Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019

Hon. Deogratias Francis Ngalawa

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Ludewa

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019

MHE. DEOGRATIAS F. NGALAWA: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kuipongeza Serikali kwa zoezi zima la uwezeshaji vituo vya afya kuweza kutoa huduma za upasuaji, jengo la mama na mtoto na maabara. Hii itapunguza kwa kiasi kikubwa wazee, akina mama na watoto kutembea umbali mrefu kupata huduma.

Mheshimiwa Naibu Spika, sisi Ludewa tunashukuru kwa kupewa shilingi milioni 500 kwa Kituo cha Afya Mlangali na shilingi milioni 400 kwa Kituo cha Afya Manda na madawa shilingi milioni 300. Kwa sasa Wilaya ya Ludewa kupitia nguvu za wananchi na wadau mbalimbali tunajenga vituo vya afya 17 ambavyo tunaweza kujenga mpaka ngazi ya uezekaji.

Mheshimiwa Naibu Spika, hivyo tunaiomba Serikali kuunga mkono jitihada za wananchi katika kutekeleza Ilani ya Uchaguzi ya CCM (2015-2020) katika ngazi ya umaliziaji majengo hayo pamoja na zahanati 22 zinazojengwa katika vijiji mbalimbali.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia tatizo la dawa limekuwa ni sugu katika baadhi ya zahanati bila kusahau watumishi katika zahanati na vituo vya afya. Ikumbukwe jiografia ya Halmashauri ya Ludewa kimiundombinu si mizuri kwani tuna vijiji 15 havifikiki kwa mawasiliano ya barabara yaani huko vilipo vijiji hivyo havijawahi ona gari toka kuumbwa kwa ulimwengu.

Mheshimiwa Naibu Spika, Halmashauri ya Wilaya ya Ludewa inaomba kupatiwa magari (ambulance) walau mawili ili kutoa huduma ya usafiri pindi itokeapo dharura ya mgonjwa anapozidiwa na anapopewa rufaa kwani miundombinu ni mbali toka sehemu moja kwenda nyingine ukizingatia hakuna huduma ya mawasiliano kwa sasa.

Mheshimiwa Naibu Spika, nawasilisha.