Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Mifugo na Uvuvi

Hon. Vedastus Mathayo Manyinyi

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Musoma Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Mifugo na Uvuvi

MHE. VEDASTUS M. MANYINYI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ili niweze kuchangia kwenye Wizara hii ya Mifugo na Uvuvi. Kwa sababu ya muda, naomba tu niende moja kwa moja kwa kusema kwamba kwa upande wa mifugo kusema kweli Wizara wala Serikali haijafanya chochote kwa ajili ya kuwasaidia wafugaji.

Mheshimiwa Naibu Spika, hata ukiangalia katika kitabu chetu kwamba fedha kiasi gani zimetengwa kwa ajili ya kuwasaidia wafugaji, yaani ni kituko kabisa. Kwa hiyo, tunadhani Serikali ina changamoto kubwa, ione ni kwa kiasi gani, inahitaji ijipange kuhakikisha kwamba inawasaidia wafugaji.

Mheshimiwa Naibu Spika, suala lingine ni la mbegu bora. Mifugo mingi ya Tanzania pamoja na kwamba Tanzania ni nchi ya tatu, tuna ile mifugo ambayo ni aina ya zebu. Kwa hiyo, tunaifuga kwa muda mrefu lakini tija yake ni ndogo. Kwa hiyo, ushauri wangu, hebu Serikali iangalie kupitia hizi ranch zake iweze kuzalisha ng’ombe bora wa mbegu na iweze kusambaza kwa gharama nafuu. Tunadhani kwa namna hiyo, itaweza kuwasaidia Watanzania wengi waweze kufuga kwa tija kuliko ilivyo hivi sasa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nitoe tu ushauri, kwa sababu sisi mojawapo ya kazi yetu ni kushauri, ukiangalia hata ranch zetu za Serikali zote tulizonazo, nenda Kongwa na hizo za NARCO, zote zimekufa. Yaani ni kwamba zile ranch hazina tija. Ni vizuri wale Mameneja wa Ranchi zile badala ya kuteua tu kwamba tunadhani fulani ni mwaminifu tumkabidhi ranch, Mheshimiwa Waziri atangaze nani anaweza kusimamia? Naamini atapata watalaam wazuri wanaoweza kusimamia na wakaziendesha vizuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, haiwezekani ranch inaweza kubeba ng’ombe 16,000, unaipatia ng’ombe 4,000. Tafsiri yake ni kwamba tunawasaidia tu wale Mameneja pamoja na wale wahusika walioko kule, lakini hazina manufaa yoyote na hata sisi hatuwezi kujifunza kupitia zile ranchi. Kwa hiyo, huo ndio ushauri wangu kwa upande wa mifugo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa upande wa uvuvi, yawezekana nikatofautiana kidogo na wenzangu. Binafsi napongeza suala la ukomeshaji wa uvuvi haramu, kwa sababu gani? Maana wanasema penye ukweli lazima tuseme ukweli kwa sababu tunahitaji kuisaidia Serikali.

Mheshimiwa Naibu Spika, pale kwangu Musoma Mjini, baada ya zoezi la kukomesha uvuvi haramu kuendelea kwa muda, leo ukienda pale ukimwuliza kila mmoja anakubali kwamba sasa samaki wameongezeka. Kwa hiyo, hilo ni jukumu ambalo tuna kila sababu ya kupongeza kwa kazi hiyo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nimwambie Mheshimiwa Waziri, kuna yule ambaye ni DC wangu wa pale mjini, anasaidia sana suala la uvuvi haramu. Nimefanya mikutano mingi, wale wale waliokuwa wanachukia wakati ule wakisema wanakandamizwa, leo kila mmoja anakubali kwamba kweli samaki wanapatikana. Kwa hiyo, nampongeza Mheshimiwa Waziri kwa hilo.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa pamoja na haya mafanikio, yako matatizo na changamoto ambazo lazima tujipange tuone namna ya kuzimaliza. Ile timu ya Mheshimiwa Waziri inayofanya kazi ile, wako wengine wanafanya kazi kwa uaminifu, lakini wengine wanatumia nafasi zile kuwaumiza wale wavuvi pamoja na wale raia wa kule. Shida iliyoko pale, wakati mwingine naweza kuita ile timu, kama ilivyokuwa Operesheni Tokomeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, labda nitoe mfano, bahati nzuri Mheshimiwa Waziri na mimi tumewasiliana mara nyingi. Moja, unakuta labda wale watu wanapofanya operesheni zao, wakikuta tu kwenye ile gari labda hawana ile koleo ya plastic, anaambiwa faini shilingi milioni moja hadi shilingi milioni tatu, wakati vile vitu ni vya kuelimishana tu. Mtu yule hana gumboot anapigwa faini ya shilingi milioni moja hadi shilingi milioni tatu. Kwa yule mvuvi wa kawaida anayefanya biashara hiyo, maana yake ni kwamba tunamfilisi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mara nyingi nimekwenda kwa Mheshimiwa Waziri kuhusiana na wafanyabiashara wa Musoma wanaosafirisha samaki. Wote tunafahamu, samaki wote tunaokula huku hatuna magari yenye refrigerated system yanayoweza kusafirisha samaki. Wanaweka kwenye Fusso, wanafunga kwenye maboksi wanasafirisha.

Mheshimiwa Naibu Spika, wale samaki wakiwa kule Musoma, kabla ya hawajaondoka, wanaenda pale kwenye Kituo cha Uvuvi, ndipo wanapakilia, wanakaguliwa. Wanapofika Singida, hatuna storage system. Ile Fusso inafunguliwa, wanacheki box moja moja, zinakutwa kilogram tatu kwenye tani 14. Wakikuta kilogram tatu wanapiga faini shilingi milioni sita. Hivi hiyo ni tokomeza au ni kuendeleza uvuvi? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kibaya zaidi, bahati nzuri mimi na Mheshimiwa Waziri tumekuwa tukiwasiliana na kusema kweli mambo mengine amekuwa akiyamaliza. Nitoe mifano kwa machache ambayo tumewasiliana na tuone namna ya kuyarekebisha ili mambo yaende. Hili gari moja walipofungua pale Singida wakakuta hakuna kilogram tatu, ni under size walipigwa faini ya shilingi milioni sita. Waliponiambia, nikazungumza na Mheshimiwa Waziri. Akaniambia hiyo gari kama ina kilogram tatu peke yake hebu iachieni.

Mheshimiwa Naibu Spika, wale watu walionesha kiburi wakasema wanarudi ku-check upya. Badala ya ile sampling waka-check upya. Kwenye kilogram 14, maana yake ile kazi waliifanya kwa siku mbili. Tafsiri yake ni kwamba hilo gari siyo refrigerated. Kwa hiyo, matokeo yake wale samaki wote walifika Dar es Salaam sokoni wakiwa wameharibika. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kibaya zaidi walipo-check tena kila box, wakapata kama kilogram 30 zikiwa ni under size. Ile faini ikarushwa kutoka shilingi milioni sita mpaka shilingi milioni 20. Hivi tunategemea hiyo ni Operesheni Tokemeza au hiyo ni kusaidia kumaliza tatizo? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, ndiyo maana nasema kwamba pamoja na nia nzuri ya Serikali, ihakikishe kwamba samaki wanapatikana, lakini lazima tuangalie namna ya utendaji wa kazi unavyofanyika. Kibaya zaidi, wale watu wakisikia tu kwamba Mheshimiwa Waziri kaambiwa jambo, kalalamikiwa hapo ndipo wanakuja zaidi.

Mheshimiwa Naibu Spika, mfano wa pili, maana ni vizuri tukaenda kwa mifano. Ilitokea kwa mtu mmoja, kwa kawaida wale wanaofanya biashara ya kununua samaki, akinunua samaki anapaswa awe na watu wengine nadhani kama wanne hivi. Kwa bahati mbaya wakati anakata leseni akalipia wale watu wote lakini jina likaandikwa la kampuni yake peke yake. Walipomshika mtu wake wakati yeye hayupo, matokeo yake akapigwa faini. Kwa bahati nzuri nilimweleza Mheshimiwa Waziri na akafuatilia. Hapo sasa ndiyo wakasema wanamtafuta na mwenye mzigo naye wanataka wampige faini. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, ndiyo maana tunasema kwamba ukiangalia zoezi lenyewe ni nzuri, lakini kwa maana ya kwamba tunategemea kama sisi watu wa Musoma pale tuna viwanda visivyopungua vinne vya samaki ambavyo vyote vimekufa. Hata hivyo, leo furaha yangu ni kuona kwamba viwanda sasa vinachipuka kwa maana vinafunguliwa na samaki wanapatikana. Sasa kupatikana kwa samaki huku lazima kuendane na kuwapa watu wetu elimu kuliko hiki kinachofanyika sasa, badala ya kuwaendeleza badala yake tunawamaliza.

Mheshimiwa Naibu Spika, suala lingine hata zile nyavu tunapozishika, Mheshimiwa Waziri mwenyewe anajua; tunashika nyavu haramu, zile nyavu tuna haki ya kuziteketeza. Sasa hebu tuelezwe, ile boti, zile engine, tuna haja gani ya kuziharibu? Maana yake ni kwamba unachoma ile boti, tafsiri yake ni kwamba unataka yule mtu afilisike. Kwa hiyo, huyo mtu unapotaka afilisike, sasa kesho ataendeshaje maisha yake? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, pamoja na kazi nzuri ambayo ndugu zetu wanaifanya, lakini hebu waone namna gani wanaweza wakaifanya kwa uzuri zaidi. Ushauri wangu, ni vizuri kwenye ile timu watu wengi wakahusika mle; watu wa usalama, Polisi na wenyewe wakawemo mle. Ule mchanganyiko tunadhani utasaidia kuwafanya watu wawe na mbinu nzuri za kufanya ile Operasheni ambayo kazi…

TAARIFA . . .

MHE. VEDASTUS M. MANYINYI: Mheshimiwa Naibu Spika, hiyo taarifa naipokea kwa maana kwamba, Mheshimiwa Waziri ajue sasa kwamba hizo ni changamoto ambazo anahitaji kuzirekebisha kwa haraka, otherwise badala ya huu uvuvi kutusaidia, basi utaendelea kuwa kero.

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo, nami naunga mkono hoja, lakini hayo yote yarekebishwe ili mambo mazuri yaendelee kufanyika. Ahsante sana.