Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa mwaka wa Fedha 2018/2019 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora

Hon. Mussa Bakari Mbarouk

Sex

Male

Party

CUF

Constituent

Tanga Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa mwaka wa Fedha 2018/2019 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora

MHE. MUSSA B. MBAROUK: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Labda kwanza nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu, lakini pia niwashukuru wapigakura wangu wa Jimbo la Tanga.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kumshukuru Mwenyezi Mungu nitaanza na hotuba ya bajeti ya Utumishi. Sekta ya Utumishi ni sekta muhimu na vile vile katika kila nchi basi sekta hii inakuwa na changamoto, lakini kwetu niseme imezidi. Kwa nini nasema hivyo; kwa sababu kwanza kuna tabia ya kuwacheleweshea watumishi wetu michango yao ya Mifuko ya kijamii katika NSSF, LAPF, WCF, GEPF na kadhalika. Sasa namwomba Mheshimiwa Waziri alifanyie kazi suala hili ili hii michango iwe inapelekwa mapema.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia pale wafanyakazi au watumishi wanapostaafu kumekuwa kuna tabia ya kucheleweshewa mafao yao. Sasa wale wanaohusika na malipo ya mafao wajijue na wao pia kwamba ni wastaafu watarajiwa, kwa hiyo wanavyowafanyia wenzao na wao wakija wakistaafu wajue watakuja kufanyiwa hivyo hivyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine, miongoni mwa changamoto ni kwa wale ambao walifukuzwa kazi. Katika Bunge hapa tumeambiwa kwamba Serikali imesema watarudishwa kazini, lakini mara tu jambo lolote linapotoka juu likienda kule chini kuna tabia unaambiwa kwamba waraka bado haujafika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nina mfano hai katika mambo mbalimbali; kwa mfano mwaka jana tulipitisha hapa kwamba road license isamehewe, lakini ukienda ukafanya transfer kule unalipishwa na TRA, ukiwauliza wanakwambia kwamba bado waraka haujafika. Jambo likiwa la kuwasulubu wananchi hawaulizi waraka, moja kwa moja linafanyiwa kazi, kwa hiyo hii tabia nayo naomba iachwe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa wale wafanyakazi ambao waliachishwa kazi kwa kisingizio cha vyeti feki au hawana vyeti vya darasa la saba; kuna wengine wameachishwa kazi wakiwa tayari katika QT, wamefanya mitihani na wanasubiri vyeti vile vya form four, lakini wameachishwa kazi. Sasa hili la kuwarudisha ni jambo jema lakini pasiwe na kisingizio cha kwamba waraka haujafika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo nataka kulizungumzia ni vibali vya ajira katika halmashauri. Zoezi hili pia limetuathiri katika baadhi ya vituo vya afya, zahanati na maeneo mengine ya huduma muhimu, watu wamefukuzwa kazi; matokeo yake vituo vya afya havina manesi, hata baadhi ya Madaktari hakuna. Hata katika halmashauri tumepata tatizo kubwa la kuwa na watendaji ambao wanakaimu kwa muda mrefu; hili la kukaimu nalo pia lifanyiwe kazi. Mtu kukaimu zaidi ya miaka miwili inakuwa sio vizuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Halmashauri yetu ya Jiji la Tanga tuna mitaa 181, lakini watumishi waliopo ni 123, na tuna upungufu wa watendaji wale wa mitaa 58. Pia tunazo kata 27, tuna watendaji 13 tu, bado tuna upungufu wa watu 14 kama watendaji kata. Kwa hiyo hilo naomba lifanyiwe kazi. Ushauri wangu kwa Serikali ni kwamba vibali vya ajira pia vipelekwe katika halmashauri ili tuweze kujaza nafasi za wale watendaji ambao hawapo, hiyo ni kwenye utumishi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikija kwenye suala zima a TAMISEMI sasa. Kabla sijaanza, najua TAMISEMI inaendana na shughuli nyingi, ni idara au ni taasisi pana ambayo inabeba mambo ya watu wengi. Pamoja na yote katika suala zima la utawala bora kuna kipengele kimeeleza kwamba mazingira ya utulivu na amani ni fursa adhimu katika kujenga uchumi imara na endelevu katika nchi yoyote ile. Sasa sisi bado kuna baadhi ya maeneo yamekuwa yanatupa shaka kidogo; huu mpango wa watu kukamatwa halafu hawajulikani walipo lakini familia zao zinahangaika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano kuna tatizo lililotokea tarehe 3, Aprili, 2018 kule Pemba kuna vijana sita walikamatwa, watatu wameachiwa ambao walikuwa ni; Juma Abdallah Kombo (miaka 16), Abdallah Hamisi Abdallah (miaka 19) na Said Shaabani Mohamed (miaka 16), hawa waliachiwa. Bado kuna wengine watatu hawajulikani walipo, mmoja wapo ni Thuwein Nassoro Hemed (miaka 30), Hamisi Abdallah Mattar (miaka 25) na Khalid Hamisi Abdallah (miaka 30). (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naona kuna mambo mengine, kama alivyozungumza mzungumzaji mmoja jana, kuna baadhi ya mambo yakifanyika ni kama kuitia doa Serikali. Ni bora wale vijana huko walipo wakaachiwa…

T A A R I F A . . .

MHE. MUSSA B. MBAROUK: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, taarifa nimeipokea. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, labda kwenye suala la Serikali za Mitaa, nianze kwa kumshukuru na kumpongeza Waziri wetu wa TAMISEMI, Mheshimiwa Jafo, lakini Mheshimiwa Kapteni Mkuchika sijamsahau, ukizingatia alikuwa ni Mkuu wetu wa Mkoa wa Tanga; nampongeza, lakini haya niliyoyasema ayafanyie kazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika TAMISEMI naanza kwenye elimu. Wanafalsafa mmojawapo, bwana Nelson Mandela, amesikika akisema; education is the most powerful weapon which we can use to change our world; lakini pia wapo wengine waliosema education is the key of life. Sasa kwa nini natoa mfano huu; Mheshimiwa Jafo katika elimu yetu Tanzania tumekuwa na mitihani mingi sana, bado kuna matatizo ya ukosefu wa walimu wa masomo ya sayansi kama biology, chemistry, physics na mathematics.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vile vile pia bado kuna uhaba wa matundu ya vyoo. Mwaka jana nilisema hapa kwamba kuna tangazo la Haki Elimu linaonesha kwamba mwalimu na wanafunzi wanasukumana kuingia chooni, choo ambacho kiko wazi juu hakina paa, kumejaa maji machafu, wanakanyaga kwenye mawe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, bado inahitajika bidii kubwa ya Serikali kuwekeza. Kama vile tulivyonunua magari ya maji ya kuwasha, basi tuhakikishe tunapeleka hata vile vyoo vya bei nafuu katika shule zetu ili kuepukana na tatizo hilo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mitaala yetu ya kielimu; tumekuwa na matatizo ya mitaala kuanzia kwenye nursery schools, primary schools, secondary schools, colleges na universities; bado kuna matatizo makubwa ya hii mitaala. Kwa mfano katika nursery kila mtu anafundisha anavyojua mwenyewe, yaani Serikali haikuweka mtaala maalum, kwamba nursery wanatakiwa wafundishwe kupitia nyanja hizi, hakuna hilo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa mimi naishauri Serikali kwamba ni lazima tuwe na utaratibu mzuri. Haiwezekani katika nchi zote za Afrika Mashariki sisi Watanzania mfumo wetu wa elimu, mimi kwa maoni yangu naona tumepitwa na wenzetu wote. Kwa sababu ukienda Rwanda na Burundi leo ni one child one laptop. Ukienda Kenya kwa wenzetu wametangaza kwamba elimu bure lakini ni kuanzia standard one mpaka university, tena hakuna mambo ya mikopo ya wanafunzi wala hakuna matatizo, wanafunzi kazi yao ni kusoma. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini hapa kwetu kwa sababu mifumo yetu imekuwa ikiingiliana na mambo mbalimbali, matokeo yake kumekuwa na migomo ya mara kwa mara, wazazi wanashindwa kulipa ada kwa baadhi ya watoto wa familia za maskini. Tumetangaza elimu bure lakini kisiasa, kwa mantiki hiyo wengi wana akili, wamefaulu lakini wanabaki nyumbani. Naamini Wabunge wenzangu ni mashahidi hapa; kama hawakufuatwa na watoto 20 basi 30, kila mtoto amefaulu lakini hana school fees, hana viatu, hana madaftari na kadhalika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naishauri Serikali, kama tunasema elimu bure basi angalau kidogo tuwaige wenzetu wa Kenya ili watoto wetu wapate elimu. Unakuta mtoto ananyongeka, yeye amefaulu amefanya kazi ya kusoma lakini familia haina uwezo, mtoto anakaa nyumbani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine, juzi tarehe 11 Rais Uhuru Kenyatta amesaini sheria kwamba wanafunzi wote wa kike Serikali ya Jamhuri ya Watu wa Kenya itakuwa inawapa taulo za kike (pads) bure, free, no charge. Sasa najiuliza; ukiitazama Kenya Mbuga ninazozijua mimi ni Tsavo na Maasai Mara. Sisi tuna mbuga za wanyama, tuna bandari tatu, Kenya wana bandari moja, tuna Mlima Kilimanjaro Kenya hawana, tuna mkonge, katani, pamba, pareto, alizeti na mambo mengine… (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa mzungumzaji)