Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 – Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki

Hon. Fakharia Shomar Khamis

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 – Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki

MHE. FAKHARIA SHOMARI KHAMIS: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Kwanza, sina budi kuipongeza Wizara kwa hatua nzuri wanayofikia katika majukumu yao Waziri, Naibu Waziri, Katibu Mkuu na Kurugenzi yake yote kwa utendaji wao mzuri.

Mheshimiwa Naibu Spika, la pili, sina budi kumpongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuwasamehe wafungwa na kuwa huru kwa mujibu wa Katiba na ndani yake ndiyo Mheshimiwa Mbilinyi na yeye kapata msamaha leo tunaye hapa Bungeni na tunaweza kuwa naye na kuchangia naye katika Bunge letu hili Tukufu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nazungumzia diplomasia ya uchumi; diplomasia ya uchumi inasaidia kwa Wizara na nchi nzima kuweza kujua jinsi Mabalozi wetu wanavyokwenda nje nini majukumu yao ya kufanya. Hata hivyo, ilivyo Wizara bado haijajipanga kuweza kupatikana sera mpya yao ya Wizara ikaungana na hii ya diplomasia ya uchumi ikaenda pamoja, vikawa vitu viwili sambamba tukaweza kufanikiwa katika majukumu ya utendaji wetu wa kazi na Wizara mpaka leo sijui inasubiri nini na kushindwa kutoa sera mpya ya Wizara ya Mambo ya Nchi za Nje. Mheshimiwa Waziri naomba atakapokuja atuambie wanakwama nini hata wanashindwa kutoa sera mpya itakayoendana na sera ya uchumi ya diplomasia. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sera hiyo ya diplomasia ya uchumi itasaidia kutupatia masoko, kutuletea watalii tena siyo wale wa makundi tunataka waliokuwa na hadhi za juu, itaweza kutuletea wawekezaji maana tuna sera ya viwanda, tunataka kuanzisha viwanda Tanzania ili tuweze kutanua uchumi wa Watanzania. Zanzibar kuna fukwe nzuri za watalii, Bara kuna Kilimanjaro nzuri kwa watalii, tuna mbuga za wanyama, kuna bahari au bustani ndani ya bahari ambavyo hivyo vyote ni vivutio kwa utalii.

Mheshimiwa Naibu Spika, niende kwa Mheshimiwa Waziri, kama inavyozungumzwa, anavyopeleka watendaji katika Balozi zetu, apeleke watendaji ambao wanaendana na diplomasia ya uchumi ili waweze kutusaidia katika majukumu yetu tunayotaka kuyaanzisha.

Mheshimiwa Naibu Spika, tukija kwa upande wa Zanzibar, Zanzibar tunataka au tungependa tuwe na jengo letu kama Ofisi ya Wizara ya Muungano, kama walivyo Mambo ya Ndani, kama walivyo Wizara nyingi za Muungano zina Ofisi zao wenyewe wamejenga. Sasa tunashangaa Mambo ya Nje mpaka leo kuanzia 1964 hadi leo hamna jengo, wana jengo lile ambapo wanasema wapo kwenye mazungumzo na mazungumzo hayo haijulikani yatamalizika lini.

Mheshimiwa Naibu Spika, tunawaomba viwanja Zanzibar kwa kujenga Ofisi vipo. Waache mazungumzo, waombe viwanja waweze kujenga lakini wakisubiri wanazungumza hii kama inabidi wanavuta muda na wakati, wakati muda wa kujenga hawajakuwa nao na wala hawajakuwa na tamaa ya kujenga. Mheshimiwa Waziri naona Kamati imemwambia kwamba tunataka Kurugenzi za Zanzibar na wao wafanye kazi katika jengo linaloridhisha na linaloitwa kwamba ni jengo la Ofisi siyo nyumba imegeuzwa jengo wanasema ni Ofisi, hiyo haitowezekana.

Mheshimiwa Naibu Spika, makazi ya Ofisi za Ubalozi wetu wa nje pamoja na Ofisi zao hayaridhishi na kwa nini hayaridhishi? Kwa sababu kuanzia sasa pesa nyingi tunapoteza kulipa katika majengo. Ikifika mwaka lazima tutenge bajeti ili tulipe pesa za Ofisi. Kwa mwaka huu tayari Wizara imeshatenga bilioni 21.6. Pesa hizi ni za kodi za walalahoi tunazokwenda kulipa, kwa nini tunashindwa kujenga? Tungejenga ili kunusuru pesa za walipa kodi wetu tena maskini wa Tanzania walalahoi.

Mheshimiwa Naibu Spika, namwomba Mheshimiwa Waziri, hili wazidi kuliangalia maana hizi pesa zitatoka nyingi na pesa hizi kama wangekuwa wanatoa kidogo kidogo huku wanaanza kujenga Ofisi zetu za Ubalozi tungekuwa tayari tuko mbali na tungeweza kupata mafanikio.

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine, Ubalozi wa Oman umetoa kiwanja Muscat. Tayari Mheshimiwa Rais Mstaafu Dkt. Jakaya Kikwete amekwenda kuweka jiwe la msingi. Hata hivyo, toka mwaka 2012 hadi hii leo hakuna kinachoendelea na wako tayari wenyewe kuchukua sehemu yao kwa sababu wameshatuona hatuna maendeleo ya kuyafanya. Ingawa aliomba 1.8 billion lakini mpaka leo hajapewa.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia naiomba Wizara ya Fedha wangefanya kila mbinu, hizi pesa zikatoka angalau tukaonekana na sisi tunajihangaisha kuleta maendeleo. Ikiwa watu wamesema ukibebwa na wewe jikaze, wametupa kiwanja, wako tayari kutusaidia ina maana sisi kujiendeleza tunashindwa? Mheshimiwa Waziri akishirikiana na Wizara ya Fedha, naomba hili waliangalie na liweze kufanikiwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, unyanyasaji wa wafanyakazi wa majumbani nje. Unyanyasaji huu umekuwa mkubwa na vijana wetu wengi wanaondoka kinyemela, Wizara au Serikali inakuwa haijuii, Balozi kule za nje hawajui kama vijana wetu wapo. Sasa hili walitilie mkazo na waweze kujua mbinu wanazopita na waweze kujua Ma-agent wanaosimamia ili hili jukumu liweze kumalizika.

Mheshimiwa Naibu Spika, mtoto yeyote anauma, lakini akiwa wa mwenziwe, mtu anajifanya punguani anamwuona haumi, lakini mtoto anauma na hasa akiwa katika nchi yako akaondoka, akaenda nchi nyingine na nchi yenyewe ina ubalozi na akafika akateseka bila Wizara kujua au ubalozi kujua na hiyo yote inaelekea kwamba wanaondoka hawajui, watafute mbinu wanapita vipi, inakuwaje mpaka wanafika waweze kuwasaidia. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naiomba bado Wizara ya Fedha kwa bajeti hii ingawa safari hii imepanda kidogo kwa 17 percent basi waweze kusimamia hii bajeti itoke kwani ikitoka ndiyo manufaa kwa Tanzania. Tunamwona Mheshimwia Waziri anavyohangaika, anavyokwenda safari zote ndani na nje ili kuisaidia Tanzania na hali tunaiona Tanzania tunavyopiga hatua. Naomba Mheshimiwa Waziri hizi pesa zitoke, Balozi zetu zipate pesa, waweze kufanya kazi na tufaidike. Haitofaidika Balozi itafaidika Tanzania nzima. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa haya machache, naunga mkono hoja.