Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Maliasili na Utalii

Hon. Mbaraka Kitwana Dau

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mafia

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Maliasili na Utalii

MHE. MBARAKA K. DAU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa fursa hii. Nami nianze kwa kuwapongeza sana watoa hoja, Mheshimiwa Waziri Dkt. Kigwangalla na wasaidizi wake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi natambua sana kwamba Mawaziri wa Serikali ya CCM ni wasikivu sana. Kwa bahati mbaya sana Mawaziri wa Wizara hii, Waziri na Naibu wake nashindwa kuelewa sijui kwa nini hawataki kunisikiliza mimi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tatizo la viboko waharibifu katika kisiwa cha Mafia nimeshalisema kwa Mawaziri wote wawili zaidi ya mara tano. Humu ndani pia nimeshalizungumza zaidi ya mara mbili lakini majibu ninayopata ni ya kusikitisha sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hali katika Kisiwa cha Mafia ni mbaya sana. Nilisema kwamba Mafia; na wala siyo suala la kusema ni suala ambalo linafahamika; Mafia ni kisiwa eneo ni dogo viboko wamezaliana wameshafika zaidi ya 40 sasa, viboko wameshaua mpaka wananchi licha ya kuharibu mazao. Wanakwenda wataalam wanapiga picha, wanaangalia, wana-camp siku mbili, siku tatu wanarudi. Hali bado ni mbaya sana, shughuli za maendeleo zimesimama, wananchi hawafanyi kazi, wanafunzi hawaendi mashuleni; viboko imekuwa ni hatari kabisa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mara ya mwisho wamekwenda kiasi cha wiki mbili zilizopita wakaua kiboko mdogo, ni kama ndama wa kiboko. Sasa hii siyo rocket science, eneo dogo, viboko wengi; kuna options mbili tu; tuwavune ama muwakamate muwahamishie katika maeneo ambayo wanaweza waka-arrange vizuri bila matatizo yoyote. Sasa tusisubiri, nilisema hapa tena kwa uchungu kabisa, jamani mnahitaji watu wangapi wafe ndipo mwende mkawaondoe wale viboko pale Mafia? Hali sio nzuri. Mheshimiwa Waziri leo hii mimi mara yangu ya mwisho kulisema humu ndani hili jambo, siku akifa mtu mimi nachukua familia yote nakuletea wewe Waziri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye ukurasa wa 61 wa kitabu hiki cha Mheshimiwa Waziri limezungumziwa suala la miradi ya kusimamia maliasili na kuendeleza utalii wa Kanda ya Kusini unaofadhiliwa na Benki ya Dunia. Nilikuwa na maoni na ushauri kwenye hili. Natambua kwamba sasa hivi wako katika mchakato wa usanifu, basi kuwe na kipengele cha utalii wa maeneo ya fukwe ambayo katika hili huna namna ukakiacha Kisiwa cha Mafia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Kisiwa cha Mafia kimejaliwa kuwa na vivutio vingi sana vya utalii akiwemo samaki anayeitwa papa (whale shark) kwa kizungu. Ni samaki ambaye anapatikana maeneo machache sana duniani. Pamoja na sifa za papa kuwa ni mkali lakini aina hii ya papa ni mpole sana, ana tabia kama za dolphin, anacheza na watalii, anaogelea nao na wala hana madhara nao, wanapatikana Mafia peke yake lakini nani anayejua kuhusu papa (whale shark)? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sana Mheshimiwa Waziri pamoja na Naibu muangalie namna gani mnaweza mka-promote hivi vivutio vinavyopatikana katika Kisiwa cha Mafia. Vivutio hivi viko vingi, kuna sport fishing, kuna maeneo mazuri sana ya diving, kuna fukwe nzuri, kuna magofu ya kale, kuna mji unaitwa wa Kisimani Mafia, mji maarufu sana ambao umezama ndani ya bahari, uko chini ya bahari mpaka leo majengo yapo lakini sijui Mheshimiwa Waziri na timu yako mnajua kisi gani kuhusiana na hazina hii inayopatikana katika Kisiwa cha Mafia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ushauri mwingine ni kwa Wizara nne kwa pamoja, Wizara ya Habari, Wizara hii ya Utalii, Wizara ya Mifugo na Uvuvi pamoja na Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi, hii package ambayo najua inafadhiliwa na Benki ya Dunia, kwenye ku-promote utalii katika Kisiwa cha Mafia lazima tuweke miundombinu sawa. Tatizo la Mafia sasa hivi ni accessibility, hakuingiliki, usafiri ni mbaya sana, hakuna boti, hakuna gati na hakuna miundombinu ambayo inaweza ika-support watalii wakaja kwa wingi. Kwa hiyo, mimi ningependa sana Mheshimiwa Waziri na timu yako mliangalie hili ni namna gani mnaweza mkaboresha kwa kushirikiana na Wizara nyingine, ikiwemo Wizara ya Ujenzi, namna gani mnaweza mkaboresha miundombinu ya gati pamoja na meli ili Mafia iweze kuwa na meli ya kisasa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, juzi tu hapa niliongea na Waziri wa Ujenzi, ipo meli pale ameitoa Bakhresa inaitwa Seabus, ile meli imetolewa bure kwa Serikali na wamepewa Wizara ya Ujenzi wamepewa ile taasisi inaitwa DMI ya mabaharia pale Dar es Salaam, hawana kazi nayo, ni meli kubwa ambayo inabeba takribani abiria 400. Tungeomba sana Mheshimiwa Waziri kwa kushirikiana na Waziri mwenzio wa Ujenzi angalieni namna gani mnaweza mkawashawishi DMI wakatupatia ile meli ikafanya kazi baina ya Nyamisati na Kilindoni.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine katika kuhakikisha kwamba utalii katika Kisiwa cha Mafia unatiliwa mkazo, ukurasa wa tisa wa kitabu hiki Mheshimiwa Waziri amesema vizuri tu kwamba katika kuunga mkono juhudi za kukuza utalii wa ndani Mheshimiwa Rais amejikita katika kuhakikisha analifufua Shirika la Ndege la ATCL. Pale Mafia tuna uwanja mzuri na wa kisasa kabisa, umekarabatiwa kwa Mfuko wa Millennium Challenge. Runway yetu ni kubwa na ni ya kutosha na abiria wapo. Tulikuwa tunaomba sana muangalie namna gani bombardier sasa inaweza ikaja Mafia hata kama kwa kuiunganisha na maeneo ya Mtwara, kwa maana itoke Dar es Salaam inatua Mafia inakwenda Mtwara halafu inarudi the same route.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri Mkuu alipokuja Mafia tulimpa hili ombi akasema kwa sasa tuna bombardier mbili itakapokuja ya tatu, tutaangalia uwezekano wa kuifungua route hii ya Mafia. Kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri nalileta hili kwako na wewe uangalie namna gani mnaweza mkatusaidia ili Mafia tuweze kuwa na usafiri wa bombardier kwa sababu itakapokuja pale itanyanyua sana sekta ya utalii sambamba na kufanya marekebisho madogo katika terminal building yetu ya Kiwanja chetu cha Mafia ambapo imechoka kidogo lakini runway iko sawa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ni suala la kodi, tozo, ada, zimekuwa nyingi sana kwenye tasnia hii ya utalii, nyingi mno kiasi kwamba inafikia wakati mpaka inaanza kuwapa mzigo watalii na watalii wengine wanasema utalii wa kwenda Tanzania ni very expensive kwa sababu kumekuwa na hizo multiple za kodi kila mahali. Kwa mfano, Mafia pale Mheshimiwa Waziri pengine kwa kushirikiana na Waziri mwenzio wa Uvuvi kuangalia namna gani mnaweza mkapunguza ile kodi ambayo kila mtalii anayeingia Mafia katika maeneo ya hifadhi ya bahari anatakiwa alipe dola 24 bila kujali gharama za hoteli, chakula au kitu kingine. Kitendo cha yeye kuingia eneo la hifadhi anatakiwa alipe dola 24 kila siku na hizo unazizidisha mara siku atakazokaa. Kwa kweli ni pesa nyingi sana na watalii wengi wanashindwa kuja wanaona kwenda Zanzibar ni bora zaidi kwa sababu hakuna hii tozo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.