Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Ofisi ya Waziri Mkuu

Hon. Kiswaga Boniventura Destery

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Magu

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Ofisi ya Waziri Mkuu

MHE. KISWAGA B. DESTERY: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru sana kwa kunipa nafasi hii niweze kuchangia nami hotuba ya Waziri Mkuu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wanatheolojia wanatufundisha kwamba ili Mungu akusikilize lazima uanze kumsifu kwanza. Kwa hiyo, ili Serikali iweze kunisikiliza ni vizuri nikasema mazuri ambayo inayafanya.

Kwanza napenda kumshukuru na kumpongeza Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kazi kubwa anazozifanya likiwemo hili la ununuzi wa ndege. Unajua historia wanaweza watu wasiifahamu sana. Nchi yetu ilikuwa na ndege ambazo tuligawana kutoka East Africa na ndege mpya ikanunuliwa sasa ya Rais na Benjamin William Mkapa. Kwa hiyo, tangu hapo huyu ni Rais wa kwanza kununua ndege mpya za nchi ya Tanzania. Kwa hiyo ni jambo ambalo limeingia katika historia na atakumbukwa milele. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni vizuri tukafahamu hilo, lakini tujue pia kwamba yale mambo yote yanayofanyika ya kitaifa ni kwa ajili ya kuhakikisha kwamba Watanzania wanafikishwa mahali ambapo wanahitaji, tunampongeza sana Mheshimiwa Rais. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nampongeza Mheshimiwa Waziri Mkuu kwanza kwa uhamasishaji wake wa mazao matano ya kibiashara ikiwemo pamba. Ili uchumi ukue ni vizuri mazao ambayo yanaleta uchumi yahamasishwe na kusimamiwa na Serikali. Serikali ya Awamu ya Tano imefanya hivyo chini ya Waziri wa Kilimo pamoja na Waziri Mkuu. Tumepata madawa ya kutosha ya pamba na pamba tunaamini kwamba inaweza kuwa nyingi. Kinachotakiwa sasa ni kuhakikisha kwamba wanunuzi wanapata fedha za kutosha ili mkulima asiweze kukopwa, ni kazi kubwa sana ambayo Waziri Mkuu ameifanya ya kuhamasisha pamoja na kufanya mambo mengine ambayo anayasimamia katika Serikali yake. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, haya yote yanaweza kuwepo maneno, lakini nataka nikwambie kwamba katika zawadi ambazo Mwenyezi Mungu ametujalia Tanzania ni pamoja na kuwa na Kiongozi, Rais wa Jamhuri ya Muungano Ndugu John Pombe Magufuli, Waziri Mkuu Majaliwa pamoja na Makamu wa Rais hizi ni zawadi ambazo Mwenyezi Mungu ametupa Watanzania, ni vizuri tukawaombea kwa sababu wanafanya kazi ile ambayo wananchi wanaihitaji, ile ambayo hata Mwenyezi Mungu anaihitaji, kwa hiyo lazima tuwapongeze.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tangu mwanzo Wafalme wakiendelea walikuwa wanalalamikiwa hivi hivi, Mfalme Daudi alilalamikiwa sana, lakini katika utenzi wake wa nyimbo zake Zaburi ya 34:19 alisema maneno mafupi tu kwamba; “Mateso ya mwenye haki ni mengi lakini Bwana humponya nayo.”

Kwa hiyo, tunaamini mateso, mahangaiko ambayo viongozi wetu mnahangaika nayo mnateseka nayo, Bwana Mungu atawaponya nayo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sasa nianze kuchangia yale ambayo wananchi wanayahitaji. Ofisi ya Waziri Mkuu ina mradi wa MIVARP ambao unaongeza thamani kwa mazao ya wakulima kwa kujenga barabara pamoja na masoko.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mradi huu ni muhimu sana umefanya mambo makubwa sana, yako maeneo ambayo wananchi walikuwa hawawezi kusafirisha mazao yao sasa wanasafirisha. Lakini mradi huu sasa ni vizuri ukaendelea. Kwa mfano, kule Magu tunalo eneo bovu sana sasa ambalo tunategemea wakulima wabebe pamba yao kwa tela za ng’ombe kutoka kilometa tano mpaka kilometa kumi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni vizuri MIVARP kwa wakati huu sasa maeneo yale ambayo tunataka kusafirisha mazao ikapeleka nguvu za ziada ili ziweze kutengeneza barabara hizo na kuongeza thamani ya zao la mkulima, kwa sababu bila barabara hizo hatutasafirisha pamba yetu kuleta kwenye soko na barabara hiyo ni Ng’haya - Mwabulenga ni barabara muhimu sana kiuchumi na ndiko wananchi pia wanalima mpunga wao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tukiziachia TARURA hizi barabara nina imani kulingana na uwezo mdogo wa kibajeti havitatosha. Pia niombe kwenye TARURA hapa; mfumo ambao tumeuweka kwenye TARURA nadhani si rafiki sana kwa sababu TARURA haina bodi sasa, haingii hata kwenye Baraza la Madiwani, kwenye Kamati ya Fedha, je, barabara hizo zinahojiwa na nani? Mpaka twende Road Board ndipo tukakutane na matatizo hayo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni vizuri ukatengenezwa mfumo wa kiwilaya, ikawepo Bodi ya TARURA ya Wilaya ili Waheshimiwa Wabunge na Waheshimiwa Madiwani na viongozi wote wa Serikali waweze kwanza kudhibiti upungufu wa barabara zilizopo kwenye Halmashauri ndipo sasa twende kwenye Road Board. Kwa hiyo, naomba sana hilo liweze kuangaliwa kwa makini zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kila Mheshimiwa Mbunge anahitaji maji hapa, kila tunaposimama tunahitaji maji; mimi nadhani ni wakati muafaka sasa wa kuangalia kama Taifa. Kama ambavyo hotuba ya Waziri Mkuu imesema kwamba tunao uwezo wa kukopesheka, hivi hatuwezi kukopa tukaweka miundombinu ya maji ili wananchi waweze kupata maji salama kwa ukaribu? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuishauri Serikali hii ambayo ipo tayari kuwatumikia Watanzania, tukope, tuweke miundombinu ya maji ili wananchi akina mama ambao wanateseka kwa muda mrefu kuchota maji, wanachelewa kwenda kuzalisha shughuli za kiuchumi tuweze kuwawekea mtandao wa maji unaostahili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, na mimi nalalamika kila Bunge ninaposimama hapa, kila ninapochangia hotuba hizi za Waziri Mkuu, TAMISEMI na Maji yenyewe, Waziri wa Maji, Tarafa ya Ndagalu ni kilometa 58 kutoka Magu Mjini, ni kilometa 65 kutoka Ziwa Victoria lakini haina hata mto. Ni Tarafa kame inapakana na kwa Mheshimiwa Chenge kule naye ana shida ya maji, imepakana na Itilima na Maswa kule nako kuna shida ya maji. Ni vizuri tukaangalia namna ambavyo tunaweza kuisaidia Tarafa hii, ni Tarafa kubwa lakini wananchi wake wanateseka, haina mto wala mabwawa. Mheshimiwa Waziri nikuombe sana uangalie utakapokuja kwenye bajeti yako uweze kuona utaisaidiaje Tarafa hii ya Ndagalu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lipo suala la walemavu, bahati nzuri Serikali ya Awamu ya Tano inawajali kikamilifu walemavu na ndiyo maana hata Naibu Waziri ikamteua yule anayelingana na mazingira ya hawa ambao nataka kuwasemea.

Mheshimiwa Mwenyekiti, walemavu bado hatujawaangalia sawasawa hasa kwenye mikopo ya uzalishaji mali, tunawaunganisha tu kwenye mifuko ya vijana na wanawake, lakini hii mifuko tungeweka mfuko kwa sababu ya kuwawezesha walemavu ili waweze kujikomboa kwenye biashara ndogo ndogo, wawe na uchumi ambao unaweza kuwasaidia katika maisha yao na familia zao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, yapo malalamiko ya watumishi ambao wakati huo walikuwa wanachangia NPF na baadae wakahamishiwa NSSF kwamba zile fedha zao walizokuwa wamechangia NPF wanapokwenda kustaafu wanategemea NSSF itakuwa imeziingiza na zile, wanajikuta hizo fedha hazipo, wanahangaika kweli.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikuombe Waziri wa Fedha kwenye jambo hili litazame kwa moyo wako wa huruma maana hawa watumishi wametumika kwa muda mrefu sana, wanapokosa mafao haya wanapata taabu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini Mfuko huu wa NSSF inaonekana mteja anapochangia kwa maana ya mtumishi, hakuna ongezeko lolote ambalo linaongezeka kwenye mchango wake. Anapokwenda kulipwa mafao yake analipa mafao yale yale, hilo ndilo lalamiko la watumishi wengi hasa waliopo kwenye Idara ya Afya. Niombe sana hili jambo Serikali iweze kuliangalia vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niungane na wenzangu kuzungumzia suala la Watendaji wa Vijiji ambao waliajiriwa kwa darasa la saba, hawakuwa na kiwango cha elimu ya sekondari. Hawa wametumika kwa nchi hii na hawa si wengi sana waliobaki, ni vizuri tukawaangalia namna pekee ya kuwasaidia ni kuwarudisha kazini kwa sababu wamebakiza muda mchache. Mambo ambayo wanayafanya yanalingana kabisa na elimu yao, hawa ndio waliojenga shule za msingi, zahanati, sekondari na ndio walinzi wa amani kwenye vijiji hivyo, leo tukiwaacha hawa hiyo ndiyo adhabu yao? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niombe sana, Mheshimiwa Waziri wa Utumishi yupo hapa, Makatibu Wakuu wapo na Waziri Mkuu yupo, muone namna, hatuna sababu ya kuendelea kujadili Bungeni hapa, ni kutoa waraka tu hata kama ni kesho ili warudishwe kazini wale ili baadaye sasa tuangalie utaratibu wa wale wanaoendelea kuajiriwa wenye sifa zinazostahili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, na mimi nataka niwaambie hawa wanafanya kazi…

(Hala kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MHE. KISWAGA B. DESTERY: Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja ahsante sana.