tayari kupeleka pesa ya kutosha ili miradi hiyo iweze kukamilika?

Mheshimiwa Spika, swali langu la pili; kwa kuwa Makao Makuu ya Wilaya za Kibondo na Kakonko upatikanaji wa maji umekuwa ni wa kusuasua, na wilaya hizo zina watu wengi kutokana na ongezeko la watu wengi wakiwemo wakimbizi, na zipo taasisi nyingi ambazo ziko pale zikiwemo hospitali, shule pamoja na ofisi za mashirika ya wakimbizi. Ni lini sasa Serikali itapeleka pesa katika Wilaya za Kakonko na Kibondo kumaliza tatizo la maji katika miji hiyo mikuu ya wilaya hizo? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Spika, kwanza naomba kutumia nafasi hii kumpongeza Mheshimiwa Mbunge kwa juhudi zake kubwa za kuhakikisha kwamba anapigania akinamama wa Wilaya za Kakonko na Kibondo waweze kupata maji safi na salama na yenye kutosheleza.

Mheshimiwa Spika, katika jibu langu la msingi nimesema kwamba Serikali itatoa pesa ili iweze kukamilisha mradi ambao ulikuwa umekwama na tayari kazi hiyo imekwishafanyika, na sasa hivi Wizara inakamilisha taratibu ili kazi ambayo ilikuwa inasababisaha miradi hiyo isikamilike iweze kukamilika.

Mheshimiwa Spika, katika swali lake la pili, naomba kumfahamisha kwamba katika Wilaya ya Kibondo, tayari Serikali ilipeleka pesa shilingi milioni 500 kwa ajili ya mradi wa maji, na katika Wilaya ya Kakonko taratibu zinaendelea ili waweze kupatiwa pesa kwa ajili ya kukamilisha, tunafahamu kwamba eneo hili lina watu wengi, na hasa wakimbizi kama alivyosema.
MHE. JOSEPHINE J. GENZABUKE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante, barabara ya kutoka Uvinza kuelekea kwenye Daraja la Kikwete - Malagarasi, barabara hii iliahidiwa kujengwa kwa pesa za kutoka Abu Dhabi. Nataka Serikali iniambie ni lini sasa kipande hiki cha kilometa 48 kitakamilika?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa Spika, ni kweli kwanza nikupongeze Mheshimiwa Genzabuke kwa sababu unafahamu na unafuatilia sana juu ya barabara hii na ni faraja kwa wakazi wa Kigoma na Tabora na wananchi wengine kwa ujumla kwamba hii barabara muhimu kutoka Tabora kwenda Kigoma sasa maeneo yote pamoja na hili eneo yameshapata mkandarasi kwa maana ya ujenzi, kwa maana hiyo zile taratibu za kimanunuzi zilikuwa zimekamilishwa na kweli tumepata fedha kutoka Abu Dhabi na pia tumeonyesha kwenye bajeti Mheshimiwa Mbunge anafahamu kwamba tumeonesha kwamba ujenzi unakwenda kuanza.

Kwa hiyo vuta tu subira zile taratibu za kimanunuzi zinaendelea vizuri na nikuhakikishie muda siyo mrefu utaona mkandarasi yuko site anaendelea na ujenzi katika eneo hili la Uvinza-Malagarasi kilometa 48 ambazo Mheshimiwa Mbunge unafahamu na umeizungumza hapa.
MHE. JOSEPHINE J. GENZABUKE: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana. Nina swali moja la nyongeza; katika halmashauri zetu zipo SACCOS za vijana na wanawake ambazo zimeundwa na wanawake na vijana, lakini SACCOS hizo hazikopeshwi kupitia Mifuko ya Halmashauri. Sasa, ni lini Serikali italeta sheria Bungeni ili SACCOS hizo za vijana na wanawake ziweze kukopesheka kupitia Mfuko wa Halmashauri?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Naibu Spika naomba kujibu mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Josephine Genzabuke, Mbunge Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika kuhusiana na SACCOS za vijana na wanawake kutokopesha kupitia halmashauri na wazo lake ni lini Serikali italeta sheria ili utaratibu huu uweze kutendeka, naomba nichukue wazo la Mheshimiwa Mbunge, tukalifanyie tathmini kama Serikali na kuona uwezekano wa kutekeleza jambo hili na kuona faida zake na changamoto zake ili tuweze kufanya maamuzi stahiki.
MHE. JOSOPHINE J. GENZABUKE: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi ili niulize swali la nyongeza. Pamoja majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, nina swali moja la nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, wakulima wetu wakiwemo wanawake na vijana wanatumia nguvu nyingi, wanatumia muda mwingi, lakini pia wanatumia pembejeo ambazo wanakuwa wamezikopa kwenye vikundi mbalimbali. Wanakopa pesa, wananunua mbolea na dawa; na wanapokuwa wamelima na wamevuna wanakosa soko hatimaye wanashindwa kulipa madeni pale walipo kopa pesa.

Je, Serikali ina mpango gani na inachukua hatua gani kuwa inauza mazao nje ya nchi? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo naomba kujibu swali la Mheshimiwa Genzabuke, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali ni mmoja tu kati ya wanunuzi na sisi kama Wizara tumekuwa tukichukua hatua mbalimbali kwa ajili ya kusaidia Serikali yenyewe ama taasisi, ama wafanyabiashara wa Kitanzania kuuza mazao yetu nje ya nchi. Miongoni mwa hatua kama taasisi za Serikali, mfano Bodi yetu ya Mazao Mchanganyiko sasa hivi inaanza utaratibu wa kufungua mawakala katika nchi za Kongo, DRC na vilevile katika nchi ya Kenya kwa ajili ya kuuza mazao yetu moja kwa moja kupitia mawakala wa upande huo.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini hatua nyingine ambayo tunachukua kama Serikali, ili kuhakikisha wakulima wanapata soko la uhakika ni kuzijengea uwezo taasisi zetu kwa maana ya NFRA na CPB na ndio maana nimesema katika jibu langu la msingi kwamba, sasahivi tuna mazungumzo na wenzetu wa hazina, ili kuruhusu taasisi zetu hizi mbili ziweze kuchukua fedha katika taasisi za benki na zinunue kama taasisi za kibiashara waweze kuuza mazao mbalimbali, lakini vilevile tunatumia balozi zetu kuwasaidia wafanyabisahara wa kitanzania kuuza mzao yetu yaliyochakatwa nje.

Mheshimiwa Naibu Spika, na kupitia Bunge hili nataka niwaombe wachakataji wa mazao hasa ya mahindi, hakikisheni mashine zenu mmezifungia kitu kinaitwa fortification ili unga wetu uwe unga fortified na uweze ku- meet international standards. Hili ni jambo ambalo linatukwaza katika kuuza mazao nah ii ni peoject ambayo inatakiwa sekta binafsi waweze kuifanya. Kwa hiyo, Serikali inachukua hatua hizo. (Makofi)
MHE. JOSEPHINE J. GENZABUKE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Pamoja na majibu ya Mheshimiwa Naibu Waziri, nina maswali mawili ya nyongeza:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa usanifu ulikamilika na kuwa usanifu unaofanyika ni uhuishaji wa usanifu wa awali. Je, Serikali haioni haja kutenga fedha mwaka ujao wa fedha ili kujenga daraja hilo 2021/2022 ili kunusuru maisha ya wanawake na watoto wanaopoteza maisha kwasababu ya kutokuwa na kivuko hicho?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali langu la pili. Kwa kuwa, kivuko kinaanca kazi saa 01:00 asubuhi na kuishia saa 01:00 jioni. Je, Serikali haioni umuhimu wa kuongeza saa ili kivuko hicho kifikie saa 06:00 usiku kuweza kuwanusuru wananchi wanaopoteza maisha kutokana na saa hizo kuwa fupi?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye jibu langu la msingi nimeeleza kwamba, tumetenga, kama bajeti itapitishwa kama ilivyoombwa, tumetenga milioni 400 kukamilisha usanifu wa kina.

Mheshimiwa Naibu Spika, ninaomba nimueleze Mheshimiwa Mbunge kwamba, daraja hili ni kati ya madaraja makubwa yatakayojengwa Tanzania, Mto Malagarasi ni kati ya mito mikubwa katika Tanzania hivyo, tutakapokamilisha usanifu wa kina ndio ujenzi utaanza.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali lake la pili ni kivuko kinafanya kazi kuanzia saa 01.00 hadi saa 01.00 jioni.

Mheshimiwa Naibu Spika, naungananae, na kwasababu ya changamoto ya Mto Malagarasi ambao ni mto mkubwa una zaidi ya kilometa 300 na unapita kwenye misitu mikubwa ambayo inabeba magogo na miti, lakini pia kuna wakati unafurika na mpaka zile sehemu zake za ku-park vile viuvuko huwa hazipo ndio maana Serikali imeona isifanye kazi usiku kwasababu, inaweza ikapeleka kivuko ziwani na hata kukipindua hicho kivuko kwa sababu ya hayo magogo na miti.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini Mheshimiwa anafahamu kwamba tumeweka utaratibu pale ambapo kuna dharura, watu hao wapo na wamekuwa wanafanya kazi. Hata hivyo, ili kuondokana na changamoto hiyo kabisa ndiyo maana Serikali sasa imekuja na mpango wa kujenga daraja, ahsante.
MHE. JOSEPHINE J. GENZABUKE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, nina swali moja la nyongeza:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kipande cha barabara ya kutoka Uvinza hadi Malagarasi, kilometa 48, Serikali iliahidi kukijenga kwa msaada wa pesa za Falme za Kiarabu. Tangu mwaka juzi, 2019 Serikali imekuwa ikisema kwamba kipande hicho kitajengwa kwa pesa hizo za msaada wa Falme za Kiarabu:-

Je, ni lini sasa Serikali itajenga kipande hicho cha kutoka Uvinza hadi Malagarasi? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Naibu Spika, Barabara ya Malagarasi hadi Uvinza yenye urefu wa takribani kilometa 53 ni kati ya barabara kuu ambayo inaunganisha Mkoa wa Kigoma na Tabora. Naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba barabara hiyo fedha ipo na muda wowote, hata kabla ya mwisho wa mwaka wa fedha huu, itatangazwa kwa ajili ya kuanza ujenzi kwa kiwango cha lami ili sasa tuweze kukamilisha barabara kwa kiwango cha lami kutoka Kigoma – Malagarasi – Kaliuwa – Urambo – Tabora hadi Dodoma. Ahsante sana.
MHE. JOSEPHINE J. GENZABUKE: Mheshimiwa Spika, ahsante. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, nina swali moja la nyongeza. Kutokana na majibu yaliyotolewa na Serikali, inaonyesha ni dhahiri ni Halmashauri mbili tu kati ya Halmashauri 184 nchi nzima ambazo zimepatiwa pikipiki. Hali hii inaonyesha jinsi ambavyo upo uhitaji mkubwa katika Halmashauri nyingine. Je, Serikali ina mkakati gani wa makusudi kuhakikisha kitengo hicho kinawezeshwa kibajeti katika Halmashauri zote? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO (MHE. MWANAIDI ALI KHAMISI): Mheshimiwa Spika, kwanza napenda kumpongeza Mheshimiwa Josephine kwa kufuatilia Maafisa hawa na kuona umuhimu wa kazi zao wanazozifanya.

Mheshimiwa Spika, ni kweli Maafisa hawa wana changamoto kubwa ya vitendea kazi. Mimi mwenyewe binafsi baada ya kumalizika Bunge la Bajeti niliweza kutembelea mikoa mitatu pamoja na Wilaya zake, yaani Mkoa wa Tabora, Iringa na Ruvuma na nimekutana na Maafisa hawa wa Ustawi wa Jamii wakanielezea changamoto zao.

Mheshimiwa Spika, kwa sasa Wizara inaendelea na mikakati ya kuwasiliana na wadau wa Maendeleo ya Jamii ili pamoja na miradi ambayo wanaitekeleza na wadau hao, kuwawezesha Maafisa hawa wa Jamii kuendelea kupata vifaa vya kufanyia kazi kulingana na mazingira yao waliyokuwa nayo.

Mheshimiwa Spika, Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mama yetu Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, inawajali sana wafanyakazi pamoja na wananchi wake. Kwa hili tumelipokea na tutaendelea kulifanyia kazi suala hili la upatikanaji wa vitendea kazi kwa mikoa yote nchini Tanzania. Ahsante, napenda kuwasilisha.
MHE. JOSEPHINE J. GENZABUKE: Mheshimiwa Spika, nakushukuru nina swali la nyongeza kwa Mheshimiwa Waziri wa Ujenzi. Kipande cha barabara ya kutoka Uvinza mpaka Malagarasi kilometa 51 kiliahidiwa kujengwa tangu kwenye utawala wa Rais wa Awamu ya Nne Dkt Kikwete. Kipande hicho mpaka leo hakijaweza kujengwa lakini Chagu mpaka Kazilambwa nayo haijakamilika. Ni lini Serikali itakamilisha ujenzi wa kipande hicho cha kilometa 51?
WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI: Mheshimiwa Spika, ninaomba kumjibu Mheshimiwa Mbunge kama ifuatavyo. Barabara ya Uvinza Malagarasi yenye urefu wa kilomita 51 hivi sasa tuko kwenye mpango wa kutafuta fedha kwa ajili ya kumalizia kipande hicho ili sasa wananchi waweze kufaidi kutoka Dar es Salaam mpaka huko Kigoma barabara yote iwe na lami kwa asilimia 100.
MHE. JOSEPHINE J. GENZABUKE: Mheshimiwa Spika, ahsante, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri nina maswali mawili ya nyongeza.

Swali la kwanza; kazi kubwa katika kusimamia vyama vya ushirika ipo kwenye wilaya zetu. Je, vifaa hivi vilivyozungumziwa vinaelekezwa kwenye Wilaya au Mikoa? (Makofi)

Pili, Taarifa ya Shirika la Ukaguzi (COASCO) ya mwaka 2019/2020 inaonesha ni vyama 6,021 vilifanyiwa ukaguzi, kati ya vyama hivyo ni vyama 289 nivyo vilivyopatiwa hati safi, sawa na asilimia 4.8.

Je, Serikali haioni kwamba ipo haja ya kuwawezesha maafisa ushirika ili waweze kufanya kazi hiyo kwa ufanisi zaidi? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Josephine Genzabuke, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, pikipiki hizi 137 zimeelekezwa katika Halmashauri za Wilaya na kama nilivyosema hapo awali, pamoja na hiyo pia Wizara imeona kuna umuhimu wa kuanza kuandaa bajeti ya kutenga fedha za kununua magari kwa ajili ya kusaidia zoezi la ushirika katika mikoa yetu. Kwa hiyo nimuondolee hofu Mheshimiwa Mbunge kwamba kazi hii ya ushirika tunaipa thamani kubwa na tunatambua umuhimu wake katika kumuendeleza mkulima wa Tanzania.

Mheshimiwa Spika, la pili ni linalohusu kuiwezesha COASCO kufanya ukaguzi ili kuweza kupata hali halisi ya vyama vyetu vya ushirika hapa nchini.

Mheshimiwa Spika, katika bajeti yam waka 2021/2022 Serikali tumetenga shilingi milioni 700 kwa ajili ya kuhakikisha kwamba tunavifikia vyama vingi vya ushirika na kufanya ukaguzi. Lengo lake ni kuweza kufikia maeneo mengi zaidi kuliko ilivyokuwa awali.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo Serikali tumeona umuhimu na tumeendelea kuongeza katika eneo hili.
MHE. JOSEPHINE J. GENZABUKE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa majibu mafupi. Nina swali moja la nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wilaya ya Kibondo ni kati ya Wilaya kongwe nchini, Wilaya hiyo haina Chuo cha VETA. Je, ni lini Serikali itajenga Chuo cha VETA katika Wilaya ya Kibondo?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Naomba kujibu swali dogo la Mheshimiwa Genzabuke, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli Wilaya ya Kibondo bado hatujaweza kuifikia kwenye Vyuo vyetu vya VETA, ingawa tuna Chuo kikubwa kilichojengwa Kasulu ambapo ni karibu kabisa na wenzetu wa Kibondo. Kwa sasa tunawashauri wananchi wetu wa Kibondo waweze kupata huduma hii katika chuo chetu kikubwa ambacho tumejenga katika Wilaya ya Kasulu wakati Serikali inaendelea na mchakato wake wa kutafuta fedha kwa ajili ya ujenzi katika eneo hili la Kibondo. Nakushukuru sana.