Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2017 na Mpango wa Maendeleo ya Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019; na Mapendekezo ya Serikali Kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019

Hon. Dr. Philip Isdor Mpango

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Nominated

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2017 na Mpango wa Maendeleo ya Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019; na Mapendekezo ya Serikali Kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019

WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Spika, napenda nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa Rehema zake na kuniwezesha kusimama tena mbele ya Bunge lako Tukufu kuhitimisha mjadala wa Hotuba ya Bajeti Kuu ya Mwaka 2018/2019.

Mheshimiwa Spika, siku ya Alhamisi tarehe 14 Juni, 2018 niliwasilisha mbele ya Bunge lako Tukufu Taarifa ya Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2017 na Mpango wa Maendeleo wa Mwaka 2018/2019 na pia Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio Mapato na Matumizi kwa mwaka wa fedha 2018/2019.

Mheshimiwa Spika, katika hotuba hizo nilieleza mambo mbalimbali yaliyotekelezwa na Serikali kwa kipindi cha mwaka 2017/2018. Matokeo ya utekelezaji, changamoto zilizojitokeza, mambo ya msingi ambayo Serikali inakusudia kutekeleza katika mwaka 2018/2019 na mapendekezo ya bajeti.

Mheshimiwa Spika, baada ya mawasilisho hayo, Waheshimiwa Wabunge walipata nafasi kwa siku saba; tarehe 18 – 22 na tarehe 25 na leo tarehe 26 Juni, 2018 ya kujadili Hotuba ya Bajeti ya Serikali kwa mujibu wa Kanuni ya 106(1) ya Kanuni za Kudumu za Bunge, Toleo la Januari, 2016. Hivyo napenda kutumia fursa hii kukushukuru kwa dhati kabisa wewe binafsi, Naibu Spika na Wenyeviti wa Bunge kwa kuendesha mjadala huu vizuri ambao unatarajiwa kuhitimishwa leo jioni kwa kura.

Mheshimiwa Spika, kabla sijaendelea zaidi, napenda kutambua michango mizuri iliyotolewa na Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti chini ya Mwenyekiti wake Mheshimiwa Hawa Ghasia, Mbunge wa Mtwara Vijijini. Pia Makamu Mwenyekiti, Jitu Soni, Mbunge wa Babati Vijijini.

Mheshimiwa Spika, nakiri kuwa Kamati hii ilihoji mambo mengi na pia kutoa ushauri kuhusu hatua mbadala au maboresho. Mimi na wenzangu katika Wizara ya Fedha na Mipango, tunaahidi kutoa ushirikiano wa hali ya juu kwa Kamati maana tunaamini kwamba Wajumbe wote wa Kamati ya Bajeti wataendelea kuongozwa na maslahi ya Watanzania walio wengi, hasa wanyonge katika kuishauri Serikali. Ahsanteni sana Kamati ya Bajeti.

Mheshimiwa Spika, aidha, nawashukuru Waheshimiwa Wabunge wote waliochangia kwa kuzungumza na kwa maandishi. Jumla ya Wabunge 208 wamechangia hoja niliyowasilisha. Kati ya hao, 180 wamechangia kwa kuzungumza na 28 kwa maandishi. Naomba niseme kwa niaba ya Serikali, ahsanteni sana Waheshimiwa Wabunge kwa michango yenu mliyoitoa kwenye bajeti hii kwa niaba ya wananchi mnaowawakilisha.

Mheshimiwa Spika, nawashukuru pia wananchi wote waliotoa maoni na ushauri juu ya Hotuba ya Bajeti ya Serikali kupitia majukwaa mbalimbali na vyombo vya habari. Napenda kuwahakikishia kuwa Serikali inathamini sana michango hiyo, nami na wataalam wa Wizara ya Fedha na Mipango na taasisi zilizo chini yake tumeyapokea na tumejipanga kuyafanyika kazi mambo yote waliyotushauri kwa maslahi ya Tanzania. Baadhi tutayazingatia katika bajeti hii na mengine katika bajeti zijazo.

Mheshimiwa Spika, naomba niweke wazi kabisa, tumeyapokea pia mawazo ya Wabunge kutoka Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni. Hata hivyo, napenda nisisitize kuwa tumepokea yale tu yanayoendana na Dira ya Maendeleo ya Tanzania 2025 (The Tanzania Development Version 2025), Mpango wa Pili wa Maendeleo wa Miaka Mitano uliopitishwa na Bunge lako Tukufu na Ilani ya CCM kwa ajili ya uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2015 ambayo imebeba ahadi za Chama Tawala kilichochaguliwa na wananchi na kukipa ridhaa ya kuongoza nchi.

Mheshimiwa Spika, nyaraka nilizozitaja ndiyo chimbuko la ajenda za Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, Rais wetu wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzania. Kamwe hatutasita kumsifia Rais wetu kwa kazi nzuri iliyotukuka anayowafanyia Watanzania wote. Hatuko tayari kuyumbishwa na agenda za kuandikwa. Sisi tunaandika wenyewe na tunatekeleza. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, wananchi wa Tanzania wanayo macho na hawalazimiki kuambiwa tazama. Wale wa Bukoba Mjini wanaona Shule ya Sekondari ya Ihungo iliyojengwa upya baada ya kuharibiwa na tetemeko la ardhi. Wananchi wa Mwanza wanafurahia daraja la waenda kwa miguu la Furahisha na kivuko kipya katika Ziwa Victoria. Wakazi wa Jiji la Arusha wanaona barabara mpya kutoka Arusha mpaka Tengeru ilivyopendezesha Jiji lao. Wananchi wenzangu wa Kigoma wanaona barabara ya Kidahwe hadi Kasulu imeanza kuwekwa lami. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, wananchi wa Dar es Salaam wanaona barabara za juu katika makutano ya TAZARA ikielekea kukamilika na bandari ikipanuliwa na kuongezewa kina. Wanaifakara sasa wanavuka mto Kilombero kupitia Daraja la Magufuli kwa usalama. Wananchi wa Mtwara wanaona uwekezaji mkubwa wa upanuzi wa Bandari ya Mtwara.

Mheshimiwa Spika, vilevile, wananchi wa Masasi sasa wataondokana na adha ya ukosefu wa maji, kufuatia ukarabati wa miundombinu ya kusambaza maji na ujenzi wa matenki ya kuhifadhia maji Chiwambo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, wakazi wa Jiji la Dodoma wameikaribisha Serikali na sasa tuko hapa. Wananchi wa Tanga wanashuhudia kuanza kazi ya ujenzi wa bomba la mafuta kutoka Hoima, Uganda hadi Chongoleani, Tanga. Upatikanaji wa dawa na vifaa tiba umeongezeka nchi nzima. Watoto wetu kote nchini wanafaidi elimu bila ada na kadhalika. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa yote hayo na mengine mengi, kwa nini tusiisifie Serikali ya CCM na Jemedari wetu Dkt. John Pombe Joseph Magufuli? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba nirejee kwa muhtasari mapendekezo yaliyoungwa Mkondo na wachangiaji wengi. Kwanza, kufuta kodi ongezeko la dhamani kwa taulo za kike; pili, kupunguza kiwango cha kodi ya Mapato ya makampuni kutoka asilimia 30 hadi asilimia 20 kwa wawekezaji wapya wa viwanda vya madawa ya binadamu na viwanda vinavyotengeneza bidhaa za ngozi; na kulinda wawekezaji wa ndani kwa kuongeza ushuru kwenye bidhaa zinazotoka nje ya nchi ambazo zinaweza kuzalishwa na viwanda vya ndani. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nne, ni kusamehe VAT kwenye vifungasho vya madawa ya binadamu vinavyotengenezwa mahususi kwa ajili ya viwanda vinavyozalisha dawa hapa nchini; na tano, kusamehe VAT kwenye virutubisho vinavyotumika kutengeneza vyakula vya mifugo kwa lengo la kupunguza gharama kwa wafugaji na kuhamasisha ufugaji bora.

Mheshimiwa Spika, sita, ni kuanzisha utaratibu maalum wa kusamehe kodi ambao unalenga kusamehe malimbikizo ya nyuma ya riba na adhabu kwa kiwango cha asilimia 100 na pia kuweka msisitizo katika utekelezaji wa miradi mikubwa ya kimkakati ikiwemo ujenzi wa reli kwa kiwango cha standard gauge, mradi wa kufua umeme Rufiji, mradi wa makaa ya mawe na chuma, Liganga na Mchuchuma.

Mheshimiwa Spika, pia mradi wa kusindika gesi asilia kuwa kimiminika kule Lindi. Pia kuna shamba la miwa na shamba la sukari Mkulazi na uendelezaji wa maeneo maalum ya uwekezaji. Hatua zote hizi zililenga kuhamasisha ujenzi wa viwanda hapa nchini. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba pia niseme kwa kifupi hoja na ushauri uliotolewa na Waheshimiwa Wabunge kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, kwanza tulishauriwa kuongeza tozo ya Sh.50/= kwa lita ya dizeli na petrol lakini pia zilitolewa hoja kuhusu pendekezo la Serikali la kuanzisha mfumo wa stamp za kodi za kielektroniki kwamba itekelezwe kwa uangalifu. Pia tulishauriwa kwamba Serikali itoe mara moja bakaa ya fedha za ushuru wa korosho zinazosafirishwa nje ya nchi kwa Bodi ya Korosho; nne, kwamba kwenye kuanzishwa kwa akaunti jumuishi ya Hazina tuelezwa kwamba hatua hii ni kinyume cha Katiba ya nchi na vilitajwa vifungu; tano, kuongeza bajeti ya Wizara ya Kilimo kwa kuzingatia umuhimu wa sekta hii.

Mheshimiwa Spika, pia kulikuwa na hoja kuhusu uhalisia wa bajeti ya Serikali, umuhimu wa kuboresha mazingira ya uwekezaji na kufanya biashara nchini. Vile vile ilitolewa hoja kwamba kasi kubwa ya ukuaji wa uchumi siyo halisia.

Mheshimiwa Spika, ilielezwa kwamba ni muhimu kuboresha mifumo ya ulipaji kodi na kuheshimu sheria zinazosimamia masuala ya ukusanyaji wa kodi, lakini pia ilielezwa kwamba mwenendo wa Sekta ya Fedha hauridhishi; lakini pia kwamba vyanzo vikuu vya mapato ya Halmashauri vinachukuliwa na Serikali Kuu bila kuvirejesha. Lingine ni kwamba Serikali sasa ichukue hatua za madhubuti zaidi kulipa madai mbalimbali na kwamba deni pia la Taifa linakua kwa kasi mno na hivyo lidhibitiwe.

Mheshimiwa Spika, mawazo mengine ni pendekezo la kufuta sheria iliyoanzisha Tume ya Mipango kwamba siyo jambo jema kwa maendeleo ya nchi. Pia kulikuwa na masuala mbalimbali yanayohusu mahusiano ya kiuchumi na kibiashara kati ya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar na Serikali na Muungano wa Tanzania; na vile vile tulishauria kwamba Serikali iangalie tena baadhi ya hatua mpya za mapato kwa mwaka wa fedha 2018/2019.

Mheshimiwa Spika, kama ulivyosema mwenyewe, ni wazi kabisa kuwa hoja na michango mbalimbali iliyotolewa kwa siku saba na Waheshimiwa Wabunge haiwezi kufafanuliwa kwa muda wa hizi dakika 40. Hivyo kama ilivyo ada, napenda kuliahidi Bunge lako Tukufu kuwa Wizara yangu itatoa ufafanuzi wa kina wa hoja zote na kuziwasilisha kwa maandishi kupitia kwa Katibu wa Bunge kwa ajili ya rejea ya Waheshimiwa Wabunge.

Mheshimiwa Spika, napenda nitumie nafasi hii kuwashukuru sana Waheshimiwa Mawaziri, Naibu Mawaziri na Mheshimiwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwa kufafanua vizuri baadhi ya hoja zinazohusu sekta wanazozisimamia.

Mheshimiwa Spika, wakati wote wa mjadala humu Bungeni kuhusu mapendekezo ya Serikali ya Makadirio na Mapato ya Matumizi kwa mwaka ujao wa fedha, Serikali ilisikiliza kwa makini maoni na ushauri kutoka kwa Waheshimiwa Wabunge.

Mheshimiwa Spika, napenda kuliarifu Bunge lako Tukufu kuwa Serikali sikivu ya CCM ilipokea na kufanyia kazi ushauri wa kizalendo kutoka kwa Waheshimiwa Wabunge na wadau mbalimbali na sasa napenda kuwasilisha mbele ya Bunge lako Tukufu mapendekezo ya kufanya marekebisho ya baadhi ya kodi na tozo kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, kwanza ni Sheria ya Michezo ya Kubahatisha Sura ya 41. Napendekeza kuwianisha viwango na msingi wa ukokotoaji wa kodi ya Michezo ya Kubahatisha hasa inayoshabihiana. Kwanza, kubashiri matokeo (Sport Betting for land based and on line). Pili, ni sehemu ya mashine 40 (forty machine sites); ya tatu ni Bahati Nasibu ya SMS Lottery na Casino za mtandao (internet casino).

Mheshimiwa Spika, kiwango cha kodi kinachopendekezwa katika michezo hii inayoshabihiana ni asilimia 25 ya mauzo halisi (Gross Gaming Revenue - GGRA) badala ya viwango na wigo uliopo sasa. Pili, kwa michezo ya Bahati Nasibu ya Taifa (National Lottery) napendekeza kutoza kodi kwa kiwango cha asilimia 20 kwa mauzo halisi (GGR) badala ya asilimia 10 ya mauzo ghafi (Gross Sales) inatozwa sasa.

Tatu, ni kuongeza kiwango cha kodi kwenye zawadi ya ushindi (Gaming Tax on Wining) kutoka asilimia 18 hadi asilimia 20 kwenye Bahati Nasibu ya SMS Lottery. Michezo ya kubashiri matokeo Sports Betting, Slot Machine Operations, Bahati Nasibu ya Taifa, sehemu ya mashine 40 na casino ya mtandaoni (internet/online casino). Nne, kupunguza kiwango cha kodi, kwenye zawadi ya ushindi yaani Tax on Winnings kwa michezo ya Casino ya ardhini (Land Based Casino) kutoka asilimi 18 hadi asilimia 12 au chini.

Mheshimiwa Spika, mapendekezo hayo ya marekebisho ya Sheria ya Kodi ya Michezo ya Kubahatisha, yanatarajiwa kuongeza mapato ya Serikali kwa kiasi cha shilingi bilioni 29.7.

Mheshimiwa Spika, napendekeza pia kufanya marekebisho kwenye Sheria ya Kodi ya Ongezeko la Thamani, Sura 148 ili kwanza kutoa msamaha wa kodi ya ongezeko la thamani kwenye mashudu yanayotumika kutengeneza chakula cha mifugo kama ifuatavyo:-

(a) Mashudu ya Soya HS Code 2304.00.00;

(b) Mashudu ya Pamba HS Code 2306.10.00; na

(c) Mashudu ya Alizeti HS Code 2306.30.00.

Mheshimiwa Spika, lengo la marekebisho haya ni kwa kuwawezesha wafugaji kupata chakula cha mifugo kwa bei nafuu zaidi na hivyo kuhamasisha ufugaji bora na kuongeza mchango wa Sekta ya Ufugaji katika pato la Taifa.

Mheshimiwa Spika, lakini pili, ni vifaa vya kukusanyia kodi taxi instruments ambazo ni stamp za kodi za kielektroniki HS Code 4907.00.90 na pili, ni mashine za kielektroniki za kutolea risiti (Electronic Fiscal Devices) HS Code 8470.50.00.

Mheshimiwa Spika, lengo la mapendekezo haya ni kutoa msamaha wa Kodi ya Ongezeko la Thamani, kwenye stamp za kodi za kieletroniki na mashine za kielektroniki za kutolea risiti ili kuwapatia unafuu wazalishaji wa bidhaa zinazobandikwa stamp za kodi za kielektroniki pamoja na kutoa hamasa juu ya matumizi ya mashine za kielektroniki za kutolea risiti. Hatua hizi pia zinatarajiwa pia kuimarisha usimamizi na udhibiti wa mapato ya Serikali.

Mheshimiwa Spika, mapendekezo haya ya Sheria za Kodi za Ongezeko la Thamani yatapunguza mapato ya Serikali kwa kiasi cha shilingi bilioni 1.6.

Mheshimiwa Spika, marekebisho ya Sheria ya Michezo ya Kubahatisha pamoja na Sheria ya Kodi ya Ongezeko la Thamani kwa ujumla wake yataongeza mapato ya Serikali kwa shilingi bilioni 639.0 hadi shilingi bilioni 646 sawa na ongezeko la shilingi bilioni saba. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Waheshimiwa Wabunge wengi walichangia hoja kuhusu marekebisho katika Sheria ya Tozo ya Huduma ya Bandari, Sura 264 kwa kurekebisha kifungu cha (3) kinachohusu kuongeza tozo za huduma za bandari kutoka Sh.500/= hadi Sh1,000/= kwa wasafiri ambao ni wakazi nchini na kutoka Dola za Marekani tano (5) hadi 10 kwa wasafiri ambao ni wageni nchini na kuomba kuwa msamaha uendelee kutolewa. Serikali imewasikia na msamaha huo utaendelea kutolewa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Waheshimiwa Wabunge walizungumzia pia marekebisho katika Sheria ya VAT aya ya 22, sehemu ya kwanza ya jedwali, kwa kufuta msahama wa kodi ya ongezeko la thamani kwa ndege ndogo za kukodisha na kuiomba Serikali iendelee kutoa msamaha huo. Nichukue fursa hii kulieleza Bunge lako Tukufu kwamba Serikali ya CCM imefanyia kazi hili na sasa msamaha huo utaendelea kutolewa kama kawaida. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, katika ukurasa wa 75 wa hotuba yangu nilipendekeza kufuta leseni ya kukidhi matakwa ya Sheria ya Afya na Usalama. Napenda kufanya marekebisho eneo hilo lisomeke, “kufuta ada ya leseni ya kukidhi matakwa ya Sheria ya Afya na Usalama.”

Mheshimiwa Spika, nirudie tena kusema, Chama cha Mapinduzi kimeielekeza Serikali yake kuwa sikivu na maboresho niliyoyaeleza yanathibitisha hilo. Aidha, tutaendelea kufanyia kazi mapendekezo yote na ushauri uliotolewa na Waheshimiwa Wabunge na wananchi wengine kwa maslahi ya Taifa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sasa niende kwenye baadhi ya hoja na ushauri uliotolewa na Wabunge wengi. Kwanza kulikuwa na hoja kwamba Serikali iongeze tozo ya Sh.50 kwa lita ya mafuta ya petrol na desel kwa ajili ya Mfuko wa Maji ili kuwe na chanzo kinachotabirika (ring fence).

Mheshimiwa Spika, Serikali inatambua uwepo wa changamoto ya upatikanaji wa maji katika sehemu mbalimbali nchini, mijini na vijijini. Katika kutatua changamoto hii Serikali imekuwa ikitenga fedha kwenye bajeti kwa ajili ya miradi ya maji. Aidha, baadhi ya miradi iligharamiwa moja kwa moja na wadau wa maendeleo wa nje ya nchi.

Mheshimiwa Spika, pamoja na juhudi hizi za Serikali na wadau wa maendeleo, bado maeneo mengi mijini na vijijini yanakabiliwa na uhaba wa maji. Kutokana na hali hii, Waheshimiwa Wabunge walipendekeza kuongeza tozo ya Sh.50/= kwa kila lita moja ya mafuta ya petrol na diesel kwenye bajeti ya mwaka ujao wa fedha.

Mheshimiwa Spika, Serikali imechambua kwa kina pendekezo hili. Pendekezo hili ni zuri lakini wakati huu sio muafaka kwa sababu zifuatazo:-

Mheshimiwa Spika, kwanza, tumetazama mwenendo wa matarajio bei ya mafuta kwenye Soko la Dunia na tunaona wazi kabisa kwamba kwa takwimu tulizonazo mwenendo wa bei ya mafuta ulimwenguni inakwenda juu, kwa hiyo, huu siyo wakati muafaka. Tutatoa takwimu kupitia kwenye Ofisi ya Katibu wa Bunge, kuonesha uchambuzi ambao tumefanya.

Mheshimiwa Spika, kutokana na Ripoti ya Hali ya Uchumi wa Dunia (World Economic Outlook ya IMF) iliyotolewa mwezi Aprili, bei ya mafuta ghafi inatarajiwa kuongezeka hadi kufikia kati ya wastani wa Dola 60 hadi 70 kwa pipa, ikilinganishwa na matarajio ya awali ya Dola za Marekani 50 mpaka 60 kwa pipa kwa mwaka 2018.

Mheshimiwa Spika, kwa mwaka 2019, bei ya mafuta ghafi inatarajiwa kufikia wastani wa Dola 65.5 kwa pipa na ongezeko hilo linachangiwa na makubaliano ya kupunguza uzalishaji wa mafuta kwa wanachama wa OPEC na baadhi ya wazalishaji wasio wanachama wa OPEC na hali hii inaweza kusababisha ongezeko la kasi ya mfumuko wa bei, nchini. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kodi na tozo zilizopo kwenye mafuta kwa sasa ni nyingi sana; na bidhaa za mafuta ya petrol na diesel zina kodi nyingi. Pendekezo lililotolewa na Waheshimiwa Wabunge kama lingekubaliwa, ingekuwa ni mzigo mkubwa sana. Kwanza kuna tozo na kodi kwa ajili ya mamlaka mbalimbali za umma, hizo ziko 11; ziko kodi za Serikali Kuu tatu, ziko kodi na tozo za mauzo ya jumla ya mafuta, ziko mbili; kuna tozo na kodi kwa mauzo ya rejareja ya mafuta, ziko tatu.

Mheshimiwa Spika, kwa kuzingatia kodi na tozo hizi, ni wazi kabisa kwamba bidhaa za mafuta ya petrol na diesel zimebebeshwa mzigo mkubwa sana katika kuchangia maendeleo ya nchi yetu.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, baada ya kufanya tathmini, tumeona kwamba tozo hii ingeongeza bei ya mafuta nchini na kusababisha kupanda kwa pump prices ya mafuta ya diesel na petrol. Tunayo mifano ambayo tumechambua kwa Dar es Salaam, kiasi gani ambacho bei ya mafuta ingeongezeka. Vile vile ingeleta athari kwenye utulivu wa uchumi kwa ujumla (macroeconomic stability) na kusababisha bei za bidhaa na huduma ambazo zinazalishwa hapa nchini kuongezeka (second round effect).

Mheshimiwa Spika, wakati wa Hotuba ya Wizara ya Maji na Umwagiliaji, zilielezwa njia mbadala za Serikali katika kugharamia Miradi ya Maji Nchini. Kwa hiyo, nisingependa kuzirejea, itoshe tu kusema kwamba tumetenga shilingi bilioni
673.2 kwa bajeti ya mwaka ujao wa fedha kugharamia miradi ya maji mijini ya vijijini.

Mheshimiwa Spika, ahadi ya Serikali ni kwamba tuna dhamira ya dhati ya kupeleka fedha kwenye utekelezaji wa miradi ya maji kama ilivyopitishwa na Bunge lako Tukufu kwa ajili ya mwaka ujao wa fedha. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, vile vile tumepokea fedha katika mwaka uliokwisha. Tumeshasaini mkataba na Benki ya Exim ya India, Mkopo wa Dola za Marekani milioni 500 kwa ajili ya utekekelezaji wa miradi ya maji katika Miji 21, Tanzania Bara na Zanzibar. Pia tumeshakamilisha majadiliano na Benki ya Dunia ambapo Dola za Marekani milioni 350 zinatarajiwa kupatikana na kati ya kiasi hicho Dola za Marekani 60 sawa na asilimia 17 kitatolewa mwezi Julai, 2018.

Mheshimiwa Spika, kulikuwa na hoja juu ya pendekezo la Serikali la kuanzisha mfumo wa stamp za kodi za kielektroniki. Serikali ilishauriwa itengeneze yenyewe mfumo wa ETS ili kiasi cha fedha ambacho kitalipwa kampuni ya CIPA iwe ni sehemu ya mapato ya Serikali, badala ya mapato yatokanayo na stamp ya kuchukuliwa na Kampuni Binafsi.

Mheshimiwa Spika, tumelichambua sana hili, niseme tu kwamba teknolojia ya kutengeneza mfumo huu ni mpya hapa nchini na hivyo hapakuwa na kampuni au taasisi ya Serikali iliyokuwa na uwezo wa kutengeneza mfumo huo. Kutokana na hilo, ililazimu Serikali itangaze Zabuni ya Kimataifa kwa uwazi na ndipo tulipompata Mzabuni mwenye uwezo na uzoefu wa kutengeneza mfumo huu kati ya Makampuni tisa yaliyojitokeza na hapakuwepo Kampuni ya ndani iliyojitokeza.

Mheshimiwa Spika, pia uwekezaji wa mradi huu ni zaidi ya mwaka mmoja na hivyo gharama za mradi zimezingatia muda huo ili kufidia gharama ya uwekezaji. Mapato yatokanayo na stamp za kodi kwa muda wa mwaka mmoja hayawezi kulingana na gharama za uwekezaji wa mradi huo katika mwaka wa kwanza.

Mheshimiwa Spika, vilevile mfumo huo utakapokamilika kujengwa, utaanza kuunganishwa kwenye viwanda vya uzalishaji kwa awamu kulingana na uhatarishi wa upotevu wa mapato katika bidhaa husika.

Mheshimiwa Spika, napenda niseme tu kwamba mfumo huu una faida nyingi sana ambazo zinazidi hizo gharama ambazo ilikuwa ni wasiwasi wa Waheshimiwa Wabunge.

Mheshimiwa Spika, niseme kuhusu ushuru wa korosho zinazosafirishwa nje ya nchi na matumizi yake. Mheshimiwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali na Waziri wa Kilimo walifafanua jambo hili kwa ufasaha jana na nisingependa kurudia. Ni vyema niseme na Watanzania wasikie na ikae kwenye Kumbukumbu Rasmi za Bunge lako Tukufu. Mimi Phillip Mpango siwezi kamwe kuwahujumu wananchi, wakulima wa korosho wa Mikoa ya Mtwara na Lindi au mkoa mwingine wo wote ule. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, niwahikikishie Watanzania kuwa Mtwara na Lindi nitakwenda, iwe katika kutelekeza majukumu yangu ya kikazi au kuwatembelea ndugu na marafiki. Hakuna anayeweza kunizuia, ni haki yangu na uhuru wangu kama Mtanzania ambayo haiwezi kupokonywa kwa vitisho. Hata ikibidi kufa katika kutumikia Taifa na iwe. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, katika nafasi mbalimbali nilizotumikia Serikali ya CCM na Taifa hili kwa ujumla, nimetumia uwezo wangu wote kuwatumikia Watanzania wa mikoa yote, nimefundisha wanafunzi wakiwa ni pamoja na wanaotoka Mikoa ya Kusini, nilipokuwa Mhadhiri Chuo Kikuu cha Dar es Dar es Salaam bila upendeleo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, aidha, kati ya mambo niliyofanya nikiwa Mshauri wa Rais, Uchumi katika Serikali ya Awamu ya Nne na nilipokuwa Mkuu wa Tume ya Mipango, nilikuwa mstari wa mbele kuishawishi Serikali kuifanya Mtwara iwe kitovu cha ukuaji wa uchumi hapa nchini (Mtwara Growth Pole) na kuingiza miradi mikubwa ya maendeleo, kwa mfano upanuzi wa Bandari ya Mtwara, LNG Plant Lindi, Barabara za uchumi na kadhalika katika Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano.

Mheshiomiwa Spika, mimi na wenzangu tuliishauri Serikali kutenga nafasi za upendeleo kwa vijana kutoka Mikoa ya Kusini kusoma masomo ya sayansi ili baadaye waweze kufanya kazi katika viwanda vinavyohusiana na Sekta ya Gesi Asilia; niliapa kuilinda na kuitetea Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inayotaka pamoja na mambo mengine kuhakikisha maendeleo ya Uchumi wa Taifa yanakuzwa na kupangwa kwa uangalifu na kwa pamoja ambayo iko kwenye Ibara ya 9 (d). Iweje leo niwahujumu wananchi wa Mtwara na Lindi?

Mheshimiwa Spika, kama yupo mtu ana chuki binafsi na Phillip Mpango, pasipo chembe ya ukweli, mimi namwombea msamaha kwa Mungu. Nasema tena, sitayumba katika kusimamia matumizi bora ya fedha za umma kwa mujibu wa sheria. Nawakumbusha wabadhirifu wa fedha za umma, wajue wanakula sumu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, najua muda siyo rafiki, nilitarajia ningesema sana leo, lakini naomba niseme jambo moja kabla sijaenda kwenye kuhitimisha. Kulikuwa na hoja kuhusu mapendekezo ya Serikali ya kufuta sheria iliyoanzisha Tume ya Mipango.

Mheshimiwa Spika, nilieleza katika hotuba niliyowasilisha tarehe 14 Juni, kwamba mapendekezo hayo ni mabadiliko ya kimuundo na siyo kufuta kazi muhimu za kupanga mipango ya maendeleo ya Taifa letu kwa kipindi cha muda wa kati na muda mrefu. Ukifuatilia historia ya muundo ya Taasisi ya Tume ya Mipango, iko wazi kuwa imekuwa inahama, kwa nyakati tofauti toka tulipopata Uhuru, Taasisi hiyo kuna kipindi ilikuwa peke yake kama Wizara kamili au Tume na wakati mwingine ikawa sehemu ya Wizara ya Fedha.

Mheshimiwa Spika, tena jambo hili siyo kwa Tanzania pekee, hata katika nchi jirani za Uganda na Rwanda hivi sasa, fedha na mipango vinaunda Wizara moja (Ministry of Finance and Economical Planning). Lengo kuu ni kuwianisha Mipango ya Maendeleo ya Taifa na ugawaji wa rasilimali fedha, jambo ambalo ni gumu pale ambapo Taasisi hizi zinapokuwa zimetenganishwa.

Mheshimiwa Spika, kama nilivyoeleza, kazi ya kuandaa na kusimamia mipango ya maendeleo ya Taifa ndani ya Wizara ya Fedha na Mipango, itaongozwa na Kamishna atakayekuwa na fungu lake kuwezesha utekelezaji wa kazi za idara hiyo. Kazi hizo zimeendelea kufanyika vizuri baada ya kuhamisha wataalam wa iliyokuwa Tume ya Mipango ndani ya Wizara ya Fedha.

Mheshimiwa Spika, naomba kuhitimisha. Kama nilivyoeleza katika hotuba yangu, hatua zilizopendekezwa kwenye Bajeti hii zinalenga kujenga msingi madhubuti wa uchumi wa viwanda na kupanua fursa za ajira na biashara. Dhamira yetu sote ni kufikia kiwango cha uchumi wa kipato cha kati itakapofika mwaka 2025. Ili kushiriki katika mafanikio hayo, ni lazima kila mmoja wetu ashiriki katika shughuli halali za kuzalisha na afanye hivyo kwa juhudi na maarifa ili kuleta tija.

Mheshimiwa Spika, kufanikiwa kwa Bajeti hii kunahitaji nidhamu ya hali ya juu katika usimamizi wa mapato na matumizi. Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere alituusia, nitasema kwa Kiingereza; mwanzo wa kunukuu: “our watch word must be frugality, this must run through the whole expenditure.” Mwisho wa kunukuu.

Mheshimiwa Spika, hii inatoka kitabu cha Freedom and Socialism. Ili kufikia azma hii, juhudi za pamoja kati ya Serikali na wadau wote zinahitajika ikiwa ni pamoja na kuhamasisha ushiriki wa sekta binafsi katika uchumi kwa kuwekeza zaidi katika maeneo ya kipaumbele. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, najua Watanzania tuna kiu kubwa ya kuendelea, tena haraka, lakini tukumbuke kuwa kila safari inaanza na hatua moja ikifuatiwa na nyingine. Vile vile njia ya maendeleo ina vikwazo vingi na haiwezekani kutatua changamoto zote za nchi hii kwa mara moja.

Mheshimiwa Spika, hata nchi zilizoendelea kama Marekani na Uingereza na kadhalika bado wanazo changamoto, bado nao wanajenga barabara, reli, hospitali na kadhalika. Hivyo ni muhimu Watanzania tuendelee kufanya kazi kwa juhudi na maarifa na kudumisha amani na umoja wa Taifa letu. Changamoto zitaendelea kuwepo.

Mheshimiwa Spika, mwisho, nawashukuru sana Waheshimiwa Wabunge wote, mjadala wetu wa siku saba umeyatendea haki mapendekezo ya Bajeti niliyowasilisha tarehe 14 Juni, 2017. Kukosoa kwa haki ili kujenga (constructive criticism) na kujikosoa ni sehemu muhimu sana katika harakati za maendeleo ya Taifa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa jambo kubwa la Kitaifa kama hili la Bajeti ya Serikali, ningestaajabu sana kama kila Mbunge angesimama na kusifia tu mapendekezo niliyowasilisha. Ndiyo maana mwanzo kabisa mwa Hotuba ya Bajeti Kuu nilibainisha kwa makusudi changamoto kubwa zinazotukabili kama Taifa na kwa ukweli, ili tujielekeze kwa pamoja katika kuzitatua.

Mheshimiwa Spika, imani yangu ni kuwa lazima tuwe wa kweli sisi wenyewe na kwa Taifa letu, lakini ni muhimu pia tuishi katika dunia, tusiishi katika dunia ya kufikirika. Kwa Kiingereza, we have to be honest ourselves, honest to our country and be as pragmatic as possible. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hatukuandaa bajeti hii kujifurahisha. Tumekuwa wakweli katika kutathmini utekelezaji wa Bajeti 2017/2018, tuliyoifanya. Katika mapendekezo tuliyoleta hapa Bungeni juu ya hatua ambazo tunaamini kwa dhati zitatupeleka mbele kama Taifa. Ukweli ni kwamba ni rahisi sana kusema, rahisi sana kwa rafiki zangu wa upande wa pili kukosoa, lakini nao wanajua kuwa ni vigumu kutenda, ndiyo maana hata walichokisema ni Bajeti Mbadala waliandikiwa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba nimalize kwa kumshukuru tena Mwenyezi Mungu kwa rehema zake. Namshukuru sana Naibu wa Waziri wa Fedha na Mipango, Mheshimiwa Dkt. Ashatu Kijaji, wewe mama ni mahiri kweli kweli, umekuwa ni msaada mkubwa sana. Namshukuru sana Katibu Mkuu na Wataalam wote wa Wizara ya Fedha kwa kuendelea kufanya kazi nzuri sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mwisho kabisa, nawaomba sana Waheshimiwa Wabunge wote kuunga mkono Bajeti hii ya Serikali kwa mwaka 2018/2019 ikiwa ni hatua nyingine thabiti ya Kujenga Uchumi wa Viwanda Nchini Tanzania na kuboresha maisha ya wananchi wetu. Natanguliza ahsante kwa kura yenu ya ‘Ndiyooo!’

Mheshimiwa Spika, naomba kutoa hoja.