Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa mwaka wa Fedha 2018/2019 - Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa na Ofisi ya Rais, Utumishi na Utawala Bora

Hon. Esther Lukago Midimu

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa mwaka wa Fedha 2018/2019 - Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa na Ofisi ya Rais, Utumishi na Utawala Bora

MHE. ESTHER L. MIDIMU: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi ili niweze kuchangia. Kwanza kabisa namshukuru Rais kwa kazi nzuri anazozifanya kwa kazi nzuri anazozifanya Mwenyezi Mungu ambariki sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, namshukuru Makamu wa Rais, Waziri Mkuu, Mwenyezi Mungu awabariki sana kwa kazi nzuri wanazozifanya. Pia nampongeza sana Waziri wa TAMISEMI na Naibu Mawaziri wake pamoja na Katibu Mkuu kwa kazi nzuri wanazozifanya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naipongeza sana Wizara ya Afya kwa kuendelea kuboresha miundombinu ya afya. Katika Mkoa wetu wa Simiyu tuna tatizo la upungufu wa wafanyakazi. Katika vituo vya afya na hospitali hatuna watumishi kabisa. Tunaiomba Serikali yangu sikivu itusaidie ili tuweze kupata watumishi katika hospitali zetu za Mkoa wa Simiyu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naishukuru Serikali kwa kutenga pesa ili tuweze kujenga Wilaya mpya ya Itilima na Busega, wametenga bilioni tatu. Naiomba Serikali yangu sikivu hizo pesa zije kwa wakati, tujenge hospitali kwa wakati ili iweze kusaidia Wanabusega na Wanaitilima kwa ujumla. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wananchi wa Wilaya ya Busega wanahangaika sana na wa Itilima, wanafuata matibabu Wilaya ya Bariadi na Wilaya ya Bariadi inategemewa na Wilaya tatu, hivyo, kuna msongamano wa wagonjwa sana. Sasa naiomba Serikali yangu sikivu iweze kukamilisha hizo hospitali haraka. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hospitali ya Wilaya ya Meatu haina Daktari bingwa kabisa wa magonjwa ya akinamama. Akinamama wa Wilaya Meatu wanahangaika sana, wanafuata matibabu Wilaya ya Bariadi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wewe ni mtu wa Simiyu, mtu atoke Kata ya Mwabuzo kufuata matibabu Bariadi na hiyo hiyo Wilaya ya Bariadi ina Daktari bingwa mmoja anategemewa na Wilaya nne; Wilaya ya Bariadi, Wilaya ya Meatu, Wilaya ya Busega na Wilaya ya Itilima. Tunaomba katika hospitali ya Meatu mtuletee Daktari Bingwa wa magonjwa ya akinamama. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, elimu, naishukuru Serikali kwa mpango wake wa elimu bure. Katika Wilaya Maswa tuna sekondari 36, maabara zilizokamilika ni saba, maabara 29 bado, zimejengwa na zimeezekwa kwa kupitia Halmashauri na nguvu za wananchi. Naiomba Serikali sasa itusaidie ili maabara ziweze kukamilika na shule bila maabara bado haijakamilika kwa sababu wanafunzi wanatakiwa kusoma masomo ya sayansi yaani chemistry na physics. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tatizo lingine ni upungufu wa Walimu katika shule za msingi na shule za sekondari. Naiomba Serikali yangu itusaidie Walimu katika shule zetu za Simiyu za sekondari na za shule ya msingi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna mradi wa maji wa Ziwa Victoria, kwanza niishukuru sana Serikali mwaka jana kwa kutenga pesa za mradi wa maji wa Ziwa Victoria unaokuja Simiyu. Mradi huu mpaka sasa haujaanza na hakuna dalili zozote zinazoonekana kwamba mradi unaweza ukaanza. Mheshimiwa Waziri wa Maji nilimuuliza swali kuhusu mradi huu, Waziri akanijibu vizuri sana kwamba mradi huo unaweza ukaanza mara moja. Huo mradi utaanza na Wilaya ya Busega, Bariadi pamoja na Itilima kwa awamu ya kwanza ambao ujenzi wake utachukua miaka miwili. Akasema awamu ya pili atamalizia na Maswa na Meatu, lakini mpaka sasa hakuna kinachoendelea kule. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wewe ni mtu wa Simiyu unajua akinamama wanavyohangaika kutafuta maji, hivyo, mradi huu utawasaidia sana akinamama ambao wanahangaika kutafuta maji kuliko kufanya kazi za maendeleo. Pia utasaidia kwenye taasisi za Serikali kama shule, zahanati na vituo vya afya. Vilevile tutalima na kilimo cha umwagiliaji, sisi ni wachapakazi njaa kwetu itakuwa ni ndoto. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna mradi mwingine wa Maswa wa chujio, yaani huu mradi umekuwa ni kizungumkuti. Mradi huu una miaka mingi wananchi wa Maswa wanakunywa maji siyo safi na salama. Nilishawahi kuuliza swali humu, Mheshimiwa Waziri akanipa moyo akasema baada ya miezi mitatu huo mradi utakamilika, huu mradi unasua sua. Mkandarasi huyu kila akiongezewa muda hamalizi, miaka nenda rudi anaongezewa muda huu mradi hauishi, wananchi wetu wanaendelea kuhangaika. Serikali ina kigugumizi gani kuvunja huo mkataba na mwekezaji huyu, ikafunga mkataba na mwekezaji mwingine? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naendelea kuishukuru Serikali yangu sana ya Chama cha Mapinduzi ikiongozwa na Mheshimiwa Rais Dkt. John Pombe Magufuli, mchapakazi, Mwenyezi Mungu ambariki, naendelea kuishukuru sana kwa Wilaya ya Itilima inaendelea kutuletea fedha za kujenga miundombinu. Sasa hivi tumejenga jengo la utawala, zahanati zinaendelea na vituo vya afya vinaendelea, Mwenyezi Mungu ambariki sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsate sana na naunga mkono hoja.

Whoops, looks like something went wrong.