Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2016 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018

Hon. Yussuf Kaiza Makame

Sex

Male

Party

CUF

Constituent

Chake Chake

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2016 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018

MHE. YUSSUF KAIZA MAKAME: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Kwanza naunga mkono hoja ya Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni kuhusiana na hili jambo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili, nataka niweke sawa record au Hansard kwamba wakati jana Mheshimiwa Ali Salim akichangia, alipewa taarifa na Mbunge mmoja kwamba kwenye Taifa hili haikumbukwi Tanganyika. Hili ni jambo la upotoshaji na tunajua kwamba Muungano wetu huu ni wa Watanganyika na Wazanzibari.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, Tanganyika ipo. Hapa pia tukiwa Bungeni tunasema kuna mambo ambayo siyo ya Muungano. Hayo siyo mambo ya sehemu nyingine, ni mambo ya Tanganyika na hakuna jambo ambalo ni la Tanzania Bara. Hakuna Taifa lililozaliwa Tanzania Bara na hakuna uhuru tunaousherehekea ukawa wa Tanzania Bara, ni uhuru wa Tanganyika. Kwa hiyo, naomba tuweke record sawa katika hili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili ambalo nilitaka niliseme leo hii ni hili suala la mchanga. Suala la mchanga kidogo limetutoa kwenye ajenda kuu ya bajeti kwa Bunge zima. Sizungumzii Wapinzani wala sizungumzii watawala; nasema kwamba limetutoa na pengine ni mkakati maalum, uliotengenezwa ututoe katika ajenda ya msingi ya bajeti. Watu wengi kwa asilimia 70 bajeti hii, wanazungumzia makinikia ya mchanga, hawazungumzii bajeti. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilisema kwenye kuchangia hotuba ya Wizara ya Nishati na Madini na nasema tena. Katika jambo ambalo linahitaji mshikamano na umoja wa Kitaifa ni hili, lakini mshikamano huo hauwezi kupatikana kwa maneno tu, tunahitaji kubadilisha sheria zetu na ikibidi twende juu zaidi kwenye Katiba yetu ya nchi kufanyia yale mapendekezo yaliyoletwa na Tume ya Jaji Warioba, yaletwe tena basi tuyapitie na tupitishe Katiba mpya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala hili mnadhani kana kwamba linaongelewa kijuujuu. Kama neno alilolitumia Mheshimiwa Bilago, kama kuna watu wanaoenda na maandamano ya mioyo ni Wazanzibari. Suala la Muungano siyo suala la mchezo mchezo la kuangaliwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo tunazungumzia mikataba ya madini na tunazungumzia tume zilizoundwa. Leo tumempongeza Mheshimiwa Rais lakini tume zilizoundwa kuangalia masuala ya madini ni nyingi na findings zake zilisomwa, lakini utekelezaji wake haukufanyika. Leo Mheshimiwa Rais kaja, kazungumza aliyoyazungumza, kawa na ujasiri kafanya alichokifanya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Mungu katika Taifa hili kwamba aje Mheshimiwa Rais azione tume zilizopitia masuala ya Muungano au jambo hili la Muungano na mapendekezo yao, aje aseme kwamba sasa ipo haja ya kuunda Serikali tatu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu jambo hili lipo na tume zote zaidi ya nane zilizoundwa kwenye nchi hii toka kipindi cha Mwalimu Nyerere mpaka leo zote zimependekeza Serikali tatu. Leo tukizungumzia suala la Muungano humu ndani ni kana kwamba unazungumzia kitu cha ajabu. Wapo waliozungumzia madini tunayoibiwa mkawaona wa ajabu; leo ndiyo mnaona hili jambo ni jema zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la utawala wa sheria, haki na demokrasia; hatuwezi kuendesha bajeti zetu hizi kama hakuna haki, hakuna demokrasia ya kweli katika nchi yetu. Hili jambo mnaweza mkaliona nila mchezo mchezo sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wamekosa maji, wamekosa umeme, wamekosa na huduma nyingine muhimu kutoka misaada ya nje ……(Kicheko)

TAARIFA . . .

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimefuta hayo maneno. Nasema kwamba utawala wa sheria ambao unafuata haki na demokrasia, sawa sawa! Hapa tunachokizungumza hasa ni uchaguzi ule wa Zanzibar; na hapa mimi sizungumzii nini kinachoendelea Zanzibar, nazungumzia impact ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano kutokana na uchaguzi wa Zanzibar kwa kulazimisha viongozi ambao hawakuchaguliwa na wananchi kukaa katika madaraka. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Watanzania sasa hivi ni karibu milioni 50. Sisi Wazanzibari hatufaidiki na REA, lakini wanaoathirika ni Majimbo yenu hayo mnayopigia kelele. Kwa hiyo, ili utekelezaji wa bajeti uende vizuri, ni lazima Serikali ikubali utawala wa sheria, haki na demokrasia katika nchi yetu kwa sababu tumekubali mfumo wa vyama vingi vya siasa nchini. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la Mfuko wa UKIMWI; ninachotaka kuzungumza hapa kuna Watanzania wenzetu wanaoishi na virusi vya UKIMWI, wengi sana. Donors wamejitoa au wengi wamejitoa kutoa misaada katika masuala haya ya UKIMWI. Pengine huko tunakoenda hali itakuwa mbaya zaidi. Sasa ninachotaka kushauri kwa Serikali hii, tuwa-serve Watanzania wenzetu kwa pesa zetu za ndani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumetengeneza percent ya kuingia kwenye REA, basi tutengeneze percent ya kuingia kwenye mfuko wa UKIMWI kwa ajili ya kuwa-serve Watanzania wenzetu wanaoishi na virusi vya UKIMWI. Mfano, tumeweka tozo ya Sh.40/= kwa kila lita ya mafuta, tunaweza aidha, kupandisha ikawa Sh.42/= ama kwa hiyo hiyo iliyowekwa tukaweka Sh.2/= kwa kila lita ikaingia kwenye Mfuko wa UKIMWI ili waweze kujiendesha wenyewe. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wenzetu wa Zimbabwe tumeambiwa hawategemei misaada kwenye suala hili. Kwenye suala la UKIMWI Wazimbabwe pamoja na kasoro zao walizonazo, suala la UKIMWI wanategemea fedha zao za ndani. Kwa hiyo, nasi tujitathmini katika hili, linapoteza nguvu kazi kubwa ya Taifa. Kwa hiyo, tuweke tozo japo ya Sh.2/= kwenye lita ya mafuta ama kwenye bia. Kwenye bia tumeongeza Sh.765/= kutoka Sh.729/=. Sasa hapa kwenye Sh.765/= tunaweza tukatoa Sh.5/= tukaingiza moja kwa moja kwenye Mfuko wa UKIMWI kwa ajili ya kwenda ku-serve Watanzania wenzetu. Hii itaenda na yale malengo ya kwamba 2030 UKIMWI uwe haupo tena Tanzania au katika dunia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ni suala la ajira kwa vijana, bajeti hii haikuzungumza kabisa suala la ajira na Serikali hii haijazungumza kabisa toka iingie madarakani suala la ajira. Wanafunzi wanaomaliza vyuo ni numbers...

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa mzungumzaji)