Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia

Hon. Omari Mohamed Kigua

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kilindi

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia

MHE. OMARI M. KIGUA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nichukue fursa hii kumpongeza Waziri, Naibu Waziri, Katibu Mkuu na watumishi wote wa Wizara hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika hotuba hii nitajikita katika maeneo yafuatayo; moja, ni ukweli usiopingika kuwa Vyuo vya Ufundi Stadi (VETA) ni muhimu kwa sasa ukizingatia kuwa nchi hii inaelekea kuwa ni nchi yenye mwelekeo kuwa ni nchi ya viwanda vidogo, vya kati na vikubwa, hivyo, tunahitaji wataalam wa ufundi katika kuendesha mashine katika viwanda hivi na suluhisho la wataalam hawa litapatikana kwenye vyuo hivi. Niipongeze Serikali kwa jitihada inazozichukua kujenga vyuo hivi. Nishauri vyuo hivi vijengewe katika Wilaya na Mikoa yote nchi nzima.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ujenzi wa vyuo hivi pia utasaidia katika kupunguza changamoto ya ajira kwani vyuo hivi vitasaidia katika kufanya vijana wote wajiajiri katika maeneo mbalimbali ya ufundi. Niuombe uongozi wa Wizara uharakishe zile asilimia tano za Skill Development Levy zinazokusanywa na Wizara ya Fedha zinafuatiliwa na kupelekwa katika VETA na FDC’s. Umuhimu wa vyuo hivi nimeuona katika Mkoa wa Shinyanga jinsi VETA inavyofanya kazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pili ni ukaguzi wa shule. Eneo hili nalo lina changamoto katika kuimarisha ubora wa elimu, utendaji wa kazi wa walimu na tathmini ya elimu yetu yote. Haya hayawezi kufanyika bila kuimarisha Idara ya Ubora na Ukaguzi wa Elimu. Maeneo mengi katika Wilaya au Majimbo yote Idara hii haipo vizuri kwa kukosa vitendea kazi kama magari mfano ni Jimboni kwangu Kilindi. Jiografia ya Wilaya imekaa vibaya, lakini hakuna gari.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tukiimarisha eneo hili hakika malalamiko ya kudidimia kwa elimu katika shule za msingi na sekondari yatapungua. Vilevile kuna umuhimu kwa Serikali kuboresha maslahi ya watumishi wote wanaosimamia eneo hili la elimu, hayo yamezungumzwa sana. Zamani kitengo hiki kilikuwa imara na matokeo yake yalikuwa yanaonekana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tatu, ni kuhusu Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi. Napongeza mamlaka hii kwa kazi kubwa inayofanya ikiwa ni pamoja na kusimamia ukarabati wa shule zetu za sekondari nchini. Hili ni jambo jema sana kwa sababu shule hizi zilikuwa zimechakaa sana. Maamuzi haya hakika yanafanya hata watoto wetu wanaosoma katika shule hizi ufaulu wao kuongezeka kwa sababu watasoma katika mazingira mazuri, hiki ni kigezo cha kuinua ufaulu pia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo, zipo changamoto ambazo naomba zifanyiwe kazi. Mamlaka lazima iwe na utaratibu mzuri unaoeleweka katika shule zote, mfano kama mtatumia force account basi itumike katika shule zote. Mfano ukarabati wa Shule ya Sekondari ya Wasichana Bwiru wametumia mfumo wa force account na kazi imefanyika vizuri, lakini katika Shule ya Sekondari Nganza Girls zote hizi zipo Mwanza wametumia mkandarasi. Wote hawa walitengewa kiasi cha shilingi milioni 900.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kilichotokea ni kwamba mkandarasi wa Nganza sekondari ametumia jumla ya shilingi 1,300,000,000 ongezeko limekuwa ni kubwa. Hivi TEA walifikiria au walitumia vigezo gani katika utaratibu wa kazi yenye madhumuni yanayofanana? Nashauri Serikali isimamie eneo hili kwa sababu dhamira ya Serikali ni kukarabati shule zote za sekondari Tanzania, tusipokuwa makini ni shule chache zitakarabatiwa. Wizara isimamie vinginevyo majukumu ya ukarabati yatolewe katika Mamlaka hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nne, ombi kwa Shule ya Sekondari ya Kilindi Girls kupatiwa fedha za uzio. Katika Jimbo la Kilindi tunayo shule ya sekondari moja ya wasichana ambayo inapokea wasichana kutoka maeneo mbalimbali ukiacha Kilindi, Handeni, Korogwe na Wilaya jirani wote wanakuja kusoma hapo ila tatizo kubwa hatuna uzio unaozunguka shule na hii ni hatari kwani shule hii inazungukwa na makazi ya watu. Ili kulinda usalama wa watoto wetu na pia katika kuleta ufaulu katika masomo. Niombe Wizara itusaidie kutujengea uzio (fence).

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.