Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2017 na Mpango wa Maendeleo ya Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019

Hon. Dr. Pudenciana Wilfred Kikwembe

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Kavuu

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2017 na Mpango wa Maendeleo ya Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019

MHE. DKT. PUDENCIANA W. KIKWEMBE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipatia nafasi niweze kuchangia katika bajeti hii iliyoko hapa mbele yetu. Kwanza kabisa, napenda niishukuru Serikali yangu kwa namna ambavyo imekuwa ikijitahidi kwa namna pekee kutatua matatizo ya wananchi japo kuna changamto mbalimbali hasa katika ukusanyaji wa pesa.

Mheshimiwa Naibu Spika, napenda niwashukuru Mawaziri, viongozi na watumishi wa Wizara hii kwa namna ambavyo wameweza kuyapokea baadhi ya maoni ambayo tuliweza kuyatoa katika bajeti ya mwaka 2016/2017 ambayo ni pamoja na kuondoa baadhi ya kodi kwenye bidhaa mbalimbali zikiwemo taulo za kike kwa ajili ya watoto wetu wa kike, nashukuru.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika hili, nimwombe Mheshimiwa Mpango ashirikiane na sekta zingine kwa ajili ya kudhibiti ubora wa hizi bidhaa ambazo mmeziondolea kodi. Kwa sababu wakati mwingine zitakuwa zinamnufaisha yule mfanyabiashara mkubwa na siyo mtumiaji. Kwa hiyo, tunategemea sana hizi bidhaa zitashuka bei. Naomba sana muangalie hilo na uwe ni uangalizi wa hali ya juu kwa sababu mara nyingine tutajikuta tunamsaidia tu yule mfanyabiashara mkubwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nije kwenye mapato ya ndani na naomba niongelee ukwepaji wa kodi.

Si kwamba wananchi hawapendi kulipa kodi, wananchi wetu wakipata elimu ya kodi wako tayari kulipa kodi na waelimishwe ni kodi zipi wanapaswa kulipa. Kumekuwa na mlolongo wa kodi nyingi mno ndizo hizo zinamfanya mtu aone kwamba kwa nini kodi zimekuwa nyingi, leo una hii, kesho hii na hii. Ndiyo maana unakuta wananchi wakati mwingine wanaona maafisa wa TRA wanatoweka, siyo kwamba hawapendi, wapeni elimu ili wananchi waweze kulipa kodi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nilishampa Waziri maombi yangu aniletee wataalam wa TRA wa kodi waje jimboni kwangu, wawafundishe wananchi haya mambo waweze kuzijua hizo kodi mbalimbali wanazotakiwa kulipa. Zipo kodi zenye kero mpaka leo kama hotel and service levy katika baadhi ya halmashauri. Naomba mliangalie upya na muweze kulichanganua wananchi walielewe hata kwa kutumia vyombo vya habari. Naomba wananchi wapewe elimu wanapaswa kulipa nini kwenye hii hotel and service levy hasa kwenye zile guest house ndogo za vijijini ambazo zinasubiri siku ya mnada wale wauza ng’ombe waende wakalale pale, naomba mziangalie sana. Kwenye halmashauri zingine hasa ya kwangu wananchi bado wanateseka na hawazielewi lakini halmashauri wanalazimika kukusanya kutokana na miongozo waliyopelekewa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lingine naomba niongelee kodi za zimamoto. Kodi za zimamoto ni kero. Leo ukienda kununua kiwanja lazima utaambiwa ulipe kodi ya zimamoto, ni mchimbaji mdogo mdogo utalipa shilingi milioni mbili ama tatu, hazina kiwango, hazieleweki, unaanza ujenzi unatakiwa kulipa kodi ya zimamoto. Sasa zimamoto hiyo huduma iko wapi mpaka mtu unamchaji hiyo kodi ya zimamoto? Kwa mfano, kwangu Kavuu, hiyo zimamoto iko wapi? Wanatoka Mpanda Mjini wanaenda kulala kule kwa ajili tu ya ku-harass wafanyabiashara wadogo wadogo wenye guest houses kwa ajili ya hizi kodi za zimamoto. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nimeshampelekea Waziri malalamiko haya ya wananchi wangu naomba suala hili alisughulikie. Waziri alinipa Kamishna wa Kodi akaniletea bundle la sheria, mimi sio mwanasheria. Kwa hiyo, naomba sana tunapoleta concern zetu zinazotoka kwa wananchi mzishughulikie. Naomba hili la zimamoto lishughulikiwe specifically katika Jimbo langu la Kavuu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niongelee suala lingine la ulimbikizaji wa madai mbalimbali ambayo bado wanaendelea kuhakiki. Uhakiki umeanza muda mrefu, sasa ifike mahali tuumalize huo uhakiki tuwalipe stahiki zao watumishi hasa katika sekta ya afya na sekta ya elimu. Naomba tufike mahali uhakiki sasa uishe na tuendelee mbele. Mheshimiwa Chenge ametoka kusema hapa tusipende kwenda mbele na kurudi nyuma, naomba twende mbele. Tukitembea haturudi nyuma hatua zinakwenda mbele na sisi tunataka twende, mbele ndiyo maendeleo. Kwa hiyo, naomba sasa tufike mahali tuwe na ukomo wa huu uhakiki, twende mbele ili tuone tunataka kuwasaidiaje watumishi wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nije kwenye vipaumbele katika bajeti hii, nianze na kilimo. Kwa kweli bado hatufanyi vizuri, naomba tukiri ukweli katika sekta ya kilimo, uvuvi na mifugo. Hata leo tukiangalia bajeti yao, ukiijumlisha sidhani kama inafika shilingi bilioni 100 kwa sekta zote tatu. Sasa hivi tumejikita kwenye miundombinu, reli hizo zinajengwa najua itafika mpaka Karema kwetu kule ili tuvushe mizigo mpaka Kalemii (Kongo) lakini tutasafirisha nini? Kama kwenye production hatutaki kwenda sambamba na uwekezaji katika miundombinu, haya mazao hayapo, miundombinu ipo sidhani kama inakaa vizuri. Kwa hiyo, kama kweli tuna nia ya dhati, naomba tuwe na ulinganisho kati ya production na hizi means za usafirishaji. Kwa maana kwamba mazao yetu sasa ndiyo yatabebwa na hizo reli ili yaweze kusafirishwa tupate kurudisha pesa ambayo tutakuwa tumeitumia katika kujenga reli hiyo.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia upatikanaji wa pembejeo bado ni tatizo. Mwaka jana katika bajeti hii niliongea, nikasema nawaomba muangalie jiografia na hali ya hewa ya maeneo mbalimbali. Kwa mfano, Mikoa ya Kusini Magharibi mvua zake zinaanza mapema, sasa mvua zinaanza mwezi wa tisa unapeleka pembejeo mwezi wa kumi au kumi na moja, unategemea nini kwa mkulima?

Mheshimiwa Naibu Spika, pia angalia katika msimu wa mwaka huu kilimo cha mahindi imekuwa ni kilio kila sehemu na huyo mdudu mnayesema ametoka America sijui alikuja na nini, hata sijui? Kutoka America mpaka Tanzania tena Tanzania yenyewe Kavuu ambako sina hata barabara sasa sijui huyo mdudu alikujaje, ninyi wataalam mnajua. Naomba sana myaangalie haya mambo pindi mnapokuwa mnaleta vitu hivi hasa pembejeo kwa wakulima. Kama mnafanyia utafiti wa kutosha ni vyema mkaleta kule lakini ni vyema pia zikawahi.

Mheshimiwa Naibu Spika, tuangalie pia kwenye uvuvi na mifugo. Leo hii gumzo ni kupima samaki kwa rula, jamani! Hebu tufike mahali tuone tunafanyaje kazi, tusikurupuke.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nije kwenye huduma za jamii hasa upatikanaji wa maji. Tulipendekeza kwenye bajeti iliyopita kwamba iongezeke tozo ya Sh.50. Sasa hivi tuna tozo ya Sh.50, tukapendekeza iongezeke Sh.50. Leo umekuwa shahidi maswali ya maji yaliyokuwa yakiulizwa ni upatikanaji wa maji kwenye shule za msingi, sekondari, A- Level. Siyo hivyo tu, akinamama wanabakwa na wanauawa kwa imani za kichawi wanapokwenda kutafuta maji na mama sasa hivi hawezi kutembea peke yake. Nayaongea hayo wenzangu wa Shinyanga mnayafahamu, jimboni kwangu yanatokea, wanawake hawawezi kwenda kuchota maji sasa hivi kutokana na umbali mrefu kuogopa imani za kichawi za kunyongwa na kutupwa hovyo.

Mheshimiwa Naibu Spika, namwomba Waziri aongeze tozo hii ili maji yaweze kutosha tuwe na tozo ya Sh.100 katika Mfuko wa Maji. Nina uhakika tutayatatua haya matatizo na tutawaondolea vifo ambayo si vya lazima akina mama. Kwa sababu sasa hawaendi mabombani kwa kuogopa kunyongwa, ni mbali. Hebu ongezeni hii pesa ifike Sh.100. Tumepunguza bei ya hizi pads kwa nini sasa tusiwawekee maji shuleni? Unakuta mtoto ana fagio, dumu na begi anaenda shuleni. Naomba sana ongezeni tozo ya Sh.50 ili tuwe na uhakika wa kupata maji. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile kwenye elimu na afya, naomba muongeze pesa na iweze kutoka kwa wakati. Halmashauri hazina pesa za kutosha kutekeleza miradi, naomba Serikai yangu sasa ule ucheleweshaji wa kupeleka pesa kwa ajili ya miradi kwenye halmashauri na wenyewe ufikie ukomo. Pindi tunapopitisha bajeti, pesa ziende kwa wakati na miradi itatekelezwa kwa wakati.

Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana, mengine nitaandika kwa maandishi lakini naunga mkono hoja. Ahsante.