Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia

Hon. William Tate Olenasha

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Ngorongoro

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia

NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunijalia afya njema na kuniwezesha kusimama mbele ya Bunge lako Tukufu kutoa maelezo mafupi kuhusu hoja zilizotolewa na Waheshimiwa Wabunge katika kujadili bajeti ya Wizara yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kuchukua nafasi hii kumshukuru sana Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli kwa kuendelea kuniamini na kuniteua kutumikia katika Wizara hii nyeti. Itoshe kusema kuwa, napata furaha sana kufanya kazi na Serikali hii ya Awamu ya Tano ambayo katika kipindi kifupi imefanya mambo makubwa yanayolenga kumkomboa Mtanzania na hasa Mtanzania mnyonge. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, namshukuru sana Mheshimiwa Profesa Joyce Lazaro Ndalichako, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia kwa maelekezo na ushauri wake kwangu ambao umeendelea kunijenga siku hadi siku. Pia nawashukuru Katibu Mkuu, Naibu Makatibu Wakuu na watendaji wote wa Wizara na taasisi zake kwa ushirikiano wanaonipa katika kutekeleza majukumu yangu ya kila siku ndani ya Wizara. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kutumia fursa hii kipekee kabisa kumshukuru mke wangu mpendwa na watoto wangu kwa upendo, maombi na uvumilivu wao katika kipindi ambacho nimekuwa mbali nao nikilitumikia Taifa. Vilevile nawashukuru sana wapiga kura wangu wa Jimbo la Ngorongoro kwa kuendelea kuniamini na kunipa ushirikiano katika utekelezaji wa shughuli zangu za maendeleo Jimboni. Napenda kuwaahidi kuwa sitawaangusha. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikushukuru wewe binafsi na Waheshimiwa Wabunge wa Bunge lako tukufu kwa michango yao mizuri tangu kuwasilishwa kwa hotuba ya bajeti ya Wizara yetu. Nawaahidi kuwa nitaendelea kushirikiana nao ili kuhakikisha kwamba tunatoa elimu bora kwa watoto wa Kitanzania na kwa maendeleo ya nchi yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya shukrani hizo, sasa naomba nitoe ufafanuzi kuhusu baadhi ya hoja ambazo zimechangiwa na Waheshimiwa Wabunge. Mtaniwia radhi kwa sababu ya wingi wenu na muda nilionao sitaweza kuwataja lakini naomba nizijibu hoja kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, baadhi ya Waheshimiwa Wabunge waliopata fursa ya kuchangia hoja yetu waliitaka Serikali kutoa ufafanuzi juu ya suala la upatikanaji wa vitabu hasa vya Darasa la IV wakieleza kuwa kuchelewa kwa vitabu hivyo kutaathiri wanafunzi wa darasa husika ambao wanatakiwa kufanya Mtihani wa Taifa mwaka huu. Serikali inatambua kuwa upatikanaji wa vitabu ni muhimu sana katika suala zima la ufundishaji na ujifunzaji wa mtoto na wote ni mashahidi kuwa suala hili limekuwa ni kipaumbele cha Serikali kwa muda mrefu. Kuthibitisha hili mtakumbuka kuwa pale vitabu vya darasa la pili na tatu vilipokosewa, Wizara haikusita kuchukua hatua mara moja za kiutendaji na kinidhamu kwa wote waliohusika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kulitaarifu Bunge lako tukufu kuwa vitabu vya kiada vya darasa la kwanza hadi la nne vinaendelea kuzalishwa na kusambazwa kwa shule zote kwa masomo yote. Zoezi la usambazaji wa vitabu hivyo limeanza katika mikoa 12 na litakamilika tarehe 30 Mei, 2018 kwa mikoa yote nchini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vitabu hivi vimechelewa kuchapishwa na kusambazwa kutokana na zoezi kubwa la kurudia uhariri wa uchapishaji wa vitabu vya darasa la kwanza hadi la tatu vilivyobainika kuwa na makosa ya kiuchapaji na kimaudhui. Zoezi la uhariri na uchapishaji limefanyika kwa umakini mkubwa na kwa kuwashirikisha wataalamu mbalimbali wa vyuo vya ualimu na vyuo vikuu ili kuhakikisha tunakuwa na vitabu vyenye ubora unaotakiwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna baadhi ya Wabunge ambao wametoa hoja kwamba vitabu ambavyo vinasambazwa vina makosa. Sitakuwa na nia ya kujaribu kujibizana na Waheshimiwa Wabunge ambao walidai kwamba kuna makosa kwa sababu kwa sasa sijajiridhisha na nakala za vitabu wanavyotumia, lakini mimi na Wizara tuko tayari kukaa nao kuangalia vitabu wanavyosema vina makosa ni vitabu gani na kama kawaida iwapo kuna makosa tutasahihisha lakini vilevile wale ambao wamehusika watachukuliwa hatua stahiki.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baadhi ya Waheshimiwa Wabunge waliopata fursa ya kuchangia hoja yetu waliitaka Serikali kuhakikisha kuwa Bodi ya Kitaalamu ya Walimu inaanzishwa mapema ili kuweza kuwa na walimu ambao wana ubora. Napenda kulitaarifu Bunge lako tukufu kwamba Rasimu ya Muswada wa Sheria ya Bodi ya Kitaalam ya Walimu ya 2018 ambao pamoja na mambo mengine, utaweka masharti ya Sheria ya Uanzishwaji, Utawala na Uendeshaji wa Bodi ya Kitaalamu ya Walimu, tunategemea kwamba Muswada huu utakamilika baada ya kufanyiwa kazi na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali na Wizara inatarajia kuwasilisha Bungeni katika kipindi kifupi kijacho.

Kwa hiyo, niwahakikishie Waheshimiwa Wabunge kwamba hoja yenu hiyo ya msingi imetiliwa maanani na hivi karibuni tunategemea kuwa na sheria hiyo ili Bodi hiyo ya Kitaalamu ya Walimu iweze kuanza kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baadhi ya Waheshimiwa Wabunge waliopata fursa ya kuchangia hoja yetu walitaka kujua ni Wanzanzibar wangapi wanapata mikopo ya elimu ya juu, kiasi kinachotengwa kwa wanafunzi kutoka Zanzibar na ni kwa nini wanafunzi Wanzanzibar hawapati mikopo kwa asilimia 100. Lengo la kuanzishwa kwa Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu mwaka 2004 ni kuwawezesha wanafunzi wasiokuwa na uwezo wa kumudu gharama za elimu ya juu kupata elimu hiyo. Serikali inakaribisha wadau wengine zikiwemo taasisi za kifedha kuwakopesha wanafunzi kwa masharti wanayoweza kuyamudu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mujibu wa sheria iliyoanzisha Bodi ya Mikopo, mikopo ya elimu ya juu inapaswa kutolewa kwa Watanzania wahitaji na wenye sifa (needy and eligible). Sheria pia imetaja vigezo vikuu vinavyopaswa kuzingatiwa kuwa ni lazima mwombaji awe Mtanzania, awe amepata udahili wa masomo ya shahada au stashahada katika taasisi inayotambuliwa na Serikali na asiwe na vyanzo vingine vinavyogharamia masomo yake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mujibu wa sheria hiyo, Bodi inayo mamlaka ya kuweka utaratibu wa kuwabaini wahitaji. Kwa sababu hiyo, kila mwaka Bodi huandaa mwongozo kwa kushirikisha wadau unaopaswa kuzingatiwa na waombaji na kuweka masharti ya utoaji mikopo kwa mwaka husika. Kwa mwaka 2017/2018 mwongozo uliotolewa ulizingatia waombaji wenye mahitaji maalum wakiwepo wale waliofadhiliwa katika masomo yao ya sekondari au stashahada, yatima na wenye ulemavu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mikopo ya elimu ya juu hutolewa kwa Watanzania wahitaji wenye sifa kutoka eneo lolote la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Kwa upande wa Zanzibar katika mwaka wa masomo 2017/2018 jumla ya Watanzania 1,380 wanaosoma katika vyuo vitano vilivyopo Zanzibar walipata mikopo kutoka Bodi na hii ni sawa na asilimia 41 ya wanafunzi waliodahiliwa katika vyuo hivyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa mikopo haitolewi kwa kuzingatia eneo analotoka mwombaji, sifa kuu ya wanufaika hao 1,380 waliopata mikopo ni Utanzania wao na wanaweza kuwa wanatoka katika eneo lolote la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, lakini wanaosoma katika vyuo vilivyopo Zanzibar. Hivyo basi, siyo rahisi kupata takwimu za Wazanzibar au wanufaika wengine kutoka eneo lolote la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Msisitizo ni kwamba mikopo haitolewi kwa kuzingatia kwamba mwombaji ametoka upande gani wa Jamhuri yetu ya Muungano, kinachotakiwa ni kwamba sifa ni Utanzania, lakini na zile sifa zingine ambazo zimeainishwa kwenye sheria inayoanzisha Bodi ya Mikopo.

Aidha, napenda kusisitiza kuwa, ni muhimu kufahamu kuwa Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu inafanya kazi kwa karibu na Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu Juu Zanzibar ili kuhakikisha kuwa hakuna Mtanzania mwenye sifa anakosa mkopo wa elimu ya juu na anapata mkopo kutoka katika taasisi zote mbili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mambo mengine ambayo Waheshimiwa Wabunge wamezungumzia katika utoaji wa mikopo ni uwiano wa kijinsia kwa wanufaika; ukomo wa ada wa masomo inayotolewa na Bodi ya Mikopo na umuhimu wa kuboresha Bodi ya Mikopo ili iondokane na utegemezi.

Kuhusu uwiano kati ya wanufaika wa mikopo 122,623 kwa mwaka 2017/2018 wanawake ni asilimia 34.5 na wanaume ni asilimia 65.5. Aidha, kuhusu ukomo wa ada, ni muhimu kufahamu kuwa kwa sasa Serikali imeweka ukomo wa ada itakayotolewa kwa mnufaika wa mikopo kuwa ni ile inayotozwa katika vyuo vya umma.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu kuimarisha Bodi ya Mikopo, kwa sasa Serikali inaendelea kusimamia maboresho ya kimfumo ili kuimarisha ufanisi utakaoongeza tija na kuiwezesha Bodi ya Mikopo kuelekea kwenye kujitegemea.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baadhi ya Waheshimiwa Wabunge waliopata fursa ya kuchangia hoja yetu walitaka kujua kwa nini shule nyingi za Zanzibar katika matokeo yake ya kidato cha nne na sita ndiyo hushika mkia na walitaka vilevile kujua kama Bodi ya NECTA inajumisha wajumbe kutoka Zanzibar. Upangaji wa shule katika viwango vya ubora na ufaulu hufanyika kwa vigezo vikubwa viwili ambavyo ni wastani wa ufaulu wa wanafunzi kimadaraja na wastani wa ufaulu wa wanafunzi katika masomo yao. Nafasi ya shule katika ubora wa ufaulu inategemea wastani ambao shule imeupata katika vigezo vilivyoainishwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Baraza la Mitihani la Tanzania hutumia mfumo madhubuti wa usahihishaji unaofahamika maarufu kama (conveyor belt) ambapo msahihishaji mmoja husahihisha swali moja tu alilopangiwa na hivyo kufanya script moja ya mtahiniwa kusahihishwa na watahini wengi, jambo ambalo huondoa uwezekano wa upendeleo kutokea. Nchi nyingi za Afrika zinatumia mfumo huu baada ya kujifunza kutoka Tanzania. Mifano ya hizo nchi ambazo zimejifunza kwetu ni pamoja na Zimbabwe, Zambia, Uganda na Ghana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kulijulisha Bunge lako Tukufu kuwa Bodi ya Baraza la Mitihani la Tanzania inajumuisha wajumbe kutoka Zanzibar ambao hushiriki katika shughuli zote za usimamizi na maamuzi ya Baraza la Mitihani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baadhi ya Waheshimiwa Wabunge waliopata fursa ya kuchangia hoja yetu walitaka kufahamu na kutaka Serikali itoe ufafanuzi juu ya suala la kumsimamisha masomo mwanafunzi Abdul Nondo wakieleza kuwa utaratibu uliotumika ni kinyume na Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na haki za binadamu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sitaingia katika merits za kesi kwa sababu kesi iko Mahakamani, lakini itoshe tu kwa sasa kusema kwamba napenda kulijulisha Bunge lako tukufu kuwa Taasisi za Elimu ya Juu, ikiwa ni pamoja na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam huongozwa na sheria ndogondogo za wanafunzi. Sheria hizi ndogo zimewekwa kwa minajili ya kuwalinda wanafunzi, kwani kuna kanuni za kitaaluma zinazomtaka mwanafunzi kutimiza kiwango maalum cha chini cha mahudhurio cha mahudhurio (75%) ili kuendelea na masomo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mwanafunzi mwenye kesi kama hii ingekuwa vigumu kukikidhi kanuni hiyo na wakati huo huo kutimiza matakwa ya mahakama. Hata hivyo, mwanafunzi anaposhinda kesi hurudishwa chuoni na kuendelea na masomo kama kawaida. Kwa hoja hii ni dhahiri kwamba uamuzi ambao unachukuliwa kutokana na by laws za University of Dar es Salaam unalinda haki ya huyo mwanafunzi zaidi ya kuziminya kwa sababu inamfanya asiweze kufukuzwa chuo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ambalo limeibua hisia na limejadiliwa kwa muda sasa ni lile ambalo limekuwa likizungumzwa sana na Mheshimiwa Goodluck Mlinga na hilo ni suala la kutaka Serikali kutoa ufafanuzi juu ya tabia ya baadhi ya walimu wa vyuo vikuu kuwafelisha wanafunzi kwa kutaka rushwa ya ngono. Serikali imelipokea suala hili, naomba itambulike kuwa Serikali ya Awamu ya Tano haina uvumilivu kwa vitendo vyovyote vya rushwa ikiwemo rushwa ya ngono shuleni au vyuoni. Nitoe wito kwa Mheshimiwa Mbunge na wananchi wote kutoa taarifa kwa mamlaka husika kuhusu vitendo hivi pindi wanapovibaini. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda vilevile nilitaarifu Bunge lako Tukufu kwamba mwanafunzi mpaka ahesabike kwamba amefeli haitokani na mtizamo wa mwalimu mmoja tu. Kuna taratibu ambazo zimewekwa kupitia marks ambazo amepata pamoja na kazi zake kwa ujumla ili kuweza hatimaye kuamua kama amefeli au hajafeli. Kwa hiyo, niwaondolee shaka kwamba hata kama ikitokea kuna mwalimu mmoja anafanya vitendo hivi haiwezi ikawa ndiyo inaathiri ufaulu wa mwanafunzi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vyuo vikuu vina taratibu maalum za kushughulikia masuala ya unyanyasaji wa kijinsia. Kwa mfano, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kina sera iitwayo Anti-Sexual Harassment Policy ambayo inatoa mwongozo wa namna ya kushughulikia masuala haya. Hata hivyo, wanafunzi wengi inavyoonekana hawatumii sana msaada huu. Tunaendelea kuwasihi kama watapata matatizo kama haya waende kwenye Ofisi ya Mshauri wa Wanafunzi (Dean of Students) na watapata msaada unaotakiwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na kwamba suala hili linazungumziwa vyuoni, nataka nitoe rai kwamba suala la maadili ni la kitaifa. Wakati Mheshimiwa Mlinga alivyotoa hoja hii kwenye mitandao ya kijamii watu wengine vilevile wameendelea kuonyesha kwamba unyanyasaji wa kijinsia au mahusiano yasiyosaidia wanafunzi hayafanyiki katika ngazi za vyuoni tu lakini wamesema hata baadhi ya Waheshimiwa Wabunge nao wamejiingiza kwenye mahusiano ambayo hayasaidii wanafunzi.

Kwa hiyo, nitoe rai kwamba kwa sababu suala la maadili ni la kitaifa, hata sisi Waheshimiwa Wabunge tuhakikishe kwamba hatuingii kwenye mahusiano ambayo hayawasaidii wanafunzi wetu na tuwaache wamalize masomo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo machache, nawashukuru sana na naunga mkono hoja, ahsanteni kwa kunisikiliza.