Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Azimio la Bunge la Kuridhia Makubaliano ya Paris chini ya Mkataba wa Umoja wa Mataifa kuhusu Mabadiliko ya Tabianchi

Hon. Richard Phillip Mbogo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Nsimbo

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Azimio la Bunge la Kuridhia Makubaliano ya Paris chini ya Mkataba wa Umoja wa Mataifa kuhusu Mabadiliko ya Tabianchi

MHE. RICHARD P. MBOGO: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa nafasi moja kwa moja niseme tu kwanza naunga mkono hoja ya kupitisha hili azimio kwa ajili ya makubaliano ya Paris kuhusu kuboresha utekelezaji wa mkataba wa mabadiliko ya tabianchi.

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la kwanza ambalo ningependa kuchangia kwanza tukubaliane na hili Azimio kwa sababu tuna faida nyingi ambazo Mheshimiwa Waziri ameweza kuzieleza kama nchi ambavyo tunaweza kufaidika; la kwanza ni mkakati wa kutekeleza utunzaji wa mazingira, upatikanaji wa fedha, masuala ya kuweza kupanda miti ambayo itaweza kunyonya gesijoto, lakini kikubwa ni kwamba uhai wa mwanadamu upo kwenye mazingira, duniani nchi zote tunafanya shughuli za kimaendeleo lakini tunaangalia na uhai wa kwetu sisi wanadamu.

Mheshimiwa Naibu Spika, ongezeko la joto duniani lina athari nyingi sana kama ambavyo tumeweza kuelezwa pamoja ikiwa ni uchafuzi wa mazingira, kuleta ukame, magonjwa, uharibifu wa miundombinu na mambo mengine mengi sasa kwa misingi hiyo tunavyokubali azimio hili na kila nchi kuweza kutaekeleza ili Azimio katika kusimamia kutunza mazingira tutaenda kuonyesha kwamba uhai wetu sisi wanadamu utakuwa na uhakika wa kuwepo na kuishi.

Sasa kutokana na vifungu mbalimbali vya makubaliano ambavyo vimeweza kuelezwa ningependa kama nchi kwa sababu haya ni mabadiliko yamepitishwa mwaka 2016 basi tuombe kwenye mabadiliko ambayo yatakayofuata mbeleni katika haya maazimio tusisitizwe sana kwenye nchi ambazo zinachangia katika uharibifu na kuleta joto duniani ziweke vipengele ambavyo vitahakikisha kwamba wanatekeleza utoaji wa fedha kwa ajili ya nchi zinazoendelea katika kutunza mazingira.

Mheshimiwa Naibu spika, hilo litakuwa ni jambo la umuhimu sana katika kuzibana hizi nchi na pia katika mawasilisho imeonekana kuna baadhi ya nchi ambazo zinakuwa haziko tayari zikiangalia kwamba zenyewe zinaathirika zaidi katika shughuli zao za kiuchumi kutokana na kubanwa kwenye shughuli zao.

Kwa hiyo, tuombe katika maazimio mbeleni huko marekebisho ambayo yatafanyika tuone namna ya kuzibana hizi nchi na hasa hizi nchi ambazo tena zilizoendelea zinazoshindana zaidi na zinakuwa zinapinga maazimio kama haya basi tuone namna ya kuzibana ili ziweze kutekeleza kwa namna ambayo na sisi ambao ndio nchi maskini tunaoendelea na ndio ambao wengi tunaotunza mazingira na dunia angalau inakuwa ya ina uhakika kwamba tutaendelea kuishi duniani kwa sababu ya nchi hizi ambazo tunazoendelea ambazo tunatunza mazingira.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mfano Tanzania asilimia 30 ya nchi yetu iko kwenye uhifadhi kwa hiyo, tuna uhakika wa kuendelea kutunza na dunia ikapata nafuu.

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kuangalia upande wa kimataifa naomba nije kwa upande wa kama nchi Tanzania, tunajua tunazo sheria, tuna sera, na tuna uongozi, lakini ni kwa namna gani tunasimamia hizi sera upande wa mazingira na tunasimamia sheria zetu ili ziweze kutunza mazingira tumeona changamoto sehemu mbalimbali za nchi yetu kumekuwa na uharibifu mkubwa sana wa mazingira na hasa kufanya kazi za maendeleo kutoka kwenye kingo za mito kama sheria inavyosema mita 60 na mita 500 kutoka kwenye vyanzo vya maji.

Mheshimiwa Naibu spika, lakini kuna wamiliki wa mabonde, tunayo TAMISEMI na tunayo Wizara husika ila usimamizi katika maeneo mbalimbali huku hafifu mno matokeo yake shughuli za kibinadamu, za mifugo, za kulima wamekuwa wanaingia mpaka maeneo ya vyanzo vya maji na kingo za mito kwa hiyo inapelekea kuharibu mazingira, na kwa misingi hiyo changamoto mojawapo ninayoiona ni uwezeshaji wa Halmashauri zetu kupitia hii Wizara jinsi gani wanazishikisha katika kusimamia na kikubwa pia tunashindwa kuwatumia namna fulani sijapenda kuielewa Wakuu wetu wa Wilaya ambao ni Wenyeviti wa Kamati za Ulinzi na Usalama katika Wilaya kwanza hawana OC za kutosha kuweza kuzunguka na kusimamia vizuri watendaji walio chini.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, niombe Serikali tuangalie namna gani tunaongezea OC Wakuu wetu wa Wilaya waweze kusimamia Halmashauri zetu katika kulinda mazingira na kijumla maana imekuwa ni changamoto na mpaka maeneo mengine Wakuu wetu wa Wilaya hawana vyombo vya usafiri vya kutosha au vingine vimechakaa na havifai katika utendaji wa kazi.

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine ni suala la kiuongozi kiujumla jinsi gani tunashirikisha kuanzia Wenyeviti wa Vijiji, Wenyeviti wa Kitongoji katika kulinda mazingira elimu je, wanayo na inatumika ipasavyo kwa hiyo tuombe tena Wizara tuone namna gani tunawashirikisha.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna suala la nishati katika matumizi ya kawaida ya nyumbani mambo ya kupikia mkaa na kuni ndio vinatumika kwa asilimia 98 na je, mkakati wa Serikali katika kulinda mazingira nishati mbadala kwenye matumizi ya nyumbani mkakati uko namna gani, matumizi ya mkaa kwa mfano Jiji la Dar es Salaam ndio linaloongoza katika nchi hii je nishati mbadala iko vipi, tuna taasisi za Serikali sasa hivi wananchi wengi na wataalam wengi wanatengeneza biogas kwa kupitia taka na vyanzo vingine na wanatumia kwenye matumizi ya nyumbani kwa ajili ya kupikia, sasa mkakati wa Wizara hii husika kupitia Ofisi ya Makamu wa Rais hili fungu linalopatikana toka kwenye nchi wahisani wanaotoa kwa ajili ya kutunza mazingira watenge kwa ajili ya kuelemisha na kufundisha na watu kuwawezesha kutumia biogas kwa ajili ya matumizi ya nyumbani.

Mheshimiwa Naibu Spika, na kwa mfano unaweza ukaanza na taasisi kama Magereza, taasisi hizi kama vyuo vikuu, mashule watengeneze biogas kwa ajili ya kupikia. Hizi shule za bweni maana yake wanapikia wanafunzi chakula je, wanatumia nishati gani? Pia tukienda kwenye shughuli za kilimo kwa mfano mazao ya biashara kama tumbaku sasa hivi wakulima wanakausha tumbaku, wanakata miti sawa Serikali imeleta mabanio ambayo kidogo yanatumia kuni zile ndogo ndogo chache, lakini wengine hawatekelezi je tuna nishati mbadala tuache kukata miti?

Kwa hiyo, niombe sana Serikali kupitia hii Wizara waje watueleze biogas na nishati mbadala tuachane na mkaa na kuni katika kupikia ambayo ndio inayokata miti sana katika nchi yetu namna gani tunaenda kuwezesha kwa kupitia haya mafungu yanayotoka kwenye nchi zilizoendelea zinazotoa kwa ajili ya kusaidia kupunguza athari za ongezeko la joto humu duniani. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kumalizia niombe sasa kwa upande wa hizi halmashauri mlizilazimishsa kwamba Serikali ilisema kila Halmashauri ipande miti 1,500,000 na waliweka kwenye bajeti sasa utekelezaji mpaka sasa hivi kila halmashauri wamepanda miti mingapi hiyo utakuta ni hafifu na watu hata wakipewa ile miti, je, wanaisimamia wanahakikisha kwamba na inakua kwa hiyo, usimamizi katika upande wa mazingira tuone namna gani tunaongeza juhudi ili tuhakikishe kwamba utekelezaji wake wa haya maagizo tunayotoa yanasimamiwa ipasavyo.

Mheshimiwa Naibu Spika, la mwisho ni Wizara ya maliasili na utalii ina maeneo mengi yaliweza kuathirika kutokana na watu kuvamia kwa shughuli za kilimo mbalimbali lakini je, tunahusisha vipi kuingia ubia na halmashauri zetu kupanda miti rafiki kama ilivyo katika maeneo mengine kwa mfano kama mazao ya korosho ili tuweze kuboresha hayo maeneo.

Mheshimiwa Naibu Spika, na la mwisho ni elimu tumesema kwamba tupande miti ambayo itaenda kunyonya gesi je, hii miti tunayowaambia wataalamu wetu huko na wananchi wetu tunawaelimisha kwamba miti hii mnayopanda ndio ambayo itaenda kunyonya gesi elimu hiyo inatolewa na kwa kiasi gani inatolewa na fedha za kusaidia kutoa elimu Halmashauri zetu tunazozipata.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuunga mkono hoja na nashukuru.