Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia

Hon. Bernadeta Kasabago Mushashu

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia

MHE. BENARDETHA K. MUSHASHU: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi. Kwanza kabisa na mimi nimpongeze Mheshimiwa Waziri, Naibu Waziri na watendaji wote wakuu katika Wizara kwa kazi nzuri wanayofanya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaipongeza Serikali kwa mpango wake wa elimu bila malipo. Serikali imetoa hela nyingi, inatoa zaidi ya shilingi bilioni 23.8 kila mwezi kugharimia elimu lakini katika waraka uliotoka na wazazi walipewa majukumu fulani, wazazi walibakiwa na jukumu la kuhakikisha kwamba wanatoa uniform pamoja na chakula kwa ajili ya watoto wao. Wasiwasi wangu ni maelekezo yaliyotoka Wizarani au tuseme TAMISEMI kwamba hiki chakula ili mwanafunzi aweze kukila shuleni utaratibu utakuwa tofauti na ule uliokuwa unatumika kawaida.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wote tunatambua umuhimu wa chakula au umuhimu wa lishe. Mtoto akiwa na njaa hawezi kujifunza na akaelewa. Tunatambua kwamba Watanzania chakula cha jioni tunakula kati ya saa 11.00 jioni mpaka saa 2.00 usiku, mtoto tangu saa hizo hajapata kitu chochote, anaamka asubuhi hakuna breakfast anaenda shuleni anasoma tangu asubuhi mpaka jioni, hawezi kuelewa kitu chochote.

Naomba basi Wizara ya Elimu ile ya kusema kwamba chakula kikichangwa, michango ikichangwa, wazazi wenyewe waji-organise awepo mtu atakayeratibu kukusanya hivyo vyakula ndiyo viweze kupikwa mashuleni watoto wale, nafikiri si sahihi. Hili ni jukumu la msingi la walimu, kwa hiyo, jukumu la chakula kinaliwa na nani na saa ngapi waachiwe walimu lakini wazazi watimize jukumu lao la msingi la kuhakikisha kwamba watoto wao wanapata chakula mashuleni.

Mheshimiwa Mwenyekiti, upungufu wa walimu mashuleni ni mkubwa sana kitaifa, lakini vilevile ukiangalia kwenye Mkoa wa Kagera ninakotoka kuna upungufu wa walimu zaidi ya 6,773 katika shule za msingi na katika shule za sekondari kuna upungufu mkubwa sana wa walimu wa sayansi na hisabati. Najua kila nchi ina mipango yake na ina namna ya kuandaa wataalam. Napendekeza kwa hili Serikali ingefanya mpango, tuna Chuo Kikuu cha Dodoma hapa, kina majengo yako pale, wangeweka mkakati sasa wa kwamba hicho chuo sasa hivi kitumike kuwaandaa walimu wa sayansi, hisabati pamoja na walimu wa shule za msingi ambao wanakosekana kusudi katika miaka miwili, miaka minne tuwe tumemaliza hili tatizo. Chuo cha Dodoma kipo na kinaweza kikafanya mpango huo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tafiti zinaonesha kwamba kwenye shule za msingi namba ya watoto wa kiume na wa kike inalingana; ukienda sekondari namba ya watoto wa kike na wa kiume zinakaribiana na ukienda kwenye vyuo vikuu namba ya watoto wa kike inaendelea kupungua lakini kwenye masomo ya sayansi imepungua sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi niko kwenye Kamati ya Huduma na Maendeleo ya Jamii, wamegundua kwenye vyuo viwili kuna 17% tu ya wasichana wanaosoma masomo ya sayansi kwenye vyuo vikuu. Hii ni hatari, haiwezekani Tanzania tukasema kwamba tunaendelea wakati nusu ya Watanzania wanaachwa nyuma ambao ni wanawake. Pia tukumbuke kwamba hawa wasichana ambao mnawaona kwamba ni wachache sana katika masomo ya sayansi kwenye vyuo vikuu ni walewale watoto wa kike ambaye akitoka shuleni, akirudi nyumbani kwanza amsaidie mama kutengeneza chakula na kufanya usafi. Yule yule mtoto wa kike ikitokea mzazi au mlezi ni mgonjwa lazima abaki nyumbani kumsaidia. Hawa watoto wa kike akiwa shuleni anashawishiwa na watoto anaolingananao, anashawishiwa hata na mababa watu wazima, yote inamletea msongo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, akiwa kwenye jamii au darasani kuna mtazamo kwamba masomo ya sayansi na hisabati ni kwa ajili ya wanaume, wasichana hawafai huko. Kwa hiyo, siku za nyuma tulikuwa na mpango kila walipokuwa wanamaliza form six wale watoto wote wa kike ambao walikuwa wanakaribiana na ufaulu ambao unatosha kumuingiza chuo kikuu walikuwa wanapelekwa chuo kikuu wiki sita kabla ya kufungua vyuo vikuu, wanapewa some kind of an induction course na baada ya hiyo course walikuwa wanapewa mtihani, wanashinda na wengi walifanya hivyo na wakashinda kuliko hata wale waliopata division one. Niiombe Serikali huu mpango urudishwe ili watoto wa kike wanaomaliza form six ambao ushindi wao ni mzuri kidogo yaani wameteremka kidogo kuliko ule unaohitajika wapelekwe chuko kikuu kusudi waweze kufanyiwa hiyo induction course. Hii itaweza kungeza wanafunzi katika vyuo vikuu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mkoa wa Kagera mnajua kwamba lilitokea tetemeko na shule nyingi ziliharibiwa, miundombinu iliharibiwa na watu walifariki. Niipongeze Serikali kwa kazi nzuri mliyoifanya pale Iyungo secondary school, mmeijenga imekuwa ya kileo ni maghorofa matupu. Hongereni sana na Nyakato inaendelea kutengenezwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini nataka kuwaambia kwamba bado kuna shule kama Bukoba secondary school na Rugambwa secondary school zote ni za Serikali, ni shule kongwe na ziliathiriwa na tetemeko. Nauliza Serikali ina mpango gani wa kuzikarabati shule hizi kwa sababu walimu na wanafunzi kwenye shule hizo wanaishi katika hali hatarishi kwa sababu kwanza yale majengo ni ya zamani, halafu yalitetemeka lakini sijaona mpango uliopo kwa ajili ya kuzitengeneza au kuzirekebisha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ili tuweze kufikia uchumi wa kati ambao utatawaliwa na viwanda na ili hii ndoto itimie lazima watoto wajifunze sayansi. Tuna upungufu mkubwa sana wa maabara. Mkoa wa Kagera tu tuna upungufu wa maabara 352 ambayo ni 62% ya mahitaji na hizi maabara zote zimejengwa kwa nguvu za wananchi. Napendekeza Serikali ingetenga hela maalum kwa ajili ya kuhakikisha kwamba wanajenga maabara kila shule za chemistry, physics, biology, geography na ikiwezekana computer lab ili tuweze kufikia kwenye huo uchumi wa viwanda ambao tunauzungumzia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho ni vyuo vya VETA. Napongeza mpango wa Serikali wa kuendelea kujenga hivyo vyuo vya VETA. Uchumi wa viwanda utahitaji hawa mafundi wa katikati. Ni bahati mbaya sana mimi wakati nasoma na nafundisha tulikuwa hata na shule za ufundi lakini na zenyewe zimekufa. Napendekeza kwamba tuendelee na mpango huohuo ili katika kila…

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa Mzungumzaji)