Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa mwaka wa Fedha 2018/2019 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora

Hon. Raphael Michael Japhary

Sex

Male

Party

CHADEMA

Constituent

Moshi Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa mwaka wa Fedha 2018/2019 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora

MHE. RAPHAEL J. MICHAEL: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi hii ya kuchangia. Nami nichukue fursa hii kupongeza kazi kubwa ambayo Mheshimiwa Waziri anafanya, Waziri wa TAMISEMI na Naibu Mawaziri wake. Naamini kwamba ana Naibu mzuri ambaye amebobea kwenye mambo ya Serikali za Mitaa, huenda anaweza akamsaidia sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba pamoja na hayo yote niliyosema ya kumpongeza Waziri, pamoja na jitihada ambazo Waziri anaonekana kufanya, lakini nina hofu kwamba, dhamira ya Serikali hii ya Awamu ya Tano ni kutengeneza Serikali za Mitaa dhaifu, kufanya Halmashauri zetu ziwe dhaifu na kwenda kinyume kabisa na dhamira ya maboresho ya Serikali za Mitaa yaliyofanywa tangu 1998 mpaka mwaka 2014 na Serikali ya Awamu ya Tatu na Serikali ya Awamu ya Nne. Kwa sababu theory zote zinaonesha kwamba, Serikali zote ambazo zinataka kufanya kazi kama zinavyotaka huwa zinahakikisha kwamba Serikali za Mitaa zinakuwa dhaifu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ndiyo maana leo sote tuko hapa tunalalamika jinsi ambavyo Wakuu wa Mikoa wanaweza wakaziingilia Serikali za Halmashauri. Tunalalamika jinsi ambavyo Wakuu wa Wilaya wanaweza wakaziingilia Halmashauri kwa sababu ya dhamira inayoonekana yenye mwelekeo wa kufanya yale mawazo yote ambayo yaliwekezwa fedha nyingi sana ya kufanya maboresho ambayo yangezipa Mamlaka za Serikali za Mitaa kuwa ni mamkala kamili katika maamuzi katika rasilimali yanakuwa hayana nia njema katika Serikali hii ya Awamu ya Tano, kwa maoni yangu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa ushauri wangu kwa Mheshimiwa Waziri ili aweze kufanya kazi yake vizuri ni lazima ajielekeze sana katika kujenga Serikali za Mitaa imara. Tukijenga Serikali za Mitaa imara hata hii dhana kubwa kwa Waheshimiwa Wabunge wengi kwamba kila wakati tunadhani kitu tunatakiwa tuombe Serikali Kuu. Barabara za vijijini tuombe kwenye Serikali Kuu, barabara za mitaani tuombe Serikali Kuu itapungua.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hii ndio ilikuwa dhamira halisi ya kuimarisha Serikali za Mitaa. Kuzifanya ziwe na maamuzi sahihi ziwe na rasilimali za kutosha rasilimali watu na rasilimali fedha jambo ambalo kwa Serikali hii inaonekana siyo jambo la mkazo sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Mheshimiwa Waziri urejee sana katika hilo la kufanya maboresho yale ya Serikali za Mitaa yaliyozalisha sera ya D by D yafanyiwe kazi za kutosha ili kufanya mahusiano kati ya Serikali Kuu na Serikali za Mitaa yawe ni ya ushirika na siyo ya Baba na Mtoto. Kwa hali ilivyo hapa sasa hivi hapa ni kwamba Serikali Kuu inakuwa ni baba, Serikali za Mitaa zinakuwa ni mtoto, kwa hiyo mtoto ni kulalamika kwa Serikali Kuu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lengo la maboresho lilikuwa kuzifanya Serikali za Mitaa ziwe na autonomy ili ziweze kujitegemea vizuri. Mheshimiwa Waziri naomba sana ajitahidi katika hilo, ni vizuri akaweka sheria itakayozipa uimara, itakayotengeneza taasisi imara ya Serikali za Mitaa itakayoweza kujiendesha ili tuondoe huu mfumo wa watu kutegemea kila saa kuja kuomba, kupiga magoti hapa na ndiyo maana imefika mahala ambapo inaonekana sasa hivi katika nchi hii bila kuvunja heshima na hadhi ya Mheshimiwa Rais na ikionekana kwamba sasa fedha ya nchi hii ni fedha ya Mheshimiwa Rais na siyo fedha ya walipa kodi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwamba sasa hivi kila mtu anamshukuru Rais amempelekea hiki, amempelekea kile, amempelekea kile wakati Rais amechaguliwa na wananchi wote kama mtumishi wa wananchi na mabosi wake ni wananchi wanaolipa kodi ili awatumikie. Kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri nadhani kwamba ni eneo muhimu sana la kulifanyia kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili; kumekuwa na malalamiko makubwa sana ya kuhusu Mfuko wa Vijana na Akinamama. Mara nyingi kumekuwa na hoja hizi kwamba fedha hazikusanywi lakini kubwa zaidi ni kwamba hata hizo zinazokusanywa kidogo hizo zinazopatikana zinatumiwaje. Kwa sababu fedha zile zinaingia Hazina, namwomba Mheshimiwa Waziri ajitahidi kuwe na akaunti maalum ya Mfuko wa Akinamama na Mfuko wa Vijana ile asilimia 10 iingie kwenye hiyo akaunti, kwa sababu ule mfuko ni revolving ili zikitoka kwa wakopeshwaji zirejeshwe kwenye mfuko ule, lakini hela ile ikitoka kwa wakopeshwaji inarejea kwenye Mfuko Mkuu wa Halmashauri, bado inaingia kwenye matumizi mengine ya Halmashauri, kwa hiyo haieleweki ni fedha zipi zimetoka kwa ajili ya bajeti na ni fedha zipi zimerejeshwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ni vizuri aelekeze Halmashauri ziwe na mfuko maalum na aushauri Mheshimiwa Rais akubali kuwa na Mfuko maalum kwa ajili ya fedha hizi za Mfuko wa Vijana na Mfuko wa Akinamama ili sasa mwisho wa siku tuweze baada ya muda tuwe tumetengeneza fedha ya kutosha kwenye hizi akaunti na baada ya miaka kadhaa tukazipa viwango maalum Halmashauri, mwisho wa siku tusizipelekee tena fedha ili zile fedha ziwe kwa ajili ya maendeleo, kwa ajili ya vijana na kwa ajili ya akinamama.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri ni vizuri ajitahidi sana na hili kwa sababu zile fedha kwa sasa hivi hapa hazijulikani zinapoingia kwenye matumizi ya kawaida ni wakati zinaitwa za vijana ni wakati zinaitwa za akinamama, ni wakati gani zinaitwa za matumizi ya Halmashauri. Kwa hiyo, nafikiri ni jambo la muhimu sana kwa Mheshimiwa Waziri kuliangalia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, fedha zilizokuwa zinatengwa za retention asilimia 30 za ardhi ambazo leo hazirejeshwi katika Halmashauri na Mheshimiwa Waziri anajua katika nchi hii kila Halmashauri ardhi ndiyo rasilimali yake kubwa. Ile asilimia 30 ilikuwa inasaidia sana Halmashauri kujiendesha leo zile hela hazirejeshwi, ni vizuri angeshauriana na Wizara ya Ardhi zile fedha asilimia 30 zikarejeshwa katika Halmashauri, zikasaidia mambo ya Halmashauri yakaenda. Kwa sababu mambo ya Halmashauri hayaendi na watakuwa wanazi- commit Halmashauri wakati hazina uwezo wa kupata fedha na vyanzo vyote wamevichukua.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hii spirit ya kuchukua vyanzo vya Halmashauri ni vema Mheshimiwa Waziri akamshauri Mheshimiwa Rais ambaye ni Waziri akaiondoa. Serikali Kuu ina maeneo mengi ya mapato makubwa tu ina bandari na maeneo mengi. Haya maeneo ambayo ndiyo Halmashauri kwa mujibu wa makubaliano ya maboresho ya Serikali za Mitaa yaachwe yabaki katika Halmashauri ili yaweze kusaidia Halmashauri. Kwa hiyo, naomba asilimia 30 ya Halmashauri iachwe irejee katika Halmashauri ibaki katika Halmashauri isaidie Halmashauri kuliko kuichukua wakaipeleka Serikali Kuu asilimia 30 ya kodi ya ardhi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna suala la posho ya Wenyeviti wa Mitaa, Wenyeviti wa Vijiji na Vitongoji. Hebu tusifanye wale watu kama vile wao sio miongozi mwa watu ambao ni muhimu katika Taifa hili. Wale watu tunategemea kuwatumia katika mambo mbalimbali yanayohusu maendeleo ya nchi hii. Hata wao wanawatumia katika sera mbalimbali, maelekezo mbalimbali na makusanyo mbalimbali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wale watu ni vizuri waelekeze Halmashauri zitenge zile fedha angalau Sh.20,000/= mpaka Sh.50,000/= kwa ajili ya Wenyeviti wa Vijiji, Vitongoji ili waweze kufanya mambo yao. Tumewafanya wale watu wamekuwa kama ni watu ambao hawana mtu wa kuwasaidia. Wamekuwa watu ambao ni ombaomba, wamekuwa wakiishi kwa majamvi ili watu wagombane wapate fedha, lakini wale watu ni watu ambao wamechaguliwa kwa mujibu wa sheria wanapaswa kusaidiwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba wale Wenyeviti wa Mitaa, Wenyeviti wa Vijiji na Vitongoji watengewe fedha kwa ajili ya mambo yao.