Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2016 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018

Hon. John Peter Kadutu

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Ulyankulu

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2016 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018

MHE. JOHN P. KADUTU: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nikushukuru sana kwa kunipatia nafasi hii kuchangia hoja iliyoko mbele yetu, hoja muhimu kwa maisha ya Serikali yetu pamoja na wananchi wetu, wakati huu tunapohangaika na maisha ya Watanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nachukua fursa hii kuwapongeza Mheshimiwa Waziri, Mheshimiwa Naibu Waziri pamoja na timu ya uongozi wote wa Wizara ya Fedha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, iko tofauti ya bajeti ya mwaka unaokwisha na hii iliyoletwa mwaka 2016 na mwaka huu wa 2017 kuna tofauti kubwa, kuna maboresho, lakini bado yapo mambo ambayo tunapaswa kuyatilia mkazo ili maisha ya wananchi wetu yaende vizuri na yawe bora.

Mheshimiwa Mwenyekiti, zipo huduma tunazozingumzia hasa barabara. Toka mwaka 2016 tumekuwa tunazungumzia barabara inayotoka Mpanda kupitia Kaliua, Uliyankulu hadi Kahama. Barabara hii ni muhimu sana kwa sababu itakuwa inaunganisha mikoa karibu mitatu au minne.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama azma ya Serikali yetu kuunganisha mikoa kwa lami, basi baada ya kipande cha Chaya na Nyahuwa kupata pesa, basi naomba Wizara ya Fedha na Wizara ya Ujenzi mwelekeze sasa nguvu zote kwenye barabara hii inayotoka Mpanda kupitia Uliyankulu mpaka Kahama. Ni kilomita 428 na nina imani wakipatiwa Wakandarasi kama watatu, kazi inaweza kwenda vizuri, badala ya kila mwaka kuizungumza kwenye Ilani lakini utekelezaji wake hakuna. Tunataka pia tupate performance ya utekelezaji wa mradi huu umefikia wapi?

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna jambo moja ambalo tunalizungumza hapa, lakini Serikali bado inakuwa ipo kimya. Suala la Mfuko wa Maji; tumezungumza sana lakini Serikali ije basi na kauli, tunakubaliana au hatukubaliani? Maana unapozungumza halafu mwenzako kakaa kimya, maana yake labda unachozungumza ni msamiati wa Kichina au Kijapani, maneno ambayo ni michoro michoro ambayo huwezi kuielewa. Serikali ije hapa na majibu: Je, tumekubaliana juu ya mfuko wa maji? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ndugu zangu, tatizo la maji vijijini ni kubwa kuliko tunavyodhani. Mpo wengine hapa ndani mkienda vijijini kwenu mnabeba maboksi ya maji. Hakuna mtu anayekwenda kunywa maji ya kijijini. Yawezekana mkaona hakuna haja kwa sababu huku ndani mjini mnaoga vizuri, mnakunywa vizuri, maji ya kupikia mazuri, hakuna anayejali. Kwa nini Serikali isije na majibu basi! Toka mwaka 2016 tunazungumzia Mfuko wa Maji, lakini tunaona kama vile mmeziba masikio. Njooni na ufumbuzi wa tatizo la maji. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, juzi wiki nzima nilikuwa Jimboni, kila eneo ukienda ni shida ya maji, lakini humu Bungeni kila mmoja akiulizwa swali la maji, maswali ya nyongeza Bunge zima linasimama, hata wewe Mwenyekiti unapata tabu sasa nani aulize na nani aache kuuliza? Hiyo ni kuonesha ni jinsi gani ambavyo suala la maji lina umuhimu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la ukamilishaji wa mradi wa umeme; tunakwenda tumeshaanzisha REA III. Naiomba sana Serikali, sasa tusiichie njiani, maana yake shida ni kwamba watu wote tunaelekea kenye madini; wote mazungumzo yamekuwa ni madini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la kukamilisha REA III liende kweli likatatue matatizo yaishe. Siyo tena tuje tuambiwe kuna REA IV na V. Itafika wakati hata pesa hatutapeleka kwenye umeme, kwa sababu umeme utaonekana siyo tena jambo la umuhimu. Kwa hiyo, nashauri hilo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, liko suala lingine juu ya suala la ujenzi wa Zahanati pamoja Vituo vya Afya. Jambo hili kama tunawaachia wananchi zaidi, hatuwezi kulikamilisha. Lazima Serikali ielekeze nguvu huko. Sasa tulisema kila Kata ijenge Kituo cha Afya; mabadiliko yamekuja, kila Kata mbili zijenge Kituo cha Afya; tunaanzisha tena migogoro kituo hicho kijengwe wapi? Kila Kata inapiga chepuo kujenga eneo lake. Kwa hiyo, nadhani Serikali kwa makusudi kabisa tuelekeze nguvu huko kwenye ujenzi wa Vituo vya Afya pamoja na Dispensary.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ningumzie hili suala la madini, migodi na kodi; mimi kabla ya kuingia hapa Bungeni, nimekuwa mfanyakazi huko kwenye migodi. Mwaka 2008 wakati issue ya Buzwagi inaletwa hapa, mimi nilikuwa mgodini. Sisi wafanyakazi wa kule tumekuwa tukipaza sauti sana juu ya matatizo haya ya uibiwaji wa mali hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaziona ndege, tunasema, lakini watu walikuwa hawasikii. Tumezungumza sana juu ya mambo haya! Kule mgodini pia kuna mambo ya unyanyasaji, kuna ubaguzi mkubwa na hasa raia hawa wa Kizungu wanaotoka South Africa, wananyanyasa. Sasa wakati wafanyakazi mgodini wanaponyanyaswa, wanapaza sauti juu ya wizi wa mali hii, lakini hakuna aliyesikia. Leo hata tukisema, hao wanaokuja kufanya kazi migodini, hawana elimu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kule nimeshuhudia watu wana vyeti vya semina ya siku tatu; na wenzetu wapo makini sana. Ukipiga semina hata ya siku moja, unapata cheti. Ukipiga semina ya siku mbili, unapata cheti; ndizo CV walizonazo. Ukienda Idara ya kazi, vibali vinatoka kila siku watu wafanye kazi, ambapo masharti yanataka mtu mwenye elimu zaidi, lakini awe na mpango wa kufundisha wazawa. Hakuna anayejali. Watu wapo migodini wanakamatwa na bangi, wanafikishwa Mahakamani, lakini kesho yake mtu huyo huyo anaomba kibali anaruhusiwa kufanya kazi ndani ya ardhi ya Tanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumzie ukwepaji kodi. Wote hapa akili sasa ipo kwenye Barrick na Acacia, lakini migodini, Mheshimiwa Waziri wa Fedha anisikie vizuri, zipo Kampuni nyingi zaidi kuliko kampuni tunayoizungumza, lakini hawa watu wanaiba, wanakwepa kodi kwa njia mbalimbali. Pesa zao wao wanalipana juu kwa juu, hakuna malipo ya moja kwa moja. Maana yake hata kodi haijulikani ni kiasi gani. Hata mifuko ya jamii hii hawachangii, kwa sababu wao wanarekodi mishahara midogo kuliko mishahara wanayolipwa kule nje. Mimi ni shahidi na niko tayari kueleza jinsi kodi inavyoibiwa kwa sababu nimekuwepo kule.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo Mheshimiwa Waziri wa Fedha ajaribu kuangalia sana, tusijikite kwenye Kampuni moja tu kubwa, wakati mle mgodini kuna kampuni nyingi zinafanya shughuli hiyo. Kwa hiyo, nashauri, kuchunguza kwa makini zaidi wizi au ukwepaji wa kodi wa kampuni zile ndogo ndogo ambazo zimepewa kazi na makampuni ya migodi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna suala la shilingi milioni 50. Imekuwa ni msumari huu, kila ukizunguka kwenye majimbo swali kubwa ni shilingi milioni 50, hatuna majibu! Serikali ije na majibu hapa. Siyo dhambi kusema kwamba tumeahirisha au tutafanya mara nyingine. Tuondokane na jambo hili au liletwe katika mpango mwingine kuliko kung’anga’na tutatoa shilingi milioni 50; huu ni mwaka wa pili sasa hatujatekeleza. Hatujafanya hata majaribio. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, la mwisho kabla hata kengele haijanililia kama kawaida yangu, fedha za maendeleo zinazopelekwa kwenye Halmashauri zetu, hata mwaka 2016 nilisema, lazima tuhakikishe fedha zinazokwenda kwenye Halmashauri ziende kwa wakati.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama fedha…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa mzungumzaji)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.