Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2016 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018

Hon. Desderius John Mipata

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Nkasi Kusini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2016 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018

MHE. DESDERIUS J. MIPATA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi. Niungane na wenzangu kumshukuru Mwenyezi Mungu kutujalia uzima, lakini pia nimpongeze Mheshimiwa Waziri na Mheshimiwa Naibu Waziri kwa kuja na hotuba nzuri sana. Hotuba hii ni nzuri sana, tofauti na wenzangu wanaosema ina matatizo. Mimi niko hapa Bungeni kwa muda wa kutosha, miaka sita, nasema hotuba hii ni nzuri sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kabla sijaendelea, nampongeza Mheshimiwa Rais kwa kazi nzuri anayoifanyia Tanzania. Rais huyu ni wa pekee! Waswahili wanasema, “Kila zama na kitabu chake.” Kitabu cha Mheshimiwa Rais Magufuli kitaandikwa kwa wino wa dhahabu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, utendaji huu ni message kwa wanasiasa wengine wanaotafuta nafasi kama ya kwake. Una kiatu cha kujaa hapo? Una mguu? Kiatu chako kinatosha? Mguu wako unatosha hicho kiatu? Ni message kwa Watendaji Serikalini, huyu Rais anataka Watendaji wa namna gani kwenye Serikali yake? Ni message kwa wananchi wote. Tumuunge mkono kwa sababu dhamira yake ameiweka wazi, ni ya kizalendo kupita kiasi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vile vile ni message kwa nchi nyingine kwamba Tanzania kuna viongozi wana macho na wanajua kulinda nchi yao. Nampongeza sana Mheshimiwa Rais. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nije kwenye bajeti. Bajeti hii ni nzuri, imekonga mioyo ya Watanzania wengi. Imefuta ada ya motor vehicle licence, imepunguza ushuru wa mazao ya biashara kwa wakulima wadogo wadogo na wafanyabiashara wadogo wadogo ambao mara nyingi wako kwenye wigo wa gunia 10 hizo hizo. Imemfanya mkulima sasa ajisikie kwamba kile anacholima kina thamani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashauri pia tuone kwenye ushuru kama dagaa na samaki na zenyewe tunaziachaje? Isiwe kimya namna hii, ili kama ni ushuru, basi tuwapunguzie wale wafanyabiashara wa samaki na dagaa katika kiwango kidogo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, bajeti hii inaenda kutekeleza ahadi za Mheshimiwa Rais alizoziweka. Tena aliweka ahadi ya kwanza kabisa kwamba anataka nchi yetu iende kwenye uchumi wa kati. Bajeti hii imeweka mipango mizuri kabisa ya kuboresha ujenzi wa barabara zetu, ujenzi wa reli katika standard gauge, ujenzi wa mifumo ya usafiri wa anga, majini lakini vile vile mfumo wa uendelezaji umeme ambao ni muhimu sana katika uchumi wa viwanda. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninachoweza kushauri ni kwamba utendaji lazima uwe makini; tutumie fursa tulizonazo hasa za kijiografia kuhakikisha kwamba haya mazingira tunayoyaweka tunafanya uzalishaji mzuri zaidi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano, Mkoa wetu wa Rukwa ni wa kilimo. Leo hii hali ya hewa ni nzuri sana Mkoa wa Rukwa, lakini bado kilimo siyo kizuri sana vile tunavyotaka. Bado hatujaingia kwenye kilimo cha kutumia matrekta, kilimo cha kibiashara ambacho kinaweza kikatukomboa na lazima watumishi waangalie, Mawaziri mjue kwamba kilimo kinabeba watu wengi; kinaajiri watu wengi. Ukiimarisha kilimo, kwa vyovyote vile unakuwa na wigo mpana wa kubadilisha uchumi wa nchi na kusaidia watu wengi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba bajeti hii ambayo naiunga sana mkono inisaidie mambo yafuatayo katika Jimbo langu. Vipo vijiji ambavyo vilisahaulika kupelekewa umeme na sikuviona kwenye orodha na niliweza kupata nafasi ya kumwona Mheshimiwa Waziri lakini na Mtendaji Mkuu wa REA. Vijiji hivi ni vijiji vya Katani, Malongwe, Nkana, Sintali, Ifundwa, Nkomachindo na Nchenje.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba umeme pia uende Kata ya Ninde iliyo na vijiji saba; Kata ya Kala ina vijiji saba, Kata ya Wampembe ambayo Waziri alitembelea mwenyewe ina vijiji vitano na hawa ni wavuvi wamekuwa wakivua samaki zao wanapeleka Zambia. Akiwapelekea umeme hawa amewakomboa na bajeti hii ni ya ukombozi. Kwa hiyo, naomba umeme ufike katika Kata hizi za mwambao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba pia bajeti ninayoiunga mkono sana iniunge mkono katika juhudi ya maji katika Jimbo langu la Nkasi Kusini. Tuna tatizo la maji katika Kata ya Nkhandasi ambayo ina Vijiji vya Kasu, Milundikwa, Malongwe, Katani na Kisula. Vijiji hivi vimekuwa na shida ya maji muda mrefu sana na juzi tumehamisha Shule ya Milundikwa tukapeleka kwenye Kata hii hapa. Kwa hiyo, naomba…

TAARIFA . . .

MHE. DESDERIUS J. MIPATA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naikubali sana taarifa yake na nilikuwa naendelea huko. Kwa hiyo, Vijiji vya Chonga, Makupa, Talatila na Miyula vina shida kubwa ya maji na ina mitambo na mtandao wa maji unafika pale. Kwa hiyo, ni suala la kufufua na kuanzisha. Namshukuru sana Mheshimiwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, bado ipo miradi ya maji katika Vijiji vya Nkundi na Kalundi. Vijiji hivi vina bwawa la Kawa ambalo tumekuwa tukilizungumza muda mrefu. Hatua zake ni nzuri, naomba Serikali ikamilishe ili wananchi waweze kupata matunda ya jasho la Serikali yao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mradi mwingine ni mradi wa maji wa Zuma, Isale ambao utahudumia vijiji vya Ntemba, Kitosi na Ntuhuchi. Mradi huu uko katika hatua za mwanzo. Naomba Watendaji waharakishe ili pesa ambazo tulitengewa kwenye bajeti ya mwaka 2016 zisirudi kwa sababu zipo za kutekeleza mradi huu. Kwa taarifa nilizozipata sasa hivi, karibu utekelezaji uanze.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho, bajeti hii inisaidie kutenga pesa kwa ajili ya Vituo vya Afya. Kipo Kituo cha Afya cha Kandasi, wananchi wameamua kujenga wenyewe, tunachohitaji hapa ni nguvu za Serikali, mtusaide. Kipo Kituo cha Afya cha King’ombe, Kata ya Kala. Kata ya Kala iko na umbali wa zaidi ya kilometa 150 kutoka Makao Makuu ya Wilaya. Akinamama na Watoto wamepoteza maisha yao kwa sababu ya umbali wa barabara isiyofikika. Bajeti hii ninayoiunga mkono leo ikawe mkombozi kwa vifo vya akinamama na watoto kutoka Kata ya Kala na Kituo cha Afya cha King’ombe kiweze kujengwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba pia Kituo cha Afya kijengwe Kate na Ninde na wananchi tumewahimiza na wako na utayari wa kutosha katika kuanza kujenga majengo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, bajeti hii ninayoiunga mkono, naomba ikawe mkombozi wa kuleta uchumi kwa wafanyabiashara wadogo waliotambuliwa leo, wasinyanyaswe tena ili pamoja na kutambuliwa kwao, basi Serikali ione namna ambavyo inaweza ikatumia vyombo vya fedha kuwasaidia watu hawa kwa kutoa mikopo midogo midogo ili waweze kupata mitaji na kuchangia katika uchumi wa Taifa pamoja na uchumi wa familia zao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Jimbo la Nkasi Kusini ni miongoni mwa Jimbo ambalo liko kwenye maeneo ambayo yana changamoto nyingi. Zipo barabara za Kitosi - Wampembe; barabara ya Kana - Kala; na barabara ya Namanyere – Ninde. Barabara hizi zimekuwa na changamoto kubwa sana, ukiziachia Halmashauri peke yake haiwezi kumudu kuwasaidia wananchi. Nomba bajeti hii ninayoiunga mkono sana, mtutengee pesa pia ya kuweza kuhakikisha kwamba barabara zetu zinapitika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, bajeti hii naomba itusaidie pia kuhakikisha kwamba mazao ambayo tumelima sisi watu wa Rukwa yanapata ununuzi kwa bei nzuri kidogo. Sasa hivi bei siyo nzuri sana, lakini gharama ya uzalishaji imekuwa kubwa. Mkipandisha bei mnatusaidia zaidi katika kuweka bei elekezi.