Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa mwaka wa Fedha 2018/2019 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora

Hon. Livingstone Joseph Lusinde

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mtera

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa mwaka wa Fedha 2018/2019 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora

MHE. LIVINGSTONE J. LUSINDE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nikushukuru sana kwa uongozi wako na Mungu aendelee kukujalia kwa namna unavyotenda haki.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jana hapa kuna Waheshimiwa Wabunge walikuwa wanataka kubomoka lakini leo nataka kusema ukweli sasa, maana yake Tanzania ukweli watu hawaupendi, nami nataka leo niseme ukweli halafu nitatumia kauli ya mdogo wangu Mwenyekiti wa Vijana wa CCM Ndugu Kheri James kuwaomba wanipigie makofi kwa kusema ukweli. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nachukua nafasi hii kumpongeza sana Mheshimiwa Waziri wa TAMISEMI pamoja na Waziri mzoefu Kaka yangu Kapt. George Mkuchika. Nawapongeza sana Waheshimiwa Naibu Mawaziri wa TAMISEMI, Katibu Mkuu, Mhandisi Iyombe pamoja na timu yako mnafanya kazi nzuri. Wakati nikiwapongeza niwashukuru kwa kunipatia milioni 700 kwa ajili ya kujenga kituo cha afya pale Mpwayungu, milioni 400 kwa ajili ya ujenzi na 300 kwa ajili ya vifaa. Hii itasaidia sana wakazi wa Tarafa ya Mpwayungu kupata huduma za afya kwa urahisi sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niwaombe tu watu wa TARURA watengeneze daraja lile la Manda limevunjika kwa mvua, hii inatupa shida sana ambulance kupita pale kuleta wagonjwa kwenye kituo cha afya cha Mpwayungu. Kama ambavyo Wabunge wengi wameeleza tunaomba bajeti ya TARURA na utendaji wao wa kazi uwe wazi ili Wabunge waweze kuasaidiana nao kuhakikisha kwamba maendeleo yanakwenda. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo nataka nilitolee ufafanuzi kabla sijaingia kwenye utawala bora, nizungumzie kuna baadhi ya Wabunge walikuwa na mashaka juu ya kugawana mali za Chama. Wengine wanafikiri kwamba mali ambazo walizijenga kabla hawajahama CCM wana haki nazo. Ndugu zangu hata Maaskofu hilo mkiwauliza watawasaidieni.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiwa Muislam ukachangia matofali siku utakayokuwa Mkristo yale matofali ya Msikiti hayatakuhusu tena, wala huwezi kuyadai tena, ukiwa Mkristo ukachangia matofali ya kujenga Kanisa siku utakayohama kwenda kuwa Muislam matofali yale ukidai ni ugomvi. Kwa hiyo, ndugu zangu muelewe tu kwamba ile michango mliyoitoa wakati wa Chama kimoja kuijenga CCM mkitaka kufaidi rudini CCM ili muweze kufaidi vizuri. Hata kwenye harusi tu, michango ya harusi inaishia mlangoni huingii chumbani kwa maharusi kwa sababu ya mchango uliotoa. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kuyasema hayo sasa ninukuu tu kwenye Biblia huo mstari siukumbuki. Kuna mstari unasema toa kwanza boriti jichoni mwako ndipo uone vema kibanzi kilicho kwenye jicho la mwenzako. Wapinzani wa nchi hii, tuoeni kwanza boriti iliyomo kwenye macho yenu kabla hamjaona boriti iliyopo kwenye Serikali ya CCM. Nasema hivi kwa sababu nataka niingie sasa kwenye ukweli mtupu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukisoma kwenye ripoti ya CAG ukurasa 266 nanukuu “mkopo ambao haukuthibitishwa mapokezi ndani ya Chama cha CHADEMA, mnamo tarehe 11 Aprili, Menejimenti ya CHADEMA (Mkopaji) iliingia makubaliano na mwanachama wake (Mkopeshaji) kuhusu kukopeshwa kiasi cha bilioni mbili.” Mnisikilize hapo, wanakopa hewa yaani deni hewa hilo. Mkopo waliingia makubaliano na mwanachama wake mkopeshaji kuhusu kukopeshwa shilingi bilioni mbili kwa shughuli za Chama. Hakuna nyaraka zinazoonesha kuwa kiasi cha mkopo walichokubaliana kilitolewa na kupokelewa na Chama husika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, CAG anaendelea tarehe 26 Agosti, kiasi cha shilingi milioni 866 kililipwa kwa mwanachama kwa niaba ya Chama kwa ajili ya mabango ya matangazo yaliyotolewa na kampuni ya MS Milestone International Company Limited nje ya deni hilo. Kiasi cha shilingi milioni 715 kililipwa kwa mwanachama kama marejesho ya fedha iliyokopwa kulipia ununuzi wa mabango bila ya kuambatanisha makubaliano ya kisheria. Wajinga ndio waliwao, mmeng’ang’ania maandamano mnaacha wenzenu wanapiga hela. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukaguzi wangu wa taarifa ya makusanyo ya Chama umebaini kiasi cha Sh. 2,302,305,500 kilikusanywa bila kuingizwa kwenye akaunti ya Wadhamini.” Angalia mambo hayo! Hazikupelekwa benki na matumizi yake hayakutolewa kwa ajili ya ukaguzi. Kutokupeleka makusanyo benki kunaonesha Chama kutokuwa na mfumo mzuri wa udhibiti wa fedha. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, manunuzi yaliyofanyika, nimebaini kuwa CHADEMA kimefanya manunuzi ya bidhaa na huduma zenye thamani ya Sh.24,216,625,309 bila kufuata utaratibu.” Wajinga ndio waliwao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wajinga ndio waliwao kuna Kwaya imeimba. Badala ya kushughulikia matatizo makubwa ya ufisadi ndani ya Chama chao wameng’ang’ana kila siku kukosoa Serikali, kukosoa Chama chenye Serikali. Ndugu zangu ndani ya Chama chenu kuna wizi na ubadhirifu mkubwa wa pesa, watu wanakula hela na ninyi mpo hapo! Madeni hewa yanatengenezwa, helcopter hewa zinakodiwa ninyi mmekaa hapa mnang’ang’ania CCM, toeni kwanza boriti kwenye macho yenu ndiyo muone vibanzi vilivyopo kwenye Serikali. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka Watanzania waelewe kwamba ufisadi mkubwa upo kwenye Chama kinacholalamikia ufisadi kumbe wao ndani hawajikagui. Kwa mara ya kwanza ipo humu na ndiyo maana nasema hakuna mtu atapinga kwa sababu haya ni mawe ya uhakika. Nipigieni makofi kwa ukweli ninaowapa. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Mwenyekiti, huu ni ukweli mtupu, ndugu zangu mkienda mkajisimamia mkawa wakweli kwenye mambo yanayowagusa ninyi mtakuwa na haki ya kutukosoa, lakini kama ninyi wenyewe mnakumbatia ufisadi na wizi wa mabilioni ya pesa yanakusanywa kwa wanachama yanaingia kwenye Chama chenu, watu wanagawana wanakula, michango ya Wabunge inaliwa, mmekaa hapo mmenyamaza kazi yenu kukosoa hii! Nawaambia hamtakaa mfike popote. (Makofi/Vigelegele)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ndiyo maana nimewaambia huu ni ukweli mchungu, nimesema natumia maneno ya Kheri Denice James kwamba ifike mahali kama tunataka kutengeneza Upinzani tutengeneze Upinzani wenye kusema kweli. Ukianza kumulika nyoka anzia kwenye miguu yako ndipo uanze kumulika kule. Niliwaambia hata juzi mna Chama kilichopokea ruzuku zaidi ya bilioni 10 hakina Ofisi hata moja wilayani, hakina ofisi hata moja mikoani, mnataka kufanana na Chama cha Zitto! (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo mnazungumzia utawala bora nataka niwaambie, Mheshimiwa Zitto yupo peke yake anahangaika. Wapo Wapinzani Wazalendo, mimi nataka niseme kwenye Bunge hili mtakuja kunikumbuka, Mheshimiwa Zitto wewe ni hazina lakini badili Chama, njoo CCM uje ufanye kazi ya wananchi, kubaki huko unapoteza muda bure, tutakukosa mtu mzuri kwa sababu ya muda na huko unakopoteza muda. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka niwambie hivi tangu CHADEMA imesajiliwa, nazungumzia utawala bora, tangu CHADEMA imesajiliwa imezaa vyama viwili. SAU imevunjika kutoka CHADEMA, ACT imevunjika kutoka CHADEMA, sasa Chama hiki kingekuwa na Serikali si kingekuwa kimeleta vita kubwa sana ndani ya nchi? Kingeleta vita kubwa ndani ya nchi. (Kicheko/Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hivyo, tunapozungumzia utawala bora tuanze kujitazama sisi wanasiasa, tutazame miongozo na mienendo ya Viongozi wetu. Kuna Vyama hapa vina Mwenyekiti wa kudumu, kila unapokuja uchaguzi Mwenyekiti wa kudumu, Chama cha namna hiyo hakiwezi kujenga demokrasia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitumie Bunge lako Tukufu kuwaomba Waheshimiwa Wabunge, tukikosoa tuanze kujikosoa wenyewe ndipo tuende tuwakosoe watu wengine tunaotaka kuwakosoa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hotuba hizi zote mbili na naunga mkono kwa asilimia mia moja. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana.