Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Augustine Vuma Holle (1 total)

MHE. AUGUSTINO V. HOLLE: Mheshimiwa Spika, kwanza nishukuru kwa majibu mazuri ya Naibu Waziri, lakini nina swali moja la nyongeza. Kwa kuwa kama Mkoa bado hatujaunganishwa kwenye Grid ya Taifa na kumekuwa na tatizo kubwa sana la kukosa nishati hii muhimu na kupelekea mkoa wetu kuwa miongoni mwa mikoa maskini; sasa je, Wizara ya Nishati imejipangaje vipi kuhakikisha kwamba inakamilisha kwa haraka na kwa ufanisi mradi wa REA awamu ya tatu katika Mkoa wa Kigoma ambao kimsingi umezinduliwa muda umeenda sana katika Kijiji au Kata ya Lusese? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Naomba nimpongeze sana Mheshimiwa Mbunge kwa kazi nzuri ya kufuatilia changamoto ya nishati. Ni kweli Mkoa wa Kigoma pamoja na Mkoa wa Katavi kazi za upelekaji umeme kupitia mradi wa REA awamu ya tatu mzunguko wa kwanza zilichelewa kutokana na matatizo ambayo yalikuwa nje ya uwezo wa Wizara yetu ya Nishati pamoja na Wakala wetu Vijijini. Hata hivyo mradi huo umeshazindua rasmi na mkandarasi anaendelea na kazi ya survey na watakamilisha hivi karibuni.
Mheshimiwa Spika,aomba niwatoe hofu wakazi wa Mkoa wa Kigoma pamoja na Katavi kwamba kwa kweli kwa maelekezo ya Serikali na mkandarasi aliyeteuliwa ana uwezo na hivyo atafanya kazi kwa haraka iwezekenavyo nakushukuru. (Makofi)