Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2016 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018

Hon. Gibson Blasius Meiseyeki

Sex

Male

Party

CHADEMA

Constituent

Arumeru-Magharibi

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2016 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018

MHE. GIBSON B. MEISEYEKI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi ya kuchangia hotuba ya Waziri wa Fedha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nami nianze kwa kuunga mkono maoni ya Msemaji wa Kambi ya Upinzani kwa Wizara hii. Kama alivyosema mwenzangu, Waziri achukue muda kwenda kupitia mapendekezo hayo kutoka Kambi hii, wataalam wetu wamepitia na kuja na mapendekezo ambayo yangeweza kumsaidia sana kuweza kutekeleza majukumu yake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwa kuiasa Serikali kutekeleza majukumu yake kwa kufuata utawala wa sheria. Tutapona sana na itakuwa na manufaa makubwa sana kwa nchi yetu kama tutaongozwa kisheria. Hivi karibuni tumekuwa tukiongelea sana masuala ya Sheria zetu za Madini, kumekuwa na maneno ya ajabu ajabu kupinga wengine ambao wanatoa mapendekezo lakini tunashukuru kwamba kwa namna fulani Serikali imechukua mapendekezo ya baadhi ya watu ambao wanaitwa waropokaji na sasa tunaona kwamba sheria hiyo inataka kuletwa hapa Bungeni kufanyiwa marekebisho.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ningeomba wataalam wetu wa sheria, Waziri wetu wa Sheria asisite kutumia rasilimaliwatu walioko upande huu katika kuleta marekebisho ya Sheria hiyo ya Madini ili tuweze kupata sheria ambayo italinusuru Taifa hili katika kutokupoteza rasilimali madini tuliyonayo katika nchi hii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile sitasita kumshukuru Mheshimiwa Lissu kwa uelewa wake katika eneo hili. Ningependa kama inawezekana Serikali bila kuona aibu isisite kuchukua maarifa ambayo wataalam au kwa watu ambao wamebobea kwenye maeneo hayo wakatengenezea kitu ambacho tukija hapa kama ilivyo desturi yetu tutapitisha tu kwa ‘ndiyo’ tupitishe kitu ambacho kimefanyiwa kazi vizuri na kiko balanced ili tuweze kunufaika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, juzi Maazimio yalikuja hapa ya kumpongeza Rais, lakini mimi niseme kwa uelewa wangu msingi mkubwa wa hasara ambayo tumeipata kwenye madini na matatizo yote haya yamejikita kwenye Katiba yetu, ni sheria lakini na Katiba pia. Ningekuwa mtu wa kwanza kabisa, tena na kubeba mabango ikiwezekana nitaingia huku na vuvuzela kumpongeza Rais kama angetuletea Mapendekezo ya Warioba, ile Rasimu ya Pili ya Warioba ikaletwa hapa Bungeni tukapitisha kama Katiba yetu. Tutakuwa tumelitatua hili tatizo pale kwenye kiini chake lakini haya mazingaombwe ambayo naona yanataka kufanyika hapa katikati hayatatufikisha popote kwa sababu msingi wa makosa yote umejikita sehemu ambayo hatutaki kuigusa. Kwa hiyo, mimi ningeomba tukali-attempt hili maana Wazungu wanasema you can not solve a problem with the same mind that created it. Nasema kwamba tuilete Katiba, tuibadilishe hapa, tutakuwa tumetatua kwa kiasi kikubwa sana mlolongo wa haya matatizo ambayo yako kwenye sheria zetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia niseme hivi karibuni kumekuwa na kulipukalipuka kwa watu kutekeleza mapendekezo au tuseme sheria mbalimbali zilizopo. Hivi majuzi nimeona watu wakiingilia kwenye mashamba ya wawekezaji tena moja la Mwenyekiti wetu, wakaenda wakafanya uharibifu mkubwa. Nasema huko ni kukurupuka na tukikurupuka tutaipeleka nchi hii kama walivyosema wenzangu, wataipeleka kama ilivyo Zimbabwe sasa hivi ambako wote tunafahamu kwamba Zimbabwe haitumii currency yake sasa hivi kwa sababu, kwa bahati mbaya neno ambalo lilikuwa linakuja sio zuri, wamejiharibia wenyewe. Ilifika wakati wanaenda kununua kilo ya sukari kwa mfuko wa fedha na sasa hivi wanatumia fedha za kigeni kama bill of exchange kwenye nchi yao. Sasa tukikurupuka kurupuka na sisi kwenda kuvamiavamia watu nadhani tutaishia pabaya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mashamba ambayo yana sifa kama alilokuwa nalo Mheshimiwa Mbowe yako mengi sana na kama Wakuu wengine wa Wilaya wao hawatatekeleza kama alivyotekeleza yule pengine siku moja wendawazimu wengine kama sisi au mimi tutaenda kuwasaidia kuharibu. Maana katika Wilaya yetu ya Arumeru wawekezaji wenye mashamba ya maua ambayo yamekaa pembezoni mwa maji au mito ni karibu mashamba yote lakini sijui ni nani huyo na akili zake ziko vipi amekurupuka ameenda kuvunja shamba la Mwenyekiti wetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mienendo kama hii haitatupeleka pazuri. Kama ni operesheni ya kuondoa mashamba ambayo yako pembezoni mwa mito basi mashamba mengine yote ya maua, miwa, mpunga nafikiri ni vyema yakahakikiwa na yenyewe ili hii kama ni sheria basi ile pande zote lakini tuwe na tahadhari, tusije tukaipeleka nchi yetu kwa akina Zimbabwe na Venezuela. Nilitaka niseme hivyo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikitaka kwenda kwenye bajeti nianze kwa usemi wa mwanamuziki hayati Bob Marley maarufu kwa taste ile ya reggae, aliwahi kuimba kwenye wimbo wake wa get up, stand up akasema, you can fool some people sometimes but you can not fool all the people all the time. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hii bajeti iliyoletwa hapa inataka kututegatega. Watanzania wa sasa hivi ni werevu sana, tusidhani ni kama wale watu wa miaka ya 60, 70, watu wamezidi kujanjaruka kwa hiyo huwezi kutudanganya. Nimwombe tu Waziri wa Fedha hili suala mnalosema elimu bure kwa bajeti hii tuanze kulifuta kwa sababu umedanganya kwa upande huu halafu sasa kwa upande huu unakuja ku- balance. Watoto wengi ambao wanasoma kwenye shule zetu za msingi ni zile familia ambazo kiukweli hata umeme wanausikia tu hawajawahi kuuona. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo unapowawekea hizi Sh.40/= kwa kila lita moja ya mafuta hao ni kwamba unaenda kuwatoza zile hela zako ulizosema elimu bure, kwa hiyo tuifute. Utapitisha bajeti yako hii kwa Sh.40/= kwa kila lita moja ya mafuta ya taa, nazungumzia mafuta ya taa, petroli na dizeli tutajua huko mbele lakini mafuta ya taa, maana yake ni kwamba unakwenda kuwatoza Watanzania ile pesa ya ada ya shule waliyokwenda kuilipa, ndiyo maana yake na wajanja wameshajanjaruka. Kwa hiyo, hapa hamna elimu bure, you are charging us. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia Mheshimiwa Waziri mwaka jana tulizungumza mengi kuhusiana na bandari.

Walikwenda pale wakasema hata zikiingia meli mbili kama zile nyingine haziingii, sasa kule kumetetereka amekuja hapa anatuambia kwamba uchumi wa dunia umeyumba, sio kweli! Siku hizi tunakaa na simu zetu hapa, tunaangalia Beira, Mombasa, Tanzania sasa hivi Bandari yetu ya Dar es Salaam inakaribiana na Kismayo Somalia kule kwenye ma-pirates kwa jinsi ambavyo hakuna meli sasa hivi. Sasa wasituambie kwamba uchumi umetetereka, hapana! Walizinyima hizo meli jana kuja na tuliwaambia wakakataa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumewaambia tena kuhusiana na VAT kwenye utalii, wameleta ndege sijui nani atazipanda hizo Bombadier ambayo tunajua moja tayari iko grounded na ilikuwa mpya. Hawawezi wakaleta ndege, apande nani wakati utalii huku kwao wana-discourage? Wenzetu wa nchi za jirani wamefuta VAT, wao wamekomalia. Sasa utalii utaanguka halafu mwakani atakuja kutudanganya kwamba kuna mtikisiko wa kiuchumi. Hii tunai-note na mwakani sijui atatuambiaje. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye bajeti hii naomba tunapo-set priorities tuzisimamie. Rais alipokuwa anaomba kura hata na sisi wote tatizo la maji tuliliona tumeli-address na akasema anaenda kuleta suluhu ya shida ya maji nchini. Hata hivyo, wameingia madarakani cha ajabu ni kwamba hela nyingi wamezipeleka kwenye kuleta ndege mpya ukilinganisha na walizozipeleka kwenye maji. Pesa za kununua ndege zimezidi karibia bilioni 50 pesa walizopeleka kwenye maji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna shida ya maji, Arumeru yangu tuna kiu sana ya maji tuangalie priority zetu, tunapopata fedha tusikengeuke, twende kwenye zile areas ambazo tulisema kwamba tunaenda ku-accomplish. Kwa hiyo, naomba tu-stick kwenye bajeti kama tulivyokuwa tumeipendekeza ili tuweze kumaliza kero nyingi ambazo wananchi wanazo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna shida sana, tunahitaji barabara, mwaka jana swali langu moja lilijibiwa na Naibu Waziri, nafikiri ni wa Ujenzi, akasema kwamba barabara yetu inayounganisha Arusha na Simanjiro inafanyiwa upembuzi yakinifu. Walisema shilingi milioni 600 imeshapelekwa pale isije ikawa tena miaka mitano. (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa mzungumzaji)

Mheshimiwa Mwenyekiti, siungi mkono hoja. Ahsante.