Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maji na Umwagiliaji kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019

Hon. Lucy Fidelis Owenya

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maji na Umwagiliaji kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019

MHE. LUCY F. OWENYA: Mheshimiwa Naibu Spika, maji ni uhai na ni rasilimali muhimu sana kwa maendeleo ya binadamu katika kila sekta, kilimo kinahitaji maji, viwanda, binadamu, wanyama na viumbe vyote hai bila maji haviwezi kuishi, hivyo maji ni kitu muhimu sana kwa uhai hata mwisho wa uhai wa mwanadamu bado hawezi kuzikwa lazima atumie maji kusafishwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, maji safi na salama bado ni tatizo katika Mikoa mingi mfano hapa Dodoma bado maji siyo salama kupelekea wananchi wengi kupata magonjwa ya mlipuko na pia kuwepo na typhoid. Kwa kuwa Dodoma ni Makao Makuu na ni mji tunategemea kuwepo na ongezeko kubwa sana la watu. Je, Serikali ina mkakati gani ya kuboresha mfumo wa maji taka kuwa mkubwa zaidi ili uweze kubeba maji yote na kuwepo na dampo la kutupa taka? Hii ikiwa ni sambamba na kupata maji safi na salama ya kunywa. Kwa mfano, Manispaa ya Moshi mbona ina maji safi na salama kama iliwezekana kule, hata hapa itawezekana.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu mradi wa maji uliopo Jimbo la Moshi Vijijini, Kata ya Mbokomu mradi uliofadhiliwa na ADB, mradi huu umejengwa chini ya kiwango na chanzo cha maji kilivyojengwa hakina uwezo wa kudhibiti uchafuzi wa maji isitoshe maji yameelekezwa kwenye chamber ya bomba kwa kutumia mfumo ya sandarusi (sulphate) iliyojazwa udongo na chamber ya kutolea maji ilifunikwa bati yenye kutoa kutu hivyo maji kupita kwenye bomba bila kuchujwa, hii ni hatari sana kwa afya za wananchi wa kule. Nashauri Serikali ije itembelee mradi ule uliojaa ufisadi, isitoshe hata maji ya uhakika hayatoki na ichunguze walioidhinisha kwa kutia saini kwamba mradi huu wa maji umekamilika na kuidanganya Serikali ili wawajibishwe na mradi ule ule ukarabatiwe upya.

Mheshimiwa Naibu Spika, tatizo la kutua mama kubeba maji kichwani hasa vijiji bado ni tatizo kubwa sana la maji, Serikali imekuwa ikitenga fedha kwa ajili ya maji vijijini na miundombinu yake lakini panakuwepo na changamoto nyingi mfano kufikia mwaka 2018 Serikali kwa kushirikiana na wadau ilijenga vituo mbalimbali 125,068; vituo hivi vilikuwa vihudumie watu milioni 30.9 sawa na asilimia 85.2 ya wananchi milioni 36.3 wanaoishi vijijini, cha kusikitisha ni vituo 86,877 pekee vinavyotoa huduma kwa watu milioni 21.7 sawa na asilimia 59.8 ya wananchi waishio vijijini. Hivyo vituo 38,209 vilivyojengwa havifanyi kazi sawa na asimilia 30.5 ya vituo vyote. Je, kwa mtindo huu Serikali ina mikakati ya ukweli ya kumtua mama kubeba maji kichwani?

Mheshimiwa Naibu Spika, je, mpaka sasa Mfuko wa Maji una kiasi gani, Serikali ina mpango gani? Bado naendelea kutoa pendekezo la kutoza shilingi 50 kwenye mafuta ili zirudi kwenye Mfuko wa Maji. Ni lini mradi wa maji uliopo Kata ya Old Moshi Magharibi, Jimbo la Moshi Vijijini, kijiji cha Manda utakamilika?