Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Mifugo na Uvuvi

Hon. Susanne Peter Maselle

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Mifugo na Uvuvi

MHE. SUSAN P. MASELLE: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi.

Mheshimiwa Naibu Spika, Hatukatai wala hatupingi Operation Uvuvi Haramu, lakini tunapinga operation hii inavyoendeshwa. Operation hii inaendeshwa bila kufuata weledi, wavuvi wetu wamekuwa wakiombwa rushwa kutokana na hii operation, utakuta mvuvi anaombwa rushwa ya mpaka milioni ishirini. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hawa watu ni watu wa chini sana, unaenda unamwomba rushwa ya milioni ishirini, wakikataa wanakamata nyavu zao hata kama ni halali kwa uvuvi, wanaenda kuzichoma. Huu ni uonevu wa hali ya juu sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, wavuvi wetu wamekuwa wakionewa sana, wanalipishwa fine ambazo haziko kwenye Sheria ya Uvuvi ya Mwaka 2003. Mtu analipishwa fine mpaka milioni hamsini. Huyu ni mvuvi wa hali ya chini, unategemea afanye nini? Matokeo yake wanaenda wanauza mpaka rasilimali zao, wanauza nyumba zao, wengine mpaka wamekufa kwa pressure kwa sababu ya hizi fine. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, najua sheria hii inafanyiwa marekebisho na Wizara, lakini naomba sana Wizara inapofanya marekebisho haya iwahusishe wavuvi ambao ni wadau na ambao wataitumia hii sheria kuliko wao kukaa wenyewe na kufanya marekebisho.

Mheshimiwa Naibu Spika, ni kwa nini Wizara inaogopa kukutana na hawa watu? Kuna shida gani? Ni vizuri Wizara ikawashirikisha; (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, wakati Wizara imetoa tangazo la hii operation ya kukamata nyavu ambazo si halali, lakini vile vile imezuia nyavu halali kuingia nchini. Kuna nyavu ambazo zimezuiliwa mipakani, sasa wanataka hawa watu watumie kitu gani? Hii sekta imeajiri zaidi ya watu milioni nne, sasa mnataka wafanye shughuli hii kwa kutuimia vifaa gani? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na kwamba wamezuia lakini sioni Wizara ikiweka mkakati wa kuweza kuwasaidia hawa wavuvi kwa kuwapatia vifaa vya kisasa kwa ajili ya kuvua. Wamekuwa wakivua kwa kutumia nyavu zisizokuwa halali kwa sababu hawana vifaa na Serikali nimeona kwamba, haina makakati wowote wa kupeleka pesa kwenye hii Wizara kwa ajili ya kutatua haya matatizo ya wavuvi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pia hakuna elimu ambayo inatokewa kwa hawa wavuvi. Wavuvi wengi wamezaliwa wakakuta wazazi wao wanafanya shughuli hii ya uvuvi, kwa hiyo wakaingia tu kwenye hii shughuli na kuanza kuvua, hawajui hata sheria zipi ambazo zinatakuwa kuwaongoza, na Wizara imekaa tu, inatangaza operation bila hata kutoa elimu kwa hawa watu, ili waweze kujua ni nini wanatakiwa wafanye. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nizungumzie kuhusu viwanda. Hakuna viwanda vya kutosha vya kuchakata samaki. Tungeomba Wizara ije itueleze ina mkakati gani wa kuongeza viwanda kwa ajili ya kuchakata samaki kwa sababu, viwanda vilivyopo ni vichache na haviendani na mahitaji ya samaki wanaopatikana. Vile vile pia wametangaza Operation Number 3 ambayo wamesema kwamba kutakuwa na mahakama ambazo zinatembea.

Mheshimiwa Naibu Spika, hii Mahakama itakuwa inafanya kazi gani, kwa sababu wamesema kwamba watakuwa wanaenda moja kwa moja kwa wavuvi wakiwakamata wanawahukumu hapo hapo; hawa wavuvi wataweza kujitetea wakati gani? Kwa sababu hawatakuwa na muda wa kuweza kutafuta watu wa kuwatetea. Wamesema kwamba, watakuwa wanaenda wanatoa hukumu hapo hapo, hiyo si sawa.

Mheshimiwa Naibu Spika, niombe tu kwamba Bunge liunde tume ambayo itaweza kufuatilia hizi operation; kwa sababu kumekuwa na matamko. Tangu matamko yametoka watu wamefanya kama mradi wa kujipatia pesa, kila mmoja anakuja na la kwakwe mpaka wavuvi wamekuwa hawaishi kwa raha. Tukumbuke kwamba hawa ni watu wanyonge na wamesema kwamba Serikali yao inasimamia watu wanyonge. Watu wanyonge ndio hawa wavuvi wetu, sasa wanataka wasimamie watu gani? Naomba kwenye hilo tuweze kulisimamia kabisa kwa sababu hizi operation zinaumiza wavuvi wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nizungumzie kuhusu mifugo...

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa mzungumzaji)