Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019

Hon. Pascal Yohana Haonga

Sex

Male

Party

CHADEMA

Constituent

Mbozi

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019

MHE. PASCAL Y. HAONGA: Mheshimiwa Naibu Spika, Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Mheshimiwa Ummy Mwalimu, alipokuja Halmashauri ya Mbozi alielezwa changamoto nyingi za Wizara hii. Mojawapo ya changamoto hizo ni ukosefu wa magari ya wagonjwa katika vituo vya afya na hospitali; Kituo cha Afya cha Itaka kinahudumia Kata nne za Itaka, Nambinzo, Bara na Halungu.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Waziri alipofanya ziara Mkoa wa Songwe aliahidi kuwapatia gari la wagonjwa wananchi wa Mbozi ili lisaidie Kituo cha Afya cha Itaka kutokana na kituo hiki kuhudumia wagonjwa wengi. Litakuwa jambo jema endapo Waziri wa Afya atatimiza ahadi yake.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia Serikali ya Awamu ya Nne ilijenga Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete iliyopo Hospitali ya Muhimbili, sio jambo baya, ni jema, ila tatizo ni kwamba taasisi hii muhimu haina baadhi ya vitendea kazi. Serikali inunue vitendea kazi (vifaatiba) ili kuendelea kupunguza tatizo la wagonjwa, hasa wenye magonjwa makubwa kama ya moyo kwenda kutibiwa nje ya nchi. Fedha zote zinazoidhinishwa wakati wa bajeti kwa ajili ya taasisi hii muhimu ni vema zitolewe zote na kwa wakati.

Mheshimiwa Naibu Spika, Hospitali ya Wilaya ya Mbozi ina changamoto nyingi zinazohitaji utatuzi, mfano, kuna OPD ndogo, hakuna wodi ya wazazi, hakuna maji hivyo ni vema Serikali ikatatua kero hizi ili wananchi wanufaike.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu upungufu wa watumishi wa afya; Wilaya ya Mbozi ina upungufu wa watumishi wa Idara ya Afya; zaidi ya watumishi 600 wanahitajika. Upungufu huu unazikabili hospitali zote mbili, Hospitali ya Wilaya ya Mbozi na Hospitali ya Mbozi Mission. Hospitali ya Mbozi Mission inaendeshwa kwa PPP hivyo watumishi wanaotakiwa kuajiriwa na Serikali ni wachache sana. Naishauri Serikali kuajiri watumishi katika hospitali hii, pia Vituo vya Afya vya Isanga, Itaka, Iyula na zahanati havina watumishi wa kutosha.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuwasilisha.