Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019

Hon. Zainab Mndolwa Amir

Sex

Female

Party

CUF

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019

MHE. ZAINAB M. AMIR: Mheshimiwa Mwenyekiti, naipongeza Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji chini ya Waziri Mheshimiwa Charles J. P. Mwijage, pamoja na Naibu Waziri wake Mheshimiwa Engineer Stella Manyanya kwa kazi kubwa wanayofanya katika Wizara hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza, naishauri Serikali ifufue viwanda vilivyopewa wawekezaji mfano, Kiwanda cha Nguo cha Karibu Textile Mills (KTM) ili kiweze kufanya kazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, naishauri Serikali kupitia upya viwanda vilivyo katika Mkoa wa Morogoro, mfano Morogoro Shoes Company, Polyester, Magunia, Tannaies, Ceramic, Canvas, Moprocco ambapo katika miaka ya 1980 vilikuwa vinazalisha bidhaa mbalimbali, pia vilikuwa vinatoa ajira kwa Watanzania na pia kuongeza pato la Taifa letu. Hivyo wawezeshaji ambao wameshindwa kuviendeleza viwanda hivyo wapokonywe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tatu, Serikali ijenge Kiwanda cha Matunda (juice) ili wakulima wa Mkoa wa Tanga waweze kuuza matunda katika kiwanda hicho. Hivyo ni muhimu Serikali ijenge kiwanda katika Mkoa wa Tanga kwa sababu Mkoa wa Tanga wananchi wake hulima kwa wingi matunda ya aina mbalimbali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nne, naishauri Serikali iishauri Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) iwakadirie wafanyabiashara mapato mara baada ya miezi mitatu (grace period) ndipo TRA wafanye makadirio ya mapato na siyo kuwakadiria kabla ya kuanza biashara. Hii hupelekea wafanyabiashara hao kushindwa kuendelea na biashara na kufunga na kulikosesha Taifa mapato.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tano, naishauri Serikali ikutane na watendaji wa taasisi ya Fair Competition Commission (FCC) ili iwashauri FCC watoe elimu kwanza kwa wafanyabiashara kabla hawajaagiza bidhaa kutoka nje ya nchi. Siyo FCC kusubiri wafanyabiashara walete bidhaa kisha kuanza kuwatoza faini kubwa na mara nyingine kuziteketeza na kuwasababishia hasara kubwa wafanyabiashara hao na pia kulikosesha Taifa mapato.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sita, naishauri Serikali ionane na kikosi cha Zimamoto cha Mkoa wa Dar es Salaam ili kuondoa bugudha iliyopo, maana wafanyabisahara wanalazimishwa kununua fire extinguisher kilogramu tano kwa shilingi 200,000 kisha kila mwaka kulipia shilingi 40,000.

Mheshimiwa Mwenyekitik, ushauri wangu ni kwamba Zimamoto wawaelekeze wamiliki wa majengo ya biashara Dar es Salaam (Kariakoo), waweke fire extinguisher katika corridor za nyumba hizo na siyo ndani ya maduka, sababu moto ukiotokea usiku fire extinguisher limefungiwa ndani ya duka halitasaidia kuokoa mali za mfanyabiashara.

Mheshimiwa Mwenyekiti, saba, naishauri Serikali itenge maeneo maalum kwa wafanyabishara ndogo ndogo (Wamachinga) wa Mkoa wa Dar es Salaam na siyo kuweka biashara zao mbele ya maduka ya wafanyabishara. Hii itasaidia Wamachinga kuweza kulipa pato la biashara zao, huduma za jiji, huduma za usafi kwa urahisi na kuweza kuliingizia pato Taifa letu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho, nawatakia kazi njema na Mwenyezi Mungu awape afya njema na umri mrefu katika kuyaendea majukumu yenu ya kila siku.