Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Mifugo na Uvuvi

Hon. Dr. Christine Gabriel Ishengoma

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Mifugo na Uvuvi

MHE. DKT. CHRISTINE G. ISHENGOMA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipatia nafasi. Nianze kwa kuunga mkono hoja hii. Pia nawapongeza Mheshimiwa Waziri, pamoja na Naibu Waziri na Watendaji wote kwa kazi nzuri waliyoifanya kwenye Sekta hii ya Mifugo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ili uwe na mifugo na ufugaji wa kisasa ni lazima elimu itumike na hii elimu inatolewa na Afisa Ugani. Afisa Ugani ni watu muhimu sana. Kwa upande wa uvuvi kuna uhaba wa Afisa Ugani. Wanaohitajika ni 16,000 lakini waliopo ni 750 tu. Kwa hiyo, kuna Afisa Ugani 15,250. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nikija kwa upande wa mifugo na wenyewe kuna uhaba na hata hao waliopo, hawafanyi kazi vizuri. Kwa hiyo, nashauri Wizara kwa kushirikiana pamoja na TAMISEMI iangalie jinsi ya kuwapa mwongozo na utaratibu hawa Afisa Ugani wa Uvuvi na hasa wa Mifugo waliopo waweze kufanya kazi kwa kujituma.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sababu mpaka sasa hivi ninapoongea, hawawatembelei wakulima na hasa Maafisa Ugani wa Mifugo. Inabidi uwaite ndiyo waje wakutembelee. Siyo kama zamani walivyokuwa wanajituma. Kwa hiyo nashauri Serikali iangalie. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna sekta nyingine ambayo huwa haiongelewi sana, nayo ni ufugaji wa kuku wa kienyeji. Nikisema ufugaji wa kuku wa kienyeji, napenda sana nimpe pongezi rafiki yangu Profesa Salome Mtayoba kwa kuwa Mwenyekiti wa Bodi. Hongera sana kwa upande wa ufugaji. Ufugaji wa kuku wa kienyeji ni kitu kizuri sana kwa sababu unanufaisha sana familia kwa kuinua kipato na kuwapa ajira ya mara moja vijana.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, naomba licha ya Wizara kuona inaweka msisitizo, lakini naona kuwa msisitizo uwe zaidi na zaidi kuhusu hawa akinamama pamoja na vijana, pamoja na familia tuweze kuinua kipato, tuweze kuinua lishe. Sasa hivi tumefikia 32% ya Watanzania wengi hasa watoto ambao ni wadumavu (malnutrition). Kwa hiyo, kwa upande wa lishe, lazima tukazanie kwenye upande wa kilimo hasa ufugaji wa kuku wa kienyeji. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine ambalo nataka kuongelea ni ufugaji wa samaki kwenye upande wa mabwawa (fish ponds au aquaculture). Elimu hii haijaenea sana kwa wakulima au wafugaji. Hiki kilimo cha mabwawa ni rahisi sana kufanyika hata nyumbani kwako. Mahali popote unaweza ukafanya ili mradi una maji.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, kwa kuinua ufugaji wa samaki ambao hauna shida kukamatwa nyavu na kupigwa mabomu, naona Wizara ihimize kilimo cha uvuvi wa samaki kwenye mabwawa, kwa kifupi ni fish ponds, ambayo unaweza ukaenda wewe mwenyewe, hata mwanamke mwenyewe ukachukua samaki wako ukaja ukapika mara moja, watoto wako wakapata lishe na familia nzima ikapata lishe na kupandisha kipato. Kwa hiyo, nauliza upande wa Serikali, mkakati mkubwa sana waliouweka kwenye upande wa ufugaji wa samaki kwenye mabwawa ukoje? Naomba utiliwe mkazo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa niongelee migogoro ya wafugaji pamoja na wakulima. Kwa upande wa Mkoa wa Morogoro, hii bado ipo, hatuwezi kusema imekwisha. Imetulia kidogo kwa sababu sasa hivi kuna mvua, majani yanapatikana, malisho yanapatikana, ndiyo sababu imetulia. Ukienda kilosa kwenye Kijiji cha Mabwegere bado kuna matatizo ya wafugaji pamoja na wakulima. Akinamama hawapati raha kwenda kulima, kama mnavyojua wakulima wengi, zaidi ya asilimia 70 wanaotoa chakula ni wanawake.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, naomba sana waliangalie hilo. Dawa yenyewe iliyopo ni matumizi bora ya ardhi. Kwa hiyo, tuendelee kupima ardhi kusudi watu waweze kupata ardhi yao na waweze kuona ni wapi pa kulishia.

Mheshimiwa Naibu Spika, lingine ni elimu ya malisho. Jambo lingine ambalo linaweza likaondoa migogoro ya wafugaji pamoja na wakulima ni Elimu ya Malisho. Elimu ya Malisho bado haijaenea sana. Naomba sana wawahimize hao wafugaji na hii inawezekana wakiipata hii elimu hata kuhama hama kwa hawa wafugaji kutaacha, kwa sababu wataweza kustawisha malisho yao na wataweza kuyatumia wakati wowote na inaweza ikasaidia hata wakati wa kiangazi kwa sababu watatengeneza hay ambayo wanaweza kulisha mifugo yao. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, fedha za maendeleo, kama tulivyoona, kwa msimu wa mwaka 2017/2018 kwa upande wa mifugo iliinidhishwa shilingi bilioni nne na kwa upande wa uvuvi shilingi bilioni sita. Mpaka Machi mwaka huu 2018, hakuna hela yoyote ya maendeleo ambayo ilikuwa imeshatolewa. Sasa kama hela za maendeleo hazitolewi, miradi itaendeleaje au itafanyikaje? Kwa hiyo, naomba kama tunaidhinisha hela humu Bungeni, tujitahidi Hazina pamoja na Serikali kwa ujumla hela ziweze kutolewa kwa wakati.