Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Lucy Thomas Mayenga (7 total)

MHE. LUCY T. MAYENGA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali dogo la nyongeza. Kwa kuwa uchumi wa nchi yetu umekuwa ukiimarika na mikakati ambayo imeendelea ambayo imekuwa ikifanywa hivi sasa inaonyesha kwamba nchi yetu itakuwa ni Taifa bora. Lakini vilevile kwa kuwa idadi ya watu inazidi kuongezeka na kwa miaka mingi ya nyuma Serikali yetu imekuwa ikisomesha Watanzania wengi katika nchi mbalimbali lakini baadhi ya Watanzania ambao ni Madaktari waliamua kuondoka hapa Tanzania na kwenda nje kwa ajili ya sababu kuwa zikiwa ni maslahi.
Je, Serikali ina mkakati gani maalum wa kuweza kuwarejesha Madaktari hawa ambao sasa wamepata uzoefu mkubwa.
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza ni kweli kwamba Serikali yetu imekuwa ikiongeza udahili kwa ajili ya kufundisha Watanzania wenzetu kwenye fani za tiba kwa kiasi kikubwa sana katika miaka ya hivi karibuni. Hivi tunavyozungumza hapa kwa mwaka mmoja tuna uwezo sasa hivi wa kuzalisha takribani Madaktari wa tiba 1,000. Hiki ni kiasi kikubwa sana na ni uwekezaji mkubwa sana ambao umefanywa na Serikali yetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na kutambua uwekezaji huu mkubwa uliofanyika ni kweli nakiri kwamba tumekuwa na uwezo mdogo wa kuwa- absorb kwenye system wale wote wanaohitimu kwenye fani za tiba na utabibu kwa ujumla wake. Serikali ya Awamu ya Tano tayari ina mkakati mahsusi wa kuhakikisha tunaongeza kiasi cha Madaktari ambao wanakuwa absorb kwenye system ya kutolea huduma za afya ili tuwe na Madaktari wengi zaidi ambao wanafanya kazi kwenye Serikali.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu maslahi mpaka hivi ninavyoongea hapa Madaktari ni mojawapo ya fani za kitaalamu hapa nchini ambao wanalipwa vizuri sana kuliko wengine. Hivi ninavyoongea Daktari anayemaliza masomo yake ya Degree analipwa vizuri sana kuliko ukilinganisha na fani zote zile kwenye Serikali na tunavyoongea kwenye sekta binafsi sasa wanaanza kupata shida kuajiri Madaktari ambao wamehitimu kwa kuwa ndani ya Serikali maslahi ni mazuri zaidi kuliko hata yale ya kwenye sekta binafsi na ni jambo la kujivunia. Kwenda nje pia siyo jambo la kusema ni baya, kwa sababu wa navyoenda wengi wao wanakaa miaka mitatu, miaka sita wanarudi nchini kuja kutoa tiba hapa na tayari wanakuwa wameshapata uzoefu wa kufanya kazi nje ya nchi. Kwa hivyo, ni fursa na hatuwezi kuwabana kwa njia nyingine yoyote ile zaidi ya kusema tuboreshe maslahi ndani ya Serikali ili Madaktari waweze kutoa huduma kwa Watanzania wengi hapa nchini.
MHE. LUCY T. MAYENGA: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa majibu ya Waziri. Kama majibu yalivyo yanadhihirisha kabisa kwamba kuwataka au watu wa Kahama kuendelea na umeme wa jenereta wakati Watanzania wote na yeye mwenyewe anafahamu kwamba Wilaya ya Kahama ni kati ya Wilaya ambazo ni kitovu cha uzalishaji wa chakula especially mchele na kwa jinsi hiyo kuwazuia kwa namna moja au nyingine wasifanye uzalishaji wenye tija. Nimeshukuru amesema kwamba utaratibu umeanza wa kuwapatia umeme wa uhakika. Ningetamani sana kuona kuwa hili linapatiwa ufumbuzi haraka na ningetaka sasa aseme ni lini ambapo umeme huo utapatikana kwa uhakika?
Mheshimiwa Spika, swali la pili, tatizo la kukatika kwa umeme siyo la Kahama peke yake, ni la maeneo mengi sana Tanzania, likiwepo eneo la Kigamboni, Dar es Salaam, ambapo kule mnaamka mnaulizana kwenu upo? Leo umeme upo? Mheshimiwa Naibu Waziri wa TAMISEMI anaweza kutusaidia kujua kwamba eneo la Kigamboni sasa litaacha kukatiwa umeme kila siku, kila mara especially siku za Jumapili kuanzia lini? Ahsante.
WAZIRI WA NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Spika, kwa swali la kwanza la Mheshimiwa Mbunge ni kwamba, Kahama imeunganishwa kwenye lane ya Shinyanga ambayo msongo wake ni wa KV 33 na sisi tunajua kwamba umeme huo ni mdogo, ulitosha kwa wakati huo lakini siyo kwa sasa. Kwa hiyo kinachofanyika, nadhani hata kabla ya bajeti yangu kwisha, Ijumaa atawaona watu wa TANESCO wako pale, wameondoka leo, wamekubaliana na Mgodi wa Buzwagi, Buzwagi ndiyo iko karibu sana na Kahama. Kwa hiyo, umeme utavutwa kutoka Buzwagi 33 KV kwenda Kahama. Kwa hiyo, huku watakuwa na wa Shinyanga, huku watakuwa na wa Buzwagi, tatizo hilo litakwisha.
Mheshimiwa Spika, mbali ya hilo la umeme kukatika katika, ndugu zangu Waheshimiwa Wabunge na Watanzania wote lazima tufanye maamuzi. Tukiwa tunajenga hii miundombinu kuna wakati lazima tuzime umeme. Watu wa upande wa Ziwa Victoria kila Jumapili umeme unakatika, lakini wanatangaziwa kwamba tunajenga miundombinu ya kusafirisha umeme mwingi kutoka Iringa mpaka hapa Dodoma, tunatoka kwenye KV 220 mpaka KV 400. Tunatoka hapa Singida, Shinyanga mpaka Nyakanazi KV 400. Sasa hii tunaizindua Septemba.
Mheshimiwa Spika, sehemu zingine Tanzania nzima, hata ndugu zangu wa Arusha waliokuwa wanasema umeme unakatikakatika, tunajenga kutoka Singida kwenda Arusha KV 400, halafu kutoka Da es Salaam kupitia Tanga kwenda Arusha KV 400. Hiyo ndiyo TANESCO mpya. Ahsante.
MHE. LUCY T. MAYENGA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali dogo la nyongeza. Kwa kuwa suala hili la Kipunguni Dar es Salaam kutokana na jibu la msingi limekuwa likileta malalamiko mengi na limekuwa likizungumzwa kwa muda mrefu na kwa kuwa ofisi ya Wizara hii ipo Dar es Salaam:-
Je, kwa nini Serikali hasa Mheshimiwa Naibu Waziri asitoke yeye aende Kipunguni pamoja na wataalam ili aweze kupata majibu ya kujiridhisha badala ya kumsubiri Mheshimiwa Mbunge yeye ndiyo alete majibu hapa Bungeni.
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Naibu Spika, wananchi hawa wa Kipunguni walishafika ofisini kwetu, nikaondoka nao nikaenda kwa acting CEO wa Uwanja ule wa Ndege na baada ya kujadiliana kwa mpana ndiyo hayo majibu ninayoyatoa hapa yanatokana na vikao hivyo. Mimi mwenyewe nimekutana nao ofisini baada ya wao kuja na baadaye tulifanyia vikao Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Dar es Salaam tukiangalia maeneo yote yale matatu ya Kipunguni, Kipawa na Kigilagila. Kwa hiyo, namhakikishia kwamba hicho nachokisema hapa ni kutokana na kile nilichokifanyia kazi. Ndiyo maana nasema huu utofauti kati yangu na Mheshimiwa Mbunge wa figure alizoleta hapa ningependa nipate ushahidi wa hicho anachokiongea.
Mheshimiwa Naibu Spika, nachokisema, waliobakia ni 742 na tutawalipa mara fedha zitakapopatikana, ni kutokana na kazi kubwa niliyoifanya katika eneo hilo. Hata hivyo, bado nitaendelea kuliangalia suala hilo nikishirikiana na hawa Waheshimiwa Wabunge ikiwa ni pamoja na Mheshimiwa Kaluwa kuhakikisha kwamba hicho tunachokisema ndicho sahihi.
MHE. LUCY T. MAYENGA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Kwa kuwa tatizo hili la maji lipo kwenye categories mbalimbali kwa nchi nzima, wapo watu ambao hawana kabisa miradi katika maeneo yao kwa sisi Wabunge hapa ndani Bungeni, lakini pia yapo maeneo ambayo miradi ipo lakini haijakamilika kutokana na sababu mbalimbali, lakini yapo maeneo katika nchi yetu ambayo maji yanapatikana lakini kumekuwa na manung’uniko ya chini chini ya wananchi kwamba jinsi bili zinavyotoka kunakuwa hakuna usawa.
Mheshimiwa Naibu Spika, matatizo haya yamekuwa yakisemwa kwa wananchi kwa muda mrefu na yamekuwa takribani kila Mbunge anaposimama hapa wengi wamekuwa wakigusia kuhusu tatizo la kutokuwa na usawa wakati wa kutoa bili.
Mheshimiwa Naibu Spika, Wizara badala ya kusema kwamba wananchi au sisi Wabunge twende kwenye bodi kutoa malalamiko au wananchi waende kule kwenye taasisi za kutoa huduma ili kwenda kupeleka malalamiko yetu.
Je, Wizara hii haioni sasa umefika wakati kuchukulia tatizo hili kwa ukubwa wake kama tatizo la kitaifa, kuunda timu maalum itakayopita kila maeneo na kuweza kujua kwamba maeneo haya yana matatizo haya tuweze kuyatatua vipi na eneo hili matatizo yake tuweze kutatua vipi? (Makofi). Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. (Makofi)
WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Lucy Mayenga ameuliza swali zaidi ya moja; anazungumzia habari ya matatizo ya upatikanaji wa maji, lakini pia anachanganya tena na masuala ya bili. Sasa ni vitu viwili tofauti. Masuala ya upatikanaji wa maji, Serikali inaendelea kutekeleza.
Mheshimiwa Naibu Spika, suala hili la matatizo ya bili nimeshalitolea majibu, labda nirudie kwa kuweka msisitizo. Ni kwamba Wizara inatambua yapo maeneo ya mtu mmoja mmoja kulalamikia bili, siyo kwamba kila mmoja analalamikia bili. Sasa nasema, kama ni isolated cases, hatuwezi kuchukulia kama ni tatizo la Kitaifa. Hili ni tatizo la mtu mmoja ambaye ana tatizo, amepewa bili ya miezi mitatu hajapata maji.
Sasa hili naomba tulifuatilie kwa maana ya kwa huyo mtu ambaye anatuletea ni isolated case tuishighulikie. Siyo jambo la kusema tulitolee mwongozo kama Taifa kwa maana ya kwamba tumeshakubaliana kwamba maji ili yawe endelevu, upatikanaji wake ni lazima tuchangie.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, kulipa bili ni lazima ili tuwe na uhakika wa kuwa na maji. Sasa kama kuna matatizo mahali, tutayashughulikia kwa mujibu wa sheria na kwa mujibu wa taratibu tulizojiwekea.
MHE. LUCY T. MAYENGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipatia nafasi ya kuuliza swali dogo la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa Wizara hii imekuwa ikijitahidi sana kwenye suala zima la usambazaji wa umeme katika maeneo mbalimbali kupitia miradi ya REA pamoja na taratibu nyingine.
Je, Wizara hii iko tayari sasa kuweza kuwasaidia wananchi wetu wa Wilaya ya Shinyanga Mjini na hasa Jimbo langu la Shinyanga ambako natoka ambapo tunakabiliwa na tatizo kubwa sana la kukatika sana sana kwa umeme; kwa taarifa nilizonazo ni kwamba kituo cha kusambazia umeme cha Ibadakuli kimezidiwa nguvu.
Je, Serikali ipo tayari sasa kuweza kusaidia kituo hiki kukiongezea nguvu ili umeme wa uhakika uweze kupatikana? Ahsante sana.
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa fursa hii. Ni kweli kufuatia utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa msongo wa KV 400 kutoka Iringa mpaka Shinyanga, mradi ule una taratibu za upanuzi wa vituo vya kupokea na kupoozea umeme kimojawapo ikiwa ni Ibadakuli.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naomba nimthibitishie Mheshimiwa Mbunge kwamba kituo kile pamoja na kuzidiwa, mradi huu wa kukikarabati na kukiwezesha kutoka kwenye KV 220 na kufika KV 400 utakwenda kutatua tatizo la wananchi wake wa Shinyanga ambako amekuwa akifuatilia sana mahitaji wa umeme. Ahsante.
MHE. LUCY T. MAYENGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali dogo la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imekuwa ikipata takribani shilingi bilioni 5 kutokana na meli za nje zinazoingia Tanzania kwa ajili ya kufanya uvuvi mkubwa. Je, Serikali sasa na hasa Wizara hii iko tayari kuanzisha bandari maalum ya uvuvi kwenye Bahari ya Hindi ambayo itakuwa inasaidia meli kubwa kutoka nje zinazokuja kwa ajili ya uvuvi ziweze kufanya kazi ili Serikali iweze kupata faida? Kwa sababu sasa hivi meli hizi kubwa zimekuwa zinapata takribani shilingi bilioni 500 na nchi yetu imekuwa ikipata shilingi bilioni 5 tu. Je, Serikali iko tayari kuchukua wazo hili kuanzisha bandari hiyo ili nchi yetu iweze kufaidika? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ENG. ATASHASTA J. NDITIYE):
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Lucy Mayenga, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali tuko tayari kuchukua wazo hilo na tutashirikiana kwa karibu sana na Wizara ya Uvuvi na Mifugo kuhakikisha kwamba wanatuonesha maeneo stahiki kwa ajili ya kujenga bandari hizo.
MHE. LUCY T. MAYENGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipatia nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Watumiaji wa madawa ya kulevya hivi sasa Serikali kutokana na jitihada kubwa na nzuri za mapambano dhidi ya madawa sasa hivi wamegeuza kibao wameanza kutumia dawa kama pethidine, benzodiazepine dawa hizi zimekuwa zikisabisha kwamba watu ambao wanatumia madawa kulevya madawa hakuna wanatumia dawa hizi. Je, Serikali iko tayari sasa kuleta sheria ambazo zitakuwa kali sana ili kuweza kudhibiti usambazaji na manunuzi ya dawa hizi ili zifanane na jitihada kubwa na nzuri zinazofanywa na Mamlaka ya Udhibiti wa Madawa ya Kulevya Tanzania?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali zuri la Mheshimiwa Lucy Mayenga, Mbunge Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kama nilivyosema kwenye majibu yangu ya awali tumeanza kuona ongezeko
la madawa ya hospitali ama prescription drugs zikianza kutumika ndivyo sivyo kama mbadala wa madawa haya ya kulevya. Sisi kama Wizara tumeanza kuchukua hatua na ni mambo ambayo tunaendelea kuyafanya kama ndani ya Serikali. Kuanza kutoa elimu kama ambayo nimeitoa hapa kwamba hizi dawa zinatakiwa zitumike kwa malengo ambayo yamekusudiwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini la pili tumeanza sasa kuweka utaratibu mzuri wa kufanya udhibiti wa hizi dawa kuhakikisha pale tangu zinapoingia mpaka kwa mtumiaji wa mwisho. Niseme kwamba uratibu huu tumeshauanza ndani ya Wizara na tutaendelea nao. Sheria tulizonazo za matumizi ya madawa ya kulevya zinaongelea vilevile hizi dawa za prescription drugs na sheria ni nzuri tu zinajitosheleza kwa adhabu.