Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019

Hon. Joram Ismael Hongoli

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Lupembe

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019

MHE. JORAM I. HONGOLI: Mheshimiwa Naibu Spika, nishukuru kwa kunipa nafasi ya kuchangia katika Wizara hii. Nianze kuwapongeza sana Mheshimiwa Waziri na Mheshimiwa Naibu Wazri kazi kubwa ambazo wanazifanya kwa ajili ya kuboresha afya za Watanzania nawapongeza sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa muda hautoshi nichangie kidogo juu ya afya na usafi wa mazingira. Naipongeza Serikali kwa kuanzisha hii kampeni ya usafi wa mazingira na kuhakikisha kwamba Watanzania wanatumia vyoo bora. Ni dhahiri kwamba kama inavyooneshwa kwenye taarifa matumizi ya vyoo bora imeongezeka toka 1,996,413 mwezi Juni, 2017 na mpaka hadi sasa hivi kuna vyoo milioni 2,414, 094 ilipofika Desemba. Nipongeze sana ni dhahiri kwamba tunapoboresha vyoo ni kwamba tunapunguza magonjwa ambayo yanasababishwa na uchafu. Kwa hiyo, ninapongeza kwa kufanya hivyo maana yake tunapunguza gharama za kutibu haya magonjwa ambayo yanatokana na kukosa vyoo.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika Halmshauri ya Wilaya ya Njombe imekuwa ikiongoza katika usafi huu wa vyoo na mazingira bora toka mwaka 2013, ilikuwa ya kwanza mwaka 2014 kijiji cha Wagenyi kilikuwa cha kwanza na Halmashauri ilikuwa ya kwanza, mwaka 2015 kijiji cha Image kilikuwa kijiji cha pili na Halmashauri ilikuwa ya pili, mwaka 2016 kijiji cha Wanginyi kilikuwa cha kwanza, Matiganjola kikawa cha pili Sovi cha tatu na Halmashauri yangu ilikuwa ya kwanza ninaishukuru Serikali ilitupatia zawadi ya gari Land Cruiser.

Mheshimiwa Naibu Spika, mwaka 2017 kijiji changu ambako mimi natoka ninakoishi kijiji cha Kanikere kiliongoza nchi hii na kuwa cha kwanza, lakini kijiji cha pili kilikuwa kijiji cha Nambara cha kutoka Mara, kijiji cha tatu kilikuwa kijiji cha Lyalalo kutoka Jimbo la Lupembe, Halmashauri ya Wilaya ya Njombe na kijiji cha nne kilikuwa cha Image.

Mheshimiwa Naibu Spika, ninataka nijue vizuri Waziri utakaposimama utueleze vizuri maana yake nilikuwa napiga hesabu hapa, hesabu ndogo tu ilitumika hapa ukipiga hesabu utakuta kwamba Halmashauri ambaye ilitakiwa iwe ya kwanza ni Halmashauri ya Wilaya ya Njombe, maana kuna vijiji vitatu vipo namba moja, namba tatu na namba nne lakini cha kushangaza tukaambiwa kwamba sisi ni namba mbili Halmashauri ambayo ina kijiji kimekuwa namba moja. Sasa nataka nipate ufafanuzi ni kwa nini Halmashauri tena haikuwa ya kwanza wakati kuna vijiji namba moja, kijiji namba tatu, kijiji namba nne kinatoka Halmashauri ya Wilaya ya Njombe, lakini kijiji cha Nambara ambacho kipo Meru kilikuwa cha pili na Halmashauri ikawa ya pili.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa katika simple arithmetics naona kama kidogo inagoma, basi utanisaidia mwishoni kutoa ufafanuzi ilikuwaje na hesabu zilipigwaje Halmashauri yangu ikawa ya pili badala ya kuwa wa kwanza. (Makofi)

Pia ninaipongeza Serikali kwa kuja na mpango huu wa hasa huduma ya CHF kuhakikisha kwamba tunatoka kwenye CHF ambapo mwananchi alikuwa anakatia kwenye kituo cha afya au zahanati hapo na anatakiwa kutiwa kwenye eneo lake husika tu na kuna maeneo mengine tunaenda mbali tukawa tunatibiwa kwenye Kata kwenye Halmashauri moja ndani ya Halmashauri anaweza akatibiwa sehemu yoyote ile, lakini sasa hivi Serikali imeenda mbali zaidi kuhakikisha kwamba kwa mpango huu unoitwa ICHF sasa wananchi wataweza kutumia hiyo CHF iliyoboresha kutibiwa ndani ya Mkoa kwa maana wataweza kutibiwa mpaka kwenye Hospitali ya Rufaa.

Mheshimiwa Naibu Spika, hii ni hatua kubwa sana naipongeza sana Serikali, naamini kwamba kupitia mpango huu wananchi wetu hasa ambao wanaishi maeneo ya viijini ambao kwao tiba imekuwa ni changamoto kubwa, hasa wanapotoka nje ya Halmashauri sasa watapata matibabu kirahisi zaidi.

Mheshimiwa Naibu Spika, ninaishukuru Serikali na niunge mkono hoja. Ahsante sana.