Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi kwa mwaka wa fedha 2016/2017.

Hon. George Mcheche Masaju

Sex

Male

Party

Ex-Officio

Constituent

None

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi kwa mwaka wa fedha 2016/2017.

MWANASHERIA MKUU WA SERIKALI: Mheshimiwa Naibu Spika, namshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunipa fursa hii nami niweze kuchangia. Nianze kwa kusema tu kwamba naunga mkono hoja. Naomba nitoe ufafanuzi wa masuala matatu ya kisheria ambayo yamejitokeza hapa. La kwanza ni hili ambalo limekuwa likijirudia, nadhani na lenyewe linahitaji kutolewa ufafanuzi kila linapojirudia.
Mheshimiwa Naibu Spika, suala la ile Hati ya Rais ya mgawanyo wa madaraka kwa Mawaziri anaowateua; tumewahi kutoa ufafanuzi kwenye Bunge hili Tukufu na kwa sababu pengine Waheshimiwa Wabunge wanapenda kujua zaidi, nami nitaendelea kutoa ufafanuzi huu.
Mheshimiwa Naibu Spika, niseme kwamba hata kama ile hati ingechelewa kutolewa, kwa sababu Rais alipokuwa alikuwa anakamilisha Serikali yake, kutokuwepo kwa ile hati isingekuwa ni sababu kwamba Mawaziri na Serikali washindwe kuwa na Mwongozo wa kufanya kazi zao.
Mheshimiwa Naibu Spika, mwongozo wa Serikali na kama ilivyo kwa raia yeyote wa Tanzania, ni Katiba ya nchi, sheria zenyewe, sera zilizopo na Ilani ya Chama kinachotawala. Ndiyo maana hata Mawaziri walipokuwa wanafanya kazi yao kabla ya hiyo Hati ya Mgawanyo wa Madaraka yao haijatoka, hakuwahi kutokea mgongano wowote. Kama nilivyosema, kukitokea mgangano kwa mujibu wa ile sheria, Mahakama itasema tu kwamba hili liende kwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali. Mwanasheria Mkuu wa Serikali atakachokifafanua ndiyo itakuwa mwisho wa hilo suala.
Mheshimiwa Naibu Spika, nachukua fursa hii kulifahamisha Bunge lako Tukufu kwamba, Mheshimiwa Rais tayari ameshatoa hii Hati ya Mgawanyo wa Madaraka ya Mawaziri, kupitia tangazo la Serikali Namba 144, lililochapishwa tarehe 22 Aprili, 2016 na mwongozo huu siyo kama labda ndiyo unawaelekeza kwamba wafanye hiki, wasifanye hiki; siyo mpango kazi wala siyo strategic plan au plan yenyewe. Wenyewe unachokifanya, unatoa tu mgawanyo kwamba Wizara fulani itashughulika na hili.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mfano, nitoe mfano Wizara hii ya leo ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi, wao watashughulikia yafuatavyo, nitasoma kwa Kiingereza:-
(a) Policies on agriculture, livestock, fisheries, food security and cooperative and their implementation;
(b) Agriculture, livestock and fisheries land use planning;
(c) Agricultural research and extention services on agriculture, livestock and fisheries;
(d) Food security management;
(e) Crop warehouse licensing;
(f) Strategic food reserve management;
(g) Commodit exchange;
(h) Development of Societies and Cooperatives;
(i) Cooperative Savings and Credit Societies;
(j) Agriculture live stock and fisheries infrastructure development;
(k) Marketing and value addition for agriculture, livestock and fisheries products;
(l) Livestock and fisheries product development;
(m) Veterinary services;
(n) Fish farming;
(o) Perfomance, improvement and development of human resources under this Ministry; and
(p) Extra Ministerial Department, Parastatal Organization, Agencies, Programme and Projects under this Ministry.
Kwa hiyo, wenyewe huu haukuongozi kwamba kafanye hiki; ni mwongozo tu. Hilo la kwanza ambalo naomba Waheshimiwa Wabunge walifahamu, kwamba siyo kitu ambacho kinapaswa kiwe kinawasumbua sana.
La pili ambalo naomba kulitolea ufafanuzi ni hili suala la ripoti ya Tume iliyoundwa na Mheshimiwa Rais kuchunguza jinsi Operesheni Tokomeza ilivyoendeshwa. Tume hii iliundwa chini ya sheria inayoitwa Commission of Enquiry Act na Mheshimiwa Rais, hii Tume anapaswa aiunde pia kwa kutumia Government Notice. Kupitia Government Notice Namba 131 ya tarehe 2 Mei, 2014, aliunda hii Tume na Tume ikishaundwa kwa mujibu wa sheria hii, haileti ripoti yake Bungeni, inaundwa na Rais na ripoti yake inaenda kwa Rais.
Mheshimiwa Naibu Spika, hii Tume ilishamaliza kazi yake, iliripoti kwa Mheshimiwa Rais, naye akaelekeza na ana mamlaka chini ya sheria hiyo ya Commission of Enquiry Act kuamua kwamba hiki kitu kiwe public, yaani kiwe cha wazi au kibaki jinsi ilivyo. Alichokifanya, ameelekeza; kutokana na mapendekezo yalitolewa na ile Tume, zile Taasisi zinazohusika zishughulikie. Kwa mfano, Maliasili wana maelekezo yao; Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Idara ya Mashtaka ina maelekezo yao; Wizara ya Mambo ya Ndani, Jeshi la Polisi wana maelekezo yao na wanachukua hatua. Kwa hiyo, hakuna sababu ya kulileta humu, muiachie Serikali itekeleze hiyo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, la mwisho ninalotaka kutoa ufafanuzi ni hili suala la kesi ya Tawariq1. Baadhi ya Waheshimiwa Wabunge wamesema kwamba ilikuwa ni maamuzi yasiyozingatia sheria. Tusiilaumu Mahakama jamani. Mahakama haiwezi kufanya maamuzi halafu tukasema ni maamuzi yasiyozingatia sheria. Hata Mkurugenzi wa Mashtaka alipoamua kulitoa lile shitaka Mahakamani, alikuwa amezingatia mamlaka yake aliyonayo chini ya Ibara ya 59(b)(4) inayosema kwamba katika kutekeleza mamlaka yake, Mkurugenzi wa Mashtaka atakuwa huru, hataingiliwa na mtu yeyote au mamlaka yoyote na atazingatia mambo yafuatayo:-
Nia ya kutenda haki, kuzuia matumizi mabaya ya taratibu za utoaji haki na maslahi ya umma. Kwa hiyo, tuna kila sababu ya kuamini kwamba Mkurugenzi wa Mashtaka alipoondoa lile shauri Mahakamani, haya yamezingatiwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, la mwisho, mpaka sasa hakuna amri yoyote ya Mahakama iliyosema kwamba tulipe fidia ya shilingi bilioni mbili.
Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja.