Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia

Hon. Joseph George Kakunda

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Sikonge

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPH G. KAKUNDA): Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana. Kwanza, nampongeza sana Mheshimiwa Profesa Ndalichako na Mheshimiwa Ole Nasha, Waziri na Naibu Waziri kwa kazi yao nzuri sana wanayoendelea kuifanya katika sekta ya elimu na sisi katika Ofisi ya Rais, TAMISEMI tunaendelea kuwategemea sana katika utendaji wetu wa kila.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, naipongeza Kamati wametoa maoni, ushauri mzuri sana. Kwa kweli nakiri kwa mwaka huu wametoa ushauri ambao utatusaidia sana katika utendaji wetu wa kila siku. Ushauri kuhusu namna bora ya kuendesha sekta ya elimu, kuboresha ushirikiano wa wadau mbalimbali ikiwemo namna ya bora ya kutoa huduma za elimu kwa watoto wenye ulemavu, nasema tumeupokea na tunaufanyia kazi na tumeupokea kikazi zaidi. Nawapongeza Waheshimiwa Wabunge wote ambao wametoa maoni na ushauri na ushauri wao tumeupokea. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, msingi wetu wa utekelezaji wa kazi za kila siku katika Halmashauri na mjadala wa kitaifa, Halmashauri zote hutekeleza kazi zao kwa mujibu wa Katiba, Ibara ya 145 na 146 na sheria mbalimbali za Serikali za Mitaa. Uwezeshaji wao unasimamiwa na Sheria Na.19 ya Tawala za Mikoa. Kwa hivyo, usimamizi kwa ujumla katika Serikali za Mitaa ni wa Serikali Kuu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika utekelezaji wote tunaofanya katika sekta ya elimu tunaongozwa na Sera ya Elimu na Mafunzo ya mwaka 2014. Kwa muktadha huo, maoni na ushauri kuhusu kuwa na mjadala mpana wa kitaifa kuhusu mfumo wa elimu, majukumu ya wadau, uwajibikaji, tunajua pale wilayani kuna Idara tatu zote zinasimamia elimu: Kuna Afisa Elimu wa Wilaya, Mdhibiti wa Ubora na kuna Katibu wa TSC. Wote hawa wanahusika na maendeleo ya elimu kwa majukumu mbalimbali katika wilaya. Vilevile kuna masuala ya kuhusu ngazi za vidato, haki za watoto wa kike na watoto wenye ulemavu.

Kwa hiyo, suala la kuwa na mjadala mpana wa kitaifa kuhusu masuala mbalimbali kama hayo, sisi katika Ofisi ya Rais, TAMISEMI hatuna tatizo nao kabisa na tumeupokea. Wiki ijayo tutakutana katika ngazi ya Naibu Mawaziri na mwenzangu wa Wizara ya Elimu, tutazungumzia namna ya kuuandaa huo mjadala pengine labda baada Bunge hili la Bajeti likikamilika basi tunaweza tukauitisha kama ambavyo tumeshauriwa na Waheshimiwa Marais Wastaafu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu madai ya walimu, namshukuru Naibu Waziri wa Fedha amegusia, walimu 15,000 tayari wameshalipwa. Hata hivyo, napenda kuliambia Bunge lako Tukufu kwamba tumekamilisha uhakiki wa madeni ya walimu 126,893 ambapo madai yao sasa yamepungua hadi shilingi 61,515,587,938 na haya tumewasilisha Hazina kwa ajili ya hatua zaidi. Serikali imeshaahidi madai yote yatakayothibitika kuwa halali yatalipwa. Kwa hiyo, tunaomba walimu wote wawe na subira. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu uhamisho wa walimu wa masomo ya sanaa kutoka sekondari kwenda shule za msingi, tumesikia maoni lakini tunapenda kusisitiza kwamba uhamisho huu uliwahusu walimu 21,165 wa masomo ya sanaa ambao walikuwa wamezidi idadi kwenye shule za sekondari kwa maana kwamba walikuwa na vipindi vichache sana. Kwa hiyo, ili kusudi waendelee kuwa katika ajira ya utumishi wa umma kama walimu hadi watakapostaafu tuliona kwamba ni matumizi sahihi ya rasilimali za Serikali kuwahamishia kwenye shule za msingi ili wakaendelee na kazi kwa mshahara ule ule na kwa daraja lile lile. Serikali inaamini kwamba ukiacha wale ambao hawana uzoefu na zana za kufundishia shule za msingi ambao watahitaji mafunzo maalum elekezi ya muda mfupi, wale waliojiendeleza na wakahamia sekondari kutoka shule za msingi hawahitaji sana mafunzo hayo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo, nakiri kwamba zimekuwepo changamoto kadhaa katika utekelezaji wa zoezi hilo ikiwemo baadhi ya waliostahiki kupata kulipwa posho hawakulipwa na hili natoa agizo kwamba pale ambapo Wakurugenzi wamekosea wafanye marekebisho haraka sana. Vilevile kulikuwa na malalamiko ya kuhamishwa wale wenye degree na wakaachwa wale wenye diploma, isipokuwa kama mwalimu mwenye diploma yuko peke yake anafundisha somo hilo ina maana kumhamisha mwalimu yule watoto wale watakosa somo hilo hata kama ni Historia au kiingereza, mwalimu huyo mwenye diploma anayefundisha somo hilo peke yake itabidi abaki wataondoka walimu wengine. Kwa hiyo, suala hili linahitaji umakini sana katika kulifuatilia. Waliokosea tumeshawaagiza warekebishe na naomba walimu wote wenye malalamiko watuandikie kupitia Katibu Mkuu, TAMISEMI ili hatua zichukuliwe haraka na hiyo ni pamoja na wale waliosimamia mitihani hadi sasa posho hawajalipwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu makato ya asilimia mbiliya CWT. CWT iliundwa kwa mujibu wa sheria sawa na vyama vingine vya wafanyakazi. Kwa hiyo, masuala ya kwamba wamekatwa asilimia mbili wanatakiwa wayajadili kwenye vikao vyao vya kisheria ili kusudi wakubaliane kama wataendelea kukatana au namna gani kwa sababu hatuwezi kuwaingilia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu ajira za walimu, sasa hivi tunaandaa mchakato wa kuajiri walimu 16,130; kati ya hao 10,130 ni wa shule za misingi na 6,000 wa sayansi katika sekondari kwa ajili ya kukabiliana na upungufu wa walimu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu madaraja, zoezi ambalo lilikuwa limesimama limeanzishwa tena tangu Novemba, 2017. Kwa sasa upandishaji wa madaraja unaendelea nchi nzima.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu shule ya sekondari ya Lindi, napenda kuwaondoa wasiwasi Wabunge wote kutoka Mkoa wa Lindi. Shule ile itajengwa na itakamilika mwaka 2018/2019 na wiki kesho itakuwa ni agenda mojawapo katika kikao chetu cha Naibu Mawaziri wanaoshughulikia elimu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo ambayo ni ya ujumla makubwa napenda kuunga mkono hoja.