Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia

Hon. Kiza Hussein Mayeye

Sex

Female

Party

CUF

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia

MHE. KIZA H. MAYEYE: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa nianze na kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunipa afya njema. Vilevile nipende kukupongeza Mheshimiwa Waziri wa Elimu, mama yangu, Mheshimiwa Profesa Joyce Ndalichako, kwa jitihada na kazi unayoifanya katika kuhakikisha elimu yetu inapiga hatua mbele. Lakini pamoja na jitihada za Serikali, bado sekta ya elimu ina changamoto kubwa sana, hivyo kwa bajeti ambayo imetengwa hamtaweza kumaliza changamoto zifuatazo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu mishahara ya walimu; walimu ni watu muhimu sana katika maisha yetu kwani wote tumefika hapa tulipo kutokana na walimu, lakini leo hii mwalimu anaonekana kama hana thamani na ni kazi ya waliofeli kuwa waimu wa shule za msingi kwani mishahara wanayopata ni midogo sana kiasi kwamba walimu wanaishi kwa shida na pesa wanayopata ni ndogo sana. Niiombe sana Serikali, mwalimu apewe kipaumbele, aongezewe mshahara ili naye afurahie kazi yake. Walimu wengi hawafurahii kazi ya ualimu, wanafanya kwa shida tu kutokana na wanachokipata kuwa kidogo sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa upande wa miundombinu ya shule zetu; shule nyingi hazina miundombinu mizuri vijijini na hata mijini, madarasa mengi hayapo katika mazingira mazuri, wanafunzi wanateseka sana kwani hata vyoo vya shule zetu nyingi bado ni changamoto kubwa. Sasa tujiulize hawa watoto wanasomaje bila kuwa na vyoo? Kwa hali hii lazima watoto hawa wataendelea kupata magonjwa kama kipindupindu. Lakini hata vyoo ambavyo vipo ni vichafu sana, hakuna hata maji, niiombe sana Serikali iweke maji katika shule zetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, shule zetu nyingi hakuna madarasa ya kutosha, watoto wanasoma chini ya miti, jua na mvua, vyote vyao. Ninaiomba sana Serikali ijenge madarasa ya kutosha. Kwa mfano katika Wilaya ya Kigoma Vijijini, shule nyingi hazina madarasa ya kutosha, kama vile shule za Nkema, Mwandiga, Nyamhoza, Kizenga, Bugamba, Kiziba na Nyamigura madarasa ni machache sana, lakini vyoo hakuna, madawati hakuna. Niiombe sana Serikali iweke miundombinu ya shule zetu kuanzia katika madarasa, madawati, vyoo na vifaa vya kufundishia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu watoto wenye mahitaji maalum; watoto hawa katika suala la elimu bado wamesahaulika sana, kwani bado shuleni hawapo wengi lakini pia miundombinu ya shule zetu bado inambagua mtoto mlemavu. Watoto hawa hawana vifaa vyao maalum na vilevile walimu wa watoto hawa bado ni wa kutafuta, vyoo vilivyopo watoto hawa wanapata shida sana kutumia kutokana na jinsi vilivyojengwa, havimpi support mlemavu huyu ili aweze kuvitumia. Wapo watoto hawawezi kutembea kabisa, wanatambaa na vyoo ni vichafu sana, hakuna maji, tunamuweka mtoto huyu katika hali gani?

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Kata ya Mwandiga, Kigoma Vijijini kuna shule ya Nkema, ina watoto walemavu lakini shule hii haina madarasa, vyoo, watoto hawa wanapata shida kubwa, walimu wa watoto hawa hakuna. Niombe sana Serikali iwajali watoto hawa kuanzia katika vifaa, walimu, miundombinu ya ujenzi, madarasa na vyoo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu chombo cha kusimamia elimu; kama kweli tunataka kupandisha hadhi elimu yetu, ni muhimu Serikali iunde chombo kimoja ambacho kitakuwa na kazi ya kusimamia elimu yetu. Chombo hiki kiwe maalum kwa kuangalia elimu yetu, kiweke mikakati ya kuhakikisha elimu yetu inapiga hatua; chombo hiki kisimamie kuanzia ngazi ya shule za msingi mpaka vyuo vikuu, hii itatusaidia sana kuboresha elimu yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu upandishaji madaraja kwa walimu; hii imekuwa changamoto kubwa sana kwa walimu. Serikali imekuwa ikipandisha walimu madaraja kutoka daraja moja A kwenda B, lakini mwalimu huyu anaishia kupata barua tu, stahiki zake kama ongezeko la mshahara hapati kwa wakati na wapo ambao wamestaafu lakini mafao yake amepigiwa hesabu kwa daraja A wakati alipanda daraja miaka 16 iliyopita; hii siyo haki kabisa. Kiukweli walimu wanateseka sana na jambo hili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niombe sana Serikali mtu apewe stahiki yake mara tu aapopanda daraja, kama ametokea daraja A mwezi Mei, basi mwezi huo huo apokee mshahara wake wa daraja jipya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu michezo ya UMITASHUMTA, michezo ni uhai kwani hujenga afya na vilevile hutengeneza mahusiano mazuri ya ujirani mwema. Lakini sasa hivi michezo hii haina nguvu, imesahaulika sana. Niombe sana Serikali irudishe michezo shuleni, inasaidia sana wanafunzi kiafya, kimwili na kiakili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu walimu wa sayansi, hili limekuwa tatizo sugu, shule zetu hazina walimu wa sayansi, hii inafanya wanafunzi kuchukia masomo ya sayansi, sasa kama tunataka kuwa nchi ya viwanda ni lazima tuweke walimu wengi wa sayansi ili tupate wataalam wengi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, naunga mkono hoja.