Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maji na Umwagiliaji kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019

Hon. Joyce Bitta Sokombi

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maji na Umwagiliaji kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019

MHE. JOYCE B. SOKOMBI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kupata nafasi nami kuchangia kwenye Wizara hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunatambua fika kwamba maji ni uhai, 2016/2017, fedha za maendeleo zilikuwa shilingi bilioni 915.1 lakini hadi kufikia Machi, 2017, zilitolewa asilimia 17.8 tu na 2017/2018 fedha za maendeleo zilikuwa shilingi bilioni 408.6 lakini hadi kufikia Machi, 2018 zilitolewa asilimia 22 tu, maana tumeona pia hata kwenye kitabu cha Kamati imeelezea hivyo kwa fedha za maendeleo na asilimia 1.8 tu kwa fedha za nje.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Tume ya Taifa ya Maji Fungu Namba 05 zimeainishwa shilingi bilioni 5.6 tu na hadi kufikia Desemba, 2017 hakuna fedha za ndani zilizotoka, zilitoka fedha za nje tu ambazo ni asilimia 1.8. Kufikia mwaka 2018 Serikali na wadau wa maji walijenga vituo 125,086 vya maji vijijini ambavyo ilikuwa vihudumie watu milioni 30.9, sawa na asilimia 85.2 ambao ni wananchi milioni 36.3 waishio vijijini. Jambo la kusikitisha vituo vinavyofanya kazi kati ya hivyo vituo vyote ni vituo 86,877 tu ambavyo vinahudumia watu milioni 21.7 sawa na asilimia 59.8 ya watu waishio vijijini. Kwa hiyo kuna hasara ya vituo 38,209 havifanyi kazi, sawa na asilimia 30.5 ya vituo vyote. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye kitabu cha Waziri sijaona mahali popote ambapo wameelezea namna ya kuvikarabati vituo hivyo au kuhakikisha vituo hivyo vinafanya kazi. Sasa tunasema kwamba tunahitaji kumtua mwanamke ndoo kichwani, kwa hali hii ukiangalia kweli mwanamke wa kijijini tutamtua ndoo kichwani? Ndivyo wanavyoishi watu wengi vijijini, sisi tuko mijini maji yakikatika kidogo tu tunaanza kulalamika, je, wale akina mama wanaoamka saa kumi alfajiri kwenda kufuatilia maji? Haya, ameamka saa kumi alfajiri, kurudi saa sita mchaa! huyu mwanamke ataleta maendeleo kwenye familia kweli? Tunahitaji watu wa vijijini wawe na maendeleo, walete maendeleo, kwa hali hii anahangaikia maji muda wote maendeleo atayafanya saa ngapi? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninapenda kuishauri Serikali, hasa Waziri wa Fedha, Mheshimiwa Dkt. Mpango atueleze fedha zinazoidhinishwa za mwaka jana kwanza zilienda wapi? Zinavyoidhinishwa ihakikishwe fedha zote ziende kwa wakati ili miradi ifanye kazi kama inavyokusudiwa.(Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaomba sana, mimi ni mwanamke, nawaonea huruma sana wanawake wenzangu wa vijijini. Tunaomba tafadhali sana, tunajua pale Mheshimiwa Waziri wa Maji hakikisha unaongea na Waziri wa Fedha unapata pesa kwa wakati ile miradi ifanye kazi vijijini. Kwa mfano, Mkoa wangu wa Mara tumezungukwa na Ziwa Victoria mwaka jana niliongea hapa, tumezungukwa na Ziwa Victoria, lakini fikiria Serikali inaweza kutoa maji Ziwa Victoria inapeleka maji Shinyanga, lakini sisi wa Mkoa wa Mara hatuna maji, inasikitisha!(Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba tafadhali sana hakikisheni Mkoa wa Mara tunapata maji hasa Bunda hatuna maji ya kutosha, Musoma Vijijini hatuna maji ya kutosha. Pale Musoma tu tupo lakini hatuna maji ya kutosha, Tarime ni sehemu ya mjini tu, sehemu za vijijini watu hatuna maji ya kutosha.