Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa mwaka wa Fedha 2018/2019 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora

Hon. Kabwe Zuberi Ruyagwa Zitto

Sex

Male

Party

ACT

Constituent

Kigoma Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa mwaka wa Fedha 2018/2019 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora

MHE. KABWE Z. R. ZITTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, Manispaa ya Kigoma Ujiji ina changamoto kubwa ya mapato ya ndani. Mfano, mwaka 2016/2017 makadirio yalikuwa shilingi bilioni 3.3, lakini makusanyo yao yalikuwa bilioni 1.4 tu sawa na asilimia 42. Mwaka 2017/2018 makadirio ni billion 2.3 na mpaka sasa tumekusanya asilimia 33 tu na miezi imebaki miwili tu kabla ya mwaka wa fedha kwisha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hivi sasa ushuru wa masoko haukusanywi kwa sababu Katibu Mwenezi wa CCM amekataza wafanyabiashara kulipa tozo ya 50,000 kwa mwezi na Serikali ipo kimya. Serikali itoe kauli hapa Bungeni ili watendaji waende kukusanya ushuru. Shughuli zimesimama. Serikali ielekeze watendaji kukusanya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, fedha za Mfuko wa Maendeleo wa Wanawake na Vijana asilimia 10. Kwa miaka 24 sasa MSM zimekuwa zinatenga asilimia 10 kutoka mapato ya ndani lakini changamoto bado ni nyingi na zile zile, nadhani tubadili mfumo. Napendekeza kuwa fedha hizi zitekelezwe kupitia mfumo wa Hifadhi ya Jamii ambapo vikundi vya vijana na wanawake wanufaishwe na Mifuko ya Hifadhi ya Jamii na kupitia fedha hizi MSM zichangie asilimia 50 ya michango ya mwezi na vijana na wanawake wachangie asilimia 50 iliyobaki. Hii ingejenga tabia ya kuweka akiba na pia kuwezesha vijana na wanawake hawa kuwa na bima ya afya kupitia mifuko hii. Hii pia ingewezesha kuwepo na fedha za uwekezaji wa miradi ya kimkakati kati ya MSM na Mifuko ya Hifadhi ya Jamii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano, mwaka 2016/ 2017, MSM zilikusanya shilingi bilioni 544 ambapo asilimia 10 ya hizi ni bilioni 54 ambazo zingewekwa akiba kwenye mifuko. Kwa kuwa vijana na wanawake wangechangia asilimia 50 ya michango yao, jumla ya fedha za michango zingefika bilioni 108. Hizi zingekuwa zinaongezeka kila mwaka (2017/ 2018 shilingi bilioni 687, mwaka 2018/2019 bilioni 735) na hivyo kujenga mfuko mkubwa ambao fedha zinatunzwa vizuri kuliko sasa ambapo fedha nyingi hupotea.

Mheshimiwa Mwenyekiti, napendekeza tufanye hili ili kulinda fedha hizi kwani zingekuwa na uhakika kwani mifuko ingefuatiliwa, ingejenga utamaduni wa kuweka akiba kwa watu wetu na ingewezesha watu wetu kupata bima ya afya na kupata mikopo yao kupitia mifuko hii. Wataalam walitazame hili jambo la kimaendeleo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, usimamizi wa fedha MSM; kuna changamoto kubwa kuhusu uwezo wa watendaji wetu kufanya kazi na Madiwani, hawasikilizi, hawajali na dharau. Manispaa ya Kigoma Ujiji ni ushahidi tosha wa uzembe wa watendaji kupelekea kupata hati chafu. Rejea barua ya Meya wa Manispaa kwa TAMISEMI tarehe 30 Juni, 2017 kumb na. A20/448/Vol.11/7) na majibu kutoka TAMISEMI (15 Septemba, 2017) kumb. RALG(PCF.5211).

Mheshimiwa Mwenyekiti, barua hizi pamoja na barua nyingine zote zilionesha malalamiko dhidi ya watendaji. Manispaa iliomba Taasisi ya Wajibu ya Bw. L. Utouh kutusaidia kupata ufumbuzi. Watendaji hawakutekeleza kabisa ushauri. Ukisoma ukurasa wa 270-272 wa Taarifa ya CAG utaona sababu za hati chafu zote zinahusu ufuatiliaji wa watendaji. TAMISEMI haikumsikiliza Meya wa Manispaa. Nashauri uchunguzi unaofanywa sasa uwe mpana, utazame uwezo wa watendaji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mapato ya ndani kwa mujibu wa CAG MSM zilishindwa kukusanya 17% ya makadirio (shilingi 104 bilioni) mwaka 2016/2017 wastani wa miaka ya nyuma ni 10% tu. Pia property tax kuchukuliwa na TRA ni changamoto. Hii maana yake ni kuwa fedha za vijana zitakuwa ndogo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Serikali itoe maelezo kuonya wanasiasa kuingilia sheria. Katibu Mwenezi wa CCM Bwana Polepole alikuja Kigoma kuagiza ushuru usikusanywe na kuvunja sheria. Kwa nini TAMISEMI haikemei mambo haya? CAG ametaka tuongeze mapato lakini wanasiasa wanazuia?