Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019

Hon. Hamoud Abuu Jumaa

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kibaha Vijijini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019

MHE. HAMOUD A. JUMAA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa napenda kuanza kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuniwezesha kufika hapa na mimi nashiriki kikao hiki kujadili hotuba hii ya bajeti ya Wizara hii ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji kwa mwaka 2018/2019. Hotuba hii imeandaliwa kwa kuzingatia mwelekeo wa nchi hivi sasa kuwa Tanzania ya viwanda. Napenda kuipongeza Wizara kwa kuandaa bajeti nzuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kuipongeza Serikali kwa hatua mbalimbali inazoendelea kuzichukua hasa kusimamia na kaulimbiu ya Serikali ya Awamu ya Tano ya kujenga uchumi wa Taifa unaotegemea viwanda. Kwa maelezo ya Serikali ni kwamba hadi kufikia mwezi Februari 2018 viwanda vipya 3,306 vimeanzishwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, aidha, Serikali inaendelea kuhamasisha uwekezaji katika viwanda kwa kutoa vivutio vya kodi na visivyo vya kodi kwa wawekezaji mahiri, hii itasaidia kuongeza hamasa kwa wawekezaji wa ndani na wa nje. Hata hivyo naipongeza Serikali kwa kuendeleza na kuboresha miundombinu wezeshi kama vile barabara, reli, bandari, umeme na maji, haya ni maandalizi rafiki na ya kuvutia kwa wawekezaji watakaokuja na kuwekeza. Lakini haikuishia hapo, Serikali imeendelea kuhuisha sera, sheria na kanuni pamoja na kufuatilia utendaji wa viwanda vilivyobinafsishwa na kuchukua hatua stahiki kwa wamiliki walioenda kinyume na mikataba ya mauzo, ni hatua nzuri kwani kuna baadhi ya wawekezaji wasiokuwa waaminifu wamekuwa wakitumia viwanda hivyo vilivyobinafsishwa kwa matumizi tofauti na yale yaliyokusudiwa na Serikali wakati wa sera ya ubinafsishaji. Mpango wa Serikali kwa Mikoa na Halmashauri zote nchini kuwaelekeza kutenga maeneo ya uwekezaji wa viwanda ni mpango mzuri wenye tija na malengo chanya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imehakikisha Sekta ya Hifadhi ya Jamii inashiriki kikamilifu katika ujenzi wa uchumi wa viwanda, pamoja na miradi mingine, NSSF na PPF kwa kushirikiana na Jeshi la Magereza wanatekeleza mradi mkubwa wa uzalishaji wa sukari Mkoani Morogoro, ni mpango mzuri na wa kupongezwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lengo hasa la mradi huo ni kuzalisha tani 250,000 za sukari na umeme MV 40, ni mkakati mzuri na wa kupongezwa hasa katika kipindi hiki ambacho Serikali ina mpango wa kufanya nchi yetu kuwa ya viwanda.

Mheshimiwa Mwenyekiti, uchumi wa viwanda unaendana hasa na masuala mazima ya kisayansi, hivyo ni budi Serikali kuendelea kufanya tafiti mbalimbali ili kuwezesha kugundua changamoto zilizopo na kukabiliana nazo. Viwanda vina faida kubwa sana kwa maendeleo ya nchi,viwanda hukuza ajira na kuleta maendeleo chanya, nchi kubwa duniani zenye uchumi mkubwa ziliwekeza zaidi katika viwanda na kuweza kuzalisha bidhaa mbalimbali na kuziuza nje ya mipaka yao na hivyo kupata fedha za kigeni. Dhana nzima ya viwanda isibezwe kwani ni mpango wenye malengo mazuri kwa maendeleo ya Taifa letu na ni mpango endelevu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imeendelea kuwa karibu na sekta binafsi, ni jambo la kupongeza kwani sekta binafsi ina mchango mkubwa katika ukuaji wa uchumi nchini, kushirikiana kunaiwezesha Serikali kujua changamoto inazokabiliana nazo sekta binafsi na kuja na suluhisho la kitatuzi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naishauri Wizara kuendelea kuwa walezi wa sekta binafsi na kupokea ushauri ili uchumi wa nchi yetu uweze kuwa endelevu katika ukuaji. Kuna changamoto mbalimbali ambazo sekta binafsi inakutana nazo hasa katika masuala mbalimbali ya kikodi na kadhalika, lakini Wizara inatakiwa kuwa karibu na wadau hawa ili changamoto hizo ziwezekutatuliwa. Nampongeza Mheshimiwa Rais wetu kwa kukaa na sekta binafsi na kuwapa nafasi ya kuwakilisha kero zao, maoni na ushauri na kwa baadhi ya changamoto kuzifanyia kazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nchi yetu ina fursa nyingi sana za kiuwekezaji, tuna maeneo mengi ambayo yanavutia kwa wawekezaji, tunahitaji wawekezaji wa ndani na wa nje, ni wajibu wa Wizara kuendelea kuwavutia wawekezaji kuweka mazingira rafiki ili tuweze kupata wawekezaji wengi zaidi kuja kuwekeza katika nyanja mbalimbali na kuzalisha ajira kwa wingi kwa watu wetu. Naishauri Wizara kuendelea kuwachukulia hatua wawekezaji ambao wamekalia baadhi ya maeneo kama viwanda, kuvifunga au kubadilisha matumizi, wanyang’anywe na kupewa wawekezaji wengine wenye nia njema na kuendeleza maeneo husika. Kibaha Vijijini tuna maeneo yaliyopimwa kwa ajili ya uwekezaji, maeneo ni mazuri na ukizingatia Kibaha Vijijini ni mji unaokuwa sasa na hata mazingira ya kiuwekezaji ni mazuri, miundombinu ipo vizuri, hivyo naomba Wizara itupe kipaumbele pale inapopata wawekezaji basi waje Kibaha Vijijini kuwekeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.