Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Ofisi ya Waziri Mkuu

Hon. Naghenjwa Livingstone Kaboyoka

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

3

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Ofisi ya Waziri Mkuu

MHE. NAGHENJWA L. KABOYOKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi hii kuchangia hotuba ya Waziri Mkuu. Nasikitika sauti yangu kidogo siyo nzuri nilikuwa na flu lakini nisameheni.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitajikita katika mambo mawili, matatu hivi. La kwanza nitaangalia hii kaulimbiu ya awamu ya tano kuhusu viwanda, lakini pia nitaangalia jinsi ambavyo Serikali inajipanga kuwekeza katika kuboresha miundombinu ambayo itasaidia viwanda hivi viweze kufanya kazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika taarifa ya Waziri Mkuu amesema kwamba hadi kufikia Februari, 2018 viwanda vipya 3,306 vilikuwa vimeanzishwa. Nasema wazo la kuanzisha viwanda ni zuri maana nia ni kuboresha nchi yetu kufikia katika uchumi wa kati. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tatizo langu kubwa ni jinsi ya utekelezaji wa hii miundombinu. Rais alivyotamka hilo kama ndiyo kipaumbele chake nilitegemea kuwe na mkakati madhubuti ambapo sekta mbalimbali zinakaa, Wizara zinakaa kuangalia kwenye kila Mkoa kuna opportunity gani za kuanzisha kiwanda gani. Katika hizo kuangaliwe miundombinu imeboreshwa? Je, kuna barabara za kwenda sehemu iliyotengwa kuwekwa hicho kiwanda? Je, kuna maji? Je, kuna umeme? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kitu nachokiona hapa ni kwamba imefika hatua Tanzania sasa hivi tunafanya kazi kama maroboti. Inatamkwa watu wanakimbia, tunapata sifa kwamba tumeanzisha vitu hivi, je, tunaangalia sustainability yake au tunajua kuanzisha tu? Je, tumejifunza vile viwanda vyote vilivyokufa viliuawa na nini? Je, kutokana na hapo tunajiwekaje vizuri ili hivi tunavyoanzisha visije navyo vikafa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nasema hivyo kwa vile nina mfano mdogo tu, Kamati yangu ya PAC ilivyokuwa inatembelea viwanda mbalimbali nilipata shock kidogo nilivyofika kwenye Kiwanda cha Kibaha cha Kutengeneza Matrekta. Matrekta yale yamejazana pale ndani hayana soko na ukiuliza hakuna mtu anayejua hawa wanaotengeneza matrekta haya kutoka nchi za nje chini ya Wizara wamejitangazaje, yanajulikana au kuna mahali ambapo yamefanyiwa hata testing ili kuangalia ubora wake? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunasema Mkoa wa Pwani una viwanda vingi, nafikiri hata hiki cha trekta kimewekwa lakini yamejazana ndani mle, hayafanyi kazi, hayajafanyiwa testing kuonesha kama yanahimili ardhi za kwetu. Kibaya zaidi ni kwamba hata watu kufundishwa bado hawajafundishwa ku-assemble tunategemea hao wenzetu kutoka nje, Wazungu ndiyo tunapanga mkakati wa kupeleka wanafunzi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, uone nchi yetu tunavyofanyakazi upside down kwamba Mkuu wa Nchi ametamka watu wote wanakimbia hatukai tukafaya analysis, kwanza tuka-evaluate huko nyuma tulikotoka tulikosea wapi na mkoa gani uko endowed kuweza kufanya kitu ambacho kweli kitakuwa productive kwenye nchi yetu kikawekewa miundombinu yote ili uchumi wetu ukaanza kukua kupitia pale. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, angalia matrekta ya Suma JKT huko yalikopelekwa. Kwanza hayajulikani yamepelekwa wapi which means hata Wizara ya Kilimo hawajatathmini matrekta haya ya Suma yaliyokopeshwa watu mbalimbali yamewezaje kuboresha kilimo badala yake tunaona kilimo ambavyo kimeanguka, mwaka hadi mwaka kilimo kinaanguka. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna dawa hizi za kuua viluwiluwi vya mbu na dawa hii inatengenezwa Kibaha, tumefika pale maboksi kwa maboksi yamejazana. Wakalalamika kwamba Halmashauri nyingi walishapelekewa au walishakopeshwa lakini ni kama moja au mbili ambazo zimelipa nyingine zote hazijalipa. Waheshimia Wabunge tuliokuwa nao wakasema kwenye Majimbo yao au Wilaya zao hawajui kama hata hiyo dawa ipo wala hawajui Halmashauri hizo walishachukua hizo dawa. Maana yake ni kwamba zimewekwa hapo Halmashauri, hazitumiki kuua viluwiluwi vile. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, dawa zile wanasema vile viluwiluwi vikishaota mabawa dawa ile haiwauwi, kwa hiyo inawauwa kwenye septic tanks yale maji machafu sasa imagine huko vijijijni wangapi wana hayo matenki ya maji machafu, wengine vyoo vyao viko pembeni pembeni huko. Kuna wenzangu ambao vyoo vyao bado ni kwenye migomba, sasa sijui hiyo dawa au hicho kiwanda kitakuwa sustained kiasi gani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa ninachosema with due respect napenda sana tuijenge nchi yetu maana hii nchi ya watu wote, lakini kama tunafanya vitu kwa pupa, talk of numbers siyo quality, hatutafika popote. Tutakuwa na viwanda 10,000 au milioni but at the end of the day tunaweza kuona kwamba return ya zile investments ni zero. Sasa viwanda kama hivyo tunavi-sustain namna gani? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, labda nitoe mfano kidogo tu kule kwenye Jimbo langu la Same Mashariki kuna Kiwanda cha Tangawizi. Kiwanda hiki sitatoa historia yake lakini nipende tu kusema LAPF wameungana na wakulima, wamechukua asilimia 60 ya ownership na wakulima asilimia 40, well and good. LAPF wamefikia hatua sasa hivi wanataka ku-install mashine kubwa, wameshapitia michakato yote ili kiwanda kianze kazi, sheshe linakuja barabara kwanza ya kutoka Mkomazi kwenda Same imekuwa historia miaka nenda rudi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara hii inatumiwa na wananchi wa Majimbo kama manne au matano ya Korogwe Vijijini, Mlalo, sehemu ya Lushoto, Same Mashariki na Same Magharibi. Barabara hii tumepiga kelele miaka nenda rudi. Kilichonishangaza mwaka 2015/2016, Wizara ya Miundombinu ilisema imetenga pesa ambayo ilikuwa shilingi milioni 145 kwanza kufanya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina wa Mkomazi – Kisiwani - Same, hizo zilikuwa pesa za bajeti ya maendeleo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mfuko wa Barabara ulitenga shilingi milioni 450 kwa ajili pia hiyo hiyo ya usanifu wa kina wa barabara hiyo, total ni shilingi 595 milioni kwa ajili ya usanifu huo, lakini mpaka leo hakuna hata kilometa moja ambayo imetengezwa. Sasa unajiuliza hivi hiki Kiwanda cha Tangawizi ambacho Mfuko huu wa Jamii wa LAPF wanataka waanze na ilikuwa waanze soon mwezi huu watapita wapi? Ukiangalia hata wakulima wenyewe miundombinu ya maji hawajatengenezewa, hiyo production ya kiwanda kikubwa watapata malighafi kutoka wapi? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa mzungumzaji)

MHE. NAGHENJWA L. KABOYOKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana.