Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019

Hon. Dr. Faustine Engelbert Ndugulile

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kigamboni

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019

NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza naanza kumshukuru Mwenyezi Mungu mwingi kwa rehema yako kunijalia afya njema na kuniwezesha kusimama mbele ya Bunge lako tukufu ili niweze kuta hoja za Waheshimiwa Wabunge.

Katika kipindi hiki cha utendaji wa kazi nikiwa kama Naibu Waziri nimepata ushirikiano mkubwa kutoka kwa viongozi na wafanyakazi wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto. Shukurani za pekee kabisa nazielekeza kwa Mheshimiwa Dkt. Ummy Mwalimu namuita daktari, Waziri wa Afya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa ujuzi wake na ubobezi katika sekta ya afya na kwa ushirikianoa ambao amenipa katika kutkeleza majukumu yao. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, aidha napenda kuwashukuru Makatibu Wakuu Dkt. Mpoki Ulisubisya pamoja na Sihaba Nkinga kwa mchango wao kwa kuwezesha utekelezaji wa majukumu yangu. Vilevile nawashukuru Profesa Mohamed Bakari - Mganga Mkuu wa Serikali, na pia nachukua fursa hii kuwashukuru watendaji wa wizara taasisi za Wizara pamoja na Waganga Wakuu wa Mikoa na Wilaya, Waganga Wafawidhi wa Hospitali, Vituo vya Afya na Zahanati; Vyuo vya Mafunzo vilivyo chini ya Wizara yetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile natoa shukurani zangu kwa ushirikiano ambao wameendelea kutupa katika sekta ya afya maendeleo ya jamii na ustawi wa jamii na wananchi wote kwa ushirikiano.

Mwisho natoa shukurani zangu za dhati kwa watoa huduma wote katika sekta ya afya kwa kazi kubwa na nzuri ambayo wameendelea kuitoa na uzalendo wao. Sifa tunazipata sisi Mawaziri lakini kazi kubwa zinafanyika huko chini. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa naomba nijielekeze katika kujibu hoja za Waheshimiwa Wabunge na la kwanza nitajiekeza katika hoja ambazo Wabunge wengi wamechangia kuhusiana na masuala ya miundombinu katika sekta ya afya. Serikali imekuwa inafanya kazi kubwa sana kuboresha zahanati, vituo vya afya na hospitali kwa mujibu wa Mpango wetu wa Maendeleo ya Afya ya Msingi ambapo zinaelezea kwamba kila kijiji kitakuwa na zahanati na kila kata itakuwa na kituo cha afya. Tumeboresha kwa kiasi kikubwa sana vituo vya afya na Waheshimiwa Wabunge wengi humu ndani mtakuwa mashuhuda kwamba vituo vingi vya sasa hivi vimeboresha, zaidi 208 .

Mheshimiwa Naibu Spika, katika bajeti ya TAMISEMI ambayo tumeipitisha hivi karibuni tumesema kwamba tutajenga Hospitali za Wilaya 67; katika mapendekezo ambayo tunaleta katika Bunge lako tukufu hili baada ya Serikali kutukabidhi Hospitali za Rufaa za Mikoa tutaanza ujenzi wa hospitali sita za rufaa za mikoa pamoja na kuboresha hopsitali nyingine za rufaa katika maeneo ya afya ya mama, mtoto na huduma za dharura. Kwa hiyo, tumeendelea pamoja na hilo kuboresha huduma mbalimbali katika Hospitali zetu za Kikanda, Hospitali zetu Maalum na Hospitali za Rufaa za Muhimbili.

Mheshimiwa Naibu Spika, sambasamba na kuboresha masuala ya miundombinu tumejielekeza katika kuboresha ubora wa huduma za afya. Moja ya jambo ambalo tumeweza kulifanya kama Serikali ni kuanzisha mfumo wa star rating ambao unaweka viwango vya ubora katika utoaji wa huduma na kwa kiasi kikubwa tumeweza kufanikiwa sana. Tuliweza kufanya tathimini ya awali ambapo zaidi ya asilimia 33 ya vituo vya kutoa huduma ya afya vilikuwa na viwango vya nyota sifuri; lakini baada ya kuja kufanya tathimini na maboresho makubwa viwango vile vimepungua sna kwenda chini ya asilimia 10 ni mafanikio makubwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa hivi tunaka tujielekeze zaidi kwenda mbali zaidi, tutatoa viwango vya ubora katika utoaji huduma. Sambasamba na hilo tunataka tuanzishe utaratibu wa kutoa leseni kwa vituo vyetu vya utoaji huduma vya afya ambavyo sasa badala mtu kuwa kutoa huduma tu pasipokuwa na kuzingatia viwango vya ubora tutaanza kutoa leseni na leseni hii inahuishwa na viwango vya ubora ambavyo anavyo.

Mheshimiwa Naibu Spika, hoja nyingine ambayo iliibuka kutoka kwa Waheshimiwa Wabunge ni kwamba ni nani mwenye mamlaka ya kupandisha hadhi vituo vya afya na zahanati. Niseme tu, kwa mujibu wa instrument tuliyo nayo Wizara ya Afya ndio mamlaka pekee ambayo ina mamlaka kisheria ya kupandisha hadhi zahanati na vituo vya afya; na hii inaendana sambamba kabisa na majukumu ambayo Wizara ya Afya inayo. Wizara ya Afya itasimamia sera, masuala yote ya viwango na miongozo.

Mheshimiwa Naibu Spika, sambamba na hilo Wizara ya Afya itasimamia Wizara zote za Rufaa za Mikoa, Hospitali za Kanda, Hospitali Maalum na Hospitali za Taifa. Wenzetu Ofisi ya Rais, TAMISEMI majukumu yao ni kusimamia utekelezaji wa sera, viwango na miongozo inayotolewa na Wizara ya Afya, lakini sambamba na hilo watasimamia Zahanati, Vituo vya Afya na Hospitali za Wilaya; huo ndio mgawanyo wa majukumu ambao tunao.

Mheshimiwa Naibu Spika, nijielekeze kidogo katika suala la dawa, na hoja zimekuwepo nyingi na Waheshimiwa Wabunge wamechangia sana. Niseme tu kwamba katika awamu hii ya tano bajeti ya dawa imeongezeka kutoka bilioni 31 mwaka 2015/2016 kufika bilioni 269 katika mwaka huu wa fedha na mwakani tutakuwa na bilioni 270. Tumekwenda mbali zaidi kuimarisha mifumo yetu, takribani kama wiki tatu/nne tulikuwa tunazindua magari mapya 181, na mfumo ambao tunautumia ni kuhakikisha kwamba dawa tunazipeleka mpaka katika kituo cha kutoa huduma za afya.

Mheshimiwa Naibu Spika, sambasamba na hilo tumeweka mwongozo wa utoaji wa huduma na hili nilitaka nilisisitize. Tumeweka mwongozo wa kutoa huduma za afya za dawa, tunasema dawa gani itatolewa wapi kwa ngazi gani kwa ugonjwa gani. Kwa sababu tulikuwa tunapata changamoto katika hospitali kubwa kwamba kampuni za dawa zilikuwa zinaenda kwa watoa huduma, wanawaambia andika dawa hii na utakapokuwa umeandika dawa hii ikawa inanunuliwa kwa wingi na sisi tutakuwa tunakupa commission. Na hii wakati ikasababisha zile dawa zisiwe zinapatikana pale kwa sababu tu wale wafanyabiashara walikuwa ndio wanatoa mwongozo wa jinsi gani ya dawa kutumika.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo tumeweka mwongozo wa kutoa dawa ambao sasa utatoa mwongozo dawa gani inatumika wapi na katika aina gani ya ugonjwa. Lakini sambamba na hilo, tumekwenda mbali kuweka label katika dawa zetu. Kwa hiyo, ninaamini mifumo hii ambayo tunaendelea kuiboresha itahakikisha kwamba dawa tunazipata kwa kiasi cha kutosha. Hata hivyo nitoe rai, na kwa Waheshimiwa Wabunge kwa sababu wengi wameniuliza mbona dawa fulani haipatikani. Kuna dawa zipo katika ngazi tofauti tofauti, hatutegemei tukakuta dawa kwa mfano insulin katika zahanati, hatuwezi tukazikuta zile. Zile dawa ziko katika ngazi tofauti kwa sababu dawa zile zinategemea na aina ya utaalam ya wale ambao wanatakiwa kuzitoa.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini tunatambua kwamba magonjwa yasiyoambukizwa yanazidi kuongezeka na sisi tutakuwa tunapitia miongozo yetu mara kwa mara kuangalia wapi tunahitaji kuboresha.

Mheshimiwa Naibu Spika, kulikuja na hoja nyingine ya masuala ya CT Scan na MRI katika hospitali za Rufaa za Mikoa. Kwa sasa hivi kwa mujibu wa miongozo yetu, huduma hizi haziwezi zikapatikana katika Hospitali za Rufaa za Mikoa. Ngazi ambazo CT Scan na MRI zinaweza zikaanzia, kwa mujibu wa miongozo yetu ni katika ngazi ya Rufaa za Kanda. Hata hivyo kadri nchi yetu inavyozidi kuongezeka na huduma zinazidi kuboreshwa tutafanya mapitio kuangalia kama tunaweza sasa tukaruhusu teknolojia hizi zikaweza kutumika katika ngazi hii kwa sababu changamoto hii si suala tu la kuwa na vifaa hivi ni suala vilevile kuwa na wataalam ambao wanaweza kusimamia vifaa hivyo.

Mheshimiwa Naibu Spika, suala lingine lilikuwa ni suala la rasilimali watu. Tunakiri kwamba tumekuwa na changamoto kubwa ya rasilimali watu na nimshukuru sana Mheshimiwa Mkuchika, ameainisha vizuri sana kwamba katika mgao utakaokuja na sisi tutapata mgao katika watumishi wa afya. Naamini katika hili litatusaidia sana kupunguza changamoto ya watumishi ambayo tunayo.

Mheshimiwa Naibu Spika, suala lingine ambalo lilikuwa limeongelewa na hili nataka niwapongeze watoa huduma kwa kweli kwa kiasi kikubwa sana, kelele za wananchi kuhusu utoaji wa huduma zimepungua sana. Lugha za matusi na masuala ya rushwa kwa watumishi wa afya tumepunguza sana; na hii niwashukuru sana na kuyapongeza mabaraza ya kitaaluma na maadili ambayo yako chini ya Wizara ya Afya. Tumezidi kuyaboresha na tumeendelea kuhakikisha kwamba tunafanya mabadiliko ya kisheria kuhakikisha kwamba taaluma hizi tunazisimamia vizuri. Moja ya mikakati ambayo tumeiweka ni kuhakikisha kwamba sasa kada zetu zote tunatoa leseni.

Mheshimiwa Naibu Spika, msije mkashangaa, tumepitisha Sheria ya Madaktari ambayo itahitaji hata mimi Naibu Waziri ambaye nimesimama hapa ni daktari, baada ya muda mtakuwa na mimi mnaniona dispensary pale natoa huduma au Hospitali ya Benjamin Mkapa ili kuhakikisha kwamba tunapata mafunzo endelevu kuhakikisha kwamba na mimi ili niendelee kuitwa daktari na ku-practice kama daktari ninakuwa na leseni yangu na ninapata mafunzo endelevu na yote hii ni mikakati ya Serikali kuhakikisha kwamba watoa huduma wote wanakuwa… muda umekwisha?

NAIBU SPIKA: Endelea.

NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Naibu Spika, sasa nijielekeze sasa katika ngazi ya maendeleo ya jamii. Kuna hoja kama mbili/tatu ambazo nazo ziligusiwa sana na Waheshimiwa Wabunge na moja lilikuwa suala la NGO’s, kwamba kuna NGO’s nyingi hapa nchini. Nyingi ni NGO za Kimataifa lakini zimejisajili kama NGO za hapa nchini. Sambamba na hilo kuna fedha nyingi ambazo zinakuja kwenye NGOs na hazijulikani zinakwenda wapi. Tatu, ilikuwa ni kwamba kuna baadhi ya NGO’s zimekiuka majukumu yao ya kikatiba na kuanza kujiingiza katika mambo mengine ikiwa ni pamoja na siasa.

MheshimiwaNaibu Spika, kupitia idara yetu ya NGO tumefanya tathmini ya NGOs zote, kuangalia usajili wao, kuangalia mifumo yao ya fedha, kuangalia wanafanya shughuli gani, kuangalia kama je wanawasilisha taarifa muhimu zote ambazo zinatakiwa kwa mujibu wa sheria na tumekuta NGOs nyingi ambazo zimekuwa zinakiuka masharti haya na baadhi tumeshazifuta na nyingine zimepewa maonyo.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa hivi tumewekeza nguvu kubwa sana kuhakikisha kwamba sasa tunazisimamia vizuri hizi NGOs ili ziweze kutimiza majukumu yake. Hatuna shida na NGO’s; ni wadau wakubwa sana wa Serikali na sisi kama Serikali tuna-appreciate sana kazi kubwa na nzuri ambayo wanaendelea kuifanya. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, suala lingine la mwisho ambalo nilitaka nigusie lilikuwa ni suala la wazee. Sisi kama Serikali kupitia Sera ya Afya ya mwaka 2007 tunatambua umuhimu wa wazee na katika sera yetu imesema kwamba wazee watapewa matibabu bure. Mheshimiwa Waziri amekuwa kinara katika hili kuhakikisha kwamba tunatenga madirisha ya wazee na wazee wetu wanapata vitambulisho vya kuweza kuwatambua na kuweza kupata matibabu.

Mheshimiwa Naibu Spika, tunakiri kwamba tumekuwa na changamoto kidogo katika utekelezaji wa hili, lakini na sisi tutaongeza juhudi zaidi kuhakikisha kwamba tunasimamia kwa karibu.

Mheshimiwa Naibu Spika, imekuja hoja ambayo ilikuwa raised hapa kuhusiana na Sheria ya Wazee. Tuna Sera ya Wazee ya mwaka 2003, sasa hivi tunaifanyia mapitio na baada ya hapo tutaileta kwa ajili ya kuleta hiyo rasimu ya sheria ili iendane na mazingira ya sasa ya hali ya wazee tuliokuwa nao hapa nchini.

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo machache, mimi nikushukuru sana na niwashukuru watoa hoja wote kwa michango mizuri ambayo wameweza kuitoa katika bajeti yetu. Sisi tunaamini kwamba michango hii itatusaidia sana kuboresha utendaji wetu wa kazi. Nawashukuru sana.