Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa mwaka wa Fedha 2018/2019 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora

Hon. Daniel Nicodemus Nsanzugwako

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kasulu Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa mwaka wa Fedha 2018/2019 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora

MHE. DANIEL N. NSANZUGWANKO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Natumaini nina dakika kumi leo. Nami kama walivyosema Waheshimiwa Wabunge wenzangu nianze kwa kuwapongeza sana wenzetu katika Wizara hii muhimu sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimekuwa nikiitazama TAMISEMI kama Serikali ndani ya Serikali yenyewe. Mheshimiwa Jafo na timu yake hongera sana kwa kazi nzuri, yeye na Naibu Mawaziri wake, Katibu Mkuu wake, Alhaji Iyombe, wanafanya kazi nzuri sana na Naibu Makatibu Wakuu, mama Zainab na Naibu mwingine anayeshughulikia masuala ya elimu, hongera sana kwa kazi nzuri na kubwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nianze haraka haraka na hili la hili la takwimu. Ukiangalia hotuba ya Mheshimiwa Jafo ukurasa wa 58, anazungumzia habari ya program ya kuijengea uwezo miji 18, ameitaja pale. Katika ile miji 18 aliyoitaja sikuona Mji wa Kasulu kwa sababu baadhi ya miji aliyoitaja imesajiliwa sanjari na Miji wa Kasulu na Mji wa Kasulu ni mji wa siku nyingi sana. Kwa hiyo, naomba sana katika kumbukumbu zao waweke Mji wa Kasulu katika program ile kwa sababu miji ambayo imesajiliwa pamoja na Mji wa Kasulu wameiainisha pale.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukurasa wa 59, Mheshimiwa Jafo amezungumzia juu ya kitu kinachoitwa program ya kuendeleza miji 18; bahati nzuri ile miji hakuitaja na amezungumzia habari ya kuboresha na kupanga na uandaaji wa mipango ya master plan katika miji. Ni kweli jambo la kupanga miji yetu ni jambo la msingi sana ili miji yetu isiharibike. Sasa ile miji hakuitaja pale, sasa sikuelewa kama hiyo miji ndiyo ile miji 18 au ni miji mingine?

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukurasa 115, ameendelea kusisitiza juu ya program ya ujenzi wa barabara za kuimarisha miji 18. Sasa hoja yangu iko hivi; ukurasa wa 58 anazungumza miji 18, ukurasa wa 59 anazungumza miji 18, ukurasa 115 anazungumza miji 18. Sasa nataka kujua ni miji ipi hiyo? Ni hiyo hiyo? Kama miji ni hiyohiyo pengine wanatumia criteria gani kwamba mji huu tunaupanga na mji huu tunauboresha na huu mji tunajenga barabara zake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni dhahiri kabisa kwamba hoja hii inahusu halmashauri za miji na si halmashauri za vijiji; na pale ukurasa wa 59 amekiri kwamba takribani billioni tisini na moja zitatumika kwa kazi hiyo. Sasa naomba sana; Mji wa Kasulu ni mji wa siku nyingi uko mpakani mwa nchi yetu na ni mji uliosajiliwa tangu mwaka 1974, ni mji wa siku nyingi sana; usiachwe kuingizwa kwenye Town Authority ambayo imefanywa sanjari na miji mingine kama Bariadi, Geita na Korogwe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo naomba sana, ule ni mjini wa siku nyingi, naomba watuingize kwenye program na hasa hizi program mbili, hii ya kupanga miji (master plans) na hii ya kuboresha miji, kwa maana ya kujenga barabara za mijini. Hilo la kwanza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili nijielekeze alikoishia rafiki yangu huyu, kuhusu hoja ya Walimu. Nichukue line kwamba kwa Walimu lipo tatizo kubwa la msingi, wana madai mengi sana. Labda nitoe mfano, Walimu wa shule ya msingi katika Mji wa Kasulu wanadai malimbikizo yao tangu Juni, 2016, shilingi milioni mia tatu tisini na sita, almost milioni mia nne, hawajalipwa. Fedha za likizo, masomo, matibabu, uhamisho, kujikimu na kadhalika. Kama alivyosema ndugu yangu Ryoba pale, hawa Walimu wanakuwa hawana incentive jamani, matokeo yake ni lazima elimu itashuka tu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilikuwa najaribu kuangalia ile hoja aliyokuwa anaijenga Rais wetu Mstaafu Mzee Mkapa ya kuwa na mjadala wa kitaifa kuhusu elimu, lakini yako mambo hata kabla ya mjadala huo tunaweza tukaanza nayo. Huwezi kuwa na Mwalimu anadai matibabu yake tangu Juni, 2016 hajalipwa, hiyo ni kwa msingi.

Mheshimiwa Spika, ukija sekondari kwa sekondari zilizopo katika Mji wa Kasulu wana madai yao ya shilingi bilioni sabini, hawajalipwa hawa. Kama anavyosema mwalimu aliyetangulia hapa, kuna Walimu wa sayansi humu hawana incentives hawa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nafikiri, nadhani Mheshimiwa Kakunda ndiye anayeshughulikia sekta hii, kuna mambo ambayo wanaweza wakayafanya sasa ambayo nina hakika kama Walimu wakilipwa mafao ambayo ni stahili zao nina hakika kabisa suala zima hili la elimu tunaweza tukapiga hatua.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli, pamoja na shida zote hizi niwapongeze sana Walimu nchini, niwapongeze Walimu wa Halmashauri ya Mji wa Kasulu, wanafanya kazi kubwa sana katika mazingira magumu. Nafikiri wakati umefika kabisa Waheshimiwa Mawaziri wote wawili, wa Utumishi na TAMISEMI kwa kweli kuangalia namna ya kuwapa incentives watu hawa, wanafanya kazi kubwa iliyotukuka. Watu hawa kwa kweli ndio wanaolea Taifa letu pamoja na mazingira yote magumu wanayokumbana nayo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jambo la tatu ambalo ningependa niliseme ni kuhusu suala la afya. Nakushukuru Mheshimiwa Naibu Waziri alikuja Kasulu na bahati nzuri alinikuta tukamtembeza, tunamshukuru Mheshimiwa Naibu Waziri Kandege. Ushauri wake tuliuzingatia na kile Kituo cha Afya alichokitembelea cha Kiganamo kinakaribia kukamilika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo nilimweleza jambo moja mahsusi kabisa, sisi katika mji ule tumepata kituo kimoja cha afya na Mji wa Kasulu una wakazi 270,000, yaani Kasulu Mjini na viunga vyake. Naomba sana. Viko vituo vya afya tumeanza kujenga katika Kata za Murufiti, Heru Juu pamoja na Muhunga, tunaomba sasa nguvu ya Serikali ijumuike na nguvu ya wananchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kusema kweli mimi hata Mfuko wangu wa Jimbo nimeu-surrender kwa kazi hiyo ili akinamama hawa wasipate shida kusafiri kilometa 30 mpaka 35 kufuata huduma katika maeneo ya kutolea huduma Kasulu Mjini, naomba sana.

Mheshimiwa Mwenyeketi, kuhusu sekta ya afya, katika hotuba ya Mheshimiwa Waziri amezungumzia masuala ya kujenga vituo vya afya; jambo jema sana, jambo lenye afya jambo lenye akili kabisa. Hata hivyo, sikuona hata sentensi moja waliyozungumzia kukarabati hospitali za wilaya kongwe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ziko hospitali za siku za nyingi, kwa mfano Wilaya kama za Kasulu, Kibondo zina hospitali za siku nyingi na hizo hospital zimekuwa ndizo zinazotoa huduma kwa kweli; na zimekuwa zikitoa huduma hata kwa halmashauri za jirani ambazo hazina hospitali ambazo ndizo wanazijengea sasa hivi. Kwa mfano Hospitali ya Wilaya Kasulu ambayo ndiyo ya Mji wa Kasulu inatoa huduma Buhigwe, Kasulu DC pamoja na Uvinza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo bado ni hospitali ya siku nyingi. Nafikiri kuliko tu kutuachia ile CDG Mheshimiwa Waziri ambayo inatusaidia kwenda kurabati kuwe na program maalum kama ilivyofanyika 2009 ya kukarabati hospitali za Mikoa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama mnakumbuka, Waziri wa Afya atakuwa anakumbuka na TAMISEMI watakumbuka walitoa takriban milioni mia sita kwa hospitali nyingi za mikoa kwa ajili ya ukarabati. Ziko hospitali za wilaya, nina hakika ziko wilaya nyingi ambazo zina hospitali kongwe ambazo zinahitaji ukarabati na wangekuwa na special program kwa ajili ya kazi hiyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la Waganga na Madakrati, nalo hili wangeliangalia kwa umakini sana, hasa kwa mikoa ile ambayo ni disadvantaged, mikoa ya pembezoni, mikoa yenye shida.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimweleze Mheshimiwa Waziri, sisi watu wa Kigoma referral hospital yetu ipo Bugando-Mwanza ukiacha ile regional hospital…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa mzungumzaji)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja naomba Mheshimiwa Jafo ayatilie maanani yote niliyozungumza. Ahsante sana.