Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Fedha na Mipango

Hon. Shally Josepha Raymond

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Fedha na Mipango

MHE. SHALLY J. RAYMOND: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa nafasi hii. Kipekee kabisa namshukuru Mungu kwa kutupa sisi sote zawadi ya uhai, tupo hapa tunazungumza mambo ya maendeleo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nakupongeza tena na niungane na mwenzangu aliyetangulia kwa wewe jana kupokea ripoti zile mbili na kuzikabidhi Serikalini, Ripoti ya Natural Gas na ile Ripoti ya Uvuvi. Tumeona kazi yako na nia yako njema katika kudhibiti mianya yote ambayo inatupotezea mapato katika nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba nichukue nafasi hii nimpongeze sana Mheshimiwa Waziri wa Fedha na niipongeze hotuba yake ambayo kwa kweli imeandikwa vizuri na tumeielewa na ndiyo maana unaona mijadala yote iko moto.

Mheshimiwa Spika, kabla sijasimama nilipokuwa najiandaa ilinilazimu kwenda kule Library nikachukua Hansard ya mwaka 2017 ambayo pia wenzetu walikuwa wamechangia. Niseme wazi kwamba nimei-miss michango yao na sijui kwa nini mpaka leo hatupati michango ya upande wa pili? Kwa nini nimevutiwa kwenda kuchukua michango yao? Nilitaka kuona mambo waliyoyazungumzia mwaka 2017 leo yameendaje? Mengi waliyokuwa wamelalamikiwa yametekelezeka na lazima niseme wazi kwamba Mheshimiwa Waziri Mpango mambo yako yako vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Wizara ya Fedha ni moyo wa uchumi na ndiyo maana wote wanaozungumza wanaipiga mawe, lakini tunasahau kwamba kuna mambo mazuri yamefanyika hapa katikati. Mwaka 2017 kipindi kama hiki kila mtu alikuwa analalamika bei juu, walio kwenye Mwezi Mtukufu wa Ramadhani vyakula viko juu, sukari hakuna, mahindi hakuna, mchele ghali; lakini leo kila mtu amekaa raha mustarehe. Kila kitu kinapatikana, Mwenyezi Mungu amesikia kilio chetu, uji upo, mchele upo na sukari ipo. Mambo hayo yote wanadamu tumezoea kila siku kulalamika; hata mambo mazuri hamwoni sasa? Hata mvua zilizokuja hamzioni? Hata watu wanafuturu vizuri, wakiwepo na Waheshimiwa Wabunge wanafuturishwa kila leo, hawaoni? Bado wanalalamika. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mtu akiwa na hulka ya kulalamika, hakuna namna unavyoweza kumbadilisha, lakini namshukuru Mungu mfungo huu umekuwa mzuri. Niseme kwamba na hiyo iweze kumpa pia, ahueni huyu Mheshimiwa Waziri wa Fedha.

Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo, naomba niende katika ule ukurasa wa 87 wa Hotuba ya Mheshimiwa Waziri unaozungumzia uratibu wa mikakati ya kupunguza umasikini. Nilipokwenda Library nilichukua pia kitabu cha Wizara hiyo cha mwaka 2017, kama hiki na nikaenda ukurasa huo huo katika uratibu wa mikakati ya kupunguza umaskini. Kilichozungumzwa mwaka 2017, mwaka jana ilikuwa ukurasa wa 76 mwaka huu ni 87, hayapishani sana. Ni mambo mazuri ndiyo, lakini yote ni kwenye makaratasi.

Mheshimiwa Spika, mwananchi wa kawaida ukimwambia unapunguziwa umaskini kwa kuzidi kuboresha au kuandika maandiko ya SDGs, maandiko ya Poverty Monitoring System, tunazidi kuboresha mifumo, tunazidi kuboresha, haimuingii akilini. Nami pia niliyetumwa hapa na wanawake wa Kilimanjaro wanaonisubiri waone tumepiga hatua kwenye kupunguza umaskini, naomba kutamka kwamba sielewi. Ni kwa nini sasa sielewi?

Mheshimiwa Spika, nilitaraji sasa baada ya wasomi kuangalia hizo SDGs waje na pendekezo au waje na maagizo kwa Serikali; jamani, tumeamua kupunguza umaskini, tunaomba au tunaagiza sasa tupeleke projects ambazo wananchi watazisimamia na wanawake walio hapa wengi ni Viti Maalum, wanajua ambavyo wanaombwa kule kwenye maeneo yao semina ya kujifunza ujasiriamali, semina za kuboresha maeneo, za mazingira, semina za ufugaji, l akini wanafuga nini? Hakuna mifugo iliyoboreshwa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, namwomba Waziri wangu wa Fedha akatuzungumzie kunakopatikana mitamba bora, wanawake wakopeshwe. Miaka ya nyuma Mwalimu Nyerere peke yake katika awamu zote aliweza kutoa projects ambazo zinafanya kazi watu wakarejesha. Ilikuwa inaitwa kopa ng’ombe lipa ndama; na mpaka leo ndiyo iliyowatoa watu. Watu waliweza kuboresha maisha yao, wanapata maziwa, wanapata samadi, wanapata nyama nzuri na ngozi.

Mheshimiwa Spika, ni Mwalimu tu katika awamu zote tano, yeye alitoa projects na zikalipa mpaka leo. Ndiyo akaweza kuchanganya wale ng’ombe wa kiasilia na ng’ombe wa kisasa. Maeneo mengi yaliyoboresha kipato ni yale ambayo yaliweza kufaidi mradi huo. Namwomba Mheshimiwa Waziri, Dkt. Mpango aangalie ni projects zipi zitaweza kwenda kuboresha kipato cha akinamama?

Mheshimiwa Spika, tumeona wanawake wanaingia kwenye VICOBA, Serikali inasema kwamba inakwenda kusimamia VICOBA, mnasimamiaje VICOBA ambavyo hamjui vimeanzishwaje? VICOBA hivyo ni vya kudunduliza, amechangia mmoja akasema na ile hela ya VICOBA sasa inakwenda kwenye kucheza kamari. Tunafanyaje? Tunatokaje hapo? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba wanawake hawa wapewe elimu ya VICOBA kila mara. Hapa wenyewe sisi, wengi wa Wabunge wako ni wasomi, lakini kila leo umejitahidi kutuletea semina za mambo mbalimbali ili tuweze kuendana na wakati. Sasa wanawake wale tunawapelekeaje semina hizo? Haitoshi kabisa kuzungumzia vitu vyao walivyoanza halafu tukasema tunasimamia SACCOS. Unasikia Serikali inaingia kwenye SACCOS. SACCOS ni uanzishaji wa hiari. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nashukuru kwamba Serikali imeweza kwenda kuangalia wasiuze zile mali za SACCOS, lakini uanzishwaji wa SACCOS ni wa hiari. Wenyewe wanakaa wanakubaliana. Maeneo ambayo SACCOS zimeshamiri ni kule ambako hazijaingiliwa. Leo Serikali ukienda ukaingilia, umeharibu.

Mheshimiwa Spika, nakuomba, dakika chache zilizopita umesimama umetoa amri. Najua, amri yako au your wish ni kutekelezwa na ikitekelezwa kwenye hili jumba lako Tukufu wewe ndio umesema. Naomba siku moja ikupendeze, zile hela zinazotolewa au zilizowahi kutolewa na Marais siku za nyuma zikaenda kwa wanawake, zikaenda kukopeshwa, halafu zikaishia ziliko, mimi najua ziko kwenye benki kwenye suspense accounts. Tuma Tume yako fedha hizo zikakaguliwe, iwe ni NMB, iwe ni NBC, iwe ni CRDB, zile hela zirudi kwenye mzunguko. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, zile hela ni revolving funds, zirudi. Hazina inajua ni kiasi gani kilitoka. Mara ya mwisho tulipata mabilioni ya JK, mpaka leo yako wapi? Waliojifurahisha wameyafungia, zime-lock mahali. Utashangaa hata viongozi wakubwa au wake wa viongozi walienda na wao wakakopeshwa. Hivi walikuwa wanastahili hizo hela? Nakuomba, siku itakapokupendeza zile hela zirudi kwenye mzunguko, wanawake wakopeshwe, vijana wakopeshwe hela hiyo ikombolewe. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwenye ripoti tumeelezwa wazi ubia kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi, hili ni jambo jema. Naomba ubia huu usimamiwe na Serikali sasa iwe makini kuangalia ni jinsi gani ubia huu unaendeshwa. Tuna bahati moja nzuri sana ya kupata Wakaguzi wa Serikali ambao ni makini, ambapo tulikuwa huko nyuma na Uttoh, sasa hivi tuna Profesa Assad. Ukiona ripoti zake, ziko wazi, hakuna anapoficha. Pamoja na madaraka yake hayo makubwa, nafasi yake amepewa; tukitaka sasa kujua value for money kwenye projects inashindikana maana naona wataalam hawa hawapo.

Mheshimiwa Spika, mara nyingi ameagizwa, lakini amepewa majukumu na amefungwa mikono, hana namna ya kuajiri watu ambao wana uelewa kwenye eneo hilo. Sasa inamwia ngumu. Tunamhoji tunasema, aah, umemaliza ukaguzi sasa tunataka tuwe tena na ukaguzi ule mahususi…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa mzungumzaji)

Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Naunga hoja mkono.