Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia

Hon. Dr. Pudenciana Wilfred Kikwembe

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Kavuu

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia

MHE. DKT. PUDENCIANA W. KIKWEMBE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi na mimi niweze kuchangia katika sekta hii ya elimu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna mtu amesema nakuja kupongeza ni kweli napongeza na ninaanza kupongeza kwa kusema kwamba naishukuru Serikali yangu kwa namna ya pekee ambavyo imeweza kuanzisha mpango wa elimu bure ambayo imeweza kusaidia watoto wengi kuingia shuleni.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo nasema naipongeza Serikali kwa sababu hata wazazi wamejitokeza na wameweza kuchangia na kuongeza madarasa, naongelea katika Jimbo langu la Kavuu ambalo Mheshimiwa Ndalichako nilikwishakuja nikakuambia tayari nina maboma 69 katika kuongezea katika idadi ya wanafunzi walioingia, kwa hiyo naomba unisaidie tu shilingi milioni 48 kwa ajili ya kuezeka maboma hayo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, napenda kuishukuru Serikali yangu, tayari katika Jimbo langu la Kavuu nimeweza kutatua tatizo la madawati, nilikuwa na upungufu wa madawati 1,000 na nimeyatatua na sasa hivi nayagawa shuleni.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niende moja kwa moja katika Vyuo vya Maendelo ya Wananchi. Vyuo vya Maendeleo vya Wananchi vinatuchanganya na kozi ambazo zimekuwa zikitolewa na VETA, niombe sana hili liangaliwe na wakati mwingine tunashindwa kuelewa ama viko chini ya Wizara ya Afya kwenye Maendeleo ya Wananchi ama viko Wizara ya Elimu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano, chuo kilichopo Mkoa wa Katavi cha Maendeleo ya Wananchi, Chuo cha Msanginya bado hakijaanza kufanya lolote na miundombinu yake siyo. Naomba ukiangalie kwa hali ya kipekee ili tuweze kupeleka watoto wetu pale hasa wa kike ambao hawafiki form four waweze kujifunza maarifa mbalimbali ambayo yanaweza kuwasaidia kutatua matatizo yao katika maisha yao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine naomba niongelee kuhusu malipo na madai mbalimbali ya walimu. Kimekuwa ni kilio cha muda mrefu. Mimi ni mwalimu, nimeanza kufundisha Chuo cha Ualimu Sumbawanga kama first appointment yangu pale, ninafahamu matatizo ya walimu. Nimefundisha Mpanda Girls ambapo niliomba ni shule iliyokuwa na form one mpaka form four na ilijengwa kwa msaada wa DANIDA. Kwa hiyo ninaomba kwa sababu sasa hivi mmeiweka kama form five na form six naomba ianze form one boarding mpaka form six ili na sisi Mkoa wa Katavi watoto wetu wapate nafasi ya kuweza kusoma katika ile shule ambayo ni moja ya shule kongwe ambazo zilijengwa kwa ajili ya kuwasaidia watoto wa kike pale Mpanda Girls. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niongelee suaa la TEHAMA, suala hili naomba uliangalie vizuri. Katika shule zangu za msingi, nimefanya ziara katika shule zangu za msingi Jimbo zima, TEHAMA shuleni wanasoma kwa nadharia. Kwa hiyo ninaomba computer, Serikali ifanye utaratibu wa kupeleka madarasa ya computer pamoja na computer kwa ajili ya walimu wa shule za msingi na wanafunzi wa shule ya msingi angalau kila shule moja iwe na darasa moja na upendeleo uanze na Jimbo la Kavuu ili tuweze kufanya maendeleo kwa sababu ni Jimbo ambalo liko vijijini. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niongelee hili suala la kuhamisha walimu kuwatoa sekondari kuwapeleka shule za msingi. Kwa kweli halijapokelewa vizuri, kwa mwalimu linaonekana kama ni adhabu, basi naomba wapelekwe special course kwa ajili ya kufundisha shule za msingi kwa sababu wao walifundishwa methodology shuleni kwa ajili ya kufundisha shule za sekondari.

Kwa hiyo, tunaomba sasa kama mnawapeleka kule, muwapeleke na special course kwa ajili ya kujielekeza katika masomo ya shule za msingi bila kuathiri madaraja yao pamoja na vyeo vyao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda niongelee suala la asilimia mbili ambayo walimu wamekuwa wakikatwa kwenye mshahara. Tunaelewa kuna kipindi Bunge lililopita tuliongea hapa tukasema kuwe na mikataba, wanaopenda wasaini wakatwe na wasiopenda wasikatwe. Tunajua ni jambo la kisheria lakini sheria inaweza ikaletwa hapa na pia ikafanyiwa kazi ili tuone walimu tunawasaidiaje. Tunawakata asilimia mbili katika mshahara wao kila mwezi na Chama cha Walimu, Chama cha Walimu kina ghorofa pale ni mtaji lakini walimu bado wanashindwa kukopeshwa kwa ajili ya maendeleo ya maisha yao. Wanashindwa kukopa katika mshahara ambao wanakatwa waweze kujenga maisha yao yawe vizuri hasa kwenye nyumba zao wanazotakiwa kuishi. Kwa hiyo, niombe sana hili mlifikirie na mliangaie. Walimu wengi wamekuwa wakilalamika kuhusu hii asilimia mbili ambayo na mimi nilikwishakatwa na ninaidai kwa sababu siko huko tena, kwa hiyo napenda irudishwe. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niongelee usawa wa elimu. Tunajua elimu ni haki ya kila mwanafunzi. Naongelea shule za private na shule za Serikali. Kwa kuwa matokeo ya ufaulu yanaonesha bado ni tatizo na shule nyingi za Serikali ziko vijijini, mwanafunzi wa kijijini anatembea umbali mrefu. Kuna sababu nyingi zinazoweza kusababisha mwanafunzi wa Serikali asifanye vizuri hasa aliyeko kijijini. Ninaomba muangalie namna mtakavyokuwa mnaandaa mitihani sasa kwa ajili ya watoto hawa wanaoenda na magari, wanaokula shuleni na wale wanaotembea kwa miguu ili usaili wao uwe tofauti, usiwe unaofanana kwa sababu wako katika mazingira tofauti ili tuweze kuona tatizo liko wapi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niongelee shule yangu Maalum ya Majimoto. Nina shule pale ya Majimoto Mheshimiwa Profesa Ndalichako. Ninaomba kama utaweza kutuma wasaidizi wako wakafika katika ile shule, Halmashauri yangu imejitahidi imejenga miundombinu mizuri, tuna mabweni lakini bado tuna mambo machache ambayo tunahitaji Serikali Kuu itusaidie na tunaomba shule hiyo sasa irudi Serikali Kuu itoke Halmashauri ili iweze kuwasaidia watoto wote wenye mahitaji maalum. Ni shule nzuri tumejitahidi kuitengeneza pale, naomba Profesa kwa jicho la pekee utume watalaam yako ije iangalie ile shule tuweze kuona tunaweza kuifanyaje ili iweze kuwasaidia watoto wenye mahitaji maalum hasa wale wenye ulemavu na wengineo ni shule ambayo tayari tuna mabweni matatu tumekwishajenga, tuna madarasa manne na tuna vyoo ambavyo tumetengeneza miundombinu kwa ajili ya watu wenye ulemavu wa aina mbalimbali. Kwa hiyo, nakuomba sana shule yangu hii kama kawaida yangu nitakuletea special request na mahitaji yake ili muweze kuona mnatusaidiaje.

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda niishukuru Serikali yangu na naipongeza kwa namna pekee ambavyo imekuwa ikifanya kazi chini ya Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli. Napenda niwashukuru Wizara ya Elimu, Mawaziri wote wa Serikali hii kwa sababu wamekuwa ni wasikivu. Ndugu yangu Joyce Ndalichako ni msikivu sana, ni mwalimu wangu wa statistics wakati nikiwa chuo kwa sababu mimi nilisoma elimu ya MEMKWA mpaka nimepata Udaktari na hivi naenda kupata Uprofesa. So lazima nijipongeze. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo nakuomba sana Mheshimiwa suala la elimu tuliwekee mkazo ili na sisi kule watoto wetu kule vijijini wawe maprofesa, wawe wahandisi, tunajua tunaenda kwenye mfumo wa viwanda lazima turekebishe mfumo wetu wa elimu. Lazima tuone kwenye sayansi na teknolojia kuanzia kwenye vyuo vya ufundi, kwenye VETA ambao wakati mwingine tunaweza tukawa tunawadharau lakini hawa ndio watu wazuri ambao wanaweza wakatufanyia miradi yetu mizuri sana katika uchumi unaokuja na viwanda ambavyo tunatarajia kufunguliwa na Serikali yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakuomba sana Mheshimiwa Joyce Ndalichako, suala la elimu sawa naomba muangalie na mitaala pamoja na mitihani mtakayoweza kuwa mnaitunga kwa differences ya mazingira kati ya wanafunzi hasa wa vijijini na wale wanaokwenda na mabasi ya Martin Luther, Ignatius na kadhalika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba kabisa kwa namna ya pekee uweze kuliweka hili suala ili uweze kuona ni namna gani ambavyo tunaweza kuwasaidia watoto wetu.

Kwa hiyo, naomba kabisa suala hili Serikali mlitilie mkazo. Ni mawazo yangu binafsi ambayo baada ya kutembelea hali halisi na kuiona shuleni ni mawazo yangu binafsi ninayowasilisha Bungeni kama Mbunge kuishauri Serikali.