Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Ofisi ya Waziri Mkuu

Hon. Magdalena Hamis Sakaya

Sex

Female

Party

CUF

Constituent

Kaliua

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Ofisi ya Waziri Mkuu

MHE. MAGDALENA H. SAKAYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, pongezi kwa Waziri Mkuu, Mawaziri na Naibu Mawaziri walioko Ofisi ya Waziri Mkuu kwa kuandaa hotuba hii na kuiwasilisha Bungeni.

Mheshimiwa Mwenyekiti, elimu; ongezeko kubwa la wanafunzi mashuleni haliendi sambamba na kuongezeka kwa miundombinu ya madarasa, ofisi za Walimu, matundu ya vyoo na kadhaili. Serikali iweke mkakati maalum wa ujenzi wa madarasa ili watoto wote wakae madarasani katika shule za primary na secondary.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kauli ya Serikali kwamba elimu ni bure na hivyo hakuna michango inayoruhusiwa mashuleni inapokelewa kwa uelewa tofauti na wazazi na hata vyakula mashuleni Serikali inatoa. Serikali itoe ufafanuzi kuhusu kauli yake kwa kuwa kwa sasa wanafunzi wengi hawapati vyakula mashuleni kwa sababu wazazi au walezi hawataki kuchangia vyakula kwa watoto wao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mtoto mwenye njaa hafundishiki, hali hii inatishia uelewa wa wanafunzi na hivyo kushusha elimu. Walimu wengi kutopandishwa madaraja kwa wakati katika mashule ya primary na secondary katika Wilaya ya Kaliua.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Tanzania ni nchi ya pili Afrika kwa kuwa na mifugo mingi, lakini pato/mchango wa sekta ya mifugo katika pato la Taifa bado ni mdogo sana. Sheria ya nchi inaelekeza maeneo ya malisho ya mifugo kutengwa, kulindwa na kutangazwa kwenye magazeti ya Serikali. Viwanda vya kuchakata mazao ya mifugo (processing plants) ili kutoa masoko ya uhakika kwa wafugaji. Maafisa ugani (mifugo) wenye weledi na vitendea kazi ili watembelee wafugaji mashambani na watoe elimu. Kuwepo na mashamba darasa ya mifugo katika wilaya zote na kata zinazofuga ili wafugaji wafuge kisasa kwa ubora na si kwa wingi usiokuwa na tija.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunamwomba Mheshimiwa Waziri Mkuu awaagize Wizara ya Maliasili na Utalii kurejesha vyeti vya vijiji 26 katika Wilaya ya Kaliua ambavyo vilisajiliwa Kisheria ndani ya hifadhi za misitu na baadaye Afisa wa Maliasili walifika kwenye vijiji hivyo na kupora vyeti vya usajili wa vijiji hivyo vyote. Suala hili linaathiri sana wananchi wa vijiji hivyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mwaka huu 2018 kampuni za ununuzi wa tumbaku kama vile JTI, TLTC na Alliance one wametoa maelekezo kwa vyama vya msingi kwenye vijiji hivyo 26 kwamba hawatawapa makisio ya ununuzi wa tumbaku yao (mikataba) kwa vijiji ambavyo hawana vyeti vya usajili kwa sababu hawawezi kutekeleza mpango shirikishi wa utunzaji wa misitu (CBFM). Hili litaumiza uchumi wa Wilaya ya Kaliua na wakulima wa tumbaku wa Kaliua.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wakurugenzi wa Wilaya walipewa waraka na Serikali kwa kuwatoa kazini Watendaji wa Vijiji na Kata walioajiriwa tangu mwaka 2004 wenye elimu ya darasa la saba. Ni vyema Serikali ikaliangalia agizo hili kwa jicho tofauti ili kuondoa matatizo yanayoendelea kutokea ikiwa ni pamoja na Serikali kupelekwa Mahakamani na kupoteza fedha nyingi na muda mwingi kwa kushughulika na kesi wakati tuna mambo ya msingi ya kuyashughulikia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Wilaya ya Kaliua wanaondolewa walioajiriwa tangu miaka ya 2001. Watendaji hawa wana barua za ajira walibaki kuthibitishwa, walipelekwa mafunzo kwenye Chuo cha Hombolo na maeneo mengine, pamoja na kupewa semina mbalimbali. Watendaji hawa hawatendewi haki, wengine ni wazee lakini pia wana familia zimeathirika sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wilaya ya Kaliua na Jimbo la Kaliua tumepanga kuongeza vituo vya afya viwili katika Kata ya Usinge na Kata ya Ukumbi Siganga katika bajeti ya mwaka 2018/2019. Wananchi wanaendelea kuchangia ujenzi huo na pia Mheshimiwa Rais alipofika Kaliua alichangia shilingi milioni kumi ku-support Kituo cha Afya cha Usinge. Tunaiomba Serikali itenge fedha ku-support nguvu za wananchi katika ujenzi wa vituo vya afya viwili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tatizo la maji katika Wilaya ya Kaliua halijapatiwa ufumbuzi na hakuna mikakati ya muda mfupi kwa Serikali kuwapatia Wanakaliua maji safi na salama. Mradi wa maji mkubwa wa kutoa maji katika Mto Malagarasi ni wa muda mrefu, leo ni mwaka wa nne tangu uanze lakini bado uko kwenye hatua ya upembuzi na usanifu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaomba mwaka huu 2018/2019 Serikali ilete mpango mkakati wa muda mfupi wa kuwatua wanawake wa Kaliua ndoo kichwani, watoto wa kike wapate muda wa kuhudhuria masomo shuleni na si kusaka maji kwenye madimbwi.