Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Questions from Hon. Josephine Johnson Genzabuke (27 total)

Ujenzi wa Barabara ya Kidahwe - Kasulu - Nyakanazi
MHE. JOSEPHINE J. GENZABUKE aliuliza:-
Je, ni lini barabara ya Kidahwe – Kasulu – Nyakanazi itakamilika kwa lami?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Josephine Genzabuke, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, ujenzi wa kiwango cha lami wa barabara ya Kigoma - Kidahwe - Kasulu hadi Nyakanazi yenye urefu wa kilometa 330 unafanyika kwa awamu kulingana na upatikanaji wa fedha ambapo sehemu ya barabara hii kutoka Kigoma hadi Kidahwe yenye urefu wa kilometa 28.2 imejengwa kwa kiwango cha lami na kukamilika, sehemu ya Kidahwe - Kasulu yenye urefu wa kilometa 50 na sehemu Kibondo - Kakonko mpaka Nyakanazi yenye urefu wa kilometa 50 zinaendelea kujengwa kwa kiwango cha lami.
Aidha, kazi ya kufanya mapitio ya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina wa sehemu zilizobaki kati ya Nyakanazi na Kasulu, pamoja na barabara ya Kasulu hadi Manyovu zenye jumla ya kilometa 250 inatarajiwa kuanza Aprili, 2016 kwa kutumia fedha za NEPAD kupitia Benki ya maendeleo ya Afrika chini ya utaratibu wa Sekretarieti ya Jumuiya ya Afrika Mashariki. Kazi za ujenzi kwa kiwango cha lami kwa barabara hii inatarajiwa kuanza baada ya kukamilika kwa mapitio ya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina.
Pori la Akiba la Kagera Nkanda lililopo Wilaya ya Kasulu lilianzishwa kipindi ambacho Wilaya ya Kasulu ilikuwa na wakazi wachache na kwa sasa idadi ya watu katika Wilaya hiyo imekuwa kubwa na kufanya mahitaji ya ardhi kuwa makubwa, pia hivyo kusababisha mgogoro baina ya wakulima na wafugaji na mamlaka za misitu na wanyaa pori.
Je, Serikali imejipanga vipi kumaliza migogoro hii na kuwasaidia wananchi?
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Maliasili na Utalii naomba kujibu swali la Mheshimiwa Augustine Vuma Holle, Mbunge wa Kasulu Vijijini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Kagera Nkanda ni kijiji kilichopakana na Hifadhi ya Msitu wa Makere Kusini na si Pori la Akiba. Msitu huu ulihifadhiwa kwa Tangazo la Serikali Namba 250 la mwaka 1956 na una ukubwa wa hekta 99,682.7. Uhifadhi wa msitu huo unatokana na umuhimu na faida zake kwa Taifa ikiwa ni pamoja na kuwa chanzo kikuu cha maji yanayoingia kwenye Mto Malagarasi, ushoroba wa wanyamapori kati ya Pori la Akiba Moyowosi na Kigosi, sehemu ya eneo la ardhi oevu lenye umuhimu wa kimataifa (The Malagarasi Moyowosi Ramsar Site), Hifadhi ya viumbe na mimea na hivyo kusaidia kupunguza madhara ya mabadiliko ya tabianchi.
Mheshimiwa Naibu Spika, chanzo cha migogoro na wananchi wanaoishi jirani na hifadhi hii ni mahitaji ya ardhi kwa ajili ya shughuli za kibinadamu hususani kilimo. Swali hili limejibiwa na Serikali mara mbili ndani ya Bunge lako Tukufu, ambapo mara moja lilijibiwa na Wizara ya Maliasili na Utalii tarehe 26 Juni, 2014 na mara nyingine lilijibiwa na Ofisi ya Waziri Mkuu, TAMISEMI mnamo tarehe 18 Juni, 2015.
Mheshimiwa Naibu Spika, viongozi mbalimbali akiwemo Mheshimiwa Waziri Mkuu wa Awamu ya Nne walifanya ziara katika eneo husika na kusikiliza hoja kutoka kwa wananchi, lakini kumbukumbu zinaonesha kuwa hakuna madai yaliyotolewa kuhusiana na uhitaji wa ardhi ya hifadhi kutoka kwa wananchi ispokuwa kwamba baadhi ya wananchi walivamia msitu wamekuwa wakiomba na kuruhusiwa kuvuna mazao waliyoyapanda kabla Serikali haijatekeleza operesheni ya kuwaondoa katika hifadhi ya msitu.
Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na majibu haya, wakati wa zoezi la kushughulikia matatizo ya ardhi kwa nchi nzima ikihusisha Wizara sita, zoezi ambalo litaanza baada ya Bunge la Bajeti, Wizara yangu itazingatia wito uliotolewa Bungeni kupitia jibu la msingi lililotolewa na TAMISEMI mnamo tarehe 18 Juni, 2015 kuhusu mgogoro huu.
MHE. JOSEPHINE J. GENZABUKE aliuliza:-
Mkoa wa Kigoma umekumbwa na wimbi kubwa la wakimbizi wa kutoka Burundi na Congo (DRC), kutokana na wimbi hilo ujambazi umeongezeka sana.
Je, Serikali iko tayari kuongeza ulinzi wa kutosha na vitendea kazi vya kutosha ili mamlaka husika iweze kukabiliana na tatizo hilo?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI NCHI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Josephine Genzabuke, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, ikumbukwe kwamba suala la wakimbizi kuja nchini hutokea mara nchi jirani zinapokuwa katika hali tete ya usalama katika nchi zao.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imekuwa ikiongeza ulinzi pamoja na vitendea kazi ikiwemo magari na pikipiki kwa lengo la kudhibiti uhalifu unapojitokeza katika maeneo mbalimbali. Aidha, hivi karibuni Mkoa wa Kigoma umepokea magari 11 na Serikali itaendelea kuongeza na kuimarisha ulinzi katika Mkoa wa Kigoma na mahali pengine popote nchini ambapo kutakuwa na tatizo kama hilo.
MHE. JOSEPHINE J. GENZABUKE aliuliza:-
Kwa muda mrefu sasa kumekuwa na malalamiko baina ya wakulima na Mamlaka ya Mapori ya Hifadhi ya Misitu, kwa sababu ya kuongezeka kwa watu lakini ardhi haiongezeki, hivyo kufanya ongezeko hili la watu wakose ardhi kwa shughuli zao za kilimo na mambo mengine yahusuyo ardhi:-
Je, ni lini Serikali italeta Bungeni Muswada wa Sheria husika ili kufanya marekebisho katika mipaka ya Hifadhi hizo ili kupata eneo la kilimo kwa wananchi walioongezeka ambao hawana maeneo ya kilimo.
WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Josephine Genzabuke, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kuwa idadi ya Watanzania inaongezeka siku hadi siku, ambapo 75% ya watu hao wanaishi vijijini na kwamba wananchi wengi wa vijijini wanategemea rasilimali za misitu na ardhi kwa ajili ya maisha yao. Pia, inaeleweka wazi kuwa kasi ya ongezeko la idadi ya watu linachangia katika kuongezeka kwa mahitaji ya mazao ya misitu na ardhi kwa ajili ya kilimo, ufugaji pamoja na makazi. Kukosekana kwa mipango ya matumizi bora ya ardhi ya vijiji, inachochea kuongezeka kwa kasi ya uharibifu wa misitu na ukosefu wa ardhi.
Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na mahitaji makubwa na umuhimu wa ardhi katika kukidhi mahitaji ya wananchi na maendeleo ya kiuchumi, Serikali inatambua misitu ni muhimu kwa maisha ya viumbe hai, katika kupunguza hewa ukaa, kulinda hewa safi, kupunguza joto la ardhi, kutunza vyanzo vya maji, upatikanaji wa nishati na shughuli mbalimbali za kibinadamu. Hivyo, kwa kutambua umuhimu wa ustawi wa maisha ya wananchi na uhifadhi wa misitu, Serikali inaendelea kuchukua hatua zinazozingatia uwiano kati ya mahitaji ya maendeleo ya wananchi na uhifadhi wa misitu.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kutambua changamoto zinazotokana na upungufu wa ardhi, Wizara inawashauri wananchi wote na Serikali za Vijiji vyote vinavyozunguka misitu ya hifadhi kushirikiana na sekta husika katika kuandaa mipango ya matumizi bora ya ardhi itakayolenga kutenga maeneo kwa matumizi mbalimbali kufuatana na mahitaji katika maeneo yao.
Mheshimiwa Naibu Spika, Wizara yangu itaendelea kutoa ushirikiano katika kuandaa mipango ya matumizi bora ya ardhi ikiwa ni pamoja na hifadhi ya misitu. Vilevile, tunawaomba Waheshimiwa Wabunge kuwahamasisha wananchi kutumia mbinu za kilimo bora chenye tija na kuibua shughuli nyingine za kiuchumi ambazo hazihitaji matumizi makubwa ya ardhi kama vile ufugaji wa samaki, ufugaji wa nyuki, uanzishaji wa viwanda vidogovidogo na shughuli nyingine ambazo ni rafiki wa mazingira.
MHE. JOSEPHINE J. GENZABUKE aliuliza:-
Mkoa wa Kigoma una madini ya chokaa, dhahabu,
platinum na kadhalika:-
Je, Serikali imechukua hatua gani kuendeleza utafutaji na uchimbaji wa madini katika mkoa huo?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nishati na Madini, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Josephine Johnson Genzabuke, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kuwa Mkoa wa Kigoma una madini ya aina mbalimbali yakiwemo madini ya chokaa, chuma, cobalt, dhahabu, galena, nickel, shaba na platinum.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kupitia Wakala wa Jiolojia Tanzania (GST) ilifanya utafiti wa awali wa madini nchi nzima na kuandaa ramani za jiolojia nchini. Utafiti huo utasaidia kutangaza fursa za uwepo wa madini yanayogunduliwa ili wawekezaji wa ndani na nje ya nchi waweze kuwekeza katika tafiti za kina na uchimbaji wa madini.
Mheshimiwa Naibu Spika, mwaka 1959 hadi 2010 Wakala wa Jiolojia Tanzania (GST) walifanya utafiti wa jiolojia katika Mkoa wa Kigoma na kutengeneza ramani za jiolojia 22 kwa nchi nzima na hasa katika Mkoa wa Kigoma. Kati ya mwaka 2013 hadi 2014, GST kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo ikiwemo kampuni ya Beak Consultants GmbH ya Ujerumani na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam walifanya utafiti wa awali kubainisha uwepo wa madini mbalimbali Mkoani Kigoma kama ifuatavyo:-
Madini ya tin katika maeneo ya Bwuhinika, Kabogo, Kapalagulu na Lugufu; madini ya shaba katika maeneo ya Gagwe, Kampisa na Nyamori; madini ya barite katika eneo la Ilagala; chumvi katika eneo la Uvinza; dhahabu katika maeneo ya Isabika, Lumbwa, Lusahunga pamoja na Mwiruzi; madini ya agate katika maeno ya Kabingo, Kasulu, Keza na Nkuba; madini ya nickel katika eneo la Kapalagulu na madini ya chokaa katika maeneo ya Lugufu, Makere, Matiaso pamoja na Kasuku. Utafiti wa kina unahitajika ili kubaini kiasi halisi cha mashapo yaliyopo.
Mheshimiwa Naibu Spika, hadi kufikia mwezi Machi 2017, Mkoa wa Kigoma ulikuwa na jumla ya leseni 15 za utafutaji wa madini ya dhahabu, leseni 20 za utafutaji wa madini ya shaba na leseni 2 za utafutaji madini ya platinum. Vilevile kuna leseni 25 za uchimbaji mdogo wa madini ya dhahabu na leseni 118 za uchimbaji mdogo wa madini ya chokaa, kadhalika kuna leseni 716 za uchimbaji mdogo wa madini ya shaba katika maeneo mbalimbali Mkoani Kigoma.
MHE. JOSEPHINE J. GENZABUKE aliuliza:-
Wilaya za Kakonko, Buhigwe na Uvinza ni Wilaya mpya ambazo hazina Hospitali za Wilaya.
Je, ni lini Serikali itajenga Hospitali za Wilaya katika Wilaya hizo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPH G. KAKUNDA) alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Josephine Johnson Genzabuke, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika bajeti ya mwaka wa fedha 2017/2018 Halmashauri ya Wilaya ya Kakonko imeidhinishiwa jumla ya shilingi milioni 500 kuanza ujenzi wa Hospitali ya Wilaya. Ujenzi wa hospitali hiyo unatarajiwa kugharimu shilingi bilioni 1.5 hadi kukamilika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Halmashauri ya Wilaya ya Uvinza imetenga eneo la ekari 80 na imekamilisha michoro ya jengo la Hospitali ya Wilaya. Halmashauri imeshauriwa kuweka kipaumbele na kutenga bajeti katika mwaka wa fedha 2018/2019 ili kuanza ujenzi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Halmashauri ya Wilaya ya Buhigwe inaendelea na ujenzi wa Hospitali ya Wilaya kwa kuanza na jengo la wagonjwa wa nje, utawala na maabara unaogharibu shilingi milioni 450. Katika mwaka wa fedha 2017/2018 Halmashauri imetengewa shilingi milioni 500 kuendelea na ujenzi. Kazi hii inatekelezwa na SUMA JKT na kazi inaendelea. Ujenzi wa hospitali unafanyika kwa awamu kulingana na upatikanaji wa fedha na unakadiriwa kugharimu shilingi bilioni 6.4 hadi kukamilika.
MHE. JOSEPHINE J. GENZABUKE aliuliza:-
Serikali imekuwa ikitoa ruzuku ya pembejeo kwa njia ya vocha kwa lengo la kuwasaidia wakulima, lakini utaratibu ukiwanufaisha Mawakala wa Mbolea kuliko wakulima ambao ndio walengwa.
Je, Serikali inachukua hatua gani ya kuweza kubadilisha utaratibu huo na kuja na utaratibu mwingine utakaoweza kuwasaidia wakulima?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI,VIJANA NA AJIRA (K.n.y WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI) alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Josephine, Johnson Genzabuke, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, mara ya mwisho ya utaratibu wa vocha ulitumika msimu wa mwaka 2013/2014 na mwaka 2014/2015, utaratibu uliotumika ulikuwa wa vikundi na msimu wa 2015/2016 utaratibu wa vocha ulitumika tena kwa kuwa wakulima wengi hawakuwa kwenye vikundi na hivyo kutonufaika na ruzuku. Aidha, Serikali msimu wa mwaka 2016/2017 imetumia Kampuni ya Mbolea ya TFC kusambaza ruzuku ya pembejeo moja kwa moja kwa wakulima kupitia mawakala waliowachagua wao wenyewe na waaminifu na sio kutumia vocha tena.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara imeunda Kanuni ya Uingizaji mbolea kwa wingi (Bulk Fertilizer Procurement Regulation 2017) kwa kuanza na mbolea za urea na DAP. Lengo ni kuwa uagizaji huu utasababisha mbolea kushuka bei na hivyo Serikali kutokulazimika kutoa ruzuku ya mbolea hizo. Utaratibu huu utaendelea kutumika kwa aina nyingine endapo zitakidhi kanuni hiyo, hususan uwingi wa mahitaji yake.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tarehe 19/05/2017 awamu ya kwanza uchambuzi wa wazabuni ilifanyika, kati ya kampuni 20 zilizoomba kampuni 17 zimepitia awamu ya kwanza, kati yake kampuni kumi ni za ndani na Saba ni za nje ya nchi. Hii inaonesha muitikio mkubwa wa waagizaji wa utaratibu huu na hivyo matarajio ni bei kushuka na kila mkulima kujinunulia. Utaratibu mwingine ni kuwa Serikali inahimiza ujenzi wa viwanda vya mbolea hapa nchini ili kuondokana na uagizaji wa mbolea kutoka nje ya nchi kwa gharama kubwa.
MHE. JOSEPHINE J. GENZABUKE aliuliza:-
Zahanati nyingi za Vijiji vya Mkoa wa Kigoma katika wilaya zote zina upungufu mkubwa sana wa watumishi wa afya na baadhi ya zahanati hazina Waganga hivyo huduma zinatolewa na Manesi Wasaidizi tu:-
Je, ni lini Serikali itapeleka watumishi wa afya wa kutosha katika maeneo hayo ili kuimarisha utoaji wa huduma za afya vijijini?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE) alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Josephine Johnson Genzabuke, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Mkoa wa Kigoma una jumla ya vituo vya kutolea huduma za afya 278, hospitali sita (6), vituo vya afya 32 na zahanati 240. Kati ya vituo hivyo, vituo vya Serikali ni 224 sawa na asilimia 80%, hospitali tatu (3), vituo vya afya 23 na zahanati 198. Idadi hii inajumuisha vituo vya mashirika ya dini, kambi za wakimbizi, binafsi na taasisi za umma kama Magereza, Polisi, Jeshi na TRL.
Mheshimiwa Spika, mahitaji ya watumishi wa sekta ya afya kwa mujibu wa ikama mpya ya mwaka 2014 katika vituo vya umma kimkoa ni 5,007, watumishi waliopo ni 1,663 sawa na asilimia 33.2 ya mahitaji na upungufu ni 3,344 sawa na asilimia 66.8. Mkoa pamoja na halmashauri zimeendelea kukabiliana na changamoto hii kwa kushawishi wadau wa sekta ya afya wakiwemo THTS, East African Public Health Lab Net, Engender Health na UNICEF kusaidia kuajiri watumishi muhimu kwa muda/mkataba, pamoja na kuweka katika bajeti kwa ajili ya kuajiri watumishi wapya.
Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2017/ 2018, Mkoa wa Kigoma umepatiwa watumishi wa afya 95 wakiwemo Madaktari watano (5), Matabibu 24, Wauguzi 33, Wafamasia 17 na Wataalam wa Maabara 16. Katika mwaka wa fedha 2018/2019, mkoa umeomba kutengewa nafasi za ajira 1,667 kwa kada mbalimbali za afya.
MHE. JOSEPHINE J. GENZABUKE aliuliza:-
Moja ya jukumu la Serikali ni kuhudumia wafungwa kwa maana ya kukwapatia huduma za msingi kama vile chakula, mavazi na matibabu:-
Je, Serikali inafanya nini ili kuhakikisha huduma hizo za msingi katika Gereza la Kasulu zinapatikana kwani wana hali mbaya sana hasa kimavazi?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, napenda kujibu swali la Mheshimwa Josephine Johnson Genzabuke, Mbunge Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, huduma za wafungwa magerezani hujumuisha chakula, mavazi, matibabu pamoja na huduma nyingine muhimu ambazo hutengewa fedha katika bajeti ya Serikali ya kila mwaka. Ili kupunguza tatizo la uchakavu wa sare za wafungwa kwa mwaka wa fedha wa 2017/2018, Serikali ilitenga kiasi cha shilingi milioni mia sita kwa ajili ya kushona sare za wafungwa nchi nzima. Aidha, kwa mwaka 2018/2019, Serikali imetenga shilingi milioni mia moja kwa ajili ya sare za wafungwa nchi nzima.
MHE. JOSEPHINE J. GENZABUKE aliuliza:-
Upatikanaji wa maji safi na salama katika Mji wa Kasulu bado ni changamoto kubwa sana, kwani maji yanayotoka kwenye mabomba ni machafu.
Je, ni lini Serikali itatoa pesa kwa ajili ya kununua chujio la maji ili wananchi waweze kupata maji safi na salama?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Maji na umwagiliaji naomba kujibu swali la Mheshimiwa Josephine Johnson Genzabuke, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inatambua tatizo la maji katika Halmashauri ya Mji wa Kasulu ikiwa ni pamoja na miradi ya maji kutokuwa na miundombinu ya kutibu maji katika bajeti ya mwaka 2017/2018. Kupitia Programu ya Maendeleo ya Sekta ya Maji, Halmashauri ya Mji wa Kasulu imetengewa shilingi bilioni 3.35 kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu ya maji ikiwemo ujenzi wa miundombinu ya kusafisha na kutibu maji. Hadi sasa usanifu wa miradi minne ya Muganza, Marumba, Muhunga na Kimobwa katika Halmashauri ya Mji wa Kasulu umekamilika na taratibu za kuwapata Wakandarasi watakaotekeleza ujenzi wa miradi hiyo zinaendelea.
Mheshimiwa Naibu Spika, ujenzi wa miundombinu ya kutibu maji ni sehemu ya mradi wa maji wa Kimobwa ambao utaambaatana na uchimbaji wa visima virefu vitano, usambazaji wa bomba la kilometa 14, ujenzi wa tenki lenye ukubwa wa mita za ujazo 225 na ukarabati wa vyanzo vitatu vya maji kwa ajili ya eneo la mji wa Kasulu.
Mheshimiwa Naibu Spika, miundombinu ya kutibu na kusafisha maji itasaidia kuondoa kero ya ubora duni wa maji yanayotumika hivi sasa hususan maji yanayotoka katika vyanzo vya maji vya Miseno, Nyanka, Nyankatoke na Mto Chai. Hivyo ubora wa maji, uzalishaji na usambaji wa maji kwa pamoja utaongezeka. Lengo ni kuhakikisha maji yanayosambazwa kwa wananchi ni safi, salama na yanayokidhi mahitaji.
Mheshimiwa Naibu Spika, zabuni kwa ajili ya kazi hiyo imetangazwa tarehe 24 Machi, 2018 na utekelezaji wake utaanza mara tu baada ya mikataba ya ujenzi kusainiwa.
MHE. JOSEPHINE J. GENZABUKE aliuliza:-
Mwaka 2017 wakati Mheshimiwa Rais akiwa katika ziara Mkoa wa Kigoma, katika Wilaya ya Kasulu aliwaruhusu wananchi waliokuwa wakilima katika maeneo ya Hifadhi ya Makere (Kagera Nkanda) kwa sharti kwamba wasiongeze maeneo mengine zaidi ya yale waliyokuwa wakilima:-
Je, kwa nini TFS wanapingana na agizo la Mheshimiwa Rais na wanawatesa wananchi kwa kuwapiga na kuwanyan’ganya baiskeli na pikipiki?
NAIBU WAZIRI MALIASILI NA UTALII alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Maliasili na Utalii napenda kujibu swali la Mheshimiwa Josephine Johnson Genzabuke, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, baada ya Mheshimiwa Rais kuagiza kumegwa kwa sehemu ya msitu wa Makene Kusini ili kutoa maeneo kwa wananchi kulima Wizara kwa kushirikiana na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Kigoma na Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Kasulu ilitekeleza agizo kikamilifu kwa kupima eneo la msitu huo.
Mheshimiwa Spika, kufuatia upimaji huo jumla ya hekta 10,012.61 zilitengwa kwa ajili ya kilimo kwa wananchi wa maeneo hayo. Hivyo Kijiji cha Uvinza kilipewa hekta 2,174 na Kagera Nkanda kikapewa hekta 2,496; na eneo lingine la hekta 5,342.61 zilitengwa kwa ajili ya wananchi wengine wa vijiji vya Nachenda, Mgombe na Nyakitonto.
Mheshimiwa Spika, hata hivyo, kijiji cha Uvinza kililalamika kuwa eneo walilopata halitoshi hivyo wakaomba waongezewe eneo ambalo ni ardhi chepechepe yaani ardhi oevu karibu na Mto Makene na Mto Malagarasi ambalo kitaalam hairuhusiwi kulima kwa sababu itasababisha uharibifu mkubwa na kupotea kwa sifa ya uhifadhi. Mto Malagarasi ni muhimu kwa ikolojia na kwa ajili ya ujenzi wa mitambo ya umeme wa maji katika maporomoko ya Mto Malagarasi.
Mheshimiwa Spika, kwa sasa wananchi wanaendelea na shughuli za kilimo katika maeneo hayo yaliyotengwa na kuridhiwa na vikao vyote vya Mabaraza ya Mkoa na Wilaya. Wizara kwa kushirikiana na Kamati za Ulinzi na Usalama za Mkoa imekamilisha mchakato wa ramani mpya ya msitu huo.
Mheshimiwa Spika, tatizo lililojitokeza sasa ni kwa wananchi wachache kwa maslahi yao kukataa kufuata taratibu na kutaka kulima ndani ya msitu nje ya maeneo yaliyotengwa huku wengine wakiendelea na uwindaji haramu wa wanyamapori. Wananchi hao wasiofuata sheria ndio waliozuiwa na mamlaka husika kwa Sheria ya Misitu namba 14 ya mwaka 2002, Sura 323 katika kifungu cha 26 ambacho kinakataza kufanya shughuli zozote za kibinadamu ikiwa ni pamoja na kilimo na ufugaji ndani ya msitu wa hifadhi. Mtu yoyote akibainika kufanya hivyo hatua za kisheria hufuatwa.
Mheshimiwa Spika, natoa rai kwa wananchi kuendelea na kilimo katika maeneo yaliyotengwa na kuachana na kilimo cha kuhamahama ambacho ndicho kinachowafanya kuvamia maeneo ya hifadhi za misitu. Aidha, natoa ushauri kwa wananchi kufuata kanuni bora za kilimo kwa kutumia mbolea ili mashamba yao yaendelee kuzalisha mazao wakati wowote.
MHE. JOSEPHINE J. GENZABUKE aliuliza:-

Wanawake Mkoani Kigoma wameitikia wito wa kujiunga katika vikundi vya ujasiriamali kama vile vikundi vya kilimo cha muhogo, kurina na kuchakata asali na VICOBA:-

Je, Halmashauri za Wilaya za Mkoa wa Kigoma zimechangia kiasi gani kwa vikundi hivyo kama sheria inavyotamka?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. MWITA M. WAITARA) alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Josephine Johnson Genzabuke, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, katika mwaka wa fedha 2017/2018, Halmashauri za Mkoa wa Kigoma zilitoa shilingi milioni 250 kwa ajili ya vikundi vya wanawake na vijana. Kati ya fedha hizo, shilingi milioni 129 zilitolewa kwa vikundi vya wanawake. Aidha, katika mwaka wa fedha 2018/2019 hadi Februari 2019, Mkoa wa Kigoma umetoa shilingi milioni 249 kwa ajili ya vikundi 171 vya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu. Kati ya fedha hizo shilingi milioni 181 zimetolewa kwa vikundi 120 vya wanawake.

Mheshimiwa Naibu Spika, Ofisi ya Rais - TAMISEMI itaendelea kusimamia sheria inayozitaka Halmashauri kutenga, kutoa mikopo na kusimamia marejesho ya fedha hizo kutoka kwenye vikundi vilivyonufaika. Ahsante.
MHE. JOSEPHINE J. GENZABUKE aliuliza:-

Maeneo ya mipakani katika Wilaya za Kakonko, Kibondo, Kigoma Vijijini, Buhigwe na Kasulu yanakabiliwa na tatizo la mawasiliano ya simu kutokana na kukosekana kwa minara ya simu:-

Je, ni lini Serikali itajenga minara ya simu katika maeneo ambayo hayana minara Mkoani Kigoma ili kuondoa tatizo la mawasiliano kwa Wananchi?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ENG. ATASHASTA J. NDITIYE) alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Josephine Johnson Gezabuke, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote mwezi Julai 2019, ilitangaza zabuni kwa ajili ya kufikisha huduma za mawasiliano katika kata 521 zenye vijiji 1,222 nchini. Zabuni hii ilifunguliwa Oktoba, 2019 na baada ya tathmini yake maeneo yaliyopata wazabuni nchi nzima na maeneo mbalimbali ni kama yafuatavyo:-

(i) Kwa upande Wilaya ya Kakonko, nikizungumzia Mkoa wa Kigoma kata zilizopata miradi ni Kata za Nyamtukuza na Rugenge, Kijiji cha Kasongati;

(ii) Katika Wilaya ya Kigoma Vijijini, ilikuwa ni Kata ya Ziwani ikijumuisha Vijiji vya Kalalangabo na Kigalye;

(iii) Katika Wilaya ya Buhigwe, tulikuwa na Kata ya Mugera, Kijiji cha Katundu; na

(iv) Katika Wilaya ya Kasulu, ilikuwa Kata ya Kitanga na Kijiji cha Kitanga.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa maeneo yaliyopata wazabuni, utekelezaji utaanza mapema mwezi wa Desemba, 2019.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa Upande wa Wilaya ya Kibondo, Kampuni ya Simu ya Viettel (Halotel) itajenga mnara ili kufikisha huduma za mawasiliano katika Kijiji cha Kibuye ambapo wanatarajiwa kuanza mwisho wa mwezi Desemba, 2019.
MHE. JOSEPHINE J. GENZABUKE aliuliza:-

Mwezi Novemba, 2018, Waziri wa Maji alifanya ziara Wilayani Kakonko na Kibondo na kukagua miradi ya maji iliyokwisha tumia zaidi ya shilingi bilioni moja lakini haifanyi kazi:-

Je, ni lini miradi hiyo itakamilika?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII (K.n.y. WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI) alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Maji, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Josephine Johnson Genzabuke, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, katika Miradi ya Maji ya Muhange, Kiduduye na Nyangwijima iliyopo Wilaya ya Kakonko baada ya kujengwa na kukamilika kulijitokeza changamoto zilizosababisha chanzo cha maji cha Mradi wa Muhange kujaa tope na kusababisha kazi ya kuondoa tope mara kwa mara. Aidha, katika Miradi ya Maji ya Kakonko, Nyabibuye na Gwanumpu sababu kubwa zilizosababisha miradi hiyo kutokamilika kwa wakati ni uwezo mdogo wa fedha kwa wakandarasi waliotekeleza ujenzi wa mradi huo.

Mheshimiwa Spika, katika kutatua changamoto zilizojitokeza katika Miradi ya Maji ya Muhange, Kiduduye na Nyagwijima, Halmashauri ya Wilaya ya Kakonko kwa kushirikiana na Mkoa wa Kigoma imefanya mapitio ya usanifu wa miradi na kupendekeza namna ya kuboresha miundombinu na kutatua changamoto zilizopo ambapo gharama za kufanya marekebisho ya miundombinu ya vyanzo vya maji (intake structures) imekadiriwa kuwa shilingi milioni 373.99. Serikali itatoa fedha hizo ili kuhakikisha marekebisho hayo yanafanyika kwa upande wa Miradi ya Maji ya Kakonko, Gwanumpu na Nyabibuye. Halmashauri imechukua hatua kwa wakandarasi wanaochelewesha miradi kwa kuwaandikia barua ya kusudio la kuvunja mikataba endapo watashindwa kukamilisha miradi kwa wakati.

Mheshimiwa Spika, kwa Halmashauri ya Wilaya ya Kakonko, miradi iliyotekelezwa kipindi cha miaka mitano, miradi hiyo imetekelezwa katika Vijiji vya Nyankwi, Nyabitaka, Kibingo, Kagezi na Minyima. Miradi ya Maji ya Nyankwi, Nyabitaka na Kibingo inafanya kazi na Jumuiya za Watumiaji Maji (COWSO) zimekabidhiwa kuendesha na kusimamia miradi hiyo. Serikali itaendelea na marekebisho yaliyojitokeza katika Miradi ya Kagenzi na Minyinya ili iweze kutoa maji kwa wakati.
MHE. JOSEPHINE J. GENZABUKE Aliuliza:-

Je, Serikali ina mpango gani wa kutafuta soko la uhakika la mazao ya mahindi, maharage na mihogo?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO Alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo naomba kujibu swali la Mheshimiwa Josephine Johnson Genzabuke, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo;

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inaendelea kutekeleza mikakati mbalimbali ya kutafutia wakulima masoko ya mazao ya kilimo ikiwemo Serikali yenyewe kununua mahindi na maharage kupitia Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula, Bodi ya Mazao Mchanganyiko, kufanya makubaliano ya (Government to Government), masoko ya kikanda, pamoja na kuwatafutia wafanyabiashara ambao watanunua mazao ya wakulima moja kwa moja katika masoko ya nchi za nje vilevile kupitia Balozi zetu. Aidha, Serikali imeendelea kuondoa urasimu katika mifumo ya kutoa vibali vya kusafirisha na Serikali haijafunga mipaka ya kuuza mazao nje ya nchi. Kila mfanyabiashara ambaye atapata soko, Wizara ya Kilimo itaendelea kumsaidia kumpatia vibali vinavyostahili. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, katika kipindi cha 2019/2020 Serikali iliuza jumla ya tani 111,846 za mahindi katika nchi za Afrika Mashariki na kati ya hizo Kenya walinunua jumla ya tani 69,000; Uganda tani 19,000; Zambia tani 900; Rwanda tani 13,000; Burundi tani 7,000 na DRC tani 1150. Aidha, sambamba hilo Serikali bado inandelea kutoa vibali vya kusafirisha mazao nje ya nchi bila ya masharti.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika kipindi cha mwezi Mei hadi Desemba Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula walinunua jumla ya tani 73,000 za mahindi kutoka kwa wakulima na vikundi vya wakulima. Serikali inaendelea kujenga ghala kwa ajili ya kuongeza uwezo wa uhifadhi. Bodi ya Mazao Mchanganyiko imenunua jumla ya tani 24,000 za mahindi kutoka kwa wakulima na vikundi vya wakulima. Aidha, Wizara imeomba kibali kutoka Hazina kwa ajili ya kuruhusu taasisi zake ziweze kuchukua fedha katika taasisi za benki na iweze kununua moja kwa moja mazao kutoka kwa wakulima.

Mheshimiwa Naibu Spika, Wizara inaendelea kuhamasisha ununuzi wa mazao ya mihogo ambapo kampuni nne za nje ambazo ni Dar Canton, Jielong Holdings, TAEPZ na EPOCH Agricultural Development Company zimenunua jumla ya tani 300 za mihogo mikavu kutoka kwa wakulima. Wizara inaendelea kutoa elimu na kanuni za uzalishaji wa mihogo bora ili iweze kukidhi mahitaji ya masoko ya kimataifa.
MHE. JOSEPHINE J. GENZABUKE aliuliza:-

Je, ni lini Serikali itajenga Daraja kwenye Mto Malagarasi ili kuunganisha Kata ya Ilagara na Kata ya Sunuka katika Wilaya ya Uvinza?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE) alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, ninapenda kujibu swali la Mheshimiwa Josephine, Johnson Genzabuke, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Daraja la Malagarasi (Lower Malagarasi Bridge) linaunganisha Kata ya Ilagala na Kata ya Sunuka katika Wilaya ya Uvinza kupitia Barabara ya Simbo – Ilagala hadi Kalya.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kutambua umuhimu wa daraja hili katika bajeti ya mwaka huu wa 2020/2021, Wizara yangu imetenga shilingi milioni 345 kwa ajili ya kufanya kazi ya Upembuzi Yakinifu na Usanifu wa Kina wa Daraja hili la Malagarasi. Aidha, katika mapendekezo ya bajeti ya mwaka wa fedha wa 2021/2022 daraja hili limetengewa shilingi milioni 400 kwa ajili ya kuendelea na kazi ya Upembuzi Yakinifu na Usanifu wa Kina. Kwa sasa taratibu za ununuzi wa Mhandisi Mshauri wa kufanya kazi hiyo zinaendelea. Baada ya kazi hiyo kukamilika, ujenzi wa daraja hili utaanza kadiri ya upatikanaji wa fedha utakavyokuwa. Asante.
MHE. JOSEPHINE J. GENZABUKE aliuliza:-

Je, ni lini Serikali itakipatia Kituo cha Afya cha Muyama Wilayani Buhigwe vifaa vya Ultrasound na X-ray?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE) alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais-TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Josephine Johnson Genzabuke, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Kituo cha Afya cha Muyama katika Halmashauri ya Wilaya ya Buhigwe hakitoi huduma ya uchunguzi wa Ultrasound na X-ray kutokana na ukosefu wa majengo lakini na vifaa hivyo.

Mheshimiwa Spika, Serikali inamuelekeza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Buhigwe kupanga kununua Ultrasound kupitia mapato ya ndani wakati Serikali Kuu inaendelea kutafuta fedha kwa ajili ya kununua X-ray. Aidha, ikiwa mapato ya ndani ya Halmashauri hayatoshelezi, Serikali inamshauri Mkurugenzi kukopa kupitia NHIF na kununua mashine ya Ultrasound wakati Serikali inapanga kununua X- ray.
MHE. JOSEPHINE J. GENZABUKE aliuliza: -

Je, ni kwa kiasi gani Serikali imewezesha Maafisa Maendeleo ya Jamii ambao wamepewa jukumu kubwa la kuanzisha na kusimamia shughuli za vikundi vya Maendeleo kwenye Halmashauri ili waweze kutimiza majukumu yao ipasavyo?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO (MHE. MWANAIDI ALI KHAMISI) alijibu: -

Mheshimiwa Spika, ahsante. Kwa niaba ya Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Josephine Johnson Genzabuke, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali inawezesha Maafisa Maendeleo ya Jamii kupata vitendeakazi kadri Bajeti inavyoruhusu, ambapo hadi sasa imewapatia pikipiki 29 Maafisa wa Maendeleo ya Jamii wa Halmashauri ya Wilaya ya Chamwino Mkoani Dodoma na Halmashauri ya Wilaya ya Tanganyika Mkoani Katavi.

Mheshimiwa Spika, aidha, Serikali kupitia Ofisi ya Rais, TAMISEMI imetoa kanuni za utoaji na usimamizi wa mikopo kwa vikundi vya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu, marekebisho haya ya mwaka 2021. Kupitia kanuni hii, Maafisa hawa hutengewa fedha kutoka kwenye marejesho kwa ajili ya ufuatiliaji wa mikopo hiyo.

Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Naomba kuwasilisha. (Makofi)
MHE. JOSEPHINE J. GENZABUKE aliuliza: -

Je, Serikali imewezesha kwa kiasi gani Maafisa Ushirika kuweza kufanya shughuli zao kwa ufanisi, ikizingatiwa kuwa kumekuwa na msukumo mkubwa sana wa kuanzisha Vyama vya Ushirika?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo napenda kujibu swali la Mheshimiwa Josephine Johnson Genzabuke Mbunge Viti Maalum kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali inaendelea na jitihada za kuhamasisha uanzishwaji wa Vyama vya Ushirika katika sekta mbalimbali nchini ili kujenga umoja na mshikamano katika ukuzaji uchumi wa Watanzania kupitia Ushirika. Jitihada hizo pia hufanyika sambamba na kuweka mazingira wezeshi kwa maafisa ushirika ambao wanalo jukumu la kuhamasisha uanzishwaji na uendelezwaji wa Vyama vya Ushirika. Lakini pia utoaji mafunzo ya usimamizi na uendeshaji wa ushirika kwa viongozi na wanachama wa Vyama vya Ushirika.

Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha wa 2021/ 2022 Serikali kupitia Tume ya Maendeleo ya Ushirika Tanzania ilitenga jumla ya shilingi bilioni 2.7 kwa ajili ya: -

(i) Kununua magari 13 ambayo taratibu za manunuzi zipo katika hatua za mwisho, pikipiki 137 zimenunuliwa ili kuwezesha ofisi za Warajisi Wasaidizi wa Mikoa 26 ya Tanzania Bara kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi;

(ii) Mafunzo ya usimamizi wa Vyama vya Ushirika nchini kwa Maafisa Ushirika 184 yametolewa;

(iii) Kutoa mafunzo ya uendeshaji wa Vyama vya Ushirika kwa maafisa ushirika 100;

(iv) Kuunda Mfumo wa TEHAMA utakaowezesha ufuatiliaji na usimamizi wa Ushirika nchini; na

(v) Kuendelea na kazi za usimamizi na kaguzi za mara kwa mara katika Vyama vya Ushirika 9,185.

Mheshimiwa Spika, Serikali itaendelea kuhakikisha kwamba elimu ya kutosha inatolewa kwa viongozi na wanachama wa Vyama vya Ushirika nchini. Aidha, Serikali haitasita kuwachukulia hatua kali viongozi wote wasio na uadilifu ili kuwezesha wanachama wa Ushirika wananufaika na ushirika wao.
MHE. JOSEPHINE J. GENZABUKE aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itajenga Kituo cha Afya Kata ya Kagera/Nkanda Wilayani Kasulu?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE) alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais- TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Josephine Johnson Genzabuke Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo.

Mheshimiwa Spika, Serikali katika mwaka wa fedha 2021/2022 ilipeleka Shilingi Bilioni 1.4 kwenye Halmashauri ya Wilaya Kasulu kwa ajili ya ujenzi wa Vituo vya Afya vya Kitanga, Nyenge na Rungwe Mpya. Ujenzi wa vituo hivi upo hatua mbalimbali.

Mheshimiwa Spika, Serikali katika mwaka wa fedha 2023/2024 itatenga fedha Shilingi Milioni 500 kutoka kwenye mapato ya ndani ya Halmashauri kwa ajili ya ujenzi wa Kituo cha Afya katika Kata ya Kagera/Nkanda.
MHE. JOSEPHINE J. GENZABUKE aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itatoa vibali ili kuajiri walimu na kuondoa upungufu wa walimu uliopo nchini?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE) alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais - TAMISEMI naomba kujibu swali la Mheshimiwa Josephine Johnson Genzabuke, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imeendelea kutatua na kukabiliana na changamoto ya upungufu wa walimu nchini kwa kutoa vibali vya ajira za walimu ambapo kwa mwaka wa fedha 2020/2021 iliajiri walimu 14,949 na mwaka wa fedha 2021/2022 iliajiri walimu 9,800.

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali itaendelea na mpango wa kuajiri watumishi wakiwemo walimu ili kukabiliana na upungufu kulingana na mahitaji na upatikanaji wa fedha.
MHE. FLORENCE G. SAMIZI K.n.y. MHE. JOSEPHINE J. GENZABUKE aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itamaliza tatizo la ukosefu wa Watumishi wa Kada mbalimbali katika Hospitali nchini pamoja na ukosefu wa Vifaa tiba?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE) alijibu: -

Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Kwa niaba ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Josephine Johnson Genzabuke Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali katika mwaka wa fedha 2020/2021 iliajiri Watumishi wa kada za afya 2,726 ambao walipelekwa kwenye vituo vya kutolea huduma za afya nchini. Aidha, katika mwaka wa fedha 2021/2022 Serikali inatarajia kuajiri watumishi 7,612 wa kada mbalimbali za afya ambao watapelekwa kwenye Halmashauri zote nchini.

Mheshimiwa Spika, Ofisi ya Rais - TAMISEMI imetenga Shilingi Bilioni 69.95 kwa ajili ya ununuzi wa vifaa tiba kwa Zahanati, Vituo vya Afya na Hospitali za Halmashauri zilizokamilika.
MHE. SHALLY J. RAYMOND K.n.y. MHE. JOSEPHINE J. GENZABUKE aliuliza: -

Je, ni lini Serikali italeta Sheria Bungeni kuruhusu Halmashauri kuzikopesha SACCOS za vijana na wanawake?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE) alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Josephine Johnson Genzabuke, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, mikopo ya asilimia 10 inatolewa kwa mujibu wa kifungu cha 37A cha Sheria ya Fedha za Serikali za Mitaa Sura ya 290. Kifungu hicho kimeeleza kwamba Halmashauri zote zinapaswa kutenga asilimia 10 ya mapato yake ya ndani kwa ajili ya mikopo isiyo na riba kwa vikundi vilivyosajiliwa vya Wanawake, Vijana na Watu wenye Ulemavu.

Mheshimiwa Spika, mikopo ya SACCOS huendeshwa kwa Sheria ya Huduma Ndogo za Fedha (Vyama vya Ushirika wa Akiba na Mikopo) ya mwaka 2019 ambapo mikopo hiyo hutolewa kwa wanachama wa SACCOS kwa riba. Hivyo, mapendekezo ya kurekebisha Sheria ya Fedha za Serikali za Mitaa Sura ya 290 ili kuzikopesha SACCOS kutaondoa kusudio la kutoa mikopo isiyo na riba kwa wanawake, vijana na watu wenye ulemavu.
MHE. JOSEPHINE J. GENZABUKE aliuliza: -

Je, lini Serikali itajenga barabara kwa kiwango cha lami kutoka Simbo hadi Kalya?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE) alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Josephine Johnson Genzabuke, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imeanza maandalizi kwa ajili ya ujenzi wa barabara ya Simbo – Kalya yenye urefu wa kilometa 234 kwa kuanza na kazi ya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina wa Daraja la Lower Malagarasi ambalo lipo katika barabara hii. Kazi za Usanifu zinaendelea na zinatarajiwa kukamilika Novemba, 2023. Baada ya Usanifu kukamilika Serikali itatafuta fedha kwa ajili ya kuanza ujenzi wa daraja na kuanza kazi ya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina kwa barabara ya Simbo – Kalya urefu wa kilometa 234.
MHE. JOSEPHINE J. GENZABUKE aliuliza: -

Je, lini Serikali itamaliza ujenzi wa Kituo cha Afya cha Kata ya Kizazi – Kibondo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE) alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa kuwa leo ni siku yangu ya kwanza kusimama mbele ya Bunge lako Tukufu kwa takribani miezi mitatu tangu nipate changamoto za kiafya, naomba kwa dhati ya moyo wangu nitoe shukrani zifuatazo: -

Mheshimiwa Spika, kwanza, namshukuru Mwenyezi Mungu, Mwingi wa Rehema aliyenijalia uhai, afya njema na kuniwezesha kurejea kuungana na Waheshimiwa Wabunge wenzangu katika kulijenga Taifa letu la Tanzania.

Mheshimiwa Spika, pili, kwa dhati ya moyo wangu, nitumie fursa hii ya Bunge tukufu kumshukuru sana Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa namna ambavyo ameniwezesha kwa upendo wake na wema wake kwangu na Watanzania wote na kuniwezesha kupata matibabu na hatimaye kurejea kuendelea kulijenga Taifa letu. Namshukuru sana Mheshimiwa Rais na tunamwombea sisi Watanzania aendelee kuwa na afya njema aendelee kuliongoza Taifa letu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tatu, nawashukuru sana Viongozi Wakuu wa Serikali, nikianza na Mheshimiwa Dkt. Philip Isdor Mpango, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ninamshukuru sana. Namshukuru sana Mheshimiwa Kassim Majaliwa Majaliwa, Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Namshukuru sana kwa ushirikiano wake.

Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana wewe mwenyewe binafsi Mheshimiwa Dkt. Tulia Ackson, Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Spika wa viwango mwenye upendo. Ninakushukuru sana sana kwa ushirikiano wako na Mwenyezi Mungu akubariki sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nitumie fursa hii kumshukuru Bosi wangu, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, Mheshimiwa Angellah Jasmine Kairuki, alikuwa nami muda wote na katika kila hatua ya matibabu yangu; na pia Mheshimiwa Naibu Waziri mwenzangu, Mheshimiwa Deo Ndejembi; Katibu Mkuu Ndunguru; na timu nzima ya Ofisi ya Rais TAMISEMI; ninawashukuru sana.

Mheshimiwa Spika, nawashukuru sana Mawaziri wote, Waheshimiwa Naibu Mawaziri wote na Waheshimiwa Wabunge wenzangu, nawashukuru sana, sana kwa upendo wenu na Mwenyezi Mungu awabariki sana kwa maombi yenu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nawashukuru viongozi wangu wa Chama cha Mapinduzi wa Jimbo langu la Wanging’ombe, Baraza la Madiwani, viongozi wa Serikali, wananchi wenzangu wa Jimbo la Wanging’ombe kwa maombi yao siku zote. Niwahakikishie kwamba nitaendelea kuchapa kazi kuijenga Wanging’ombe na pia kujenga Taifa letu la Tanzania.

Mheshimiwa Spika, mwisho lakini siyo kwa umuhimu, namshukuru sana mke wangu mpenzi, Alafisa Moses Dugange kwa namna alivyokuwa karibu nami katika kipindi chote cha matibabu. Ninawashukuru sana, sana na Mungu awabariki sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo, sasa naomba nianze kujibu maswali ya Waheshimiwa Wabunge.

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Josephine Johnson Genzabuke, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha wa 2023/2024, Serikali imetenga shilingi milioni 500 kwa ajili ya ujenzi wa Kituo cha Afya katika Kata ya Kizazi Halmashauri ya Wilaya ya Kibondo. Bajeti hiyo itatekeleza ujenzi wa jengo la wagonjwa wa nje (OPD), jengo la maabara, jengo la wazazi, jengo la upasuaji na jengo la kufulia, ahsante sana.
MHE. JOSEPHINE J. GENZABUKE aliuliza:-

Je, Serikali ipo tayari kuzungumza na wenye viwanda vya mbolea ili kuwe na ujazo wa kilo tofauti na 50?

NAIBU WAZIRI WA KILIMO alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyeketi, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Josephine Johnson Genzabuke, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mujibu wa Kanuni ya 32, (4) na (5) pamoja na Kanuni ya 33(1) ya Kanuni za Mbolea za mwaka 2011, wazalishaji au waingizaji wa mbolea wanaruhusiwa kufungasha mbolea katika ujazo unaofaa kwa watumiaji mbalimbali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mbolea zilizo katika hali ya yabisi (solid fertilizers) zinapaswa kufungashwa katika ujazo wa kilo tano, 10, 25 na 50. Mbolea zilizo katika hali ya kimiminika (liquid fertilizers) zinapaswa kuwa katika ujazo wa mililita tano, 10, 20, 50 na 100. Aidha, visaidizi vingine vya mbolea kama vile chokaa mazao (agricultural lime) na jasi (gypsum) hufungashwa katika ujazo wa kilo tano, 10, 20, 50 na 100.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali itaendelea kusimamia wazalishaji wa mbolea kuzalisha mbolea kulingana na mahitaji.
MHE. JOSEPHINE J. GENZABUKE aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itatekeleza ahadi ya ujenzi wa Kituo cha Afya Kata ya Mulungu Jimbo la Muhambwe?
NAIBU WAZIRI OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI) alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI naomba kujibu swali la Mheshimiwa Josephine Johnson Genzabuke, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Katika Mwaka wa Fedha wa 2023/2024 Serikali imetenga bajeti ya shilingi milioni 500 katika Halmashauri ya Wilaya ya Kibondo kwa ajili ya ujenzi wa Kituo cha Afya Kizazi. Aidha wananchi wa Kata ya Kizazi wamejenga jengo la OPD hadi kufikia hatua ya lenta.

Mheshimiwa Spika, Serikali itaendelea kutenga bajeti kwa ajili ya ujenzi wa Vituo vya Afya kwenye Kata za kimkakati kote nchini ikiwemo Kituo cha Afya katika Kata ya Mulungu.