Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi kwa mwaka wa fedha 2016/2017.

Hon. Joseph Kizito Mhagama

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Madaba

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi kwa mwaka wa fedha 2016/2017.

MHE. JOSEPH K. MHAGAMA: Mheshimiwa Naibu Spika, awali ya yote, napongeza sana hotuba ya Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, Mheshimiwa Mwigulu Lameck Nchemba Madelu. Hotuba hii imesheheni mipango na mikakati madhubuti ya kuliondoa kundi la Watanzania wafikiao asilimia 80 na kuwafikisha kwenye uchumi wa kati. Umadhubuti wa Mipango na Mikakati iliyopo katika hotuba hii ni kielelezo cha umadhubuti wa Mheshimiwa Waziri Mwigulu Nchemba. Napenda nimthibitishie kuwa wananchi ninaowawakilisha, Jimbo la Maduba wanatambua sana umahiri na umadhubuti wa Mheshimiwa Mwigulu Nchemba.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nielekeze mchango wangu katika maeneo yafuatayo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza, ni matumizi ya mbegu bora za kilimo. Kadiri ya Utafiti wa Masalwala (2013), asilimia 93 ya mbegu zinazotumiwa na wakulima katika misimu mbalimbali ni recycled from previous crops. Hii inatokana na gharama za mbegu hizo, upatikanaji, ubora wa mbegu hizo na uelewa wa wakulima juu ya matumizi na umuhimu wa mbegu hizo. Napongeza kuwa Wizara imeliona hilo na tayari imejipanga kuongeza uzalishaji wa mbegu kutoka tani 10,270.86 hadi tani 40,000 ikiwa ni mara nne. Ni hatua kubwa sana. Naomba Wizara isimamie hili, tujipime kwa kiasi hiki na mwaka ujao twende mbali zaidi.
Mheshimiwa Naibu Spika, aidha, ni muhimu katika mikakati ya kufanikisha zoezi hili, makampuni ya ndani yapate kipaumbele kujengewa uwezo wa kuzalisha mbegu. Yapo makampuni yenye nia na yamethubutu kuanza. Ni vema yakapata ruzuku kuyawezesha kuzalisha mbegu za mazao ya kilimo.
Mheshimiwa Naibu Spika, pili ni mfumo wa upatikanaji wa pembejeo. Nimpongeze sana Mheshimiwa Waziri Mwigulu Nchemba kwa kuamua sasa kupitia upya mfumo wa usambazaji wa pembejeo kwa kuzingatia malalamiko makubwa ya mfumo wa sasa wa ruzuku. Mkakati huu mpya ni mzuri.
Mheshimiwa Naibu Spika, mapendekezo yangu ni kuharakisha mapitio haya. Case studies ni nyingi, zipo Asasi na wadau wengi waliojaribisha models mbalimbali. Miongoni mwa wadau hao ni AGRA, SNV, RUCODIA, RUDI, BRTENS na kadhalika. Wadau hawa tayari wana models mbalimbali za usambazaji wa pembejeo. Jambo muhimu ni kwamba mfumo mzima wa usambazaji pembejeo uwe enterprise led. Ni vema Wizara ikakutana na wadau hao na kuchukua uzoefu wao katika suala zima la Agro-Dealers Development.
Mheshimiwa Naibu Spika, tatu ni mazingira wezeshi ya kilimo-biashara. Hotuba ya Mheshimiwa Mwigulu imefafanua vizuri mazingira wezeshi ya kilimo-biashara. Katika aliyosema Mheshimiwa Waziri, ningependa kuongeza yafuatayo:-
(i) Mafanikio ya kilimo yanategemea sana mafanikio ya miundombinu ya barabara vijijini, upatikanaji wa rasilimali fedha na elimu ya kilimo; na
(ii) Model ya mradi wa MIVARF uliopo chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu ni nzuri sana ya comprehensive approach ambayo kama Wizara itachukua model hizi, maendeleo ya kilimo chenye tija tutayapata kwa haraka sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, nne, Chuo cha Mafunzo ya Mifugo LITA (Madaba). Tunaomba chuo hiki kitoe pia mafunzo ya kilimo na kipandishwe hadhi na kuwa chuo kikuu kwani Mikoa ya Kusini mahitaji yetu katika eneo hilo ni makubwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja.