Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Kilimo

Hon. Mahmoud Hassan Mgimwa

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mufindi Kaskazini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Kilimo

MHE. MAHMOUD H. MGIMWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nikushukuru kwa kunipa nafasi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa namna ya kipekee naomba nimshukuru sana Mheshimiwa Dkt. Charles Tizeba pamoja na dada yangu Mheshimiwa Dkt. Mary Mwanjelwa kwa kazi nzuri wanayoifanya katika Wizara yao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nichukue fursa hii kumshukuru sana Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli. Juzi kwenye hotuba yetu ya maji tulizungumza sana tatizo la Maafisa Ugani kwenye eneo la maji, siku ya pili akalitolea maagizo kwamba Maafisa Ugani sasa hivi wawajibike direct kwenye Wizara ya Maji pamoja na Ardhi. Tunamuomba tena Mheshimiwa Rais Maafisa Ugani hawa kwenye eneo la kilimo tunaomba wawajibike direct kwa Katibu Mkuu ili kusudi wawe na control moja kwa moja kutoka Wizarani otherwise tatizo litaendelea kuwepo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, asilimia 75 ya Watanzania ni wakulima wamejiajiri katika sekta hii. Kwa masikitiko makubwa sana bado hatuitendei haki hii asilimia 75. Ukiangalia kwenye bajeti yetu na ukiangalia kwenye makubaliano yetu na nchi za Afrika Mashariki na zile za Kusini Mashariki za SADC na sisi Watanzania tulisaini Maputo na Malabo Agreement kwamba asilimia 10 ya bajeti kuu itengwe kwenye sekta ya kilimo, lakini ukliangalia kwenye analysis mpaka sasa Tanzania ndiyo nchi ya mwisho tuna asilimia 3.1, hii ni aibu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika eneo ambalo tunaajiri Watanzania wengi hakika tunatakiwa tupeleke bajeti ya kutosha. Kwenye eneo hili tunategemea kutengeneza ajira ya kutosha na ndiko itakakopatikana raw material ya kutosha kwa ajili ya viwanda vyetu. Tumekusudia kwenda kwenye uchumi wa viwanda, tunaendaje kwenye uchumi wa viwanda kama hatuna uhakika wa kupata raw material ya kutosha? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ushauri wangu tunaiomba Serikali iangalie upya kwenye eneo hili. Hata kama hatuwezi kufika asilimia 10 ya bajeti kuu tufike hata 6 au 7 tulingane na wenzetu wa Uganda na Kenya, lakini kuendelea kuwa kwenye mstari wa mwisho kwa asilimia 3.1 haifurahishi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo lingine ambalo nilitaka kulizungumzia ni Benki ya Maendeleo ya Kilimo. Tulipokuwa tunatamka kwamba tunataka tuanzishe Benki ya Maendeleo ya Kilimo tulikuwa tunaamini kabisa benki hii itakuja kwa ajili ya manufaa ya wakulima, lakini ukiangalia structuring yake utakuta kwanza yenyewe haipo kwenye site ya wakulima, makao makuu yako Dar-es-Salaam, haya tujiulize Dar-es-Salaam kuna mashamba makubwa kiasi gani? Taratibu za kumsaidia mtu apate mkopo kama ana shida ya kupata mkopo aende Dar-es-Salaam akatafute mkopo mtu kutoka Mufindi au Njombe? Kwa hiyo, Serikali iangalie upya itengeneze matawi nchi nzima na ilenge wakulima kwenye site, tunataka tupate matawi ya kutosha. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia katika analysis mpaka sasa hivi mtaji walionao Benki ya Kilimo ni shilingi bilioni 67 na mahitaji ya Watanzania ni shilingi bilioni 800, tofauti ni kubwa sana. Kwa hiyo, naomba sana Serikali tuongeze mtaji kwenye benki hii ili kusudi tupate uhakika wa kuajiri Watanzania walio wengi kwenye eneo hili na ambako inapatikana raw material ya kutosha. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa masikitiko makubwa lazima niliseme jambo hili tena. NFRA ambao ndiyo wanahakikisha usalama wa mazao yetu na chakula chetu hapa nchini waliomba shilingi bilioni 86, lakini kwenye bajeti tumewatengea shilingi bilioni 15. Mgogoro mkubwa wa wakulima wa mahindi unaanzia hapa na kwenye eneo hili kama Mheshimiwa Waziri hatakuja kuonesha kwamba ataongeza hela nitakuwa mtu wa kwanza kushika shilingi hapa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka jana tumepata tatizo kubwa sana kwenye eneo la mahindi. Kwa mfano, sasa hivi kwetu Mufindi debe la mahindi ni Sh.3,000 ambalo lina kilo 20, kilo moja ya sukari ni Sh.3,000 wapi na wapi? Kwa hiyo, mtu akitaka sukari kilo moja ni lazima auze debe moja la mahindi, itafika sehemu tutakata tamaa kulima mahindi. Serikali isipotamka kupagusa hapa kwenye NFRA nitawashawishi Wabunge wenzangu tunaotoka Mufindi na maeneo mengine kwamba tunapigwa. Hatuna jambo la kujivunia katika Mikoa ya Iringa, Njombe na Mikoa yote ya Kusini kama mahindi yetu tuliyokuwa nayo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaipongeza Serikali imeamua kujenga maghala na vihenge ya kisasa kabisa katika Kanda Nane, sasa kwa shilingi bilioni 15 tutaweka nini humu? Tumejenga majengo ambayo yanagharimu fedha nyingi lakini hela za kuweka hayo mahindi kwenye maeneo haya, hazipo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tusiendelee kuwaonea watu wa Mufindi na wa maeneo mengine kwenye eneo hili, mimi sipo tayari. Waziri ni rafiki yangu tumekua wote na mimi ndiye Mwenyekiti wake wa Kamati lakini leo nasema najivua Uenyekiti wa Kamati, nabaki kama Mbunge wa Mufindi Kaskazini. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naipongeza sana Serikali, kulikuwa kuna jambo la madeni ya mawakala Serikali ikasema lazima ihakiki. Haya Serikali mmehakiki baada ya kuhakiki what next? Kwa nini tusiseme mawakala hawa wanadai, hawa hawadai, kusudi Serikali iwalipe ambao wanadai? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nimalizie. Hawa mawakala wengine wanakufa, wanauziwa majumba yao, wana hali mbaya kwenye maeneo mbalimbali. Ifike wakati Serikali itoe tamko mawakala wanaodai ni hawa na hawa hawadai. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna Maofisa wa Serikali ambao wameshiriki kwenye utapeli, kwa nini wasichukuliwe hatua za kisheria? Tunaenda kushughulika tu na mawakala? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, nataka niseme tu kwamba naunga mkono hoja lakini nasema hivi Mheshimiwa Waziri asipokuja na majibu kuhusu kuongeza hela NFRA nitashika shilingi yake.