Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia

Hon. Capt. (Mst). George Huruma Mkuchika

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Newala Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi. Nitangulie kusema kuwa naunga mkono hoja hii na Mheshimiwa Waziri mimi Mbunge wa Newala Mjini watu wangu wamenituma nikuambie kwamba wanaridhishwa sana na utendaji kazi wa Wizara yako, wanapongeza sana mlivyopanua Kiuta sekondari sasa kuwa high school, ulivyosaidia kule Mnyambe na ulivyosaidia madarasa. Wananchi wanasema wataendelea kushirikiana na Serikali kutekeleza wajibu wao pale inapobidi nguvu za wananchi zinahitajika. Kwa sababu tunavyofahamu Serikali yetu haikuwahi kuahidi kwamba kila kitu kitatolewa bure, tunafanya ubia kati ya Serikali na wananchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, nataka niseme leo nimesoma press release ya Mbunge, namheshimu sana lakini mambo yaliyosemwa mle mengine wanasema ukikaa kimya, quietness means consent, ndiyo maana nimeamua nisikae kimya, nijibu hoja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hoja inayozungumzwa pale kwamba Mheshimiwa Rais aliahidi kuongeza mshahara mwaka huu.

Naomba mnisikilize, watu wazima wakikaa kwenye faragha wanasikilizana, mimi hamjaniona nawazomea hata siku moja. Mnasema mambo wakati mwingine yanaudhi lakini nakaa kimya, ndiyo nidhamu ya Bunge. Hivi mzee mzima na mvi kama hizi nianze kuzomea ooh, ooh, aah. Basi mna mtu wa kumuiga mfano mbona hamniigi mfano? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jana nilikuwa Iringa, Mgeni Rasmi alikuwa Rais nimemsikiliza live, hayo mnayosema moja, maana unajua Kiswahili kigumu, inawezekana tukasikiliza wote wawili mimi nikaelewa vingine na wewe ukaelewa sivyo lakini kwa sababu ni mtaalam wa lugha ya Kiswahili nataka kusema alivyosema Rais jana. Amesema hivi, mwaka jana sikuahidi kupandisha mishahara. Akasema siku zote Serikali inapandisha mishahara kulingana na uwezo wa kifedha. Lingine akasema kupanga ni kuchagua, tuna shida ya kujenga reli, reli ile ya kwenda Kigoma zinaanguka kila siku tangu 1905 mpaka leo zaidi ya miaka 100, tunajenga reli ya kisasa, tumenunua ndege, hauwezi ukaleta watalii kutoka nje unawapeleka Ngorongoro unataka wapande ndege nazo za nje, domestic flights.

Mheshimiwa Mwenyekiti, akasema nawaomba Watanzania wenzangu tuchape kazi. Waliopo mashambani waongeze uzalishaji kama mimi mkulima wa korosho, mliopo ofisini mchape kazi na mliopo viwandani muongeze uzalishaji. Hali ya uchumi itakaporuhusu, maneno ya jana ya Rais na mimi nilikuwa pale futi moja kutoka kwake, sasa ooh nilisikia, nilisikia, mimi nilikuwa futi moja pale ubavuni kwake, akasema hali ya uchumi itakaporuhusu nitapandisha mshahara tena sitangoja sikukuu ya May Day.

Sasa nikuambieni pale kupanga ni kuchagua, yeye akasema kwa ufahamu wake kupanga ni kuchagua, akasema ilibidi tuamue, je, tuongeze mishahara tubaki tulivyo na barabara mbovu, bila ndege, bila reli (standard gauge).

Kuzomea ndiyo tabia yenu lakini hakuachi mimi kusema. Mimi siwezi kuacha kusema kwamba kuna watu wameamua ku-behave kana kwamba wako sokoni, mimi nitasema tu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, akasema hali ya uchumi itakaporuhusu nitapandisha mshahara, sitangoja May Day, nikiambiwa tu mahesabu kule Hazina yamekubali siku hiyo hiyo napandisha, ndivyo alivyosema. Kupanga ni kuchagua, akasema ilibidi tuamue, je, tutekeleze haya kwanza au tugawane hela kwa kuongeza viwango vya mishahara. Leo mtu anasimama hapa anasema Rais kasema uongo, mwaka jana alituahidi, mwenyewe amekanusha hakusema, msimtie maneno mdomoni ambayo hakuyasema. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tena aliyetoa press aliwahi kufanya kazi utumishi, kuna mahali anasema watumishi sisi tunalipishwa…

(Hapa baadhi ya Wabunge walizungumza bila kufuata utaratibu)

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA: Nasoma hapa ninyi, humu ndani unaruhusiwa kuwa na note book siyo kusoma risala, mimi naandika hapa point form, mimi ni mwalimu najua kuandika lesson notes, najua namna ya kujiandaa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ile press release inasema wafanyakazi wanalipishwa skills development levy, wrong. Skill development levy analipa mwajiri halipi mfanyakazi. Hivyo hayo maneno unategemea uyapate kwa mtu senior citizen, senior retired civil servant hajui kama skills development levy inalipwa na mwajiri na hawezi kwenda kufuta ile maana ameiandika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilitaka niweke sawa hilo, sasa nataka nichangie upande wa ajira ya walimu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama mtakavyokumbuka Oktoba, 2016 tulifanya zoezi la uhakiki wa watumishi. Katika uhakiki ule ilibainika baadhi yao walikuwa na utumishi hewa wakiwemo na walimu. Mara moja baada ya kuona idadi ya walimu imepungua kilichotokea ni kwamba Serikali imeajiri watumishi tayari…

KUHUSU UTARATIBU . . .

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa darasa ulilotoa. Unajua wakati mwingine unaweza ukaongea kwa jazba ukasahau hata ulichokuwa umekisema. Serikali inasimama hapa kujibu hoja za Wabunge. Hili ninalolisema mmelisema. Hivi mlitaka mkisema jambo la uwongo tukae kimya tu? Quietness means consent. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naamini dakika wanazoninyang’anya hizi utanifidia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hoja nyingine ambayo imezungumzwa na pande zote mbili; upande wa upinzani na upande wa CCM ni suala la msingi la ajira kwa walimu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la ajira kwa walimu jana Mheshimiwa Rais alipohutubia kule Iringa aliwaambia wafanyakazi kwamba watumishi 22,150 wataajiriwa mara moja. Katika hao 7,000 sawa na asilimia 31.6 watakuwa ni walimu. Hii tunatekeleza bajeti ya mwaka huu tulio nao sasa na tutakapoanza mwaka mpya, juzi mmepitisha bajeti ya watu wengine 49,000. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nataka niseme kwamba hakuna mtu ndani ya Serikali anayependa pawe na uhaba wa walimu, kila jitihada zitafanyika. Kama nilivyosema kwa upande wa afya siku ile, nilisema kama kuna zahanati yoyote iliyofungwa kwa kukosa watumishi nileteeni, wako walioniletea tumeshafanya utaratibu tunawapeleka watu kwa sababu niliahidi hakuna zahanati itakayofungwa kwa kukosa watumishi. Nasema tena kwa upande wa elimu hapa nilipo mimi ndiyo Waziri wa Utumishi, hakuna shule itakayofungwa kwa kukosa walimu, unayo jimboni kwako nenda kaniletee tutafanya mpango kupeleka walimu mara moja. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine nataka niseme kuna halmashauri nyingine walimu mnawarundika shule moja hasa shule za mjini. Tunaomba Waheshimiwa Wabunge wote hapa tushirikiane pale ambapo walimu wamezidi tuwapeleka sehemu ile ambako kuna shida ya watumishi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, mimi nilisimama hapa kuunga mkono hoja, haya niliyosema sijaogelea nje ya…

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa Mzungumzaji)

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nilikuwa najibu hoja ambazo zimetolewa na Waheshimiwa Wabunge wa pande zote mbili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.