Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019

Hon. Tunza Issa Malapo

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019

MHE. TUNZA I. MALAPO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, miongoni mwa pesa nyingi za dawa zinapotea kwa ajili ya kununulia dawa za malaria. Wakati tuko kwenye Kamati tumefika Kibaha kwenye kiwanda kinachozalisha dawa za viuadudu, viluilui wa mbu, lakini kusema ukweli tumekuta hakuna jitihada za makusudi za kutangaza dawa ile ili watu waweze kuitumia na kuua yale mazalia ya mbu, ili watu wasing’atwe na mbu na kupata ugonjwa wa malaria.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo namshauri Mheshimiwa Waziri watilie maanani utumiaji wa dawa hii kwa ajili ya kuua hivi vimelea, ili pesa ya kununua dawa za malaria ipungue na tufanye mambo mengine katika sekta ya afya kwa sababu, ina mambo mengi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu Hospitali ya Kanda ya Kusini, wenzangu wengi wameongea na mimi naomba niongee. Sisi tumechoka, tumechoka kwa sababu kila siku tunaongea. Safari hii imetengwa bilioni moja, bilioni moja ni pesa ndogo lakini tunaomba hiyo hiyo ndogo iende. Maana hapa tunaongea ndogo, lakini hatimaye hata hii ndogo haiendi. Mmetutengea bilioni moja kwa mwaka huu wa fedha unaokuja, tunaomba hii pesa iende, ili ikaweze kujenga hospitali ile na sisi tupate huduma za afya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu Hospitali ya Rufaa ya Mkoa ya Ligula. Ukifika pale ni masikitiko makubwa, mvua hizi za masika zinaponyesha jengo la OPD linavuja. Vile vile theatre yetu ya Hospitali ya Mkoa wa Ligula inahitaji matengenezo makubwa. Kama mwenzangu alivyosema X- Ray mbovu, jengo lenyewe linahitaji ukarabati mkubwa. Kwa mwezi OC inakwenda shilingi milioni ishirini na tano, ni ndogo, hospitali ile inatoa huduma ya watu wengi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama hivi tunavyosema hatuna hospitali ya kanda, tunategemea hiyo hospitali ihudumie watu wengi, lakini mazingira yake ni magumu, mazingira yake ni duni. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri Mkuu alikwenda pale Machi, 2016 palikuwa na matatizo. Madaktari 13 wakahamishwa, tangu Machi, 2016 mpaka leo ninapoongea hata daktari mmoja hajaletwa. Tunatarajia hawa waliopo wafanye kazi kwa kiwango kipi? Hawa wahudumu wenyewe wa pale wana madeni, mpaka sasa hivi wanadai si chini ya milioni mia tano na kuendelea. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo sisi watu wa Kusini, sisi watu wa Mkoa wa Mtwara pia tunahitaji huduma bora za afya. Tunaomba waone kwamba kule kuna watu ambao wanahitaji huduma bora. Tuna korosho tunachangia pato kubwa la Taifa hili; kwa hiyo nasi pia tunahitaji tupate huduma, si kwamba kila siku tukiingia humu tunaongea yanawekwa kwenye vitabu wanafunika, tukirudi kwenye bajeti nyingine mambo ni yaleyale, kitu kama hicho hatukipendi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye ile hospitali, tunaisemea hii hospitali kwa sababu kama unakuja Mkoa wa Mtwara huwezi kuacha kuongelea Hospitali ya Ligula. Ni hospitali tunayotaraji iwe na mazingira mazuri kwa ajili ya kuwahudumia watu. Tukienda kwenye wodi ya wazazi majanga, wodi ni ndogo, watu wanarundikana, hospitali mmesema ya rufaa ya mkoa, lakini inatoa huduma utasema labda ni hospitali ya wilaya. Watumishi wana madai mengi, watumishi wako asilimia 39 tu, maana unapohitaji watumishi 10 wewe unao wanne tu, tunategemea watafanya kazi katika mazingira gani? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaposema Wizara inahusika na watoto pia tunajua ina wajibu wa kulinda haki zao. Leo watoto wanadhalilishwa kwenye vyombo vya habari, wanadhalilishwa kwenye mitandao ya kijamii; mtoto ametelekezwa na mzazi wake, pata picha kama ni mwanao wewe kesho anaambiwa na wenzie shuleni; wewe baba yako alikutelekeza; hivi kweli huyo mtoto ataweza kujifunza? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tusifanye vitu just for kwa ajili ya show up, tuonekane.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mtoto yule tunampa athari ya kisaikolojia. Mimi ni Mwalimu najua mtoto hawezi kujifunza vizuri.

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)